Hadithi ya kusisimua- Mimba ya Jini

Hadithi ya kusisimua- Mimba ya Jini

Hadithi ya kusisimuwa: Mimba ya jini-36-


ILIPOISHIA :
"Ila mpenzi kwa mwezi mzima hatutaonana, nakwenda nyumbani mara moja kufanya mambo ya kimila baada ya kupata ujauzito."
"Mmh! Mpenzi nitateseka, nilikuzoea sana."
"Usiwe na wasiwasi nitakuwa nawe karibu muda wote."
"Tutakuwa pamoja kivipi wakati hautakuwepo kwa mwezi mzima?"
"Kila siku nitakuwa katika ndoto zako na ukiamka wala hutakuwa na majozi, usiku utakuwa kama mchana tena upo na mimi."
SASA ENDELEA...


"Sawa," Mustafa hakutaka kubishana na Shehna kwa kuamini kabisa alikuwa akipewa moyo kwa kujua siku zote furaha ya ndotoni ni maumivu ya asubuhi.
"Nilitaka kusahau, sasa hivi ruksa kukutana kimwili na mkeo."
"Hata bila ya dawa?"
"Yaleyale mafuta mtajipaka sehemu za siri kabla ya kukutana, ila lazima mkutane mara mbili kwa wiki, Jumatatu na Ijumaa."
"Kwa nini tukutane siku hizo?"
"Ndizo siku zenye nyota ya mtoto zaidi ya hapo mtakuwa mnatenga maji kwenye kinu."
"Basi tunaweza kukutana siku zote ila Jumatatu na Ijumaa ndiyo muhimu."
"Mustafa hiyo unapanga wewe, hii ni dozi ya kutafuta mtoto mkienda kinyume na hapo mtoto mtamsikia kwa kilio, akilia nyumba ya jirani."
"Nimekuelewa mpenzi."
"Najua sasa hivi huna matatizo ya fedha, kama utakuwa na shida amka usiku, washa udi utaweza kuniona ndotoni na kunieleza matatizo yako, kama ni fedha kabla ya kuondoka washa udi acha ufunguo mnapouacha ili niweze kukuletea hela."
"Shehna hivi wewe ni nani hasa?"
"Kivipi?"
"Bado nipo njia panda, wewe ni mganga au ji.., hapana sivyo ila naomba uniweke wazi maana mpaka sasa nipo njia panda," Mustafa alimuuliza huku amemkazia macho.
"Mustafa kipi kimekufanya unitilie shaka hivyo mpenzi wangu?" Shehna alimuuliza Mustafa huku machozi yakimtoka, kitu kilichomfanya Mustafa ajutie swali lake.
"Basi samahani mpenzi kama swali langu nimekukwaza."
"Mustafa mpenzi kipi nimekufanyia kibaya mpaka unifikirie hivyo au umenichoka mpenzi wangu?
Mapenzi yote ninayokupa unayaona bureee?" Shehna aliendelea kulia huku machozi yakimtoka kama maji.
Mustafa alijikuta akijilaumu kwa swali lake ambalo liliharibu furaha yake ya siku ile.
Alijutia nafsi yake kwa swali la kipumbavu lakini aliendelea kumbembeleza Shehna amsamehe kwa swali lake lile.
"Shehna mpenzi nisamehe kwa swali langu la kipuuzi."
"Mustafa mpenzi nikujali vipi? Siku zote nimekuwa nikikujali mbona sijawahi kukuuliza swali kama hilo?
"Au wema wangu wa kujitolea kwako ndiyo umeniponza?" Shehna alilia mpaka akawa mwekundu.
Mustafa alichanganyikiwa na kujikuta akitoka kwenye kiti chake na kwenda kupiga magoti mbele ya Shehna na kuanza kulia huku akiomba msamaha kwa kuamini Shehna ni mtu muhimu sana katika maisha yake kutokana na kumsaidia vitu vingi.
Kilio cha Mustafa kuomba msamaha kilimshtua Shehna ambaye siku zote hakupenda kumuona Mustafa akitoa machozi mbele yake.
Alimshika na kumnyanyua na kutazamana kila mmoja, macho yake yakiwa yamejaa machozi.
Machozi ya Shehna yalimfanya aongezeke uzuri maradufu na kuzidi kuutesa moyo wa Mustafa, kumpoteza kiumbe mzuri kama yule.
"Mustafa," Shehna alimwita kwa sauti ya kinanda.
"Naam."
"Nisamehe mpenzi," Shehna alisema huku akimfuta machozi kwa mtandio.
"Shehna huna kosa, mwenye makosa ni mimi niliyetoa machozi yako."
"Hapana Mustafa nakupenda sana, nimeumizwa na machozi yako, narudia tena naomba unisamehe."
"Nimekusamehe japo sioni kosa lako, naomba na mimi unisamehe."
"Nimekusamehe mpenzi wangu nami nashukuru kwa kunisamehe."
Walikumbatiana kila mmoja akirudisha furaha yake. Baada ya utulivu wa muda, Shehna alimuomba Mustafa atoke nje mara moja. Alimruhusu hakuchelewa alirudi baada ya dakika mbili akiwa na vinywaji mkononi. Aliviweka juu ya meza na kwenda kwenye friji ndogo na kutoa glasi mbili.
Itaendelea Jumapili wiki ijayo.
 
Akiitoa yote, nahisi ktk gazeti itakosa soko... Ndo maana anaendana na toleo la gazetini... Nahisi hivyo.
 
Hadithi ya kusisimuwa: Mimba ya jini-37-

ILIPOISHIA:
Walikumbatiana kila mmoja akirudisha furaha yake, baada ya utulivu wa muda Shehna alimuomba Mustafa atoke nje mara moja. Alimruhusu hakuchelewa alirudi baada ya dakika mbili akiwa na vinywaji mkononi. Aliiweka juu ya meza na kwenda kwenye friji ndogo na kutoa glasi mbili.
SASA ENDELEA...


Alimimina kinywaji kile kwenye glasi na kumpa Mustafa.
"Karibu mpenzi."
"Asante," Mustafa alisema huku akikipokea.
Alikunywa funda mbili na kumumunya midomo kisha alisema:
"Aaah! Mpenzi kinywaji kitamu sana umepata wapi?"
"Nilituma mtu nyumbani alete wakati nakuja kukuaga."
"Ni kitamu hakika sijawahi kukinywa toka nitoke tumboni kwa mama yangu."
"Utazidi kuvipata maadamu tuko pamoja utakula vitamu zaidi ya hiki. Hii chupa utakuwa ukichukua glasi moja kila siku. Mpaka narudi nitakuta hujamaliza."
"Shehna wewe ni mtu muhimu sana katika maisha yangu, nitakupenda, nitakutunza na kukuheshimu siku zote za maisha yangu."
"Mustafa mpenzi mimi si mkaaji, nilikuja kukujulisha habari za ujauzito wangu na kukuaga."
"Sawa mpenzi nimekuelewa nami nitafuata yote uliyonielekeza bila kufanya makosa."
"Nitafurahi, kumbuka nakupenda sana Mustafa."
"Najua."
"Naomba usinisaliti."
"Nakuahidi sitafanya hivyo labda nife."
Walikumbatiana kwa muda kila mtu aliyasikia mapigo ya moyo wa mwenzake kisha waliachiana na kusindikizana nje. Alipofika mapokezi Shehna alimuaga Sara.
"Shoga nikukimbieni."
"Jamani, lini utakuja kwangu tuongee?"
"Tutapanga."
"Haya shoga sisi tunaendelea na kazi."
"Ila zingatia yote tuliyozungumza ili uishi kwa amani."
"Nitafanya hivyo."
"Haya kwa heri."
"Haya shoga."
Mustafa alitoka na Shehna hadi nje, alishangaa kutoona usafiri wowote nje uliomleta, alijiuliza ataondokaje.
"Shehna unatumia usafiri gani?"
"Utanisindikiza mpaka njia panda kuna gari la nyumbani litanipitia."
"Sawa." Waliingia kwenye gari la Mustafa na kumpeleka mpaka sehemu aliyotaka na kumwambia.
"Niache hapa kuna gari litanipitia sasa hivi."
"Sawa."
Mustafa alisimamisha pembeni ya barabara kwenye mti wenye kivuli na kumwambia:
"Haya mpenzi nenda salama daima nitakukumbuka."
"Jamani Mustafa si mwezi tu."
"Kwa umpendaye siku moja mwaka."
"Najua, hata mimi nilipenda ujauzito huu niulee na wewe, lakini mila lazima nifanye tambiko bila hivyo naweza kupoteza wanangu."
"Haya mama naheshimu kwa vile ni kwa ajili yetu."
Waliagana kwa kukumbatia kwa muda kisha Shehna aliteremka kwenye gari na kwenda kusimama chini ya mti, Mustafa aliondoa gari kurudi ofisini. Siku ile Shehna hakutaka kuondoka kwa mtindo wake wa kutoweka ghafla, alihofia baada ya utata uliojitokeza kwa Mustafa ilibidi afanye vile ili wajue ni kiumbe cha kawaida wala si kama wanavyomdhania. Baada ya kumuona Mustafa ametoweka naye alitoweka ghafla na kurudi chini ya bahari.
***
Sara baada ya kumaliza kazi aliondoka kuelekea kwa mganga wake ili apate ukweli wa kitu kilichomsumbua. Ili kukwepa foleni alichukua bodaboda kuelekea kwa mganga Vingunguti kwa vile walitumia usafiri ule waliweza kukwepa foleni za barabarani na kutumia nusu saa kufika kwa mganga.
Kwa vile hakutaka dereva wa bodaboda ajue anakwenda wapi, aliteremka mbali kidogo na nyumba ya mganga ambayo ilikuwa vigumu mtu kujua mpaka aelekezwe. Alitembea hatua kama hamsini na kutokea uani kwa mganga, alikuta wateja zaidi ya nane waliokuwa chini ya mti, wanawake sita pamoja na yeye jumla wakawa saba na mwanaume mmoja alikaa kwenye benchi palipokuwa na nafasi.
Kwenye mkeka kulikuwa na wanawake watatu walikuwa wamejionyoosha na kuchukua nafasi kubwa. Baada ya kuketi na kuwasalimia kwa vile alikuwa mzoefu alitoa simu yake kwenye mkoba na kumtumia ujumbe mganga kumjulisha alikuwa nje.


Itaendelea Jumatatu jioni.....
 
Naona wengi wameamua wasisome mpaka ifike mwisho waisome yote.
 
Hadithi ya kusisimuwa: Mimba ya jini-38-

ILIPOISHIA:
Kwenye mkeka kulikuwa na wanawake watatu walikuwa wamejionyoosha na kuchukua nafasi kubwa. Baada ya kuketi na kuwasalimia kwa vile alikuwa mzoefu, alitoa simu yake kwenye mkoba na kumtumia ujumbe mganga kumjulisha yupo nje.
SASA ENDELEA...


Baada ya muda alitoka kijana mmoja mwenye umri isiozidi miaka 30 akiwa amevaa suruali ya jinsi na tisheti, ukimuangalia harakaharaka utajua brazameni.
Hakusema neno lolote, alimwita Sara kwa ishara ya mkono na kumwelekeza apite ndani.
Baada ya kuingia alikutana naye nje ya chumba cha uganga.
"Karibu."
"Asante, za siku?"
"Nzuri, umeadimika sana."
"Mambo mengi ustaadh wangu."
"Karibu ndani, maana nimefanya upendeleo."
"Najua ndiyo maana nikatuma ujumbe, niliogopa kupiga," Sara alisema huku akiingia ndani ya chumba cha mganga na kuketi kwenye mkeka.
"Mmh! Lete habari," mganga alisema.
"Habari nzuri, ile kazi ilikwenda vizuri yule bwana alirudi na alifanya kama ulivyosema, kwa sasa amekwenda nje kikazi, akirudi anakamilisha kila kitu."
"Sasa mbona hukurudi tumalize kazi?"
"Ndugu yangu kuna mambo yalinitokea ambayo sijawahi kutokewa toka nizaliwe."
"Mambo gani?"
Sara alianza kumueleza mauzauza yaliyokuwa yakimtokea kuanzia kupotea njia mpaka kuona nguruwe na sauti alizokuwa akisikia, pia wasiwasi wake kwa Shehna.
Mganga baada ya kumsikiliza alichukua kitabu cha uganga, karatasi na kalamu na kuandika vitu kwenye karatasi nyeupe kisha alifungua kitabu kuangalia alichoandika kilimaanisha nini kutokana na maelezo ya Sara.
Baada ya kusoma kwa muda alimuangalia Sara na kumuuliza swali;
"Unasema sauti ilisemaje?"
"Ilisema nisifuatilie mambo yasiyonihusu la sivyo nitageuzwa nguruwe kabisa."
"Kwa nini unafuatilia?"
"Kuna mambo yananitatiza."
"Ndiyo kuna kitu nimekiona hapa, inavyoonekana hakuna tatizo lolote zaidi ya kufuata maelekezo uliyopewa na ile sauti. Hutakiwi kupewa dawa yoyote zaidi ya kuisikiliza ile sauti. Kinyume cha vile mganga yoyote atakayejifanya anajua, moto utamuwakia."
"Kwa nini?"
"Hapana hakuna, tatizo unalo wewe kutaka kuingilia visivyo kuhusu achana nayo uwe salama, zaidi ya hapo utajuta kuzaliwa."
"Sasa utanisaidia vipi?"
"Msaada ni kuacha kufuatilia visivyokuhusu."
"Una maana ile hali haitatokea tena?"
"Ikutokee vipi nawe umeacha kufuata mambo yasiyokuhusu."
"Nitamjuaje anayenifanyia mchezo huo?"
"Sara kuwa muelewa, achana na mambo yasiyokuhusu, umjue ili iweje? Zaidi ya hapo sina msaada wowote wa kukusaidia."
"Hakuna kinga yoyote?"
"Kinga ya nini?"
"Inaweza kunitokea tena."
"Kama utayapuuza yale maneno na kujifanya unajua utageuzwa nguruwe na hakuna wa kukurudisha."
"Mmh! Sawa."
"Una lingine?"
"Kwa leo sina ila mwisho wa wiki nitakuja kwa ajili ya mambo yangu."
"Karibu sana."
Sara aliagana na mganga wake na kutokea mlango mwingine na kutoa nafasi kwa wateja wengine kupata huduma. Alitembea taratibu hadi kwenye kituo cha bodaboda na kukodi mpaka nyumbani kwake. Baada ya kufika kwake alikuwa mtu mwenye mawazo mengi kutokana na majibu ya mganga.
Alijiuliza kwa nini mganga alikataa kumsaidia, bado hakukata tamaa. Alipanga kwenda kwa mganga mwingine ili kupata ukweli aliamini kabisa mganga yule wa awali uwezo wake mdogo.
Kwa vile ilikuwa bado mapema, alichukua simu yake na kumpigia shoga yake anayeishi Kigogo.
Baada ya simu kuita kwa muda, ilipokelewa upande wa pili.
"Haloo Sara."
"Eeh! Mwaju za sahizi?"
"Nzuri, vipi shoga?"
"Eti mzee Gogo yupo?"
"Yupo, kwani vipi?'
"Nilikuwa nina shida naye."
"Kwa lini?"
"Leo hii."
"Mbona usiku?"
"Siwezi kulala mpaka nimuone kuna mambo yananitatiza."
"Mambo gani hayo ambayo lazima uende usiku huu."
Sara alimweleza sababu ya kutaka kuonana na mzee Gogo, baada ya kumsikiliza, alishusha pumzi na kusema:
"Mmh! Shoga una haki ya kwenda muda huu kwa mzee Gogo."
"Sasa tunafanyaje?"

"Nakusikiliza wewe."

Itaendelea wiki ijayo siku kama leo....
 
Hadithi ya kusisimuwa: Mimba ya jini-39-

Ilipoishia
“Mmh! Shoga una haki ya kwenda muda huu kwa mzee Gogo.”
“Sasa tunafanyaje?”
“Nakusikiliza wewe.”

Sasa endelea...

“Basi kodi Bajaj nipitie nitalipa.”
“Nipe dakika ishirini nitakuwa hapo jiandae nikifika tunaondoka.”
“Wala sina shida ya kujiandaa utanikuta nje nakusubiri.”
Sara hakutaka kuoga alichukua pochi yenye pesa na kutoka kumsubiri shoga yake, baada ya muda Mwajuma alifika na Bajaj ambapo Sara aliingia na kuelekea Tandale kwa mzee Gogo. Kwa vile walipitia njia za nyuma walikwepa foleni na kufanikiwa kufika kwa mzee huyo mapema.
Walikuta watu bado hawajaondoka, walikaa kwenye benchi kusuburi muda wa kuingia ndani. Wakiwa wamekaa kwenye benchi alitoka mzee wa makamo kichwa chote kilikuwa kimejaa mvi aliyekuwa amevaa fulana ya mikanda chini alijifunga kaniki. Kwa vile alikuwa amezoeana na Mwaju alipomuona alishtuka na kumuuliza.
“Vipi tena mama, mbona usiku?”
“Shida tu mzee wangu.”
“Karibu hapa ndiyo kwa mzee Gogo asiyeshindwa na kitu.”
“Asante, vipi tutapata upendeleo?”
“Nipe dakika kumi nitakuiteni.”
Mzee Gogo alikwenda kwenye mti uliokuwa pale uani na kuchukua vitu kisha alirudi ndani kuendelea na kazi. Baada ya muda alitumwa mtu kwenda kuwaita, waliingia ndani na kukaa kwenye mkeka.
“Karibuni.”
“Asante.”
Mzee Gogo alitulia kwa muda akipanga vizuri dawa zake kisha alinyanyua macho na kusema:
“Mmh! Mabinti mna tatizo gani?”
“Shoga yangu ndiye mwenye tatizo.”
“Eti mama una tatizo gani?” alimgeukia Sara.
Sara alimueleza mikasa iliyomkuta na jinsi mganga aliyekwenda jioni ile kukataa kumtibu. Baada ya kumsikiliza alichukua kikopo kilichokuwa na unga mweupe ambapo alichota kidogo na kuumwaga mbele yake na kutulia kama anatazama kitu. Alitulia akikaza macho kwenye unga ule kisha alisema:
“Ni kweli kabisa ni jini.”
“Nani?”
“Huyu mpenzi wa bosi wako.”
“Mungu wangu una maanisha Shehna?”
“Ndiyo.”
“Sasa tutafanyaje?”
“Wewe unataka tumfanyeje?”
“Tumpoteze kabisa.”
“Kumpoteza itakuwa vigumu kwa vile tayari amekuwa mpenzi wa bosi wako.”
“Na ndiye aliyenitesa vile?”
“Ndiyo.”
“Tumfanyeje ili kuvunja penzi na bosi wangu pia asinifuatefuate?”
“Kuvunja urafiki ni vigumu kwa vile tayari ana ujauzito wa bosi wako.”
“Sasa tutafanya nini?”
“Labda kumuua tu.”
“Sawa.”
Baada ya kusema vile alichukua chupa ndogo na bakuli dogo na kumimina maji yake kisha alizungumza maneno ambayo hawakuyaelewa. Ghafla mganga alinyamaza na kuanza kung’ata maneno mara mtetemeko mkubwa ulitokea ndani ya chumba cha uganga lakini nje hakuna aliyejua nini kinaendelea.
Wakiwa wameingiwa na wasiwasi walishtuka kumuona mganga akijishika mikono shingoni kama anamzuia mtu asimkabe na kuliacha bakuli likianguka chini na kumwaga maji.
Sara na shoga yake walishtuka kumuona mganga akihangaika kama anapigana na mtu aliyeonekana kumkaba shingoni ambaye hawakumuona. Mara walimuona akianguka kama mzigo huku mikono yake ikiwa bado shingoni na kuanza kurusha miguu na kufanya dawa zilizokuwa pembeni yake kutawanyika ovyo.
Walinyanyuka walipokuwa wamekaa kwa woga, mganga aliendelea kurusha miguu kama kuku aliyekatwa kichwa kisha alitulia. Baada ya kutulia waliogopa kumsogelea na kutoka nje kumwita msaidizi wake. Aliingia na kwenda alipokuwa amelala mzee Gogo. Walimkuta macho na ulimi vimemtoka nje akiwa amekufa.
Sara na shoga yake waliona msala utawageukia walitoka taratibu bila kuaga na kurudi nyumbani. Njia nzima Sara alijiuliza maswali na kukumbuka maneno ya mganga wa Vingunguti aliyemweleza kuwa mganga yeyote atakayetaka kuingilia kesi ile lazima moto umuwakie. Alipofika kwake aliteremka na kumuacha shoga yake akirudi nyumbani kwake Kigogo.

Itaendelea
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom