5
Afande Chaku alipotoka katika eneo la maafa alirejea moja kwa moja ofisini kwake. Simu za mara kwa mara toka hapa na pale zilimpa tabu katika kuhimiza usukani wa gari. Hata hivyo, alifika salama. Robo tatu ya wasaidizi wake walikuwa tayari wamerejea wakimsubiri kwaajili ya kutoa taarifa na kusubiri maelezo zaidi.
Muda mfupi baadaye, kikao kilifunguliwa. Kilianza kwa kupokea taarifa toka kwa wasaidizi hao.
Aliyekuwa akifuatilia mwenendo wa pesa alitoa taarifa ambazo zilimshangaza kila mmoja; wingi na idadi ya pesa ambazo zilikuwa zikipaa au kutua ndani ya nchi kila baada ya dakika chache. “Nani anasema Tanzania ni masikini? Ni masikini kwetu tuliokaa hapa na wakulima wa vijijini. Kwa wenzetu mabilioni ya fedha yanatembea huko na kule kama kumbikumbi. Kwa kweli, ni vigumu sana kupata jibu la haraka juu ya fedha ambazo zinastahili kutiliwa shaka,” alisema na kuongeza, “Hata hivyo ninayo orodha ya watu kama ishirini hivi ambayo bado naifanyia kazi. Naendelea kuipunguza kila baada ya uchunguzi wa kina.”
Afisa huyo alipiga hatua kubwa zaidi ambayo ilimsisimua Afande Chaku. Alichunguza pia akaunti za marehemu na kuona kama zingeweza kuwa na kitu cha kutilia wasiwasi. “Anazo shilingi milioni tatu tu, zilizotokana na mshahara wake. Hiyo ni akaunti yake ya CRDB. Akaunti yake nyingine CBA, ina elfu arobaini na haijatumika kwa miaka miwili.’
“Mshahara wake shilingi ngapi?” Afande Chaku aliuliza. “Laki tatu na themanini. Analipwa na Ikulu kupitia hazina.”
Chaku alinukuu mambo kadhaa katika daftari lake dogo. Kisha alimgeukia yule aliyetumwa kupata orodha ya watu waliokuwepo hotelini hapo. Chaku hakuitazama orodha hiyo iliyoandikwa vizuri kwa mwandiko wa mkono.
“Muuaji hakuwa ndani ya hoteli, alikuwa nje. Hilo halina mjadala. Lakini kuna mtu aliyeondoka na briefcase ya marehemu. Hatuna hakika kama alikuwa na uhusiano na tukio hili ama la. Lakini tunamtaka. Na tunaitaka briefcase irudi ndani ya masaa ishirini na nne. Ondoka, rudi hotelini pale. Tazama tena na tena chochote kilichopatikana katika zile kamera zao za ulinzi. Fanya mahojiano na kila mtu anayeweza kukusaidia. Zaidi tumia uwezo wako wa ziada, ikibidi muamshe bibi yako au babu yako aliyekufa akuwezeshe kurudi hapa ama na briefcase hiyo, ama kichwa cha aliyeichukua.”
Wawili watatu walicheka. Havikuwa vicheko vya anasa, kwani haukuwa mzaha.
Taarifa ziliendelea kumiminika. Uwanja wa ndege uchambuzi uliendelea, na kadhalika na kadhalika.
Mtu mmoja akamletea Afande Chaku chai na keki mbili. Ndio kwanza Afande Chaku akakumbuka kuwa alikuwa hajatia chochote kinywani kwa takribani masaa kumi na mbili, akaitazama saa yake. Ilikuwa saa nne na robo usiku. Aliinywa chai hiyo na kuteketeza keki kilafi. Akaagiza maji ambayo alikunywa glasi mbili haraka haraka na ya tatu taratibu.
Afande Chaku akakumbuka jambo jingine. Siku hiyo alikuwa hajanywa! Akatabasamu. Akaamua kurudi nyumbani kwake na kupata usingizi ili kesho yake aendelee na shughuli hizo.
Simu ya Inspekta Matata ambayo hakuitegemea iliingia ghafla. “Unaendeleaje?” Mzee huyo aliuliza bila salamu za kawaida.
“Tunaendelea. Bado tupo katika hatua za awali. Sijaona jambo la maana la kuripoti,” Afande Chaku alijibu kisha alikumbuka kuongeza neno, ‘Afande.’
“Nataka kujua kila hatua uliyopiga. Nataka kujua hata kila mnachofikiria. Unajua huku kuna sokomoko?”
“Najua, afande.”
“Basi utakuwa unajua pia kuwa umekalia kuti kavu,” simu ikakatwa.
Chaku alitafakari kwa muda kabla ya kuvuta kompyuta yake na kuanza kuandaa taarifa ambayo hakuwa tayari kuiandika. Ilikuwa kazi ngumu kuliko hata ile ya kumtafuta muuaji.
***
Frank Mwaipula hakupata usingizi. Toka alipofika nyumbani kwake jana, akiwa na briefcase ya watu mkononi, alihisi akilizake zikiwa hazifanyi kazi vizuri. Hakujua kwanini aliondoka na begi hilo. Hakujua kwanini haondoki kwenda kulirudisha. Zaidi ya yote hakujua kwanini alilifungua!
Mwaipula alikuwa akiishi peke yake, katika nyumba yake binafsi ambayo alianza kuijenga miaka minne iliyopita.
Pato lake lilitokana na ‘Kuzima’ habari moja nzito ya tajiri aliyekuwa akiingiza chakula kichafu isivifikie vyombo vya habari lilimwezesha kununua kiwanja kidogo, Sharif Shamba. Alikusudia kujenga nyumba ya vyumba sita, lakini kwaajili ya ulevi wa kupindukia aliishia vyumba viwili. Kwa jitihada za mke wake, waliweza kupata umeme na bomba la maji. Halafu, pesa zikakatika na ulevi ukaongezeka maradufu. Halikuwa jambo la ajabu kwa Mwaipula kutofika nyumbani kwa siku mbili na alipofika alikuwa taabani kwa ulevi, mfukoni akiwa hana hata senti moja. Hali hiyo ilisababisha kutoweka kwa amani nyumbani humo hata yakamshinda mkewe. Usiku mmoja Mwaipula hakumkuta mkewe wala mtoto wao wa miaka mitatu. Hakumtafuta. Kwa namna moja aliona kama faraja kutokuwa na mtu wa kumsumbua kwa maswali na mahubiri.
Hivyo, Mwaipula alikuwa na faragha ya kutosha kuhangaika na briefcase hiyo hadi alipofanikiwa kuifungua. Lilikuwa begi la kisasa, lililofunguliwa kwa namba. Alicheza na namba zile kwa muda mrefu kabla ya kuipata ile iliyokusudiwa.
Kama alitarajia fedha katika begi hilo, hazikuwemo. Lakini kilichokuwemo kilimsisimua zaidi ya fedha. Zilikuwemo hotuba za Rais zenye sahihi yakechini. Aidha zilikuwemo nyaraka mbalimbali za Ikulu zilizoandikwa ‘Top Secret’ ambazo bila shaka zilikusudiwa kwaajili ya macho ya Rais pekee na wateule wake wachache. Kama mwandishi, ilimsisimua sana kujiona akiwa sambamba na Ikulu kwa mambo ambayo si kila mtu angepata kuyajua.
Hata hivyo, kengele za hatari zilikuwa zikisikika masikioni mwake. Hisia zilimwambia kuwa kwa kuifungua briefcase ile alikuwa akijiweka matatani bila sababu za msingi. Gereza linakuita Mwaipula… funga begi la watu lipeleke polisi mara moja… Alihisi nafsi ikimwambia.
Nafsi ya pili, ilikuwa na mamlaka zaidi, ilimshurutisha kuendelea na udadisi. Alitoa barua zile chini na kuanza kulipekua begi hilo kwa umakini Zaidi. Lilikuwa na mifuko mbalimbali ya pembeni. Mwaipula aliikagua yote, mmoja baada ya mwingine. Alipata nyaraka zaidi, daftari la kumbukumbu za kila siku na namba kadhaa za simu. Wakati akianza kufunga mfuko huo iliaendelee kusoma nyaraka ndipo alipobaini kuwepo kwa mfuko mwingine, wa siri zaidi, nyuma ya kabrasha lililofunika funiko juu ya begi hilo. Alipapasa, akahisi kitu. Akapeleka vidole vyake na kupekenyua kitu hicho.
Ilikuwa flash! Yenye ukubwa wa kidole chake cha shahada.
Flash, katika dunia ya leo ya maendeleo makubwa katika sayansi na teknolojia hakikuwa kitu kigeni. Watumiaji wote wa kompyuta walijua kuwa flash ni teknolojia ya kisasa zaidi ya kuhifadhi nyaraka na kumbukumbu, badala ya kuitegemea kompyuta yenyewe, disketi au CD ambavyo ni vikubwa na uwezo mdogo wa kuhifadhi mambo. Flash na udogo wake ina uwezo wa kubeba majalada ya vitabu vingi vyenye ukurasa miatatu au nne, hata elfu moja, kila kimoja.
Lakini si hilo lililomsisimua Mwaipula. Kilichomsisimua zaidi ni jinsi flash hiyo ilivyofichwa vilivyo, katika hali ambayo haikukusudiwa ionekane kwa urahisi. Maandishi juu ya flash hiyo pia yalimvutia.
‘Top Secret: Mikataba ya Kishetani,’ yalisomeka. Aliishika flash hiyo kwa mkono unaotetemeka na kuikodolea macho kama anayejaribu kutabiri kilichomo ndani yake.
Ni hilo lililomnyima usingizi na kumwacha akigalagala kitandani usiku kucha. Alfajiri, wakati jogoo wa majirani wakianza kuwika, mlango wake uligongwa. Mwaipula alishituka sana. Hisia za hatari, alizokuwa nazo usiku mzima zilimrejea kwa nguvu zaidi. Hakupata kugongewa alfajiri kama hiyo kwa miaka.
Mlango uligongwa tena, kwa nguvu kuliko awali. Mwaipula alichupa toka kitandani na kusukumia briefcase ile uvunguni. Aliduwaa na flash mkononi akitafakari wapi aifiche.
Mara mlango ulipigwa teke, kwa nguvu zaidi, ukafunguka. Watu wawili waliofunika nyuso zao kwa matambara meusi waliingia, kila mmoja akiwa na bastola mkononi.
“Wewe ndiye Frank Mwaipula…, Mwandishi?”
“Ndi… ndiyo. Kuna nini?”
“Mjinga huyo,” mwenzie alimjibu. Akamgeukia Mwaipula, aliuliza, “kwanini leo hukukesha kwenye mabaa na vilabu vya usiku kama kawaida yako? Unajua umekwisha tuharibia siku yetu? Haya toa!”
“Nini?”
Kofi kali lililotua usoni mwake lilimfanya Mwaipula apepesuke na kuanguka chini. Teke lililofuata hapo, lilimwingia barabara tumboni.
“Toa,” aliamriwa
“Nitoe…nini?”
“Hujui sio? Haya subiri tukuonyeshe” alijibiwa.
***
Nilishusha pumzi ya ghafla mara baada ya kurudi hotelini na kujifungia. Nikajitupa kitandani kujipumzisha na kutuliza akili yangu. Haikutulia. Kengele za kuashiria hatari zilikuwa zikigonga katikati ya ubongo wangu kila nilipojiuliza nini ninachokifanya, kama kazi yangu nilishaifanya, tena kwa ufanisi mkubwa kabisa. Kama malipo niliyapokea, tena makubwa kuliko nilivyotegemea. Ya nini basi kujitia katika hatari ati kwaajili ya shahuku tu ya kumfahamu mwajiri wangu? Ya nini kusumbua kichwa changu kujua ilikuwaje nikapewa maelezo yasiyo na shaka juu ya mhanga wangu?
“Nahitaji kuondoka mara moja.” Nilijikumbusha. Haikuwa kuondoka pekee. Nilihitaji kuhama hoteli hiyo pamoja na kuhama katika sura ya umbile la kike. Watu walioniona pale msibani si wachache. Bila shaka, tayari watakuwa wakiulizana maswali mengi yasiyo na majibu juu ya mwandishi huyu wa kike aliyejitanda baibui gubigubi.
Nahitaji kubadilika pia. Inapendeza kuwa kijana wa kiume mwenye mvuto zaidi ya msichana mrembo. Kazi ya kujibadili haikuwa rahisi, inahitaji muda, umakini na usiri wa hali ya juu. Sikuwa na budi kuifanya. Sudi ya maisha yangu ilikwisha nitupa katika mkondo huo.
Nililala pale siku nzima, mchana na usiku wake, kando ya maiti zote zile, bunduki ikiwa bado mkononi mwangu. Ilikuwa kama ndoto, asubuhi ya siku ya pili mlango ulipofunguliwa ghafla na wazungu waliovalia kijeshi kuingia ndani. Walishangazwa na wingi wa miili iliyolaliana huku ikiwa imegandiana damu. Walishangazwa Zaidi kuniona mtoto mdogo nikiwa hai, bunduki ikiwa imemwelekea maiti mwingine aliyefunika tambara usoni.
“Ni wewe uliyemuua huyu?”
Nilitikisa kichwa kukubali. Wakatazamana kwa mshangao. Mmoja wao alinitazama kwa makini zaidi, jicho kwa jicho kwa dakika nzima kabla hajatikisa kichwa chake kwa namna ya kujiridhisha kwa jambo fulani kichwani mwake.
Pilikapilika zikaanza. Watu wengine waliovaa majoho meupe, yenye nembo za ‘Red Cross’ waliingia na kuanza kubeba maiti za wazazi na ndugu zangu, moja baada ya nyingine. Hadi leo, sijui zilipelekwa wapi, pengine katika makaburi ya halaiki kwaajili ya wingi wa vifo vilivyokuwa vikitokea katika kipindi kifupi.
Mimi nilipelekwa hospitali. Kutembea kwa miguu yangu ilikuwa kazi ngumu.Yule mshenzi alikuwa ameniumiza. Nilipata matibabu kwa siku kadhaa kabla ya kutolewa hospitalini hapo. Nilitegemea kupelekwa katika kambi zilizofunguliwa kwaajili ya mamia ya yatima walioibuka ghafla kufuatia mauaji haya ya kimbari. Lakini nilishangaa nilipotengwa na wenzangu kwa maelezo ya yule askari aliyenitazama sana kwamba “huyu si wa kawaida.”
Ulikuwa mwanzo wa safari yangu mpya ya kimaisha, safari ambayo ilianza kwa kuhamishiwa katika eneo ambalo sikulijua, ambamo nilipatiwa chakula pamoja na malazi mazuri sana kwa takribani mwezi mmoja. Wakati wote huo nilikuwa nikiiitwa ofisini ambako niliulizwa maswali mengi kwa muda mrefu. Baadhi ya maswali yalikuwa ya kipuuzi, baadhi yakirudiwa mara kwa mara, niliyajibu yote bila kujali hili tayari limeulizwa au la. Baadaye nilibaini kuwa maswali hayo yalilenga kupima ujasiri, upeo wangu wa fikra na ustahimilivu.
Kisha nilihamishwa. Nilipelekwa katika nchi nyingine ambayo pia sikuhifahamu na kuanza kupewa mafunzo ya nguvu. Nilifundishwa kutumia silaha mbalimbali, kutega na kutegua mabomu, kubuni silaha n.k. Kwa mfano, nilionyeshwa jinsi chupa ndogo ya mafuta ya taa au kibiriti inavyoweza kuwa bomu kubwa ambalo lingeweza kubomoa jumba la ghorofa kumi.
Zaidi nilifundishwa shabaha.
Kila silaha ina namna yake ya kupata shabaha. Kisu cha mkononi kina namna yake ya kukishika na jinsi ya kukirusha. Bastola ina njia zake na bunduki kubwa pia. Yote hayo niliyapokea kwa furaha, nikifurahia kila somo. Zoezi la kutumia mikono na miguu hata kuua mtu kwa vidole tu nililifurahia zaidi. Nilijiona kama mfalme au Mungu mtu kila nilipojumuika na watu wengine ambao ningeweza kuwaua kana kwamba namuua mende.
Pia nilijifunza lugha mbalimbali; Kiswahili, Kiingereza, Kiarabu, Kifaransa, Kichina, Kijerumani na lugha zingine nyingi. Lugha zote hizi nilizisoma kwa bidii.nikijitahidi kufanya vizuri katika kila lugha tulizofundishwa.