Hadithi: Mikataba ya kishetani

nameless girl

JF-Expert Member
Apr 22, 2012
4,195
2,677
1

ALIKUWA mwanamke! Tena mwanamke wa haja! Alisimama pale, uso wake ukiwa umeelekezwa kwangu; kama anayesubiri nifanye kazi yangu! Naapa kuwa, kwa mara ya kwanza, katika maisha yangu ya udunguaji, nilisita kubonyeza tufe la mwanangu, AK 47 ambaye nilimpenda kuliko wanangu wengine wote niliopata kuwatumia.

Alikuwa pale, kasimama, huku uso wake ukielekea kwangu mara kwa mara.

‘Ananisubiri!’ Niliwaza.

Sikujua kwa nini nilisita. Maelekezo yote niliyopewa yalikuwa barabara; atakua amevaa suruali ya kitambaa, yenye rangi nyeusi na koti lake la rangi ile ile juu ya shati yenye rangi ya bendera ya taifa. Atatoka nje ya mlango wa hoteli saa nne na robo, akiwa katikati ya Rais wa Nchi kulia kwake na mgeni wake, bilionea wa viwanda na machimbo ya madini upande wa pili. Pale mlangoni watasita kidogo kuagana kabla ya kuelekea kwenye hafla maalumu. Mwondoe akiwa pale pale mlangoni.

Maelekezo yalikuwa sahihi. Muda ulikua uleule uliopangwa. Na zaidi ya yote mavazi, yalikuwa yaleyale yaliolekezwa. Wala si hayo tu, mamilioni ya dau langu lililolipwa katika fedha za kigeni tayari yalikuwa yamekwisha ingia kwenye akaunti yangu ya benki wiki moja iliyopita na kuhamishiwa katika benki mbalimbali, kwa majina tofauti, kabla ya sehemu ya pesa hizo kuja Dar es Salaam kwa matumizi yangu madogo madogo.

Purukushani za wapigapicha wa televisheni na magazeti zilikuwa nyingi. Kila mmoja alikuwa akihangaikia kupata picha bora zaidi, ama ya Rais ama ya mgeni, au wote kwa pamoja. Vichwa vyao na kamera zao zilipita mbele yao kwa namna iliyonifanya nipoteze shabaha. Lakini hilo lisingenizuia. Walengwa wangu walikuwa juu ya wapiga picha kwa ngazi moja. Isitoshe, mimi ni mtaalamu. Sekunde moja tu ya kutikisa kichwa ilitosha kabisa kumdungua muhanga wangu bila tatizo.

Hata hivyo, nilisita kumtekenya mwanangu.

Kitu gani basi kilifanya nisite kumbonyeza kidogo tu mwanangu ili nimalize kazi hiyo na kuendelea na ziara yangu ya kutembelea ziwa Tanganyika ambako nilikusudia kuwinda viboko kijiji cha Buhingu na kisha kuwashuhudia sokwe wa milima ya Kasoge? Kitu gani kiliutia uzito moyo wangu wa kishetani, ambao daima ulifurahia kuiona risasi yangu ikimpaisha mtu angani na kisha kumdondosha chini huku akiwa tayari ametokwa na uhai wake? Kitu gani? Kitu gani? Kitu ga…

Mara nikakumbuka. Zilikuwepo sababu nyingi, kubwa zikiwa mbili. Ya kwanza, ilikuwa urahisi wa kazi hii. Katika maisha yangu haya, sijapata kazi rahisi kama hii, upewe hela nyingi Zaidi ya ambazo ungeomba, upewe wajihi wa mtu unayetakiwa kumwondoa, siku, saa na vazi atakalokuwa amevaa! Ilikuwa nyepesi mno. Natumaini ni wepesi huo ulionitia mchecheto kiasi cha kunifanya nisite kufanya vitu vyangu.

Sababu ya pili, mhanga wangu alikuwa mwanamke, tena mzuri! Sijapata kumuua msichana mzuri kama huyu wala kuombwa kumuondoa duniani mwanamke. Hili pia lilinikoroga kichwa.

Kulikoni? Nilijiuliza. Kisha nikajikumbusha taratibu za kazi zetu. Ukishapokea malipo yako, ukishaweka utaratibu madhubuti wa kumuondoa mhanga wako, kamwe usianze kujiuliza maswali. Hiyo ni kazi ya polisi na wapelelezi na anayewajibika kujibu ni mteja wako, sio wewe.

Wazo hilo lilinifanya nimnyanyue tena mwanangu mpenzi, kumwelekeza kule alikokusudiwa. Nikarekebisha lensi na kuzivuta nyuso zao kwangu. Ilikuwa imepita nusu dakika tu toka niliposita kuibonyeza. Walikuwa wangali palepale mlangoni. Raisi alikuwa amegeuka kusalimiana na mtu fulani. Ningeweza kumwondoa, kupitia kisogo chake kwa urahisi kabisa. Kwa bahati, sikutumwa kufanya hilo. Yule bepari wa viwanda na madini naye alikuwa pale, kaduwaaduwaa. Ningeweza kumwondoa kwa bei rahisi vile vile kupitia upande mmoja wa sikio.

Mhanga wangu alikuwa kama anayeendelea kunisubiri. Uso wake mzuri ukiwa umeelekezwa kwangu na macho yake yalikuwa na dalili za wasiwasi na vitone vya jasho jembamba katika paji lake la uso, paji ambalo nilililenga vizuri kana kwamba nipo katika mazoezi ya shabaha. Nikamtekenya mwanangu. Sekunde moja, mbili, tatu… Mara mhanga wangu alipaa kama futi moja angani na kisha kutua kama gunia miguuni mwa Rais, akiwa tayari mzoga. ‘Mkono wa Jibril haujapata kukosea’ niliwaza nikicheka kimoyomoyo.

Purukushani iliyofuatia hapo haikuwa na kifani. Nilitamani sana kuitazama walao kwa dakika mbili pindi wanausalama wakicharuka kama waliopigwa ufunguo. Wanne, waliokuwa nyuma ya msafara huo; walichupa angani, mmoja akimpitia Rais kwa kumbo ambalo lilimwangusha na kumlalia kama ngao huku wenzake wakiwavuta na kurejea ndani. Wakati huohuo ving’ora vililia, polisi wakiivamia barabara na kufunga mitaa. Raia wa kawaida, waandishi na wafanyakazi wengine walikuwa taabani zaidi, huyu akianguka pale, yule akikimbilia kule kana kwamba wamepagawa. Sikuweza kujizuia kucheka.

Nilimwona mwanausalama mmoja akitazama huko na huko, kisha macho yake yakaelekea upande wa pili wa mtaa, katika jengo nililokuwepo mimi na kutoa maelekezo kwa wenzake ambao walianza kujipanga kulizingira jengo hilo.

Ulikuwa wakati wangu wa kuondoka. Nilimbusu mwanangu ambaye bado alikuwa na joto la risasi ile moja aliyotema. Nikamfungua na kumkunja taratibu na kisha kumweka katika briefcase yake vizuri. Juu yake nilirudishia vitu mbalimbali vya kudanganyia, ambavyo vingemlaghai mtu yeyote ambaye angepata wazimu wa kuikagua.

Haikuwa kazi kubwa kuliacha jengo hilo. Watu wote walikuwa wameduwaa, wakishangazwa na purukushani ambazo zilikuwa zikiendelea upande wa pili wa mtaa. Nikaipuuza lifti na kufuata ngazi ambazo zilinitoa ghorofa ya tano na kunipeleka ya nne, ya tatu, ya pili. Hapo nilipanda lifti hadi chini. Wakati nikitoka nje ya lifti hiyo watu wawili, waliovaa suti waliingia harakaharaka, mikono yao ikiwa mifukoni.

Hatukutazamana usoni, lakini sikuhitaji kuambiwa kua hao walikuwa wana usalama wakifuatilia uelekeo wa ilikotokea risasi. Nilitamani kuwapa pole. Nilitamani kuangua kicheko. Lakini yote hayo sikuyafanya. Niliondoka zangu bila kuangalia nyuma nikihisi macho yao yakilitazama umbo langu la nyuma hadi mlango wa lifti ulipojifunga.

Sikuwa na wasiwasi. Nilijua wasingenishuku kwa lolote. Nani anaweza kumshuku msichana mrembo, aliyevaa nguo fupi na viatu vya mchuchumio huku nywele zake ndefu kaziachia kama msichana wa Kihebeshi? Nani angepata muda wa kushuku wakati harufu ya marashi aliyopaka yalitawala katika chumba cha lifti alichokiacha punde?


***

Alikuwa mwanamke mzuri, zaidi ya uzuri wa haja. Picha zake katika televisheni na kurasa za kwanza za magazeti yote ya siku hiyo zilithibitisha hilo. Angeweza kushiriki urembo wa dunia na akashinda; angeweza kucheza filamu yoyote ile na akawa kivutio. Picha zilifichua uso wake mzuri uliojaa ucheshi, huku macho yake yakionyesha ung’aavu na hekima. Kiwiliwili chake chenye urefu wa kadiri, kilichojaa uhai na matumaini yote katika maisha. Hata sauti yake, pale televisheni moja iliporusha maneno yake mawili matatu enzi za uhai wake, ilithibitisha jambo moja; hakuwa mtu wa kufa.

Lakini tayari alikuwa marehemu! Mipango ya mazishi yake bila shaka ilikuwa ikiandaliwa!

Kwa jina aliitwa Cleopatra. Mumewe aliitwa Twalib. Kwasababu alizozifahamu mwenyewe, Cleopatra hakupata kulitumia jina la mumewe katika shughuli zake za kiofisi zaidi ya lile la baba yake Abeid ingawa Twalib lilikuwa jina zito katika jamii.

Magazeti yalisema na kudodosa hili na lile juu ya kifo chake. Hata hivyo, lililokuwa wazi katika kauli na maandishi yote ni utata juu ya kifo chake. Wingu zito lilitanda juu ya kifo hicho kutokana na swali zito lililokuwa likisumbua vichwa; muuaji alimkusudia yeye kweli au alikuwa amemlenga Rais?

Gazeti moja lilikwenda mbele zaidi, katika habari yao ambayo iliandikwa pia kama maoni, ilibebwa na kichwa cha habari; KWA VYOVYOTE VILE HAKUWA MTU WA KUFA.

Nani atafikiria kumuua Cleopatra? Liliandika.Hakuna hata sababu moja iliyowazi ya kupelekea mtu yeyote, awe na akili timamu au mwendawazimu kuchukua uamuzi wa kumuua kinyama tausi huyu ambaye hakupata kuwa na madhara kwa jamii wala mwanajamii yeyote.

Cleopatra alikuwa msomi, mwenye shahada ya Udaktari aliyoipata akiwa na umri usiozidi miaka thelathini na mitano. Alipata kuwa na kipindi muhimu sana cha ushauri wa kijamii katika televisheni mbili tatu nchini. Alikuwa mtumishi mwaminifu na mchapakazi hodari katika Ikulu ya Dar es Salaam. Hata kifo kimemkuta wakati akilitumikia taifa, tena mbele ya Rais aliyekuwa katika hafla nzito ya kumshawishi tajiri mkubwa wa viwanda duniani kuwekeza nchini.

Tunasema hakuwa mtu wa kufa! Bado tunaamini kuwa risasi iliyomuua haikumkusudia yeye. Ni kwa mtazamo huo ndipo tunaposisitiza haja kubwa ya uchunguzi makini wa haraka, kujua kitu gani hasa kilitokea hata mshumaa huu uliokuwa nuru kwa wanawake wote duniani na mfano kwa kila mwanaume, kuzimika ghafla…

Gazeti jingine lilizifuatilia habari hizo kwa mtindo wake. Liliwasiliana na ofisi ya Rais kutaka kujua Rais anajisikiaje kuponea tundu la sindano katika tukio hilo na iwapo anadhani risasi ilimkusudia yeye au marehemu.

No comment!

Pengine comment pekee ambayo uchunguzi wa gazeti hilo ulifanikiwa kupata ni pale walipofanikiwa kuzungumza na mume wa marehemu. Aliwashangaza, kama alivyowashangaza pia wasomaji, kwa taarifa yake kuwa yeye na Cleopatra walikuwa wametengana kwa zaidi ya miezi sita iliyopita! Kisa?

No comment.

Picha ya Twalib Khalfan ilitoka sambamba na ya marehemu mkewe katika habari hizi. Kila mmoja alikuwa akiitazama kamera huku anacheka. Mapenzi yalikuwa wazi kabisa katika macho ya tausi hawa wawili. Gazeti hilo halikuishia hapo. Lilivuka mipaka kwa kupendekeza kuwa kwa uzoefu wao, katika maswala yenye utata kama hayo yupo Mtanzania mmoja tu ambaye angeweza kuaminika katika kuyapatia ufumbuzi. Walimtaja mtu huyo kama Joram Kiango. Madai hayo yalifuatiwa na maelezo mafupi ya mikasa mingi ya kitaifa na kimataifa aliyopata kuitatua ama kwa ubongo wake ama kwa risasi ya bastola yake.

Waliyapamba maelezo hayo kwa picha ya Joram Kiango, akiwa ameketi katika bustani moja nchini, macho yake yakiwa yameinamia gazeti. Kando yake alikuwepo mwandani wake, msichana mwenye umbile nadra kwa uzuri wa ziada ambaye maelezo chini ya picha yake yalimtaja kwa ufupi ‘Bi Nuru’

Gazeti hilo lililalamika kuwa jitihada zao zote za kumpata Joram Kiango ili walao atoe maoni yake juu ya tukio hilo la aina yake, ziligonga mwaba. Kwamba walifika nyumbani kwake Ilala na kubaini kuwa hajaonekana kwa miezi. Walipita katika hoteli zote maarufu ndani na nje ya jiji na kupata jibu lilelile; hajaonekana kwa miezi.

Yuko wapi Joram Kiango?

Ilimalizia kauli ya mwandishi wa habari hiyo katika hali ya kukata tamaa.


***

Joram Kiango alizipokea habari hizo kwa njia ya mtandao wa intaneti akiwa angani. Alikuwa ndani ya ndege ya Emirates, aliyoipanda Amsterdam baada ya kushuka toka katika City Hopper ya KLM iliyomtoa Frankfurt. Alikuwa njiani toka nchini Ujerumani, katika mji wa Maizn, ambako alikuwa masomoni akipigania shahada yake ya udaktari wa falsafa. Mhadhiri wake Profesa Oed Matzke alikuwa nae sambamba kwa miezi miwili akinakili awamu ya mwisho ya kazi yake ili aweze kuvishwa hadhi ya Udaktari.

Akiwa amechoka kusoma kitabu cha Bill Clinton, The Art of Giving, aliamua kufungua kompyuta. Ndege hii ya kisasa ilikuwa na kompyuta kwa kila abiria, ambayo unaweza kuitumia kwa kutazama filamu, intaneti, kupiga simu pamoja na kuona wapi uliko katika anga hilo.

Kama kawaida yahoo ilikuwa na habari kadhaa za kimataifa; mtafaruku wa uchaguzi nchini Kenya, mauaji ya Bi Bhitto nchini Pakistan, purukushani za Hillary Clinton na Obama katika mbio za kuwania kuteuliwa kugombea Urais nchini Marekani kwa tiketi ya Democratic na kadhalika.

Habari iliyomshtua ni ile ya nyumbani, ‘RAIS ANUSURIKA KUUAWA,’ambayo ilichukua nafasi ya nne ya habari hizo za siku hiyo. Hakuitegemea. Hivyo, ilimshtua sana, kwani kwa utamaduni na hulka ya Watanzania hilo lilikuwa jambo geni.

Aliisoma habari hiyo kwa kituo mara tatu, akihariri kati ya taarifa halisi na ushabiki wa mwandishi. Haikumchukua muda kujikuta akijiuliza swali lilelile lililokuwa likisumbua vichwa vya watu wengi; walikusudia kumuua Rais?

Jibu halikuwa rahisi kiasi hicho. Aliamua kuachana na habari hizo na kufungua e-mail yake; jkiangoyahoo.com. Kama alivyotegemea alikutana na ujumbe toka kwa Nuru. “Nimekutafuta sana kwa simu hupatikani. Una habari kuwa Rais ameponea chupuchupu…” Joram alizisoma tena habari za tukio lile la Dar es Salaam kwa mtazamo wa Nuru. Alimsoma katikati ya mistari na, hivyo, kuona matarajio ya msichana huyo kumshawishi ili ajitome katika uchunguzi wa tukio hilo.

Alitabasamu.

Ili kujiepusha na blaablaa nyingi za simu ambazo zingeweza kumvurugia mkondo wa masomo yake, Joram alikuwa ametoa kadi yake ya simu ya nyumbani na kuweka ya muda. Hivyo akiwa katika anga la Kenya, kuelekea Nairobi, aliitupa kadi ile ya Ujerumani na kuirejesha ya Tanzania. Hazikupita dakika tano, simu iliita. Na hakuwa mwingine zaidi ya Nuru. “Umepata e-mail yangu?” aliuliza

“Naam” alimjibu

“Kwahiyo una maoni gani?”

“Maoni gani?” Joram aliuliza baada ya kucheka. “Nuru naona umeanza. Mimi na wewe ni nani katika nchi hiyo hata tusumbue vichwa vyetu mara kwa mara kwa matukio yasiyotuhusu? Nimesema na narudia kusema kuwa tukio la Mtambo wa mauti lilikuwa la mwisho.”

Joram alimsikia Nuru akicheka upande wa pili wa simu. Kisha alisema, “Tusidanganyane Joram. Mimi nakufahamu vilivyo. Wewe si mtu wa kukaa kimya wakati Rais wanchi yako anatishiwa kuuawa.”

“Hatuna hakika kama walikusudia kumuua,” joram alimkumbusha.

“Na ni hilo lililofanya kila mtu akufikirie. Hatuwezi kukaa kimya wakati kitendawili cha tukio hili hakijateguliwa,” alisema kabla ya kuuliza, “Unarejea lini?”

“Leo, muda mfupi baadaye tutakuwa pamoja. Kumbuka nakuja kupumzika. Siji kufanya kazi za wavivu wanaofura matumbo na kusahau wajibu wao. Watu wanaowasahau raia na kutumia vyeo vyao kuwalinda mafisadi”

Kicheko cha Nuru kilimkatiza Joram

“Sasa unacheka nini?”

“Nimefurahi. Huyu ndiye Joram Kiango ninaemfahamu.”
 
2

Nilisoma gazeti hilo na mengine yote yaliyoandika chochote juu ya kifo cha Cleopatra. Hali kadhalika, nilifuatilia habari zote katika televisheni na redio kwa makini kabisa. Kwa muda huo mfupi, kwa kupitia picha mbalimbali za magazeti na televisheni nilikwisha mfahamu vilivyo marehemu kama ninavyofahamu kiganja changu. Na kwa maelezo ya vyombo hivyo niliweza kujua mengi kuhusu maisha yake kama ninanvyomjua binamu yangu.

Katika yote niliyoyasoma au kuyasikia kitu kimoja kilikuwa dhairi, kama alivyoandika yule mwandishi kuwa “Cleopatra hakuwa mtu wa kufa” dhana ambayo ilinipa kitendawili kizito sana, hasa nikizingatia ukweli kuwa kazi ya kumuua ilikuwa nyepesi sana, kama kuua mbu ndani ya chandarua.

Kwa kawaida katika shughuli zetu hizi tunashauriwa kupanda ndege ya kwanza mara baada ya tukio kukamilika. Hivyo ingekuwa busara kuwa badala ya kuwa juu ya kitanda laini, katika hoteli murua, nikifuatilia tukio nililolianzisha mwenyewe ningestahili kuwa angani nikielekea nje ya nchi na nje ya bara. Lakini tukio hili lilinitia ushawishi mwingi, hata nijikute na hamu kubwa ya kufahamu mengi ambayo kitaaluma hatuhitajiki kuyafahamu. Nilitamani kujua mwajiri wangu ni nani na alikuwa na uwezo gani kiasi cha kunirahisishia kazi namna ile.

Hayo ndiyo yaliyoimeza kiu yangu ya kwenda kuwawinda viboko wa ziwa Tanganyika, badala yake yananizalia hamu ya kujiingiza katika utafiti wa kumpeleleza mwajiri wangu. Muuaji anapogeuka mpelelezi wa mauaji yake mwenyewe! Shit

Wakati mkondo huo wa mawazo ukichukua kasi katika ubongo wangu, nilikuwa nikimalizia kazi ya kumfumua mwanangu na kumtawanya katika sehemu mbalimbali za begi langu. Kila sehemu ilifunikwa kwa mifuko maalumu ya nailoni ambayo scanner yoyote katika viwanja vya ndege isingeweza kubaini. Hali kadhalika, ingehitaji mkaguzi mwenye ujuzi na akili za ziada kuibaini katika begi hilo maalumu hata kama angeachiwa saa nzima ya kulikagua. Hivyo, sikuwa na wasiwasi kwamba watumishi wadadisi wa hoteli hiyo wasingeweza kushuku chochote katika begi hilo.

Kazi ngumu ilikuwa ya kujibadili. Kutoka katika jinsia hii kwenda ile. Hii ilihitaji umakini na utulivu mkubwa. Aidha, ilihitaji si chini ya saa tatu hadi nne kujivua usichana na kuvaa uvulana. Yalihitajika mafuta maalumu ya kulainisha mwili ili kuitenganisha ngozi na zile plastic laini zilizofanana vilivyo na ngozi asilia. Mafuta ambayo pia yalisaidia katika kuondoa nyusi, matiti na kucha za bandia pamoja na kuvua lile wigi maalumu lenye nywele za Kihabeshi kwa kila mwanamke aliyenitazama na kushawishi kwa kila mwanaume. Jukumu la kufuta poda, rangi za midomo na kuipoteza harufu ya pafyumu mwilini ilikuwa ndogo, kama ambavyo ingekuwa rahisi kubadili mavazi yale ya kike na kuvaa ya kiume.

Hata hivyo, hayo sikuyafanya kwa sasa. Nilikodi chumba hicho kwa jina la kiume, kwa njia ya mtandao, nikitumia jina la Freddy Macbain na mke wangu Monalisa Macbain ambaye angetangulia. Nilihakikisha kupatiwa chumba hicho kwa simu, nikiitumia ile sauti yangu nzito ya kiume.

Hivyo, niko hapa kama Monalisa anayemsubiri mumewe, Dkt. Freddy Macbain, mhadhiri katika chuo kikuu kimojawapo nchini Hispania. Ili kumpa uhai Dkt. Mcbain nilipenyeza vitu fulani katika mtandao kwa kumfanya aonekane kama msomi mashuhuri aliyekuwa akifanya fukuto ili kubaini kiini cha Waafrika walio wengi kugubikwa na imani za kishirikina hadi katika karne hii ya ishirini na moja kuliko wazungu ambao wengi wao wanazipuuza. Katika hali hiyo sikuona umuhimu wa kujibadili mapema kuwa mwanaume hadi wakati utakapojiri na Macbain kuhitajika. Isitoshe huchukua siku nne hadi tano kabla ya mwili huo wa bandia kuanza uasi.

Nikaendelea kuwa Monalisa, mrembo wa haja, aliyejilaza kifudifudi, peke yake, juu ya kitanda cha kifalme, ndani ya chumba cha kimalkia, akitazama Tv na kusoma magazeti. Chumba ambacho kwa ajili ya kitanda hicho, televisheni, viyoyozi na pengine vinywaji mbalimbali katika jokofu, kilinigharimu shilingi laki nane kwa siku. Pesa ambazo, hata hivyo, niliziona kama uchafu tu katika akiba yangu iliyokuwa ikifurika kwa mamilioni ya fedha za kigeni.

Nilitabasamu peke yangu pale nilipoilinganisha starehe niliyokuwa nikiifanya na hali halisi ilivyokuwa enzi za utoto wangu, hata nikurupuke kuwa mmoja wa wadunguaji wenye hadhi ya juu duniani.

Ilikuwaje?

Laiti ingekuwa ajali. Na kama ajali basi ilikuwa imeandaliwa vizuri sana na viumbe wale ambao binadamu tunawaita wanasiasa. Pande zote mbili wafuasi wa Wahutu walijua wanachokifanya hadi ilipofika April 6, siku iliyobadili kila kitu katika maisha, fikra na ubongo wangu.

Tarehe hiyo ya mwaka 1994 ilinikuta nikiingia katika mwaka wa kumi na nane katika uhai wangu hapa duniani. Kesho yake ingekuwa sherehe yangu ya kuzaliwa, jambo ambalo halikutokea na kamwe halitatokea tena katika maisha yangu, kwani pigo hilo liliambatana na mabadiliko ya historia yangu ikiwa pamoja na tarehe yangu ya kuzaliwa.

Ni siku hiyo ziliposika taarifa za kifo cha kutatanisha cha aliyekuwa Rais wa Rwanda, Generali Habyarimana. Ndege yake, akitokea Arusha, ilitunguliwa. Taarifa hizo zilizofuatiwa na kufumka kwa lile wingu zito, lililokuwa limetanda kwa muda mrefu katika anga zima la Rwanda na miale yake kumwagikia nchi nzima, maafa mazito ya kinyama yaliyokuja kufahamika baadaye kama mauaji ya kimbari yakafuatia. Mauaji hayo yanaaminika kuteketeza watu wasiopungua laki nane, baba, mama na ndugu zangu wote wakiwemo.

Hadi wingu hili linajikusanya sikupata kuwaza kuwa kuning’olea ndoa ya baba aliyekuwa Mhutu na mama mwenye asili ya kitsusi ilikuwa nuksi. Waliishi kwa upendo, miaka yote ya uhai wao nikiwa mvulana. Baba alikuwa mrefu, mng’avu mwenye sura na umbile ambalo mara kwa mara lilizua ubishi kuwa alijifanya Mhutu wakati ki-asili yeye ni Mtsusi, maoni ambayo baba aliyapuuza. Kwa upande wake, mama alikuwa lulu kwa sura yake ya kuvutia, umbile la kusisimua na mrembo wa mahesabu. Kama angeishi enzi za za mfalme Suleiman nina hakika angekuwa mmoja wa wake zake mia nne, kama angeishi Hollywood angecheza filamu zote maarufu.

Tukiwa tumerithi vinasaba vya baba na mama, watoto pia tulikuwa simulizi. Dada zangu walikuwa gumzo kwa kila mtu, wazee kwa vijana, wenyeji kwa wageni. Walipata shida shuleni, walipata kero mitaani. Bila shaka walikumbana na vishawishi vya kila aina. Kwa bahati, baba akiwa akiwa mfanyabiashara mahiri alitulea katika hali ya kutoshawishika kwa lolote, toka malazi hadi mavazi.

Mimi niliondokea kuwa simulizi zaidi. Nilirithi kila kitu kwa baba, isipokuwa urefu wa kupindukia na kila kitu kwa mama isipokuwa nywele zake ndefu za Kihabeshi. Mara kwa mara wageni walipata shida ya kunitofautisha kati ya mvulana na msichana, hali ambayo ilinikera sana. Rafiki zangu shuleni na mitaani waliponitania kwa hilo nilianza ubishi na kuishia kupigana kwa mikono yangu. Hali iliyonifanya niwe sugu wa kupiga na kupigwa. Kwa bahati hakuna kipigo chochote kilichoharibu sura yangu wala kuning’olea meno yangu.

Nje ya hayo, maisha yangu yalikuwa tafrija, tafrija ambayo ilikoma usiku ule wa April 6, pale baba aliporudi nyumbani akiwa katika hali ya wasiwasi. “Kila mtu akae ndani. Nisione mtu yeyote akitoka nje.” Alionya.

Hatukupata kumwona baba katika hali ya taharuki kama ile. Hakuna aliyethubutu kumuuliza kuna nini. Tulipomtazama mama tulishangaa zaidi kumwona akitokwa na machozi. Maswali yetu yalijibiwa muda mfupi baadaye pale milio ya risasi na vilio vilipoanza kusikika katika mitaa mbalimbali ya mji mzima wa Kigali. Baba na mama walitazamana katika hali ya kukata tamaa.

“Pigeni magoti tumwombe mungu” Mama alipendekeza. Alianza yeye kupiga magoti bila kusubiri. Baba alimfuatia. Wote tukapiga magoti na kujiinamia huku mama akiongoza sala.

Sala haikupata kufika mwisho wake. Dakika tano tu baadaye mlango uligongwa kwa nguvu mara kadhaa. Tulipochelewa kuufungua, ulipigwa na kitu kizito, ukaachia. Watu wapatao sita, waliovalia matambara meusi usoni waliingia. Wawili kati yao walikuwa na bunduki, waliobakia walishikilia mapanga na marungu.

“Bwana Rumiya, chui anayevaa ngozi ya kondoo! Unafahamu kuwa tumekuja kukuua?” Mmoja wao, aliyeonekana ni kiongozi wa msafara alisema. Sauti yake haikuwa na mzaha wowote ndani yake.

Baba aliinuka na kuwauliza, “Kosa langu ni lipi?”

“Hulifahamu?” Yule msemaji aliuliza kwa kebehi.

“Tukuambie kosa sio? Hukumbuki mara ngapi tumekuonya kuachana na huyo mwanamke nuksi hukutaka kutusikia, huamini katika jamii. Adhabu ya msaliti ni kifo.

Baba alijaribu kujitetea. Lakini mtu mmoja aliyekuwa na rungu alimpiga nalo kichwani huku akisema, “Naona mnamchelewesha.”

Mama aliinuka toka pale alipokuwa amepiga magoti na kumrukia mtu huyo huku akijaribu kumpiga ngumi za uso. Risasi moja tu ya kisogo ilifanya kichwa cha mama kifumke, mchanganyiko wa ubongo na damu vikimwagika na kumtangulia wakati akienda chini kama mzoga.

Dada zangu walipiga yowe. Wauaji hao waliwafuata na kuwapiga makofi. Huku wenzi wao wakiwa wamewashikilia, wengine walitatua mavazi yao na kuwaacha kama walivyozaliwa. Kisha waliwatupa chini na kuwabaka bila kujali kelele zao. Baada ya vitendo hivyo vya kinyama waliwaua kwa risasi mmoja baada ya mwingine.

Binafsi nilikuwa bado nimepiga magoti, wakati yote hayo yanatokea. Nilijihisi kama niliyeishiwa nguvu na uwezo wa kufikiri. Badala yake nilitumbulia macho kila kitendo kana kwamba natazama mchezo wa kuigiza katika mkanda wa video. Nilizinduka pale walipoanza kuondoka zao baada ya kuhakikisha kuwa walengwa walikuwa wamekata roho.

Nadhani nilipiga kelele. Nadhani nililia kwa sauti. Ninachokumbuka ni mmoja kati ya wauaji, aliyekuwa nyuma ya wenzake, kugeuka na kunitazama. Kitu fulani kilinasa macho yake na yangu kwa dakika moja hivi. Mara akawaambia wenzake, “Tangulieni, bado nika kazi ndogo na huyu.” Sikuelewa alikuwa na kazi gani na mimi hadi alipoitua chini bunduki yake na kisha kuniinua pale chini. Mara akaanza kunivua kaptula yangu. Nilijaribu kujitetea lakini teke la tumbo nililopigwa na kunifanya nianguke chali lilinimaliza. Sikuwa na uwezo wa kufanya lolote pindi nikivuliwa nguo zangu zote na kutupwa chini kifudifudi na baadae kutendewa kile ambacho sikupata kukifikiria maishani. Nilipiga kelele za maumivu huku nikihisi kifo, lakini ndio kwanza mtu huyo alichekelea huku akinong’ona “unajua kuwa wewe ni bora kuliko dada zako?”

Sikuwa na uwezo wa kumjibu. Alipomaliza kiu yake aliinuka na kuifuata khanga ya mama, ambayo aliitumia kujifuta. Bunduki yake ilikuwa pale juu ya kochi alipoweka. Hadi leo sifahamu nilipata wapi nguvu, ambazo zilinifanya niinuke, niichukue na kumlenga. Alipogeuka alikutana na mtutu na bunduki yake ikimtazama. Alishituka sana. Kisha alicheka kwa kuamini kuwa nisingeweza kuifyatua. Alikuwa amekosea sana. Baada ya kutazama filamu nyingi za Kimarekani, baada ya kushuhudia muda mfupi uliopita akiitumia dhidi ya familia yangu, sikuwa na namna ya kushindwa kubonyeza tufe la kufyatulia. Risasi tatu zilitoka moja baada ya nyingine kabla sijakiondoa kidole changu. Adui yangu alikuwa tayari amedondoka chali damu zikiwa zimetapakaa kifuani mwake. Hakupata walao wasaa wa kupapatika.

Kisha mie pia nikaanguka chini, bunduki ikiwa bado mikononi mwangu.
 
Eheeee......endelea......
Naomba unitag pls........
 
3

Wakati wanahabari wakicheza na tafrija hiyo ya tukio ambalo kwa mujibu wa kazi yao lilikuwa la kusisimua, wanausalama walikuwa katika wakati mgumu kuliko wakati mwingine wowote ule. Walihangaika kimwili na kiakili, jasho likiwatoka, hasa kwa kutokujua wapi kwa kuanzia, wapi kwa kuishia.

Walikusudia kumuua Rais? Ni swali la kwanza kabisa ambalo lilivisumbua vichwa vyao. Waliteseka zaidi kwa kutokuwa na jibu rahisi kwa swali hilo. Hivyo, maswali yaliyofuatia; Ni nani, au akinanani? Sababu ya malengo yao ni ipi? Na wangenufaika vipi na kitendo chao? Yalipita katika vichwa vyao na kuwachanganya zaidi.

Bila ya jibu lolote kwa maswali hayo liliibuka lile kubwa zaidi ambalo si kwamba liliwasumbua tu; bali pia liliwatisha sana; tukio hilo ni mwanzo au mwisho wa makusudio ya muuaji au wauaji hao?

Maisha ya Rais si mchezo. Rais ni moyo wa nchi. Hatima ya maisha au kifo chake ni hatima ya nchi na wananchi wake. Kwa mantiki hiyo tukio la kutisha au kuchezea maisha yake, kwa risasi ambayo ilimwacha futi moja tu kutoka aliposimama halikuwa jambo la kawaida. Nusu saa tu baada ya kitendo kile cha tukio tayari ilikuwa imeundwa kamati ya ufuatiliaji ambayo iliwashirikisha viongozi wa majeshi pamoja na mratibu wa shughuli za usalama Ikulu. Ofisi ya muda iliandaliwa katika moja ya majengo yanayomilikiwa na Usalama wa Taifa kwa siri, kando kidogo ya jiji la Dar es Salaam. Kwa pamoja walipokea na kupeana taarifa, kila mmoja akitoa maelekezo katika kitengo chake kwa mujibu wa upatikanaji wa habari.

Shinikizo la kuikamilisha kazi hiyo kwa siku tatu, muuaji akiwa amepatikana, liliwasumbua sana. Hasa ikizingatiwa kuwa kwa mujibu wa mkuu wa jeshi la polisi, amri hiyo ilikuwa imetolewa na Rais mwenyewe kwa njia ya simu muda mfupi tu baada ya kunusurika. “Amesema anamtaka ama akiwa hai au maiti. Pia, anataka taarifa kamili ya uchunguzi wa kitendo hiki. Sijapata kumsikia Rais akifoka kwa ukali kiasi kile, utadhani amezungumza na mtoto mdogo.” Alisema mkuu wa jeshi la polisi.

“Achana na hayo ya ukali” alidakia mkuu wa majeshi ya ulizi na usalama, “Mimi nataka kujua Rais yuko wapi, na iwapo yuko salama kwa kiasi gani wakati huu.” Aliongeza akimtazama mkuu wa Usalama wa Taifa.

Kwa sauti ya kujiamnini afisa huyo alisema “Rais yuko salama. Tumemshawishi kwa tabu kuhama makazi yake ya Ikulu kwa muda, kwa bahati ameafiki…”

“Yuko wapi?” mkuu wa majeshi alihoji tena.

“Hapana. Hilo ni jambo pekee ambalo sitalieleza katika kadamnasi hii.”

Kauli hiyo ilimkera mkuu wa majeshi. Sioni kama hii ni kadamnasi,” alimrushia. “Hii ni kamati mahususi yenye jukumu muhimu la kulinda uhai wa Rais wetu, nchi na wananchi wake. Tuna haki ya kufahamu aliko.” Alitazama huku na huko, kila mmoja kwa zamu, kabla hajaongeza “Mimi kwa mfano, tayari majeshi yangu yote yako katika hali ya hadhari. Hakuna ndege inayoruka toka nje au ndani ya nchi bila kupitiwa na macho ya rada zetu. Mipaka yote pia imedhibitiwa. Hakuna shambulio lolote toka nje ambalo halitadhibitiwa kwa nguvu zote.”

“Kwa bahati,” alidakia mkuu wa usalama. “Taarifa ambazo zimetufikia, toka nchi adui na rafiki zinaonyesha kutokuwepo kwa fununu yoyote ya nchi yoyote, au mashirika yoyote kujihusisha na hili. Inaonekana wote wameshangazwa na tukio hili kama sisi tulivyoshangazwa. Hata hivyo tunaendelea na kupokea taarifa na kuzifanyia tathmini ya kina.”

Wasikilizaji wake wote walipigwa na butwaa. Badala ya taarifa hiyo kuwafariji iliwaongezea msiba. Kwao ilibashiri ugumu wa kazi yao kupata ufumbuzi katika siku tatu walizopewa.

“Hata hivyo, bado nahitaji kujua alipo Rais” mkuu wa majeshi alisisitiza, madai ambayo yaliokolewa na simu aliyopigiwa na mkuu wa polisi na kubadilika sura na sauti ghafla kana kwamba anapokea habari za msiba. Alipoitua chini, alijiinamia kwa muda kabla ya kusema lolote.

“Kuna nini?” Mtu mmoja aliuliza.

“Nadhani hii ni habari nyingine njema jioni ya leo.” Alieleza. “Marehemu alikuwa na briefcase iliyokuwa na nyaraka mbalimbali, zikiwemo za Rais, muda mfupi kabla ya kifo chake.”

“Kwahiyo?” mwingine alidakia.

“Briefcase hiyo imetoweka!”

“Nini!” mkuu wa majeshi alifoka. “Ama kweli hiyo ni habari njema ya leo”


***

Kati ya wasaidizi wakubwa wa kamati hiyo ya muda iliyojumuisha vigogo wa ulinzi na usalama alikuwamo Afande Chaku. Alikuwa amevalishwa ghafla joho la kuongoza kikosi maalumu cha wapelelezi, toka idara mbalimbali, kwa masharti ya kupata ufumbuzi ndani ya siku tatu alizotoa Rais.

Afande Chaku jina lake halisi likiwa Chakubutwa Mwanakereke. Alikuwa na cheo cha juu katika kikosi chake mahususi kwa maswala ya aina hii, kikosi ambacho awali kiliongozwa na Inspekta Kombora aliyestaafu miaka mitatu iliyopita. Viatu vyake vilivaliwa na Inspekta Halfani Matata, aliyehamishwa toka usalama wa Taifa. Chaku na Inspekta Matata walikuwa kama mbwa na chatu. Siku zote Chaku alijichukulia kama mbwa ambaye alikuwa akicheza mbele ya chatu anayesubiri kwa hamu kummeza. Kwa mtazamo huo huo Chaku aliamini kabisa kuwa kitendo cha kuteuliwa kuongoza kikosi maalumu, kwa muda maalumu ilikuwa sehemu ya chatu huyo kufanikisha azma yake ya kumtafuna akiwa hai.

Mtafaruku baina yake na bosi wake huyo ulianza siku chache tu baada ya kuingia kwake madarakani na kupekua majalada mbalimbali ambayo yalikuwa yakifanyiwa kazi. Jalada moja lilimvutia zaidi. Lilikuwa swala la kigogo mmoja wa ndani ya chama, ambaye pia alikuwa mbunge aliyetuhumiwa kuhusika na tuhuma za kumbambikia kesi mwandishi wa habari, ambaye alikuwa akifuatilia tuhuma hizo na kuhakikisha anapelekwa gerezani ambako alifariki katika hali ya utata siku chache baadaye. Jalada hilo alikuwa nalo afande chaku na tayari alikuwa amekusanya ushahidi wa kutosha ambao ungeweza kumtia hatiani kigogo huyo.

Inspekta Matata alimwita Chaku ofisini kwake na kudai maelezo ya kina juu ya sua;la hilo. Chaku allijieleza vizuri na kudokeza kuwa allikuwa akimkamilishja taarifa rasmi ya swala hilo ili aikabidhi ofisi.

“Unayo taarifa ambayo umeiandika tayari? Bosi wake aliuliza.

“Naam. Asilimia tisini na tisa imekamilika.”

“Ilete niione.” Bosi aliamuru.

Chaku alirejea ofisini kwake na kuleta ripoti yake yenye kurasa tisa na vielelezo vya kimaandishi kurasa nane. Inspekta alizipokea na kuzisoma kwa umakini kisha alichukua kiberiti chake cha chuma akakiwasha na kuanza kuteketeza taarifa hizo moja baada ya nyingine. Afande chaku hakuyaamini macho yake. Alipandwa na hasira na kumfuata akiwa amekunja ngumi tayari kumtandika.

“Keti!” Inspekta Matata alimwamuru.

Kwa sauti yenye hasira kali Chaku alinguruma, “Nimetumia mwaka mzima kufanya kazi hiyo. Nimetumia muda na pesa nyingi za walipa kodi. Unajua unachokifanya Inspekta?”

“Keti!” Inspekta Matata aliamuru tena.

Chaku akajikumbuka. Nidhamu ya kijeshi ikamrejea. Akakirejea kiti chake na kuketi ingawa alikuwa bado akitetemeka.

“Labda hutanielewa,” bosi wake alimwambia baada ya kuketi. “Naamini hutanielewa. Lakini nafanya hili kwa kukupenda.”

“Kunipenda!” Chaku alinguruma tena, macho yake yakiwa yamemtoka pima. “Kunipenda! Kwa kuharibu kazi nzuri ambayo niliifanya kwa uadilifu mkubwa! Unajua vishawishi vingapi vya hongo nilikutana navyo katika upepelezi wangu? Unajua vitisho vingapi viliniandama?”

“Kumbe sasa unanielewa,” Inspekta alimjibu baada ya kucheka kidogo, “Nchi hii sio ile ya akina Nyerere uliyoifahamu wewe. Hii ni Tanzania mpya. Ina wenyewe na wenyewe hao sio mimi wala wewe. Hivyo ninashauri, kwa mapenzi kabisa, usijitie ushujaa ambao unaweza kuiletea familia yako kilio na kuwaacha waoga wakikucheka.”

Chaku hakuyaamini masikio yake. Alimtazama bosi wake huyo kwa mshangao mkubwa. Kisha aliinuka na kuanza kutoka.

“Unakwenda wapi?” Inspekta alimuuliza

“Kuandika barua ya kuacha kazi.” Alijibu

Inspekta alitabasamu kabla hajamuuliza, “Unadhani hilo litakusaidia? Usalama wako uko hapa, nje ya hapa maisha yako yapo mnadani.”

Chaku alimkazia macho. Hakuona mzaha wowote katika macho au sauti yake. Akatoka na kuufunga mlango kwa nguvu nyuma yake. Toka siku hiyo hadhi yake katika ofisi hiyo iliporomoka. Inspekta Matata alimpuuza kwa kumchukulia kama hayupo, isipokuwa kwa majukumu ya kitoto, ambayo alihisi yalikusudiwa kumtoa nje ya ofisi hiyo mara nyingi ilivyowezekana. Chaku akaanza kuwa mlevi. Akaanza kusahau usafi. Akawa mtu wa kuingia ofisini muda anaotaka na kutoka muda aupendao. Hakuna aliyemuuliza.

“Tunataka utupatie muuaji…Tunataka kujua kama walimkusudia Rais au la…Tunataka kujua dhamira ya kitendo chao hicho…. Unazo siku tatu tu za kufanikisha jukumu hilo.” Alielezwa.

Ulikuwa mtihani. Afande Chaku alikusudia kuushinda. Hivyo, badala ya kuduwaa akitafakari aliitisha kikao cha maafisa wote ambao angeshirikiana nao kwa nia ya kufahamiana. Kisha walipeana majukumu. “Wewe nenda pale hotelini. Tunataka majina ya wapangaji wote waliopo na waliokuwepo katika siku tatu zilizopita. Tunahitaji kupata orodha ya waandishi waliokuwepo na sehemu zao za kazi, ikiwezekana na taarifa ya kila mtu aliyekuwa hotelini hapo wakati wa tukio.

“Wewe chukua jukumu la kukagua viwanja vyote vya ndege nchini kujua watu gani waliingia na waliiondoka mara baada ya tukio.

Ndugu yangu wewe pita katika mabenki na taasisi zote za kubadili fedha, jaribu kupata taarifa za uingiaji na utoaji.”

Na kadhalika na kadhalika.

“Na wewe?” Afisa mmoja alimtupia swali.

“Mimi nakwenda Muhimbili.”

“Kufanya nini?”

Chaku alimtazama kwa mshangao. “Hujui naenda kufanya nini? Tunafanya uchunguzi wa mauaji ya mtu tusiyemfahamu. Zaidi ya habari na picha za kwenye vyombo vya habari mimi binafsi sijapata kumtia machoni marehemu. Naenda kuitazama maiti yake. Huwezi jua, kwa kumtazama marehemu anaweza kutunong’oneza nani alimuua.”

Kila mtu akacheka.

“Haya… Tukutane hapa saa tatu baadaye kwaajili ya tathmini ya jitihada zetu.”

Wakatawanyika.

Afande Chaku alitumia gari yake binafsi hadi Muhimbili. Haikumchukua muda kumpata Dkt. Hashimu, Mkuu wa kitengo cha Uchunguzi wa maiti. Daktari alionekana kuvutiwa na Chaku, pengine kwakuwa wote walikuwa wakipumua hewa iliyogubikwa na harufu kali ya pombe walizokunywa usiku uliopita. Ndevu nyingi kuliko ilivyostahili, nywele ambazo hazikuchanwa na shati ambalo lilionyesha kutumiwa kwa zaidi ya siku tatu havikumsumbua Dt Hashim mara baada ya kutazama kitambulisho cha Chaku kumthibitisha.

Dkt alimwongoza Chaku hadi chumba cha maiti. Maiti ya Cleopatra ilivutwa toka katika jokofu na kulazwa juu ya meza. Alikuwa ametulia, akiwa amevaa mavazi yale yale aliyokufa nayo. Isipokuwa kwa tundu la risasi katika paji la uso wake na damu ambayo ilizuiliwa kwa pamba angeweza kuwa amelala usingizi wa pono, akiota ndoto zake. Afande Chaku alishtushwa na uzuri wa sura na umbile lake. Kwa mara ya kwanza aliamini ambacho kiliandikwa na waandishi wa habari juu ya uzuri wake. Aliyelala pale hakuwa binadamu, alikuwa malaika. Mara moja alimchukia kwa moyo wake wote mtu aliyemwua msichana huyu. Kimoyomoyo aliapa kumpata na kumfikisha mbele ya vyombo vya sheria.

“Hatujamsafisha wala kumbadilisha nguo. Hata kumshika tumetumia uangalifu mkubwa kwa kuogopa kuvuruga kazi za wataalamu wenu wa alama za vidole. Tunasubiri ruksa yenu ili tuendelee na taratibu zetu nyingine.” Daktari alieleza.

“Tena nimekumbuka,” Daktari Hashimu alitamka. “Nimepigiwa simu hapa na mtu aliyetaka kujua iwapo gari la wagonjwa lililomleta marehemu liliacha mkoba wake hapa. Nimemwambia kuwa hakuja na mkoba wala begi lolote.”

Akili za Chaku zikazinduka. Alitambua moja ya picha za marehemu zilizopigwa takribani dakika tano kabla ya kifo chake akiwa na briefcase mkononi. Chaku hakukumbuka kusikia chochote kikiongelewa juu ya mkoba huo. Kama kweli haujapatikana, haikuwa ajabu kuwa uliporwa katika purukushani zile. Kilichomtisha hapa ni kitu kilichokuwepo ndani ya mkoba wenyewe. Inawezekana kabisa taarifa nyeti za Ikulu zikawa zimeangukia katika mikono ya watu wasiostahili.

Alimwomba Daktari namba hiyo ya mtu wa Ikulu ili afahamu iwapo tayari mkoba umepatikana au la. Daktari aliitafuta katika simu yake ya mkononi alipoipata alimtajia Chaku ambaye aliipiga mara moja. “The number you are calling is not reachable…” mtambo wa Vodacom ulimjibu. Chaku hakuelewa. Baada ya kujaribu mara mbili zaidi alikata tamaa. Akawapigia Vodacom wenyewe kuulizia juu ya namba hiyo. Jibu lilimshangaza zaidi. Kwamba namba hiyo ilikuwa mpya, ambayo kwa kumbukumbu zao ilitumika mara moja tu!

Daktari alisoma mshangao katika macho ya Chaku. “Kuna nini?” alimuulliza.

“Haipatikani.” Alimjibu kwa ufupi.

Alipiga simu nyingine mbili tatu kwa maafisa kadhaa wa usalama kuhakikisha kuwepo kwa mkoba huo. Kila mmoja alionekana kushtushwa na swala hilo. Ilikuwa dhahiri kuwa mkoba huo ulikuwa umetoweka. Ndipo Afande Chaku alipowaarifu vigogo waliokuwa wakiumiza vichwa vyao kwa mauaji. Akawa amewaongezea mzigo mwingine.

Wakati Chaku akimshukuru na kuanza kuondoka, Dkt. Hashimu alimzuia na kumwambia, “Lakini kuna hiki. Nimechukua ridhaa ya kukitoa katika mfuko wa marehemu kwa kuhofia kuwa kingeharibika kwa baridi ya jokofu.” Alisema akitoa bahasha toka kwenye mfuko wake wa suruali na kumkabidhi Chaku.

Ilikuwa bahasha ndogo ya kawaida. Juu ya bahasha hakukuwa na maandishi yoyote. Chaku aliifungua. Ndani kulikuwa na karatasi ndefu, nyeupe, yenye ukubwa wa A5, ambayo katikati iliandikwa maneno matano tu kwa lugha ya Kiingereza: I Love you King Suleiman.

Chaku alitamani kuitupa. Kisha alibadili mawazo na kuitumbukiza katika mfuko wake wa shati. Akamshukuru tena Dkt. Hashim na kisha kuliendea gari lake.

Kwaajili ya kukwepa msongamano wa magari barabarani, Chaku aliamua kuiepuka barabara ya Umoja wa Mataifa ambayo ingemfikisha katika barabara ya Morogoro. Angeifuata barabara hadi Pwani ya Bahari ya Hindi ambako angeishika ile ya Sokoine hadi Magogoni nyuma ya ofisi za Ikulu zilipokuwepo ofisi zao za muda. Badala yake aliingia Umoja wa Mataifa na kuichukua ya Upanga. Aliupita ubalozi wa Congo na kuteleza hadi alipolifikia jengo maarufu la Diamond Jubilee na kutokea barabara ya Ali Hasaan Mwinyi. Aliifuata hadi kwenye mzunguko ulioigawa njia hiyo, moja ikiwa Ohio na ya pili U.W.T. Wakati akisubiri taa alipatwa na wazo. Alikuwa bado na dakika arobaini na saba za ziada kabla ya kikao chake cha kwanza cha tathmini. Toka hapo alipokuwa hadi eneo la tukio umbali haukuzidi mita mia tatu. Akaamua kuutumia muda huo kuvinjari jengo hilo.

You never know…unaweza kupata harufu ya muuaji na ikakusaidia.’ aliwaza. Akahama njia na kuingia Ohio. Hoteli ya Sheraton ilikuwa kushoto kwake. Alipita hadi katika eneo la maegesho, akashuka.

Harufu ya maafa ilimlaki. Askari wenye magwanda na makachero walikuwa tele hapa na pale. Kila aliyeingia au kutoka aliulizwa maswali mengi ama kwa macho au kwa sauti. Chaku, alikuwa mtu ambaye hakupata kuvaa magwanda toka alipojiunga na fani hizi. Hivyo alishukiwa kama raia yeyote wengine. Kitambulisho chake kilitazamwa, saluti zikafuata, akaruhusiwa kupita.

Akiwa tayari na maelezo ya kutosha juu ya tukio zima, hakuitaji kuingia ndani. Badala yake, alisimama mbele ya lango kuu kama ilivyokuwa kwa wapiga picha akijaribu kuvuta taswira ya hali halisi ilivyokuwa. Hapo alipokuwa, angeweza kumuua mtu yeyote aliyesimama mbele yake, ikiwa pamoja na Rais, lakini asingetoka hai. “Muuaji hakuwa miongoni mwa wapiga picha”. Alijinong’oneza. Kisha alienda mlangoni na kusimama pale aliposimama Rais, mgeni wake na marehemu. Alitazama mbele yake. Macho yake yalikutana mara moja na jengo la upande wa pili wa barabara ambalo lilitazamana vilivyo na hoteli. Akizingatia taarifa za awali na ukubwa wa tundu la risasi aliloliona katika paji la uso wa marehemu, Chaku alijiaminisha mara moja kuwa silaha iliyotumika haikuwa bastola bali bunduki kubwa. Hivyo haikuwa imefyatuliwa toka katika kadamnasi iliyokuwa hotelini hapo.

Akaiacha hoteli na kuvuka barabara.

Jengo hilo la ghorofa nane lilikuwa jipya. Ghorofa nne au tano tayari zilijaa wapangaji wa makampuni mbalimbali. Ghorofa zilizobakia zilikuwa katika hatua ya mwisho ya rangi na vitu vichache vingine. Chaku aliyabainisha hayo wakati akipanda juu ili aweze kuona vizuri kila ghorofa. Kama ilivyo kwa majengo mengi ya aina hii, kila mtu alishika hamsini zake, watu wengi walipanda au kushuka katika liftiwengine wakizungumza katika korido na kadhalika. Hakuna aliyejisumbua kumtazama Chaku. Hivyo alipanda hadi juu bila bughudha.

Vyumba vya ghorofa ambavyo vilikuwa havijakamilika vilimvuta zaidi. Alichungulia kila chumba ambacho madirisha yake yalielekea hotelini. Kimoja wapo katika ghorofa ya sita kilimvutia Zaidi. Macho yake yalienda moja kwa moja hadi mbele ya hoteli, mbele ya sura za kila anayetoka hotelini, mdunguaji yeyote mwenye bunduki mahiri angeweza kufanya kazi yake vizuri sana akiwa chumbani humu, aliwaza.

Akatazama saa yake. Alikuwa bado anazo dakika kumi na mbili kabla ya kikao. ‘Zinatosha.’ Aliwaza akitoa daftari lake dogo la mfukoni na kunukuu mambo kadhaa na hisia zake toka Muhimbili hadi hapa.

Niko katika chumba alichokuwamo muuaji. Aliandika akitaja namba ya chumba na ghorofa ya jengo. Baada ya kuwaza sana aliongeza: Nadhani.
 
4

Tanzania na pengine duniani kote, kuna waandishi wa habari ambao wanaishi kwa uandishi lakini hawaandiki, waandishi ambao badala ya kuuza habari, wao huuza maneno. Wale ambao hutumia vitambulisho vyao kuchokonoa mambo, wakiyapata huenda upande wa pili kuuza walichokipata, ama kwa vitisho ama kwa kujifanya waugwana. Kati ya hawa, wapo ambao hata hudiriki kushinda mahakamani, wakisubiri kile wanachoita ‘kesi nzuri’ ambayo ama haijavifikia vyombo vya habari ama mhusika asingependa ivifikie. Kwao hii ni ‘dili’ ambayo huwapatia mkate wao wa kila siku.

Kati ya kundi hilo wapo ambao kwao fedha sio muhimu sana. Wao ni wagonjwa wa pombe za bure. Siku zote wao wanajua wapi kuna hafla au tafrija gani, ipi bora zaidi, ipi ina bore. Hawa hawaitaji mwaliko, kwani hujialika wenyewe. Huwa ni wa kwanza kufika kabla ya waalikwa na kuanza kunywa. Huwa wa mwisho kuondoka baada ya kuhakikisha vinywaji vimekwisha na ‘mshiko’ kwa maana ya nauli imepatikana

Hawa huitwa makanjanja.

Frank Mwaipula alikua mmoja wao. Yeye alikuwa mtu wa mahoteli makubwa. Siku zote ratiba yake ilikua imejaa. Na kila siku alirudi nyumbani chakari kwa kinywaji. Mara nyingine alitoka na bia za kopo au chupa ya wiski ambayo ilipotelea katika mifuko ya koti lake jeusi, ambalo kamwe halikumtoka mwilini, kama ilivyokuwa tai yake shingoni.

Mchana huo alikuja Sheraton kwa mengine. Tafrija ya ufunguzi wa warsha ya ushirikiano wa waandishi wa Afrika ilikua ifanyike katika ukumbi mmoja wapo hotelini hapo. Kama kawaida alikuja mapema,akaketi katika makochi pale mapokezi. Hakua na haraka. Alisoma magazeti matatu ya bure kabla ya kubaini kuwa Rais na mgeni wake walikuwa wakitoka. Kama ilivyokuwa kwa watu wengine, aliinuka toka kwenye kiti kumpa hadhi mkuu wanchi. Kama watu wengine, alivutiwa sana na umbo la Cleopatra, aliyesimama kati ya Rais na mgeni wake, wakisubiri kutoka. Alikua ameiona mara nyingi sura ile katika televisheni na hakupata kuikinai. Leo kumwona ana kwa ana kulimvutia zaidi. Macho yake yalitambaa mwilini mwake, toka miguuni, kiunoni hadi usoni ambako yaliganda. Yangeweza kuganda kwa miaka kama isingetokeaCleopatra ambaye sekunde moja alisimama pale kwa madaha na ulimbwende, sekunde ya pili alipaa angani na kutua chini ambako alipepesuka na kutapatapa kabla ya kukata roho. Damu zilimiminika toka mahala fulani usoni. Watu wote walipigwa na butwaa. Lakini hawakupata nafasi ya kuendelea kuduwaa pale wanausalama walipochemka ghafla na kumpiga Rais kumbo lililomwangusha chini huku mmoja wao akimlalia kama ngao, bastola yake ikiwa tayari mkononi. Wanausalama wengine wakikimbia huko na huko, mmoja wao aliamuru kila mtu kulala chini. King’ora na filimbi nyingi zilisikika…

Frank Mwaipula hakujua kilichotokea. Alikumbuka kuanguka, kuinuka na kuanguka tena huku kitu fulani kikitambaa sakafuni na kumgonga kifuani. Kwa mikono inayotetemeka alikipapasa kitu hicho na kubaini kuwa ilikua briefcase ambayo muda mfupi uliopita aliiona ikiwa mikononi mwa Cleopatra.

Hakumbuki ilikuaje, hata akatoka nayo.

Anachokumbuka ni kujikuta yuko nayo ndani ya daladala, akielekea nyumbani kwake Kinondoni, mara alipopata fursa ya kuondoka eneo hilo. Mikono na miguu yake ilikuwa bado ikitetemeka.

***


Joto la Dar es salaam lilimlaki Joram Kiango mara ndege yake ilipotua katika Uwanja wa Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere. Alikua amevaa koti, akalegeza tai. Ili kupoteza kidogo sura yake, alivaa kofia pana iliyofunika uso wake, kisha alijiunga na wengine katika pilikapilika za kushusha mizigo yao ya mkononi. Akiwa mtuasiyependa mizigo mingi, Joram alikua na begi moja tu la mkononi, kiasi kikubwa likiwa limejaa vitabu, nyaraka na makabrasha yake mbalimbali.

Aliitazama saa yake. Ilikuwa bado ikisomeka katika mwenendo wa kijerumani, saa 10.20. Akairekebisha kuwa mbili na dakika kumi na saba, kwa saa za Afrika Mashariki.

Alikuwa miongoni mwa abiria wa kwanza kushuka, akiwaacha wengine wakisubiri mizigo yao ya ziada, akatoka nje ya uwanja. Kama ilivyokuwa kwa abiria wengine madereva wa teksi walimkimbilia kwa matumaini ya kumshawishi akodi magari yao. Aliwapuuza. Nuru alikuwa akimsubiri katika gari lake, ndani ya eneo la maegesho, utaratibu ambao waliubuni kitambo ili kuepuka kutazamwa kama wacheza sinema.

Darling” Nuru alisema akimrukia Joram na kumkumbatia kwa nguvu zake zote. Akiwa na begi lake mkononi, koti mkono wa pili, Joram angeweza kuanguka kutokana na kitendo hicho cha Nuru, kama asingekuwa mkakamavu. “Taratibu wee mwana!” alimwambia akicheka.

Nuru alimbusu mdomoni kabla ya kupokea mizigo na kuiweka ndani ya gari.walikumbatiana tena.

“Za safari?”

“Sio mbaya. Tatizo ni lile lile. Huku joto la kutisha kule baridi la kuua.”

“Pole sana”.

“Na nyie za hapa?”

“Pia hakuna jipya, zaidi ya dada wa watu aliyeuawa kinyama bila sababu za msingi.”

Joram alitabasamu kabla ya kusema “Ya kaisari mwachie kaisari. Nahitaji kuoga… Nahitaji kupumzika. Sijisikii kujadili mambo ya vifo kwa sasa.”

“Kuna ubaya gani? Nitakusaidia kupumzika vizuri kabisa. Tena nina kisasi na wewe,” Nuru alisema.

“Kwanini?”

“Kuniacha muda wote huu peke yangu, bila hata simu! Naona wajerumani walikuzingua. Nataka kufuta nyayo zao zote katika mwili na akili yako.”

Joram aliangua kicheko.

Wakaingia katika gari. Likatiwa moto na kuelekezwa mjini, wakiifuata barabara ya Nyerere.

“Alikuwa mzuri wa haja,” Nuru aliongea ghafla.

“Nani?”

“Marehemu”

“Marehemu gani tena?”

“Cleopatra”

“Nuru” Joram alisema, akikunja uso wake kwa namna ya hasira. “Nikuambie mara ngapi kuwa nahitaji kuupumzisha mwili na ubongo wangu? Uzuri! Uzuri kwa mume wake. Uzuri ninaohitaji mimi ni wa mwanamke mmoja tu duniani na hana shaka.”

“Mwanamke yupi huyo?” Nuru aliuliza akiwa ametoa macho. “Sema vizuri kabla sijakutafuna ukiwa hai,” aliongeza.

“Anaitwa Nuru. Anaishi Dar es salaam. Na kwasasa anaendesha gari akielekea mjini kumtafuna mhanga wake akiwa hai,” Joram alimjibu.

Wakaangua kicheko, kicheko ambacho nusura kiwaletee ajali pale gari lilipoyumba na kukoswa kidogo sana na daladala lililokuwa likija kasi kuelekea pugu. Baada ya hapo, waliendesha wakiwa kimya, Nuru akitazama magari ya mbele na nyuma kwa uangalifu. Muda mfupi baadae aliropoka tena, “Unadhani walikusudia kumuua Rais?”

“Watu gani?” Joram alimuuliza

“Hawa waliomuua Cleopatra…”

“Nuru!” Joram alinguruma.

***

Dkt. Twalib Khalfan aliketi chini ya kivuli kikubwa cha muembe mkongwe, mbele ya nyumba yake. Alikalia kiti cha uvivu, kilichomfanya nusu awe amekaa, nusu amelala. Mara kwa mara alifumba macho yake kama mtu anayeficha machozi, jambo lililoyafanya macho hayo yawe mekundu kuliko ilivyokuwa kawaida yake.

Nyumba yake yenye ghorofa moja ilijaa waombolezaji ndani na nje. Kifo cha cha Cleopatra hakikuwa pigo kwake peke yake bali kwa ndugu wa pande zote mbili, marafiki na majirani. Mara kwa mara sauti za akina mama wanaolia kwa uchungu zilisikika nakuzidisha majonzi.

Pamoja na msiba, kama ilivyo taratibu za Wahaya, vinywaji aina mbali mbali vilikuwepo. Waliokunywa soda walipata, wale wa bia waliendelea, wa pombe kali pia hawakuwa na malalamiko. Kwa namna fulani ilikuwa kama tafrija ambayo ilikusudiwa kupunguza hisia za msiba na majonzi.

Vinywaji havikuwa tatizo kwa Khalfani. Japo hakuwa tajiri, kwa viwango vya matajiri wa Tanzania, bado hakua masikini. Pato lake, lililotokana na biashara zake za uwakala wa majumba na usafirishaji wa mizigo ya ndani na nje ya nchi zilimfanya kushika nafasi nzuri katika mapato yatokanayo na shughuli za aina hiyo. Zaidi, utajiri wake ulitokana na roho yake nzuri. Alikuwa mtu mpole, mwema na mkarimu. Hakupata kumtupa mtu mwenye shida na alipotoa msaada na ukaupokea ni yeye aliyeshukuru badala ya kusubiri umshukuru.

“Wengi hawafahamu,” Mara nyingi alisema, “Mungu akikupa baraka hata ukawa na uwezo wa kuwasaidia wengine ni wewe mwenye haki ya kushukuru, sio anayepokea. Fikiria kama wewe ndiye mhitaji badala ya mtoaji.” Msimamo ambao ulimfanya awe mtu wa wageni nyumbani na ofisini, kila wakati. Baadhi ya wafanyabiashara wenzake walimcheka na kumtahadharisha kuwa angefilisika. Lakini yeye aliwaambiwa kuwa alichotoa alizidishiwa mara dufu.

Khalfan asingeweza kuwa mkarimu kiasi hicho na roho yake isingekuwa yenye amani, kama isingekuwa kwaajili ya ua la roho yake, Cleopatra. Kama alikuwa mwema aliamini kwa dhati kabisa kuwa Cleopatra alikuwa mwema zaidi yake. Kama alikuwa mkarimu, Cleopatra alimzidi kwa mbali. Sura na roho yake havikutofautiana, vilikuwa dinari kwa ya pili. Khalfan alipata kukiri hivyo kwa rafiki zake wa karibu.

Cleopatra ambaye hayupo tena! Aliwaza, wazo ambalo lilimfanya asahau kuhimili chozi, likamtoka na kuteleza juu ya shavu lake kabla hajalifuta kwa kiwiko cha mkono wake. Watu walioketi nae walimfariji kwa kumkumbusha kuwa mwanaume lazima atawale machozi badala ya kuacha yamtawale.

Ni wakati huo alipotokea mgeni mwingine, mwanamke. Awali mwanamke huyo aliketi miongoni mwa waombolezaji wengine wa kike, kimya, akisikiliza mwenendo wa mazungumzo na tenzi au mashahiri ya waliaji. Alikuwa amevaa baibui lililomfunika sehemu kubwa ya uso hadi miguuni, hivyo hakuna aliyemfahamu. Aidha hakuna aliyemuuliza, kwani haikuwa desturi.

Baadae ndipo aliposogelea kundi la wanaume walioketi na mfiwa chini ya mwembe na kuomba kuzungumza naye faragha. Khalfan alisimama na kumuongoza upande wa pili wa bustani. Kulikuwa na viti vilivyochongwa toka katika magogo ya misonobari. Wakaketi.

“Unasemaje mdogo wangu?” Khalfan alimuuliza mgeni wake.

Kuzungumza na mtu… tena mpole kama huyu… ambaye jana tu nimemuua mke wake… lilikuwa jambo zito kuliko nilivyotarajia. Haikuwa kawaida yangu, lakini kwa mbali nilihisi nikitetemeka. Nilikuwa nikivunja kanuni zote za taaluma yetu.

“Mimi ni mwandishi wa habari. Nilimfahamu marehemu kupitia vyombo vya habari, lakini niliondokea kuwa mshabiki wake mkubwa. Kifo chake ni pengo kubwa, pole sana Bwana Khalfan.”

“Asante. Ndiyo dunia…’ Khalfan alijibu.

Ndiyo dunia ya kishetani tunayoishi. Hakuwa mtu wa kufa! Sikujua kama alikuwa mrembo na muugwana kiasi kile. Samahani sana.

“Ndiyo dunia.” Niliunga mkono. “Sote tutafuata mkondo huo huo.”

“Ni kweli,” Dkt. Khalfan aliunga mkono. “Kwahiyo ulihitaji nini toka kwangu, Bi mwandishi?”

Nahitaji kukuomba radhi. Nahitaji uelewe kuwa sikupata kuwa na kisasi naye. Nilikuwa kazini. Kwa sauti nilisema, “Kama mwana habari kuna mawili matatu tunayohitaji kufahamu kutoka kwako.”

“Kama yepi?”

“Ni ya kawaida tu. Kwa mfano, tungependa kujua hisia zako kuhusu kifo cha mkeo. Unadhani ni nani aliyemuua na kwasababu gani?”

“Ningemjua ningemuua kwa mikono yangu kwanza na kumpeleka polisi baadaye,” Dkt. Khalfan alijibu.

Ungeniua kwanza na kunipeleka polisi baadaye! Nadhani hujui unazungumza na nani. Hujui kama umeketi na Jibril, Malaika mtoa roho. Hujui kama unacheka na shetani halisi mwenye mwili wa binadamu!!! Nilitabasamu kidogo kabla ya kuendelea.

“Inaeleweka Bwana Khalfan. Hakuna ambaye angekulaumu. Lakini hapa kuna tatizo moja. Nimesoma mahali kuwa ulikuwa umetengana na mkeo. Unaweza kuniambia ni kitu gani kiliwatenganisha?”

“Siwezi, kwasababu sijui. Hata kama ningejua sidhani kama ningeweza kukuambia ukaitangazie dunia.”

“Unadhani kuna mtu aliyeingilia ndoa yenu hata mkatengana?”

Kwa mara ya kwanza Dkt. Khalfan alitabasamu. “Cleopatra hakuwa mwanamke wa kulaghaiwa na mwanaume yeyote. Nilimfahamu fika kama yeye pia alivyonifahamu.”

“Lakini inaonekana kifo chake kilipangwa!”

Atakuwa amevaa suruali ya jeans, rangi ya buluu na jaketi la rangi ile ile na fulana yenye rangi ya bendera ya Taifa. Atatoka nje ya hoteli saa nane na robo akiwa katikati ya Rais wa nchi kulia kwake na mgeni wake… kushoto…

“Kwa vipi?”

“Mazingira yanatia mashaka. Muuaji anaonekana alijiandaa kikamilifu, kama ambaye alikusudia kumuua Rais au mgeni wake. Wewe unaonaje?”

“Nilidhani hiyo ni kazi ya polisi, sio mwandishi wa habari,” lilikuwa jibu la Dkt. Khalfan.

“Mwandishi mzuri ni yule anaewatangulia polisi kubaini mambo, sio kusubiri taarifa ambazo mara nyingi huwa hazina ukweli.”

Dkt. Khalfan alimtazama kwa makini. Kisha alimuuliza taratibu, “Samahani bibie, unaandika gazeti gani?”

Gazeti la maangamizi… wino wangu damu, meza yangu kaburi. “Naandika This Day.”

“La wapi?”

Akhera. “Hapa hapa Dar es Salaam”

“Unaitwa nani?”

Kengele za hatari zilianza kusikika masikioni mwangu. Kwa bahati nilikuwa nimejiandaa kwa hilo pia.

“Kwa sera za gazeti letu, tunajitahidi sana kuficha majina yetu halisi. Mara nyingi mimi naitwa ‘Mwandishi Wetu’.’’

“Lakini una jina!”

“Ndiyo… Josephine Mporogwa”

“Josephine… nakushukuru sana. Nadhani sina la ziada ninaloweza kukusaidia. Siku njema.”

Nilijitahidi kuficha miguu yangu na mikono yangu ambayo ilikuwa ikitetemeka kwa mbali. Nikamshukuru na kuaga baada ya kuficha daftari langu dogo ambalo nilikuwa nikinukulia mambo ya uongo na kweli. Nilipofika nje ya mtaa nilitazama huku na huko kabla ya kulichopoa lile baibui, ambalo nililikunja na kulitupa ndani ya pipa la taka.
 
Mh Jana tuu maskini nilinunua Roho ya paka n.a. mtambo wa mauti. Itabidi nikiruditena Dar nikitafute n.a. hiki@Nameless girl
 
Back
Top Bottom