Hadithi: Mikataba ya kishetani

***

Kwa mara ya kwanza risasi ya ‘Mkono wa Jibril’ilikosa shabaha na kumpata mtu ambaye hakukusudiwa? Ni swali jingine ambalo lilimsumbua Joram. Mauaji yake mengine yote yalionekana kuwa na sababu fulani. Rais aliyeuawa alikuwa katika vuta nikuvute ya madaraka na wasaidizi wake wa karibu, hatua iliyopelekea mapinduzi. Bilionea aliyeuawa anaaminika kuuzwa na mkewe kwasababu za urithi, ingawa mahakama hazikupata kuwa na ushahidi. Kiongozi wa kidini aliyefumuliwa madhabahuni anashukiwa kuwa kifo chake kiliandaliwa na uongozi wa kanisa kwaajili ya kumwondoa katika orodha ya makadinali waliokuwa wakitarajiwa kuchukua nafasi ya papa. Cleopatra anaingia vipi katika orodha hiyo? Joram alikisumbua kichwa chake.

Jogoo aliyewika toka mahala fulani alimzindua Joram. Alipoitazama saa yake alishangaa kuwa ilikuwa saa kumi na robo za alfajiri. Kazi iliyokuwa mbele yake haikuwa lele mama. Alihitaji usingizi. Alihitaji akili zake zote na utulivu wake kuanzia kesho. Akaifunga kompyuta yake na kuzima taa.

Kwa mara ya kwanza, kwa kipindi cha miaka mingi, Joram alijikuta akipiga magoti na kusali kabla ya kupanda kitandani na kuanza kuutafuta usingizi.

10

Abdul Kopa hakuzaliwa muuaji. Dunia ndiyo iliyomtengeneza kuwa hivyo. Ni pale usiku mmoja alipojikuta mikononi mwa polisi akituhumiwa kwa ujambazi. Hakuelewa,kwani dakika tano zilizopita alikuwa mtu huru, mwadilifu, akitoka zake dansini. Dakika tano baadaye alikuwa mtuhumiwa, pingu mikononi, akipelekwa mahabusu, kisa? Kwamba alikuwa jambazi.

Kesho yake alipelekwa mahakamani na kusimamishwa kizimbani. Pamoja naye walikuwepowatu wengine watatu waliodaiwa kushirikiana naye. Walisomewa mashitaka matatu ya ujambazi wa kutumia silaha na moja la kuua. Washtakiwa hawakutakiwa kujibu lolote, hivyo walirudishwa rumande kwa maelezo kuwa ushahidi haujakamilika. Kila mtuhumiwa alikuwa mgeni machoni mwa Kopa, hali iliyofanya aone kama ndoto ile pindi wakivishwa tena pingu na kupelekwa gereza la keko chini ya ulinzi mkali.

Kuna mwanasheria mmoja wa kike aliyeuawa na jirani yake, Mtanzania mwenye asili ya Kiasia, ambaye alikuwa akipiga risasi ovyo kutishia majambazi alioambiwa kuwa walikuwa wakija dukani kwake. Mwanasheria huyo, aliyekuwa mlangoni kwake akishuhudia sakata hilo, alipatwa na risasi ya ubavuni na kuanguka. Jitihada za kumwokoa zilishindikana pale alipokata roho, katika hospitali ya Muhimbili, siku tatu baada ya kufikishwa hapo. Mtuhumiwa halisi wa mauaji hayo alikaa rumande nusu saa tu, akatoka. Miezi mitatu baadaye ndipo walipopatikana akina Abdul Koba ambaye mmoja wao alidaiwa kukiri kosa hilo.

Kama kawaida ya enzi hizo, kesi ilinguruma kwa miaka. Koba na wenzake wakisota rumande kwani kesi yao haikuwa na dhamana. Waliteseka kwa chakula kibaya, malazi duni na mateso tele ya Kisaikolojia. Robo tatu ya mahabusu wenzao wakiwa wahalifu wa kweli, Koba alijikuta katika darasa la aina mpya, darasa la mbinu za kukwepa hukumu, mbinu za uhalifu na mbinu za kuishi gerezani humo. Baadhi ya ‘walimu’ wakiwa wahalifu sugu, Koba alijikuta akipokea kile ambacho Waingereza huita ‘From the Horses mouth’ aidha kwa kukaa nao pamoja kwa muda mrefu, wakishirikiana kwa hili na lile, palepale alianza kujiona mmoja wao.

Hukumu ilipotoka Abdul alifungwa miaka kumi jela. Kwa kalenda ya jela na muda aliokaa rumande, alitumikia kifungo hicho kwa miaka minne tu. Miaka ya mateso, miaka ambayo kila siku aliyoishi gerezani humo ilimfanya azidi kupandwa na hasira, hasira ambazo alizielekeza kwa jamii nzima; wanasiasa wanaolea mfumo wa kishetani kama huo, majaji na mahakimu ambao wanatekeleza, wananchi ambao wanaufumbia macho na wengineo.

Hasira ambazo zilimfanya mara alipotoka gerezani humo aamue kuwa ‘mnyama.’ Alianza kwa kushiriki ujambazi wa kuvunja majumba na kupata magari. Alishiriki pia katika wizi wa kalamu pamoja na silaha katika mabenki. Mtu yeyote aliyejifanya kizingitikati yake na kazi yake hakumwacha hai.

Mahabusu paligeuka nyumba yake ndogo. Akiwa tayari anao mlolongo mrefu wa marafiki katika jeshi la polisi na vyombo vya sheria, kuingia na kutoka mahabusu ilisababisha muda mfupi baadaye aanze kupewa ‘kazi’ na baadhi ya polisi haohao. Mambo yalimnyookea zaidi pale alipojenga urafiki na kigogo mmoja wa usalama ambaye alimpa majukumu nyeti na kumlipa ujira wa kusisimua sana.

Miaka sita baadaye, Abdul Kopa, aliyetoka gerezani hakuwa yule aliyeingia. Huyu alikuwa mtu mwingine kabisa. Alikuwa na majumba sita ya wageni, ghorofa tano. Alikuwa na duka la kuuza magari na vifaa vyake. Kadhalika, alinunua shamba la ekari mia tano, ambalo alikusudia kulima maua. Badala ya Abdul sasa aliitwa ‘Bwana Abdul’ au ‘Mzee Abdul’ kila alikopita. Hata alianza kusali, akitoa zaka kubwa na kusaidia watoto yatima. Ndoto za ‘kununua’ ubunge ili asisumbuliwe hovyohovyo zilianza kumtembelea.

Hakuna aliyejua kazi yake ya usiku. Hakuna aliyejua chanzo cha utajiri wake. Hakuna aliyejishighulisha, kwani hizo zilikuwa ndio enzi za wakati huo nchini. Kila mtu alishika lake na kufanya atakalo.

Kwa Abdul Kopakuua ilikuwa moja ya kazi zake rahisi. Kigogo mmoja alimtumia atakavyo. Taarifa muhimu za kufa na nusu malipo kabla ya kazi, nusu baada ya Koba kumaliza kazi, ama kwa mkono wake mwenyewe, ama kwa kuwatumia vijana wake. Kazi moja wapo ilikuwa nyeti zaidi na dau lake pia pana zaidi. Ilihitaji kuwaondoa duniani maafisa wazito serikalini. Watatu waliondoka baada jitihada kubwa za muda mrefu lakini mmoja aliteleza kama kambare na kubadilika kama kinyonga. Kila lilipopangwa hili dhidi yake lilitokea lile na hivyo kuhairisha kifo chake. Mbaya zaidi, mhanga huyo alitoweka nyumbani kwake na kuishi hapa na pale kana kwamba alifahamu kuwa kifo kilikuwa kikimfuatilia. Hata hivyo, kabla hajazitumia fedha alizopewa kwaajili ya kifo cha mhanga yule, Koba alishuhudia kifo hicho katika matangazo ya televisheni. Aliuawa bila shaka kwa risasi ya mdunguaji, hadharani, mbele ya Rais wa nchi, majuzi tu kama watu wengine, Abdul Koba hakupata kumfahamu muuaji wala kufahamu kama kifo kile kilihusiana na hukumu ya kigogo au la. Zaidi hakufahamu iwapo risasi ilimkusudia yeye au Rais. Lilikuwa moja kati ya mambo ambayo asingethubutu kumtaka Kigogo ufafanuzi. Hivyo, alibakia na mshangao wake.

Mkutano wake wa pili hapa na kigogo huyo ulikuwa ule wa jana pale alipoitwa ghafla na kupatiwa picha ya afisa mwingine wa polisi ambaye alitakiwa kufa mara moja. Alipewa picha ya afisa huyo na maelekezo ya wapi aliko muda huo, lipi afanye. Ilikuwa kazi rahisi sana, kumkuta mtu kaketi peke yake ufukweni. Hivyo, pale Abdul alipopokea simu ya ‘kigogo’ mwenyewe akimtaka wakutane katika msitu wa eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kazi maalumu hakusita kuondoka mara moja. Hata hivyo, kinyume cha maelekezo ya kigogo huyo, kuwa awe peke yake alimwagiza mmoja wa wasaidizi wake mahiri kumtaka atangulie na kujificha katika eneo hilo, hatua ambayo ilitekelezwa kikamilifu.

Abdul Kopa alifika hapo dakika tano kabla ya muda. Alishangaa kumwona ‘kigogo’ akiwa tayari ndani ya msitu, chini ya mtu ambao umewahifadhi kwa zaidi ya vikao vitatu vya aina hiyo.

Urafiki wa kigogo huyo na Abdul haukupata kuwa wa kawaida. Kwa ujumla, ulikuwa urafiki wa mashaka. Walikutana kwa nadra sana, kwa siri sana na walizungumza kwa ufupi sana. Mara kwa mara kigogo alikuwa na haraka, huku akifanya kila jitihada kuhakikisha Abdul hamwoni vizuri kwa kiwango cha kumfahamu mara moja. Kigogo huyo hakumtambua vizuri Abdul Koba. Hakujua kuwa Abdul Koba wa leo sio yule wa jana, kwamba hakuwana Imani na mtu yeyote yule duniani, hata mama yake mzazi. Hivyo, bila ya kigogo kujifahamu msaidizi wake mmoja alikuwa amechukua picha yao, wakati wanapeana fedha, katika moja ya vikao vyao.

Kikao hicho kilikuwa kirefu zaidi, kwa viwango vyao. Dakika zipatazo kumi na mbili zilitumika wakati kigogo akitoa orodha ya watu wanne aliotaka kukaa naye kwa dakika moja, kabla ya kutoa bastola yenye kiwambo cha kupoteza sauti, kummiminia risasi tatu na kuondoka zake, mluzi mdomoni.

Haya, leo yuko hapa tena, mbele ya kigogo, akisubiri kupatiwa jukumu jingine! Pamoja na ukweli kuwa alipenda sana pesa, pamoja na ukweli alishapoteza kitu kinachoitwa huruma katika roho na msamiati wake, bado alianza kupatwa na hisia za mashaka kwa kazi hii ya muuaji. Yanahusiana na nini? Yataisha lini? Ni miongoni mwa maswali yaliyosumbua kichwa chake.

Kana kwamba alikuwa akiyasoma mawazo ya kigogo, alimsalimu na kisha kumwambia, “Usijali, jukumu ninalokupa leo ni la mwisho. Mimi na wewe hatutawasiliana tena baada ya leo. Ni mtu mmoja tu na hayuko mbali kutoka hapa.”

Kigogo alifungua begi lake kama anayetoa nyaraka fulani au fedha. Aliuchomoa mkono wake ghafla ukiwa umeshikilia bastola ambayo aliielekeza kifuani mwa Koba.

“Leo ni zamu yako.” Alimwambia.

Abdul Koba alikwishakuwa mtu mnene, mwenye kiri-batumbo. Lakini bado alikuwa mwepesi, hivyo hakuisubiri risasi kama ilivyo kwa watu wengine. Alichupa kukwepa ya kwanza na kumfanya imchubue kidogo ubavuni. Ya pili, ambayo ilimkuta akiwa tayari na bastola yake mkononi, ilimwingia tumboni. Alifyatua yake, ambayo pia ilikuwa na kiwambo cha sauti. Hakuwa amepata fursa ya kulenga shabaha, hivyo risasi zote mbili zilimkosa kigogo kwa mbali sana. Wakati huo, risasi tano zaidi ziliingia tumboni na kifuani mwake na kumfanya adondoke chini kama gunia la mtama. fahamu zilimtoka mara moja.

Kigogo aliitazama kazi yake na kuridhika nayo, akafanya haraka kuliacha eneo hilo kwa kulirejea gari lake aliloliacha mbele ya kituo cha jirani cha mafuta ya gari.

***

Pamoja na kutoka na tabasamu usoni, pamoja na kumtilia alama ya dole yule msichana wa mapokezi ili kumtoa mashaka, bado rohoni mwangu nilijawa na wasiwasi. Mwenendo wa mambo yangu ulikuwa ukifuata mkondo ambao sikuutarajia, mkondo ambao sikuumba mimi. Kifo cha yule kijana wa hoteli ni moja kati ya mambo yaliyofanya nihisi chombo kikienda mrama. Sikutarajia kuua mtu. Zaidi sikutarajia kuua katika chumba changu, hali ambayo kwa vyovyote ingeamsha udadisi na kisha uchunguzi wa kina dhidi yangu. Kwa bahati mbaya sikuwa na njia. Kijana yule alikisaka kifo kwa jitihada zake zote. Kumuua ilikuwa halali, kumwacha hai ilikuwa hatari zaidi.

Hivyo, nilitembea mtaani harakaharaka hadi mahala nilipokodi teksi na kuielekeza nje kidogo ya mji. Huko, baada ya kuingia katika duka moja na kununua shati na suruali ya jeans, nilikodi gari jingine na kuelekea upande wa pili wa mji. Nilipata choo cha kulipia nikaingia na kubadili mavazi yangu, lile shati la yule kijana nililichana chana na kulitupa chooni. Nilipotoka kwa kiasi fulani nilikuwa mtu mpya.

Nilijua kuwa wajibu wangu ulikuwa kuiacha Dar es salaam na Tanzania mara moja. Nilitakiwa kudandia ndege ya kwanza, treni ya kwanza na hata basi la kwanza mradi nitoke nchini humu mara moja. Hata hivyo, haikuwa rahisi kama inavyozungumzika. Upepo ulikuwa haueleweki. Baharia mzoefu hawezi kujitoma baharini bila uhakika wa safari yake. Hivyo, nilifikia uamuzi wa kujibanza tena nchini kwa siku mbili tatu ili niweze kuusoma mwenendo wa mambo kabla ya kuanza mikakati ya kutoka.

Dar es Salaam sio Hong Kong ambayo maelfu ya wagenu humiminika kila siku na kufanya vyumba vya wageni viwe adimu. Wala sio Bangdadambako mgeni huchunguzwa kwa makini sana kabla ya kupatiwa chumba kwa hofu ya kumkaribisha gaidi ambaye ataishia kujilipuakatika kadamnasi. Hivyo, haikuwa kazi ngumu kupata chumba kizuri katika hoteli moja iliyoitwa Bondeni Inn Resort, kilometa tatu toka katikati ya jiji. Sasa nikiwa mvulana mtanashati, mara tu nilipopatiwa kadi ya chumba nilijifungia chumbani humo na kufanya haraka kurekebisha kasoro ndogondogo ambazo zingeweza kunifanya niunganishwe na yule msichana aliyeuawa muda mfupi uliopita. Kazi ambayo sikuwa nimeridhika nayo baada ya kuifanya kwa pupa mara baada ya kuipeleka akhera roho ya yule mjinga.

Baada ya hapo nilijilaza chali juu ya kitanda, ubongo wa mambo na namna ya kujinasua. Jitihada kubwa ambayo niliuagiza ubongo wangu kufutilia mbali ilikuwa ile shahuku yangu ya kutaka kumfahamu mwajiri wangu aliyenipa kazi hiyo rahisi sana kwa dau nono sana, ni nani? Alinufaika vipi? Alinifahamu vipi? Na anafanya lipi kwa sasa? Nilijitahidi kulifukuza hilo kwa kujua kuwa shahuku hiyo ndiyo ilinifikisha katika mazingira haya kama ningekuwa nimeifanya kazi yangu na kutoweka mara moja, nyuma ya kisogo change. Pamoja na hayo, haikuwa kazi rahisi. Kila nilipopanga mikakati ya kutoka, shahuku ya kujua kila kinachoendelea ilinijia pale katikati ya fuvu la kichwa change, na hivyo kunipa mateso makubwa kisaikolojia.

Mkakati wangu wa kwanza ulikuwa wa kumwokoa mwanangu, kipenzi changu. Licha ya ukweli kuwa naye sambamba ilikuwa hatari, bado pia sikutaka apatwe na ajali yoyote mbaya, ingesababisha tutengane naye. Kwangu yeye alikuwa mwandani, mkono wangu wa pili, mguu wangu wa pili. Hivyo, kazi ya kwanza ilikuwa kumfumua; kichwa pale, mkono pale, mguu kule na kisha kumsafirisha atangulie nyumbani.

Kazi hiyo niliianza mara moja, nilifungua begi langu na kumtoa. Alikuwa tayari katika sehemu mbili. Nikambusu na kuanza kumtatua tena. Dakika chache baadaye alikuwa katika vifurushi vitano, vilivyoandikwa ‘sample’ ndani ya mifuko maalumu ya nailoni ambayo baadaye ilifungwa pamoja ndani ya kijiboksi kilichoelekezwa kwa kampuni fulani kwa anuani fulani ambayo ni mimi pekee niliyeifahamu. Muda mfupi baadaye mwanagu alikuwa tayari kwa safari. Hapa kama ingetokea muujiza, akamatwe njiani ni watu wachache sana duniani ambao wangeweza kutambua kuwa ‘mwanangu’ huyu aliitwa AK 47.

Nisingeweza kusahau mapenzi kwa mwanangu yaliyoanza. Ilikuwa baada ya yale mazoezi marefu ya shabaha na jaribio la kusafirisha yule mwarabu. Ilifuatia kazi nyingine ambayo niliambiwa kuwa ilikuwa nyeti sana.

Nilipewa ramani ya makazi ya mhanga huyo, ratiba yake ya kutoka na kuingia kwake. Hali kadhalika nilipewa picha zake mbalimbali. Alikuwa mtu maarufu sana duniani. Pia alikuwa machachari aliyehusishwa na mambo mengi ikiwemo undumila kuwili kati ya kikundi cha kigaidi cha Wayahudi MOSSAD na magaidi wa AL KAIDA. Iliaminika kuwa yeye alikuwa mtu pekee aliyekuwa na hakika ya kukutana na Osama Bin Laden na kuzungumza naye. Kwamba pia ndiye aliyekuwa akishikilia koba lake la pesa.

Kazi ya kumwinda mtu huyu haikuwa ngumu. Yeye mwenyewe alipenda sana kuwinda wanyama. Hivyo, jioni moja alipookotwa katika mbuga ya wanyama nchini Malawi, risasi ya mwanangu AK 47 ikiwa imejikita katika paji la uso wake kila mmoja aliamini kuwa alikuwa amevuna kile alichokipanda.

Nilisoma habari zote kwa siku kadhaa katika magazeti na kuzitazama katika televisheni. Kama ilivyo ada habari hizo zilididimia na kutoweka ghafla pale zilipokua nyingine, nyeti zaidi za Marekani kuivamia Iraq na baadaye kumkata kichwa mtawala wake, Saddam Hussein.

Kazi ya kuwinda binadamu kwa minajili ya kumtoa roho ni ngumu kuliko unavyoweza kufikiria. Kwanza, wewe mwenyewe unajificha usifahamike, kisha, yeye, kama tarehe yake haijajiri atakuhangaisha hata kwa miezi mkicheza mchezo wa paka na panya. Hivyo, wakati nikifikiria dau langu nono nililolipwa nilijua kuwa ninakula fedha ambazo nilizitumikia, kwani mara mbili tatu nilinusurika kutafunwa na simba, mara moja niliponea chupu chupu kugongwa utosini na nyoka aina ya kobra aliyekuwa tayari amejaza koo lake kwa sumu.

Miezi mitatu baadaye nilipewa jukumu jingine. Hili pia lilimhitaji mwanangu, kumfuta duniani ‘mbwa mweusi’ mwanasiasa mwenye asili ya Kiafrika ambaye alikuwa akija juu katika siasa za Marekani. Nilitakiwa kumfanyia vitu vyangu hadharani ili iwe fundisho kwa watu wengine waliodhani wana haki nchini humo sawa na weupe ingawa wao pia ni wahamiaji toka ulaya.

Haikuwa kazi ngumu. Akiwa mtu wa mikutano na mihadhara kila mara nilimvizia katika moja ya mikutano yake na uielekeza risasi yangu mdomoni wakati ameufungua akisisitiza jambo. Alifia hospitalini ambako inadaiwa kauli yake ya mwisho ilikuwa ‘Aluta Continue.’

Mwaka mmoja baadaye nilihisi natumiwa kwa ujira usiolingana na zigo zito la dhambi nilizokuwa nikichuma. Ndipo nikabuni na kuandaa kifo changu mwenyewe. Lilikuwa pigo kwa waajiri wangu lakini kwangu binafsi ilikuwa faraja.
 
nakipataje hiki kitabu, na ni tsh ngapi
 
dah kama nakuona vile ukijiandaa kutupa continuation flan matata, endeleaaa....!
 
best leo umejitahidi,hauna lawama kabisa
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…