NYEMO CHILONGANI
UCHAWI WA BILIONEA BAZOKA
0718069269
SEHEMU YA 29.
Bazoka alitulia ofisini kwake huku moyo wake ukiwa kwenye hofu tele, aliogopa, hakuamini kama kweli alisababisha Sultani kufariki na wakati tangu siku ya kwanza ambayo alionana naye alionekana kuwa mtu mzuri na aliyempenda sana.
Moyo wake ukaanza kumlaumu kwa kile kilichotokea, wakati mwingine alitamani hata kuadhibiwa kwani kwa mtu kama yeye, hasa kwa kile alichokifanya hakustahili kabisa kupokea sifa za kuwa mtu bora ama mwenye huruma.
Alihitaji kutubu, alikumbuka dhahiri alisaini mkataba wa kifo kwa watu wawili, mmoja alikuwa Sultani ambaye tayari alifariki dunia akiwa chumbani kwake na mwingine alikuwa Bonge. Kwa kuwa huyo wa pili ndiye alikuwa akifuata, alitaka kumfuata na kumtahadhalisha kuwa alitakiwa kuwa makini sana.
Mbali na hivyo alihitaji kumwambia kwamba yeye ndiye aliyesababisha kifo cha Sultani kwa kuwa alitokewa na jini aliyekuwa na muonekano kama wake na kumtaka kufanya kile alichokifanya.
Hakuwa na jinsi, ilikuwa ni lazima akatubu, moyo wake haukuwa na amani hata kidogo, ili urudi na kuwa na amani tele ilikuwa ni lazima kufanya kama kile alichotaka kufanya.
Haraka sana akachukua simu yake na kutaka kumpigia Bonge, alifikiria kutubu kwenye simu lakini pia akaona hilo ni tatizo, kwa ishu siriazi kama hiyo alitakiwa kuondoka na kumfuata ofisini kwake, huko wangezungumza zaidi na kumwambia kilichokuwa kimetokea.
Akatoka ofisini kwake, akaingia ndani ya gari na kuondoka mahali hapo. Njiani mawazo tele yalikisumbua kichwa chake, alikuwa na majuto tele na ilikuwa ni lazima kufanya kile alichotaka kufanya kwa kuwa aliamini angekuwa na amani tele.
Hakuchukua dakika nyingi akafika ofisini kwa Bonge, akamuuliza sekretari ambaye alimwambia alikuwa na mgeni lakini hapakuwa na hofu, alimpigia simu na kumwambia juu ya uwepo wake mahali hapo.
Akamruhusu kuingia, akaingia ndani. Macho ya Bazoka yakatua kwa mgeni aliyekuwa amekaa kwenye kiti, alimtupia macho mgeni huyo, hakumjua, na hakuwahi kumuona hata siku moja machoni mwake.
Huyo alikuwa Shunie, baada ya Bazoka kuingia, muonekano wake ukabadilika, hakuwa yule Shunie aliyekuwa akimfahamu, alikuwa mwanamke mwingine kabisa ila kwa macho ya Bonge alionekana kuwa Shunie yuleyule.
“Karibu sana Bazoka,” alimkaribisha, Bazoka akakaa kwenye kiti kingine.
“Nashukuru sana. Naona umepata mgeni,” alimwambia.
“Yeah! Huyu anaitwa Shani,” alimwambia. Alilitaja jina la Shunie lakini masikioni mwa Bazoka lilisikika kama Shani, hiyo yote ilikuwa ni nguvu ya kijini ya mwanamke huyo.
“Oh! Nashukuru kumfahamu. Mimi naitwa Bazoka,” alimwambia.
“Nimefurahi kukufahamu!” alisema Shunie huku akijifanya kuwa na aibu kubwa.
Bazoka alikuwa na jambo lake moyoni, alihitaji kuzungumza na Bonge lakini kwa uwepo wa msichana yule asingeweza kuzungumza naye lolote lile. Mazungumzo hayo yalihitaji kuwa ya watu wawili tu.
Kwa sababu Bonge alikuwa na mgeni, akamwambia angerudi baadaye kwani alikuwa na mazungumzo naye nyeti, hilo halikuwa tatizo, akaondoka, akamuaga sekretari lakini alimwambia angerudi muda si mrefu.
Hakurudi ofisini kwake, alikwenda kwenye mgahawa uliokuwa karibu na ofisi hiyo na kutulia, moyo wake ulikuwa na shauku kubwa ya kumwambia Bonge kilichokuwa kimetokea na ni kwa namna gani alitakiwa kuwa makini sana.
Alikaa kwa saa moja, akaona kwamba tayari wawili hao walimaliza mazungumzo yake hivyo akainuka na kuelekea huko. Alipofika, akazungumza na sekretari, alimwambia bado mgeni yule hakutoka, hivyo alitakiwa kusubiri.
“Dah! Bonge bwana! Yeye na mademu wapi na wapi!” alisema Bazoka na kuanza kucheka. Alimjua Bonge, hakuwa mtu wa wanawake kabisa, alipenda kufanya kazi kuliko kulala na mwanamke kitanda kimoja.
Kwa siku hiyo alionekana kuwa tofauti, alimuhusudu mwanamke huyo kuliko yeye, hilo lilikuwa gumu sana lakini alitakiwa kukubaliana nalo. Alikaa na dada wa mapokezi kwa nusu saa nyingine, akachoka, alichotaka ni kuomba kuonana naye kwani alikuwa na jambo muhimu sana.
“Hebu mpigie simu mwambie nataka kuonana naye,” alimwambia.
Hilo halikuwa tatizo, dada yule akachukua mkonga wa simu ya mezani na kumpigia, simu ikaanza kuita, iliita na kuita lakini haikupokewa, hilo likaanza kumtia shaka.
“Vipi?”
“Hapokei!”
“Mh! Mambo yameiva,” alisema Bazoka huku akitoa tabasamu pana.
Alichohisi ni kwamba tayari Bonge alianza kufanya mapenzi na yule mrembo aliyekuja ofisini kwake. Ilikuwa ni kawaida kwenye ofisi za mabosi kufanya mapenzi na wanawake waliokuwa wakienda kuwatembelea.
Kwake, alihisi naye Bonge alianza kufanya mapenzi na yule binti na ndiyo maana hakutaka kupokea simu iliyokuwa ikiita kwa sauti mpaka wao pale walipokuwa walikuwa wakiisikia.
“Nyie wanaume popote kambi!” alisema dada wa mapokezi huku akiangua kicheko.
“Na ndiyo maana tunatakiwa kutembea na dhana zetu kwenye wallet kwa mambo kama haya. Popote tu tunafungua zipu!” alisema Bazoka, wakaanza kucheka.
Walicheka, waliendelea kuongea huku muda ukizidi kwenda mbele, walikaa tena kwa nusu saa nyingine, wakapiga simu majibu yalikuwa yaleyale, haikupokewa.
Bazoka alionekana kukasirika, alivumilia kwa saa moja lakini mwanaume huyo hakuwa amemaliza, alichomwambia dada wa mapokezi ilikuwa ni lazima kuingia kwani asingeweza kuvumilia muda wote huo.
“Ngoja niingie,” alisema na kuinuka, akaanza kuufuata mlango na kuufungua.
Macho yake yakatua kwa Bonge aliyekuwa amelala, aliangalia huku na kule, yule msichana hakumuona, alishangaa, sekretari alimwambia yule msichana alikuwepo humo ndani lakini jambo la kushangaza kabisa, hakuwepo humo.
“Mzee baba unalala sana, yaani muda wote huo simu hupokei,” alisema Bazoka kwa sauti huku akiachia kicheko cha chini.
Akakifuata kiti na kutulia, aliyatuliza macho yake kwa Bonge aliyekuwa amelala kwa kulalia meza. Alimwamsha, hakuamka, alimshika kichwa na kumtikisa lakini hakuamka, alishtuka kidogo, akainuka na kumsogelea, kitu kilichomshtua, ni damu nyingi zilizokuwa zikiendelea kuctoka puani mwake na kudondokea ardhini.
Akatoka mbio na kumrudia sekretari, akamuita, dada huyo alishtuka, kwa jinsi Bazoka alivyoita ilionyesha kabisa kulikuwa na tatizo, akasimama na kumfuata humo ndani, akamuonyesha.
Kama alivyoshtuka yeye hata yule dada alishtuka hivyohivyo, hakuamini alichokuwa akikiona. Bosi wake alifariki huku damu zikimtoka, kabla ya kufanya kitu chochote kile, simu ikapigwa mpaka polisi ambao walifika hapo haraka sana na kuanza kuuangalia mwili huo.
“Ilikuwaje?” aliuliza polisi mmoja.
Wakaanza kusimulia kilichokuwa kimetokea, polisi walisikiliza kwa makini na kushangaa sana, kilichowashangaza ni kwamba rafiki mkubwa wa Bonge, Sultan alikufa chumbani kwake huku taarifa kutoka kwa mlinzi zikisema aliingia na mwanamke na pia taarifa za kufa kwa Bonge zilisema alikuwa na mwanamke ndani.
Si hilo tu lililokuwa limewachanganya bali ni kwa jinsi wanawake hao walivyokuwa wameondoka ndani ya sehemu ya mauaji. Mwanamke ambaye aliingia na Sultani alitoweka bila mlinzi kumuona, yaani hakutoka ndani ya chumba kile ila aliondoka, hivyo ilikuwa sawasawa na kwa Bonge, mwanamke huyo aliondoka lakini cha ajabu hakuwa ameonekana akiufungua mlango wa ofisi hiyo.
“Kwa maana hiyo huyu mwanamke ni jini? Kama ndiyo! Swali jingine ni yuleyule aliyemuua rafiki yake ama? Kama ndiyo! Kwa nini anaua hivyo? Aliwafanya nini?” waliulizana polisi, kila mmoja aliyekuwa akijiuliza swali hilo, hakuwa na jibu lolote lile, aliyekuwa na jibu alikuwa mmoja tu, BAZOKA.
Je, nini kitaendelea?
Tukutane Ijumaa.