NYEMO CHILONGANI
UCHAWI WA BILIONEA BAZOKA
0718069269
Sehemu ya 34
Asha alitulia na kumsikiliza mume wake alivyokuwa akisimulia kila kitu kilichotokea. Hakuamini kama mume wake alifanya mambo hayo yote na kitu pekee alichokijua ni juhudi zake za kupambana na umasikini kumbe kulikuwa na mengi yaliyotokea.
Moyo wake ulimchoma sana baada ya kusikia alihusika katika vifo vya marafiki zake wawili, Sultani na Bonge. Aliwakumbuka watu hao, walikuwa marafiki wakubwa na mume wake lakini kumbe nyuma ya pazia mwanaume huyo aliamua kuwatoa kafara.
Ukiachana na hilo pia aliumizwa na kifo cha Yusufu, hakuamini kama mume wake aliingiwa na roho ya mauajia na kuamua kuyafanya mauaji hayo, ya mtoto mdogo, akaanza kuwafikiria wazazi wake walikuwa wakijisikiaje muda huo.
Asha alibubujikwa na machozi, yalianza kutiririka mashavuni mwake. Kwa mara ya kwanza aligundua alikuwa akiishi na mwanaume katili ila hakuwa akijua.
Hiyo haikuwa sababu ya kumuacha Bazoka, alikuwa mume wake, alikuwa na wajibu wa kupambana naye kwenye shida na raha japokuwa alifanya mauaji makubwa kwa ajili ya kupata pesa.
“Sasa kwa nini wameamua kukufanya hivi?” aliuliza mke wake huku akimwangalia.
“Ni kwa sababu nilikataa kumuua Edward!” alimjibu.
“Walikwambia umuue Edward?” aliuliza kwa mshtuko.
“Ndiyo! Nilikataa na ndiyo mwanzo wa haya yote!” alimwambia.
Asha akashusha pumzi ndefu, hakuamini alichokisikia, pamoja na ukatili wote wa mume wake ila aliamua kutokumuua mtoto wake kwa kuwa alikuwa na mapenzi ya dhati. Hapo alimsifia, ule ukatili aliokuwa akiuona machoni mwake ukatoweka na kumuona alifanya uamuzi wa kishujaa kabisa.
“Nashukuru kwa kutochukua uamuzi wa kumuua Edward,” alisema mke wake.
“Hiyo ni damu yangu. Nipo radhi nife ama nipate tatizo lolote lakini si kumuona akifa,” alisema.
Walikaa na kuzungumza sana, baada ya dakika kadhaa, mlango ukaanza kugongwa, mfanyakazi akaufungua na macho yake kutua kwa Maganza aliyekuwa amefika mahali hapo kwa kuongozwa na kijiti kile alichopewa.
Akakaribishwa na kutulia sebuleni, alikuwa akitokwa na kijasho chembamba, kile alichoambiwa na mzee yule ambaye hakujua kama alikuwa jini kilimtisha mno na kumuona Bazoka hakuwa mtu wa kawaida hata kidogo.
Baada ya dakika kadhaa, Asha na mume wake, Bazoka wakatokea sebuleni hapo, Bazoka alitulia kwenye kiti chake cha matairi huku mke wake akimsukuma. Macho ya Maganza yalipotua kwa Bazoka, akahisi moyo wake ukiiingiwa na hofu nzito, tayari alianza kumuogopa Bazoka.
Wakasalimia, alimwangalia mwanaume huyo, alishangaa, ilikuwaje awe kwenye kiti cha matairi na wakati siku chache alizoongea naye alikuwa mzima wa afya.
“Imekuwaje?” aliuliza.
“Ni habari ndefu sana!” alijibu.
“Habari ipi?”
Bazoka akaanza kumwambia kilichotokea, jinsi alivyopigiwa simu na kuambiwa kiwanda chake kilikuwa kikiteketea kwa moto na kwenda huko ambapo alipata kile alichokuwa akikiona, mwili wake ulipooza.
Japokuwa Maganza alifika mahali hapo kwa lengo la kuongea na Bazoka, amlaumu na ikiwezekana amfunge pingu lakini alishindwa kufanya hivyo kutokana na muonekano aliokuwanao mwanaume huyo.
Kumfunga pingu halikuwa tatizo lakini endapo angemfikisha mahakamani, angesema kitu gani kuhusu yale yaliyokuwa yametokea, aliyoyafanya Bazoka.
Serikali haikuamini uchawi, kama unasema Yusufu na Bi. Semeni waliuliwa na Bazoka ilikuwa ni lazima kuwa na ushahidi, je, yeye kama mpelelezi alikuwa na ushahidi gani? Yule mzee? Naye angeulizwa amejuaje? Ushahidi wake uko wapi?
“Nimejua kila kitu ulichokifanya Bazoka,” alimwambia.
“Umejuaje?”
“Kuna mzee alinifuata na kuniambia kila kitu,” alijibu.
“Mzee gani?”
“Wala simfahamu!”
“Alikwambiaje?”
Akaanza kumwambia kila kitu alichoambiwa, Bazoka na mkewe walikaa kimya wakimsikiliza, kile alichoambiwa kilikuwa kilekile kilichokuwa kimetokea, kwa kuwa huyo mzee alijua kila kitu, akamwambia hakuwa binadamu, inawezekana alikuwa jini kwani hata naye alifuatwa na mtu huyo akiwa na muonekano kama wake.
Maganza aliposikia hivyo, akaanza kuogopa, aliyaogopa majini kutokana na stori alizokuwa akizisikia lakini pia zile njozi za kutisha alizokuwa akiziota na hata lile tukio lililotokea mpaka kupelekwa hospitalini.
Alitetemeka mno. Hofu ikamjaa na kumuomba Mungu asirudiwe na lile jini kwani halikuonekana kuwa la kawaida, lilikuwa na mambo mengi maovu, kisirani na kumwaga damu za watu, na hilo ndilo lililomuweka Bazoka kitandani hapo.
“Bazoka......”
“Fanya lolote mkuu!”
“Siwezi kufanya lolote lile. Nitakuachia umalizane na jini lako! Sina ushahidi wa hayo uliyoyafanya,” alimwambia.
Walizungumza kidogo na Maganza kusimama na kuaga, akaanza kuondoka nyumbani hapo huku akimshukuru Mungu kwa kile kilichotokea, japokuwa kesi ilimsumbua sana lakini mwisho wa siku alikuja kuufahamu ukweli wa kile kilichotokea.
Huko nyuma Bazoka alizidi kuugua, kila siku mwili wake ulikuwa ukipungua, kuugua kwake ilikuwa ni tofauti na wagonjwa wengine waliokuwa wamepooza, kwake mambo yalikuwa yakibadilika kwa haraka sana.
Kwa siku saba tu tayari alikuwa amekonda mno na mgongo wake ulikuwa na mapele makubwa yaliyopelekea kutoa usaha mwingi, kidonda chake cha mguuni kiliongezeka ukubwa na kuanza kutoa funza.
Japokuwa aliambiwa waende hospitalini Bazoka alikataa, alifanya hivyo kwa kuwa alijua kusingekuwa na tiba yoyote ile ambayo ingemfanya kupona na kurudi kwenye hali ya kawaida.
Aliteseka kitandani kwa muda wa mwezi mmoja tu na baada ya hapo akahisi kabisa siku zake zilikuwa zimefika na muda wowote ule angefariki dunia hivyo alichokifanya ni kumuita mke wake na kuzungumza naye maneno ya mwisho.
Alimwambia kuhusu biashara zao, apambane kuhakikisha utajiri huo hauondoki mikononi mwake, amtunze mtoto wake na hata kama kuna siku angekuja kuolewa basi aolewe na mwanaume aliyekuwa na kiu ya kutaka kufika zaidi ya pale walipokuwa.
“Si watauchukua utajiri wao!” alisema Asha.
“Hawawezi! Endapo nisingepata matatizo haya basi wangeuchukua, ila kwa sababu wameniadhibu, hawawezi kuuchukua,” alimwambia.
Asha akanyamaza na kuanza kulia, hakuwa na hamu ya utajiri, mume wake alikuwa mtu muhimu sana kwa kipindi hicho kuliko kitu chochote kile.
Aliacha kufanya kila kitu, akawa anashinda naye tu chumbani hapo huku akiwa pembeni kitandani hapo. Siku zilikatika na baada ya wiki moja kupita, hatimaye Bazoka akafariki akiwa kitandani pale huku akiwa ametubu dhambi zake zote, maovu aliyoyafanya, alifariki huku uso wake ukiwa na tabasamu pana.
Kila kitu alichokuwa amekipata kilibaki kwa mke wake, pesa zake zilishindwa kuokoa maisha yake, alifariki huku akiwa na heshima kubwa lakini siri ya utajiri wake wakawa wanaijua watu watatu tu, mke wake na mpelelezi Maganza aliyekuwa ameambiwa kila kitu.
Kwenye msiba wake watu walijaa, viongozi wa nchi, watu walikula na kusaza na mwisho kabisa mwili wake ukaenda kupumzishwa kwenye makaburi ya Kinondoni huku kwa juu kukiandikwa mwaka wake wa kuzaliwa na kufariki dunia.
Kila kitu kibaki kwa mke wake, yeye ndiye aliyekuwa msimamizi wa mali zake, pesa na mambo mengine. Alifanya kazi kwa juhudi, alipambana mno kwa ajili ya kuubakiza utajiri wa mume wake kitu ambacho alifanikiwa sana.
***
Maganza alitulia ofisini kwake, mezani kwake kulikuwa na faili la Bazoka, jinsi alivyoanza kufuatilia kesi hiyo mpaka alipoishia, mwisho kabisa alilifunga faili hilo kwa kumaanisha sasa alimalizana na Bazoka.
Alikaa kwa dakika kadhaa, akasimama na kuanza kuelekea ofisini kwa mkuu wake, Masumbuko, alipofika huko akaanza kuzungumza naye. Alimwambia jinsi alivyofanikisha kesi ya Bazoka, mwanaume huyo ndiye aliyehusika kwenye mauaji yale yaliyotokea.
“Umejuaje?”
Alimwambia kila kitu, Masumbuko alibaki kimya, kile alichoambiwa hakukiamini, kilikuwa kama simulizi fulani ya kusisimua iliyokuwa ikiandikwa na mwandishi, Juma Hiza.
“Kwa hiyo ule utajiri ni wa uchawi?” aliuliza Masumbuko, macho yaliyomtoka.
“Yaani acha tu! Mpaka nilisisimka.”
“Tena umenikumbusha!” alisema Masumbuko.
Akasimama na kuisogelea kabati yake ya mafaili na kupekua humo, akakutana na faili moja, akalichukua na kukakaa kwenye kiti, akaliweka mbele ya Maganza na kuanza kumwambia kuhusu faili hilo.
“Nilikupa kazi ya kufuatilia mauaji yale kwa kuwa nilijua utaweza kugundua ni nani alikuwa akihusika, mwisho wa siku umenipa furaha baada ya kugundua kila kitu. Bazoka amekufa, hilo linamaanisha kila kitu kimemalizika,” alimwambia.
“Sawa kabisa mkuu!”
“Umewahi kusikia kuhusu mauaji yanayoendelea kutokea kwa wanaume hapa Dar es Salaam?” aliuliza.
“Ndiyo! Ni kama mara mbili hivi nimesikia!” alijibu.
“Inawezekana! Ila mauaji yaliyotokea ni ya watu watatu! Kila mwanaume anayekufa, mwili wake ukauka na kuwa mgumu kama jiwe,” alimwambia.
“Kwa sababu gani?”
“Kuna mwanamke anawaua watu hao!”
“Mwanamke? Mwanamke gani?”
“Hakuna ajuaye, ila kwa mauaji anayoyafanya, ametungwa jina na kuitwa Medusa,” alimwambia.
“Medusa?”
“Ndiyo! Medusa: Malkia wa Damu,” alimwambia.
“Mnamjua Medusa lakini?”
“Yeah! Anajulikana, stori zake zimeandikwa sana, yule mwanamke wa Kigiriki, nywele zake zilikuwa nyoka, kila alipokuangalia unakakamaa na kuwa jiwe. Nadhani hiyo ndiyo sababu inayowafanya watu kumuita hata huyu muuaji ni Medusa,” alimwambia kwa kirefu.
“Mmejuaje kama ni yeye ndiye anayefanya mauaji haya?” aliuliza.
“Kutoka kwa marafiki wa marehemu, kila mmoja anasema marehemu aliondoka na mwanamke mzuri kweli, halafu kesho yake wakawakuta wakiwa wamekufa kwa kukakamaa. Ninachokitaka kutoka kwako ni kufanya upelelezi na kumbaini huyu mwanamke ni nani!” alimwambia.
“Sawa haina shida.”
“Utatakiwa kuwa makini sana! Inawezekana mwanamke huyu ni jini,” alimwambia.
“Jini?”
“Inawezekana! Hatuna uhakika. Ama inawezekana baada ya kuwaua huwa anawachoma sindano na kuwafanya kukakamaa kama walivyokutwa!” alimwambia.
“Hilo linawezekana! Ila swali langu moja, kwa nini anawaua wanaume hao?” aliuliza.
“Hata mimi sijui! Ila baada ya kumkamata nadhani tutajua kwa sababu gani anawamaliza wanaume hao,” alimwambia.
“Mh! Sawa haina shida, faili lake ndilo hili?”
“Yeah! Lichukue, utafuatilia na kujua ni wapi unatakiwa kuanza napo,” alimwambia.
“Sawa mkuu!”
Maganza akasimama na kuondoka ofisini humo huku akiwa na faili hilo. Moyo wake ulikuwa na shauku ya kutaka kufahamu mauaji hayo, alipewa kazi hiyo ngumu kwa sababu tu aliaminika.
Kulikuwa na maswali mawili aliyokuwa akijiuliza, je, muuaji huyo alikuwa jini ama alikuwa akiwachoma watu hao kwa sindano na kuwafanya kukakamaa kama walivyokuwa wakikikutwa?
Hakuwa na majibu ila aliamini baada ya kuanza kufuatulia basi angepata majibu ya maswali yake hayo. Alipofika ofisini kwake, akaliweka faili lile mezani na yeye kukaa kwenye kiti, akaanza kuliangalia.
Lilikuwa faili la kesi iliyomfanya kuwa na hamu sana kuifuatilia. Juu ya faili lile kuliandikwa:
MEDUSA: MALKIA WA DAMU.
Maganza akatabasamu.
“Ni kesi nzuri sana. Nitaanza nayo hii,” alijisemea.
Tabasamu pana likautawala uso wake.
Baada ya kumalizana na Bazoka, sasa alitakiwa kuanza safari nyingine ya mwanamke aitwaye Medusa. Hakuwa akimfahamu lakini kwa sababu alikuwa mpelelezi ilikuwa ni lazima kuhakikisha anamfahamu mwanamke huyo, anamkamata na kumfikisha kwenye vyombo vya sheria.
“Zamu yako imefika Medusa. Jiandae,” alisema na kulifunga faili lile.
MWISHO.
Tukutane kwenye Simulizi ya MEDUSA: MALKIA WA DAMU kule Facebook na Instagram.
Sent from my SM-A107F using
JamiiForums mobile app