Hadithi: Uchawi wa bilionea Bazoka

Hadithi: Uchawi wa bilionea Bazoka

Nimekuletea mama yako ,,,, hhahaa huyu kama mimi kabisa nikiwa narudi home na kitu kipya usiku
 
NYEMO CHILONGANI
UCHAWI WA BILIONEA BAZOKA
0718069269
SEHEMU YA 27

Christopher ama Bonge kama alivyokuwa akijulikana na watu wengi alitulia chumbani kwake, hiyo ilikuwa ni siku ya pili kuingia lakini hakuwa amewasiliana na rafiki yake kipenzi, Sultani.
Alijaribu kumtafuta kwenye simu lakini mwanaume huyo hakuwa akipokea, simu yake ilikuwa ikiita tu na alipoendelea kupiga zaidi na zaidi, ikawa haipatikani kitu kilichomuonyesha iliishiwa chaji.
Hakujua kilichokuwa kikiendelea, alimfahamu rafiki yake huyo, kwa kila kitu kilichokuwa kikiendelea alimshirikisha, kama alikuwa akiziona missed calls zake ilikuwa ni lazima kumtafuta atakaposhika simu, ila kwa siku hiyo haikutokea hilo.
Akawa na hofu, haraka sana akampigia Bazoka na kuanza kuzungumza naye, alichomwambia ni kwamba Sultani hakuwa akipatikana, alijaribu kumtafuta kwenye simu lakini ukimya wake ulimfanya kuwa na hofu.
“Umekwenda kumcheki kwake? Manake hata mimi nilimcheki nikaona hapokei simu, nikajiongeza kwamba atakuwa bize,” alisema Bazoka.
“Sijakwenda. Hebu acha niende!” alisema Bonge.
Hakutaka kupoteza muda, haraka sana akaondoka kuelekea nyumbani kwa Sultani, hakuchukua muda mrefu akafika, mlinzi akafungua geti na kuliingiza gari ndani, akateremka.
“Vipi! Sultan yupo?” alimuuliza mlinzi.
“Yeah! Yupo hajatoka kwa siku mbili,” alimjibu.
“Kwa nini?”
“Aliingia na kademu fulani kakali kishenzi!” alijibu mlinzi huku akicheka.
“Kwa hiyo yupo naye?”
“Yeah!”
Acha nimcheki!” alisema.
Akaanza kupiga hatua kuelekea ndani. Akaufungua mlango wa sebuleni na kitu cha kwanza kukutana nacho kilikuwa ni harufu kali ya kitu kilichoonekana kuanza kuharibika.
Hilo likamtia hofu, haraka sana akaanza kuelekea chumbani kwa Sultani, kadiri alivyokuwa akipiga hatua kuelekea huko ndivyo ambavyo harufu hiyo ilivyozidi kuongezeka.
“Kuna nini?” alijiuliza.
Akaufikia mlango na kuufungua, kitu alichokutana nacho ni mwili wa Sultani ukiwa kitandani, ulianza kuharibika, alikufa chumbani humo. Akapigwa na mshtuko, haraka sana akatoka mpaka kwa mlinzi na kumwambia kilichotokea.
Naye alichanganyikiwa, hakuamini alichokuwa amekisikia kwani mara ya mwisho Sultani kuingia chumbani humo alikuwa na mwanamke, alikuwa na uhakika alikuwa chumbani huko, sasa kama yeye alikufa, tena chumba ukiwepo mwili wake tu, huyo mwanamke alikuwa wapi?
Ikabidi simu ipigwe mpaka polisi ambao baada ya dakika kadhaa walifika mahali hapo na kuanza kuwahoji. Mlinzi aliwaambia kila kitu, hakumuona mtu yeyote akitoka na hakuwa na mazoea ya kutoka hapo, na kama alikuwa akifanya hivyo, mwanamke yule hakuonekana chumbani, alikuwa wapi?
Hawakuwa na majibu yoyote yale, ila walichokifanya ni kumchukua mlinzi kwa maelezo zaidi kituoni na kisha Bonge kuanza kuwasiliana na marafiki, ndugu na majamaa kuwapa taarifa ya kilichotokea.
Kila mtu alishtuka kusikia hivyo isipokuwa Bazoka tu ambaye alijua vilivyo kilichotokea. Haraka sana akaonana na Bonge, akajifanya kuwa na huzuni kuliko hata watu wengine.
“Mlinzi anasema marehemu aliingia na mwanamke?” alimuuliza huku naye akijifanya kushangaa kuliko hata mshangao wenyewe unavyoonekana.
“Ndiyo!”
“Ikawaje?”
“Akasema mwanamke hakutoka!”
“Alikuwa wapi? Mbona hata chumbani hakuonekana?” aliuliza Bazoka.
“Yaani na mimi ndiyo ninalolishangaa hilo!” alisema Bonge.
Kwa kipindi hicho kila mmoja alikuwa na huzuni tele, pamoja na huzuni hizo lakini kama binadamu moyo wa Bazoka haukuwa na furaha, ulikuwa na majonzi tele kwani alijiona kabisa kushiriki kifo cha rafiki yake huyo.
Mazishi yalifanyika huku akiwa hana hata furaha, hata alipompa taarifa mkewe na kwa jinsi alivyoufahamu ukaribu wao, hata alipomuona mumewe akiwa na mawazo tele, alikuwa akimpa pole tu.
Maisha ya Bazoka ni kama yalibadilika, kuua haikuwa tatizo kwani tayari alifanya hivyo kwa watu wawili lakini kilichokuwa kikimuuma mno kwa mwanaume huyo ni ule ukaribu ambao walikuwanao.
Alikuwa masikini sana, hakuwa na mbele wala nyuma, alikuwa na maisha mabovu mno na huyohuyo Sultani ndiye ambaye aliyabadilisha maisha yake, kutoka kule alipokuwa mpaka hapo, sasa leo hii aliamua kushiriki kumuua mwanaume huyo.
“Kwa nini nilifanya hivyo?” alijiuliza huku akionekana kuwa na majuto mno.
Chumbani hakupata usingizi, kichwa chake kilikuwa na mawazo tele, mkewe alimfariji muda wote, alijua ni kwa namna gani mumewe alikuwa akipitia wakati mgumu kama aliokuwa akiupitia.
Siku zikakatika na baada ya siku mbili baada ya kifo cha Sultani, akarudiwa tena na lile jini lililokuwa na munekano wake na kumwambia sasa ulikuwa wakati wa kumuua Bonge.
“Hivi kwa nini mnafanya hivi?” alimuuliza.
“Ni kwa sababu ya maisha yako!”
“Maisha yangu kivipi?”
“Unahisi tukiendelea kuwaacha watu hawa, wao watakuacha?” aliuliza.
“Mnanichanganya sana!”
“Bazoka! Wewe ni mtu muhimu sana kwetu, unajitoa mno, si kama hawa wenzako!” alimwambia.
“Kivipi?”
“Hawataki kufanya kazi sana, wanajitoa lakini si kwa vile tunavyotaka sisi. Wakipewa kazi za kutoa kafara, huchukua muda mrefu sana, tunataka tuanze upya kabisa, kusafisha kulipokuwa na uchafu,” lilisema jini hilo huku likimwangalia Bazoka.
“Na ikitokea na mimi nikachelewa kutoa kafara kama wao, uamuzi wenu utakuwa upi, kama hawa ama?” aliuliza Bazoka huku akimwangalia.
“Hahaha! Naamini haitoweza kutokea hivyo. Bazoka, hivi karibuni utapokea tena taarifa ya kifo cha Christopher. Pumzika kwanza,” alimwambia na jini hilo kupotea.
***
Maganza alipokea taarifa kuhusu kifo cha Bonge akiwa ofisini kwake, ilikuwa ni taarifa kama zingine za watu waliokuwa wamekufa chumbani mwao huku kukiwa hakuna mtu hata mmoja.
Ilikuwa ni taarifa yenye mvuto kwake kuisikiliza lakini hakuwa na haja ya kufanya hivyo kwani alikuwa na kesi nyingine za kufanya lakini si la kufuatilia kifo cha mwanaume huyo.
Alipelekewa kila kitu mezani, kwenye ripoti kuhusu mauaji hayo, kulikuwa na namba za watu wanne, marafiki zake marehemu ambao walikuwa karibu naye, polisi waliamua kuziandika namba hizo kwa sababu ya kuanza kufuatilia kuhusu tukio hilo.
Macho yake yalipotua kwenye jina lililoandikwa Emmanuel Bazoka, akashtuka, hakuamini alichokuwa amekiona, kichwa chake kikaanza kujiuliza maswali kuhusu huyo Bazoka, sasa akaanza kuhisi kulikuwa na kitu.
Tukio la mauaji ya Bi. Semeni halikuwa limesahaulika, na hata ufuatiliaji wake ulikuwa ukiendelea, hilo likiwa halijamalizika, tayari kulikuwa na taarifa nyingine ya kifo, mtu aliyekuwa rafiki na Bazoka.
“Bazoka....” alijikuta akilitamka jina hilo.
Akaanza kuifuatilia, akamwambia polisi aliyekwenda nyumbani kwa marehemu kujua kilichokuwa kimetokea. Akapewa namba ya mlinzi ambayo aliichukua na kumpigia.
Akahitaji kuonana naye, hilo halikuwa tatizo, haraka sana mlinzi akaelekea kituoni na kuongozwa mpaka kwenye chumba cha mahojiano kwa lengo la kumuhoji maswali kadhaa.
“Aliingia na mwanamke, baada ya siku mbili mwili wake ukakutwa chumbani,” alisema mlinzi huku akimwangalia Bazoka.
“Na hukumuona huyo mwanamke?”
“Nilimuona wakati akiingia naye, ila sikumuona alipokuwa ametoka,” alimjibu.
“Labda aliruka ukuta kwa nyuma?”
“Ni vigumu. Ile nyumba mbali na kuzungushiwa ukuta, pia juu ya ukuta kuna nyasa za umeme, zipo tatu, yaani kila nikijiuliza aliondokaje nashindwa kufahamu!” alisema.
“Labda alisubiri utoke na yeye ndiyo atoke?”
“Sikuwahi kutoka, na mara zote nikitoka huwa ninafunga geti kwa ufunguo!” alimjibu.
“Na chakula?”
“Huwa naletewa hapohapo!”
“Doh!”
“Yaani mkuu nashangaa sana!”
“Sawa. Na vipi kuhusu hawa marafiki zake, kuna marafiki nimepewa majina yao hapa,” alisema na kuanza kumtajia.
“Wamefanyaje mkuu?”
“Unawajua wote?”
“Ndiyo! Tena nawajua vizuri kabisa.”
“Huyu Christopher vipi?”
“Ni jamaa mmoja poa sana, anapenda kusaidia watu, jamaa ananitoaga sana pesa akija,” alimjibu.
“Na Bazoka?”
“Na huyo naye yupo poa sana. Hana maneno, ni mwanaume mwenye akili sana!” alimjibu..
“Unamaanisha nini kusema ana akili?”
“Hana papara, ni mtu mwelewa sana,” alimjibu.
“Kingine kuhusu yeye?”
“Najua hayo tu!”
“Anaishi wapi?” alimuuliza.
“Mbezi Beach!”
“Unapafahamu kwake?”
“Hapana! Ila bosi anasemaga anaishi Mbezi Beach,” alijibu.
Maganza akashusha pumzi nzito, kile alichoambiwa ndicho ambacho alikifahamu kuhusu mwanaume huyo. Tatizo lilikuwa moja tu kwamba alipokuwa naye ndani ya gari kwa lengo la kuelekea kwake, alishindwa kupafahamu mahali huko na wakati aliwahi kufika.
Sasa akapata uhakika kuwa yeye alikuwa sahihi kabisa, Bazoka alikuwa akiishi Mbezi Beach na si Kinondoni kama alivyokuwa amempeleka, ila tatizo kubwa ni pale kila alipotaka kwenda huko, kumuhakikishia Bazoka kwamba ni nyumbani kwake, alishindwa kupakumbuka.
“Na kuhusu huyo mwanamke, ulimuona?”
“Ndiyo!”
“Yupoje?”
“Ni mzuri sana!”
“Simaanishi muonekano wa urembo wake!”
“Oh! Ni mrefu kidogo, mweupe, ana vishimo mashavuni, ana umbo namba na....”
“Sikiliza! Nashukuru sana!” alisema Maganza manake aliona sasa lile swali lilikuwa likipewa jibu la uzuri wake tu.
Maganza aliona kabisa hakuwa na muda wa kukaa hapo, sasa maswali yake yakaanza kujiuliza kuhusu watu wawili, mwanamke ambaye aliingia na Bonge chumbani, pia Bazoka ambaye naye alionekana kuwa rafiki na mwanaume aliyeuawa chumbani kwake.
Kichwa chake zaidi kikaanza kujuliza kuhusu Bazoka, ilikuwa ni bahati mbaya kwake kuwa karibu na watu waliokuwa wamekufa ndani ya kipindi kifupi sana, alichanganyikiwa, akahisi inawezekana kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea lakini alishindwa kupata jibu.
Bi. Semeni aliuawa chumbani kwake, alikuwa na uhakika kulikuwa na mtu aliyemuua kutokana na mazingira yaliyokuwa humo, alikwaruzwa na kucha kubwa kama za mnyama, hakujua zilikuwa za nani, sasa akili yake ikaanza kumwambia inawezekana Bi. Semeni alikufa kwa uchawi.
Ukiachana na hilo pia kulikuwa na kifo cha Bonge, naye alikutwa akiwa amekufa chumbani mwake, kama ilivyokuwa kwa Bi. Semeni ila huyu aliingia na mwanamke, mwanamke ambaye hakuwa ameonekana baada ya kuingia naye.
Alikuwa mzuri.
Mweupe,
Mwenye figa namba nane.
Mrefu kidogo.
Hizo zilikuwa sifa ambazo aliambiwa na mlinzi, kwa mantiki ya uzuri, ilikuwa ni rahisi kuufahamu uzuri huo kwa kuwa huyo Bonge alikuwa na pesa hivyo kila mwanamke aliyekuwa akimchukua ilikuwa ni lazima kuwa mzuri.
Ukiachana na hayo yote, pia kulikuwa na suala la Bazoka kuishi Mbezi Beach, hilo lilikisumbua sana kichwa chake na hakuwa akijua ni kitu gani hasa kilichokuwa kimetokea.
Aliwahi kwenda nyumbani kwake, akazungumza na mkewe baadaye aliporudi huko akiwa na Bazoka ndani ya gari, hakuweza kupaona, yaani alipasahau na hakukumbuka kitu chochote kile.
“Au Bazoka mchawi?” alijiuliza.
“Hapana bwana! Hana muonekano wa kichawi hata kidogo. Nadhani kuna kitu hapa!” alijijibu mwenyewe.

Je, nini kitaendelea?
Tukutane Alhamisi hapahapa.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom