HADITHI: KIVULI CHEUSI
SEHEMU YA SABA:
TULIPOISHIA.............
"Majura?" Raymond akauliza kwa jazba. Sauti ile upande wa pili ilijibu kwa kicheko cha dharau na kisha kukata simu. Raymond hakujijua kuwa ameshasimama na kukizunguka chumba chake mwenyewe mara ngapi, alichokitambua yeye ni kuwa yupo nje akimfuata Majura, mbio.
"Majura ulikuwa unasemaje?" alimuuliza.
Majura alitoa boksi moja kubwa lililonakshiwa na kumpatia Raymond "pole sana bosi kwa matatizo. Aliileta babu mmoja, huku akisisitiza ni ya muhimu sana uipate usiku wa leo" alisema. Akili ya Raymond haikuwa katika kusikiliza hadithi za Majura.
Alikwishalifungua boksi lile muda mrefu, kilichokuwemo ndani ya boksi kikamfanya kupoteza fahamu.
Kama asingekuwako Majura karibu yake, basi kisogo cha Raymond kingeisalimu ardhi iliyojaa changarawe. Umapepe wa Majura ukamfanya aropoke.
"Nisaidieni jamaani!!!!!" Kila mtu aliyeisikia sauti ya Majura, alitoka mbio kuelekea getini.
TUENDELEE...............
Vanessa ni mwanamke wa ajabu sana. Aliwashangaza wengi katika uvutaji wake wa sigara. Alizivuta zile sigara kubwa zilizoitwa ‘cigar' Katika ulabu alipendelea haswa zile wine tamu tamu, kama sweet anna na sinzano. Huyo ndiye mpelelezi aliyekataa kujiunga na kikosi maalumu cha usalama wa taifa na kubaki kama mwandishi wa habari wa kujitegemea.
Siyo kwamba hakufuatwa, hata Raisi mwenyewe aliwahi kupoteza dakika zake na kumuandikia barua ya kumomba ajiunge na kikosi hicho. Alikataa bila sababu, lakini sababu aliijuwa mwenyewe. Vanessa aliupenda uhuru wa kufanya kazi zake binafsi. Hakutaka mtu wa kumshinikiza afanye hiki na kile. Magazeti yalimuandika kwa kumtukuza na hata waandishi wengi wa riwaya wakamtaja katika riwaya zao kama mwanamke wa chuma. Akawashinda wanaume katika mapigano na hata upeo wa kufikiria.
Leo alikaa ofisini kwake nyuma ya kiti kikubwa kinachozunguka kama tiara. Glass ya sinzano ilikuwa mkono wa kulia, sigara ikashikwa mkono wa kushoto. Kichwa kikaegemea kiti kikiwa katika tafakuri nzito. Aliwaza kuhusu mauaji ya kutisha.
Mara akakumbuka kitu.
Aliinama kwenye meza yake iliyojaa picha mbali mbali za maiti ya Bertha na Pamela. Akauvuta mtoto wa meza hiyo, kisha kuibuka juu na bahasha iliyohifadhi kitu Fulani. Vanessa aliiangalia bahasha iliyohifadhi nakala moja ya picha ile ya kivuli cheusi aliyojipiga Moses.
Wakati akiitazama picha ile, simu yake ya mezani ikapata uhai.
"Vanessa" ilikuwa ni sauti ya Inspekta Jafary Hiza
"habari yako Hiza?"
"salama, umepata majibu yeyote juu ya mpigaji wa picha hiyo?" Hiza aliuliza
"hapana na bado najiuliza kwanini mtu huyu ameamua kuuacha ushahidi huu kama sehemu ya kuendeleza mauaji yake" alisema Vanessa "sawa, pia majibu ya Postemoterm kuhusu ule mwili wa yule binti mwingine tuliyemkuta pale sebuleni"
Vanessa akauliza "yule aliyeibusu ardhi akielea juu ya mapovu?"
"Acha mzaha Vanessa, Majibu yametoka na yanasema kuwa, alikunywa sumu kali iliyomnyang'anya uhai wake"
Inspekta Hiza alihitimisha hivyo na kuikata simu mara baada ya kuagana. Vanessa akabaki akiwa hajaelewa jambo.
Alijidumbukiza kwenye tafakuri nyingine nzito, hata pombe iliyoanza kumkolea, ikimsaliti na kubaki mweupe. ‘ina maana alianza kufa yeye au Bertha? Ni nani alikuwa wa kwanza kuuwawa? Ni nani alikuwa mlengwa wa mauaji haya?' alijiuliza Vanessa akiishirikisha nafsi yake.
Alisimama akakizunguka chumba chake. Akaongeza kinywaji kwenye glass akakifuta chote. Alienda pale, akarudi kitini alipotaka kukaa wala hakukaa, alikuwa akiwaza tu. Ghafla alitabasamu, tabasamu lililochanua na kuufanya uso wake kuwa mzuri na kuonesha taswira ya umalaika. Hakika Vanessa alipendeza akicheka katika raha. Mashavu yake yakabonyea na kujenga dimples. Alimuita katibu muhtasi wake, alieyemchukulia kama mdogo wake. Yeye aliitwa Naima, mtoto wa kitanga. Binti aliyeiacha shule kutokana na shida za kuilima ardhi iliyonuna kustawisha mazao yake. Aliyetundikwa mimba kabla hajalimaliza darasa la saba na siku ya kujifungua mtoto wake alikataa kutoka akiwa hai. Alifia tumboni baada ya kukosa pumzi. Kipindi hicho Naima alikuwa na miaka kumi na nane.
Alikutana na Vanessa katika harakati zake za kutafuta maisha, alikuwa akiuza mchicha, sukuma wiki na mnafu. Ni nani ambaye hakutokwa na mate alipomtazama Naima? Ni nani ambaye, hakuacha kumsifia alipotazama kifua chake kilichotuna kiuchokozi na kufanyiza mfano wa matiti kifuani mwake? Alikuwa na kiuno kilichobeba mapaja manene na mguu uliofaa kuitwa wa bia. Huyu ndiye Naima mwenye asili ya kiarabu kutoka Tanga, hakutumia mkorogo wowote katika weupe wake.
"nimepata wazo" alimwambia Naima
"wazo gani?"
"kuhusu haya mauaji"
"mauaji ya hawa mabinti wawili waliouwawa huko kiitonyama?" Naima alimuuliza.
"ndiyo. Nimepigiwa simu na Hiza, amenieleza kuwa huyu mmoja" Vanessa alikuwa akiongea huku ameshika picha ya Pamela, akiwa ameyalalia mapovu. "ameuwawa kwa sumu. Hivyo inavyoonyesha, huyu alikuwa wa pili baada ya huyu wa kwanza aliyekatwa kichwa" macho yakamtoka pima Naima na kubaki mdomo wazi. Hakujuwa ni vipi Vanessa akili yake ilifanya kazi haraka hata kutambua hayo yote bila kumfahamu muuaji.
"Inawezekana huyu msichana hakuwa katika njama hizi, ila kihere here chake kilifanya hata akaupoteza uhai" alinyamaza akiyameza mate kwa raha huku akitabasamu kama kawaida yake
"inawezekana huyu aliingilia harakati za muuaji na kutaka kuitoa siri ya mauaji haya"
Naima kicheko kikamponyoka na kumwambia Vanessa "sielewi wewe ni binadamu wa aina gani, nimeanza kukuogopa"
Vannesa akaendelea kumwambia "na ndio maana hata pale eneo la tukio, hatukukuta simu. Inawezekana simu zingetuwezesha kupata ushahidi mwingi. Zilipofuatiliwa namba zilizokuwa zikiingia katika simu ya huyu Bertha.." akashika picha ya Bertha "hakuna historia yeyote. Hivyo inaonekana huyu muuaji kuna mchezo mchafu ameucheza na hawa watu wa mitandao kama sio hawa wajanja wa IT"
XXXXX
Raymond alipokuwa akikimbizwa hospitali, aliipata nafuu. Gari ilikuwa ikienda kasi sana akiwa mapajani mwa Bi Furahiya. Alijishika kichwa na kumtazama mkewe.
"niko wapi?"
Bi Furahiya alishituka kumuona mumewe ameamka, alifurahi sana na kumwambia dereva asimamishe gari. Wote waliokuwemo walishangaa na kumshukuru mungu kwa pamoja.
"mungu mkubwa!!!"
Raymond alitoa amri yakurudishwa nyumbani kwa kuwa alijiona hakuwa na tatizo la kumpeleka hospitali.
"sawa baba Bertha kama ni hivyo, lakini ilikuwa muhimu wewe kwenda kufanyiwa check up.."
"Nimeshasema ulikuwa ni mshituko wa kawaida" Raymond akafoka.
Raymond alikumbuka kila kitu kilichotokea na kuwahadithia kila kitu. Aliwahadithia Bi Furahiya na kaka yake Nyato Chilambo, kuhusu ujio wa lile boksi na alichokiona ndani yake. Boksi lililonakshiwa, lililomfanya apoteze fahamu. Kwa kuwa Bi Furahiya alifahamu yote yanayoendelea, alianza kupatwa na hisia mbaya. Alitetemekwa na mwili sanjari na mapigo ya moyo yaliyomuenda kasi zaidi. Alitamani kulia machozi hayakutoka. Alibaki kuwa mnyonge akisubiri litakalotokea.
Walipokuwa njiani, ndipo gari yao ilipata pancha na kuwalazimu wakae zaidi ya nusu saa eneo hilo la barabara iliyosuswa kupitiwa na magari mara kwa mara. Milango ilikuwa wazi, upepo ukiwapiga. Bi Furahiya alimpatia Raymond barua iliyoandikwa kwa damu. Barua hiyo iliandikwa na Moses. Barua yenye vitisho na masharti ya kuogofya.
Raymond aliisoma huku akitetemeka na moyo kumuenda kasi zaidi. Alitoa onyo. Yeyote aliyeyasikia hayo, asitoe habari hiyo kwa yeyote. Wote wakatii. Tairi likarekebishwa na kuwekwa la spare.
Safari ya kurudi nyumbani ikaendelea
XXXXX
ITAENDELEA..............