HADITHI: KIVULI CHEUSI
SEHEMU YA KUMI NA NANE
TULIPOISHIA....
Akaiacha pikipiki aliyokodisha akaiendea taksi iliyompeleka hoteli ya Rayberth hotel. Hotel iliyomilikiwa na Raymond kwa fedha haramu. Hotel iliyochipuka ghafla huko pembezoni mwa ufukwe wa bahari. Hakupenda kulaza damu kabla Raymond hajapata habari za vifo vya mke wake na mfanyakazi wake wa siku nyingi.
Moses alipokuwa chini ya ghorofa ya hotel hiyo akimlipa dereva ujira wake, akaliona gari analolifahamu. Aliliona mara ya kwanza katika apartment ya rafiki yake, McCuthbert. Gari ya Jafari Hiza.
*****
ENDELEA..........
Mara tu baada ya kuachana na Moses hotelini, Vannesa alienda hadi zilipo ofisi zake. Huko alikutana na Jafari Hiza akiwa anajiandaa kuondoka.
"Umekula ng'ombe mzima umelishindwa Jicho?" Akamtania Jafari Hiza.
Jafari hakucheka, akataka kutoka bila kuzungumza chochote. Vannesa akamzuia kwa kumshika kifuani
"Unaenda wapi sasa?"
"Mke wa Raymond amefariki" akajibu kwa hali ya kughafirika. Jibu hilo likamshangaza sana Vannesa
"Amekufa!?" Jafari hakujibu kitu, kutokana na bumbuwazi ya kifo cha Bi Furahiya iliyomkumba ghafla Vannesa, akaongozana na Inspekta Jafari Hiza mpaka nyumbani kwa Raymond.
Vannesa akapanda gari ya Jafari kuelekea huko. Wakiwa njiani, Jafari Hiza aliamua kumpigia Raymond. Simu yake ilipopokelewa sauti haikuwa ya Raymond.
"Unasema?.. Basi tunakuja sasa hivi"
Jafari akamueleza Vanessa yote kuhusu taarifa aliyoipokea kutoka kwa mfanyakazi wa Raymond; kuwa Raymond amepoteza fahamu na amezinduka dakika chache zilizopita, hivyo amepumzika.
Vannesa akasema "Unaonaje tukapitia ofisini kwake kisha tuelekee nyumbani. Kwa sababu
tunaweza kupata chochote huko"
"Sawa"
Jafari Hiza alikubali ushauri wa Vannesa. Akaligeuza gari yake na kuelekea kawe ilipo hoteli ya Raymond. Kwa mwendo wa speed kali, kutokea zilipo ofisi za Vannesa walichukua dakika ishirini pekee kuwafikisha kwenye hoteli ya kifahari ya Raymond. Hawakutaka kupiga simu kwa kuwa walipafahamu mpaka ofisini kwake.
Jafari Hiza aliongoza mbele akifuatiwa na Vannesa.
Walikuwa wakipanda lifti kuelekea ghorofa ya tatu zilipo ofisi za Raymond. Hiyo ni baada ya kuliegesha gari yao eneo la maegesho. Walikaribishwa ofisini kwa Raymond baada ya kuonesha vitambulisho vyao. Raymond alikuwa akihema kwa uoga akashusha pumzi ndefu baada ya kumuona Jafari Hiza.
"Afadhali umekuja Jafari" Akapata nguvu ya kusimama. Machozi yakiendelea kumtoka, akawakaribisha Jafari na Vannesa. Aliwaondoa wafanyakazi wake waliokuja kumjulia hali.
"Mke wangu Jafari"
Alikuwa ameinamisha uso wake, alipouinua, ulikuwa umelowa machozi.
"Pole sana Raymond"
"Nitapoa vipi wakati amesema anaitaka roho yangu?" Raymond akawa mkali. Lakini hiyo haikumtisha vannesa kuuliza.
"Wewe unadhani ni nani anahusika"
"Wewe mwanamke una kichaa?"
Akavuta kamasi jepesi na kumuuliza kwa hasira "ina maana Jafari mnafanya nini mpaka sasa?"
"Tupo hapa kukusaidia, mzee"
"Mnanisaidia kumtafuta nani?"
"Muuaji wa mke wako"
"Sasa muuaji wa mwanangu ndiye muuaji wa mke wangu." Alinyanyuka akawa anazunguka kila upande wa ofisi "anajiita kivuli cheusi"
Vannesa naye alikuwa amenyanyuka na kwenda upande wa dirishani huku akimuuliza swali Raymond
"Natumaini Raymond hili ni jambo unalolifahamu kuhusu..." Kabla Vannesa hajaendelea kuzungumza, alinyamaza ghafla. Alinyamaza mara baada ya kumuona mtu ambaye anayemfahamu. Alipotazama kwa makini,
"Hapana"
Akajisemea'Inawezekana namfananisha' Bila kujua wote waliokuwepo ofisini humo wakimtazama yeye, alitoka mbio na kuikimbilia lifti ya kumshusha chini. Bila kuelewa Jafari Hiza akaelekea dirishani kuchungulia chini ya ghorofa ya hoteli hiyo hakuona cha maana.
XXXXX
Moses baada ya kuliona gari ya Jafari Hiza, akataka kumfahamu mtu huyo vizuri. Bila shaka alikuwa na hakika mtu huyo yupo katika ofisi za Raymond. Akataka kufahamu uhusiano uliopo kati yake na Raymond pamoja na Vannesa.
Sawa alijua Vannesa kuwa ni mpelelezi, mpelelezi aliyetumia kivuli cha uandishi wa habari kuficha uhalisia wake. Lakini yeye akamuona Vanessa kama shushu mwenye njaa anayependa kufuatilia mambo ya hatari kuiepusha njaa ya siku chache badala ya kifo cha milele.
Akajipa moyo na kuzifuata lift za kumpandisha mpaka juu. Aliifahamu vyema ofisi ya Raymond kwa kuwa haikuwa mara ya kwanza kuingia katika jengo hilo. Lakini alipofika ndani ya lift na kutaka kubonyeza nambari ya kuelekea zilipo ofisi za Raymond, roho yake ikasita. Iliposita hakubonyeza kitufe cha namba na kubonyeza kile cha kufungua mlango.
"Hapana siendi"
Roho yake ilipokataa, akaitii. Alitoka mpaka nje tena, na kuifuata ilipo barabara. Ni hapo ndipo Vannesa akiwa juu ya ghorofa ndani ya ofisi ya Raymond, alimuona Moses. Kwa kuwa alihisi amemfananisha hakutaka kuamini tu kwa kumfananisha.
Alitaka kujiridhisha kwa macho.
Alitaka kumuona huyo aliyefanana na Moses kuanzia utembeaji, nguo alizovaa pamoja hata na umbo lake. Vannesa akawa ameshuka na kumuona Moses akiwa kwa mbali kidogo. Umbali uliowatenganisha kwa miguu isiyopungua ishirini. Akashindwa hata kumuita, lakini alipata uhakika kabisa ndiye Moses anayemfahamu.
Akarudi ofisini kwa Raymond akiwa na mawazo.
Mawazo ya kujiuliza Moses amefuata nini katika hoteli hiyo? Sawa ni hoteli na kila mtu alikuwa na uhuru wa kufika katika hotel aipendayo, lakini si kwa Moses aliyemuacha hotelini kule kinondoni.
Kulikuwa na mtu alikuwa na miahadi naye? Akaitazama saa yake. 'Hapana' akajisemea. Haiwezekani amuache saa nne asubuhi hotelini tena kitandani halafu saa nane awe amefika katika hoteli hiyo. Ni saa ngapi ameshakutana na mtu huyo na kuzungumza naye? Kwanini awe hana gari? Kuna uwezekano ana uhusiano wowote na Raymond?
Akajiondoa hofu na kusema inawezekana alikuwa ni mteja kama wateja wengine waliofuata huduma ya hoteli ya Reyberth kama wengine. Akaufungua mlango wa ofisi ya Raymond. Hata alipoingia ndani ya ofisi ya Raymond, bado alikuwa akiwaza kuhusu Moses.
Lakini hawakukaa sana ndani ya ofisi hiyo, wote watatu walitoka kwa nia ya kurudi nyumbani kwa Raymond. Vannesa na Jafari Hiza walipanda kama walivyokuja, raymond akawa peke yake.
Walipofika tu katika mtaa aliokuwa akiishi Raymond, simanzi ilionekana katika kila nyuso ya mkazi wa mtaa huo.
Ni mmoja tu ambaye alipata nguvu ya kuisimamisha gari ya Raymond.
Alikuwa ni mwanamke wa makamo aliyelowa machozi. Alilia kwa uchungu.
Raymond alimfahamu fika
"Habari yako mama Koku"
"Si nzuri jirani yangu" akajifuta machozi kwa upande wa kanga, "tafadhali usiingie ndani ya nyumba yako kwa sasa"
"Kwa nini?" Raymond alihamaki kwa mshangao. Vannesa na Jafari nao walikuwa wameshashuka kutoka katika gari lao wakisikiliza kilichokuwa kikisemwa na mama huyo aliyekuwa akivukwa na nguo kwa kilio.
"Nipo na Merce nyumbani kwangu, nusu saa zilizopita amekuja na kunieleza kuwa kuna mauaji yametokea nyumbani kwako. Ndipo akanieleza kuwa kuna mgeni aliyekuja nyumbani kwako"
Mwanamke yule akawa anamuhadithia Raymond. Mgeni huyo alifika nyumbani bila mtu yeyote kumfahamu. Ni Majura pekee mlinzi wa getini ndiye alikuwa akimfahamu. Akaeleza kuwa mgeni huyo pia Bi Furahiya alikuwa akimfahamu hivyo alikaribishwa sebuleni na Bi Furahiya kwenda kumuandalia kinywaji. Hakukuwa na mtu sebuleni zaidi ya mgeni anayeshukiwa ni muuaji na Bi Furahiya. Mara Merce alipoenda kuwaandalia chakula ndipo alifahamu kifo cha Bi Furahiya. Hatimaye walinzi waliokuwa wakilipwa na Raymond pia kati yao akaeleza kuhusu kifo cha Majura getini.
Wote walionekana kufa kifo kimoja.
Wote walitoa mapovu na walikufa haraka. Walilala usingizi wa milele kwa aina moja. Hadithi hiyo ya mama koku ikazidi kumtia uchungu Raymond. Akashuka garini na kutaka kuingia ndani kwa jazba.
Mama Koku akamzuia. "Tafadhali usiingie" Raymond akasimama "naomba usubiri nimalize kuzungumza"
Baada ya kufahamika Majura na Bi furahiya wamefariki, kosa lingine likafanyika. Hapo moyo wa Vannesa ukaanza kwenda mbio. Wakasikiliza kwa makini.
Jafari Hiza na Vannesa walikuwa wakisikiliza kwa makini sana. Mama koku akawa anaendelea huku akivuta kamasi jepesi lililokuwa likijipenyeza katika pua zake. Kuna mmoja kati ya wale walinzi sita aliokota kopo la manukato. Macho ya Jafari Hiza yakamtoka pima.
Mama Koku akaendelea. "Akaipuliza ile hewa aliyodhani ni manukato. Kati ya walinzi wale sita hakuna aliyehimili kusimama kwa miguu yake. miongoni mwa wafanyakazi wote wa ndani ya nyumba ya Raymond aliyepata nafuu ya kutoka nje akiwa hai alikuwa ni Merce. Hewa ile ndani ya chupa ya manukato ilikuwa ni hewa ya sumu...Mimi ndiye nilimsaidia Merce kumpa maziwa. Ndiye aliyenihadithia hadithi yote hii"
Mama Koku hakumalizia hapo akaishia kwa kumwambia kama ushauri Raymond "unaweza kuchagua kuingia ama kusubiri taarifa ya wauguzi waliokuja kuchukua miili ya watu wako"
Jafari Hiza akazungumza "Hiyo sumu ndiyo ile niliyokuambia Vannesa" akamwangalia Vannesa kisha akagota kwenye uso uliomvimba Raymond kwa kulia "Huyu muuwaji ndiye huyu huyu aliyemuua mwanao Bertha na wote niliokupa taarifa juu ya vifo vyao. Huyu ndiye aliyewaua wamiliki wa apartment aliyofanyia mauaji ya shahidi namba moja aliyekuwa akimfahamu kule masaki kwa sumu hiyo hiyo" akawaeleza aina ya sumu ambayo aliitumia kwa kuichanganya katika chupa ya manukato. Habari hiyo haikumfanya Raymond kuacha kulia. Alilia kama mtoto.
Jafari Hiza akaeleza kuwa "hewa hiyo yenye sumu hudumu kwa dakika tano tu hewani, hivyo hakuna shaka kama tukiingia"
Wote wakaingia na kukuta miili ya watu kumi na moja ukiwemo wa bi Furahiya, Majura, walinzi sita na wafanyakazi watatu. Walikuwa wamefunikwa katika mifuko maalumu ya maiti.
******
ITAENDELEA............