Hadithi: Nyuma Ya Machozi

Hadithi: Nyuma Ya Machozi

SEHEMU: 20
MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
SIMU: 0713 646500

ILIPOISHIA:
Kauli ile ilimshtua sana Kilole na kujiuliza Jimmy uwezo ya kutoa fedha kiasi kile ameutoa wapi, wakati maisha yake yalikuwa ya kubahatisha mpaka apige picha na muda mwingi alishinda kijiweni.
Wakati akijiuliza maswali yasiyo na majibu ndani mazungumzo yaliendelea.
“Ha..ha..lafu mpenzi siku hizi unafanya kazi gani maana fedha zimeibuka kama uyoga?”
SASA ENDELEA...

“Maisha kama kalata ukijua kuzichanga kila kitu kina kwenda kilivyopangwa.”
“Au unauza dawa za kulevywa?” “Kwani dia tatizo lako nini?”
“Naogopa nisije kukupoteza wakati nakuhitaji.” “Ungekuwa unanihitaji ungeridhika na nilivyokupa.”
“Sawa, hata kama unauza unga kuwa makini.”
Kilole alijikuta akijawa na maswali juu ya maneno ya Jimmy kuonesha ndani ya wiki ile atampatia yule mwanamke milioni tatu. Pia siku ile alimpa milioni moja na laki sita. Akili ya haraka aliamini fedha hizo huenda ndipo aliziombwa azitoe ili azipate picha zake.
Alikubaliana na wazo lake la awali kuwa Jimmy ndiye mhusika mkuu wa mipango yote. Wakati akiwaza vile alisikia simu ya Jimmy ikiita, alimsikia Jimmy akimwambia mwanamke wake.
“Samahani nakuja.” “Unakwenda wapi?”
“Sipendi maswali ya kijinga nimekueleza nakuja,” Jimmy alijibu kwa ukali.
“Najua na wanawake zako tu, “ alimsikia mwanamke akilia wivu.
“Wewe si unataka gari sasa kwa nini unapenda kufuatilia mambo yangu?”
“Sawa, basi nenda.”
Kilole alisikia mlango ukifunguliwa kuonesha Jimmy alikuwa akitoka nje kusikiliza simu. Kilole akiwa ametulia pembeni ya ukuta kwenye choo cha nyumba ya jirani.
Alisikia sauti za viatu zikielekea nyuma ya nyumba, kwa haraka alijificha nyuma ya choo. Jimmy bila kujua kuna mtu alisimama pembeni ya choo na kupiga simu iliyopokelewa upande wa pili.
“Sema Rich mbona usiku?”
“Aisee nina tatizo kubwa ya fedha,” kutokana na utulivu wa hali ya hewa Kilole alisikia mtu aliyekuwa akizungumza upande wa pili.
“Shida gani mzee, si leo nimekupatia mgao wa milioni?” “Ni kweli, si unajua nyumba za uswahili baada ya leo kununua sofa nimepandishiwa kodi ghafla na kutakiwa nilipe mwaka mzima na fedha yake anataka kesho. Sasa sijui utanisaidia vipi naomba basi unikope milioni ili kesho kama tukilipwa ile fedha nitakurudishia.”
“Sikiliza Rich leo nimempa shemeji yako milioni mbili kwa ajili ya sofa na kulipia nyumba, kwa sasa sina kitu ila jitahidi kumtisha yule mwanamke ili tupate hiyo fedha ikiwezekana hata kesho saa tano asubuhi.”
“Okay, nitajaribu kumsomesha.”
“Atakuelewa tu, jitahidi kesho tuzipate zote milioni kumi sawa?”
“Sawa nimekuelewa.”
“Basi usiku mwema, unajua umenitisha sana, wasiwasi wangu yule mwanamke kujua kama ni mimi ndiye namchezea mchezo huu.” “Walaa, nawe usiku mwema.”
Baada ya kukata simu Jimmy alirudi ndani na kumuacha Kilole akiwa amepata kitu ambacho mwanzo alikidhania lakini siku ile ukweli ulijulikana. Aliona hakuna haja ya kuendelea kuwa pale. Aliondoka na kurudi nyumbani huku moyo ukimuuma kwa kitendo alichotendewa na Jimmy.
Alifika kwake na kuingia ndani bila mtu yeyote kujua kama alitoka, alipanda kitandani na kujilaza. Kutokana na kutingwa na mawazo muda mwingi alifikiria jinsi ya kumuadabisha Jimmy. Moyoni aliapa kabla ya kuwapa hizo milioni kumi lazima wote wawe wamelamba udongo.
****
Teddy mwanamke hatari muuza unga baada ya kumaliza kuuza mzigo wake alimuaga Deus na kumweleza kila kitu kitakavyoendelea atamjulisha. Muda wote alikuwa na maswali juu ya mtu aliyemchoma katika kitengo cha madawa ya kilevya.
Alijiuliza nani aliyekuwa akijua kuondoka kwake zaidi ya mdogo wa marehemu mumewe ambaye alinyongwa China baada ya kukamatwa na madawa ya kulevya. Tokea kifo cha mumewe mdogo wa mumewe alikuwa akimfuatilia na kumtaka kimapenzi. Lakini hakuwa tayari kutembea na familia moja kwa vile alikuwa na uamuzi wa kumchagua nani awe mpenzi wake. Muda mwingi kulikuwepo na kutoelewana kwa shemeji yake kulazimisha mapenzi na yeye kumkatalia. Mwanzoni alifanya kazi na mumewe ya uuzaji wa madawa na ndiye aliyemfundisha kuifanya kazi ile. Baada ya kifo cha mumewe alimshirikisha mdogo wa mumewe ambaye baada ya kupata fedha alianza nyodo na kuendelea kumtaka kimapenzi huku akimuahidi kumfanyia kitu kibaya kama ataendelee kumtolea nje.
Teddy bado hakutishwa na vitisho vya shemeji yake ambaye bado aliendelea kufanya naye kazi ya kusambaza dawa za kulevya kila kona ya dunia. Hata siku ya kuondoka mara ya mwisho aliyekuwa akijua safari ile ni yeye na washirika ambao wote walikula kiapo cha kuficha siri ya kazi yao na kuwa tayari kumsaidia mwenzao kwa gharama yoyote anapopatwa na tatizo. Wazo lake lilimpekeka huenda ni shemeji yake ndiye aliyefanya mchezo ule ili kumkomoa baada ya kumkataa kimapenzi.
Aliapa kumfanyia kitu kibaya kama ni yeye na adhabu yake ilikuwa ni kifo kwa vile nia yake ilikuwa ni kumpoteza. Teddy alipofika Italia alikwenda moja kwa moja kwenye nyumba aliyokuwa akiishi pamoja na shemeji yake.
Mara zote alipokuwa akisafiri na kurudi alikuwa akiwasiliana naye hata kumpokea, lakini siku ile alirudi kimya kimya. Alipofika nyumbani kwake aliingia ndani bila hodi, shemeji yake aliyekuwa na rafiki zake wakinywa na kujiachia na wanawake na muziki mkubwa alipomuona alishtuka sana.
“Ha! Teddy wewe si ulikamatwa?” “Wapi?” “Si..si.nilisikia umeshikwa Tanzania?” “Nani aliyekuambia?”
“Au alinidanganya?” “Nani mbona sikuelewi nani amekwambia mimi nimeshikwa?”
“Au umetoa rushwa?” “Ili?” Teddy alimuuliza huku akimtazama usoni kutafuta ukweli. “Tu..tu..achane na hayo, na..na mbona umekuja bila taarifa.” “Tatizo nini? kwa nini umegeuza nyumba yangu club?”
“Kwani tatizo nini?” “Mose unanitafuta huwezi kuigeuza nyumba yangu kama kilabu cha pombe ya kienyeji zinazouzwa Afrika.”
“Oya washikaji tutimke mambo yamekwisha haribika.”
“Sasa sherehe tunaihamishia wapi?” Mwanamke mmoja aliyekuwa amelewa sana na kuvaa nusu uchi aliuliza.
“Oya Rose, hii tunakwenda kuimalizia club Royal clasic.”
“Sasa kuna faida gani ya kupoteza muda, na huyu nani?” “Shemeji yangu.”
“Si ulisema umenyongwa au kafufuka?”
“Sitaki maswali hebu tuondokeni.”
Mose aliondoka na washikaji wake waliokuwa wamelewa na kwenda kumalizia starehe zao club.
Teddy alianza kufanya usafi ili kuirudisha nyumba katika hali nzuri. Macho yake yaliona simu kwenye kochi, aliacha kufanya usafi kuichukua simu ile na kuanza kuipekea kwenye sehemu ya ujumbe.
Jicho lake lilikutana na ujumbe ulioonesha shemeji yake alimtumia mtu aje kwenye sherehe ya kupotezwa kwake. Ilisomeka: yule fala nimemmaliza njoo tusherehekee njoo na demu wako. Palepale alipata picha kuwa shemeji yake ndiye aliyemtengenezea mtego ule. Aliapa kummaliza na kutoroka Italia na kwenda kuishi nchi yoyote kutokana na uwezo ya kifedha.
*****
Siku ya pili Kilole aliwahi kuamka ili aweze kuzungumza na Kinape kuwa asiondoke ili wazungumze. Kama kawaida Kinape alijichelewesha kwenda kazini. Baada ya Deus kuondoka alimfuata chumbani kwake ili apate muafaka wa jambo walilozungumza jana yake. “Mhu! Umefikia wapi?” Kilole alimuuliza Kinape.
“Kuhusu nini?” “Kuhusu huyo mwanamke wako.”
“Kwa kweli bado sijapata jibu, tena jana Deus ndio kaniachanganya zaidi.”
“Kivipi?”
“Amesema kesho niende na Happy kijijini.”
“Eti nini?” Kilole alishtuka kusikia habari zile.
“Mumeo kasema kesho niende na gari kanipa ili kuhakikisha sina cha kujitetea.”
“Wewe ulimjibu nini?”
“We unafikiri ningemjibu nini?”
“Si ungemwambia umebadili umamuzi kuwa hutamuoa tena Happy.”
“Ningeanzia wapi wakati kila siku nimekuwa nikiomba msaada wake kufanikisha ndoa yangu.” “Mmh! Kumbuka akiishafika kijijini mimi sina changu.”
“Lakini kwa nini tulazimishe mambo wakati yamekwisha onesha vikwazo?” “Kinape hunielezi lolote nikakuelewa, nimejitoa kwako sitarudi nyuma.”
“Sasa nitafanyaje maana leo jioni happy na mama yake watakuja kujua hatima ya uchumba wetu.”
“Lakini kwa nini tusimfutilie mbali Deus, huoni anatuwekea kivingu?”
“ Ni haraka sana kufanya mambo hayo, kuna kitu kimoja kizuri tukifanya haraka tutakipoteza.”
“Kitu gani?”
“Mwezi ujao kuna bilioni kama mbili hivi zinaingia kwa hiyo tukizipata tutakuwa na uwezo wa kuishi nchi yoyote tuitakayo.”
“Lakini kumbuka kila siku unaongeza siku mwisho wake picha zitamfikia na kuharibu kila kitu.” “Kilole tutakuwa wajinga kuziacha hizo bilioni mbili za bure.” “Tutazitoa wapi?”
Kinape alimueleza yote aliyoelezwa na Deus juu ya mpango wa kuhongwa na wauza dawa za kulevya. “Nimekuelewa.”
Alimkubalia ili kumaliza mazungumzo lakini moyoni alipanga wiki ile lazima afanye kitu ambacho kitakuwa simulizi midomoni mwa watu. Baada ya Kinape kuondoka kwenda kazini, Kilole alijikuta akizidi kuchanganyikiwa na kujiuliza aanze na nani kati wa watu wote watatu, mumewe, Jimmy na Happy mchumba wa Kinape.
Aliamini mtu wa kuanza naye alifaa kuwa Happy kwa kumzima usiku wa siku ile ili kuzuia safari ya kwenda kijiji, kisha Jimmy na mwisho alipanga kummaliza mumewe. Mpango ule aliufanya kwa siri ili mtu yeyote asijue kwa kuamini kama angemshirikisha Kinape angemuharibia kila kitu.
Wazo alilopata la kummaliza mumewe aliona anahitaji msaada wa mtu, na mtu wa karibu alikuwa Jimmy. Aliamini msaada wake ulikuwa muhimu lakini mwisho wa yote na yeye angemmalizia mbali. Baada ya kukubaliana na mawazo yake aliamua kumpigia simu Jimmy ili mpaka jioni mpango wake wa kummaliza mumewe ukamilike ibakie kuutekeleza. Baada ya kupiga simu ya Jimmy iliita upande wa pili na kupokelewa. “Haloo.” “Haloo Jimmy.” “Ndiyo sister.” “Samahani Jimmy nina shida na wewe.”
“Shida gani?” Sauti ya upande wa pili ilionesha kushtuka.
“Nitakueleza tukionana, sema tuonane wapi.”
“Njoo nyumbani kwangu.”
“Sawa nakuja.” “Nitakuwa nyumbani baada ya nusu saa.”
“Hakuna tatizo nitafika kwa muda huo.” Dakika tano baada ya kumaliza mazungumzo na Jimmy, simu ya Kilole iliita alipoitazama ilikuwa namba ngeni. Aliipokea. “Haloo.”
“Eeh! Umefikia wapi?”
“Kuhusu nini?” Japo sauti iliijua alijifanya kuuliza. “Hiyo milioni kumi ipo tayari?”
“Kesho itakuwa tayari.”
“Sihitaji kesho nataka leo.” “Okay, hakuna tatizo jioni ya leo nitatimiza kila kitu.”
“Na ufanye hivyo, kinyume na kauli yako kila kitu hadharani.”
“Wala usihofu, itanibidi nichukue fedha ya ujenzi wa nyumba nitazirudisha kesho.”
“Nakutakia siku njema.”
“Na wewe pia.”
Kilole baada ya kukata simu alishusha pumzi ndefu na kujikuta akili yake ikifanya kazi kama kompyuta kwa kupata jibu. Ilionesha muda alioweka Jimmy ulikuwa ni kuwasiliana na jamaa yake ili kutaka kujua fedha yao.
Alicheka kwa uchungu na kuamini siku ile mpaka inakatika itabaki kumbukumbu akilini mwake. Alikwenda kujiandaa kisha alitoka hadi kwenye mashine ya kuchukulia fedha na kuchukua milioni ishirini ambazo aliamini zingemsaidia kuifanya kazi yake vizuri.
Baada ya kuziweka vizuri fedha zake aliingia kwenye gari na kwenda moja kwa moja kwa Jimmy. Alimkuta Jimmy yupo nyumbani, kwa vile chumba alikuwa akikijua alikwenda kugonga mlango.
“Karibu,” Jimmy alitoka akiwa kifua wazi.
“Ooh! Sister karibu.”
"Asante nimekaribia,” Kilole alijibu huku akiingia ndani.
Ndani ya chumba cha Jimmy hakukuta mabadiliko makubwa zaidi ya tivii ya flati na friji ndogo. Alikaa kwenye kochi wakati huo Jimmy alikuwa akielekea chumbani kuchukua fulana. Macho ya Kilole yaliona kitu kilichomshtua, kiuoni kwa Jimmy kulikuwa na mchoro ambao ulifanana na mchoro aliouona kwenye kiuno cha mtu wa kwenye picha ya watu waliombaka.
Moja kwa moja ushahidi wake ulikamilika alijua Jimmy ni mmoja ya watu waliombaka, alijilaumu kwa kuondoka bila siraha ambayo ingemsaidia kumaliza kazi kwani ushahidi wa kutosha kuwa Jimmy ndiye mbaya wake ulikuwa umetimia. Lakini bado aliamini Jimmy alikuwa kiungo muhimu wa kufanikisha mpango wake kabambe utakaomuwezesha kutimiza lengo lake.

Itaendelea
 
SEHEMU: 21
MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
SIMU: 0713 646500

ILIPOISHIA:
Moja kwa moja ushahidi wake ulikamilika alijua Jimmy ni mmoja ya watu waliombaka, alijilaumu kwa kuondoka bila siraha ambayo ingemsaidia kumaliza kazi kwani ushahidi wa kutosha kuwa Jimmy ndiye mbaya wake ulikuwa umetimia. Lakini bado aliamini Jimmy alikuwa kiungo muhimu wa kufanikisha mpango wake kabambe utakaomuwezesha kutimiza lengo lake.
SASA ENDELEA...
Baada ya Jimmy kutoka chumbani akiwa amevaa fulana alikaa pembeni kidogo na Kilole.
“Ndiyo sister karibu sana.”
“Asante sana, mbona ndugu yangu umenitupa?” Kilole alijifanya kuchangamka japo moyoni alikuwa na hasira za kuua mtu. “Nikutupe wapi wakati kila kukicha mambo afadhari ya jana.” “Samahani sister unatumia kinywaji gani?” Jimmy aliuliza huku akinyanyuka kuelekea kwenye friji. “Walaa usisumbuke nashukuru.”
Jimmy alirudi kukaa kumsikiliza Kilole aliyeonekana na haraka.
“Sasa ni hivi nahitaji msaada wako wenye malipo mazuri sana.”
“Kazi gani tena sister?”
“Nina imani michongo ya mjini unaiju vizuri nilikuwa nahitaji unga.”
“Unga! Upi?” Jimmy alishindwa kumuelewa. “Kokeni.”
“Ha! Wa nini?” alizidi kushtuka.
“Dada yako najidunga muda mrefu lakini mtu aliyekuwa akiniletea amesafiri hivyo napata shida sana kubembea.”
“Mmh! Wa shilingi ngapi?”
“Kwa vile kuna watu wangu nao wana shida nilikuwa nahitaji wa milioni kumi.”
“Ha! Mbona mwingi?” “Tatizo mwingi au niupate, mbona kila kitu unashangaa.”
“Mmh! Ulikuwa unautaka lini?” “Leo hii na fedha ipo.”
“Na kamishina yangu kiasi gani?” “Wewe unataka shilingi ngapi?”
“Si unajua kazi za hatari hata laki mbili siyo mbaya.”
“Nitakupa milioni.”
“Ooh! Asante sana.” “Samahani Jimmy simu yako ina salio nataka nimpigie mtu wa tigo,” Kilole ambaye siku zote alijengwa uwezo wa kufanya mambo na mumewe Deus hata kumfundisha jinsi ya kutumia siraha kwa utimilifu tena kwa uhakika mkubwa.
Aliamini kupitia simu ya Jimmy ataweza kuipata namba ya mwenzake ambayo ingemsaidia kumfahamu na kuweza kumtia mikononi. Jimmy bila kujua alimpa simu yake, Kilole aliichukua na kujifanya anaingiza namba, kila alilofanya alimuangalia Jimmy ambaye hakuwa na habari naye.
Aliangalia simu iliyoingia jana yake usiku muda ambao yeye alikuwepo pale, baada ya kuiona ili kujiridhisha aliangalia iliyopigwa muda mchache baada ya Jimmy kutoka nje. Jina lilikuwa moja la Rich.
Baada ya kunukuu akilini ile namba alimrudishia simu yake, Jimmy naye bila kuhoji aliipokea simu yake. Kilole alinyanyuka kwenye kochi na kuanza kutoka nje. “Basi twende kwenye gari nikakupe hiyo fedha ili jioni nije niuchukue mzigo.”
Baada ya kusema vile Kilole alitangulia kwenye gari na kumsubiri Jimmy alipokuja alimuhesabia milioni kumi na moja kisha waliagana.
“Jimmy nakutegemea, basi usiniangushe kama zile picha ambazo ninanitia wazimu.”
“Ooh! Ina maana bado wanakusumbua?”
“Hawana lolote shida yao fedha sina jinsi nitawapa.”
“Ooh! Pole sana.”
“Ya kawaida, la muhimu nifanyie kazi yangu vizuri.”
“Hakuna tatizo sister kazi yako nitaifanya vizuri.”
Kilole baada ya kuondoka njiani aliwaza mengi huku hasira zikumpanda kichwani na kutamani kuwafanyia kitu kibaya. Lakini alikumbuka upumbavu wote anaoufanya ni kwa ajili ya kutetea penzi lake kwa Kinape. Hivyo alitakiwa kuwa makini kutekeleza mipango yake bila kumshirikisha mtu moja kwa moja hasa ya mauaji.
Kilole alirudi nyumbani kujipanga kuhakikisha kazi yake ya usiku wa siku ile anaifanya kwa umakini mkubwa japo moyo mwingine ulimshauri aachane na mpango ule wa hatari. Lakini upande wingine aliamini maji kaisha yavulia nguo lazima ayaoge na liwalo na liwe.
***
Wakati Kilole akipanga mkakati wa kummaliza Happy mchumba wa Kinape ili kuhakikisha haendi kijijini. Kinape naye alikuwa na mazungumzo na mpenzi wake sehemu tulivu waliyochagua, ambaye alikuwa akiteseka na mabadiliko ya mpenzi wake yaliyoonekana kutishia uhusiano wao.
Kinape pamoja na kujitahidi kuwa karibu na Happy lakini muda mwingi alibanwa na Kilole ambaye nia yake ilikuwa kuuvunja uhusiano ule.
“Kinape pamoja na kusema kesho unakwenda kunitambulisha kwenu bado siamini najua ni kunipoza moyo lakini hunipendi tena.”
“Happy kama kusingekuwa na umuhimu wa kwenda kukutambulisha kwetu ningekaa kimya usingejua nini kinaendelea?”
“Kinape lakini umegeuka kiasi hiki, nini nimekukosea?” Happy aliuliza kwa sauti ya kilio.
“Mambo yameingiliana tu lakini muda si mrefu kila kitu kitakuwa sawa,” Kinape alijitetea.
“Kuna kitu unanificha, Kinape una mwanamke mwingine.”
“Sina mwanamke mwingine zaidi yako.”
Kinape alijitetea japo alijua ana mtihani mzito kwa Kilole, moyoni mwake hakuwa tayari kumsaliti Deus rafiki yake kwa ajili ya mpenzi wake wa zamani.
Kilichomuumiza kichwa kilikuwa ni picha za kufanya mapenzi na Kilole ambazo kwake aliamini zilikuwa bomu ambalo kama lingepasuka kusingekuwa na usalama. Moyo alijipanga kuhakikisha anamfahamu aliyefanya mchezo ule, akiwa katikati ya mawazo Happy alimshtua.
“Ha..ha..lafu mbona simuelewi shemeji yako?”
“Umuelewi kivipi? Kinape alishtuka kidogo.
“Asingekuwa mke wa kaka yako ningesema mwanamke wako.” “Kwa nini unasema hivyo?”
“Kuna kila dalili za kuwepo siri nisiyojua kuhusu mustakabali wa penzi langu kwako. Mimi si wa kukatazwa kuingia ndani kwenu, hata kama haupo bado nina haki ya kuja kwenu.”
“Nimekuelewa lakini kila kitu kitakwenda vizuri, naomba uniamini na kesho ndiyo siku yako ya kuamini kuwa penzi letu lipo hai.”
“Mmh! Nitaamini mpaka nitakapokuwa mbele ya wazazi wako na kunitambulisha kuwa mimi ni mpenzi wako mkeo mtalajiwa.”
“Tena tumepewa lile lexus kwenda nayo kwa raha zetu.” “Usiniambie!” Happy alifurahi kwa kumkumbatia Kinape na kujisahau kama muda mfupi alikuwa akilaumu.
“Hii yote kukuonesha jinsi gani ninavyo kujali na ahadi niliyokuahidi ni ya kweli.” “Asante sana mpenzi wangu.”
“Si hilo tu, brother amenipa jana milioni 50 kwa ajili ya maandalizi ya harusi yetu.” “Jamani yaani matamani siku ifike niwe nisimame pembeni yako nikiulizwa: Happy Kinape unakubali kuolewa na Kinape kama mumeo?”
“Mmh! Utajibu nini?”
“Ndiyooooooo, tena mara mia.”
“Basi nikuache akajiandae na safari, kesho alfajiri nakupitia.”
“Sawa mpenzi wangu, katika siku ambayo nitakula chakula kiteremke sehemu zake ni leo, na siku tukifunga ndoa sijui itakuwaje bado naona ndoto ya mchana.”
“Nina imani kuanzia kesho utakula na kunywa kwa furaha baada ya kukuvisha pete ya milioni kumi.” “Haaaa!” Happy alishika mikono kifuani asiamini masikio yake.
“Nataka uamini ile ahadi niliyokuahidi inatimia.” “Kinape amini usiamini mabadiko yako kama yangeendelea kidogo nilikuwa nimewaza kufanya kitu kibaya.”
“Kipi tena mpenzi wangu?”
“Haki ya nani, leo isingepita salama nilipanga kunywa sumu nifilie mbali.”
“Aah! Happy mawazo gani tena hayo mpenzi wangu?”
“Hujui tu, nimeteseka sana, nimeumia sana, hebu nitezame mimi ndiye Happy unayemfahamu nimekuwa kama mti uliokauka.”
Happy alizungumza huku akiangua kilio ambacho kilikuwa sawa na kukamua uchungu wa moyo kutokana kuteswa na penzi la Kinape baada ya kutekwa na Kilole.
“Happy mpenzi wangu yote hayo yatakwisha hata mimi najua kosa langu lilikuwa wapi.” “Naomba usinitende nakupenda sana Kinape, sioni sisikii juu yako, bila wewe mimi sipo,” Happy aliendelea kusema huku akibubujikwa na machozi. “Basi mpenzi nimekuelewa nina imani nilikuumiza lakini nakuahidi kutuliza maumivu yako yote.”
Kinape alimpeleka Happy kwao na kuamua kwenda club ili aingie nyumbani usiku sana asionane na Kilole na alfajiri awahi kuamka na kuondoka ili kumkwepa.
****
Majira ya jioni akiwa amejipumzisha nyumbani kwake alipokea simu ikiulizia mzigo wao.
“Vipi umefikia wapi?” “Kila kitu kipo sawa ila sasa hivi nina wageni muhimu naomba univumilie kidogo.”
“Mpaka saa ngapi?”
“Sijajua ila lazima usiku huu nikupe mzigo wako wote kwa vile nimekwisha uandaa kabisa.” “Sasa tuambie saa ngapi?”
“Nimepanga baada ya mume wangu kulala nitoke mara moja, ila nilikuwa naomba uje karibu na nyumbani ili nikikukabidhi nirudi haraka kabla mume wangu hajashtuka kama nimetoka.”
“Kwa hiyo saa ngapi?” “Kuanzia saa sita usiku ila uhakika saa saba.”
“Hakikisha muda huo unatupa mzigo wetu ukifanya ujanja wowote picha zako zitasambaa kila kona ya jiji.” “Walaa usitie hofu nilichowaeleza kitakwenda kama nilivyopanga, naomba usikae mbali na simu yako ili nikikupigia utokee na kuchukua.”
“Nimekuelewa baadaye.”
Kilole baada ya kukata simu alicheka na kuuapia moyo wake usiku wa siku ile utabakia historia nzito moyoni mwake. Majira ya saa moja na nusu usiku Kilole alipigiwa simu ya Jimmy kumjulisha kupatikana kwa mzigo, walielekezana pa kuonana.
Alikwenda eneo la tukio na kupewa unga wake wa shilingi milioni moja. Baada ya kuupata aliamini kabisa utamsaidia kuifanya kazi yake kwa uhakika mkubwa. Aliagana na Jimmy na kurudi zake nyumbani na kuuficha sehemu ambayo mumewe hawezi kuiona.
Baada ya kuweka mzigo vizuri alichukua bastola ya mumewe na kuichunguza kama risasi, alikuta za kutosha aliamini zitafanya kazi yake ya usiku ule aliiweka vizuri kwa kazi ya usiku ule. Alichota unga kidogo na kuuweka kwenye chakula cha mumewe ili akila alale na yeye aweze kutoka usiku ili akafanye kazi yake nzito ambayo ilimpa mtihani mzito. Baada ya kuipanga mipango yake vizuri, alitulia kusubiri muda. Mumewe baada ya kutoka kazini alimuandalia chakula.
Baada ya kula alimuomba waende wakazungumzie chumbani. Waliingia chumbani huku Deus akikisikia kichwa kizito. Hata wakuwahi kuzungumza usingizi mzito ulimpitia. **** Ndani ya jiji Sicily nchini Italia, jiji linalosifika kwa uuzwaji wa dawa za kulevywa,Teddy bado alikuwa na hasira baada ya kugundua shemeji yake ndiye aliyemchoma kwa kitengo cha kuzuia dawa za kulevya Tanzania. Kwake alimuona ni adui mkubwa asiyefaa kuendelea kuishi.
Alipanga usiku wa siku ile amuulie mbali na yeye kutimka zake kwenda mji mwingine wa Turin kuanzisha maisha mapya kwa kuamini uwezo wa kifedha ungemwezesha kuishi sehemu yoyote duniani bila tatizo.
Baada ya kugundua kuwa shemeji yake ndiye mbaya wake hakutaka kumuonesha kukasilishwa na kitendo kile. Ili kumvuta adui yake alijifanya kubadilisha msimamo kuwa amemkubali kimapenzi. Asubuhi ya siku ile baada ya kifungua kinywa alimwita Mose na kumweleza kitu:
“Mose my sweet.”
“Teddy kauli hiyo imeanza lini?” Mose alishtuka kusikia anaitwa vile.
“Leo mpenzi, nimetafakari na kuona hakuna umuhimu wa kulikataa penzi lako kwa vile wewe ni mwanaume kama wanaume wengine pia kuwa na wewe sawa na kuwa na marehemu kaka yako.”
“Umeona eeeh,” Mose alifurahi kusikia vile bila kujua aliyekuwa anazungumza naye si Teddy aliyemzoea bali malaika wa kifo.
“Unajua Mose nimekuwa sipati jibu kila nilipojiuliza kwa nini nisikukubalie uwe mpenzi wangu, lakini ujio wa safari yangu Italy ilikuwa kuja kukueleza nimekufungulia moyo wangu kwako.”
“Ooh! Asante sana, siamini kwa kweli lazima nikueleze ukweli Teddy nimeteseka kwa muda mrefu juu yako. Nina imani sasa hivi moyo wangu utapoa.”
“Najua umeumia kwa muda mrefu, nina imani kama uliteseka juu yangu basi penzi letu litakuwa lenye upendo wa dhati. Mose mpenzi naomba usinitende.”
“Teddy amini nitakupa mapenzi zaidi ya kaka, hutajutia kunikubali kuwa mpenzi wako.”
Siku ile ilikuwa yenye furaha kwa Mose lakini moyoni kwa Teddy ilikuwa ngumu sana kwake kwa kujipanga kuhakikisha kujirahisi kule kutamlahisishia kummaliza kwa urahisi. Teddy hakuona hiyana kuutoa mwili wake kwa Mose japo alikwisha muapia labda atafanya naye mapenzi akiwa marehemu asiye na fahamu.
Siku ile alijitoa ili kumvuta karibu na kuamini kabisa anachokitafuta muda mrefu atakipata. Majira ya mchana Teddy alibuku tiketi ya ndege ya kuelekea Turin saa tatu usiku, baada ya kurudishiwa taarifa ya kupatikana kwa nafasi katika ndege ya usiku ule.
Alijipanga kuhakikisha mipango yake inakwenda kama alivyopanga na saa tatu awe kwenye kiti cha ndege akihamia jiji wa Turin kuanza maisha mapya baada ya kummalizia mbali shemeji yake Mose aliyetaka kumpoteza kwenye ramani ya dunia.
Baada ya mambo yake kwenda alivyopanga alirudi kwa Mose na kuendelea kunywa katika mahaba mazito. Mose baada ya kulewa sana Teddy alitumia nafasi ile kumpeleleza kupata ukweli. “Mose mpenzi wangu kwa nini ulinichoma?” Teddy alijifanya kulalamika katika mahaba mazito.
“Teddy ulinichanganya kimapenzi kwa kweli nilichokifanya hata sielewi nilifanya nini, nilikuwa sawa na mfa maji.”
“Lakini usirudie tena, ona sasa kama ningefungwa penzi tamu kama hili ungelipata wapi?”
“Nisamehe mpenzi wangu.”
Kauli ya Mose ilizidisha machungu moyoni kwa Teddy na kuamini wazo lake na ushahidi aliopata lilikuwa sahihi.
Alijitahidi kutengeneza tabasamu la uongo ili kuvuta muda wa kummaliza Mose. Muda wote alionesha mapenzi mazito yaliyomziba masikio asijue nini kilichokuwa kikiendelea.
Itaendelea Jumatatu
 
SEHEMU: 22
MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
SIMU: 0713 646500

ILIPOISHIA:
Kauli ya Mose ilizidisha machungu moyoni kwa Teddy na kuamini wazo lake na ushahidi aliopata lilikuwa sahihi. Alijitahidi kutengeneza tabasamu la uongo ili kuvuta muda wa kummaliza Mose. Muda wote alionesha mapenzi mazito yaliyomziba masikio asijue nini kilichokuwa kikiendelea. SASA ENDELEA...

Majira ya saa moja na nusu Teddy aliamini ule ulikuwa muda muafaka kwake kufanya alichokikusudia, hakutaka kumuua Mose kwa bastora kwa kuhofia sauti yake unaweza kufika mbali.
Kwa vile alikuwa amefunga dirisha la chumbani na kuamini sauti haitatoka nje aliona kisu kingefanya kazi yake vizuri kutokana na Mose kulewa sana asingeweza kushindana naye. Wakiwa watupu kitandani Teddy alisema kwa sauti ya mahaba: “Samahani mpenzi.”
“Bila samahani,” Mose alijibu kwa sauti ya kilevi.
“Nakuja mara moja,” Teddy alisema huku akinyanyuka kitandani.
“Basi usichelewe mpenzi, leo moyo wangu una furaha ya ajabu.” “Usihofu leo mimi na wewe mpaka lyamba.”
Teddy alikwenda hadi kwenye kabati na kuchukua kisu kikubwa na kurudi nacho kitandani. Wakati huo Mose alikuwa amejilaza chali akiwa amefumba macho kutokana na kunywa kiasi kikubwa cha pombe. Teddy alimkalia tumboni kama anataka kumuandaa kimahaba. Kwa sauti iliyojaa ukatili isiyo na chembe ya huruma alisema: “Wee mbwa Sali sala yako ya mwisho.”
“Vipi tena mpenzi?” Mose aliuliza huku alijitahidi kufumbua macho yaliyokuwa mazito kutokana kunywa pombe nyingi kupita kiasi. Macho yake hayakuamini kuona Teddy amemshikia kisu.
“Ha! Nini tena?” “Unauliza jibu, nilikueleza nini siku moja?”
“Mpenzi mbona sikuelewi.”
“Nilikueleza toka mwanzo kuwa hutaugusa mwili wangu labda maiti yangu, lakini leo umeugusa nikiwa mzima ni ishara ya kifo chako.” “Kwa hiyo unataka kuniua?”
“Si ulitaka kunipoteza? Sasa nakupoteza wewe.”
“Si..si..nimekueleza sa..sa..babu yake,” Mose alijitetea akiwa bado amelala chali mwili haukuwa na nguvu kutokana na kulewa sana.
“Fedha yote niliyopoteza baada ya kukamatwa itanunua kifo chako,”
Teddy alisema huku akikipunga kisu hewani.
“U..u..usi..ni..”
hakumalizia alikutana na mapigo ya kisu mfululizo yaliyompiga bila mpangilio.
Teddy alimshambulia Mose kwa visu mfululizo kama anatengeneza chujio la nazi. Mose kutokana na ulevi wa kupindukia hakuweza kujitetea.
Baada ya kupiga kelele za maumivu kwa muda bila msaada sauti ilizidi kupungua mpaka aliponyamaza kabisa, wakati huo kitanda kizima kilikuwa kimejaa damu kama kachinjwa ng’ombe ambazo zilizomrukia Teddy mwilini.
Teddy baada ya kuamini amemaliza kazi, alinyanyuka na kukimbilia bafuni kuoga kisha alibadili nguo na kuchukua vitu vya muhimu na kuhakikisha picha zake zote ameondoka nazo. Baada ya kubeba mizigo yake alikodi gari hadi uwanja wa ndege.
Alifika ikiwa imebakia nusu saa ndege iondoke, baada ya kupima mizigo alielekea kwenye ndege na kuketi huku akiomba Mungu aondoke kabla ishu haijashtukiwa. Hakujiamini mpaka ndege alipoondoka katika jiji la Sicily, safari yake ilikwenda vizuri mpaka alipotua katika jiji la Turin salama salimini. Alitafuta hotel yenye hadhi ya nyota tano iitwayo Principi di Piemonte.
Baada ya kupata chumba aliagiza chakula na kula kidogo kwani bado picha ya kitendo cha kinyama alichomfanyia shemeji yake ilijirudia akilini mwake. Aliamua kuagiza pombe kali ambayo alikunywa mpaka alipopoteza mawasiliano na kulala alipokuwa amekaa. Alishtushwa siku ya pili na hodi iliyokuwa ikigongwa.
Alishangaa kujikuta amelala pembeni ya kitanda kwenye zulia. Aliponyanyuka alizidi kujishangaa kukuta haja ndogo aliimalizia pale bila kujielewa kutokana na kunywa pombe nyingi kupita kiasi.
Alinyanyuka na kukimbilia bafuni na kuchukua cha kufutia kisha alifungua mlango.
“Za saizi?” mhudumu alimsalimia. “Nzu..nzuri, karibu.”
“Asante, nilikua naomba kufanya usafi.”
“Kwani sasa hivi ni saa ngapi?”
“Saa tano.” “Ooh! Kumbe nimelala sana.”
“Inaonesha ulikunywa sana.”
“Okay, fanya haraka usafi nataka kupumzika.”
Teddy alimwacha mhudumu afanye usafi, baada ya kufanya usafi alioga na kuagiza kifungua kinywa kisha alizimua kidogo. Akiwa amejipumzisha kwenye sofa huku akinywa whisky taratibu, tukio la jana yake lilimjibu kwenye akili na kujikuta akiwasha luninga labda habari za kifo cha Moze kitatangazwa.
Alifungua luninga ya taifa, alikuta kuna matangazo ya magazeti na moja ya habari iliyotawala kwenye ukurasa wa mbele ilikuwa yake. Kichwa cha habari kilisomeka unyama wa kutisha, juu kulikuwa na picha ya Mose akiwa amelala kitandani mwili wote ukiwa katika dimbwi la damu.
Picha ile ilimtisha alijikuta akifumba macho kwa woga na kuchukua chupa ya whisky na kuipeleka mdomoni kwake na kujaza kiasi kikubwa na kukimeza chote kwa shida huku amefumba macho mpaka mishipa ya kichwa ikamsimama, baada ya kutikisa kichwa alisema kwa sauti ya chini.
“Ooh! Mungu wangu, nimemuua Mose kifo kibaya sana.”
Akiwa ameinamisha kichwa huku akisikitika na machozi kumtoka kutokana na unyama aliofanya, alinyanyua macho na kushtuka kuona Mose hakufa yupo hospitali ila katika chumba cha wagonjwa mahututi. Akiwa bado anatumbulia macho habari za Mose ambaye alionekana mfu.
Alimuona mkuu wa makosa ya jinai akitoa taarifa kuwa mpaka muda ule upelelezi ulikuwa unaendelea ili kujua nani aliyefanya tukio la kikatili kama lile baada ya kukosa ushirikiano wa mgonjwa ambaye alikutwa katika hali mbaya mpaka wakati ule alikuwa akipumua kwa mashine. Taarifa za daktari zilisema mgonjwa kutokana na kupoteza damu nyingi kutokana na kutobolewa na kitu chenye ncha kali aliongezwa damu zaidi ya chupa kumi.
Habari zile hazikumfurahisha hata kidogo Teddy na kuamini kama Mose atapona na kutoa ushahidi basi atamtia kwenye matatizo makubwa na akishikwa adhabu yake ni kifo. Wazo la haraka lilikuwa kuondoka ndani ya nchi ya Italy na kwenda kuishi Afrika kati ya nchi ya Tanzania au Kenya. Aliamini upelelezi lazima utajua kuwa ni yeye mhusika aliwasiliana na washirika wake na kukubaliana akajifiche Kenya mpaka hapo mambo yatakapojulikana yamefikia wapi.
Bila kupoteza muda alipanda ndege moja kwa moja mpaka Kenya na kwenye kujificha katika jiji la Nairobi katika jumba moja la mshirika wao lililokuwa na kila kitu ndani maeneo ya Kasalani. Mwezi mmoja akiwa anaishi kwa kificho katika jiji la Nairobi aliziona habari na picha yake za kutafutwa kwake kuhusiana na jaribio la kutaka kumuua Mose.
Baadhi ya vyombo vya habari na luninga alitoa kila siku sura ya Teddy kutafutwa huku donge nono likitangazwa kwa mtu atakayetoa habari zake na kufanikisha kukamatwa. Taarifa zile zilizidi kumficha Teddy ambaye alikuwa akitoka usiku tu kwenda club za usiku na baada ya hapo alishinda ndani tu. Aliweza kumuona Mose katika hali ya umajeruhi kutokana na shambulio kali la kutaka kumuua.
Mwili wake ilionesha kuharibika vibaya hata kuzungumza kwake alizungumza kwa shida. Katika mahojiano na mwandishi wa habari mmoja alimsikia akisema kuwa akipona atamtafuta popote hata kaburini ili kulipa kisasi.

****
Majira ya saa sita za usiku Kinape alijirudisha nyumbani kwa kuamini muda ule Kilole atakuwa amelala. Alipokaribia nyumbani aliona teksi ikisimama mbele kidogo na nyumbani kwao. Aliendelea kusogea kwa vile alikuwa upande wa giza aliweza kuliona lile gari ambalo hata namba zake hazikuwa ngumu kuzinakili kichwani.
Kabla ya kupiga hatua alishangaa kumuona mwanamke aliyevaa hijabu na nikabu iliyomziba uso wake akitelemka kwenye teksi na kuelekea kwenye geti la nyumba yao na gari ile kuondoka. Alijuliza ni nani aliyevaa vazi lile kuelekea kwao muda kama ule. Ilibidi atembee kwa taadhari ili kujua yule mwanamke anakwenda kufanya nini kwao muda ule.
Alisimama nje ya uzio na kuweza kumuona yule mwanamke akifungua mlango kwa taadhari kubwa, alijiuliza yule mwanamke ni nani au mwizi. Hakutaka kumshtua alitulia kutaka kuona mwisho wake, lakini kilichomshangaza kilikuwa kufungwa mlango kwa ndani. Moja kwa moja alijua yule ni Kilole, lakini swali lilikuwa usiku ule anatoka wapi na katika vazi lile ambalo hakuwahi kuliona hata siku moja.
Hakutaka kupitia mlango wa mbale alizunguka nyuma na kuingia chumbani kwake kwa kutumia dirisha. Mara zote anapojua anachelewa kurudi alilitegesha dirisha na aliporudi aliingilia kupitia dirishani.
Baada ya kuingia ndani alibadili nguo na kwenda kuoga na kurudi kulala ili alfajiri awahi kuamka kabla Kilole hajaamka. Alikumbuka muda wote alizima simu ili kumkwepa Kilole asimsumbue, alipowasha haikuchukua muda simu iliita. Ilikuwa simu ya dada ya mchumba wake, aliipokea. “Haloo shemu.”
“She..she..mu,” hakuendelea kuzungumza alivuta kamasi za kilio kitu kilichomshtua Kinape na kutaka kujua kuna nini, kwani simu ilikuwa hewani kwa mbali alisikia sauti kama za vilio.
“Haloo shemu,” aliita lakini upande wa pili haukupokea zaidi ya kuendelea kusikia vilio vya upande wa pili.
Aliamua kukata simu na kupiga, iliitaka kwa muda mfupi ilipokelewa upande wa pili na dada ya mchumba wake.
“Shemu upo wapi?” aliulizwa.
“Nyumbani.”
“Una habari gani za Happy?” “Sina! Amefanya nini?” alishtuka.
“Amefariki.”
“Nini?” Kinape alishtuka. “Amefariki,” kauli ile ilirudiwa. “Muongo acha kunirusha roho shemeji.”
“Si kukurusha roho ukweli ni huo mchumba wake ameuawa saa mbili zilizopita.”
“Hapana sikubali Happy hawezi kufa kirahisi namna hiyo nimeachana naye jioni akiwa na mzima wa afya.”
“Hakufa kwa ugonjwa.”
“Nini kimemuua mpenzi wangu?” “Ameuawa.”
“Nini?”
“Ameuawa.”
“Na nani?”
“Hatujajua ile sasa hivi tunaupeleka mwili wa Happy hospitali.”
“Nakuja sasa hivi.”
Kinape alikata simu na kujikuta akichanganyikiwa kwa kuvaa fulana na taulo. Alikwenda moja kwa moja kugonga katika mlango wa Deus kumjulisha taarifa za mchumba wake Happy.
Aligonga mlango kwa muda, Deus aliyekuwa kama yupo ndotoni alishtuka na kunyanyuka hadi mlango. Alipofungua alikutana na Kinape aliyekuwa akitokwa na mchozi na macho yalikuwa mekundu kuonesha ana tatizo zito.
Deus alishtuka na kutaka kujua rafiki yake kipi kimemsibu usiku mkubwa kama ule.
“Best vipi?” Kinape alishindwa kuzungumza alijitupa kifuani kwa Deus na kuangua kilio bila kusema neno.
“Best kuna nini?”
“Happy.”
“Happy amefanya nini?”
“Amefariki.”
“Wewe! Acha utani, si leo asubuhi mnakwenda kijijini?” Deus alishtuka na kumshika Kinape mabegani na kumsogeza mbele yake ili kumtazama vizuri.
“Ndiyo, lakini nimepigiwa simu muda huu amefariki.”
“Alikuwa akiumwa?” “Hapana.”
“Nini kimemuua?”
“Na..na..sikia.. ameuawa.” “Ameuawa! Na nani?”
“Hata wao hawajui.”
“Mwili wa marehemu upo wapi?” “Wameniambia ndiyo wapo njiani kuupeleka hospitali.”
“Unasema kauawa, kivipi?”
“Hata najua, nakwenda kujua huko huko.”
“Nisubiri basi tuongozane.”
Deus alirudi chumbani kumjulisha mkewe habari za Happy.
“Mke wangu,” alimwita huku akimtikisa.
“A.aa..bee mume wangu.” “Kuna tatizo limetokea.” “Tatizo gani tena?” Kilole aliuliza huku akifikicha macho. “Happy amefariki.”
“Nini?” Kilole aliuliza kwa mshtuko. “Happy amefariki.”
“Acha utani, Happy mchumba wa shemeji Kinape?”
“Ndiyo.”
“Muongo, si kesho wanakwenda kijijini kumtambulisha?”
“Ndiyo.”
“Nini kimemuua?”
“Nasikia ameuawa saa mbili zilizopita.”
“Sasa inatakuwaje, kwani Kinape yupo wapi?” “Yupo ananisubiri twende hospitali.”
“Sasa hospitali kufanya nini ikiwa mnasema amekwisha kufa?”
“Wamesema wanaupeleka mwili wa marehemu.”
“Kwa hiyo twende wote?”
”Hapana nilikuwa nakutaarifu tu.”
Wakati Deus akibadili nguo ili awahi hospitali, Kilole alitoka nje na kilio hadi kwa Kinape na kujitupa kifuani kwake.
“Maskini shemeji yangu nini kimemsibu mke mwenzangu?”
“Ha..ha..ta sijui.”
“Kinape tuwahi nipo tayari,” Deus alisema huku akimtoa Kilole kifuani kwa Kinape.
“Okay twende.”
“Mbona hujabadili nguo?”
“Mbona nipo sawa.”
“Sasa utakwenda na taulo?”
Kinape alipojiangalia akijikuta amejifunga taulo, alikimbilia ndani kubadili kisha walitoka kuwahi hospitali.

Itaendelea Jumatano
 
SEHEMU: 23
MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
SIMU: 0713 646500

ILIPOISHIA:
“Kinape tuwahi nipo tayari,” Deus alisema huku akimtoa Kilole kifuani kwa Kinape.
“Okay twende.”
“Mbona hujabadili nguo?”
“Mbona nipo sawa.”
“Sasa utakwenda na taulo?” Kinape alipojiangalia akijikuta amejifunga taulo, alikimbilia ndani kubadili kisha walitoka kuwahi hospitali.
SASA ENDELEA...
****
Walipofika walikuta mwili wa Happy ndiyo umefikishwa muda mfupi ukiwa bado upo katika gari la polisi, dada yake Happy alipomuona Kinape alimkimbilia na kujitupa kifuani kwake na kuangua kilio cha sauti.
“Ooh! Shemeji mdogo wangu wamemuua.”
“Hapana si kweli Happy hawezi kufa kirahisi namna hiyo,” Kinape alisema kwa sauti ya juu huku akimkumbatia shemeji yake.
“Kweli mdogo wangu amekufa, yaani wamemuua kama jambaziii...amewakosea nini mdogo wangu mimiii,” dada yake Happy aliendelea kulia akiwa bado amejilaza kifuani.
Wakati huo kitanda cha kuuchukulia mwili wa Happy uliokuwa umefunikwa shuka kilikuwa kimesogezwa karibu kabisa na gari la polisi.
Kinape alijitoa kwenye mikono ya dada yake Happy na kwenda kwenye gari la polisi wakati huo askari walikuwa wakiushusha mwili wa Happy uliokuwa ulifunikwa na shuka jeupe lililojaa damu.
Baada ya kuulaza mwili juu ya kitanda cha magurudumu, Kinape alisogea karibu kabisa akiwa bado haamini kama kweli mpenzi wake Happy amekufa. Aliishika shuka upande wa kichwani na kuanza kuifunua huku mikono ikimtetemeka. Macho yake yalikutana na uso wa Happy aliyeonekana kama umelala.
“Happy mpenzi wangu amka,” alimwita kwa sauti huku akimtikisa taratibu.
“Shemeji amekufa mdogo wangu,” dada Happy ambaye alikuwa akilia kuliko watu wote waliokuwa pale alikwenda kuungana na shemeji yake ambaye alikuwa bado akiona kama kiini macho kilichokuwa mbele yake.
“Happy mpenzi wangu amka huwezi kufa kirahisi mpenzi wangu, huwezi kuniacha peke yangu, leo asubuhi tunakwenda kwa wazazi wangu wakakutambue. Hata kaka Deus yupo hapa ametoa gari ili lake la kifahari ili nikupeleke kijijini...Amka mpenzi amka ni wewe peke yako niliyekuchagua... Hapiiiiiiiiii,” Kinape alimtikisa kwa nguvu ili aamke lakini mwili ule haukuwa na uhai. Kinape alilia kwa uchungu, Deus alimchukua na kumuondoa kwenye kitanda na kumpeleka pembeni kumbembeleza.
“Deus niache huu ni unyama wa hali ya juu, inaniuma kwa nini wamuue mpenzi wangu nimewakosea nini?” alisema huku akipiga chini. “Pole rafiki yangu, kazi ya Mungu haina makosa.” “Noooo, hapana hii si kazi ya Mungu ni mashetani wasiopenda kuona Kinape na Happy wanaoana.”
“Basi...basi, wewe mwanaume unatakiwa kuyashinda maumivu ya moyo wako,” Deus aliendelea kumbembeleza. “Yaani Happy...hata siamini haiwezekani Happy hajafa,” Kinape alimponyoka Deus na kukifuata kitanda kilichokuwa kikielekea chumba cha uchunguzi kabla ya kupelekwa Mochwali. Alichepua mwendo huku akimwita kwa sauti kama anamsikia, lilikuwa pigo mujalabu ambalo hakulitegemea kipindi kile.
“Jamani mnampeleka wapi mpenzi wangu, Happy hajafa amelala mwambieni aamke leo asubuhi nakwenda kumtambulisha kwa wazazi,” kifo cha ghafla cha Happy kilimchanganya Kinape na kuonekana kama chizi. Lakini Deus alimuwahi na kumketisha chini rafiki yake.
“Kinape hebu kuna kuwa na moyo wa kiume.”
“Siwezi, siwezi Deus inauma sana.” “Najua inauma lakini imekwisha tokea kinachotakiwa kutafuta chanzo cha kifo chake.”
Baada ya kuufanyia uchunguzi mwili wa Happy alipelekwa mochwali kwa ajili ya kusubiri kuchukuliwa na kwenda kuzikwa.
****
Kilole alijikuta akijigeuzageuza kitandani akiyakumbuka matukio yote aliyoyafanya usiku ule. Moyo ulimuuma kwa kitendo cha kikatili lakini hakuwa na jinsi ilikuwa lazima afanye vile ili kupata anachokitaka. Matukio yalipokuwa yakijirudia kichwani alikwenda hadi kwenye friji ndogo ya chumbani na kuchukua chupa ya pombe kali na kunywa glasi nzima.
Baada ya kunywa alijikuta akipitiwa na usingizi na kujilaza nusu ya kitanda, Deus aliporudi toka hospitali alishangaa kumkuta mkewe aliyemwacha amelala akiwa katika hali ya ulevi. Alimshtua toka usingizini kwa kumwita na kumtikisa ili alale vizuri.
“Mke wangu.”
“Tafadhali, mimi sijamuua Happy,” Kilole alikurupuka usingizini baada ya kumuona mumewe amemsimamia mbele yake. “Nani kakuambia umemuua?”
“Sa..sa mahani mume wangu,” Kilole alijibu kwa sauti ya kilevi. “Mbona umekunywa pombe?”
“Hivi kweli Happy amekufa?”
“Kweli amekufa.”
“Basi kila dakika ananijia ndotoni, nikaamua bora ninywe pombe kali nilale fofofo.”
“Ooh! Pole sana.”
“Umefikia wapi?”
“Tumerudi kila kitu kitakuwa asubuhi ya leo.”
****
Siku ya pili asubuhi wakiwa sebuleni Kilole na Deus wakimsubiri Kinape atoke chumbani ili wawahi msibani huku macho yao yalikuwa kwenye runinga katika taarifa ya habari ya asubuhi ile. Katika taarifa ile ya habari vilitangazwa vifo vya watu watatu vilivyotokea usiku wa kuamkia siku ile waliouawa kwa risasi.
Mmoja wa maiti hizo alikuwemo mchumba wa Kinape, Happy, wengine waliouawa ni Jimmy mpiga picha na rafiki yake Rich. Deus alishtuka kuona na Jimmy amekufa mtu aliyekuwa akimfahamu kwa kumpiga picha nyingi zikiwemo za birthday na mkewe.
Taarifa ya habari ilielezea kwa ufasaha vifo vile kuwa mwili wa Happy ilikutwa nje ya geti la nyuma yao na miili mingine ya wanaume wawili Jimmy na Rich ilikutwa katika chumba cha Jimmy wote wakiwa wameuawa kwa risasi.
Pia taarifa iliongeza kupitia mashahidi majirani wa nyumba ile kuwa usiku wa saa sita walimuona mwanamke mmoja aliyekuwa amevaa hijabu iliyomziba mwili wote aliyeingia mule ndani.
Kwa vile hawakuwa na wasiwasi naye hawakujishughulisha naye lakini baadaye katikati ya usiku waligundua Jimmy hajafunga mlango kitu ambacho hakikuwa kawaida yake. Walipokwenda ndani ndipo walipokuta tukio lile la kutisha. Zilioneshwa picha za Jimmy na Rich zilivyokuwa zimelala kwenye kochi na sakafuni.
Lakini maiti ya Happy haikuonekana kutokana na kuchelewa kwa taarifa kufika kwenye vyombo vya habari. Kinape aliyekuwa ndiyo anafika sebuleni aliliona tukio lile. Kilichomshtua ni picha ya Jimmy.
“Jamani huyu si Jimmy mpiga picha?”
“Ndiye mwenyewe.”
“Mungu wangu na yeye kafanya nini?”
“Tena nasikia muuaji ni mwanamke,” Deus alimwambia Kinape aliyekuwa amesimama nyuma ya kochi waliokalia. “Mwanamke!” Kinape alishtuka.
“Ndiyo, tena alikuwa amevaa hijabu iliyomzima mwili wote.”
“Unataka kuniambia ndiye aliyemuua Happy?”
“Walaa, mume wangu hawakusema yule mwanamke ni muuaji bali ndiye aliyeingia chumbani kwa Jimmy,” Kilole alipinga kauli ya mumewe.
“Kwa nini ujifiche lazima atakuwa muuaji.”
“Jamani tuachane na hayo tuwahi msibani tukajue nini kinaendelea,” Kinape alikatisha ubishani wa mtu na mkewe.
Wote walinyanyuka kuelea nje kwenye gari, njiani wakiwa ndani ya gari kauli ya Deus kuhusiana na msichana aliyemshtumu kuvaa hijabu ilimshtua na kukumbuka jinsi alivyo mshangaa Kilole aliyekuwa amevaa usiku ule. Alijiuliza kama ni yeye aliyefanya mauaji yale alifanya kwa lengo gani. Alizidi kujiuliza kuhusu kifo cha Happy anaweza kuwa pia ni yeye?
*****
Msibani watu walikuwa wengi huku kila mmoja akizungumza la kwake, wengi walikuwa walionekana na huzuni hasa familia ya Happy baba, mama na dada yake ambaye alilia mpaka kupoteza fahamu. Mashoga zake nao walichanganyikiwa kwani walikuwa katika maandalizi ya harusi ambayo walipanga iwe ya kukata na shoka baada ya kuelezwa siku ile ndiyo ilikuwa ya kwenda kutambulishwa kijijini kwa mchumba wake. Kinape naye muda mwingi alikuwa amekaa chini kutokana na kutokuwa na nguvu za kusimama.
Deus alitumia muda wake mwingi kuwa karibu ya rafiki yake kumfariji kwani kila rafiki na ndugu wa Happy walipolia naye aliporomokwa na machozi. Kila aliyekuwepo msibani uso wake ulijaa simanzi nzito kutokana na kifo Happy msichana aliyekuwa bado mbichi pia mwenye malengo mazito katika maisha yake. Lakini ilikuwa tofauti kwa Kilole na wote waliokuwepo msibani, moyo wake ulijaa furaha kwa kutimiza lengo lake la kuweza kuuvunja uchumba wa Kinape na Happy ambao aliamini hautaunganika mpaka mwisho wa dunia.
Wakati watu wakiendelea kulia huku ibada ikiendelea kabla ya kuuchukua mwili wa Happy haujaenda kupumzishwa Kilole alijikuta akivuta kumbukumbu ya matukio ya kikatili aliyoyafanya jana.
Aliamini kabisa kwa Happy alifanya unyama wa hali ya juu, lakini kwa Jimmy na rafiki yake ilikuwa ni kulipa kisasi cha kubakwa kwani aliamini adhabu ya mbakaji Uarabuni au China ni kifo. Pia alikuwa kutimiza kile alichomuahidi Jimmy kama picha zake zitavuja basi angemfanyia kitu kibaya. Aliamini vifo vyao vilibakia simulizi ndani ya vinywa vya watu.
Alianza kukumbuka jinsi alivyotoka nyumbani baada ya kuhakikisha mume wake amelala fofofo baada ya kumwekea madawa kwenye chakula. Kwanza alimpigia simu Kinape ajue yupo wapi kwani alipanga na yeye siku ile naye angelishwa chakula kile na kulala fofofo ili aweze kutoka bila kutiliwa wasiwasi na mtu.
Lakini simu ya Kinape haikuwa hewani ile haikumsumbua sana japo wasiwasi wake aliwaza huenda wapo pamoja na Happy. Baada ya kuvaa vazi lake lililomziba mwili mzima, alichukua bastora ya mume ambayo aliikagua na kukuta risasi za kutosha.
Alichukua na kiwambo cha kuzuia sauti. (bomba linalowekwa mbele ya bastora au bunduki kuzuia sauti) Baada ya kuviweka vitu vyake vizuri alikwenda hadi kwenye bodaboda na kukodi. “Samahani kaka angu, Masaki shilingi ngapi?”
“Masaki ipi?”
“Mwanzoni kutokea Salenda?”
“Kwa vile usiku buku ishirini.”
“Naomba uniwahishe.”
Baada ya kupanda dereva aliondoa pikipiki kwa mwendo wa kasi kidogo, Alipokaribia nyumba ya kina Happy aliomba ashushwe mbali kidogo. Kwa vile muda ule magari hayakuwa mengi alitumia dakika kumi tu.
“Nina imani umewahi?” dereva wa bodaboda alimuuliza huku akipaki pikipiki. “Ndiyo ila naomba unisubiri hapa.”
“Dada mbona unanitisha?” aliogopa kukabwa.
“Hapana kaka yangu, bado kuna sehemu nakwenda, nafika nyumbani mara moja narudi sasa hivi.”
“Na fedha yangu?” “Chuku hii nikirudi tutapatana tena,” Kilole alipa dereva elfu arobaini.
“Poa wahi basi.”
Kilole alichepua mwendo kuwahi nyumbani kwao na Happy ambapo palikuwa na kipande chenye giza kutokana na nyumba za sehemu ile kuachana eneo kubwa. Alipokaribia alitoa simu yake ambayo aliiseti sauti ambayo muongeaji huwezi kuijua sauti yake mara moja hata laini alikuwa ameinunua siku ileile ambayo ilikuwa haijasajiliwa.
Baada ya kujipanga alipiga simu ya Happy ambaye alikuwa amejilaza kitandani akiwaza safari ya kesho yake ambayo alijiuliza sijui itakuwaje atakapo kutana na wazazi wa Kinape mwanaume aliyemkabidhi moyo wake. Happy aliichukua simu yake na kuitazama namba ambayo ilikuwa ngeni kwake, aliipokea. “Haloo.”
“Haloo Happy hongera shosti.”
“Ya nini?”
“Yaani kumbe kesho unakwenda kutambulishwa ukweni hujanijulisha.”
“Lakini hiyo si kwenda kutambulishwa lakini mambo bado, nikirudi kila kitu kitakuwa wazi, lakini mazungumza na wewe bado asijakufahamu sauti yako?”
“Mimi Betha,” Kilole alimdanganya.
“Betha yupi?”
“Happy hilo si muhimu kama hili ninalotaka kukueleza?”
“Lipi tena hilo?” Happy alishtuka na kujiweka vizuri kitandani. “Najua
naweza kuonekana mbeya lakini lazima niseme juu ya tabia za mchumba wako Kinape.”
“Tabia gani?”
“Japo kweli ni mchumba wako lakini si muaminifu, hivi ninavyozungumza yupo nje ya gari tulilokuja nalo na shoga yangu wakilana denda kibaya zaidi ni jirani na nyumba yenu kweli huu ni ustaarabu?” “U..u..unasema?” Happy aliingia kigugumizi.
“Tena kama unaweza wahi uwafumanie ‘live’ ukichelewa hata dakika kumi Kinape ataondoka.”
“Okay, nakuja.”
Happy bila kumweleza mtu alikurupuka kuwahi kumfumania Kinape, wakati huo Kilole alijiandaa kummaliza baada ya kujua anakuja.
Alitoa bastora na kufunga kiwambo na kumsubiri. Mara alimuona akitokeza kwao akiwa na gauni la kulalia bila hata ya viatu kwani aliamini angevaa kiatu angechelewa kufumania.
Kwa vile alikuwa kwenye giza alimuona Happy akisogea upande ule akipepesa macho, alitumia nafasi ile kumpiga risasi mbili za kifuani upande wa kushoto kama alivyoelekezwa na mumewe Deus jinsi ya kuua adui kwa risasi.
Alimuona Happy akiruka kwa nyuma hakutaka kuona kinachoendelea alichepua kwendo huku akiiweka bastora ndani ya hijabu. Alipofika alimwambia dereva wa bodaboda: “Tuondoke.”
“Tunaelekea wapi?”
“Mikocheni B.”

Itaendelea Ijumaa
 
SEHEMU: 24
MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
SIMU: 0713 646500

ILIPOISHIA:
Baada ya msiba Kinape alibakia kwenye kaburi na mpenzi wake ambaye usiku wa jana yake alikuwa naye kabla ya kuagana kuonana alfajiri ya siku ile kwa ajili ya safari ya kijijini. Alibakia ameliinamia kaburi huku msiba kwake ukianza upya.
Deus na ndugu na jamaa walimbembeleza sana mpaka alipokubali kuondoka makaburini. Moyoni aliapa lazima atamshikisha adabu aliyehusika na kifo cha Happ. Mwanzo alikuwa na wasiwasi na Kilole, lakini kilio alicholia kumlilia mchumba wake aliamini kabisa hausiki kabisa.
SASA ENDELEA...
****
Usiku wakiwa nyumbani Deus katika kutafuta vitu kwenye kabati alishtuka kuona kiwambo cha bastola yake kipo kwenye nguo. Alishtuka kwani siku zote hukiweka mbali kutokana na kutotumia sana kutokana na matukio ya kijibizana kwa risasi na wauza madawa ya kulevya kupungua.
Alikichukua na kukinusa kilionesha kimetumika, alijiuliza mbona kinanuka baruti kama kimetumika. Wazo la haraka lilikuwa kuikagua bastola, alipofungua droo alishtuka kuona haipo kama alivyoiweka.
Aliitoa na kuifungua upande wa risasi, alizidi kushangaa baada ya kuzikuta pungufu ya risasi sita. Alijiuliza bila kupata jibu kuwa risasi zile zimekwenda wapi, alinusa mdomo wa mtutu wa bastora na kukuta umetumika.
Alijikuta akipata wasiwasi na kumwita mkewe aliyekuwa sebuleni akizungumza na Kinape ili amulize. Kilole aliingia chumbani bila kujua anaitiwa nini.
Alishtuka baada ya kumuona mumewe ameshikilia bastora na kiwambo chake. Mshtuko wake ulikuwa dhahili ambao ulionekana wazi kwa mumewe.
Mshtuko ule aliuona na kujua kuna kitu anachokijua mkewe kuhusiana na matumizi ya bastola ile. “U..unasemaje mume wangu?” alisita kidogo.
“Nani katumia hii bastola?” alimuuliza kwa sauti ya kiaskari.
Kilole aliamini kabisa akibabaika lazima atakuwa swali la kujibu, alitulia kwa muda akipanga la kujibu mume wake ambaye alionekana amekunja uso alilirudia swali lake la mwanzo.
“Nakuuliza mbona hunijibu nani katumia siraha yangu?”
“Si..si..jui.”
“Hujui ina maana mimi ndiye niliyetumia?”
“Kama hujatumi wewea nani mwingine anaweza kuitumia hiyo bastora, mimi niitumie kwa kazi gani?”
“Hujanijibu nani katumia hii bastola na kiwambo chake pia risasi zangu sita hazipo?”
“Sijui.”
“Mke wangu sitaki utani nieleze ukweli la sivyo leo utanitambua mimi nani, unaweza kuikodisha kwa watu wafanye uharifu ili mimi niingie matatizoni.”
“Mume wangu hiyo imeanza lini, niikodishe ili iweje, nina shida gani mimi?”
“Kama huna shida nani kaitumia, kumbuka vitu vyote vinakaa sehemu ya siri tunayojua mimi na wewe.”
“Kama unataka kufanya lolote juu yangu fanya lakini mimi sijui lolote.”
Kauli ile ilimuudhi sana Deus na kuamini kabisa mke wake anajua kila kitu juu ya matumizi ya bastola ile kutokana na kushtuka alipoingia ndani na kumuona ameshika ile silaha.
Alimsogelea mkewe kumpa kipigo ili aseme ukweli juu ya matumizi ya silaha ile kwa kuamini kabisa kama silaha ile ikikamatwa inatumika vibaya basi lazima yeye ndiye atakaye julikana anafanya mchezo ule na kufia gerezani. Wakati anamsogelea amzabe makofi, simu yake iliita, aliipokea na kuzungumza
“Haloo,” alizungumza huku akitoka nje kutokana na simu kuwa ya kikazi.
Taarifa iliyomfikia alitakiwa uwanja wa ndege mara moja kuna ndege iliyosemekana kuna mtu ana madawa ya kulevya hivyo ilitakiwa akamatwe. Taarifa ile ilikuwa inatoka kwa mkuu wake, alibadili nguo harakaharaka na kupitia vifaa vya kazi na kuelekea mlangoni, kabla ya kutoka alisema:
“Nakwenda nikirudi nikute jibu la sivyo leo humu ndani patachimbika.”
Deus alitoka kutokana na kuchanganywa na matukio ya ndani, alijikuta akimsahau hata Kinape aliyekuwa amejilaza kwenye kochi, alipofika mlangoni alikumbuka hajamuaga rafiki yake aligeuka na kumsemesha Kinape aliyekuwa kwenye dimwi la mawazo mikono kichwani.
“Besti...Besti,” alimwita zaidi ya mara mbili ndipo aliposhtuka. “E..ee.eeh,” Kinape alikuwa kama umeamshwa usingizini. “Unaonekana upo mbali sana?”
“Wee acha tu, hata sielewi kama nitaweza kuidhibiti hali hii mpaka napata mawazo ya kijinga.” “Mawazo gani tena rafiki yangu.”
“Eti nami nijiue nimfuate mpenzi wangu.”
“Wewee! Mawazo gani hayo rafiki yangu, baada ya Happy kuna maisha mengine na farijiko lingine.”
“Ni kweli, siamini kama nitampata kama Happy, Deus yule mwanamke alinipenda mapenzi ya dhati toka moyoni mwake. Nina imani hata kifo chake kinatokana na kulilinda penzi letu.”
“Besti hebu tuache sheria ichukue mkondo wake.”
”Watamkamataje mtu ambaye hajulikani?”
“Mkono wa sheria ni mrefu atashikwa tu amini hilo best.”
Kauli ile ilimtisha Kilole aliyekuwa kwenye mlango wa chumbani akifuatilia mazungumzo. Wasiwasi kumjaa na kuamini kabisa mumewe kutokana na kazi yake ya kijeshi anajua siri nyingi, pengine hata tukio lile anajua yeye ndiye aliyefanya.
Alijikuta akitetemea na kujiona atafia gerezani au kinyongwa, lakini aliendelea kusikiliza kwa kuijificha. Alimuona mume akitoka nje na baada ya muda alisikia gari lake likiondoka.
Alirudi chumbani na kukaa kwenye kitanda kutafuta majibu ya maneno ya mume wake. Aliamini ile ni vita alitakiwa kumuwahi mumewe kabla hajafanya jambo lolote baya, wazo la haraka lilikuwa kwenda kwa wakuu wake hasa yule alimweleza hailewani naye baada ya kuzurumiana fedha za rushwa ya madawa ya kulevya.
Aliamini kupitia yule bwana atafanikisha mpango wake, kwa vile mumewe alisema akirudi akute jibu na yeye aliamini kabisa hakuwa na jibu la kumjibu hasa akizingatia siraha ile anayejua ni yeye na mumewe tu. Aliona kujiepusha na maswali yasiyo na majibu na mwisho wake kujulikana yeye ndiye muuaji ni kutoroka.
Aliamua kutoroka na kwenda kulala nyumba ya wageni ile kesho amtafute yule mkuu wa mumewe na kumweleza kuwa mumewe anajihusisha na dawa za kulevya.
Alijua yule bwana atataka kumkomoa na kuja kufanya upekuzi kwa vile atakuwa amwelekeza lazima atatiwa hatiani. Alichukua baadhi ya nguo za kuvaa kesho na kuziweka kwenye mkoba alimuaga mfanyakazi kwa kumwambia siri ile asimwambie mtu. “Marry hakikisha mtoto amekula vizuri.”
“Hakuna tatizo dada.”
“Na hizi utanunua chochote,” alimpa elfu ishirini.
“Asante dada.” Alitoka hadi sebuleni kumuaga Kinape.
“Shemu nakuja mara moja.” “Hakuna tatizo, wacha na mimi nikalale,” Kinape alijibu huku akielekea chumbani bila kuuliza safari ile ya wapi.
***
Siku ya pili Kilole alifika makao makuu ya kitengo cha kuzuia dawa za kulevya, alimuulizia yule mzee ambaye jina lake alikuwa analijua moja. Baada ya kuingia getini alikwenda mapokezi na kuulizia. “Samahani dada mzee Shamo yupo?”
“Wewe nani yake?”
“Mtu wake wa karibu.”
“Ameingia sasa hivi.”
“Naomba nimuone.” “Subiri,” yule dada alisema huku akinyanyua simu, baada ya kuzungumza alisema:
“ Nenda chumba namba sita.”
Kwa vile hakuwa mgeni sehemu ile alikwenda moja kwa moja chumba namba sita na kugonga mlango.
“Ingia,” sauti nzito toka ndani ilisema. Alizungusha kitasa na kuingia ndani, mbele ya meza kubwa kulikuwa na mzee mmoja aliyekuwa na mvi nyingi kichwani zilizompendeza.
“Karibu mrembo.”
“Asante, shikamoo.”
“Asante, nikusaidie nini?” Kilole alitengeneza uongo huku akiusema hata ugomvi wao, baada ya kumsiliza alimuuliza:
“Una uhakika na usemacho?”
“Mimi si ndiye mkewe sasa unataka uhakika gani zaidi ya huu?”
“Okay, muda si mrefu tunakuja kwako.”
“Asante mzee wangu.”
Kilole aliondoka moyo wake ukiwa mweupe kama seluji, moyoni alijisemea akuanzae mmalize.
Baada ya kuhakikisha kila kitu kimekwenda kama alivyopanga alirudi aliamua kurudi nyumbani kwake akiamini muda ule mumewe atakuwa kazini mpaka arudi jioni angekuwa amekwisha wekwa chini ya ulinzi.
Alipofika nyumbani alishangaa kumkuta mumewe nyumbani kumbe naye hakurudi jana alipoondoka na kurudi asubuhi ile. Japo alipatwa na mshtuko uliofanya haja ndogo imtoke kidogo alijitahidi kuuficha.
“Karibu mke wangu,” Kilole alishangazwa na hali ya mumewe ambaye hakuonesha hasira. Kilole hakujibu alikimbilia chumbani na kuangua kilio kitu kilicho mfanya mumewe amfuate na kumbembeleza.
“Mke wangu bado una yaleyale ya jana?” Deus alimuuliza mkewe kwa sauti ya upole. “Siku hizi hunipendi, nimekuwa mke mwema na muaminifu siku zote za ndoa yetu, lakini bado umekuwa huoneshi nina umuhimu kwako,” Kilole alisema kwa sauti ya kilio cha uongo.
“Mke wangu, kama kimetokea kitu cha tofauti ndani nimuulize nani kama si wewe mke wangu?”
“Ni kweli, lakini kama sijui mimi nitajibu nini, tena ulitaka kunipiga.”
“Ni hasira za mpito lakini baada ya kujua kosa langu niliamua kuliacha, lakini muhimu kuwa na uangalizi mzuri wa vitu vyetu usipovitunza wewe nani avitunze...Halafu lile gari lako linaingia mwisho wa wiki.”
“Usiniambie! Asante mpenzi wangu.”
Kilole alinyanyuka na kumkumbatia mumewe huku akiamini bado ni mshindi na muda si mrefu Deus ataionja joto ya jiwe. Wakati wao wanabembeleza kikosi maalumu cha kupambana na dawa za kulevya kilikuwa nje ya nyumba ya Deus na kugonga hodi. Deus alitoka nje kuwakaribisha alishtuka kumuona mkuu wake mzee Shamo:
“Ooh! Mzee karibu naona leo mmenitembelea.”
Waliingia wote ndani na kuketi kwenye kochi wakati huo Deus alimwita mkewe awahudumie wageni.
“Mke wangu kuna wageni hebu njoo uwasikilize wanatumia nini.” “Tunashukuru, hatuna muda tumekuja kufanya kazi moja hapa kwako.”
“Kazi moja! Ipi hiyo?” Deus alishtuka.
“Nina imani unaelewa vizuri kazi yetu ni nini?”
“Naijua, ndiyo maana hata mimi nimerudi alfajiri kufuatilia mtu mmoja aliyeingiza dawa za kulevya.” “Ni kweli, lakini huwezi kuwa msafi bila kujisafisha.”
“Una maana gani?”
“Kuna msamalia mwema mmoja amesema kuwa wewe unajishughulisha na uuzaji wa dawa za kulevya.” “Mimi?” Deus alishtuka kusikia vile.
“Unashtuka nini, sasa hivi upo chini ya ulinzi na kutuachia kufanya upekuzi.”
“Fanyeni tu, hizi ni njama za kuchafuana lakini kila kitu kitafahamika.”
Deus aliwekwa chini ya ulinzi na upekuzi ulianza mara moja, Kilole alijifanya kushtuka na kuuliza:
“Jamani kuna nini tena?”
“Siyo kazi yako,” Mzee Shamo alijibu kwa sauti kali.
“Jamani mume wangu kafanya nini?” Kilole aliendeleza usanii. “Wee waache, naona kila siku wananichokonoa lakini ukweli utajulikana,” Deus alisema bila kujua bomu lipo ndani litalipuka muda wowote.
“Hebu njoo hapa,” mzee Shamo alimwita Kilole kwa sauti ya ukali. Kilole alimfuata nakumwacha mumewe amekalishwa chini ya ulinzi, alipofika karibu alimuuliza kwa sauti ya chini.
“Kuna mabadiliko?”
“Hakuna kila kitu kipo vilevile.”
“Ipo sehemu gani?”
“Ndani ya kabati.” “Okay,” baada ya kusema vile alisema kwa sauti kali kupoteza lengo.
“Haya na wewe rudi kwa mwendawazimu mwenzako.
” Kilole alishikwa na askari mmoja na kwenda kukalishwa pembeni ya mumewe, upekuzi uliendelea huku Deus akisema kwa hasira: “Yaani mkikosa hicho mnachokitafuta walahi nitazaa na mtu.” “Mume wangu mbona wanakufuatafuata?” Kilole aliendelea kulalamika kiuongo.
“Wee waache, mwaka huu nitakufa mimi au mtu, nimechoka kuchezewa kama mpira,” Deus aliendelea kulalamika kwa hasira.
“Wee piga kelele utanyamaza muda si mrefu,” mzee Shamo alisema huku akiendelea kufanya upekezi wa uongo kabla hawajafanya kilichowapeleka pale.
Baada kutafuta sehemu nyingine mwisho waliingia chumbani na kufungua kila sehemu na mwisho walichukua briefcase iliyokuwa ndani ya kabati na kuifungua. Ndani ya briefcase kulikuwa na dawa za kulevya zilizokuwa ndani ya mifuko, mzee Shamo alisema kwa furaha:
“Amekwisha, hapa hata ateremke masihi kumtetea hatoki.”
Waliibeba na kutoka nayo hadi sebuleni na kuifungua mbele ya Deus.
“Nilikueleza mapema kuwa huwezi kuwa msafi bila kujisafisha.”
“Hiyo nini?” Deus alitaka kunyanyuka kwa hasira lakini alitulizwa na siraha zilizokuwa zimemtazama. “Deus umekwisha, nilikueleza toka zamani kuwa wewe mtoto mdogo huwezi kushindani na mimi, kwa hili utafia gerezani.” “Muongo mkubwa huwezi kuja kuniwekea madawa ili kunitia hatiani, lakini nikitoka nitakuua nakuapia,” Deus alipagawa kuona ndani briefcase yake kuna madawa ya kulevya.

Itaendelea Jumatatu
 
SEHEMU: 25
MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
SIMU: 0713 646500

ILIPOISHIA:
“Nilikueleza mapema kuwa huwezi kuwa msafi bila kujisafisha.” “Hiyo nini?”
Deus alitaka kunyanyuka kwa hasira lakini alitulizwa na siraha zilizokuwa zimemtazama.
“Deus umekwisha, nilikueleza toka zamani kuwa wewe mtoto mdogo huwezi kushindani na mimi, kwa hili utafia gerezani.”
“Muongo mkubwa huwezi kuja kuniwekea madawa ili kunitia hatiani, lakini nikitoka nitakuua nakuapia,” Deus alipagawa kuona ndani briefcase yake kuna madawa ya kulevya.
SASA ENDELEA...

“Jamani tuondoke naye kazi yetu tumemaliza, tunawaachia serikali watafanya nini sisi tena haituhusu.” Deus alitiwa pingu na kutolewa nje kama mhalifu huku Kilole akilia mpaka akagaagaa chini kwa ajili ya kumlilia mumewe, kitu kilichomshtua mzee Shamo na kujiuliza ndiye yule aliyeleta habari za mumewe au mwingine. Deus kabla ya kuondoka alimwambia mkewe. “Nenda kwa Mambo Twalipo mwambie habari hizi, sawa.”
“Sawa mume wangu lakini hizo dawa lazima wamekuwekea sisi hatuuzi dawa.” “Itajulikana wewe nenda asubuhi hii.”
“Sawa, Kinape yupo wapi?” “Ooh! Kweli alikwenda ofisini kwake, atarudi muda si mrefu, akirudi mweleze na yeye ashughulikie suala hili.”
Deus alipelekwa polisi na kufunguliwa mashtaka ya kujihusisha na kuuza dawa za kulevya.
Kilole pamoja na kupanga mpango ule alijikuta akijutia uamuzi ule wa kumfunga mumewe kwa ajili ya Kinape. Baada ya kuondoka mumewe alijikuta akilia mpaka macho yalivimba lakini bado aliamini alichokifanya kilikuwa sahihi upande wake.
****
Upande wa pili Teddy msichana hatari wa kuuza dawa za kulevya akiwa mafichoni Nairobi Kenya aliwasiliana na washirika wake waliokuwa tayari na mzigo wa kuingiza nchini Tanzania. Baada ya kupewa taarifa zile alimpigia simu Deus kuwa mzigo upo tayari, kwa vile alikuwa na uhakika na kazi yake, alimweleza awaeleze waje. Teddy naye aliwaeleza washirika wenzake wawili waliokuwa wamekuja na mzigo kidogo wa majaribio waingie nao. Hata asubuhi alimpigia kumweleza jamaa wapo njiani naye Deus alimtoa wasiwasi kuwa kila kitu kitakwenda kama kilivyopangwa. Lakini bahati mbaya kabla jioni haijaingia Deus aliangukia kwenye mikono ya polisi na kuwekwa mahabusu kusubiri kufikishwa mahakamani. Akiwa mahabusu alisubiri mtu aje amtume kwa vijana wake kuhusu mzigo utakaoingia jioni ya siku ile.
Haikuwa hivyo baada ya kukamatwa mkuu wao vijana wake wote walio chini yake walibadilishwa eneo la kazi, uwanja wa ndege waliwekwa askari wapya. Habari zile zilimkata maini Deus na kuona kama watu wake wakikamatwa atazidi kujiongezea matatizo kutoka kwa wauza dawa za kulevya ambao hawakuwa na dogo.
****
Majira ya saa moja jioni ndege ya shirika la Qatar iliwasili jijini, katika abiria waliotua siku hiyo walikuwemo washirika wawili wa Teddy. Wakati huo Teddy alikuwa ameishapiga simu zaidi ya mara kumi kumtafuta Deus. Mwanzo simu iliita bila kupokelewa na mwisho wake haikupatikana tena.
Pamoja na kumkosa hewani Deus, Teddy aliamini kutokana na makubaliano ya asubuhi lazima angekuwepo uwanjani. Baada ya ndege kufungua mlango. Tonny na Moppy walitoka taratibu wakiamini wapo kwenye mikono salama ya Deus.
Hata mizigo yake ilipowekwa pembeni hawakuwa na wasiwasi kwa kujua ndiyo njia ya kuwatoa kiwanjani salama. Kumbe siku hiyo kulikuwa na usimamizi mpya na mtu waliyekuwa wakimtegea alikuwa akinyea debe.
Walishangaa kuwekwa chini na kupewa kashikashi kisha kuchukuliwa na kupelekwa mahabusu. Walishangaa kutomuona mtu wa kuwasaidia. Washirika wenzao waliofika kuwapokea uwanjani pale hali ile iliwashtua na kumpigia simu Teddy. “Haloo Teddy, vipi mbona hatuelewi?’
”Hamuelewi nini?”
“Jamaa ameshikwa wapo chini ya ulinzi.”
“Msiwe na wasiwasi watatoka tu,” Teddy alijibu kwa kujiamini.
“Kwa hiyo tufanye nini?”
“Nendeni nyumbani watakuja wenyewe,” Teddy aliamini kabisa Deus yupo.
Kila alipopiga simu ya ya Deus haikupatikana kitu kile kilimtia wasiwasi na kuwaomba waulizie kwa vijana wake mtu anayeitwa Deus. Walifanya vile, lakini jibu lilikuwa hawamfahamu mtu hiyo.
Majibu yale yalimfanya Teddy kichwa kifanye kazi kwa kuwaomba kuwafuatilia kwa mpaka mwisho ili wajue nini kinaendelea. Kutokana na uzoefu na kazi ile walifanikiwa kuwatoa kabla hakujapambazuka, lakini mzigo wao wa fedha nyingi ulipotea. Jamaa walijikuta wakimlaumu Teddy kwa kuwaingiza choo cha kike.
Teddy kitendo cha Deus kumgeuka kilimuumiza sana na kukumbuka kauli aliyomueleza Deus juu ya kwenda kinyume na makubaliano yao. Siku ya pili Teddy alipanda ndege mpaka Dar kumtafuta Deus, alipofika alijitahidi kumtafuta Deus kila kona lakini hakumpata wala habari zake hazikupatikana.
Sehemu zote ya uwanja alimtafuta bila mafanikio, wazo lililomujia ni kumteka sekretary wake ili ajue Deus yupo wapi. Kwa hasara waliyoingia aliapa kumuua kwa mkono wake. Majira ya saa kumi na mbili muda anaotoka secretary wa Deus, ambaye hakuwa mgeni machoni mwake alimuona akiingia kwenye gari na kuondoka.
Baada ya kuondoka waliamua kulifuatilia lile gari kwa nyuma. Kutokana na wingi wa magari ilikuwa vigumu kuweza kumteka kwa urahisi. Waliliacha gari lililombeba yule msichana aliyeoneka yupo na mpenzi wake kutokana na muonekano wao ndani ya gari. Japo vioo vyote walifunga lakini walionekana ndani. Gari lilipofika maeneo ya Mbezi beach iliacha barabara kubwa na kuingia njia iliyokuwa haina rami. Teddy aliliacha gari lile litembee kidogo sehemu iliyokuwa wazi.
Baada ya kuridhika na kile anachotaka kukifanya alikanyaga mafuta na kulipitisha gari kwenye majani kwa mwendo wa kasi kidogo ili kulipita gari alilokuwa amebebwa secretary na kusimama mbele yao kwa ghafla.
Kitu kilichofanya mpenzi wa secretary kuteremka kwa hasira baada ya kumuona aliyefanya mchezo wa kijinga ni mwanamke alimfokea huku akimtishia kumpiga. “Wee malaya unatafutwa bwana.”
“Nani malaya?” Teddy aliuliza akiwa anamsogelea bila wasiwasi wowote. “Wewe hapo,” mpenzi wa secretary alisema huku akimnyooshea kidole. “Bahati yako sina shida na wewe, ungejutia maneno yako ya shombo,” Teddy alisema bila hofu kitu kilichomshangaza Secretary na mpenzi wake na kujiuliza yule msichana ni nani. “Ungeniganya nini?”
“Nakwambia sina shida na wewe nashida na huyu dada, Deus yupo wapi?” Teddy aliyeoneka akijiamini kupita maelezo alimshtua secretary kwa swali lile.
“Deus gani?”
“Bosi wako.”
“Wewe nani unayemuuliza Deus?”
“Umenisahau?” Teddy alisema huku akitoa miwani usoni.
“Siwezi kuwakumbuka wote.” “Dear kwanza mambo ya ofini asubiri kesho,” mpenzi wa secretary aliingilia kati.
“Sikiliza kaka, nakuheshimu hunijui sikujui, naweza kumchukua sijui mkeo na usinifanye lolote na zaidi ya hapo ni kukupoteza kwa sekunde chache. Mimi si mwendawazimu kuja huku,” Teddy alisema kwa sauti ya kukoroma.
“Kwani wewe shida yako nini?” secretary alikuwa mpole kutaka kumsililiza kwani alijua yule dada alikuwa na jambo la msingi. “Shida yangu Deus.”
“Nina imani unajua kazi zetu, hebu nieleze shida yako kwa Deus, naweza kukusaidia.”
“Shida yangu kuonana na Deus.”
“Wewe ni nani kwake?”
“Nina imani unanikumbuka niliisha wahi kuletwa ofisini kwa kosa la kukamatwa na dawa za kulevya na tatizo langu lilichukua muda lakini mwisho wa siku Deus alilimalizia.”
“Ooh! Nimekukumbuka, kwa sasa huwezi kumuona.”
“Kwa nini?”
“Taarifa za Deus nilipata juujuu kuwa ana matatizo makubwa sana ambayo yanaweza kumpotezea kazi na kufungwa.”
“Tatizo! tatizo gani hilo?” Teddy aliuliza huku macho yamemtoka pima.
“Japo si sheria sina budi kukueleza ukweli, Deus jana asubuhi amekamatwa kwake na dawa za kulevya.”
“Muongo mkubwa! Mmeamua kupindisha ili kumkinga kwa kitendo alichonitendea?” Teddy alikuja juu hakukubaliana na taarifa ile.
“Kwa nini unasema hivyo?”
“Juzi nimewasiliana naye na asubuhi ya jana, halafu uniambie eti ana matatizo, usalama wako ni kunipeleka alipo bosi wako la sivyo nitageuka mtoa roho sasa hivi,” Teddy alibadilika na kuwa mwekundu baada ya kuona Secretary akileta ujanja.
“Dada hunijui wala sikujui, lakini Deus yupo kwenye matatizo makubwa sana na sijui kama atatoka salama, majuzi alikesha uwanja wa ndege kikazi na asubuhi aliporudi nyumbani kwake hakutulia alikamatwa kwa kukutwa na dawa za kulevya kwenye briefcase yake.”
“Kwa sasa yupo wapi?”
“Yupo ndani na kesho anapandishwa kizimbani kama unaona nakudanganya njoo kesho mahakamani.”
“Kwa nini alinieleza niingine mzigo?”
“Tatizo hilo lazima nimtetee ilikuwa ghafla, halafu pigo kubwa lilikuwa kubadili askari wote wa uwanja wa ndege. Kwa tatizo lile bado kuna mabadiliko makubwa yanakuja hata mimi sina maisha marefu kwa vile ndiye niliyekuwa mtu wake wa karibu muda wote aliokuwa kazini.
“Hata taarifa za kuingia watu wawili wenye mzigo mimi nilikuwa najua, lakini yaliyotokea walitutisha, kama wangekuwa vijana wake wapo hata mimi ningesimamia kusingeharibika kitu.”
“Una uhakika Deus hafanyi kazi ya kuuza unga?”
“Afanye ile biashara iwe vipi, wakati kila siku anaingiza fedha nyingi kwa hao wauza unga.”
“Unafikiri ni kwa nini amekamatwa na dawa za kulevya?”
“Kuna bosi mmoja haelewani naye ndiye aliyemkamata, watu wote tunajua amembambikia ili kumharibia maisha yake.”
“Huyo bosi wake anaitwa nani?”
“Mzee Shamo.”
“Ni mkubwa wake?”
“Ndiyo.”
“Kwa nini alimfanyia vile?” “Kuna fedha za rushwa ziliingia yule mzee akamzika Deus alipodai ikawa tatizo na kufikia kutishiana maisha. Lakini walimaliza tatizo lao, lakini nashangaa mzee yule alivyommaliza vibaya Deus. Yaani bosi wangu alikuwa mzungu hana tamaa za kijinga kama wazee tunaofanya nao kazi kila kitu wanataka wao.” “Mzee Shamo anakaa wapi?”
“Nasikia yupo Kinondoni lakini sijui ni sehemu gani.”
“Una namba yake ya simu?” “Ninayo.” “Naomba.”
Secretary alimpa namba ya simu, Teddy aliisevu kwenye simu yake na kusema:
“Asante, pia samahani kwa kuwasimamisha kijeshi na kuwapotezeeni muda.”
“Bila samahani kwetu kawaida,” Secretary alijibu.
“Inaonekane kwa shemeji ni ngeni, samahani shemu,” Teddy alimuomba msamaha mpenzi wa secretary. “Kawaida dada yangu.”
“Niwaache mkapumzike, lakini hasira zangu kwa Deus zitaishia kwa huyo mzee sijui Shamo lazima atalipa mzigo uliopotea na ziada sitaki mchezo kwenye kazi yangu.”
“Haya dada siku njema.”
Teddy aliagana na Secretary kwa kuliondoa gari mbele yao na kisha kuligeuza kurudi mjini. Njia nzima alikuwa na hamu ya kuonana na mzee Shamo ili ajue atalipa vipi hasara za kumweka ndani Deus na kuwasabishia usumbufu hasara kubwa. ****
Juhudi za kumtoa ndani zilikuwa tofauti kati Kilole na Kinape, Kilole alimweleza Kinape asipoteze muda kwani kesi ya Deus yenye ushahidi kuweka wakili ni kupoteza muda.
“Sikiliza Kinape fedha tunayotaka kupoteza kumwekea wakili Deus heri tuiweke kwa ajili ya kumsomeshe mwanaye.”
“Japo ameshikwa na dawa ambazo bado siamini kama ni zake, lakini wakili anaweza kupunguza adhabu na kufungwa miaka michache.”
“Kinapeee, acha ujinga dawa zimekutwa ndani kwetu tena ndani ya biefcase yake bado unaona atapona?”
“Anaweza kupona inawezekana zile zilikuwa za ushahidi na si za kuuza.”
“Kinape hata Yesu arudi mara ya pili Deus haponi tena bahati yake ingekuwa Uarabuni angenyongwa.”
“Mbona sikuelewi nakuona kama vile una furahia tukio la Deus kufungwa?”
“Lazima nifurahie kama angesafiri na mzigo ule kukutwa ndani mimi si ndiye ningenyea debe.”
“Lakini hiyo biashara kaianza lini?”
“Muda mrefu ila aliifanya kwa siri hakupenda mtu yeyote ajue hata mimi mwanzo alinificha.”
“Sasa Deus kwa nini anajiingiza kwenye biashara kama ile wakati alikuwa kwenye mradi mzuri wa kuingiza mabilioni bila fedha.” “Ndio hivyo mshika mawili.”
“Lakini bado sikubali nitapigania kuhakikisha Deus anatoka kwa gharama yoyote,” Kinape bado alikuwa na huruma na rafiki yake.
“Kinape usiwe mjinga kwa taarifa yako Deus hatoki, hii ni nafasi ya mimi na wewe kuishi pamoja.”
“Hapana Kilole haiwezekani lazima nimpiganie Deus, mambo yangu yote haya ni kwa ajili yake sitakuwa mwizi wa fadhira.” “Kinape tulizungumza nini?” Kilole alimshangaa Kinape.
”Kuhusu nini?”
“Deus.”
“Kuhusu Deus nini?”
“Si ulinikataza nisimuue tutafute njia ya kumfanya ili tu atupishe tuwe pamoja, nafasi imepatikana unaleta kiswahili kirefu mbona sikuelewi?” Kilole alizungumza kwa lugha ya ukali.
“Pamoja na hivyo lakini tulitakiwa kumsaidia na si kumwacha aangamie, lazima tuoneshe utu katika hili.”
“Lakini kwa nini hutaki kuwa mwelewa, kila kilichotokea nimekifanya kwa ajili yako.”
“Mmh! Una maana huu mpango wa kukamatwa Deus umeufanya wewe?”
“Ndiyo, si ulinikataza nisimuue sasa huu nao unauona mbaya?”
“Kiloleee! Mbona unakuwa na roho mbaya kama mnyama, yaani unamfunga mumeo kwa ajili ya penzi haramu?” Kinape alishtuka. “Kinape kulitafuta penzi lako nimepata dhambi kubwa, hili la Deus mbona dogo.” “Kubwa lipi?”
“Unajua ila ufahamu, kwa Mungu nina kesi ya kujibu juu ya roho za watu watatu niliowaua kwa ajili yako. Ukifanya mchezo wowote Kinape tutawafuata kina Happy.” “Weweee! Unataka kuniambia wewe ndiye uliyemuua Happy?” “Ndiyo.” “Kwa nini?”

Itaendelea Jumatano
 
SEHEMU: 26
MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
SIMU: 0713 646500

ILIPOISHIA:
“Kiloleee! Mbona unakuwa na roho mbaya kama mnyama, yaani unamfunga mumeo kwa ajili ya penzi haramu?” Kinape alishtuka. “Kinape kulitafuta penzi lako nimepata dhambi kubwa, hili la Deus mbona dogo.” “Kubwa lipi?”
“Unajua ila ufahamu, kwa Mungu nina kesi ya kujibu juu ya roho za watu watatu niliowaua kwa ajili yako. Ukifanya mchezo wowote Kinape tutawafuata kina Happy.”
“Weweee! Unataka kuniambia wewe ndiye uliyemuua Happy?” “Ndiyo.”
SASA ENDELEA...

“Kwa nini?”
“Kwa ajili yako, ni wewe uliyesababisha nimuue nilikueleza muachane lakini ndiyo kwanza ulitaka kwenda kumtambulisha kwenu. Niliamini akifika kule sina nafasi ya kuwa na wewe tena.”
“Kiloleee! Kwanini umemuua Happy mtu asiye na hatia kama kosa nimefanya mimi, si ungeniua mimi Happy amekukosea nini?” Kinape alijikuta akitoneshwa donda lililokuwa bado bichi.
“Siwezi kuukata mti wangu wa kivuli, Kinape kumbuka ni wewe ndiye uliyenitoa usichana wangu na ndoto yetu kuwa mke na mume nina imani sasa ndiyo nafasi yetu ya kuwa mke na mume.”
“Lakini si kwa ukatiri na unyama kama huu, kwa nini Kilole umebadilika na kuwa na roho mbaya kiasi hiki!” “Kinape mimi na roho nzuri sana tena yenye huruma lakini nilitetea maumivu ya moyo wangu.
"Ni wewe ndiye uliyesababisha yote kwa kunipiga picha za aibu mimi nilifanya vile kwa ajili ya kuificha aibu ile kumbuka Deus angejua wewe ungekuwa katika hali mbaya tofauti na mimi. Kila ninachokifanya ni kwa ajili yako bado unaniona mpuuzi. ”
“Kwa hiyo unaniambiaje?”
“Wiki hii Deus anapandishwa kizimbani na kuhukumiwa kifungo kikubwa, baada ya kifungo chake kila kilicho chake tunataifisha kama tulivyokubaliana tunauza kila kitu tunahama mji.”
“Mmh! Sawa,” Kinape alikubali kwa shingo upande huku moyoni akiwa na maumivu makali ya kifo cha mpenzi wake Happy.
****
Kikao cha wauza dawa za kulevya kiliendelea chini ya Teddy aliyeoneka mwenye hasira kuliko wote waliokuwepo pale.
“Ehe! Vipi huko ulipokwenda?” Moppy aliyekuwa na uchungu wa mali yake iliyokamatwa jana yake.
“Sikilizeni watu wangu kuna tatizo limejitokeza ambalo ni dhalula ambayo ilikuwa ni vigumu kuiepuka.”
“Kuiepuka vipi Teddy? Usitufanye watoto wadogo,” Moppy alikuja juu kutaka maelezo kamili.
Teddy aliwaeleza kazi aliyoifanya kutwa nzima ya kumsaka Deus na majibu aliyoyapata juu ya Deus kukamatwa jana asubuhi muda mfupi baada ya kuwasiliana.
“Kwa hiyo unataka kutuambia nini?” “Nia yangu ilikuwa kumuua Deus, lakini nimeamini hana kosa hivyo basi mzeee..sijui nani,” alitoa simu yake kuangalia jina kwenye simu na kulikumbuka.
“Mzee Shamo, usiku wa leo anatakiwa kutekwa na kuja kutueleza mzigo wetu tutaupata vipi?” “Tusipoupata tutafanya nini?” Side aliuliza huku akifungua chupa ya Jacky Daniel.
“Hilo si swali, si mnakumbuka Mose shemeji yangu nilimfanya nini, pamoja na kumkosa bado namlia taimingi lazima nilibakishe jina. Na huyu mzee lazima afe kama hana maelezo ya kuridhisha.”
“Teddy una bahati sana, leo nilikuwa nakuulia hapohapo ulipokaa, niliamini kabisa umeniingiza choo cha kike. Niliamini kama wewe ulitaka kumuua shemeji yako niliona nawe ulistahili hukumu hiyo,” Tonny alisema huku akitoa bastora iliyokuwa kwenye jacket iliyokuwa tayari kukatisha maisha ya Teddy.
“Kama ningekuwa nimefanya kwa makusudi ruksa kufanya mtakalo, hata mimi sipo tayari kumsamehe adui yangu,” Teddy alitia nguvu maneno ya Tonny.
Walikubaliana usiku wa siku ile kumtafuta mzee Shamo ili wajue wataupataje Mzigo wao. Baada ya kikao Teddy alimpigia simu mzee Shamo baada ya simu kuita ilipokelewa upande wa pili.
“Haloo.”
“Haloo mzee Shamo, shikamoo,” Teddy alijifanya anamfahamu.
“Marahaba, nani mwenzangu?” mzee Shamo aliuliza. “Najua hunijui ila tukikutana utanifahamu vizuri.”
“Una shida gani?”
“Mzee Shamo haraka ya nini? Tukikutana unajua kila kitu, upo wapi sasa hivi?”
“Sasa hivi nipo Sea Cliff Hotel.”
“Okay, baada ya dakika ishirini nitakuwa hapo.”
“Hakuna tatizo.”
Baada ya kukata simu aliwageukia wenzake waliokuwa wakimfuatilia apokuwa akizungumza.
“Nakuja sasa hivi.”
“Una kwenda wapi?”
“Namfuata yule mzee.”
“Teddy utamuweza peke yako?”
“Akinishinda namtwanga risasi na kutokomea zangu.”
“Noo, usifanye hivyo usitumie hasira kila wakati, nenda na Tonny nina imani mtaweza kumfikisha hapa bila kumwaga damu,” Double D alimtuliza Teddy aliyeoneka amepandwa na mzuka baada ya kuona kifo chake kilikuwa usoni kwake kwa kuoneshwa bastora na Tonny iliyotakiwa kuchukua uhai wake.
Teddy aliongozana na Tonny kumfuata mzee Shamo, moyoni aliapa lazima atampoteza Tonny baada ya kutaka kumuua yeye alipanga kummaliza siku yoyote bila mtu kujua. Waliondoka katika gari moja kila mmoja akiwa na mawazo yake Tonny akiamini kabisa aliyoyasema yameishia palepale, lakini kumbe mwenzake alikuwa na kisasi kikali moyoni mwake. Walipofika nje ya Hoteli ya Sea Cliff, Teddy alimpigia simu mzee Shamo.
“Mzee wangu nimefika.”
“Nipo jirani na mlango wa kuelekea baharini.”
“Sawa nakuja.”
Baada ya kukata simu alimgeukia Tonny aliyekuwa bado yumo ndani ya gari akisubiri maelekezo. “
Tonny mzee anasema yupo karibu na mlango wa kuelekea baharini, sasa fanya hivi.. nenda mpaka eneo lile kisha nibip mimi nitampigia angalia nani anayepokea ili tufanye kazi kwa uhakika.”
“Hakuna tatizo.”
Tonny aliteremka kwenye gari na kuelekea ndani ya hoteli na kumwacha Teddy akigeuza gari na kuliweka vizuri kusubiri kutaarifiwa. Haikuchukua muda simu yake iliita, alipoangalia ilijua tayari Tonny amefika eneo husika. Alipiga simu moja kwa moja kwa mzee Shamo, baada ya kuita kwa muda ilipokelewa.
“Haloo upo wapi mbona sikuoni?” mzee Shamo aliuliza.
“Umesimama wapi?”
“Nipo hapa mbona unaonekana wewe upo wapi?”
“Nipo kwenye mlango wa kuelekea baharini.”
“Mbona mimi nimesimama hapa tena nipo wazi.”
“Okay nimekuona.”
Teddy alikata simu na kumpigia Tonny.
“Tonny umemuona?” “Nimemuona.”
“Msemeshe na muombe utoke naye huku nje.”
“Poa.” Baada ya kukata simu Tonny alimsogelea mzee Shamo na kumsemesha.
“Shikamoo mzee.”
“Marahaba kijana.”
“Nina imani wewe ndiye mwenyeji wetu.”
“Una maana gani?”
“Sasa hivi sister alikuwa akiwasiliana wewe.”
“Eeh! Yupo wapi?” Yupo nje kanituma nikufuate ana mazungumzo na wewe ya dakika tano kisha utaendelea na starehe zako.”
“Hakuna tatizo.”
Mzee Shamo aliongozana na Tonny nje kuelekea upande wa gari lilipokuwa, Teddy alipowaona wanasogea alilisogeza gari, wakati huo Tonny alikuwa ameisha toa bastora na kumuwekea ubavuni mzee Shamo. “Samahani mzee naomba uwe mpole ingia kwenye gari hilo hapo mbele la sivyo nakumwaga utumbo.”
“Jamani kuna tatizo gani?” mzee Shamo alishtuka. “Hakuna tatizo ila tuna mazungumzo ya kirafiki.”
Kwa vile gari lilikuwa limekwisha simama na kufunguliwa mlango mzee Shamo aliingia ndani kisha alifuatia Tonny baada ya kufungwa mlango Teddy aliondoa gari kwa kasi. Baada ya kwendo mfupi walimfunga kitambaa cheusi na gari kupelekwa moja kwa moja ndani ya ngome ya wauza dawa za kulevya. Walipofikisha ndani alifunguliwa kitambaa na kujiona yupo mbele ya watu zaidi ya nane.
“Karibu mzee Shamo,” Double D alimkaribisha kistaabu.
“Asante,” alijibu huku akijenga ujasiri. “Unatumia kinywaji gani?”
“Asante, kwa sasa sihitaji zaidi ya kujua sababu ya kuletwa hapa kama gaidi.”
“Utajua tu mzee wetu, shida yetu kupata mzigo uliokamatwa juzi.”
“Mzigo! Mzigo gani?”
“Juzi kuna vijana wawili walikamatwa uwanja wa ndege na dawa za kulevya, na sababu kubwa ni wewe..”
“Mimi?” Shamo alimkata kauli kupiga tuhuma zile.
“Ndiyo, kumbuka tukio ulilofanya asubuhi ya siku hiyo ndiyo lililoharibu kila kitu, tunajua wewe ni mtu mkubwa tunaomba ule mzigo uurudishe mara moja.”
“Usipoteze muda wenu sijui lolote kuhusiana na hicho mnachosema.”
“Mzee hatutaki tutumie nguvu, tutakuachia usiku huu kabla hakujapambazuka tunataka mzigo uliokamatwa.”
“Sasa mimi nitaupata wapi?” “Utajua mwenyewe la sivyo jina lako litabakia historia.”
“Hata mnipe mwaka mzima siwezi kuwapa kitu kilichokamatwa siku zote uharibiwa pia mimi si mtunza stoo.”
“Kwa hiyo?”
“Sina msaada wowote.”
“Teddy nina imani mzee hana jibu, mrudisheni akaendelee na starehe zake.”
“Hakuna tatizo, kwa hiyo tunamuacha hivihivi tu?” Teddy alihoji.
“Mwacheni tu.”
“Siri yetu si itatoka nje?”
“Haiwezi, kwanza hapa hajui yupo wapi.” Mzee Shamo alifungwa kitambaa usoni na kupelekwa nje kwenye gari, Double D aliwafahamisha washirika wake kwa nini amemuacha huru mzee Shamo.
“Mnajua kwa sababu gani nimeamua kumwacha hai, tukimuua leo lazima tutamuongezea matatizo yule jamaa yetu aliye mahabusu kwa kuamini kifo chake kinatokana na kukamatwa kwake.”
“Aisee, sikuwaza vile ingekuwa mimi ningemuua palepale kwenye kochi,” Teddy alisema. “Yule kifo kipo palepale kutokana na maelezo yote inaoneka kabisa jamaa yetu haponi, kwa vile hana msaada wowote kwetu hatuwezi kumsaidia kwa lolote.”
“Lakini tunaweza kucheza na hakimu.”
“Teddy hata tukimtoa hakuna faida yoyote tutayopata, tusubiri tu akifungwa tumlipie kisasi kwa kuua mbaya wake siamini tuna msaada mwingine zaidi ya huo.”
“Mmh! Sawa.”
Teddy alikubali shingo upande kwa kuamini alitakiwa aonesha naye ubinaadamu kama alivyofanyiwa na Deus alipokamatwa na mzigo. Kwa upande wake asingeweza kumsaidia kutokana na hofu ya kutafutwa baada ya kushindwa kuua shemeji yake.
Baada ya mazungumzo walimtoa mzee Shamo wakiwa njiani kumrudisha walimvutisha dawa ya kulevya zilizomlevya na kulala, kwa vile ilikuwa usiku walimrudisha jirani na hoteli Sea Cliff kumuacha sehemu iliyo salama na kurudi kujipanga upya.

Itaendelea Ijumaa
 
SEHEMU: 27
MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
SIMU: 0713 646500

ILIPOISHIA:
Baada ya mazungumzo walimtoa mzee Shamo wakiwa njiani kumrudisha walimvutisha dawa ya kulevya zilizomlevya na kulala, kwa vile ilikuwa usiku walimrudisha jirani na hoteli Sea Cliff kumuacha sehemu iliyo salama na kurudi kujipanga upya.
SASA ENDELEA...
*****
Mzee Shamo aliokotwa pembeni ya hoteli ya Sea Cliff akiwa hajitambui na kukimbizwa hospitali kupata huduma ya haraka. Alipata nafuu baada ya siku mbili, alijua wale ni jamaa zake Deus ambao alikuwa akifanya nao dili la kuvusha dawa za kulevya.
Lakini alipoulizwa juu ya kuokotwa hajifahamu ilitokana na nini. Alificha kuhofia onyo kali alilopewa na Double D kama ataitoa siri nje basi wangempoteza.
Aliamini kukaa kwake kimya ndiyo salama yake, hivyo kila alipoulizwa mara ya mwisho alikuwa wapi alidanganya alitekwa na watu asiowajua na kujikuta hosipitali. “Unasema walikuteka tu bila kueleza lolote?” Afisa mwenzake alimuuliza.
“Yaani wakati nakwenda kwenye gari langu walitokea vijana na kuniteka na kunitupia kwenye gari lao na kuondoka na mimi, baada ya hapo sikujua kilichoendelea mpaka nilipojikuta hospitalini.”
“Kwa hiyo hawakukusemesha chochote juu ya kukuteka kwako?”
“Hawakunisemesha chochote.” “Sasa kwa nini walikuteka na kukuachia bila kukufanyia lolote?”
“Inaonekana huenda waliniteka kimakosa na kuamua kuniachilia baada ya kugundua si mlengwa.”
“Lakini upo sawa?”
“Nipo sawa, kutokana na maelezo ya daktari nilinusishwa dawa za kulevya tu hakuna kitu kingine kibaya.”
“Hukumbuki hata namba za gari.”
“Kwa vile nilikuwa sijui nini kinaendelea hivyo sielewi chochote.”
Mzee Shamo aliamua kificha siri ile kwa upande wake aliamini ile ni kinga tosha ya wauza dawa za kulevya ya kutommaliza.
***
Deusi alipandishwa kizimbani akikabiliwa na kosa la kukutwa na dawa za kulevya. Upande wa msaada Kinape akiweka wakili wa siri baada ya mkewe Kilole kukataa kutumia fedha zake kumwekea wakili akiamini kabisa hawezi kupona katika kesi ile lazima atafungwa kwani ushahidi wote ulikuwepo. Kutokana na kukosa msaada kwa washirika wenzake kumsaidia Deus katika kesi yake Teddy alijitosa kumsaidia kwa kuongeza wakili mzoefu wa kesi nzito kama zile.
Kwanza alibadili mavazi na kuvaa ya heshima yenye kuuficha mwili wake kisha alijipaka piko kama mwanamke wa pwani vitu vile vilimfanya aonekane mwanamke mstaarabu mbele ya jamii.
“Nahitaji msaada wako Mr Mnyigu ili nimuokoe huyu baba, kesi imemkalia vibaya,” Teddy alimuomba msaada wa wakili wa kujitegemea.
“Kutokana na maelezo ya mtuhumiwa kesi imekaa vibaya hasa baada ya ushahidi kukutwa ndani mwake.” “Nina imani kesi kama hizi umekutana nazo sana, chonde msaidie baba wa watu.”
“Nitajitahidi lakini hii ni kesi nzito hasa kutokana na kushtakiana wenyewe kwa wenyewe kutokana na maelezo yake hii itakuwa mchezo umechezwa hivyo tusipokuwa makini tutaumbuka.”
“Huoni hapo kama unaweza kupata sababu ya kuona ni njama kwa vile kuna rekodi ya kukosana nyuma?”
“Teddy hapo utachekesha, wamekosana kwenye rushwa ya madawa ya kulevya, hilo ni kosa lingine ambalo halitakiwi kusemwa mbele ya mahakama.”
“Sasa tutafanyaje, kuhakikisha tunamwokoa.”
“Labda tuzungumze na mashahidi ambao nasikia ni mkewe na huyo mbaya wake aliyeapa lazima ampoteze.”
“Basi hiyo kazi niachie mimi nitakupa jibu leo usiku au kesho asubuhi.”
Teddy baada ya kuagana na wakili wa kujitegemea Mr Mnyigu alipanga jioni ya siku ile akasikilize mkewe amejipanga vipi kumuokoa mumewe.
*****
Majira ya saa mbili usiku alikuwa nje ya nyumba ya Deus kutokana na maelezo aliyoelezwa hakumpotea nyumba. Ndani ya nyumba kulikuwa na muziki wa rusha roho wa sauti ya juu, ulionesha kama ndani kuna sherehe. Aligonga mlango kwa muda mlango ulifunguliwa na kutoka Kilole ambaye hakuonesha uso wa majonzi.
“Karibu,” Kilole alimkaribisha.
“Asante,” Teddy alijibu huku akiingia ndani. Baada ya kutulia kwa muda akisoma mandhali ya ndani Kilole alimuuliza:
“Ndiyo dada yangu, nikusaidie nini?”
“Nina imani wewe ni mke wa Deus?”
“Mmh! Kwani vipi?”
“Dada nijibu wewe ndiye mkewe au vipi?” “Ndiyo mimi.”
“Mpaka sasa kuna juhudi gani za kumuokoa mumeo?” “Kwa kweli hakuna kwa vile amekutwa na ushahidi kabisa, tunasuburi mahakama itaamua nini.”
“Hata kama amekutwa na ushahidi bado unaweza kumsaidia.”
“Haiwezekani lazima atafungwa mtu kashikwa na ushahidi utamsaidia vipi?”
“Naomba ushirikiano wako, nina sikia wewe ulikuwepo mumewe akikamatwa na hayo madawa?”
“Unaomba ushirikiano gani?”
“Kuhakikisha tunamtoa.”
“Ni vigumu kumsaidia hasa kesi yenyewe ipo mikononi mwa serikali, kama una fedha heri unipe ili nimlee mtoto wake.” “Sikiliza, naomba ukane mahakamani kuwa mumeo hauzi madawa ya kulevya nami nitakuwa nyuma yako.”
“Siwezi kusema uongo, nitafungwa.”
“Huwezi mdogo wangu, wee siku ukipanda kizimbani kutoa ushahidi mteteee mumeo kwa nguvu zote ukisema alikuwa anauza na wewe utakuwemo.”
”Na ule ushahidi?”
“Nitashughulika nao mimi.”
“Kwanza wewe ni nani?”
“Utanijua baada ya kesi.”
“Lakini dada kwa vile nami nilikuwa shahidi namba moja kuona dawa za kulevya kwenye brifcase ya mume wangu siwezi kugeuka lazima nitafungwa.” “Huwezi kufungwa.”
“Nitafungwa, itanibidi niseme ukweli.”
“Hebu kuwa muelewa huwezi kufungwa kwa kutoa ushahidi wa kweli.” “Ukweli si ndio huo wa kuyaona madawa kwenye brifcase ya mume wangu.”
“Mume wako anauza dawa za kulevya?”
“Mmh! Sijui.”
“Hujui nini na wewe ni mke wake?”
“Labda alifanya kwa siri.” “Sasa sikiliza ninachokizungumza sasa hivi si ombo bali amri, ukifika mahakamani kana huyajui madawa yaliyokutwa ndani ya brifcase ya mumeo. Wewe hujui kuwa mumeo na mzee Shamo wana ugomvi?”
“Najua.”
“Sasa kwa nini unakubali mambo kirahisirahisi tu, huoni hizo ni njama za kumpoteza mumeo?” “Sasa mimi akifungwa ananihusu nini?”
“Ni kweli mumeo?”
“Kweli mume wangu, lakini kilanga haliliwi wala hawekewi matanga kila mtu atazikwa kaburi lake.”
“Una ugomvi na mumeo kabla ya tukio hili?” “Hakuna,” wakati huo alikuwa akiingia Kinape ambaye alimsahau Teddy kutokana na mavazi aliyokuwa amevaa.
“Kuna mgeni?” Kinape aliuliza baada ya kuingia.
“Ndiyo, sijui wakili wa Deus,” Kilole alijibu. “Karibu dada yangu.”
“Asante, nina imani wewe ni ndugu yake Deus?”
“Ndiyo.”
“Unanikumbuka?”
“Hataa.” “Naitwa Teddy, najua hujawahi kuniona lakini uliwahi kuisikia sauti hii, uliwahi kutumwa na Deus milioni 75,” Teddy alisema huku akitoa nikabu kichwani na kuweza kuonekana vizuri, Kinape alimkumbuka.
“Ooh! Nimekumbuka, karibu sana.”
“Ndiyo za siku?”
“Nzuri, kama ulivyosikia kaka yupo kwenye matatizo.”
“Najua ndiyo maana nipo hapa.”
“Lakini hali ni mbaya kila sehemu niliyohangaika imeonekana lazima atafungwa.” “Sasa sikilizeni, humu ndani wangapi wameshuhudia yale madawa?”
“Shemeji,” alijibu Kinape.
“Nimemueleza msaada mkubwa katika ile kesi ni kukana hayajui yale madawa ile itasaidia kupunguza ukali wa ile kesi.”
“Lakini kumbuka kuna mkuu wake ndiye shahidi namba moja,” Kinape alisema.
“Hiyo haisumbui, kama ukikana mahakamani kazi nyingine nitajua jinsi ya kuifanya,” Teddy alisema kwa kujiamini.
“Mimi siwezi, nitasema kweli,” Kilole alishikilia msimamo wake baada ya kumuona Kinape.
“Narudia hili si ombi, kaka unajua kazi yangu, kama mkienda kinyume nitawaua wote kwa mkono wangu,” Teddy alitoa onyo kali.
“Uniue mimi?” Kilole alishtuka.
“Ndiyo.”
“Kwa kosa gani?”
“La kumfunga mumeo.” “Sasa mimi nitafanya nini wakati kashikwa na ushahidi?”
“Nakuhakikishieni ushahidi utakuwa wa mtu mmoja, mzee Shamo hata panda kizimbani.” “Kwa sababu gani?”
“Sitaki maswali ila kesho ukipanda kizimbani toa ushahidi huo.”
“Lakin...”
“Sitaki maswali, naondoka ila mkienda kinyume mtageuka adui zangu namba moja, kwa herini.”
Teddy alisema huku akinyanyuka na kuondoka na kuwaacha Kilole na Kinape wakitazamana. Baada ya kuondoka Teddy, Kilole alimuuliza Kinape.
“Yule ni nani?”
“Ni yule msichana muuza dawa za kulevya aliyekamatwa na kutoa milioni 75 na ndiye aliyetaka kututajilisha lakini nashangaa papara yako umetukosesha kila kitu.”
“Hayo si muda wake sasa.”
“Sawa.”
“Sasa huyu mwanamke kesi hii inamuhusu nini?”
“Sijui.”
“Au mwanamke wake?”
“Hapana.” “Nakuhakikishia lazima nimfunge Deus kesi hii hatoki nitasema ukweli na aje aniue.”
“Kilole yaani nakuomba umsikilize yule dada, usimuone vile ni mafia mbaya anaweza kukuua hata palepale mahakamani baada ya kutoa ushahidi wa kumfunga Deus.”
“Sasa tutafanya nini?”
“Kwa nini tusimsaidie Deus?” “Deus tayari amenaswa na ndoano hawezi kuruka.”
“Sasa sikiliza, hata wewe ukikana bado atafungwa, huenda Deus ana wasiwasi na wewe, ukipanda kizimbani kutoa ushahidi ukane ule ushahidi kuwa huujui lakini akija mzee Shamo atamaliza kazi.” “Mmh! Yule mzee atanielewa kweli ikiwa mimi ndiye niliyetengeneza mpango mzima.”
“Fanya hivyo kwa uhai wako yule dada hatanii huenda na mzee Shamo sipande kizimbani.” “Kwa sababu gani.”
“Huenda atapewa fedha au auawe.”
“Mmh! Inatisha itanibidi nifanya hivyo.”
Teddy baada ya kutoka kwa Deus alibadili uamuzi wa kwenda kuonana na mzee Shamo kwa kuhofia kutego baada ya kutendo cha siku chache zilizopita japo hakukuwa na kitu chochote cha kuonesha wanatafutwa.
Alipanga kusikiliza utetezi wa mke wa Deus aliyekuwa akipanda kizimbani kesho na kuhakikisha mzee Shamo hapandi kizimbani kutoa ushahidi siku ya mwisho.

Itaendelea
 
SEHEMU: 28
MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
SIMU: 0713 646500

ILIPOISHIA:
Teddy baada ya kutoka kwa Deus alibadili uamuzi wa kwenda kuonana na mzee Shamo kwa kuhofia kutego baada ya kutendo cha siku chache zilizopita japo hakukuwa na kitu chochote cha kuonesha wanatafutwa. Alipanga kusikiliza utetezi wa mke wa Deus aliyekuwa akipanda kizimbani kesho na kuhakikisha mzee Shamo hapandi kizimbani kutoa ushahidi siku ya mwisho.
SASA ENDELEA...
****
Siku ya pili Kilole alipopanda kizimbani alikana kuyaona yale madawa ya kusema ameyaona baada ya kuitwa chumbani kwake, lakini mume wake hajawahi kuuza madawa yale. Alipoulizwa inawezekana ni njama za watu za kumchafua mume wake, alijibu inawezekana japo hana uhakika.
Majibu ya mke wa Deus yalimshangaza sana mzee Shamo kutokana na yeye kupeleka mchongo ule na kuahidi msaada lakini mwisho wa siku aligeuka kama kinyonga. Kesi iliahilishwa mpaka siku ya pili utakapotolewa ushahidi wa mwisho na mkuu wa kitengo cha kuzuia madawa ya kulevya mzee Shamo. Teddy aliyekuwepo mahakamani alifurahi kuona mambo yamekwenda kama alivyopanga, kazi ilibakia kwake kumaliza kazi. Mzee Shamo alimfuata mke wa Deus na kumuuliza: “Sasa umefanya nini?” “Tutazungumza,” Kilole alijibu kwa sauti ya chini. “Tutazungumza nini, nani aliyeleta taarifa hizi?” “Mimi.” “Sasa kwa nini umenigeuka?” “Lakini wewe si kesho utammaliza.” “Nimmalize kivipi ikiwa umeishapunguza nguvu, wewe ndiye aliyekuwa na kisu kikali cha kumaliza kesi, huoni kama nitabanwa kuwa nimetengeneza kesi?” “Tutazungumza, naomba niondoke eneo hili si salama kwangu.” “Mmh! Nimejua, lakini naapa haponi nitakufa na mumeo.” Kilole aliachana na mzee Shamo aliyemshangaa Kilole kwa kauli yake ya kukana wakati aliapa kutoa ushirikiano wa kutosha na mara ya mwisho usiku kabla ya kukutana na Teddy alimuhakikishia atammaliza Deus. Lakini aliapa lazima ampoteze mbaya wake. Teddy naye alijipanga kuhakikisha mzee Shamo alioni jua la kesho ili kesi ikose nguvu na kumpa nafuu Deus. Baada ya mahakama Kilole na Kinape wakiwa wanajiandaa kuondoka alifika Teddy kwenye gari lao.
“Asante mdogo wangu umenifurahisha sana,” Teddy alimpongeza Kilole aliyekuwa akifunga mkanda wa gari.
“Lakini kazi bure kesho si anapanda mwenyewe hatujafanya lolote,” Kilole alimjibu kwa sauti ya chini.
“Kazi niliyokutuma umeifanya iliyobaki ni yangu, hata akifungwa mumeo hawezi kufungwa miaka mingi.”
“Mmh! Siamini.”
“Nilimuona anakufuata alikuwa anasemaje?”
“Alikuwa akinilaumu kumgeuka.”
“Akamjibu nini?“
“ Sikuwa na jibu.”
“Najua bado atataka kujua kwa nini umemgeuka.”
“Akiniuliza hivyo nimwambieje?”
“Mwambie vyovyote vile, lakini kazi itaisha usiku huu.”
“Umeishazungumza na hakimu?”
“Utajua kesho wakati wa kutolewa ushahidi wa mwisho.”
“Haya wacha niende nikapumzike.”
Kilole aliondoka huku moyo ukimuuma kushindwa kutoa ushahidi wa kumfunga mumewe. Lakini aliamini mzee Shamo anaweza kumfunga mumewe kwa vile ndiye shahidi namba moja.
Mzee Shamo naye alikaa pembeni ya mahakama na vijana wake wakijadiliana juu ya kugeukwa na mke wa Deus mtu aliyefanikisha kukamatwa mume wake.
“Sasa mzee tutafanyaje?”
“Kwa kweli yule mwanamke kanichanganya sana.”
“Sasa tutafanyaje, kesho na wewe ndiye utakayemaliza kutoa ushahidi?”
“Dawa iliyopo ni kumshika na kumtesa aseme ukweli ili kesho niweze kupata nguvu katika ushahidi wangu bila hivyo naweza kuonekana kweli nimeutengeneza. Unafikiri wakili wa Deus akisema kuwa nimetengeneza ushahidi ili nimfunge na mkewe amekataa itakuwaje?”
“Kwa hiyo kazi tuifanye mara moja kabla hajatoka eneo la mahakamani?”
“Hapana anatakiwa akachukuliwe usiku na kupata mateso mazito na kesho atakuja mahakamani akitokea mahabusu.”
“Huoni kama anaweza kusema tumemlazimisha?”
“Kwa hiyo mnanishauri tufanye nini?”
“Mzee inatakiwa tusitumie nguvu tunatakiwa kwanza tujue nini kilichomfanya akugeuke kisha tujue tufanye nini,” kijana mmoja wake mmoja alimpa ushauri.
“Halafu kuna kitu alinieleza kuwa usalama wake ni mdogo pale mahakamani.”
“Inawezekana kuna watu wanashindana na sisi ambao ni miongoni mwetu.”
“Lakini ni yeye aliyeleta taarifa za mumewe kuuza unga sasa anageuka nini kwani tulimfuata?”
“Kwa hiyo mzee wangu tunatakiwa kufanya jambo kisomi kuliko kutumia nguvu. Inawezekana kuna kitu kimeingia katikati si umesema jana usiku uliwasiliana naye na kusema kila kitu kipo sawa.”
“Hata mimi nashangaa.”
“Ukiona hivyo ujue kuna kitu.”
“Basi usiku tutakwenda kujua sababu kipi kilichomfanya ageuke kama kinyonga.”
****
Majira ya saa kumi na mbili Teddy alikuwa amesimamisha gari lake karibu kabisa na ofisi za kupambana na madawa ya kulevya. Aliwahi makusudi ili aweze kumuona mzee Shamo na kumfuatilia. Baada ya kukaa kwa muda majira ya saa moja kasoro aliliona gari la mzee Shamo likitoka ofisini. Aliliacha lipite kisha alilifuatilia nyuma bila mwenyewe kujua.
Mzee Shamo kama kawaida yake alielekea Sea Cliff hoteli, alimfuatilia mpaka alipoingia hotelini. Hakusumbuka sana kumfuata alipaki gari lake pembeni ya gari la mzee Shamo na kumfuata ndani ya baa.
Teddy aliagiza wine na kunywa taratibu huku akifuatilia nyendo za mzee Shamo, majira ya saa mbili walitokea vijana wawili na kuondoka naye. Japo alijua ana kazi nzito lakini hakufanya papara. Aliwahi kwenye gari lake walipoondoka aliwafuata taratibu bila wao kujua wanafuatwa na mtu. Waliondoka eneo lililokuwa na taa na kuingia sehemu ya giza aliamini ile ndiyo nafasi aliyokuwa akiitaka.
Aliongeza kasi kidogo na kuwapita kisha alilisimamisha gari kwa mbele ghafla iliyosababisha gari la mzee Shamo kulikwangua kwa nyuma. Kilole hakuteremka haraka kwenye gari alitulia bila kufungua vioo. Vijana wa mzee Shamo waliteremka kwa hasira ili wamuadabishe mwenye gari ya mbele.
Teddy wakati huo alikuwa amekwisha jiandaa kwa mapigano, bastora yake ilikuwa tayari kufanya kazi.
Walifika na kuanza kutukana huku wakigonga kioo kwa ngumi ili afunge. Wakati huo mzee Shamo naye aliteremka na kusogea. Kwa vile ndani ya gari kulikuwa kiza Teddy aliteremsha kioo kidogo na kuachia risasi zilizowapata wote.
Hakuondoka haraka aliteremka na kuwaongeza risasi ili kupata uhakika kama kweli wamekufa. Baada ya kumaliza zoezi lake alikimbilia kwenye gari ili aondoke kabla ya kuondoka alisikia king’ora cha polisi kilichomshtua.
Alipowasha gari aondoke liligoma kuwaka, aliteremka na kukimbilia sehemu za baharini. Akimbilia na kwenda kujificha nyuma ya mti mkubwa uliokuwa karibu na bahari. Baada ya kujicha alichungulia na kuona gari la doria likisimama eneo la tukio, aliwaona wakiteremka na kuwanza kufanya uchunguzi.
“Aisee kuna watu watatu wamelala chini, tuweni makini,” askari mmoja alitoa taadhali baada ya kuona watu wamelala chini.
“Tena hii gari kama ya Afande Shamo?” askari mwingine alisema huku akimulika na tochi.
“Si huyu!” Teddy alimsikia mmoja akisema kwa mshtuko.
“Nani?”
“Afande Shamo.”
“My God ameuawa?”
“Pigeni simu haraka kuongeza ulinzi hali ni mbaya.”
“Afande wakati tunakaribia hapa niliona kama mtu anakimbilia baharini.”
“Hatuwezi kupambana naye hatujui uwezo wake huenda wapo wengi.”
Teddy alitumia nafasi ile kutembea pembezoni mwa bahari mpaka maeneo ya Daraja la Salenda, alichepua mwendo kufuata barabara ya Ali Hasani Mwinyi kuelekea Mwenge. Mbele kidogo gari dogo lilisimama na kushangaa kuitwa jina lake.
“Teddy.”
“Nani?”
“Ingia haraka.”
Bila kuuliza aliingia ndani ya gari, haikupita muda gari la polisi lilitokea, lakini halikushughulika nao lilipita huku likipiga king’ora cha hatari. Teddy alishtuka kumuona mbaya wake Tony ndiye aliyekuja kumuokoa.
“Vipi Tony unatoka wapi?”
“Huwezi kujua, nimetumwa na bosi nikusaidie ameona kila kitu.”
“Alikuwa wapi?”
“Hiyo haikuhusu ila safari hii moja kwa moja Air Port unatakiwa uondoke na ndege ya saa sita usiku.”
“Booking?”
“Kila kitu kipo tayari mengine utayajua ukifika chimbo.”
Tonny aliendesha gari kwa kasi hadi uwanja wa ndege na kumpatia Teddy tiketi ya kusafiri. Muda ilionesha ni saa tano kasoro sita. Tonny hakuondoka mpaka ndege ilipoondoka kuhofia Teddy kuendelea kuwepo Dar na kuleta tafrani baada ya kukosa uvumilivu wa kutenda mambo.
Walihofia huenda akafanya mauaji zaidi kwa vile alikuwa akitumia nguvu bila akili. Teddy aliwasili uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyata saa kumi alfajiri na kwenda moja kwa moja chimbo.
***
Siku ya pili Teddy akiwa sehemu yake ya maficho alishtuka kumuona shemeji yake aliyetaka kumuua akiwa mzima wa afya na akikanusha vikali kwamba Teddy ndiye aliyetaka kumuua katika televisheni ya Italy News. Maelezo yake yalimsafisha Teddy aliyekuwa amewekewa WANTED na polisi wa Italia.
Maelezo ya shemeji yake yalimchanganya sana Teddy na kujiuliza kwa nini ameamua kumsafisha vile ikiwa amemfanyia kitu kibaya cha kutaka kumuuua lakini alimsafisha mbele ya vyombo vya usalama vya Italia hata kutoka picha za kumuomba radhi Teddy kutokana na kushukiwa na njama za kumuua Moses.
Hakiwa bado haamini alipokea simu toka kwa washirika wenzake toka Italia.
“Haloo Teddy.”
“Ndiyo Jimmy.”
“Umepata taarifa za Mose?”
“Hapana,” alijifanya hajui kitu.
“Mose amekusafisha katika vyombo vya usalama, lakini...”
”Lakini nini tena Jimmy?”
“Jamaa amesema yale kwa vile ana uchungu na wewe na amesema atakusaka popote ili alipe kisasi.”
“Achana naye hawezi kitu,” Teddy alisema kwa kujiamini.
“Teddy humjui Mose! Sisi ndiyo tunamjua, amesema ndani ya mwezi mmoja atakuwa ametia mikononi. Anajua kuna watu wanakukingia kifua eti wanaume zako ataanza kudili na hao na mwisho atakumalizia na hivi ninavyosema anajiandaa kuanza kukusaka.”
“Kwani yeye anajua nipo wapi?”
“Siwezijua lakini kaa ukijua jamaa kaingia msitari wa mbele kukusaka.”
“Poa tutaona mimi na yeye nani atammaliza mwenzake.”
“Nataka pia kukueleza Moses ana jamaa zake wanapenda kuua kama hawana akili nzuri, hivyo wakati wowote wataanza kukusaka.”
“We mwache aje wala hanitishi kwa jeuri yangu nitamfuata hukohuko.”
“Wewe!”
“Jimmy hunijui hivi ninavyozungumza nimemlaza mtu mzito serikalini na vijana wake usiku wa kuamkia leo jiji Dar.”
“Na sasa upo wapi?”
“Jimmy kama umetumwa siwezi kukueleza ila mweleze wala asisumbuke kunitafuta namfuata huko huko,” Teddy alionesha jinsi gani anavyojiamini.
“Jamaa amesema anajua sijui upo Kenya sijui sehemu gani, ameniahidi ndani ya mwezi maiti yako itaokotwa barabarani kwanza atakubaka kabla ya kukuua kinyama.”
“Umesema amesema nipo Kenya?” Teddy alishtuka.
“Ndiyo.”
“Mmh! Mwache aje.”
“Kuwa makini sitajisikia vizuri nikisikia umeuawa na Mose.”
“Sawa Jimmy, nakuahidi nitammaliza yeye kabla hajanigusa.”
Baada ya kumaliza kuzungumza na Jimmy simu toka Dar toka kwa bosi wake Double D iliingia.

Itaendelea
 
SEHEMU: 29
MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
SIMU: 0713 646500

ILIPOISHIA:
“Jamaa amesema anajua sijui upo Kenya sijui sehemu gani, ameniahidi ndani ya mwezi maiti yako itaokotwa barabarani kwanza atakubaka kabla ya kukuua kinyama.”
“Umesema amesema nipo Kenya?” Teddy alishtuka.
“Ndiyo.”
“Mmh! Mwache aje.”
“Kuwa makini sitajisikia vizuri nikisikia umeuawa na Mose.”
“Sawa Jimmy, nakuahidi nitammaliza yeye kabla hajanigusa.”
Baada ya kumaliza kuzungumza na Jimmy simu toka Dar toka kwa bosi wake Double D iliingia.
SASA ENDELEA...

“Haloo bosi,” Teddy alipokea.
“Vipi ulifika salama?”
“Nashukuru sana Bosi.”
“Basi kuwa makini.”
“Sawa Bosi.”
“Umezipata taarifa za Mose?”
“Kuhusu nini Bosi,” Teddy alijifanya hajui kitu.
“Leo amekusafisha kwa vyombo vya usalama ili alipe kisasi, sasa mama vita vya ndani sijui umejiandaa vipi?”
“Mkuu utanisaidia vipi?”
“Siwezi kuingilia ugomvi wa ndani, ni wewe kuwa makini kwa vile Mose ni mwenzetu.”
“Nimekuelewa Bosi kuanzia sasa hivi nitajua niishi vipi naweza nisionekane tena mpaka nitakapomtia mkononi Mose,” Teddy alijibu mapigo.
“Kwa hiyo na wewe unamtafuta?”
“Nimsubiri animalize, vita siku zote mfuate adui yako, nitatafuta nchi yoyote kuweka kambi ili nimsake hayawani yule wa kiume mbakaji mkubwa.”
“Na biashara?”
“Sasa hivi nasimamisha kwa ajili ya msako wa huyu hayawani anayetafuta vita na mimi.”
“Lakini Mose yupo sawa,” Double D alimtaadharisha Teddy.
“Namjua vizuri lakini siwezi kumkimbia akiniwahi basi lakini nitamfanya kitu kibaya zaidi ya kile cha mwanzo.”
“Basi kuwa makini, sipendi kukupoteza kwa vile wewe ni mtu muhimu sana.”
“Sasa bosi kwa nini usinisaidie kummaliza.”
“Msaada labba kukuelekeza sehemu salama, lakini zaidi ya huo siwezi kumbuka kumgeuka Mose sawa na kumsaliti kaka yake ambaye kwangu alikuwa zaidi ya ndugu, nafikiri unafahamu kitu hicho?”
“Nafahamu Bosi sina jinsi lakini sifi kikondoo patachimbika,” Teddy alijihami.
“Sasa ukihitaji msaada wowote utaniambia.”
“Sawa bosi.”
Baada ya kukata simu Teddy aliona kimenuka kwani hakukuwa na msaada wowote wa kumlinda kutokana na Mose kuwa ni mwana kikundi na kaka yake aliyekuwa bwana ya Teddy kuwa ndiye mwanzilishi wa kundi lile. Sifa ya kundi lile lilikuwa haliingilii mgomvi wowote wa ndani hata kuuana.
Ilikuwa lazima aondoke chimbo alilojificha baada ya kusikia Mose analifahamu, kwake ingekuwa rahisi kuwakimbia polisi wa Italia hata kwa kubadili sura lakini kwa Mose ingekuwa vigumu zaidi ya kutafutana.
Kilichokuwa kikimtisha zaidi ni uwezo wa hali ya juu wa Mose kundini katika mapigano, ndiye aliyekuwa akitumiwa kuwaua watu waliokuwa wakiweka kauzibe katika biashara zao. Hivyo suala la kuua kwake lilikuwa sawa na kuzima kibatari.
Aliamini kesi ya Deus haina nguvu alijipanga kuondoka mafichoni na kwenda nchi yoyote ambayo aliamini inamfaa kwa muda ule ili kujipanga kumsaka anayemsaka.
*****

Jiji Dar kesi iliyokuwa ikimkabiri Deus iliahilishwa kutokana na kifo cha mkuu wa kitengo cha madawa ya kulevya ambaye ndiye aliyekuwa shahidi wa mwisho. Baada ya mwezi mmoja hukumu ilitolewa na Deusi kufungwa miaka saba kutokana na kuonekana kuhusika kwa njia moja ama nyingine japo ushahidi haukumtia hatiani kwa asilimia mia.
Baada ya hukumu mkewe Kilole alilia sana kuonesha kuumizwa sana na hukumu ile. Kinape alishangaa kilio cha Kilole, lakini moyoni alimshukuru sana Teddy kuweza kupunguza ukali wa kesi ile ambayo ungefanya Deus aozee gerezani.
Baada ya hukumu Deus alichukuliwa na kupelekwa gerezani kutumikia kifungo cha miaka saba. Aliondoka akijua kilio cha mkewe kilionesha jinsi gani ameiachia familia yake maumivu makali. Lakini haikuwa kama alivyofikiria, nyuma ya machozi ya mkewe kulikuwa na kicheko cha furaha cha kummaliza.
Mumewe akiwa gerezani Kilole alianza kupanga mipango ya kummaliza kabisa ili akimaliza kifungo chake asikute kitu. Cha kwanza alitaka kumuua mtoto aliyezaa na Deus kitu alichokikataa Kinape kwa nguvu zote.
“Sawa tumemfanyia unyama Deus unataka kumuua mtoto wake kwa kosa gani? Kwanza kumbuka hii ni damu yako.”
“Ni kweli, lakini anaweza kunigeuka akipata akili na kujua mimi ndiye niliyemfanyia yale baba yake.”
“Tafuta njia nyingine lakini si kumuua.”
“Sina njia nyingine zaidi ya kumua, nataka mimi na wewe tuanze upya maisha yetu yawe na mtoto wetu wenyewe.”
“Kwa hilo sikubaliani nalo.”
“Sasa tufanyeje?”
“Huyu atakaa hapahapa kama mtoto wako na tutampa matunzo yote na chochote kibaya utachokifanya sitakuwa na suruhu ya kuendelea kuwa na wewe.”
“Sawa nitafanyaje lakini simpendi hata kumuona,” Kilole alionesha jinsi gani alivyona roho mbaya hata kwa damu yake.
“Kama unaichukua damu yako mimi utanipenda vipi?”
“Hapana Kinape nakupenda kuliko nafsi yangu.”
“Basi kama unanipenda mpende huyu mtoto mara mbili yangu.”
“Nitafanya hivyo kwa ajili yako mpenzi.”
MIEZI SABA BAADAYE
Katika mapenzi yao haramu Kilole alishika ujauzito Kinape, hapo ndipo Kilole hakutaka kukubaliana na Kinape kuhusiana kuendelea kuwa na mtoto wa Deus. Lakini bado Kinape alikuwa na msimamo makali ikiwa pamoja na kumlazimisha kwenda kumuona Deus gerezani. Kilole kwa vile alikuwa akimpenda sana Kinape alikubaliana naye kwa shingo upande.
Mimba ilipoaanza kuonekana alimkataza lakini alikwenda nayo hivyohivyo na kushtua Deus ambaye hakuamini mkewe kumsarti.
“Mke wangu hii si mimba?” Deus alishtuka kumuona mkewe aliyemuacha akiwa hana kitu ana ujauzito mkubwa ambao si wake.
“Kweli gereza baya, kama kusoma hujui hata kuangalia picha huwezi,” Kilole alijibu kwa nyodo.
“Una maana gani mke wangu?”
“Hii ni mimba mume wangu.”
“Ya nani?”
“Ya kwako.”
“Si kweli, nimekuacha huna kitu na wala hukuwahi kuniambia una ujauzito.”
“Sasa unafikiri ni wa nani?”
“Mke wangu mwaka na nusu kuwa gerezani umenisarti?” Deus alisema kwa sauti ya kilio.
“Sijakusaliti bali nimempata msaidizi wa kukusaidia mpaka ukitoka gerezani unikute nipo nakusubiri.”
“Mke wangu sasa hayo ni maneno gani?’
“Kwani wewe ulikuwa unatakaje?”
“Kaitoe hiyo mimba.”
“Mume wangu niue kiumbe kisicho na hatia?”
“Sasa unafikiri utazaaje mtoto asiye na baba?”
“Mume wangu kitanda hakizai haramu, mtoto ni wako.”
“Hapana mke wangu pamoja na kufanya kosa la kunisaliti naomba uitoe hiyo mimba.”
“Yaani nikae nayo miezi nane niitoe kirahisi nikifa?”
“Huwezi kufa mke wangu.”
“Hivi huyo mwanaume akisema na yeye amuue mwanao utakubali?”
“Nikubali vipi wakati wewe ni mke wangu wa halali.”
“Sikuja kwa hayo ila kukufahamisha nimepata msaidizi wa kukutunzia mkeo na mtoto nawe utumikie kifungo kwa amani na mguu huu ni wa mwisho kuja hapa.”
“Nooo, usifanye hivyo mke wangu.”
“Siwezi kutumikia mabwana wawili.”
“Huyo msaidizi ni Kinape?” Deus aliuliza huku amepiga magoti.
“Mbona umemtaja yeye ndiye uliyempa kazi ya kukulindia mkeo?”
“Hapana mke wangu, mbona unazidi kuniumiza?”
“Umejiumiza mwenyewe kwa kufanya biashara haramu kwa siri ningejua si ningeweza kuficha. Nimekutetea mahakamani bado tu unaniona sina maana.”
“Nashukuru mke wangu, lakini miaka saba siyo mingi.”
“Najua, lakini imetokea hivi unatakiwa ukubali matokeo.”
“Nimekubali lakini usiniache bado nakupenda,” Deus alizidi kuumizwa na mkewe.
“Basi habari ndiyo hiyo nikitoka leo sitarudi tena labda mwanao,” Kilole alisema huku akiondoka na kumwacha Deus amepiga magoti huku akiendelea kubembeza na machozi kumtoka.
Askari magereza alimchukua Deus na kumrudisha ndani, Deus baada ya kurudishwa ndani alijikuta kwenye wakati mgumu maishani mwake. Tokea siku ile aliishia katika maisha magumu huku akiamini yeye ni kiumbe mwenye nuksi. maumivu ya kusalitiwa yalikuwa makubwa zaidi ya yale ya kufungwa gerezani miaka saba.
Kitendo cha usaliti wa mkewe kilimuumiza sana kiasi cha kila siku kuonekana mgonjwa mpaka siku alipoitwa na mkuu wa gereza kumkuta mwanaye ofisini na barua yake nzito toka kwa mkewe.
****
Kupelekwa kwa mtoto wa Deus gerezani kulifikiwa baada ya mvutano mkali kati ya Kilole na Kinape juu ya kauli ya Deus ya kumlazimisha kuutoa ujauzito wa Kinape uliokuwa na miezi minane.
“Hata kama alitaka kuutoa ujauzito huo bado alikuwa na haki ya kusema vile kwa vile wewe ni mkewe.”
“Komea hapohapo toka alipofungwa mume wangu ni wewe hivyo na mtoto wake naye hafai kuendelea kuishi.”
“Kwa hilo sitakuelewa.”
“Sasa nasema hivi kama hutaki tumuue huyu mtoto nitamuua kisha nitajiua na mimi.”
“Kwanini umuue, basi tumpeleke wa wazazi wake kijijini?”
“Siwezi.”
“Basi mpeleke gerezani kwa baba yake.”
“Nitampelekaje?”
“Mpeleke na kumuacha nje ya gereza na barua mkononi askari wakiumuona watamchukua na kuisoma lazima taarifa zitamfikia.”
“Huo si ujinga wakija hapa si nitafungwa.”
“Ule mpango umekamilika, nimepata mununuzi wa nyumba na magari.”
“Mbona hukuniambia?”
“Nilikuwa nikuambie leo.”
“Kwa hiyo nitampeleka baada ya kuuza kila kitu.”
“Tutabakia na Toyota Land Cruiser tutayoitumia kuuhama mji.”
“Tunakwenda wapi?”
“Mwanza.”
“Ushawahi kufika?”
“Sijawahi, lakini nasikia ni mji unakaribiana na Dar kwa ukubwa na mzunguko wa fedha.”
“Hakuna tatizo, mauzo saa ngapi?”
“Usiku wa leo.”
Usiku yalifanyika mauzo ya nyumba za Deus na magari yake tena mbele ya mwana sheria wa mnunuzi. Baada ya makabidhiano walikubaliana waondoke kesho yake, usiku wa siku ile walijiandaa kwa safari ya siku ya pili. Siku ya pili baada ya maandalizi muhimu walimchukua mtoto wa kwenda kumuacha nje ya gereza na kuelekea Mwanza kuanza maisha mapya.

Itaendelea
 
SEHEMU: 30
MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
SIMU: 0713 646500

ILIPOISHIA:
Usiku yalifanyika mauzo ya nyumba za Deus na magari yake tena mbele ya mwana sheria wa mnunuzi. Baada ya makabidhiano walikubaliana waondoke kesho yake, usiku wa siku ile walijiandaa kwa safari ya siku ya pili. Siku ya pili baada ya maandalizi muhimu walimchukua mtoto wa kwenda kumuacha nje ya gereza na kuelekea Mwanza kuanza maisha mapya.
SASA ENDELEA...

***
Ndani ya gereza Deusi Ndonga akiwa amejiegemeza kwenye ukuta huku maumivu ya moyo wake yalikuwa makubwa zaidi ya yale ya kufungwa gerezani miaka saba. Lakini kitendo cha usaliti wa mkewe Mwaka mmoja toka aingie gerezani kilimuuliza zaidi.
Akiwa bado kaegemea ukuta macho katazama juu alipata ujumbe anaitwa kwa mkuu wa gereza na kwenda kukutana na taarifa zilizozidi kumuumiza na kutamani ardhi ipasuke na kummeza.
Deus alimalizia simulizi ndefu sana iliyochukua zaidi ya saa mbili, baada ya simulizi ndefu kwa mkuu wa gereza ya sababu ya yeye kuingia gerezani na kusalitiwa na mkewe na rafiki yake kipenzi Kinape. Mkuu wa gereza aliyekuwa akimsikiliza kwa makini alijikuta akitokwa na machozi ya uchungu bila kujua.
(Kwa wasomaji wapya yote hii ni simulizi ya Deus aliyokuwa akimuhadithia Mkuu wa Gereza mwanzo wa hadithi hii baada ya mtoto wake aliyeambatana na barua kuletwa gerezani na mkewe Kilole aliyekuwa tayari ana ujauzito wa rafiki yake kipenzi Kinape.)
Mkuu wa gereza baada ya kumsiliza alishusha pumzi ndefu na kusema kwa sauti ya huruma:
“Pole sana Deus.”
“Sijapoa kila dakika maumivu moyoni mwangu yanazidi mara dufu.”
“Ni kweli, lakini wanaume tumeubwa kukabiliana nayo.”
“Ni kweli lakini inauma sana.”
“Nina imani hawa washenzi wapo nyumbani kwako?”
“Ndiyo mkuu.”
“Sasa hivi nitaomba msaada wa polisi wakamatwe mara moja.”
“Nitashukuru, japo sikupenda tufikie huko zaidi ya kutupatanisha.”
“Deus usiwe mjinga kwa hatua hii hakuna suruhu.”
“Sawa mkuu, utakachofanya chochote sawa.”
Mkuu wa gereza alipiga simu kwa mkuu wa jeshi la polisi na kumweleza kwa ufupi mkasa ule na kuomba msaada wake. Alimuhadi baada ya muda atampa jibu. Deus aliombwa arudi gerezani na mwanaye kwa kipindi kile atakuwa nyumbani kwa mkuu wa gereza.
Deus alirudi kichwa chini machozi na makamasi yakimtoka kama mtoto mdogo. Kila dakika kwake aliiona ni mateso mazito na kujiuliza baada ya yale kipi kinafuata. Alipofika alirudi sehemu yake na kuendelea kuegemea ukuta macho alitazama juu lakini hakuna alichokiona zaidi ya maumivu makali ya moyo aliohisi unavuja damu.
Mkuu wa gereza aliletewa majibu ambayo aliamini lilikuwa pigo lingine mujarabu kwa Deus. Taarifa zilizotoka polisi ni kwamba Kilole mke wa Deus aliuza nyumba na magari yote na kuondoka. Ila taarifa ilisema itafanya uchunguzi watu hao wapo wapi.
Mkuu wa gereza alijikuta akipata wakati mgumu wa kumweleza Deus unyama mwingine aliofanya mkewe. Lakini hakuwa na jinsi alimtuma mtu amwite ili ampe taarifa ambazo aliamini lazima awepo daktari la sivyo wangempoteza.
Kabla ya kumwita Deus kumpa taarifa za nyumbani kwake, mkuu wa gereza alimwita daktari mkuu wa gereza na kumwelezea taarifa zile na kumuomba awe karibu kama tukio lolote litatokea aweze kutoa huduma ya kwanza.
Baada ya kumwita daktari, mkuu wa gereza alimtuma mtu amfuate Deus gerezani.
Deus alikuwa amejiegemeza kwenye ukuta wa chumba cha gereza akiwaza na kuwazua aliyofanyiwa na mkewe Kilole na rafiki yake kipenzi Kinape. Maumivu aliyokuwa akiyapata alitamani dunia imfukie akiwa mzima baada ya kuamini hana thamani yoyote.
Alirudisha kumbukumbu jinsi alivyomsaidia Kinape na pia familia ya mkewe Kilole, hakutegemea kama wangemtendea unyama kama ule. Alishtuliwa na sauti ya kuitwa, alinyanyuka na kusogea mlangoni alikukutana na askari:
“Mheshimiwa unaitwa na mkuu.”
“Sawa,” alijibu kwa sauti ya chini.
“Nifuate,” Deus alimfuata bila kusema kitu akiamini Kilole na Kinape watakuwa wamekamatwa. Moyoni hakupenda Kilole akamatwe kwa ajili yake kwa kuamini bado ana nafasi nyingine kwake.
Aliongozana na askari mpaka nje ya ofisi ya mkuu wa gereza, kutokana na maelezo ya mkuu kwa secretary wake, walipofika aliruhusiwa kuingia ofisini.
“Deus unaweza kuingia,” secretary alimwambia Deus.
Deus aliingia ofisini kwa mkuu na kumkuta akimsubiri.
“Karibu Deus.”
“Asante mkuu,” Deus alijibu kwa sauti ya chini.
“Kaa kwenye kiti,” Deus alikaa na kutulia kumsikiliza mkuu wa gereza.
Kabla ya kusema mkuu wa gereza alimtazama Deus na kumuonea huruma kwa kuamini moyoni mwake kuna mateso mazito, lakini hakuwa na jinsi zaidi ya kumwambia ukweli.
“Deus,” mkuu alimwita kwa sauti ya upole.
“Naam mkuu.”
“Najua moyoni mwako upo katika hali gani, lakini kama mwanaume unatakiwa kupambana nayo.”
“Ni kweli, lakini nimeshtukizwa sana.”
“Ukiwa mwanaume unatakiwa kukabiliana na yote, siku zote mwanaume ni mpambanaji na kutatua matatizo mazito.”
“Ni kweli kabisa mkuu, lakini nitawezaje kukabiliana nayo wakati nipo gerezani?”
“Unatakiwa kuachana na mambo ya nje ya gereza ili utumikie kifungo chako ukitoka utakuwa na nafasi ya kukabiliana nayo. Lakini ukiwa humu ndani na kufikiria ya nje yatakuchanganya.”
“Najitahidi kufanya hivyo lakini kila dakika linazuka zito kuliko la mwanzo.”
“Yote hiyo ni mitiani ya maisha unayotakiwa kuikabili hakuna maumivu unayoweza kupokewa na mtu.”
“Nimekuelewa mkuu, vipi wamepatikana?”
“Kuna taarifa zisizo nzuri, lakini unatakiwa nazo kuzipokea kama mwanaume.”
“Taarifa gani?” Deus aliuliza huku moyo ukimlipuka.
“Mkeo ameuza kila kitu.”
“Ameuza kila kitu una maana gani sijakuelewa?”
“Mkeo ameuza nyumba na magari yote.”
“Sasa yeye kakaa wapi?” Deus aliuliza swali la kizuzu.
“Siwezi kujua.”
“Mkuu unasema kweli au unatania?”
”Ni kweli kabisa kutokana na taarifa za kipolisi kuwa zilizofika nyumbani kwako kumekutwa mtu mwingine ambaye amenunua kila kitu jana usiku. Kwa maana hiyo mkeo hajulikani hayupo ila kauza kila kitu.”
“Ooh! Mungu,” Deus alisema na kujilaza nyuma ya kiti na kuseleleka mpaka chni alipotua kama mzigo.
Mkuu alijitahidi kumuwahi lakini alichelewa Deus alikuwa amekwishafika chini, alipomuangalia alikuta amepoteza fahamu. Haraka alimwita mganga mkuu ambaye hakuwa mbali na kuja kumpa huduma ya kwanza Deus aliyekuwa hajitambui.
Walimpatia huduma ya kwanza lakini haikuweza kumsaidia Deus ambaye viungo vya upande mmoja vilionesha kupoteza mawasiliano.
“Mkuu hali ni mbaya,” dakta Fukwa alisema huku akijifuta jasho kutokana na kujitahidi kwa muda mrefu kuokoa hali ya Deus bila mafanikio.
“Sasa tutafanyaje?”
“Hatuna ujanja, tumuwahishe Muhimbili.”
“Basi tufanye haraka.”
Mkuu wa gereza aliiita gari la wagonjwa lililofika na kumchukua Deus kumuwahisha Muhimbili kupata huduma kubwa. Gari lilimchukua haraka na kumkimbiza hospitali. Walipofika Muhimbili bado Deus alikuwa hajitambui alichuliwa haraka na kukimbizwa chumba cha wagonjwa mahututi.
Baada ya kupokelewa alipatiwa huduma ya haraka ili kuokoa maisha yake, walifanikiwa kuyashtua mapigo ya moyo yaliyokuwa yakipungua kila dakika na kuweza kumwekea mashine za kupumulia.
Deus alipata ufahamu wa mbali baada ya siku mbili sehemu moja ilikuwa na mawasiliano lakini upande wa pili imepoteza mawasiliano. Hali ile ilimfanya akae hospitali zaidi ya miezi mitano kutokana na kujaribu kuutibu ugonjwa wa kupoteza mawasiliano mwilini.
****
Kilole na Kinape baada ya kufika jiji Mwanza na kukaa kwenye nyumba ya wageni huku wakijipanga kutafuta kununua nyumba ya kuishi. Kwa vile walikuwa na fedha waliweza kupata nyumba nzuri maeneo ya shule Isamilo. Haikuchukua muda mrefu walifungua maduka makubwa ya kuuza vitu vya jumla na rejareja mtaa wa Liberty.
Kwa muda mfupi maisha yao yalibadilika kutokana na kufahamika haraka kutokana na uwezo wao wa kifedha. Gari walilosafiri nalo toka Dar waliliuza na kununua lingine. Wakati huo Kilole alikuwa amejifungua mtoto wa kike waliyempa jina la Gift.
Pamoja na kufanyiwa yote yale Kinape bado alikuwa na kisasi kizito moyoni mwake cha kuuawa mpenzi wake Happy bila sababu. Kila dakika aliyokuwa peke yake alimkumbuka mpenzi wake na kupanga kumfanyia kitu kibaya Kilole ambacho hata sahau maishani mwake.
Kilole upande wake aliamini Kinape anampenda sana na ndiye mwanaume wake sahihi maishani mwake. Alipanga kumpigania kwa nguvu zote kuhakikisha hampotezi alikuwa radhi kuendelea kutoa roho ya kiumbe yeyote wa kike atakayemsogelea karibu mpenzi wake.
*****
Teddy baada ya kutoka Kenya alikwenda kujificha nchini Ujerumani katika jiji la Hamburg katika hotel ya nyota nne ya Senator. Lakini pale alikaa wiki tatu na kupewa taarifa za tahadhari kubwa. Akiwa amejipumzisha chumbani kwake alipata simu toka kwa bosi wa kikundi Double D.
“Haloo Teddy upo wapi?”
“Kwa sasa sitaki kumjulisha mtu nipo wapi wacha nipumzike.”
“Teddy kuwa serious kuna kitu kibaya kinakukabiri.”
“Kitu gani? Acha kunitisha?” Teddy aliamini ni utani.
“Mose anakutafuta ile mbaya amefika Kenya kwenye chimbo lako na kukukosa alikuja Dar na kuniuliza juu yako lakini nilisema sijui chochote. Inaonesha kuna mtu katika kundi letu anawasiliana na Mose na kumwambia mimi nafahamu kila kitu kuhusiana na wewe pamoja na kumkatalia lakini alinihakikishia lazima akutie mikononi.”
“Hawezi kujua nipo wapi,” Teddy alisema kwa kujiamini.
“Kuna taarifa kuwa upo Ujerumani.”
“Nani kawaambia?” Teddy alishtuka.
“Mtu akitaka kumkamata mtu hashindwi, nimekueleza toka awali kuwa mtu yule anajiamini sana kuna kitu anakitegemea ndiyo maana alifuta ushahidi wa kukutia hatiani ili alipe kisasi kwa mkono wake.”
“Kwa hiyo Mose anajua nipo huku?”
“Ndiyo.”
“Mmh! Nani kamwambia nini nipo huku?” Teddy hakuamini kusikia vile.
“Wewe si unaona unafanya siri lakini mambo yako mengi yapo nje, kuwa makini badili mfumo wako wa maisha la sivyo utapotea.”
“Kwa hiyo Mose sasa hivi yupo wapi?”
“Kwa taarifa nilizozipata sasa hivi Mose na kundi lake wapo Ujerumani tena katika mji wa Humburg.”
“Muongo! Acha utani.”
“Sasa hivi anafanya msako wa Hotel zote za nyota tano.”
“Mungu wangu, sasa nifanyeje?” Teddy alichanganyikiwa.
“Fanya uwezavyo uondoke sasa hivi la sivyo mpaka kunapambazuka jina lako litabakia simulizi midomoni mwa watu.”
“Niende wapi?”

Itaendelea
 
SEHEMU: 31
MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
SIMU: 0713 646500

ILIPOISHIA:
“Kwa taarifa nilizozipata sasa hivi Mose na kundi lake wapo Ujerumani tena katika mji wa Humburg.”
“Muongo! Acha utani.”
“Sasa hivi anafanya msako wa Hotel zote za nyota tano.”
“Mungu wangu, sasa nifanyeje?” Teddy alichanganyikiwa.
“Fanya uwezavyo uondoke sasa hivi la sivyo mpaka kunapambazuka jina lako litabakia simulizi midomoni mwa watu.”
“Niende wapi?”
SASA ENDELEA...

“Fanya hivi, rudi nchi yoyote ya Afrika nina imani kwake akikukosa atakutafuta kwenye nchi za Ulaya au Marekani. Ukiwa Afrika hata kama msaada wangu utahitajika nitaweza kuja kukusaidia.”
“Sasa Afrika niende nchi gani? Maana sasa hivi nimeingia woga.”
“Sitaki kukueleza nenda nchi gani wala sitaki kujua atakuwa wapi la muhimu ondoka sasa hivi ukichelewa shauri yako.”
Teddy alipakia vitu vyake kwenye begi na kuondoka usiku uleule aliona heri aende moja kwa moja nchini Ghana. Aliamua kukaa palepale mjini Accra katika hotel ya nyota mbili ya East Gate iliyopo maeneo ya East Legon.
Taarifa za kusakwa kila kona ya dunia na Mose ilimchanganya sana na kuona muda si mrefu atamtia mikononi na kumuua.
Wazo lililomjia ni kwenda kubadili sura ili aweze kumkwepa Mose japo hakupenda katika maisha yake kuibadili sura yake. Kutokana na kuona vita ni kubwa pamoja na kumkimbia bado hakutakiwa kukubali kirahisi kushindwa zaidi ya kupambana.
Siku zote aliamini mwindaji hujiamini kuliko anayewindwa naye aliona ile ndiyo nafasi yake maye kuanza kumwinda taratibu. Akiwa chumbani kwake amepumzika kama ilivyokuwa kawaida yake kupenda kutoka usiku na mchana kutulia chumbani kwake.
Alipenda sana muda ambao hakuwa na kazi za kufanya kucheza game na alipochoka alilala. Kuhakutaka kufanya chochote kwa wiki mbili ili kupumzisha akili na kuchunguza Mose atakuwa wapi ili asikurupuke na kujiingiza katika mdomo wa mamba.
Baada ya wiki mbili kukatika akiwa amejipumzisha chumbani kwake alipatwa na mshtuko baada ya kuona taarifa za kushtusha za kifo cha bosi wake mtu aliyekuwa akimtegemea Double D aliyeuawa na baadhi ya washirika wenzake aliouawa kinyama habari na picha zilizorushwa na shirika la habari la CNN. Yalikuwa mauaji yalioutikisa jiji la Dar na nchi ya Tanzania.
Teddy alichanganyikiwa ilibidi ampigie simu Jimmy aliyekuwepo Italia kuhusiana na kifo cha Double D na baadhi ya washirika. Baada ya kuipokea kwanza Jimmy alionesha kushtuka na kuuliza:
“Ha! Teddy upo salama?”
“Jimmy nipo salama kwani vipi?”
“Hali ni mbaya Mose kawa mbogo anaua ovyo.”
“Unataka kuniambia yeye ndiye aliyemuua Double D na kina Tony?”
“Ndiyo.”
“Kwa sababu gani?”
“Kwa ajili yako.”
“Kwa ajili yangu ndiyo awaue?”
“Kwa taarifa zilizonifikia baada ya Mose kujua amejificha wapi nchini Kenya, alipofika na kukukosa. Inasemekana aliyekushtua ni Double D, nasikia walikoromeana sana kuhusiana na yeye kukushtua na kuweza kutoroka kiasi cha kutishiana maisha.
“Baada ya Mose kukufuatilia aligundua upo Ujerumani katika jiji la Humburg alifika mara moja na kundi lake, lakini hakufanikiwa kukuona. Kuna mtu katika kundi sijui nani alimweleza kuwa Double D ndiye aliyekubumburusha na kutoroka tena.
“Kitendo kile kilimkasirisha sana Mose na kumfuata Double D na kuchimbana mkwara katika kujitupiana maneno Double D alimpiga Mose kama mdogo wake. Mose hakukubali alimtolea bastora na kumlipua kila aliyetaka kumsaidia naye aliuawa kisha walitoroka.”
“Mmh! Kazi ipo sasa hivi Mose yupo wapi?”
“Amerudi Italia.”
“Na ana mpango gani na mimi?”
“Siwezi kujua nataka nikuambie kitu kama anataka kumkimbia Mose nenda Tanzania kwa sasa kwa vile hawezi kwenda kwa kuhofia kukamatwa.”
“Nitajua mwenyewe niishi wapi lakini wapi nitakuwepo itabakia siri yangu ila nashukuru kwa ushauri wako.”
“Take care, Mose kapagawa kawa kama mbwa mwenye kichaa anamuua kila ajae mbele yako sijui akikushika itakuwaje anaweza kukula nyama mbichi.”
“Nimekuelewa Jimmy.”
Baada ya kukata simu Teddy alijitupa kitandani na kuamini yupo kwenye wakati mgumu na Mose. Pamoja na kuua na kukimbia bado alijua atazidi kumtafuta huenda kamtumia Jimmy ili aweze kumtia mikononi. Lakini bado hakutaka kuitoa siri nje atakufa nayo.
Akiwa amejilaza kitandani macho akitazama juu alijikuta akiingiwa na hofu kubwa ya kifo cha Double D na kina Tony kilimchanganya sana na kuamini kama wale watu aliowategemea wameuawa na Mose yeye asingekuwa kitu kwake.
Alijilaumu sana kumbakiza duniani na kujiuliza alikosea sehemu gani iliyomfanya Mose aendelee kuwa hai. Aliona kuna umuhimu wa kutafuta jeshi la kumuongezea nguvu kuweza kukabiliana na Mose na kundi lake lililomtishia maisha.
Hakutaka kuendelea kumkimbia zaidi ya kujibu mapigo kwa yeye naye kuanza kumwinda adui yake. Wazo la haraka lilimjia lilikuwa kurudi Tanzania kumtafuta Deus kufanya kila awezalo kumtoa gerezani aweze kumsaidia kwa vile alionekana ni mtu mwenye uwezo mkubwa sana wa kutumia siraha kutoka na historia yake aliyoipata toka kwa aliyekuwa sekretary wake.
Deus alichaguliwa kujiunga na kitengo cha kupambana na madawa ya kulevya kutokana na utukutu wake na uwezo wa kutumia siraha za moto na mikono kwa ufasaha mkubwa.
Teddy aliona kuna haja ya kutumia kiasi chochote cha fedha kumtoa Deus gerezani. Wakati akiwaza hayo muda huo ndiyo Deus alikuwa akitoka hospitali baada ya kupata nafuu kubwa ya kumwezesha kuendelea na kifungo kilichobakia.
Pamoja na kurudi gerezani bado kazi ngumu hakuweza kuzifanya, mkuu wa gereza alipanga katika watu watakaopata msamaha wa rais basi mmoja wapo atakuwa Deus. Aliapa kumsaidia Deus mpaka atakapomtoa gerezani kwa kumpa upendeleo wa pekee kwa kula chakula kizuri hata sehemu yake ya kulala ilikuwa nzuri.
*****
Teddy aliteremka kwenye gari ka kifahari nje ya gereza la segerea na kwenda moja kwa moja kwenye ofisi za gereza na kuomba kuonana na mkuu wa gereza. Baada ya kujulishwa alimruhusu apelekwe ofisini.
“Karibu bibie,” Mkuu wa gereza alimkaribisha msichana mrembo.
“Asante mzee wangu, shikamoo.”
“Marahaba.”
Baada ya Teddy kukaa ulipita ukimya mfupi huku akiwa ameinama kuonesha mwingi wa aibu akichezea vidole, mkuu wa gereza alivunja ukimya.
“Ndiyo mama nikusaidia nini?”
“Nilikuwa na shida na Deus.”
“Deusiii...Deus ...yupi?” alimuuliza huku akimkazia macho.
“Mfungwa wako aliyefungwa kwa tuhuma za dawa za kulevya miaka zaidi ya miwili iliyopita.”
“Sasa mwanangu si ungekwenda gerezani tu ukamuone, huku ni sehemu ya utawala tu mama yangu,” mkuu wa gereza alimjibu kwa ustaarabu.
“Kuja huku nina sababu yangu mzee wangu.”
“Sababu gani?”
“Nataka kuzungumza naye faragha.”
“Kuhusu nini?”
“Mzee wangu ungenikutanisha naye ningefurahi sana.”
“Una muda gani hujaonana naye?”
“Mmh! Muda mrefu sana nimeondoka bado hajahukumiwa, taarifa za kufungwa nilizipata nikiwa nje ya nchi. Jana nimefika nataka kumuona na kesho naondoka haitakuwa vizuri kuondoka bila kumuona.”
“Sheria za gereza haziruhusu mtu kutembelea katikati ya siku zaidi ya kusubiri siku ya kutembelea wafungwa jumapili.”
“Naomba msaada wako nina imani utafurahi mimi kuonana na Deus pia nina mazungumzo mrefu na wewe ambayo pia nina imani tutaelewana na hutanisahau maishani mwako.”
“Wewe ni nani wake?”
“Ni mtu wake wa karibu sana.”
“Unajua yaliyomtokea?”
“Zaidi ya kufungwa sijui kingine.”
“Ni mengi yamemkuta akiwa gerezani, amekaa hospitali zaidi ya miezi sita.”
“Mungu wangu nini tena?” Teddy alishtuka.
“Alipooza mwili upande mmoja.”
“Ooh! Jesus,” Teddy alisema sauti ya kukata tamaa.
“Lakini sasa hajambo japo hawezi kufanya kazi nzito.”
Teddy aliinama na kujikuta akipoteza tumaini alilolitegemea bila kutarajia machozi yalimtoka. Hali ile alioona mkuu wa gereza na kuamini kweli yule mtu wake wa karibu aliyeguswa na tatizo la Deus.
“Pole sana binti.”
“Asante, inauma sana kwani nini kilimsibu mpaka kuwa hivyo?”
“Ni historia ndefu ya kusikitisha ya kutoa machozi kwa vile mwenyewe yupo atazungumza naye.”
Mkuu wa gereza alimtuma mtu kwenda kumwita Deus gerezani, Deus alikuja akiwa na maswali mengi kwani kila alipoitwa alikutana na kitu kilichouumiza moyo wake. Alipoingia ofisi ya mkuu wa gereza hakuamini kumuona mtu alimpigania kwa nguvu zote lakini alivyopotea hakujua.
“Ha! Teddy?”
“Ni mimi Deus pole sana.”
“Asante, za siku?”
“Mmh! Wee acha tu.”
“Ukisema hivyo sisi tutasemaje?”
Mkuu wa gereza aliwapa nafasi ya kuzungumza, Teddy alitaka kujua nini kilichomsibu Deus kiasi cha kupooza mwili na kulazwa hospitali kwa miezi mingi. Deus hakumficha alimweleza yote baada ya kuondoka jinsi mkewe na rafiki yake kipenzi walivyomtenda.
Simulizi ile ilimtoa machozi Teddy na kujikuta akijifuta kamasi nyembamba na mishipa ya kichwa kumsimama.
“Amini Deus kwa maelezo yako hata zile dawa za kulevya zimewekwa na mkeo na rafiki yako nina uhakika huo kuna siku nilikwenda kwa mkeo kutafuta njia ya kukutoa gerezani. Nilimkuta mkeo anafuraha amefungulia muziki kwa sauti kubwa, nilishtuka lakini leo nimepata jibu.”
“Hata mimi naanza kuamini hivyo.”
“Kuna kitu kilinileta na kuwa tayari kutoa kiasi chochote cha fedha ili utoke tuifanye kazi moja ambayo imeniweka katika maisha ya wasiwasi. Lakini hali yako imenikatisha tamaa.”
“Kazi gani?” Deus alimuuliza akimtazama usoni
Teddy naye ilibidi aeleze mkasa toka alipokamatwa mara ya kwanza uwanja wa ndege na vijana wa Deus na kisasi achokilipa na bahati mbaya adui yake alipona kifo na kuanza kumsaka mpaka kufikia kuua sehemu kubwa la kundi lao akiwemo bosi wao Double D.
“Utani huo unataka kuniambia kikosi chote kile kimepukutika?”
“Wee acha, nimebakia mimi tu.”
“Kweli mwanaume kapania, sasa ulikuwa unahitaji msaada gani toka kwangu?”
“Msaada niliokuwa nataka tuunde jeshi la watu wawili wa kumsaka Mose na kummaliza. Lakini hali yako nina imani huwezi kutoa msaada wowote, nitakuwa nimechemka sina jinsi. Mkeo nikimuona nitamuua kwani kama nitakufa mimi sababu ni yeye.”
“Kuhusu hali yangu sasa hivi nipo sawa, ila mkuu amenieleza msamaha wa rais utakaotoka mimi nitakuwa mmoja wapo, hivyo kanieleza niendelee kuigiza bado mgonjwa ili watu waamini naumwa hata nikiachiwa wasiwe na wasi na kuachiwa kwangu.”
“Mnategemea kuachiwa lini?”
“Baada ya sherehe ya uhuru mwezi ujao.”
“Kumbe siyo mbali.”
“Siyo mbali japo sijui maisha yangu nikitoka yatakuwaje?”
“Kuhusu maisha usiwe na wasiwasi kila kitu utapata kwangu na tukifanikiwa kumtokomeza yule nduli nitakupa utajiri mara tatu ya ulioupoteza.”
“Japo najua ni kazi lakini nina imani nitamtuliza.”
“Mbona unajiamini hivyo?” Teddy alimshangaa Deus.

Itaendelea
 
SEHEMU: 32
MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
SIMU: 0713 646500

ILIPOISHIA:
“Baada ya sherehe ya uhuru mwezi ujao.”
“Kumbe siyo mbali.”
“Siyo mbali japo sijui maisha yangu nikitoka yatakuwaje?”
“Kuhusu maisha usiwe na wasiwasi kila kitu utapata kwangu na tukifanikiwa kumtokomeza yule nduli nitakupa utajiri mara tatu ya ulioupoteza.”
“Japo najua ni kazi lakini nina imani nitamtuliza.”
“Mbona unajiamini hivyo?” Teddy alimshangaa Deus.
SASA ENDELEA...

“Matukio ya hatari kama hayo ndiyo nayataka, tena usisumbuke kuongozana na mimi utanipa picha yake tu, nikitoka sirudi mtupu.”
“Deus mbona kama siamini maneno yako?”
“Nimepewa kazi na cheo kutokana na kuwatuliza watu kama ninyi. Mkono huu umetoa uhai wa wajinga wengi sijawahi kunyoosha mkono ukarudi mtupu,” Deus alisema kwa kujiamini.
“Kama ni kweli natakani utoke hata leo maana sina raha mpaka sasa sijui hatima yangu.”
“Vumilia siku zimebakia chache sana.”
“Kwa nini nisizungumze na mkuu wa gereza kwa kumpa kiasi chochote ili utoke?”
“Acha papara kwa vile njia nzuri yenye uhuru ipo tusuburi, ingekuwa kuna mizengwe ningekuruhusu.”
“Hawezi kubadili mawazo?”
“Hawezi, kila kitu humu ndani anapanga yeye hivyo hawezi.”
“Je, akihamishwa?”
“Si rahisi mbona kila kitu kipo sawa usihofu,” Deus alimtoa hofu Teddy.
“Nashukuru wazo langu limepata nguvu.”
“Wee tulia mbona nitamzima kama kibatari,” Deus alisema kwa kujiamini.
Maneno ya Deus yalimpa nguvu na kukubaliana na kauli ya aliyekuwa sekretari wake kuwa Deus ni mtu hatari sana.
“Pia nilikuwa naomba ushauri kwa sasa nikakae nchi gani kukusubiri, maana nimechanganyikiwa?”
“Kwa nini usumbuke, nenda Mwanza ukapumzike tafuta hoteli yoyote nzuri ukae hapo nina imani muda si mrefu tutakuwa pamoja.”
“Hawezi kunifuata huko?”
“Sasa hivi kukupata itakuwa ngumu kutokana na mtandao aliokuwa akiutegemea umesambalatika.”
“Kwa hiyo unanishauri niende Mwanza?”
“Nina imani ni sehemu salama, ningekushauri uende Arusha ule mji wa kitalii sana unaweza kuonekana kwa bahati mbaya, lakini nina imani Mwanza ni sahihi sana kwako.”
“Sawa nikitoka hapa nakwenda moja kwa moja uwanja wa ndege hadi Mwanza, vipi una tatizo lolote linalohitaji msaada wangu kwa sasa?”
“Kwa sasa sina, nitakuwa nalo nitakapotoka gerezani.”
“Sasa nitajuaje umetoka?”
“Kila kitu utawasiliana na mkuu.”
“Hakuna tatizo.”
“Nimepata wazo la haraka.”
“Wazo lipi hili?”
“Nakuomba ukiweza muombe mkuu upumzike kwake mpaka usiku ndipo uondoke. Mchana si mzuri kiusalama unaweza kuonekana na mtu kisha ukawa hujafanya kitu chochote.”
“Atakubali?”
“Hawezi kukataa, sasa hivi huyu mzee namuona kama baba yangu mzazi amenisaidi vingi.”
Aliitwa mkuu wa gereza na kukaribishwa kwenye mazungumzo ambayo aliisha vizuri kwa kukubaliana kumtoa Deus pia kuwasiliana muda wote kabla ya kutoka. Teddy alimuomba mtoto wa Deus awe naye muda wote wa kumsubiri kutoka gerezani.
Deus hakuwa na kipingamizi mtoto wa Rose alipewa Teddy aliyesafiri naye usiku wa siku ile. Shukurani yake kwa msaada wa mkuu wa gereza Teddy alimpatia cheki ya shilingi milioni kumi.
“Nashukuru sana mwanangu nakuahidi muda si mrefu Deus utaungana naye, nimefurahi kutokea mtu kama wewe bila hivyo niliamini maisha ya Deus yangekuwa mabaya sana.”
“Siku zote akufaae kwa jua mfae kwa mvua.”
Usiku wa siku ile Teddy alisafiri na mtoto wa Deus kuelekea Mwanza kupumzika kumsubiri Deus atoke gerezani ili ampe msaada wa kummaliza Mose anayemsaka kama gaidi.
JIJINI MWANZA
Toka wafike Mwanza pamoja na mapenzi mazito aliyopewa Kinape hakufurahia maisha aliyokuwa akiishi na Kilole. Siku zote alimchukia badala ya kumpenda kutokana na matendo yake mabaya hasa baada ya kumuua mpenzi wake Happy pia hata kumfunga mumewe ambaye ni rafiki yake kipenzi.
Aliamini kama Deus atatoka salama basi maisha yake yatakuwa hatarini kwa kujua yeye ndiye adui yake namba moja. Wazo la kwenda kuomba msamaha kwa Deus alikuwa nalo lakini alijiuliza atampokeaje na atamueleza nini amuelewe?
Akiwa dukani peke yake baada ya Kilole kwenda nyumbani, alitokea msichana mmoja aliyekuja kununua mahitaji. Macho yake yalipatwa na mshtuko wa ajabu kumuona yule msichana anafanana sana na mpenzi wake Happy.
Moyo ulimshtuka baada ya kumuona msichana yule, kwa vile alikuwa amekwenda kununua vitu dukani mwake aliamua kumsemesha.
“Habari mrembo?”
“Jamani kaka yangu, kweli umechanganyikiwa wakati naingia dukani si tulisalimiana?”
“Nitakuwa nimechanganyikiwa.”
“Kipi kimekuchanganya kaka yangu?” yule msichana alimuuliza kwa sauti ya upole huku akitabasamu, Kinape alizidi kuchanganyikiwa kuiona picha ya marehemu mpenzi yake mbele yake.
“Baada ya kukuona.”
“Sasa nini kimekuchanganya baada ya kuniona?”
“Umefanana sana na aliyekuwa mpenzi wangu.”
“Labda ndiye mimi.”
“Hapana, yeye alifariki zaidi ya mwaka na nusu.”
“Ooh! Pole sana.”
“Asante.”
“Kwa hiyo baada ya kufariki hukutafuta mpenzi mwingine?”
“Ninaye.”
“Basi, usingekuwepo ningeichukua miye,” yule msichana alimtania.
“Kwani wewe upo singo?”
“Kwa ajili yako ningekuwa singo.”
“Wewe mwenyeji wa wapi?”
“Singida.”
“Wawoo, mkoa aliotoka marehemu mpenzi wangu.”
“Inaonekana ulikuwa unampenda sana?”
“Tena sana.”
“Nini kilichomuua?”
“Ni historia ndefu sana ila hatanitoka moyoni mwangu mpaka nakufa.”
“Ooh! Pole sana.”
“Asante.”
“Basi inaonekana una bahati wa wasichana wa mkoa huo?”
“Inawezekana, unaitwa nani mrembo?”
“Happy.”
“Noo, serious?” Kinape alishtuka.
“Ndiyo, mbona umeshtuka hivyo?” yule msichana aliuliza.
“Siamini, mfanane sura, umbile na jina hata sauti....siamini.”
“Muongo! Mpenzi wako alikuwa akiitwa Happy?”
“Ndiyo! Inawezekana kabisa Mungu kakuleta ili upoze maumivu yangu.”
“Lakini wewe si una mke?”
“Ninaye kama kivuli nina imani kabisa wewe ni mtu sahihi kwangu.”
“Lakini mimi si mkaaji Mwanza natarajia kuondoka leo na ndege ya mchana mpaka Dar kisha nirudi kwangu Arusha.”
“Arusha unafanya nini?”
“Nipo katika shirika moja la kitalii.”
“Na hapa Mwanza?”
“Nimekuja kwa shangazi yangu mmoja anakaa maeneo ya Kilimahewa.”
“Kwa nini usiondoke kesho ili jioni tuzungumze zaidi, yaani siamini nakuona kama ni mpenzi wangu Happy uliyefufuka ili kunipoza machungu ya kila siku kila nimkumbukapo.”
“Itakuwa ngumu kwa vile tayari nimeishatoa taarifa yakuondoka na ndege ya mchana huu.”
“Usihofu Happy, kila kitu kuanzia sasa nitakuwa juu yangu gharama ya tiketi yako itakuwa juu yangu.”
“Hakuna tatizo, basi kuwa na ahadi za ukweli nisije ahirisha safari yangu kisha nilale pele yangu. Nitakuja kukutoa nishai mbele ya mkeo.”
“Mimi ndiye niliyekuomba ubakie hivyo siwezi kwenda kunyume.”
“Haya nipe namba ya simu.”
Kinape alimpa Happy namba ya simu kisha yule pacha wa Happy alimbeep Kinape ili kumpa namba yake na kuondoka na kumuacha Kinape akimsindikiza kwa macho asiamini kumuona Happy mbele yake. Baada ya kuondoka aliamini kabisa ile ndiyo nafasi yake ya kulipa kisasi kwa Kilole kutokana na pigo alilompiga la kumuua mpenzi wake Happy.
****
Teddy baada ya kufika jijini Mwanza alikwenda kukaa sehemu za Nyakato katika Hoteli iliyokuwa ndani kidogo ya Green Motel iliyopo maeneo ya Nyakato Nundu. Japo ilikuwa ya nyota moja aliamini kwa muda wa kumsubiri Deus kukaa sehemu ile si pabaya sana.
Vazi lake kila alipotoka lilikuwa hijabu iliyomuacha wazi usoni na kuvaa miwani, siku nyingine alivaa wigi na miwani kubwa kila alipotembea alikuwa na Rose mtoto wa Deus ambaye alimfanya kama mtoto wake kwa kumpa matunzo ya hali ya juu.
Akiwa amekwenda benki kubadili fedha kwa ajili ya matumizi, wakati anatoka kamshikilia mtoto mkono wakielekea kwenye gari alikutana na Kilole aliyekuwa akiingia benki.
Kilole alipomuona Rose alishtuka lakini aliamini kabisa kamfananisha mwanaye, alisimama na kumuangalia yule mtoto aliyeamini kabisa ni mwanaye Rose. Aliangalia aliyenaye bado hakuwa na uhakika kutokana na mwili wote kufunikwa na hijabu.
Alipotaka kuendelea na safari alimsikia yule mwanamke akimwita yule mtoto:
“Rose nikununulie ice cream.”
“Yes mamy.”
Teddy alitoa fedha na kumwita mwenye kigari cha Ice Cream, alinunua mbili kisha waliingia kwenye gari na kuondoka. Kilole alishtuka na kuliangalia lile gari ambalo lilikuwa la kukodi katika makampuni ya magari mpaka lilipotea kwenye macho yake.
Hakuingia tena benki alikimbilia hadi kwenye gari lake na kujifungua kwa ndani kisha alitoa simu na kumpigia Kinape.
“Haloo baby,” Kinape alipokea upande wa pili.
“Kinape..Kinape,” alimwita kwa sauti ya muhemo kitu kilichomshtua Kinape.
“Vipi, mbona unaniita hivyo?”
“Nimemuona Rose.”
“Rose! Rose gani?”
“Mwanangu.”
“Mwanao! Kafika vipi huku?”
“Hata sijui.”
“Umemuona wapi?”
“Hapa nje ya benki.”
“Nje ya benki! Anafanya nini?”
“Yupo na dada mmoja amevaa hijabu nina wasiwasi na yule aliyejitolea kumtetea Deus.”
“Hapana, umemfananisha tu.”
“Nooo, Kinape ni yeye damu yangu siwezi kuipotea.”
“Kama unajua damu yako kwa nini ulitaka kuitoa uhai?”
“Kinape acha utani nina wasiwasi Deus yupo jiji Mwanza inawezekana kabisa amekuja kulipa kisasi.”
“Aje Mwanza kwani kifungo kamaliza? Na huu ndiyo mwaka wake wa pili na yeye kafungwa miaka saba. Ndiyo maana nakueleza umemfananisha tu,” Kinape bado aliamini mpenzi wake amefananisha mtu.
“Kinape haki ya nani ni Rose mwanangu tena yupo na yule dada, yaani tumepishana nikashtuka kumuona Rose nilipomuangalia vizuri yupo na nani nusra haja ndogo initoke baada ya kumuona yule dada uliyesema ni mafia akiwa na Rose tena kwa mdomo wake alimwita jina lake kumuuliza amnunulie ice cream, kwa sauti ya mwanangu ninayoijua alikubali tena akikubali kwa kuitika yes mamy.”
“Bado sijakubali, utakuwa umemfananisha tu,” Kinape alizidi kukataa.
“Kinape acha ubishi Deus huenda yupo Mwanza na yule mwanamke ni mwanamke wake tu, nilikueleza mapema ukabisha tulitakiwa tumuue Deus na mtoto wake mapema yote haya yasingetokea.”
“Kilole una uhakika gani kuwa uliowaona ni wenyewe Rose?”
“Kinape sijawa kukueleza jambo hili hata siku moja, amini nilichokiona ni kweli kabisa nimemuona Rose na Deus yupo Mwanza.”
“Mmh! Sasa umeisha maliza kilichokupeleka hapo benki?”
“Hata nguvu ninazo za kuingia tena benki narudi tu nyumbani kupumzika nitarudi kesho.”

Itaendelea
 
SEHEMU: 33
MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
SIMU: 0713 646500

ILIPOISHIA:
“Bado sijakubali, utakuwa umemfananisha tu,” Kinape alizidi kukataa.
“Kinape acha ubishi Deus huenda yupo Mwanza na yule mwanamke ni mwanamke wake tu, nilikueleza mapema ukabisha tulitakiwa tumuue Deus na mtoto wake mapema yote haya yasingetokea.”
“Kilole una uhakika gani kuwa uliowaona ni wenyewe Rose?”
“Kinape sijawa kukueleza jambo hili hata siku moja, amini nilichokiona ni kweli kabisa nimemuona Rose na Deus yupo Mwanza.”
“Mmh! Sasa umeisha maliza kilichokupeleka hapo benki?”
“Hata nguvu ninazo za kuingia tena benki narudi tu nyumbani kupumzika nitarudi kesho.”
SASA ENDELEA...

“Basi wewe rudi, lazima nipate ukweli wa kitu ulichokisema.”
“Ukweli upi?”
“Kuulizia habari za Deus kama kweli ametoka au vipi.”
“Kama ametoka?”
“Tutajua cha kufanya hebu rudi basi tujue tufanye nini.”
“Yote umeyataka wewe kama ningemuulia mbali yote haya yasingetukuta, sasa tutakwenda wapi?”
“Acha kupagawa njoo tutazungumza nyumbani haya si ya kuyazungumza mbele za watu.”
“Nimo ndani ya gari.”
“Mimi nipo dukani.”
“Basi funga duka tukutane nyumbani.”
Deus alifunga duka na kutangulia nyumbani kumsubiri mpenzi wake, haikuchukua muda Kilole naye alifika nyumbani kijasho kikimtoka japo alitoka ndani ya gari lenye kiyoyozi kikali.
“Vipi mbona jasho jingi?”
“Unafikiri lililopo mbele yetu dogo?”
“Una uhakika gani kuwa ni wenyewe?” bado Kinape aliamini Kilole amefananisha.
“Kilole acha ubishi, Rose mwanangu siwezi kumpotea.”
“Kabla ya yote wacha nipate ukweli wa Deus kisha tujue tufanye nini,” Kinape alimueleza Kilole aliyekuwa bado amesimama toka aingie ndani.
“Utaupaje ukweli, Kinape mbona na wewe unanichanganya?”
“Nitampigia mtu simu wa Dar atanipa habari zote za Deus.”
“Mtu gani? Una namba ya nani?”
“Wapo rafiki zangu nitawapigia simu.”
“Utawaeleza upo wapi huoni kama hiyo ni njia ya kutujulisha tupo wapi,” Kilole alimtaadharisha.
“Si kuna kile kitabu cha Deus cha kumbukumbu zake, mule kuna namba nyingi za rafiki zake nitampigia mmoja kumuulizia lazima atakuwa anajua habari zake.”
“Utajitambulishaje?”
“Kwa jina la uongo na kujifanya ni mmoja wa mtu wake wa karibu ili niweze kumdodosa bila kujua.”
Kilole alikwenda chumbani kwenye kabati ya nguo na kutoa kitabu chenye kumbukumbu muhimu za Deus na kumpelekea Kinape. Alitafuta namba za kupiga jina la Best aliamini ndilo lililofaa kupigwa. Baada ya kuandika namba alipiga lakini haikuwa hewani, walijaribu namba zaidi ya tano ya sita ilikubali.
Baada ya kuita kwa muda ilipokelewa upande wa pili.
“Haloo.”
“Haloo Mr Mabina za siku?”
“Nzuri tu, nani mwenzangu?”
“Naitwa John Mwenge.”
“Ndiyo bwana Mwenge, jina lako kama geni, samahani hebu nikumbushe tulionana wapi?”
“Tulionana hapohapo Dar siku moja nilikuwa na Mr Deus.”
“Mr Deus yupi?”
“Yule jamaa aliyekuwa mkuu wa kitengo cha kuzuia dawa za kulevya kituo cha uwanja wa ndege.”
“Ooh! Kweli basi itakuwa muda sana, ehe lete habari.”
“Nilikuwa nataka kujua habari za Deus, maana niliondoka kabla kesi yake haijaisha.”
“Kwani upo wapi?”
“Nipo Mtwara karibu kabisa na mpaka wa kuingia Msumbiji.”
“Mmh! Kwa sasa hata sijui habari zake japo nina wasiwasi huenda amekwisha fariki.”
“Deus amekufa?” Kinape alishtuka.
“Inawezekana.”
“Alinyongwa?”
“Hapana, alipata stroke.”
“Kwa sababu gani?”
“Rafiki yangu mwanamke watu wabaya sana tunalala nao na kujifunika shuka moja lakini ni maadui zetu wakubwa. Mkewe aliyekuwa naye alikuwa zaidi ya nyoka kamfanyia kitu kibaya sana rafiki yangu. Baada ya kuhukumiwa miaka saba nasikia yule mwanamke alianzisha uhusiano na rafiki kipenzi wa Deus na kufikia hatua ya kumpatia ujauzito hiyo ikawa haitoshi wakaenda kumuachia mtoto gerezani kubwa zaidi ilikuwa ni taarifa za kuchukuliwa kila kitu nyumba na magari yake ambayo yule mwanamke aliuza na kukimbia.
“Taarifa ilipomfikia ndipo alipoanguka na kupoteza fahamu na muda huohuo akapata stroke.”
“Mungu wangu!” Kinape alipata mshtuko wa kweli toka moyoni baada ya kusikia madhara ya ubaya waliomfanyia Deus chanzo wakiwa wao hasa Kilole.
“Basi Deus kakaa hospitali miezi miwili hajui anayeingia wala anayetoka, baada ya hapo nilisafiri nje ya nchi kama miezi minne. Niliporudi nilikwenda moja kwa moja hospitali kumjulia hali yake. Nilikwenda moja kwa wadi aliyokuwa Deus nilipofika kitanda alichokuwepo nilikuta mgonjwa mwingine.
“Ilibidi niulize mgonjwa aliyekuwepo kitanda kile yupo wapi, alielezwa ana wiki tatu toka afariki.”
“Ooh! Maskini rafiki yangu Deus,” Kinape alisema kwa uchungu wa kweli toka moyoni huku machozi yakimtoka,
“Si wewe hata mimi kaniuma sana jamaa alikuwa mtu safi sana sijawahi kuona.” “Asante kwa taarifa yako.”
Kinape baada ya kukata simu aliinama na kuanza kulia baada ya kusikia rafiki yake kipenzi amefariki na chanzo ni yeye na Kilole. Kilole aliyekuwa pembeni yake alimuuliza:
“Vipi mbona hunipi jibu unainama na kulia nani kafa?”
“Deus.”
“Deus?” Kilole alishtuka.
“Ndiyo.”
“Lini?”
“Miezi sita baada ya sisi kuondoka.”
“Nani kakueleza kafa na nini kimemuua?”
Kinape alimweleza yote aliyoelezewa kwenye simu na Mr Mabina, baada ya kumsikiliza alisema:
“Sasa Rose kafikaje Mwanza?”
“Nimekueleza utakuwa umemfananisha tu.”
“Labda, lakini ni yeye Rose na yule msichana ulisema anaitwa nani?”
“Teddy.”
“Lakini naomba ufanye upelelezi zaidi juu ya ukweli juu ya kifo cha Deus ili tusiwe na wasiwasi tuishi kwa kujiachia,” taarifa zile kidogo zilishusha presha ya Kilole.
“Hakuna tatizo mpenzi.”
“Yaani huwezi kuamini nilikuwa nimeisha changanyikiwa, sasa kama Deus amekufa bado nina kazi moja muhimu.”
“Ipi hiyo?”
“Ya kumsaka Rose na kuua.”
“Kwa nini?”
“Unafikiri Rose akikuwa na kujua chanzo cha kifo cha baba yake ni sisi kutakuwa na usalama?”
“Hizo taarifa atazipata wapi?”
“Hujui dunia hii, ipo siku tutaumbuka, nitamsaka sehemu yoyote mpaka nimuue.”
“Kumbuka ni damu yako.”
“Lakini ndiyo itakayokuwa adui yangu namba moja.”
“Tena Mpenzi nilisahau kuna sherehe ya Send of ya rafiki yangu leo usiku La Cairo hotel.” Kinape aliingiza na miadi yake na Happy ya usiku ule.
“Mbona hukuniambia mapema?” Kilole alihoji taarifa zile za ghafla.
“Huwezi amini hata kadi nimeelezwa atapewa nikifika mlangoni.”
“Twende wote.”
“Noo, mtoto bado mdogo hatakiwi kutoka usiku.”
“Mmh! Sawa.”
Kilole alikubali lakini moyoni alikuwa na wasiwasi na taarifa ya ghafla aliyopewa na mpenzi wake kuhusu kwenda kwenye sherehe. Kwa vile alikuwa analea alikuwa mpole.
*****
Kinape baada ya kupata ruhusa kutoka kwa mpenzi wake alimjulisha Happy watakutana hoteli ya Gorden Crest majira ya saa tatu usiku ili wale chakula cha pamoja kabla ya kujuana zaidi. Happy naye alimweleza yeye atawahi mapema na kuchukua chumba kwa fedha yake.
Majira ya saa tatu usiku Kinape alijiandaa kama kweli anakwenda kwenye sherehe ya harusi. Baada ya mkewe kumkagua alimsifia amependeza.
“Asante mpenzi.”
“Lakini chonde mpenzi ulivyopendeza hivi nisiibiwe tu,” Kilole alilia wivu.
“Usiwe na wasiwasi najua tumetoka wapi.”
”Ukilijua hilo nina imani mali zangu zitarudi salama.”
Kinape alimbusu Kilole pande tatu kisha alitoka, alichukua gari dogo kuelekea hoteli ya Gorden Crest. Kwa vile alikuwa ameelekezwa chumba alipofika pale hotelini hakumuuliza mtu alikwenda moja kwa moja kwenye mlango wa chumba na kuingia ndani na kumkuta Happy amejaa tele katika vazi la kanga moja bila kitu ndani. Alipomuona alifurahi na kumrukia na kumkumbatia.
“Wawooo baby kweli una uhadi za kweli pia nimeamini ulikuwa ukimpenda wa jina wangu kama unavyosema tulikuwa tunafanana sina budi kusema pacha wangu.” Happy alisema kwa furaha.
“Ni kweli, ninavyokuona leo kama namuona Happy amefufuka kuja kunipoza machungu yasiyo na kifani moyoni mwangu.”
“Nina kuhakikishia hutajutia kuonana na mimi, nitajitahidi kukufurahisha japo sina uhakika kama nitamshinda pacha wangu.”
“Nina imani utaziba pengo lake, si rahisi moyo wangu kumuamini mtu lakini kwako nimekumeza mzimamzima.”
“Na mkeo?”
“Happy nakuahidi wewe ndiye mke wangu wa ndoa nitakaye kukabidhi moyo wangu na kila kitu changu ni halali yako.”
“Na dada?”
“Nitakapokuoa utajua kila kitu kwa sababu gani simpendi yule mwanamke.”
Happy aliondoka nguo zote alizovaa Kinape na kwenda wote pamoja kuoga. Ulikuwa usiku wa raha katika maisha ya Kinape toka afariki kipenzi chake Happy.
***
Kilole roho ilikuwa haimpi muda wote aliwaza anaibiwa, pamoja na mpenzi wake kutoka kisherehe bado hakumuamini kwa asilimia mia. Baada ya kunyonyesha mtoto wake na kuamini ameshiba hawezi kuamka mapema. Alibadili nguo na kuvaa track suti na raba kisha alitoka hadi kwenye gari kuelekea Hotel La Cailo iliyokuwepo maeneo ya Kirumba.
Kutoka Isamilo hadi Kirumba hakukuwa na umbali mrefu hasa usiku ule wa saa nne magari yalikuwa machache sana njiani. Alikanyaga mafuta kwa dakika saba alikuwa ameegesha gari kwenye maegesho ya Hotel La Cailo. Aliteremka na kutembea taratibu hadi kwenye ukumbi unaoshughulika na sherehe.
Ukumbi ulikuwa mtupu alizunguka kila kona hakukuwa na sherehe yoyote.
Alimfuata mfanyakazi mmoja wa kike na kumsalimia.
“Samahani dada yangu, za saizi?”
“Bila samahani dada yangu, nzuri tu,” alimjibu huku akijiandaa kuulizwa swali.
“Eti leo kulikuwa na sherehe ya send of hapa?”
“Mmh! Hapana,” alijibu huku akitikisa kichwa.
“Kwani hapa Mwanza kuna La Cailo ngapi?”
“Moja.”
“Asante.”
“Kwani vipi dada kuna mtu unamtafuta?”
“Hapana.”
Baada ya kusema vile aligeuka na kwenda moja kwa moja kwenye gari na kuondoka kwa mwendo wa kasi mpaka nyumbani. Kutokana na kwenda kwa kasi alijikuta akiligonga geti na kulivunja. Baada ya kuteremka aliingia chumbani na kuanza kulia huku akisema:
“Huyu mpumbavu hanijui mimi ni nani, mapenzi yote dhambi zote nilizozipata kwa ajili yake anaona bure. Sasa tutaona mimi na yeye nani zaidi,” Kilole alisema huku akipiga ngumi kitandani.
Wazo la kumuua aliliondoa kwa vile aliamini hakuna mwanaume chini ya jua anayempenda kama Kinape. Ila aliapa kila atakayeonja asali yake itageuka sumu na kuapa kumsaka aliyemtoa usiku mpenzi wake na kuhakikisha anampoteza kama alivyompoteza Happy.

Itaendelea
 
SEHEMU: 34
MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
SIMU: 0713 646500

ILIPOISHIA:
Wazo la kumuua aliliondoa kwa vile aliamini hakuna mwanaume chini ya jua anayempenda kama Kinape. Ila aliapa kila atakayeonja asali yake itageuka sumu na kuapa kumsaka aliyemtoa usiku mpenzi wake na kuhakikisha anampoteza kama alivyompoteza Happy.
SASA ENDELEA...

Pia alipanga kutomuuliza chochote hata akirudi asubuhi lakini atafanya uchunguzi wa siri na akimjua lazima amuue. Alishindwa kulala na kujikuta akizunguka nyumba huku akilia akiuapia moyo wake kuwa ataendelea kubeba dhambi mpaka hapo Kinape atakapojua thamani ya penzi lake.
Alishinda amekaa sebuleni macho muda wote alilia kwa hasira, alikumbuka Kinape akirudi na kumkuta analia lazima angehoji hapo angekosa la kujitetea. Alifuta machozi na kunawa kisha alipanda kitandani na kujilaza japo usingizi hakuwa nao kifua kilivimba kama kinataka kupasuka kwa hasira.
Kinape alirudi nyumbani alfajiri akioneka amelewa, Kilole alipokea bila kumwambia kitu. Kwa vile alikuwa amechoka baada ya kuoga alipanda kitandani kulala.
Kinape akiwa njiani akirudi nyumbani alifuta meseji zote hata simu alizompigia Happy. Akiwa amelala Kilole alitumia nafasi ile kuipekua simu ya mpenzi wake lakini kila alipofungua hakukuta kitu. Aliamini mtihani wa kwanza ameshindwa lakini hakutaka kuwa mkali kwani aliamini muonja asali haonji mara moja lazima atarudi hapo lazima atamkamata na kufanya alichokipanga.

DEUS GEREZANI
Baada ya Teddy kuondoka gerezani, mkuu gereza alikuwa na mazungumzo na Deus ili kujua kipi kinatakiwa kabla ya kutolewa gerezani.
“Deus kwanza nashukuru kwa mgeni wako, yaani na mimi nitamalizia nyumba yangu na kupata kigari cha kutembelea, si unajua bado miaka miwili nistaafu, mbona kaniokoa.”
“Yote inatokana na wema ulionitendea, na mimi nakuahidi nikirudi safari yangu salama nitakupa zawadi kubwa.”
“Usiwe na wasiwasi, kuna kitu nilitaka kujua kutoka kwako.”
“Kitu gani hicho mzee wangu?”
“Kwa muda huu unataka nikufanyie kitu gani ambacho unaamini kitakuweka katika hali nzuri kwa muda uliobaki.”
“Tena umeniuliza swali zuri ambalo lilikuwa likiniumiza kichwa.”
“Kitu gani? Niambie nipo tayari kukusaidia, unataka ukae nje ya gereza muda huu?”
“Hapana, kupata muda wa mazoezi ya kujiweka sawa kabla ya safari yangu ya Italia.”
“Hayo mazoezi saa ngapi?”
“Usiku.”
“Hakuna tatizo, usiku nitakuchukua mwenyewe kukupeleka kwenye gim na kukurudisha.”
“Nitashukuru.”
Baada ya mazungumzo Deus alirudi gerezani kwa mwendo wake wa kuvuta mguu kuonesha bado ugonjwa unamsumbua. Mkuu wa gereza alipanga mpango ule kuhakikisha Deus anatoka mapema kwa kuhofia yaliyomkuta kama angekaa gerezani kwa muda mrefu lazima atakufa kwa mawazo.
Usiku majira ya saa nne wakati wafungwa wote wamelala Deus alitolewa kwenye chumba alichotengewa na kuongezwa baadhi ya vitu vya kumliwaza toka Teddy alipompa mkuu wa gereza asante la milioni kumi. Deus alipelekwa gim muda ambao watu walikuwa wamemaliza na kufanya mazoezi peke yake kwa saa mbili kisha alirudishwa gerezani na kujipumzisha huku akila chakula kizuri kilichokuwa kikipikwa kwa mkuu wa gereza.

JIJI MWANZA
Penzi la Kinape na Happy alilizidi kuota mizizi kiasi cha Kinape kumuongezea wiki nzima kuwepo jiji Mwanza kuendelea kuwa naye akiamini ndiyo njia pekee ya kumuenzi mpenzi wake marehemu Happy aliyeuawa na Kilole. Mabadiliko ya Kinape yalimfanya Kilole kuendelea kupelelezi bila kuonesha ameshtukia kitu.
Kwa vile ilikuwa ni vigumu kugundua huwa anakwenda wapi, ilibidi amkodi mtu kumfuatilia Kinape kila kona ili ajue anakwenda wapi kila apoondoka nyumbani. Kijana mmoja aliifanya ile kazi kwa kufuatilia nyendo za Kinape na kufanikiwa kumuona akiingia hoteli ya Gorden Crest.
Baada ya kumuona katika hoteli ile zaidi ya mara mbili alimpigia simu Kilole kumjulisha.
“Sister huwa anakuja hoteli ya Gorden Crest.”
“Umemuona hapo mara ngapi?”
“Zaidi ya mara mbili na akiingia huchukua muda mrefu kutoka.”
“Umemuona kaongozana na nani?”
“Kwa kweli mara zote nimemuona peke yake.”
“Na akitoka huwa ameongozana na nani?”
“Hutoka peke yake.”
“Nitakuongeza fedha chunguza huingia wapi na huwa na nani.”
“Hakuna tatizo nitakuwa jibu muda si mrefu.”
Anko Jay Jay kijana aliyepewa kazi ya kumchunguza Kinape alipokata simu aliingia ndani ya hoteli ya Gorden Crest lakini alishindwa aanzie wapi na amuulize nani. Kwa vile ilikuwa vigumu kujua yupo mule kwa ajili ya mazungumzo au chumbani na mwanamke.
Akiwa amesimama kwenye korido akiwaza alimuona Kinape ameongozana na msichana mmoja mzuri. Walimpita wakizungumza na kusimama pembeni yake, aliwasikia wakizungumza:
“Sasa baby wacha nikimbie nyumbani si unajua yule mtu machale yameanza kumcheza ila nikija Arusha utanichoka.”
“Siwezi baby, yaani nitanenepa.”
“Kapumzike basi baby, kesho.”
Anko Jay Jay alishuhudia Kinape akilishana mate mbele yake kisha waliagana na Kinape kutoka nje ya hoteli na yule msichana kurudi chumbani. Anko Jay Jay aliachana na Kinape na kumfuatilia yule mwanamke aliyepanda ngazi kuelekea juu.
Alimfuata mpaka alipomuona akiingia katika chumba ambacho alinakili namba zake kisha aligeuka na kuteremka hadi chini kisha alimpigia simu Kilole.
“Haloo sister itabidi uniongeze mshiko.”
“Ukifanya kazi nzuri sitakuwa na hiyana nitakuongeza nyingine kama niliyokuahidi.”
“Basi sister nimefanya bonge la kazi.”
“Usiniambie!” Kilole alishtuka kusikia vile.
“Nimemaliza kila kitu kazi kwako.”
“Mmh! Niambie umefikia wapi?”
Anko Jay Jay alimweleza yote na kumfanya Kilole afurahie kwa kuruka juu na kusema:
“Anko Jay Jay umefanya kazi nzuri sana.”
“Kwa hiyo?”
“Njoo uchukue chako, nikiwa na shida nitakutafuta ila nakuomba siri hii usimwambie mtu,” Kilole alimuonya Anko Jay Jay.
“Siwezi sister.”
***
Kinape kutokana na kubadili ratiba yake ya kuwahi kurudi nyumbani pia mpenzi wake kutoonesha wasiwasi wowote aliamini mambo yake yanakwenda vizuri. Ilikuwa lazima aende mchana hotelini na kula chakula cha pamoja na Happy na jioni kuwa pamoja hadi saa nne usiku na kurudi nyumbani huku akimweleza Kilole kuwa na mazungumzo na rafiki zake.
Siku ya pili kama kawaida Kinape majira ya saa sita mchana alikwenda hotelini kwa Happy kwa ajili ya chakula cha mchana. Mlango ulikuwa umerudishwa kama kawaida alifungua mlango huku akiita:
“Sweetiiiii.”
Kama kawaida yao kila alipofika na kumwita vile Happy hukurupuka na kwenda kumrukia kwa furaha. Lakini siku ile alishangaa kutopokewa alipoingia ndani alimkuta Happy akiwa amelala kifudifudi kitandani akiwa katika mavazi ya kulalia.
“Babiiii,” Kinape alimwita huku akimsogelea kitandani.
“Babiii kulala gani huko, amka tukapate lunch.”
Happy hakujigeuza wala kuitikia, ilibidi amtikise huku akimwita.
“Happy..Happy, wake up baby.”
Lakini vilevile hakuonesha kushtuka kitu kilichomshtua Kinape na kumgeuza kwa nguvu ili kumshtua. Happy aligeuka mzimamzima akiwa amelegea kifuani kukiwa na damu na sehemu aliyolala kulikuwa na damu nyingi. Kinape alishtuka na kutaka kupiga kelele za kilio lakini alishika mdomo asitoe sauti.
Alipomchunguza aligundua mpenzi wake mwingine kauawa kwa risasi. Kwa haraka alitoka nje ya chumba na kukimbilia nyumbani huku akiwa katika hali ya kuchanganyikiwa. Kilole alishtuka kumuona yupo katika hali ile alimfuata chumbani na kumkuta Kinape machozi yakimtoka huku mikono ikikosa pa kushika kila alipojishika aliona hapafai.
“Honey vipi?”Kilole alimuuliza.
“Safi.”
“Mbona hivyo?”
“Wee acha tu,” alijibu huku akigeukageuka kitandani kama kuna miba.
“Kuna nini honey? Kilole alimuuliza kwa sauti ya upole.
“Hakuna kitu naomba uniache,” Kinape alijibu kwa hasira mikono ikiwa kichwani.
“Mmh! Haya ukihitaji msaada wangu utanifuata,” Kilole alisema huku akitoka nje.
Kinape alianza kulia kilio cha sauti huku akisema:
“Kwa nini lakini...Ooh! Happy kwa nini lakini? Uuuu aaa..sikubaliii Happy hawezi kufa kirahisi namna hii,” alilia huku akipiga ngumi kifuani kwa nguvu.
Kinape alijua lazima aliyefanya kitendo kile cha ukatili atakuwa Kilole tu hakukuwa na mtu mwingine ambaye angefanya mauaji kama yale.
Alikumbuka kifo cha mpenzi wake wa kwanza hakikuwa na tofauti na kile cha Happy wa pili. Moyoni alijiuliza Kilole ataendelea kuua mpaka lini. Alitoka chumbani kama mbogo na kwenda sebuleni kumfuata Kilole amueleze kwa nini amemuua Happy.
Aliapa bila majibu mazuri angemfia mikononi, alipofika alipokuwa amekaa Kilole akisoma ujumbe kwenye simu wakati huo katika luninga kulikuwa kunaoneshwa tukio la mauaji katika hoteli ya Gorden Crest. Kinape kwanza alitulia kusikiliza nini kinaendelea baada ya kifo cha Happy.
Mtangazaji alielezea tukio la kifo cha msichana aliyefahamika kwa jina la Happy Simoni Mfanyakazi katika kampuni ya Utalii Arusha aliyeuawa kwa risasi majira ya saa nne na saa tano asubuhi katika hoteli ya Gorden Crest. Mtangazaji aliendelea kusema kuwa msichana yule alikuwa amepanga pale siku ya tatu akiwa na mpenzi wake wa kiume ambaye alikuwa halali pale na kukutana mchana na usiku kisha mpenzi wake huondoka.
Taarifa ziliendelea kusema siku ya tukio mpenzi wake alionekana pale hotelini na kwenda kuweka oda ya chakula cha mchana kama kawaida, baada ya wahudumu kuona anachelewa ndipo walipokwenda chumbani na kukutana na tukio lile la kutisha bila kumuona yule mpenzi wake.
Taarifa zilizidi kuelezwa kuwa baada ya hapo walitoa taarifa katika uongozi wa hoteli kisha kuitaarifu polisi waliofika na kuichukua maiti kwa uchunguzi zaidi huku mpenzi wake akiendelea kusakwa na polisi.
Baada ya taarifa ile Kinape alimgeukia na kuuliza kwa sauti kali:
“Nani kamuua Happy?”
“Happy! Ndiye nani?” Kilole alijifanya kushangaa.
“Unajifanya hujui siyo?” Kinape alimtolea macho yaliyokuwa mekundu kwa ajili ya kulia.
“Baby mbona unataka kuniingiza katika matatizo, nimuue Happy mara mbili?” Kilole alizidi kuruka.
“Siyo mpenzi wangu wa Dar huyu aliyekufa leo hii.”
“Kinape...Mimi na sijui huyo Happy wapi na wapi, kwanza nimuue kanifanya nini?” Kilole alijifanya kushangaa.
“Nitajua tu muda si mrefu.”
“Kujua nini, kwanza nataka uniambie huyo Happy ni nani? Kinape ulikuwa na mwanamke wa pembeni?” Kilole naye alikuja juu huku akimfuata Kinape na kumvuta shati.
“Niambie Kinape kumbe ulikuwa na mwanamke unaona Mungu kakuumbua.” Kilole alisema huku akilia kwa uchungu.
“Nitajua tu.”
“Kujua nini mpenzi wangu, anayetafutwa ni wewe?”
Kinape alikaa kwenye kiti na kuanza kulia kwa sauti ya kwikwi huku akisema:
“Nini hatima ya yote.”
Kilole alimfuata na kukaa pembeni yake na kumsemesha kwa sauti ya upole:
“Baba Junior hebu nieleze kifo cha huyu msichana wewe kinakuhusu vipi?”
“Ni rafiki yangu ambaye alikuwa mfanya biashara na nilikuwa nakwenda pale kwa ajili ya mazungumzo ya kufanya biashara Mwanza na Arusha. Leo nilipofika nikakuta ameuawa kwa kupigwa risasi kifuani.”
“Anafanya biashara gani? Kama madini huenda ameuawa na majambazi, hakuibiwa kitu chochote?”
“Hata sijui huoni kama mimi nipo hatarini.”
“Nitakusaidia mpenzi wangu, itabidi uondoke kajifiche Afrika ya Kusini mpaka matatizo yakiisha urudi ukiweezekana tuhamie huko wote.”
“Yaani ikiwezekana hata leo niondoke maana nikishikwa nitanyongwa au kuozea gerezani.”
“Hakuna tatizo mpaka jioni utapata jibu la safari kuna mtu nitampigia simu ili uondoke na ndege ya saa sita usiku.”

Itaendelea
 
SEHEMU: 35
MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
SIMU: 0713 646500

ILIPOISHIA:
“Nitakusaidia mpenzi wangu, itabidi uondoke kajifiche Afrika ya Kusini mpaka matatizo yakiisha urudi ukiweezekana tuhamie huko wote.”
“Yaani ikiwezekana hata leo niondoke maana nikishikwa nitanyongwa au kuozea gerezani.”
“Hakuna tatizo mpaka jioni utapata jibu la safari kuna mtu nitampigia simu ili uondoke na ndege ya saa sita usiku.”
SASA ENDELEA...

*****
Tarehe Tisa Desemba siku ya uhuru mheshimiwa rais alipotangaza msamaha kwa wafungwa wenye vigezo vya kuachiwa, Deus alikuwa mmoja ya watu walionukaika na msamaha huo. Kama kawaida walisomewa majina wafungwa watakao achiwa na kutolewa gerezani kwa msamaha wa rais.
Baada ya kusomewa Deus alitoka katika mwendo wake wa kuvuta mguu wa kushoto kama kweli ni mgonjwa. Wafungwa wenzake walimuaga wakiamini kabisa jamaa yao ni mgonjwa ambaye hakuwa na faida yoyote kuendelea kuwepo gerezani.
Baada ya kutoka gerezani, nje ya gereza alimkuta Teddy akimsubiri na kuondoka naye ndani ya gari lililokuwa na vioo vyeusi mchana ule moja kwa moja mpaka uwanja wa ndege na kwenda naye kwenye maficho yake jijini Mwanza.
Walifika Mwanza majira ya saa tisa alasiri, baada ya kufika tu Mwanza hakutaka kupoteza muda alimuuliza Teddy.
“Ipe information ili kazi ifanyike mara moja.”
“Deus mbona haraka sana kwa nini usipumzike kwa siku mbili tatu, nina wasiwasi ulitakiwa upumzike mwezi mzima kuuandaa mwili. Kifungo si mchezo hasa magereza ya kibongo.”
“Teddy nipo fiti huu mwili unauonaje?” Deus alitoa shati kuonesha mwili uliojengeka kimazoezi.
“Ha! Deus, mwili umejengeka kimazoezi umefanya muda gani? Tena unaonesha upo fiti.”
“Ile mbaya, nimejiandaa kuifanya kazi kwa aina yoyote ya mapigano kwa siraha au mkono mtupu.”
“Kwa hiyo ulitaka twende lini?”
“Kesho.”
“Keshooo?” Teddy alishtuka.
“Teddy hebu tumalize kazi hii mara moja ili nifanye nyingine, una picha ya huyo mshenzi?”
“Sina, labda tuangalie kwenye Facebook.”
Waliwasha Lap top na kuiweka moderm na kumsachi jina la Moses Chris, lakini ilionesha ameondoa picha zake zote na kuacha kivuli tu kwenye jila lake.
“Sasa tutafanyaje?” Deus alimuuliza Teddy.
“Nimekumbuka hebu sachi jina la Jarome Moore.”
Walitafuta jina la Jarome Moore na kufunguka kisha walifungua kwenye picha zake, baada ya kutafuta kwa muda Teddy alisema.
“Huyu hapa,” alimuonesha kwenye picha aliyopiga pamoja na Jarome Moore.
“Okay, tuisevu kwenye desktop.”
Baada ya kuiweka desktop Deus aliikuza na kuitazama kwa muda kisha alisema:
“Okay, nimemuona.”
“Kwa hiyo?”
“Tayari.”
“Ina maana huchukui picha yake?” Teddy alishangazwa na uchukuaji wa picha ya Moses.
“Kazi yetu haitakiwi kutembea na picha ya mtu unaweza kutuweka katika matatizo.”
“Kwa hiyo unataka kuniambia umeisha mtambua hata ukikutana naye?”
“Wee utasikia nimefanya nini, fanya mipango ya hati za kusafiria nianze kazi mara moja ambayo nina imani itachukua siku chache kabla sijaanza msako wa kufa mtu wa wale mashetani.”
“Ukiwashika utafanyaje?”
“Nitajua nikiwashika, ila nitakachowafanya Mungu anajua.”
“Hiyo kazi nitaifanya miye.”
“Nilitaka kusahau nitaondoka peke yangu hii kazi sitaki msaada ni ndogo sana.”
“Kwa nini? Utawaweza peke yako nasikia wapo wengi.”
“Mimi peke yangu sawa na jeshi la watu mia.”
“Mbona unajiamini sana?”
“Kwa vile najiamini.”
“Kwa hiyo unataka ondoke lini?”
“Teddy, huu si muda wa kupoteza, natakiwa niondoke kesho usiku.”
“Visa nitapataje?”
“Mpigie mtu huyu.”
Deus alimpa namba ya rafiki yake kipenzi anayefanya kazi uhamiaji. Baada ya kuita alizunguza naye.
“Haloo.”
“Haloo.”
“Nani mwenzangu?”
“Deus.”
“Deus! Deus gani?”
“Mpolipoli.”
“Wee Acha utani, Deus mpolipoli ni mmoja tu ambaye mpaka sasa sijui yupo hai au amekufa.”
“Hajafa yupo hai na ndiye unayezungumza naye.”
“Wewee, acha utani! Ni wewe kweli?”
“Sasa kiliza Bon ni hivi nitafutie visa ya kusafiri kesho jioni.”
“Lakini mbona kama siamini.”
“Bon, ni hadithi ndefu unayoijua na usiyoijua, kama nikirudi salama safari yangu ya Italy tutazungumza mengi.”
“Unajua siamini.”
“Best camooon.”
“Kweli nimeamini ni wewe, nipe muda upo wapi?”
“Nipo Mwanza, usiku wa leo nitakuwa Dar kwa ajili ya safari ya Italia.”
“Siamini mpaka nikuone.”
“Utaniona la muhimu nifanyie hiyo kazi mara moja.”
Deus alikata simu na kumgeukia Teddy aliyekuwa bado ameshangaa.
“Vipi mbona unanishangaa?”
“Siamini, visa utapata kesho.”
“Kesho ni safari ya kifo.”
“Deus kwa nini tusiende wote? Unajua moyo wangu haunipi kabisa wewe kwenda peke yako.”
“Hapana kazi hii si ya kitoto.”
“Deus unanidharau kwa vile mwanamke?”
“Walaa, kazi hii tukienda wawili tunaweza kumpoteza mtu, sitaki nikuone akifa.”
“Siwezi Deus.”
“Nina uzoefu na safari za aina hii, kama jamaa anakuwinda utakuwa umepata nafasi ya kukupata kwa urahisi. Niache nicheze naye kwa vile hanijui nitamumaliza kama kuzima kibatari.”
“Deus ukifa nami nitakufa nakupenda sana.”
“Asante.”
“Sio siri nilikupenda toka siku ya kwanza na ulichonifanyia ndiyo ulizidi kunimaliza. Naomba nipasue siri yangu ambayo ilinitesa muda mrefu Deus nakupenda sana tena sana.”
“Asante.”
“Deus mbona kila kitu unasema asante au hunipendi?”
“Utajua nikirudi Italia.”
“Hapana Deus naomba uniambie kama kweli nami unanipenda, nina imani nina nafasi kubwa moyoni mwako baada ya mkeo kukutenda.”
“Nami nilikupenda toka nilipokuona lakini sikuweza kusema ningeweza kuharibu kazi.”
“Kweli Deus, nimefurahi sana kusikia kumbe na wewe ulikuwa ukinipenda.”
Walijikuta wamesahau mambo ya safari na kuingia dunia nyingine iliyoandikwa historia mpya kwa siku ile.
“Deus naomba unioe.”
“Hiyo ndiyo itakayofuata kama nikirudi salama.”
“Deus mpenzi utarudi salama nakusubiri kwa hamu kubwa.”
Kila mmoja alimpa uhuru mwenzake mikono yake uzuru pande zote za mwili, ilikuwa raha kwa wote huku Teddy akitimiza ndoto yake ya kumtamkia Deus kuwa anampenda.
****
Mpango wa Kilole kumtorosha Kunape uligonga mwamba baada mtu waliyekuwa wakimtegemea kufanya mpango wa safari kusafiri kuwa nje ya nchi kwa wiki nzima.
“Sasa itakuwaje mpaka arudi si nitakuwa nimekamatwa?” Kinape aliuliza akiwa amejawa na hofu.
“Kinape usihofu kwa vile hawakujui, we kaa ndani usitoke mpaka soo litakapoisha,” Kilole alimpa moyo.
“Kumbuka wamesema wamechukua mkanda unaochukua matukio yote ya hotalini siku ile huoni nitaonekana?”
“Hata kama utaonekana bado hujaua.”
“Hata kama sijaua huenda wakasema nimeshilikiana na muuaji?”
“Kwanza kamera zile hazina uwezo mkubwa wa kuiona picha kwa ufasaha, pia muuaji ataonekana si wewe hivyo hawatashughulika na wewe zaidi ya kumsaka muuaji.”
“Mmh! Usalama wangu ulikuwa kuondoka hapa tu,” Kinape alihofia kukamatwa na kufunguliwa mashtaka.
“Jamaa anarudi baada ya wiki usiwe na wasi akirudi tu unaondoka.”
“Itabidi nivumilie sina ujanja.”
Wakiwa wamekaa sebuleni wakisikiliza taarifa ya habari, taarifa kutoka polisi zilisema kuwa kamera la hoteli ambazo huonesha mwisho nje ya mlango wa kuingia chumbani. Majira saa saa tano na dakika tano asubuhi alionekana mtu kama mwanamke aliyekuwa amevaa hijabu akiingia katika chumba cha marehemu na kutoka baada ya dakika kumi.
Taarifa ziliendelea kusema muuaji ndiye aliyevaa jazi refu la kumziba mwili mzima. Jeshi la polisi lilikuwa likiomba mpenzi wa mwanamke yule ambaye alikuwa Kinape kwenda kujisamilisha ili kutoa msaada kwa polisi kwa kuonesha muuaji anamjua. Kauli ya mtangazaji ilimfanya Kinape alalamike kwa sauti.
“Jamani mimi nimjue wapi muuaji?” Kinape aliuliza huku akizidi kukata tamaa.
“Hebu acha kujitia presha, usijitokeze tuone watakuona wapi kwa muda huu matembezi yako yatakuwa usiku tu.”
Wakiwa katikati ya mazungumzo mtoto ndani alilia na kumfanya Kilole amfuate ndani na kumkuta amejisaidia, ilibidi amfanyie usafi kwanza. Sauti ya kuonesha katika simu ya Kilole ujumbe umeingia ulilia na kumfanya Kinape kuiona simu ya Kilole aliyoiacha kwenye kochi.
Kwa haraka aliichukua na kuufungua ujumbe ulioingia uliokuwa unasomeka.
“Sawa sister sitamwambia mtu, unatisha lakini kumbe we mafia mbaya.”
Alisoma mwingine uliotangulia ambao ilionesha Kilole aliosoma na kuujibu:
“Sister yule demu anayetembea na mumeo nimesikia ameuawa, vipi umemuua wewe?”
Ulikuwa ujumbe uliotangulia ambao Kilole aliujibu na kutumiwa mwingine ambao nao aliamini angeujibu. Aliichukua namba ya simu ya aliyetuma ujumbe na kuufuta ujumbe ulioingia ili Kilole asijue kama ameshika simu yake na kuirudisha simu juu ya kochi kama ilivyokuwa.
Moyoni alitamani kumuuliza lakini alivuta subira isionekane kama anampekua baada ya kuwekeana mipaka kwenye simu zao. Kilole akiwa chumbani alikumbuka amesahau simu juu ya kochi sebuleni. Alimweka mtoto kitandani na kutoka haraka.
Simu yake aliikuta alipoiacha aliichukua na kurudi nayo chumbani, kabla ya kuingia chumbani Kinape alimwita.
“Kilole.”
“Abee,” aliitika huku akigeuka kumtazama.
“Mbona umefuata simu kwa haraka?”
“Nilisikia ikiita kumbe masikio yangu.”
“Mmh! Haya.”
“Kwani umewaza nina mwanaume wa nje?”
“Basi tu.”
Kilole hakuongeza neno alielekea chumbani kumvisha nguo mtoto kisha alitoka naye na kukaa pembeni ya mpenzi wake ambaye aliamini ana mawazo ya kukamatwa kumbe alikuwa amepata nusu ya ushahidi wa kifo cha mpenzi wake Happy.
 
SEHEMU: 36
MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
SIMU: 0713 646500

ILIPOISHIA:
“Nilisikia ikiita kumbe masikio yangu.”
“Mmh! Haya.”
“Kwani umewaza nina mwanaume wa nje?”
“Basi tu.”
Kilole hakuongeza neno alielekea chumbani kumvisha nguo mtoto kisha alitoka naye na kukaa pembeni ya mpenzi wake ambaye aliamini ana mawazo ya kukamatwa kumbe alikuwa amepata nusu ya ushahidi wa kifo cha mpenzi wake Happy.
SASA ENDELEA...

Akiwa amekaa akimuangalia Kinape alijikuta akikumbuka jinsi alivyomuua mpenzi wa Kinape. Baada ya kukamilisha uchunguzi wa mabadiliko ya mpenzi wake na kufahamu ana mpenzi aliyempangia Gorden Crest alijipanga kwenda pale.
Majira ya saa nne asubuhi baada ya kumlisha chakula mtoto wake alimlaza kitandani na kuvalia baibui lililouficha mwili na uso na kuchukua bastora aliyoichomeka kwenye suruali na kutoka.
Alitumia gari dogo na kwenda kulipaki pembeni ya ofisi za Tanesco, gari lake lilitazamana na Maktaba kuu. Alikodi bodaboda na kuteremkia karibu na hoteli ya Gorden Crest. Baada ya kumlipa fedha dereva wa bodaboda alimuomba amsubiri.
“Samahani kaka yangu, kunisubiri kwa dakika kumi utanitoza kiasi gani?”
“Baada ya kukusubiri utaelekea wapi?”
“Nitarudi uliponitoa.”
“Ukinipa buku tatu haitakuwa mbaya.”
“Basi mimi nitakupa tano unasemaje?”
“Utakuwa umecheza sister.”
“Poa, wacha niwahi.”
Kilole alichepua mwendo kuingia ndani ya hoteli na kuelekea upande wa vyumba, kutokana na elekezo aliyopewa kuhusu jografia ya hoteli ile haikumpa kazi kufika kwenye ngazi za kupanda juu na kwenda hadi ghorofa la pili. Alipofika kabla ya kuelekea chumbani kwa mbaya wake alitulia kwa muda kuangalia kama kuna mtu anamfuatilia.
Hali ilikuwa ya tulivu hakukuna na watu sehemu ile, kabla ya kuchepua mwendo aliipapasa bastora yake kupata uhakika kuwa ipo. Taratibu alikwenda hadi mlangoni na kuzungusha kitaza kama mlango umefungwa kwa ndani.
Mlango ulitii amri na kufunguka aliingiza mkono ndani ya hijabu na kutoa bastora yake na kuingia nayo kaishikilia mkononi.
Alimkuta Happy amejilaza kwa kulalia tumbo akiwa katika vazi la kulalia, nguo ilivyokuwa ilionesha hakuwa na kitu ndani kumaanisha alikuwa akimsubiri mpenzi wake ampe burudani.
Baada ya kuingia ndani alitulia akimuangalia yule msichana kwa hasira, aliamini muda ulikuwa unakwenda kwa vile kamuona mbaya wake ilitakiwa kazi moja na kuondoka. Alifunga mlango kwa sauti kidogo kitu kilichomshtua Happy kuamini mpenzi wake amefika.
Alipogeuka alikutana na mwanamke aliyekuwa amevaa hijabu bastora mkononi iliyokuwa imemwelekea yeye.
“Vipi dada?” Happy alishtuka.
“Unashtuka nini ulipomchukua mume wangu mbona hukushtuka?”
“Sa..sa..mahani dada mi..mi..si..jachukua mume wa mtu!” Happy alijitetea huku akitetemeka.
“Kinape mumeo?”
“Si..sijajua kama ni mumeo..ni..nisamehe.”
“Sina muda wa kubishana na mwizi wangu.”
“Sasa unataka kunijfanya nini dada yangu?”
“Unataka kujua, Sali sala yako ya mwisho utajua muda si mrefu.”
“Tafadhali dada usiniue.”
“Lazima ufe kwa vile niliapa kila nitakayemkamata na mume wangu lazima nimtangulize mbele na Kinape anajua hivyo si kosa langu aliyekuponza ni huyo aliyekudanganya.”
“Dada yangu nakuapia kwa miungu yote sirudii te...”
Kilole aliona muda unachelewa alifumba macho na kuminya kifyatulio mara mbili kwa haraka, risasi mbili zilitua kwenye kifua cha Happy na kumrusha kwa nyuma.
Baada ya kukata roho, kwa moyo wa ujasiri Kilole aliuchukua mwili ule na kuulaza kitandani kisha alitoka taratibu kuelekea nje ya hoteli. Alimkuta dereva wa bodaboda akimsubiri alipanda hadi alipopaki gari lake, baada ya kumlipa alipanda ndani ya gari lake na kurudi nyumbani kwake.
Alipofika alijikausha kusubiri taarifa ya kifo cha mpenzi wa Kinape na jinsi mpenzi wake atakavyokipokea. Baada ya saa mbili ndipo aliporudi Kinape akiwa amechanganyikiwa na kumuuliza na yeye kukataa kujifanya hajui kitu. Alipanga kumweleza baada ya kila kitu kutulia.
“Kilole,” Kinape alimwita baada ya kumuona mpenzi wake amehama kimawazo.
“A..abee,” Kilole alishtuka kutoka katika dimbwi la mawazo.
“Vipi mbona kama upo mbali?” Kinape alimshtua Kilole.
“Aah! Ni..ni..po sawa kwani vipi?” Kilole alishtuka kama anatoka ndotoni na kubabaika.
“Mbona kama upo mbali?”
“Aah! Nipo sawa.”
“Basi nataka kutoka mara moja,” Kinape alisema akinyanyuka.
“Wewee! Unataka kwenda wapi umesahau unatafutwa?”
“Ooh! Nilijisahau yaani nimechanganyikiwa ile mbaya.”
Kinape alielekea chumbani kulala na kumuacha Kilole akiwa amekaa sebuleni, baada ya Kinape kwenda chumbani Kilole aliipekua simu yake labda kuna ujumbe umeingia lakini hakukuta na ujumbe wowote.
Alimtumia ujumbe yule Jay Jay asimwambie mtu pia asitume tena ujumbe wowote muda ule ili aende ndani akamliwaze mpenzi wake aliyekuwa kwenye lindi la mawazo.
****
Majira ya saa tatu usiku Kinape alimuaga Kilole kuwa anatoka mara moja.
“Safari ya wapi tena baba?”
“Si unajua leo nimekaa ndani kama utumbo ngoja nikanyooshe mwili.”
“Sawa baba, kuwa makini tu si unajua sasa hivi wewe ni lulu?”
“Hilo nalijua.”
“Unarudi saa ngapi?”
“Sichelewi.”
“Au twende wote?”
“Na mtoto umuachie nani?”
“Tutatoka naye, si hatufiki mbali?”
“Kuna baridi, huu si muda wake wa kumtembeza usiku, akikuwa tutatoka naye.”
“Haya baba, basi uwahi kurudi si unajua bila wewe nyumba inapwaya.”
“Nalijua hilo mpenzi wangu nitawahi, si unajua leo siko vizuri nahitaji kuwa karibu yako.”
“Ni kweli baby wangu.”
“Basi baadaye, nitachukua gari ndogo.”
“Mume wangu lolote ulitakalo.”
“Lazima nikujulishe,” siku ile Kinape alikuwa mpole sana lakini moyoni palifukuta kwa hasira.
Kinape alitoka na gari ndogo hakufika mbali alisimama gari na kuipiga namba iliyomtumia ujumbe Kilole. Kabla ya kupiga alikumbuka kama ataipiga huenda akashtukiwa alijaribu kwanza kutuma ujumbe kama watashindwa kuelewana basi angempigia. Alituma ujumbe unaosema:
“Oya Anko Jay Jay upo anga zipi mida hii?”
Baada ya muda ujumbe alirudi.
“Nipo Kapili Kabana, nani mwenzangu?”
“Unatoka saa ngapi huko?” aliongeza swali badala ya jibu.
“Mmh! Mpaka saa tano vipi una ishu?”
“Ndiyo.”
“Ishu gani?”
Kinape hakumjibu tena aliwasha gari na kuwahi Kapili Kabana, alipofika alipakia kwenye maegesho na kupiga simu huku macho yake yakitazama mlango wa kutokea.
“Oya, nipo nje njoo mara moja nina haraka.”
Anko Jay Jay alitoka nje haraka akiamini kuna ishu ameletewa, kwani mjini yeye alikuwa akiishi kwa misheni tauni kila kazi iliyokuja mbele yake aliifanya ikiwemo ya udalali wa kila kitu mpaka wake na waume za watu kwake ilikuwa kazi ndogo.
Alipotoka alitazama kulia na kushoto labda atamuona mtu aliyekuwa akimwita, kuhangaikakwa Jay Jay kumtafuta aliyempigia simu kumfanya Kinape amuone kwa urahisi. Akiwa na simu mkononi alipiga ili kumuuliza mtu anayemtafuta yupo wapi. Baada ya muda simu iliita na kumuamini ndiye mhusika, alikuwa kijana mmoja aliyeoneka brother men.
Hakuipokea aliteremka na kumfuata alipokuwa amesimama kwa vile alikuwa amevaa kapelo ilikuwa vigumu Anko Jay Jay kumfahamu, alipomkalibia alimpa mkono na kumsalimia.
“Habari Anko Jay Jay.”
“Nzuri, nina imani ni mtu uliyekuwa ukitafuta?”
“Kweli kabisa,” Kinape alijibu huku akitoa kofia kichwani.
‘Ha!” Anko Jay Jay alipomuona alishtuka na kutaka kukimbilia lakini hakuweza kwa vile Kinape alikuwa amemshika mkono kwa nguvu.
“Sasa unataka kukimbia nini?” Kinape alimuuliza kwa sauti ya chini.
“Siyo hivyo brother.”
“Basi sikiliza naomba uwe mtulivu tuzungumze taratibu bila hivyo nitakufanya kitu kibaya.”
“Sawa Brother,” Ako Jay Jay ilibidi awe mpole.
“Naomba twende kwenye gari langu tuzungumze kirafiki.”
“Hakuna tatizo brother.”
Waliongozana hadi kwenye gari na kuingia ndani, muda wote Anko Jay Jay alikuwa na wasiwasi mwingi. Baada ya kutulia Kinape alimuuliza kwa sauti ya chini.
“Unanifahamu?”
“Ha..hapana.”
“Kuwa mkweli, kwa nini ulitaka kunikimbilia?”
“Ulinishtua.”
“Naomba uniambie ukweli la sivyo kifo cha mwanamke aliyefariki leo wewe ndiye utakaye kuwa mtuhumiwa namba moja.”
“Siyo mimi brother, mi nilitumwa nikuchunguze tu kama una mwanamke, zaidi ya hapo sijui lolote, hata mimi nimeshtuka kusikia yule mwanamke ameuawa.”
“Nani alikutuma?”
“Mkeo.”
“Umemjuaje mke wangu mimi usinijue?”
“Nakujua brother.”
“Alikutuma nini?”
“Alinikutuma nikuchunguze kama una mwanamke wa nje, baada ya kazi yangu kwisha nilimpa ripoti na kunipa changu na mimi kuendelea na mambo yangu mengine. Leo mchana nimeshtuka kusikia yule mwanamke ameuawa kwa risasi, kwa kweli sijui lolote zaidi ya kazi ya kukuchunguza tu brother.”
“Kwa hiyo mke wangu ndiye aliyekutuma?”
“Ndiyo brother.”
“Kama yeye alikutuma nani alimuua yule mwanamke?”
“Sijui, labda yeye mwenyewe.”
“Baada ya taarifa ya kifo yeye alikuambiaje?”
“Amesema nisimwambie mtu juu ya kifo kile pia hata mpango wetu wa kuwachunguza.”
“Asante, naomba taarifa hizi usimwambie mke wangu kama tumeonana, sawa?”
“Sawa brother, nitafanya kama nilivyokueleza.”
“Okay endelea na burudani,” Kinape alisema huku akimshikisha noti mbili za elfu kumi.
“Asante brother,” Anko Jay Jay alipokea huku akiwa haamini kama ametoka salama.
Baada ya kuachana na Kinape alimpigia simu Kilole kumweleza kuhusiana na kufuatwa na mumewe usiku ule. Baada ya simu kuita sana ilipokelewa.
“Anko Jay Jay si nimekuambia usinipigia simu mpaka nikupigie mbona unakuwa si mwelewa?”
“Sister kuna jambo la muhimu limenifanya nikupigie simu usiku huu.”
“Jambo gani?”
“Mumeo kanifuata na kunibana juu ya kifo cha yule msichana na kuniomba nisikuambie.”
“ Anko Jay Jay acha utani?” Kilole hakuamini.
“Kweli sister.”
“Amevaaje?”
“Jinsi ya bluu na tishet nyekundu na kofia nyeusi na chini kavaa raba nyeupe.”
“Mmh! Ni kweli,” Kilole alishusha pumzi ndefu.
“Yaani huwezi kuamini nilishtuka kidogo haja ndogo initoke.”
“He, makubwa! Amekuuliza nini?” Kilole alishtuka sana.
”Eti nani kamuua yule mwanamke.”
“Mmh! Kwanza wewe umekujuaje?”
“Nikuulize wewe, kwa vile siri ilikuwa ya watu wawili.”
“Kosa limetendeka wapi?”
“Lazima litakuwa kwako tu.”
“Mmh! Umemjibu nini?”
“Nimwambia sijui lolote.”
“Halafu.”
“Alinibana na kutishia kunipeleka polisi kuwa mimi ndiye muuaji.”
“He! Ikawaje?”
“Nilimchoropoka na kukimbia, sasa usalama wangu utakuwaje?”
“Okay, Jay Jay nimekuelewa nitakujulisha muda si mrefu.”
“Poa sister jambo hili lifanyie kazi naweza kuozea gerezani wakati sijui lolote kuhusiana na kifo hicho.”
“Anko Jay Jay hebu niachie kazi hiyo maana hata mimi suala hilo limenishtua sana, lakini nakuapia huwezi kukamatwa nitamtuliza huyu mshenzi kabla hajafanya lolote.”

Itaendelea
 
SEHEMU: 37
MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
SIMU: 0713 646500

ILIPOISHIA:
“Alinibana na kutishia kunipeleka polisi kuwa mimi ndiye muuaji.”
“He! Ikawaje?”
“Nilimchoropoka na kukimbia, sasa usalama wangu utakuwaje?”
“Okay, Jay Jay nimekuelewa nitakujulisha muda si mrefu.”
“Poa sister jambo hili lifanyie kazi naweza kuozea gerezani wakati sijui lolote kuhusiana na kifo hicho.”
“Anko Jay Jay hebu niachie kazi hiyo maana hata mimi suala hilo limenishtua sana, lakini nakuapia huwezi kukamatwa nitamtuliza huyu mshenzi kabla hajafanya lolote.”
SASA ENDELEA...

“Sawa sister nakutegemea wewe.”
“Usikonde.”
Kilole alikata simu na kukaa kwenye kochi akiwa amechoka na kuamini itakuwa vigumu kwa Kinape kumwelewa akijua yeye ndiye aliyemuua mpenzi wake mwingine. Aliamini kama Anko Jay Jay alikimbia lazima Kinape atamtafute na kumlazimisha kusema ukweli kwa vile ameishaonesha woga lazima angesema kweli. Alijua usiku ule ulitakiwa kila mtu amzidi akili mwenzake kama Kinape aliweza kumzidi akili kwa kumgundua mtu aliyemtumia kumchunguza lazima atataka kujua nani kamuua mpenzi wake.
Baada ya kuwaza na kuwazua alipata jawabu ya kitu kilichokuwa kikimsumbua kuificha siri ile kabla Kinape hajajua ni kumuua Anko Jay Jay usiku uleule. Alichukua simu yake na kumpigia Anko Jay Jay, baada ya kuita ilipokelewa upande wa pili.
“Vipi Sister?”
“Umesema upo wapi sasa hivi?”
“Nakaribia home siku imeishaingia nuksi.”
“Tunaweza kuonana?”
“Wapi?”
“Tukutane daraja la Nyakabungo.”
“Poa nakuja.” Anko Jay Jay alikuwa anakaa jirani na shule ya Mirongo kufika Daraja la Nyakabungo isingechukua dakika tano.
Kilole alikata simu na kwenda ndani kuchukua bastora na kuifunga kiwambo cha kuzuia sauti na kuichomeka kwenye suruali ya jensi na kuvaa vazi lake analolitumia kwenye matukio kama yale.
Alitoka kwa haraka kabla Kinape hajarudi, kwa vile kutoka kwake mpaka kwenye daraja la Nyakabungo hakukuwa mbali hakuitaji kutumia gari alitembea kwa miguu kwa mwendo wa haraka kumuwahi Anko Jay Jay.
Njiani kila gari lililokuja mbele yake na kumuulika na taa aligeuka na kulipa mgongo mpaka lilipopita. Aliliona gari lao dogo na kujua Kinape ndiyo anarudi lazima angemtafuta. Alichepua mwendo hadi karibu ya daraja na kumuona Anko Jay Jay akija kwa mbele akipepesa macho huku simu ikiwa sikioni.
Kilole hakutaka kupoteza muda kwa vile alikuwa kwenye giza alitoa bastora yake na kumlenga kifuani na kuachia risasi mbili zilizomrusha Anko Jay Jay chini ya daraja. Kwa haraka aligeuka na kurudi alipotoka.
Wakati anafanya kitendo kile mlinzi mmoja aliyekuwa kwenye nyumba zilizokuwa upande wa shule ya sekondari ya Lake aliona. Kwa vile alikuwa kwenye kiza aliona tukio lile ambalo lilimshtua lakini alikaa kimya kihofia uhai wake.
Kilole baada ya kutimiza dhamila yake alirudi nyumbani, alipofika alizificha nguo kwa nje na kuelekea kwenye Bar ya karibu na kununua chips mayai kisha alirudi nyumbani. Kinape aliyefika kitambo na kushangaa kutomkuta mpenzi wake. Alipoingia chumbani alimkuta mtoto amelala kitu kile kilimuonesha hayupo mbali.
Alitulia kwenye kochi akiwa na hasira kwa Kilole, alijikuta akipata kigagaziko cha kumuuliza usiku ule. Alipanga kujifanya ametoka kutembea ili asijue chochote. Baada ya nusu saa Kilole alirudi na chipsi kwenye mfuko.
“Vipi baby umerudi zamani?”
“Kiasi, vipi ulifuata chipsi?”
“Ndiyo mpenzi, ulifika mbali?’
“Si sana.”
“Karibu chipsi.”
“Sijisikii kula mpenzi naomba nikapumzike,” Kinape alisema huku akielekea chumbani na kumuacha Kilole akimsindikiza kwa macho.
***
Baada ya kupewa maelekezo ya awali na taarifa kutoka Dar es salaam kuwa kila kitu kimekwenda vizuri anasubiliwa yeye kusafiri tu. Jioni ya siku ile walipanda ndege mpaka Dar. Waliwasili uwanja wa ndege wa J.K .Nyerere jijini Dar majira ya saa moja usiku akiongozana na Teddy pamoja na mwanaye kipenzi Rose. Walipofika walimkuta mwenyeji wao akiwa na kila kitu, mwenyeji wake alipomuona alifurahi na kumkumbatia kwa furaha asiamini kama rafiki yake yupo hai.
“Siamini...siamini Mungu mkubwa,” Bon alimkumbatia Deus kwa furaha mpaka machozi yakamtoka.
“Deus siamini naona kama ndoto yaani ninachokiona siamini,” Bon alisema huku akibubujikwa na machozi ya mshangao.
“Bon ni mitihani ya maisha ni histori ndefu.”
“Unajua siamini naona kama nimeona mzimu wako, wakati wa matatizo yako nilikuwa nje ya nchi na niliporudi nilikutana na Mr Mabina na kunieleza ukiwa gerezani ulipatwa na tatizo lililosababisha upate stroke lililosababisha ulazwe hospitali kwa muda mrefu na mara ya mwisho alikuja kukutembelea aliambiwa amefariki.
“Niliulimia sana rafiki yangu, uliponipigia simu sikuamini baada ya kunifahamisha nilifanya uliyonituma lakini hamu yangu kubwa kukuona leo. Nimefurahi sana mtu niliyelezwa alipooza sehemu mmoja na kusikia umekufa upo hai katika afya njema kweli Mungu mkubwa. Ilikuwaje maana bado naona kama ngamia kapita kwenye tundu la sindano mbele ya macho yangu.”
“Kabla ya yote kwanza nashukuru kwa kazi nzuri uliyonifanyia, naomba tusizungumze lolote niombee Mungu safari yangu nirudi salama nitakupa picha kamili.”
“Naomba hata unidokeze kidogo kwani utaniacha kama mtu aliyeota usiku alipoamka asubuhi aliyoyaona yakabakia ndotoni na si kweli.”
Deus alimdokeza kidogo lakini safari ya Italia hakumweleza anakwenda kufanya nini. Baada ya mazungumzo ya marafiki wawili waliofanya kazi pamoja kwa muda mrefu kabla Deus hajaingia kwenye matatizo walitafuta sehemu yenye tulivu kuzungumza. Deus alikuwa anaondoka usiku ule na ndege ya British Air ways saa nne usiku.
Muda mwingi walikuwa sehemu yenye mwanga hafifu ambayo ilikuwa vigumu kwa watu kuwatambua kwa urahisi. Hawakupenda kuonekana kwa ajili ya usalama wa Teddy. Majira ya saa tatu Deus kabla aliingia chumba cha wageni kujiandaa kuondoka.
Walimuomba Bon awapishe kidogo wazungumze, baada ya kusogea pembeni wapenzi wawili na mtoto wao walizungumza ya mwisho kabla ya safari.
“Sasa mpenzi naomba nikupe maelekezo ya mwisho,” Teddy alimweleza Deus.
“Sawa.”
“Ukifika katika mji wa Sicily kuna Cassino nyingi katika zote nilizokueleza, anazopenda Mose zipo mbili, ni mpenzi sana wa kucheza kamali anazozipenda ni Piedimonte San Germano na Liola Hotel (Aquino) hii Liola ndiyo yenye gharama sana na hata kamali yake ni kubwa. Kama Mose ana fedha hupendelea hoteli hii ambayo ina cassino ndani lakini akiwa ana fedha kidogo japo biashara yetu inakufanya uwe na fedha mpaka kufa, hupenda kwenda San Germano.”
“Nimekuelewa.”
“Unaweza kutembelea Cassino zingine lakini hizi huwa hakosi.”
“Kwa vile mji wa Sicily si mgeni kwangu haitanipa wakati mgumu, hii kazi ni ndogo sana kwangu.”
“Inaweza kuwa ndogo lakini jamaa wale ni wabaya kuua kwao jambo la kawaida, ukikosea mahesabu wanaweza kukupoteza.”
“Si rahisi.”
“Mpenzi mbona unajiamini sana?”
“Watu sampuli ya huyo mshenzi nimepambana nao sana.”
“Nina imani fedha uliyonayo inatosha sana.”
“Inatosha sana, hii kazi nataka kuifanya ndani ya saa 24 niwe nimemaliza kila kitu.”
“Basi nakutakia kila la heri katika safari yako.”
“Nashukuru sana, ila kama mambo yatakwenda kinyume naomba unitunzie mwanangu.”
“Bila shaka nitamlea kama mwanangu wa kumzaa, lakini sitaki ufe bado nakuhitaji baada ya maisha ya mateso nina imani tunahitaji faraja ya mioyo yetu.”
“Mwanadamu amezaliwa na kufa, hivyo hatuwezi kuepuka kufa kama tumezaliwa.”
“Ni kweli lakini Mungu atakutangulia.”
Walikumbatiana kisha alimbusu Teddy na mwanaye Rose, alimwita Bon.
“Best wacha nikajiandae na safari, shemeji yako anarudi Mwanza kesho asubuhi.”
“Hakuna tatizo nikutakie kazi njema, nakubiri kwa hamu najua una mengi ya kunieleza.”
“Tumuombe Mungu anirudishe salama.”
“Nina imani kwa dua zetu wote atakutangulia.”
“Amina.
Aliagana na wote kisha alielekea kwenye ndege kwa ajili ya safari ya kuelelea Sicily Italia.
****
Kinape aliamka siku ya pili akiwa mtu mwenye mawazo mengi kutokana na tabia ya Kilole kuwaua watu wake wa karibu kila kukicha. Alijiuliza hali ile itaendelea mpaka lini, kuwaua watu wasio na hatia. Akiwa sebuleni akitazama taarifa ya habari ya saa kumi na mbili asubuhi, katika taarifa ule ya habari alishtushwa na taarifa ya sikitisha ya kifo cha mtu aliyeamini kwake ni muhimu kuhusiana na kifo cha mpenzi wake Happy.
Katika taarifa ile habari moja ilimshtua baada ya mtangazaji kusema: Kijana mmoja anayefahamika kwa jina la Anko Jay Jay mkazi wa maeneo ya Mirongo jiji Mwanza, ameuawa usiku wa kuamkia siku ile kwa kupigwa risasi mbili za kifuani na mtu aliyekuwa amefunika mwili nzima.
Taarifa iliendelea kusema, mlinzi wa nyumba za jirani ndiye aliyeshuhudia mtu aliyekuwa ameuziba mwili mzima mithiri ya ninja, akimpiga risasi kijana aliyekuwa akija kwa mbele huku akiuliza kwa sauti “Uko wapi?” Bila ya kujua alikuwa akimpigia nani yule mwanamke alitoa bastora na kumpiga risasi iliyomrushia darajani kisha kugeuka kurudi alipotoka.
Taarifa iliendelea kusema:
Mlinzi baada ya kuona kitendo kile alikaa kimya kuhofia uhai wake na baada ya kuondoka muuaji alimjulisha bosi wake na kupiga simu polisi, baada ya polisi kufika waliuchukua mwili wa marehemu na kuupeleka hospitali ya Sekou Toure kwa uchunguzi zaidi.
Mkuu wa polisi aliwataadharisha watu wote kuhusiana na mauaji ya kutisha yanayoendelea nchini hasa jiji Mwanza yanayofanywa na mwanamke anayevaa vazi refu la kumficha kama ninja ambaye amekuwa tishio jijini baada ya kufanya mauaji mawili ya kufuruliza. Mkuu wa polisi amewaomba watu kutoa ushirikiano pale anapoonekana mtu wa aina hiyo ili kumtia nguvuni.
Wakati taarifa ya habari ikiendelea Kilole naye alisimama kwa muda kusikiliza taarifa za kifo cha Anko Jay Jay. Baada ya taarifa ili aliondoka kuendelea na shughuli zake. Kinape aliamini aliyefanya vile alikuwa Kilole lakini ushahidi hakuwa nao hivyo ingekuwa vigumu kumtia hatiani moja kwa moja hasa baada ya mtu aliyemtegemea kutoa ushahidi kumuua.
Alijuliza Kilole kamuua Anko Jay Jay kwa ajili gani? Aliamua kutoka nje ya nyumba akiwa na mawazo mengi sana na kujiuliza hali ile itaendelea mpaka lini. Aliamini mwisho wake angekuwa kama Deus ambaye kwake aliamini amekwisha fariki.
Akiwa anatembea taratibu kichwa chini mikono nyuma kuzunguka nyumba yao alishtuka kuona kitu kama furushi jeusi likiwa pembeni ya maua. Aliinama na kulitazama kwa kulipekua na kipande cha mti kwa kukinyanyua. Aliponyanyua alishangaa kuona bastora ukidondoka chini, aliiokota na kuichomeka kwenye bukta aliyokuwa amevaa na kuificha kwa fulana aliyovaa juu.
Alitupa kipande cha mti na kuinyanyua nguo iliyokuwa kimezungushiwa bastora na kugundua lile ni gauni lefu lenye mtandio wake na kutambaa cha kujifunika usoni na kuwa kama ninja. Kwa mara ya kwanza alipata ushahidi wa nani muuaji japo mwanzo alikisia bila kuwa na ushahidi.
Aliviangalia vitu vile na kukumbuka vitu vingi kuanzia kifo cha mchumba wake na mpenzi wake wote wenye majina ya Happy pamoja na Anko Jay Jay ambaye aliuawa muda mfupi baada wa yeye kuzungumza naye kwa mujibu wa shuhuda.
Aliishika bastora mkononi na kuitazama kwa muda hasira zilimpanda mpaka akaanza kutetemeka. Moyoni alijiapiza siku ile ndiyo ungekuwa mwisho wa kumvumilia muuaji mkubwa asiye na chembe ya huruma aliyemkosanisha na rafiki yake kipenzi Deus na kusababisha kifo chake.
Aliamini baada ya Anko Jay Jay anaweza kufuata yeye aliona dawa ni kumuwahi kabla hajawahiwa. Alibeba zile nguo mkono wa kushoto na mkono wa kulia alishikilia bastora na kuingia ndani kama askari aliyetumwa kumkamata mtuhumiwa wa mauaji.
“Kilole,” aliita kwa sauti kubwa.
Kilole aliyekuwa jikoni akiandaa maziwa ya mtoto, alipotoka alishtuka kukutana na mdomo wa bastora ukimtazama huku mkono mwingine ameshilikia nguo zake za kazi.
“Kinape vipi?” alimuuliza macho yamemtoka pima.
“Kilole kwa nini umemuua Happy?”
“Hilo jibu uliza swali,”Kilole alijibu kwa kujiamini.
“Kwa nini umemuua Anko Jay Jay?” alibadili swali.
“Alistahili kufa.”
“Kwa nini?”
“Sina jibu zaidi ya nililokujibu.”
“Kilole, umesababisha Deus kufungwa, umesababisha nimgeuke rafiki yangu umesababisha kifo chake na kumuacha Rose yatima. Umemuua mchumba wangu Happy umemuua mfanya biashara mwenzangu Happy na mwisho umemuua Anko Jay Jay.”
“Kinape kina kitu unajua unataka nikujibu nini?”
“Naomba jibu kwa nini umewaua?”
“Sina jibu, unataka kunifanya nini wakati unajua kila kitu?”
“Nataka na wewe uwafuate wenzako,” Kinape alisema huku akitetemeka na jasho kumtoka bastora kaielekeza kwa Kilole.
“Kwa hiyo unataka kuniua?”
“Lazima ufe Kilole, siwezi kuishi na mwanamke mwenye roho mbaya kama wewe.”
“Haya niue,” Kilole alisema huku akisogea mbele ya mdomo wa bastora.
Baada ya kusimama mbele ya bastora bila kufanywa jambo lolote alishika bastora na kuanza kunyang’anyana. Kila mmoja alitumia nguvu kwa Kilole kutaka kunyanyang’anya na Kinape kuing’ang’ania.
Kwa bahati mbaya katika kugombea kidole cha Kinape kilichokuwa katika kifyatulio kiliminya kifyatulio kilicho fyatuka na kusababisha risasi mbili zitoke na kumuingia mtu chini ya kifua.
“Aah!” ilikuwa sauti iliyoonesha risasi kumuingia.
Taratibu mmoja aliteremka chini huku damu zikimtoka chini ya kifua, mwingine alishtuka na kutaharuki na kumtazama mwenzake aliyekuwa ametoa macho pima huku akisema kwa sauti ya mawimbi. Alimuwahi na kumpakata huku mkono ukijitahidi kuziba sehemu zilipoingia risasi na kuufanya mkono mtote damu.
“U.u..u..me..ni..ua...,” ilikuwa sauti ya mawimbi.
“Nooo...samahani... bahati mbaya.. hu..wezi kufa,” alisema kwa sauti ya kilio ikifuatiwa na machozi.
“Na..na..kufa...ume..ni..ni..,” alisema kwa shida huku damu ikimtoka mdomoni na kuweka michirizi pembeni ya mdomo iliyoteremka mpaka kwenye mapaja ya aliyemkumbatia.

Itaendelea
 
SEHEMU: 38
MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
SIMU: 0713 646500
ILIPOISHIA:
“U.u..u..me..ni..ua...,” ilikuwa sauti ya mawimbi.
“Nooo...samahani... bahati mbaya.. hu..wezi kufa,” alisema kwa sauti ya kilio ikifuatiwa na machozi.
“Na..na..kufa...ume..ni..ni..,” alisema kwa shida huku damu ikimtoka mdomoni na kuweka michirizi pembeni ya mdomo iliyoteremka mpaka kwenye mapaja ya aliyemkumbatia.
SASA ENDELEA...

“Huwezi kufa...usife... mpenzi wangu kazi yote niliyofanya imekuwa bure.”
“Naomba Deus a..ni..ni..samehe sana, ni..ni..na imani nina deni zito kwa..kwa..a ke.”
“Jamani huu mkosi gani....Ki..Ki..Ki..,” alishindwa kumalizia jina kwa uchungu ulikuwa mkubwa moyoni.
“N.n.na..na..ku.ku.f..f.,” damu ilijaa mdomoni na sauti ilishindwa kutoka nuru ya macho ilipotea taratibu roho iliachana na mwili. Alimtikisa kwa nguvu huku akimwita jina lake lakini hakuwa na jibu macho yalikuwa yametulia kama alikuwa akimtazama lakini tayari roho iliachana na mwili.
****
Sauti ya tamu ya kike ya mhudumu wa ndege ya British Air ways ilimshtua Deus aliyekuwa amepitiwa na usingizi:
“Ndugu abiria wa ndege yetu ya British Air ways, ndege yetu ndiyo inakaribia kutua katika uwanja wa Sicily, tafadhali mnaombwa mfunge mikanda, tunawatakia safari njema yenye furaha, asanteni.”
Deus alifumbua macho na kuangalia saa yake ilimuonesha ni saa mbili na nusu za usiku. Alichukua mkanda wake na kujifunga kisha alitulia huku abiria wengine nao wakijifunga mkanda. Baada ya muda ndege iliteremka uwanjani na matairi kugusa rami na kutembea kwa muda kabla ya kusimama.
Deus alikuwa wa mwisho kuteremka kwenye ndege, alitoka taratibu na Brifcase yake mkononi. Baada ya kufanyiwa upekuzi alitoka nje ya uwanja wa ndege na kupokewa na dereva wa teksi.
“Habari ndugu.”
“Nzuri.”
“Karibu Sicily,” Dereva mwenye asili Kichotara alimkaribisha Deus.
“Asante.”
“Unaelekea wapi?”
“Liola Hotel (Aquino).”
“Hakuna tatizo.”
Deus aliingia kwenye gari na kuelekea mjini akilakiwa na mataa yaliyoupendesha mji wa Sicily kwa taa.
“Pole na safari?” dereva alionekana mcheshi alimsemesha Deus aliyekuwa kimya akitafakari safari yake.
“Asante.”
“Kaka wewe ni mgeni mji huu?”
“Kwa nini?” swali lile lilimfanya Deus aache kuangalia mitaa na kumtazama dereva.
“Mbona hapa jijini kuna hotel tulivu zipo pembeni ya mji karibua na upepo wa bahari unakwenda hotel ile.”
“Ni uamuzi tu, shughuli zangu huzifanyia karibu na ninapokwenda.”
“Na kweli, kuwa katika hoteli ya karibu na shughuli zako ni vizuri.”
“Nashuku kwa kulielewa hilo.”
“Umekuja kibiashara?”
“Ndiyo.”
“Biashara gani? Naweza kuwa msaada kwako.”
“Biashara yangu aihitaji msaada wa mtu.”
“Okay, nilidhani utahitaji mwenyeji.”
“Mi mwenyewe ni mwenyeji hivyo sihitaji mwenyeji mwingine.”
Wakati huo teksi ilikuwa ikikata kona kuingia Liola Hotel (Aquino), baada ya kuegesha kwenye maegesho dereva alimwambia mgeni wake.
“Nina imani tumefika salama?”
“Nashukuru.”
“Hata uendeshaji wangu nina imani umeupenda?”
“Ni kweli, wewe ni dereva mzuri.”
“Basi ndugu yangu atakapokuwa ukija hapa kwa shughuli zako usiache kunitafuta ndugu yako, kadi yangu hii hapa, naitwa Abdul.”
“Hakuna tatizo, nitakutafuta,” Deus alisema huku akipokea ile kadi ya biashara ya Dereva Abdul.
“Hakuna tatizo, vipi totoz?”
“Nikihitaji nitakutafuta.”
“Usiwe na wasiwasi sisi ndiyo wenyeji wa mji huu, ukiingia kichwa kichwa unaweza kukombwa kila kitu.”
“Hakuna tatizo.”
Baada ya kumlipa chake aliteremka kwenye gari na kuingia ndani ya hoteli na kwenda moja kwa moja mapokezi na kupokewa na msichana mrembo.
“Karibu kaka.”
“Asante.”
“Unahitaji msaada?”
“Ndiyo, nataka chumba.”
“Unataka cha juu au chini?”
“Nataka ghorofa ya pili.”
“Umepata.”
Baada ya kuandikisha mapokezi alipewa msichana aliyempeleka mpaka chumbani kwake. Baada ya kumfikisha msichana aliyempeleka alimwambia kwa sauti tamu:
“Karibu sana.”
“Asante.”
“Nina imani imeridhishwa na huduma yangu pia vyumba vyetu?”
“Ni kweli, huduma yako ni nzuri pia chumba ni vizuri sana.”
“Utahitaji huduma zaidi?”
“Kama ipi?”
“Najua usiku utakuwa mrefu sana kama ukilala peke yako, ukiniihitaji nikupe kampani nitakuwepo leo kwa ajili yako,” binti mrembo alisema kwa sauti ya wizi.
“Nashukuru, nikuhitaji nitakujulisha.”
“Naitwa Loveness na namba yangu ya simu hii piga muda wote usihofu,” yule msichana alimpa kikaratasi alichokuwa kimeandikwa namba ya simu na kumfanya Deus ajiulize ameandika muda gani ikiwa muda wote walitembea pamoja kupanda juu.
“Nashukuru,” Deus alikipokea kile kikalatasi na kumwacha yule msichana aondoke.
Baada ya kuondoka alifunga mlango na kwenda kujitupa kitandani kama mzigo macho yake yakitazama juu. Aliusikia mwili wake ulivyochoka kutokana na kusafiri saa 24 bila kupumzika. Uchovu aliousikia aliamini akijiegesha lazima atalala na yeye alitaka kazi ile aianze usiku ule. Japokuwa alikuwa amechoka sana hakutaka kupumzika
Alijinyanyua kitandani na kukaa kitako, alipoangalia saa yake ilimuonesha ni saa nne na dakika saba, baada ya kuweka mizigo yake aliteremka upande wa Cassino. Alipofika upande wa Cassino kila mtu alikuwa yupo bize na mambo yake.
Alielekea upande watu wakiokuwa wakicheza kamari huku wakinywa pombe, alizunguka taratibu kila kona bila kumuona mtu aliyemfuata. Alitulia kwa muda wa saa nzima akizunguka kila kona. Saa tano iliingia bila kumuona, alitoka hadi hotelini na kuagiza chakula kutokana na njaa aliyokuwa akiisikia.
Baada ya kula alirudi tena Cassino lakini hakumuona mtu wake, alisubiri mpaka saa sita bila dalili za kuonekana Moses. Aliamua kwenda kuoga ili amtafute Abdul ampeleke hoteli nyingine. Baada ya kuoga alimpigia simu Abdul dereva wa teksi. Baada ya siku kuita ilipokelewa:
“Haloo.” Simu ilipokelewa upande wa pili.
“Haloo mr Abdul.”
“Haloo, nani mwenzangu?” Abdul aliuliza.
“Aah! Bwana Abdul si tumeagana muda si mrefu?” Deus alishangaa kuulizwa jina, lakini alikumbuka alichukua namba ya dereva bila kumpa yake.
“Nimeagana na watu wengi, hebu nikumbushe.”
“Ndugu yangu hata sauti huijui?”
“Ooh! Mgeni wangu wa Liola Hotel (Aquino)?”
“Ndiyo.”
“Okay, unahitaji huduma gani kwa sasa?”
“Kwani una huduma ngapi?”
“Kaka si tulizungumza kama unahitaji mtoto wa kukusaidia kuuvusha usiku na usafiri.”
“Kwa sasa nahitaji usafiri.”
“Unataka kwenda wapi usiku wote huu?”
“Utajua ukifika.”
“Poa, nakuja muda si mrefu.”
Japo mwili wa ulikuwa umechoka Deus aliamini siku ile hakutakiwa kuupitisha bila kufanya kazi iliyompeleka, alikuwa radhi ya siku ile ashinde kama popo kwenye kwenye Cassino zaidi ili tu kumtafuta Moses bila kuwa na uhakika kwa kumpata kwake aliona akicheza pata potea.
Baada ya muda simu yake iliita ilikuwa namba ya Abdul, alichukua bastora yake na kuipachika kiunoni kisha aliteremka chini. Alimkuta Abdul anamsubiri alipomuona alisogeza gari karibu yake na kumfungulia mlango. Deus aliingia na kumueleza:
“Nipeleke Piedimonte San Germano.”
“Hakuna tatizo, inaonekana mzee mtu wa kujirusha, eeh?”
“Hapana kuna mtu namfuata.”
“Hakuna tatizo,” dereva alisema huku akikanyaga mafuta baada ya gari kuingia barabara kuu. Kutokana na uchache wa gari barabarani walitumia dakika kumi kufika Piedimonte San Germano. Abdul alipaki gari kwenye maegesho na kumgeukia Deus aliyeoneka anawaza kitu.
“Mheshimiwa tumefika.”
“Okay nashukuru,” Deus alijibu huku akifungua mkanda na kutoa bochi ili amlipe.
”Kiasi gani?”
“Kwani si nakusubiri au nakuacha?”
“Sijui nitachukua muda gani lakini nahitaji huduma yako kwa muda wote nitakaokuwa hapa.”
“Kwa hiyo nikusubiri?”
“Ndiyo maana yake.”
“Kumbuka kuna chaji ya kukusubiri.”
“Usihofu nitalipa.”
“Nikusibiri hapa au tuingie wote.”
“Siyo mbaya tunaweza kuingia wote.”
Walitoka ndani ya gari na kulifunga gari kwa rimoti kisha waliongozana ndani ya ukumbi. Kwa vile hakuwa mgeni wa sehemu zile alitafuta meza moja na kukaa na Abdul kisha waliagiza vinywaji. Deus alitumia nafasi ile kumuacha Abdul mara moja na kuelekea upande wa cassino.
“Mzee nakuja,” alisema huku akinyanyuka.
“Hakuna tatizo.”
“Suala la malipo usiwe na wasiwasi nitamaliza mimi.”
“Najua nipo na mtu mzito.”
Deus aliachana na Abdul na kuelekea upande cassino ambako kulikuwa kumechangamka kulikuwa na watu wengi kila mtu alikuwa bize na kucheza kamali huku akinywa pombe. Alizunguka kila sehemu bila kuiona sura ya Mose, alirudi alipokuwa amekaa Abdul akiamini sehemu ile ilikuwa ndiyo karibu na njia ya kuelekea upande wa kuchezea kamali hivyo angeweza kumuona kila aliyeingia na kutoka ndani.
Muda ulikatika bila Mose kutokea kitu kilichozidi kumchanganya na kuona njia waliyotumia kumtafuta Mose ilikuwa ya kitoto heri angemuelekeza anapoishi kuliko kumtafutia cassino. Alianza kuiona kazi inaanza kuwa ngumu, lakini hakukata tamaa aliendelea kukaa pale kuangalia waliokuwa wakiingia na kutoka.
“Mzee unaonekana haupo sawa?” Abdul alimuuliza baada ya kumfuatilia kwa muda mrefu.
“Kivipi?”
“Toka timefika unaonekana kuna kitu unakitafuta.”
“Nakuja,” Deus alisema huku akinyanyuka baada ya kumuona mtu mmoja anayefanana na Mose akipita akielekea upande wa kaunta. Kwa vile alikuwa amempa kisogo hakuwa na haraka ya kumfuata. Alimwacha asogee mbele kidogo kisha alimfuata nyuma taratibu ili amuone mtu yule anayefanana Mose anakwenda upande gani.
Alimuona amesimama kaunta na kuagiza kinywaji, hakuwa na haraka naye alimwacha mpaka atulie. Japo mtu yule alimfananisha na Mose kilichomshangaza alikuwa peke yake tofauti na maelezo ya Teddy kuwa Mose alitembea na kampani ya vijana wa kihuni.
Alimuona yule mtu akihama kwenye kaunta na kusogea sehemu ya kuchezea kamali alisogea taratibu hadi alipokuwa na kumtazama usoni kwa chati.
Alipomtaza vizuri aligundua kumbe siye mwenyewe, alijikuta akijifyonza na kurudi sehemu yake. Pamoja kuwa na Abdul mawazo yake yalikuwa mbali kila muda aliangalia saa yake ya mkono na kuuona muda ukizidi kukatika bila mhusika kutokea.

Itaendelea
 
SEHEMU: 39
MTUNZI: Ally Mbetu ‘Dr Ambe’
SIMU: 0713 646500

ILIPOISHIA:
Alipomtaza vizuri aligundua kumbe siye mwenyewe, alijikuta akijifyonza na kurudi sehemu yake. Pamoja kuwa na Abdul mawazo yake yalikuwa mbali kila muda aliangalia saa yake ya mkono na kuuona muda ukizidi kukatika bila mhusika kutokea.
SASA ENDELEA...

Mpango wa kumtafuta mtu kwenye Cassino aliuona wa kitoto badala ya sehemu anayoishi ambayo ingemfanya aifanye kazi ile kwa uhakika mkubwa, japokuwa Teddy alimweleza Mose ana tabia ya kujesha club kuliko kuwepo nyumbani.
Kila dakika alitupia jicho kwenye saa na kumuonesha muda unazidi kutaradadi, mishale ilimuonesha ni saa nane kasoro usiku. Alijikuta akijifyonza mwenyewe kila dakika kitu kilichomfanya Abdul kumuuliza.
“Kaka vipi mtu aliyemfuata amechelewa nini?”
“Aah! Kuna Cassino ngapi maarufu kwa kamari jijini?”
“Mmh! Zipo nyingi tofauti na ulipopanga na hapa kuna Piazza Marcom, Gari, Forum Palace na nyingine nyingi ila kati ya hizi moja utafurahi.”
“Sasa fanya hivi nirudishe mara moja hotelini ili unipeleke ya karibu.”
“Ya karibu ni Piazza Marcom.”
Walilipa vinywaji na kutoka huku moyoni Deus akianza kuona ugumu wa kazi iliyopo mbele yake, mwili nao ulikuwa umechoka kutokana na safari ya saa 24 angani. Alitamani kurudi hotelini kulala lakini hakukubaliana na hali ile. Abdul alikimbiza gari na kutumia muda mfupi kurudi hotelini.
“Niteremshie hapa wee kageuze,” Deus alimwambia Abdul aliyelisimamisha gari katikati ya barabara.
Gari lililokuwa kija mbele lilisimama na kupiga hodi, Abdul alipotaka kuliondoka gari Deus alimwambia:
“Waache wasubiri,” alisema huku akiteremka kwenye gari.
Waliokuwa kwenye gari la mbele walianza kutukana:
“Wee fala ondoa uchafu wako barabarani.”
Kauli ile ilimfanya Abdul azime gari kabisa na kumfanya Deus amshangae.
“Vipi Abdul,” Deus alimuuliza akiwa bado amesimama pembeni ya gari.
“Hawa watoto hawanijui, kuuza midawa yao ya kulevya haiwezi kuwafanya watudharau wakubwa zao.”
“Unawajua?”
“Nawajua si wazungu wa unga hawa.”
“Oyaa wee fala ondoa kopo lako, “ aliteremka kijana mmoja aliyekuwa amevaa kofia kwa kuigeuza nyuma na kupiga ngumi kwenye boneti ya gari.
“Ondoaa Ondoaaa.”
Kitendo kile kilimfanya Abdul kutoka kwenye gari na kwenda kumbeba mzimamzima na yule kijana na kwenda kumtupa kwenye gari lao. Wenzake walitoka kishari.
“Nyie paka hakuna hata mmoja anaweza kunigusa au mnataka nilipasue gari lenu?” Abdul aliyekuwa amejengeka kimazoezi akitamba mbele ya wale vijana.
“Basi brother unajua mwenzetu amelewa,” jamaa mmoja alisema huku akimvuta mwenzake aliyeoneka amekunywa kidogo.
“Mose waambie wenzako mimi nani?” Abdul aliendelea alijitapa.
Wakati Deus akisogea karibu na Abdul ili kumsaidia kwa lolote macho yake yalipata mshtuko baada ya kumuona mtu aliyekuwa akimtafuta sana. Mose aliwatuliza wenzake na kurudi ndani ya gari lao. Abdul aliingia ndani ya gari lake na kuitoa gari njiani.
Deus alipata wazo la haraka na kurudi kwenye gari na kumfanya Abdul amhoji:
“Vipi mbona umerudi?”
”Naomba tuwafuate hawa popote wanapokwenda.”
“Achana nao watatupotezewa muda.”
“Kuna kitu nataka kujua.”
“Gharama zinaongezeka.”
“Usiwe na wasiwasi wee fanya kazi fedha siyo tatizo.”
“Kama bado unayo yangu achana nao,” Abdul alisema huku akiliacha gari la kina Mose likiingia barabarani na kuondoka kwa kasi.
“Abdul utaniudhi ifuate ile gari hakikisha hulipotezi,” Deus alisema kwa sauti ya amri.
Abdul aliwasha gari na kuliondoa kwa kasi kulifukuza gari la kina Mose lililokuwa likimbizwa kwa kasi ya ajabu na kushindwa kuliona kila walivyokanyaga mafuta hakufanikiwa kuliona.
“Abdul tutawaonaje wale watu?”
“Mmh! Kwa kweli sijui, si unajua uwezo wa gari lao na langu, hata kama tungewafuata nyuma wangetuacha lile gari habari nyingine hata bei yake mbaya wananunua wazungu wa unga tu.”
“Sasa watakuwa wamekwenda wapi?” Deus alianza kuchanganyikiwa.
“Lazima watakuwa wamekwenda Piedimonte San Germano, ndiyo club iliyopo mbele,” Abdul alimtoa wasiwasi.
“Basi twende tuwawahi.”
“Kwani kuna nini? Wewe ni polisi?”
“Hapana, kuna mtu nina shida naye katika wale vijana.”
“Hakuna tatizo.”
“Yule anayeitwa Mose unamfahamu?”
“Ndiyo.”
“Anakaa wapi?”
“Kwa kweli sijui huwa tunakutana sehemu hizi.”
“Unamjua vipi Mose.”
“Mmh! Yule kijana ana historia ndefu kwanza inasadikiwa na fedha sana hata lile gari ni lake, pili ameponea tundu la sindano kwenye kinywa cha mauti. Inasemekana walidhulumiana mshiko na wenzake, si unajua wale wazungu wa unga.”
“Nani aliyemfanya vile?”
“Wengi walijua labda shemeji yake, lakini baadaye alikataa, mpaka sasa haijajulikana nani aliyemfanyia kitu kama kile, Kwa sasa imekuwa kimya hakuna tena habari zile.”
Abdul alipunguza mwendo ili akate kona kuingia Piedimonte San Germano, bahati nzuri lile gari waliliona na kwenda kupaki pembeni yake.
“Imekuwa vizuri tumewakuta,” alisema Abdul huku akizima gari.
“Kazi nzuri,” Deus alijibu huku akiteremka kwenye gari na kuelekea ndani ya Cassino haikupita muda Abdul alikuwa pembeni yake.
Walitembea kwa mwendo wa haraka mpaka ndani ya cassino.
“Abdul nisubiri hapa,” Deus alimuacha Abdul sehemu ya mwanzo na kuelekea kwenye kamali.
Alipofika alimkuta Moses akiwa ameshikilia bunda la dola mkononi akijiandaa kucheza, pembeni alikuwa na rafiki zake ambao walionekana ni wapambe wake. Kwa hali ile aliamini anaweza kukesha bila kufanya jambo lolote, ilibidi atumie akili za kuzaliwa kuweza kumtoa Mose sehemu ile kabla hajaingia kwenye kamali.
Alirudi hadi kwa Abdul aliyekuwa amekaliwa na mwanamke mmoja aliyekuwa sehemu ya mwili wake wazi na kuchezeana. Alisogea mpaka karibu ya Abdul na kuishika siraha yake kwa kuamini muda si mrefu itakuwa ama zao ama zake na damu itamwagika.
Alipoangalia saa yake ilimuonesha ni saa tisa na nusu za usiku ulikuwa umebakia muda mchache kuingia alfajiri ambayo ingemuharibia shughuli yake ya siku ile.
JIJI DAR ES SALAAM
Akiwa bado ameishikili mwili ambao aliamini kabisa ulikuwa umetengana na roho, aliutikisa tena huku akijiona kama amefanya kazi ya bure ya kubeba maji kwenye gunia. Akiwa kama mtu aliyekuwa akizungumza na mtu aliye hai kwa kuutikisa mwili usiokuwa na uhai.
“Mpenzi amka...amka mpenzi wangu...kuna faida gani ya mimi kuendelea kuishi kama wewe niliyekutegemea umekufa....Wewe ndiye aliyefanya nifanye yote haya.”
Aliukumbatia mwili wa mpenzi wake kama amempakata mtoto mdogo, machozi yake yaliangukia kwenye paji la uso wa marehemu.
“Mpenzi...bahati mbaya..Ki..Ki.. samahani... sikukusudia kukuua bahati mbaya...Eeh! Mungu kwa nini umemchukua mtu huyu wakati bado namhitaji sana.”
Wakati huo mtoto ndani alikuwa akilia kwa sauti kwani ndiyo alikuwa akiandaliwa maziwa. Aliuweka mwili chini bila kujifuta damu alikwenda chumbani na kumchukua mtoto na kumbeba akiwa na damu zake mkono. Alitoka naye hadi pembeni ya mwili wa marehemu alipiga magoti na kumweleza mwanaye ambaye alikuwa hajui chochote.
“Gift mwanangu huna tena baba tena... Baba yako amekufa.. Kinape amka umuone mtoto wako ataishije bila baba?” Kilole machozi ya majuto yalimtoka kama maji.
Gift kama alisikia alichoelezwa na mama yake, aliangua kilio kama kauguzwa moto, kila alivyombembeleza hakunyamaza. Kilole alijikuta naye akiangulia kilio akiwa bado amepiga magoti mbele mbele ya mwili wa Kinape aliyekuwa amefariki muda mrefu.
Akiwa hajui afanye nini, sauti ya mlango kugongwa ilimshtua, kwa haraka alikwenda hadi mlangoni na kufunga kwa ndani badala ya kufungua kisha alishusha mapazia yote. Aliuvuta mwili wa Kinape hadi chumbani na kutengeneza michirizi ya damu toka sebuleni hadi chumbani.
Kwa haraka alichukua dekio na ndoo ya maji ya kuanza kuifuta damu, wakati huo mlango uliendelea kugongwa na kuzidi kumuweka Kilole kwenye wakati mgumu na kujiuliza atakuwa nani. Alijikuta akipata wazo baya na kwenda chumbani kuchukua bastora ili kumzimisha anayegonga mlango moyoni aliapa hatakubali kushikwa kirahisi lazima afe na mtu.
Alipotaka kwenda kufungua mlango alisita kwanza alirudi ndani na kusafisha damu iliyokuwa kwenye zuria aliubeba mwili wa Kinape kwa shida na kuulaza kitandani kisha aliufunika shuka na kuhakikisha nguo zote zenye damu anaziweka bafuni.
Baada ya kuhakikisha hakuna damu sehemu zote alipuliza pafyumu ili kuondoa harufu ya damu mbichi. Baada ya kupulizia manukato kila kona alitoka hadi mlangoni na kufungua mlango. Lakini nje hakukuwa na mtu yeyote alizunguka nyumba lakini hakumuona.
Alirudi ndani na kujiuliza atafanya nini baada ya kumuua bila kukusudia mwanaume aliyemfanya afanye yote yale. Moyoni alitamani awatafute wote aliowaua kwa ajili ya Kinape ili awaombe msahama. Alitamani kulijua kaburi la mume wake Deus ili akamuombe msamaa kwani nguvu zote alizotumia ilikuwa kazi bure.
Wazo lililomjia lilikuwa kutafuta vijana wa wamchimbie shimo ili usiku amzike mwili na Kinape, kwa kuhofia kama akikaa sana na mwili unaweza kuharibika na kutoa harufu na kusababisha kutiliwa mashaka. Wazo lile lilimpa ujasiri na kumbeba mtoto wake na kufunga nyumba kisha alielekea kijiweni kutafuta vijana wa kumchimbia shimo ambalo ndilo litakuwa kaburi la Kinape
****
Nyuma ya meza kubwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai DCI Karimu Swago aliyekuwa kimya akiisoma ripoti ya mauaji ya kutisha yaliyotokea kwa muda mfupi Jiji Mwanza na muuaji alikuwa mwanamke anayevaa vazi refu jeusi linalouziba mwili wake na kuwapa wakati mgumu jeshi la polisi kumjua ni nani.
Baada ya kuisoma alimgeukia mkuu wa upelelezi Athumani Fukwa.
“Fukwa,” alimwita huku akimkazia macho.
“Mkuu.”
“Mpaka sasa mmefikia wapi mauaji haya?”
“Mkuu kwa kweli bado tunapambana lakini bado hatujajua ni nani anayefanya mauaji haya.”
“Kwa hiyo mnataka kuniambia chombo cha dola tumeshindwa?”
“Hapana mkuu, bado tunaendelea na upelelezi.”
“Hapa naona kuna mtu anaitwa Kinape, mmesisha mtia mikononi?”
“Mkuu simu yake haipatikani.”
“Kama haipatikati mmetumia mbinu gani kumpata?”
“Mkuu bado tunaendelea na upalelezi ikiwa pamoja na kuhoji waliokuwa wapenzi wa marehemu Happy aliyeuawa Gorden Crest.”
“Mmh! Na kuhusu familia ya Anko JayJay inasemaje?”
“Kwa kweli hawajui lolote kutokana na marehemu kufanya mambo yake kivyakevyake bila kumshirikisha mtu yeyote.”
“Alikuwa akifanya kazi gani?”
“Wanamwita martpapas.”
“Wana maana gani?”
“Hakuwa anachagua kazi kila kazi uliyokuja mbele yake aliifanya.”
“Hakuwa na rafiki wa kike?”
“Hilo tuliuliza, tuliambiwa hakuwa na mwanamke mmoja hivyo ilikuwa vigumu kumjua nani aliyekuwa akijua habari zake kwa siku ile.”
“Mliwatafuta na kuwahoji?”
“Ndiyo,tuliwapata wachache, wote walisema walikuwa na muda mrefu bila kumtia machoni.”
“Hana mtu wake wa karibu?”
“Yupo lakini inaonesha aliondoka siku tatu kabla ya kifo cha Anko Jayjay.”
“Alikuwa na umuhimu wa kumuhoji, inawezekana kuna vitu anavijua vinaweza kutusaidia kupata mwanga.”
“Hakuna tatizo mkuu tulimueleza tukiwa na shida naye tutamtafuta.”
“Basi atafutwe mara moja nataka jioni nipate jibu mmefikia wapi, haiwezekani tuchezewe kiasi hiki tumekaa kimya. Hamjui tunaiabisha sifa ya jeshi letu makini lenye nguvu,” DCI Swago alisema kwa sauti ya amri.
“Sawa mkuu.”
“Basi naomba kazi ifanyike mara moja naamini hatujashindwa kama hamuwezi nitaingia mwenyewe mstari wa mbele.”
“Kazi itafanyika mkuu,” Mkuu wa upelelezi Fukwa alimhakikishia mkuu wake kazi itafanyika.
Baada ya kutoka kwenye kikao na mkuu wake wa kazi, Fukwa aliwaita vijana wake wa kikosi maalumu na kutoa amri ya kijeshi.
“Nina imani mmemsikia mkuu, kwa hiyo sitaki kusikia tena muuaji bado anatamba, mpaka kesho jioni nataka tuwe tumemkamata. Sijui mtamkamata vipi, hiyo si juu yangu bali kusikia yupo mikononi mwa polisi, sawa?” Mkuu wa upelelezi Fukwa.
“Sawa mkuu,” vijana aliitikia kikakamavu.

ITAENDELEA JUMATATU
 
Back
Top Bottom