NYEMO CHILONGANI.
UCHAWI WA BILIONEA BAZOKA
0718069269
Sehemu ya 17.
Bi. Semeni alihisi kuchanganyikiwa kupita kawaida, hakuamini kama kweli kile alichokuwa akikiangalia kilikuwa gogo na si mwili wa Bazoka, hakujua ni kitu gani hasa kilikuwa kimetokea.
Akalisogelea na kuliangalia vizuri, ni kweli lilikuwa gogo, sasa nini kilitokea mpaka kuwa hivyo? Alijifahamu kwamba yeye ni mchawi mkubwa, mwenye nguvu, hapakuwa na mtu aliyekuwa akimbabaisha, sasa kwa nini ionekane alibeba gogo? Ni wale watu aliokutana nao ndiyo waliokuwa na nguvu za kumbadilisha Bazoka na kuwa gogo ama Bazoka mwenyewe ndiye aliyekuwa na nguvu hizo?
“Hapana! Huyu mtupu kabisa!” alijijibu baada ya kujiuliza kama kulikuwa na uwezekano wa Bazoka kuwa na nguvu hizo.
Alimfahamu Bazoka, hakuwa mgeni na hiyo haikuwa mara ya kwanza kumuwangia, hakuwa na nguvu zozote zile, alikuwa mtupu kama ndoo isiyokuwa na maji. Kitendo cha kujiambia kwamba inawezekana alikuwa na nguvu kilikuwa ni kosa kwa kuwa kwa macho yake aliwahi kumuwangia usiku kucha.
Alikaa na hao watu, hakuweza kuondoka, uchawi wake uliharibiwa vibaya hivyo walichokifanya watu wale ni kumpa nguvu nyingine za kuweza kupaa na kuondoka naye hapo, ila sharti lilikuwa moja tu, amuache fisi wake hapo.
“Kwa sababu gani?” aliwauliza.
“Ndiyo malipo kwetu! Au unataka tukuache hapahapa?” aliuliza mwanaume mmoja huku akimwangalia.
Kuondoka mahali hapo lilikuwa jambo jema kabisa, hakutaka kubaki mahali hapo, ilikuwa ni lazima kuondoka, hiyo ndiyo ingekuwa salama yake, akakubaliana nao, akapewa nguvu, akasimama imara na ghafla akapotea na kuibukia chumbani kwake.
Alikuwa amechoka mno, akatoka chumbani harakaharaka na kuelekea bafuni. Siku hiyo alichanganyikiwa na hakuwa na gamu ya kuendelea kuloga kama siku nyingine, ilikuwa ni lazima apate kujua ni kitu gani hasa kilitokea mpaka kwa Bazoka kuonekana gogo.
Alipomaliza kuoga, haraka sana akakimbilia ukumbini, akaufuata mlango wa Bazoka na kuanza kusikiliza ndani kuhisi kama kulikuwa na kitu ama la, alichokisikia ni mwanaume huyo kukoroma, yaani alikuwa kwenye usingizi mzito mno.
“Mh! Sasa imekuwaje?” alijiuliza.
Akarudi chumbani kwake, siku hiyo hakulala, alibaki akiwa anajiuliza ni kitu gani hasa kilichokuwa kimetokea, ilipofika majira ya saa moja asubuhi, akasikia mlango wa Bazoka ukifunguliwa, na harakaharaka naye akatoka, wakakutana ukumbini, wakaangaliana.
“Shikamoo mama!” alimsalimia huku akiwa na tabasamu.
“Marahaba! Hujambo mtoto wangu!’ naye alimsalimia.
“Sijambo tu mama! Mimi nakwenda kazini!” alimwambia.
“Sawa!” aliitikia, Bazoka akatoka na kuondoka zake.
Bi. Semeni alikuwa akimsindikiza kwa macho, alimuona kwa namna alivyokuwa akiondoka, alionekana kuwa mtu mwenye furaha kupita kawaida, hilo hakutaka kuliona, kama mchawi, furaha yake ilikuwa ni kuwaona watu wakiteseka, wakihuzunika na kulia usiku kucha.
Kwa Bazoka kuwa na furaha vile, tena ndani ya nyumba yake lilionekana kuwa kosa kubwa, yaani alijiona ni kama mtu ambaye hakuwa akiifanya kazi yake vilivyo, ilikuwa ni lazima afanye kila liwezekanalo kuhakikisha mwanaume huyo anakuwa na huzuni na maisha ya hovyo kama alivyokuwa akiwafanyia wengine.
Kwa kuwa alikuwa na unguo mwingine wa chumba cha Bazoka, akauchukua na kuufuata mlango, akaufungua na kuingia ndani. Alihitaji kujua kuhusu mwanaume huyo, alikuwa na vitu gani ambavyo vilimpa shida na kujikuta akiwa amebeba gogo badala ya kumbeba yeye mwenyewe.
Akaufungua na kuingia ndani, akaanza kuangalia huku na kule, hapakuwa na kitu chochote kile, akalifungua kabati na kuangalia ndani, alichokutana nacho ni nguo tu na vitu vingine vya kawaida.
Akalitoa godoro, chini ya uvungu wa kitanda hapakuwa na kitu chochote kile. Akili yake ilimwambia inawezekana humo ndani kulikuwa na kitu hivyo akaendelea kuangalia zaidi kuona kulikuwa na nini.
“Kutakuwa na kitu humu!” alijisemea, akili yake ikamwambia tena akaangalie kwenye kabati, haraka sana akalifuata na kuangalia ndani, alikutana na nguo zilezile ila alipolifunga kabati na kugeuka nyuma, alipigwa na mshtuko baada ya kuona hakuwa tena chumbani kwa Bazoka.
“Eeh!” alishangaa.
Alikuwa katika jangwa moja kubwa, lililokuwa na mchanga mwingi kama Sahara, alibaki akiashangaa ni kwa namna gani alifika mahali pale, jua lilikuwa kali, aliangalia huku na kule, alikuwa akiweweseka, hakujua ni kwa namna gani alifika mahali pale.
Aliyafikicha macho yake, wakati mwingine alihisi kama alikuwa akiota, kile alichokuwa akikiona hakika hakukitarajia hata kidogo. Akaanza kupiga kelele kuhitaji msaada, hapakuwa na mtu aliyemsikia, alikuwa jangwani na hakujua ni kwa namna gani angeweza kutoka mahali hapo.
Huku akiwa hajui ni kitu gani alitakiwa kufanya na jua kali likimchoma, akaanza kusikia sauti za watu kutoka mbali kabisa, hakuwa akiwaona ila alikuwa na uhakika walikuwa wakija kule alipokuwa.
Aliogopa, hakujua ni kwa namna gani angeweza kutoka mahali hapo, huku akiwa ametulia tu, akawaona watu watatu wakija kule alipokuwa, walikuwa Waarabu waliokuwa juu ya ngamia zao, walivaa vilemba na walionekana kuwa na furaha tele.
Baada ya macho yao kutua kwa Bi. Semeni, wote watatu wakapigwa na mshangao, ilikuwa ni ajabu kumuona mtu mahali hapo, kwa sehemu ya jangwani kama hiyo, hawakujua alifikaje mahali hapo, na kwa jinsi alivyovaa, alikuwa kama mtu ambaye hakujiandaa kuwa hapo.
“Wewe nani?” aliuliza mwanaume mmoja, aliuliza kwa Kiarabu lakini kitu cha ajabu kabisa, Bi. Semeni aliweza kumuelewa kwa kila neno.
“Nani? Mimi?” aliuliza huku akionekana kuogopa.
“Ndiyo! Wewe! Umefikaje hapa?” aliuliza mwanaume huyo.
“Sijui! Nimejikuta tu mahali hapa, naomba mnisaidie nirudi nyumbani,” alisema, wanaume wale wakaangaliana na kuanza kucheka.
“Sasa tutakusaidiaje?” aliuliza mwingine.
“Nimejikuta nipo hapa!”
“Umefikaje? Yaani umejikuta upo hapa tu?”
“Ndiyo!”
“Ulikuwa unafanya nini mpaka umejikuta ukiwa hapa?” aliuliza mwanaume wa tatu.
Hakujibu swali hilo, akanyamaza na kuangalia chini, alijisikia aibu kubwa mno na alishindwa kujua ni kwa namna gani angeweza kulijibu swali hilo. Kuwaambia kwamba alikuwa akiloga lilikuwa jambo gumu mno, hivyo alikuwa akifikiria uongo mwingine.
“Naomba mnisaidie,” alisema bila kulijibu swali hilo.
“Unajua upo wapi hapa?”
“Hapana!”
“Upo Misri! Na ndiyo maana tunajiuliza umefikaje!” alisema mwanaume wa kwanza.
“Au ulikwenda kumloga mtu mwenye nguvu zaidi yako?” aliuliza mwanaume wa pili.
Swali hilo ndilo ambalo lilimshtua kidogo Bi. Semeni, akayainua macho yake na kuwaangalia watu hao, sasa akaanza kuhisi kitu cha tofauti kabisa. Mwili wake ukaanza kumsisimka kupita kawaida, vinywele vikaanza kumsimama huku kijasho chembamba kikianza kumtoka, tena mfululizo.
“Unasema?”
“Angalia na watu wa kuwaloga, kuna siku utakuja kupoteza maisha!” alisema mwanaume wa pili, wote watatu wakatoa vicheko vikubwa, Bi. Semeni hakujua ni kitu gani kilichotokea lakini alimuona ngamia mmoja kwa kutumia mguu wake wenye kwato akiuinua kidogo, akauchota mchanga na kummwagia usoni, mchanga ukampiga, akayafumba macho yake kujizuia, alipoyafumbua, akajikuta akiwa chumbani kwa Bazoka.
“Mamaaaaaa....nakufaaaaa...” alipiga ukunga, haraka sana huku akionekana kuchanganyikiwa, akatoka ndani ya chumba kile, akaufungua mlango, alikuwa akitetemeka, hofu nzito iliutawala moyo wake, hakuamini kile kilichokuwa kimetokea kilimtokea.
Akakimbilia chumbani kwake, alikuwa akitetemeka kwa hofu, yaani mchawi nguli kama yeye, aliyebobea kwenye mambo ya uchawi, leo alikuwa na hofu, moyo wake ulikuwa ukiogopa kupita kawaida.
Akapanda kitandani na kukaa kwenye pembe, akajikunyata kwa kukunja miguu yake na kuanza kulia huku mapigo yake ya moyo yakidunda kwa nguvu.
“Mama nakufaaaa...mama nakufaaa...” alisema mfulilizo huku akilia.
***
Maganza hakuamini alichokuwa amekisikia kutoka kwa mkewe, alimwangalia kwa mtazamo wa kutaka kusikia tena na tena kile alichomwambia. Alisema kuwa alilala mpaka saa sita, haikuw akawaida yake lakini suala la kulala na kile kilichotokea vilikuwa vitu viwili tofauti kabisa.
Alikumbuka vilivyo alikuwa kwenye mji wa ajabu, mzuri kwa macho lakini kulikuwa na viumbe wa ajabu, waliokuwa na muonekano wa kutisha mno, waliwambia kulikuwa na mambo mengine hakutakiwa kabisa kuyafuatalia.
Alijiuliza mambo gani hayo? Kulikuwa na mambo mengi mno lakini mengine hakutakiwa kuyafuatilia hata kidogo. Kipindi hicho hakuw ana jambo jingine la kufuatilia zaidi la suala la mtoto Yusufu ambaye alitekwa na hakujua alikuwa mahali gani.
“Ni kuhusu yule mtoto?” alijiuliza.
“Unasemaje?” aliuliza mkewe, alimsikia mumewe akiwa ameongea jambo fulani.
“Hebu twende nyumbani!” alimwambia.
“Lakini unaumwa!”
“Hapana! Siumwi,’ alisema Maganza huku akitoa sindano ya dripu iliyokuwa kwenye mshipa wake.
Hakutaka kubaki hospitalini hapo, ilikuwa ni lazima kuondoka na kurudi nyumbani kwake. Alishangaa kuona moyo wake ukiwa na hamu kubwa ya kutaka kufahamu zaidi kuhusu mtoto Yusufu, ilikuwa ni lazima aujue ukweli wa kile kilichokuwa kimetokea.
Daktari alijaribu kumzuia lakini alishindwa, ilikuwa ni lazima kuondoka na kwenda kumaliza kazi aliyokuwa ameianza. Mkewe alikuwa akimshangaa njia nzima, mumewe alionekana kuchanganyikiwa, alionekana kuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea, ila hakutaka kumwambia.
Alijaribu kumuuliza maswali mengi lakini hakujibu zaidi ya kung’ang’ania warudi nyumbani kwanza, wakafanya hivyo. Walipofika, akaingia bafuni, akaanza kuoga na kuendelea kufikiria kilichokuwa kimetokea.
Hakika kilimtisha mno, wakati mwingine alihisi kama alikuwa akiota lakini cha ajabu mambo yalikuwa yakitokea kabisa kwenye ulimwengu halisi. Akiwa humo, akasikia simu yake ikiita, akamwambia mkewe aipokee.
“Ipokee tu! Ni nani?” alimuuliza.
“Kamanda Kizota!” alijibu.
Haraka sana akatoka na kuifuata simu aliyokuwanayo mkewe, akaichukua na kuipokea, alichokisikia ni sauti ya kamanda wake, Kizota akimwambia kulikuwa na jambo kubwa limetokea ofisini hivyo alitakiwa kwenda haraka sana.
“Jambo gani?”
“Juu ya uchunguzi uliokuwa unaufanya!”
“Wa mtoto albino?”
“Ndiyo!”
“Imekuwaje?”
“Njoo haraka ofisini,” alisema kamanda huyo na kukata simu. Maganza akaanza kuvaa harakaharaka ili awahi huko kazini kuona ni kitu gani hasa kilikuwa kimetokea.
Je, nini kitaendelea?