Hadithi ya kusisimuwa: Mimba ya jini-40-
ILIPOISHIA:
Sara na shoga yake waliona msala utawageukia, walitoka taratibu bila kuaga na kurudi nyumbani. Njia nzima Sara alijaa maswali na kukumbuka maneno ya mganga wa Vingunguti aliyemweleza kuwa mganga yeyote atakayetaka kuingilia kesi ile lazima moto umuwakie. Alipofika kwake aliteremka na kumuacha shoga yake arudi nyumbani kwake Kigogo.
SASA ENDELEA...
Alipofika alijikuta akizidi kukosa amani moyoni mwake na kujiuliza nini hatima yake baada ya kukaidi amri ya sauti ya kuacha kufuatilia mambo yasiyo muhusu Kilishomshtua zaidi kujua Shehna ni jini na ndiye aliyekuwa akimfanyia mauzauza yale.
Alijiuliza atamtazamaje hasa baada ya kumuasa aache kufuatilia mambo yasiyo muhusu. Alipofika nyumbani hakuwa hata na hamu ya kula, alinunua soda na keti, alikula kisha alioga na kupanda kitandani.
Usiku wa manane akiwa amelala alishtushwa na sauti kali ya vicheko mfululizo, alifumbua macho kutazama na kukutana na kiza kizito. Vicheko viliendelea mpaka kikawa kero masikioni mwake, mapigo ya moyo yalimwenda mbio kwa hofu.
Alipapasa pembeni ya kitanda na kushika swichi ya kitandani na kuwasha taa.
Ilipowaka alishtuka kuona viumbe wa ajabu mbele yake wakiwa wamesimama sambamba na ukuta. Walikuwa watu weusi sana wanne wenye mikia mifupi kama ya mbuzi na pembe ndogo kichwani. Sara alishtuka na kutetemeka kwa hofu huku haja ndogo ikimtoka bila kujijua.
Alijiuliza wale ni kina nani na wamefuata nini, wazo lake lilielekea moja kwa moja kwa wachawi. Akiwa bado hajajua nini kinaendelea aliiona ardhi ikipasuka na kuingia mwanamke aliyekuwa amekaa kwenye kiti cha dhahabu cha kifalme kilichokuwa kimebebwa mabegani na wanaume wengine wanne weusi wenye miili mikubwa na mikia kama wenzao lakini hao walikuwa na pembe moja katikati ya kichwa tofauti na wale wengine waliokuwa na pembe mbili.
Wale viumbe wa ajabu waliendelea kukibeba juu kiti kilichokaliwa na mwanamke mrembo mpaka ardhi iliyopasuka kujifunga ndipo walipomtua chini. Sara aliendelea kutetemeka huku akiwa amejikunyata upenuni mwa kitanda akiwa umesogea ukutani kabisa.
Yule mwanamke alikuwa amempa mgongo, alipopiga kofi aligeuzwa kumtazama, Sara hakuamini macho yake kumuona aliyekuwa mbele yake ni Shehna rafiki wa bosi wake. Baada ya kutulia alipiga makofi, viumbe vile vya ajabu vilitoweka na kubakia peke yake akiwa bado amekaa kwenye kiti chake cha dhahabu.
Baada ya kubaki wawili, Shehna aliteremsha pumzi nzito na kunyanyuka kwenye kiti na kusimama. Alimtazama Sara aliyekuwa bado amejikunja pembeni ya ukuta kwa woga. Alitembea taratibu kukizunguka chumba, alipompa mgongo alishtuka kumuona Shehna ana mkia mkubwa kama wa kangaroo lakini ule ulikuwa umenenepa sana.
Alipofika mwisho wa ukuta aligeuka akiwa amegeuka sura yake na kuwa ya kutisha meno yake yaligeuka kama ya ngiri juu ya paji la uso kulikuwa na pembe mbili kama za faru. Macho yake yalikuwa yakiwaka moyo, alicheka kicheko kizito kilichofanya Sara atokwe damu masikioni.
Shehna alikuwa kiumbe cha kutisha ambacho Sara hakuwahi kukiona maishani mwake, kwa sauti kali Shehna alisema huku moto ukitoka mdomoni.
Sara umenichimba sana, sasa umenijua haya niambie shida yako?
Ni..ni ..samehe She..she...
Sara sitakusameha lazima utajua faida ya kiburi chako, nilikuonya kwa sauti hukusikia nikaja mwenyewe hukunielewa, nina imani ulitaka uone nini kitatokea baada ya wewe kufuatilia mambo yasiyokuhusu. Nimekutisha ninavyojua lakini kichwa chako kimejaa kiburi nami nataka nikuonesha jeuri yangu.
Sitakuua bali nitakupa adhabu ya kipindi chote nitakapokuwa sipo chagua adhabu moja, nikugeuze Nguruwe, Chura, Funza maisha yako yote yawe kwenye kinyesi, bundi au mbwa?
Sara hakujibu, alijitahidi kumsogelea Shehna ili amuombe msamaha.
Shehna nisamehe shoga yangu.
Wewe si shoga yangu, mlitaka kuniua na mganga wako bila kosa, nimekukosea nini Sara? Shehna alirudi katika umbile la kibinaadamu na kuanza kulia machozi ya damu.
Ni sa..samehe sirudii tena.
Sitaki kusikia sauti yako, umetaka kunijua leo umenijua mimi ni jini, ujini wangu umekuathiri nini katika maisha yako?
Najua nimekukosea naomba unisamehe sirudii tena.
Sara sitakusamehe ukichelewa kuchagua adhabu yako nitakugeuza kiumbe cha ajabu kisicho na mfano.
Itaendelea wiki ijayo, siku ya Jumatano katika gazeti la Risasi Mchanganyiko.
Sara alijikuta kwenye wakati mgumu wa kuamua ageuzwe kiumbe gani, kabla hajapata jibu Shehna alipiga makofi mara walitokea viumbe wawili vya ajabu vinavyotisha sana tofauti na vyote vilivyotangulia.
Naam binti wa mfalme wa bahari ya dhahabu una shida gani?
Enyi watwana wenye roho chafu nataka mumtafutia adhabu yoyote kali huyu mwanadamu mnataka nimepa adhabu gani?
Kwa nini tusimbanike kama mbuzi karibu na jua? mmoja alipendekeza adhabu.
Hapana adhabu hiyo kali sana, nataka ya kumtesa ili atambue siri aliyoitaka kuijua faida yake ni nini.
Sisi hatuwezi kuchagua adhabu ndogo binti wa mfalme, tunaomba wewe uchague adhabu yoyote kwake tunajua amekuudhi sana. Adhabu yetu kwake ni kifo tena cha maumivu makali zaidi ya hapo hatuna adhabu.
Basi mnaweza kunipisha nitoe adhabu yangu.
Baada ya kusema vile viumbe wa ajabu alitoweka na kubakia Shehna katika umbile la kawaida la mwanamke nzuri katika vazi pana kutokana na ujauzito wake na Sara ambaye alikuwa akitetemeka mpaka utumbo. Alimuangalia kwa muda Sara aliyekuwa amejikunyata kwa woga upenuni mwa kitanda kwa sauti ya upole alimwita.
Sara.
A..a..bee.
Unaniweka katika wakati mgumu katika maisha yangu wa kukufanya kitu kibaya. Sikupenda kukufanyia chochote kibaya, narudia nimejitahidi kukuelekeza lakini umekuwa na masikio ya kenge mpaka utoke damu. Kwa vile umekataa kuchagua adhabu mimi nitakuchagulia adhabu, nilifikilia nikugeuze nguruwe lakini hiyo kwangu ni adhabu kubwa, nimejifikilia kukugeuza funza maisha yako yake kwenye kinyesi nayo hiyo nimeona ni adhabu kubwa.
Adhabu ndogo kuliko zote nimeonelea nikugeuze uwe mbwa ambaye atakuwa unazurura mitaani na kupigwa nawe na lakini sitaruhusu wakuue. Chakula chako nitakijua mimi utakula mara moja kwa siku. Nina imani utajua thamani ya kiburi chako.
Nitakuwa mbwa mpaka lini? Sara alijitahidi kuuliza.
Mpaka nitakapojifungua.
Shehna shoga yangu hakuna adhabu nyingine zaidi ya hiyo?
Sara mimi huwa sitoi adhabu bali umewaona watoa adhabu na adhabu zao, kama ningewaachia sijui ungekuwa kwenye hali gani?
Nipunguzie shoga yangu.
Sara unanichelewesha muda wangu umekwisha.
Baada ya kusema vile alinyoosha kidole ghafla Sara aligeuka mbwa, kisha Shehna alipiga makofi na viumbe wa ajabu walitokea. Aliwaonesha ishara ya macho huku akipanda kwenye kiti chake. Walikibeba juu ghafla ardhi ilipasuka na wao kuzama ndani yake kisha alijifunga na kuwa kama mwanzo.
Sara alibakia juu ya kitanda huku akiamini yeye ni mtu wala siyo mbwa, lakini bado hakuamini kilichotokea ni kweli zaidi ya kuota ndotoni. Siku ya pili aliamka asubuhi kama kawaida na kutoka nje kwenda kuoga ili awahi kazini lakini watoto wa jirani walipiga kelele kumuona mbwa.
Kitendo kile kilimfanya Sara arudi ndani lakini alishangaa kusikia.
Amekimbilia ndani kwa ma mdogo Sara, alisema mtoto mmoja.
Kwani Sara yupo wapi? alimsikia jirani yake mama Saidi akiuliza.
Sara..Sara, Happy alimwita kwa sauti.
Sara aliyekuwa chumbani kwake aliitika kwa sauti.
Abee nimo ndani, lakini ilitoka sauti ya mbwa kufoka.
Jamani mbwa huyu katokea wapi na Sara kaenda wapi asubuhi yote na kuacha mlango wazi, jirani mwingine alisikika akisema.
Jamani tufanyeni msaada wa kumtoa huyo mbwa ndani, mtu mwingine alitoa wazo huku majirani wakizidi kukusanyika.
Na kweli labda kichaa anaweza kutuuma pia hata watoto wetu.
Jirani mmoja alishika fimbo na kuingia chumbani kwa Sara na kushtuka kumuona mbwa juu ya kitanda. Alimtishia kumpiga ili atoke nje lakini Sara alitaka kujitetea kwa kuwaeleza kuwa yeye si mbwa ni mtu kama watu wengine lakini aliishia kumfokea kitu kilichoonesha anataka kumuuma. Ilibidi jirani amtandike fimbo iliyomfanya Sara atoe ukelele wa maumivu na kutoka nje ili kuokoa kipigo kile na kutokomea mitaani.
Kila mtaa alipopita watoto walimpiga mawe kitu kilichozidi kumweka kwenye wakati mgumu yeye alijifahamu ni mwanadamu na si mbwa lakini kila kona alipopita aliitwa mbwa. Alitafuta jumba bovu na kuingia humu kujificha japokuwa kulikuwa na kinyesi ambacho kilimnukia harufu mbaya. Lakini aliamini ile ni sehemu salama kwake kuliko kuzurula mitaani na kupugwa mawe na watoto.