Hadithi: "Kivuli cheusi"

Hadithi: "Kivuli cheusi"

mizambwa

JF-Expert Member
Joined
Oct 8, 2008
Posts
4,421
Reaction score
1,792
HADITHI: KIVULI CHEUSI


SEHEMU YA KWANZA

Panga boi lilikuwa linazunguka taratibu, bila kuleta dalili yoyote ya ubaridi. Sifahamu kama ilikuwa ni udogo wa chumba, ama ni hali ya hewa ya jiji la Dar es salaam? Lakini hiyo haikumsumbua mlalaji huyu mgeni, katika kitongoji duni cha keko magurumbasi.

Kitongoji kilichobeba vibaka wa simu, makahaba na zile biashara haramu; kama uuzwaji wa bangi na pombe aina ya gongo, zilipatikana kwa wingi. Karani wa nyumba ya kulala wageni, yeye alipokea bakshishi ndogo kutoka kwake. Jumamosi yake ikaelekea kuisha vizuri jioni ile ya saa kumi na mbili.

Mgeni huyo aliyehifadhiwa ndani ya kofia kuukuu, alitoa masharti ya kutomuelekeza mgeni yeyote chumbani kwake. Alidai kuwa, hakuna anayemfahamu; hivyo hakuna atakayekuja kumtafuta. Hiyo haikuwa tatizo, kuitikia kwa kichwa; haraka haraka tabasamu jepesi la kiushawishi likipita juu ya papi zake. Elfu arobaini alizisunda kibindoni. Nyongeza mara nane ya bei ya kawaida. Binafsi aliiona bahati ya ngekewa, iliyomdondokea zaidi ya nyota ya jaa. Akampatia ufunguo mgeni huyo asiyeeleweka. Macho yaliyo nyuma ya miwani mikubwa meusi na mwendo wake kama anayechechemea. Yeye aliuchukua ufunguo aliopewa na kuondoka.

Ufunguo wenyewe, ulining’inizwa kwenye kibao kilichoandikwa namba ya chumba na kulifuata korido lililopanga vyumba kwa nambari zilizofuatana kimpangilio. Baada ya kuhesabu vyumba vyote, alisimama mbele ya chumba ambacho ufunguo wake alikuwa nao yeye. Aliufungua mlango na kujitoma ndani.

Hakutaka kuwasha taa, kwa sababu mwanga hafifu wa jua lililoashiria kudondokea magharibi, ulimtosha kukiona kitanda. Alilala vile vile kama alivyoingia. Kitanda kikamlaki kama kilivyowalaki wengine. Kunguni waliifurahia damu yake, viroboto nao wakamchoma choma. Hakujisumbua kukishusha Chandarua, hivyo mbu walicheza gombania goli katika sikio lake.

Mara akaamka ghafla. Hakuamka kwa sababu ya usumbufu wa chumba hicho duni. Ni mlio wa simu ulioita ghafla, saa tano ya usiku. Muda ulikuwa umeenda kasi sana. Ilikuwa ni namba ya Bertha, mpenzi wake. Alijiuliza ni nani atakuwa anaitumia namba hiyo. Baada ya kuipokea, aliifahamu sauti iliyoongea kwa sauti ya hamaniko. Aliongea kiutulivu na kumchota akili yule aliyewehuka upande wa pili. Baada ya maongezi aliyoyafanya katika simu hiyo iliyoingia punde, Alijinyanyua kitandani na kurudi maeneo ya kijitonyama sayansi nyuma ya kanisa. Eneo ambalo alikuwa akiishi mpenzi wake Bertha.

Baada ya kumaliza shughuli iliyompeleka. Saa saba ya usiku alirudi katika chumba chake, Keko magurumbasi. Alitumia taksi iliyompeleka. Ikamsubiri na kumrudisha mpaka Buguruni na yeye kuamua kuchukua taksi nyingine mpaka hapo. Sasa akawa anautafuta usingizi akiwa na bia nane kichwani. Bia alizozinywa katika ile klabu ya usiku maarufu kwa jina la kimboka by night. Hapo kulikuwako na madada poa waliouza miili yao kama ndafu ya shereheni.

Usingizi ukamkubali.

Licha ya usumbufu wa kunguni na mbu wa usiku alioupata, unadhani hata alijigusa? Lah! Aliyafurahia maficho yake. Japo usingizi ulimpaa jirani na alfajiri. Hali hiyo ilisababshwa na jinamizi la mawazo lililokuwa likimnyonga. Mwanga hafifu wa jua la alfajiri uliojipenyeza katika dirisha la chumba chake, ndio uliyomfanya aamke kivivu huku akitanguliza kitambi chake. Hatua zake zikiwa nzito kuubeba mwili mfupi kiasi uliobeba kifua kipana na kitambi cha bia na nyama choma; zote kwake zilikuwa kheri, mpaka alipokifikia kioo kilichopachikwa ukutani.

Akashituka.

Nadhani alianza hata kuisahau sura yake. Aliyasahau macho yaliyokosa nguvu ya kope za juu na kusababisha kuwa kama anayetaka kusinzia. Hata hivyo haikua sura ngeni aliyokuwa anatazamana nayo. Akakumbuka kuwa macho hayo yalikuwa ya kawaida. Macho yaliyomuwezesha kumpora Bertha kutoka kwa rafiki yake, Yesaya. Kidevu chake kikatawaliwa na msitu wa ndevu. Lakini hiyo haikuwa sababu ya kuisahau miaka ishirini na nne aliyoifukia kwa kula na kunywa kwa anasa. Aligeuza macho kukitazama kitanda alicholalia. Godoro jembamba kama ngozi ya tembo, likamdhihaki. Akajitusi mama yake mzazi kwa hasira. Kisha kicheko kisicho na ladha yoyote ya raha kikauharibu uso wake.

Akili yake ikaanza kutafakari yaliyotokea asubuhi ya siku ya jana, iliyomfanya apahame Osterbye na kuja kujificha huku vichochoroni, Keko Magurumbasi. Ghafla ulimi wake ukapata nguvu ya kuinua matamshi kadhaa “Bertha” aliita jina la msichana aliyefanya urafiki wake na Yesaya kuangamia.

Msichana waliyesoma wote chuo cha mlimani, kitivo cha sheria. Msichana aliyeiiba nafsi yake na kuiyumbisha yumbisha kama mawimbi ya bahari. Aliikumbuka siku ya kwanza Bertha alipowasili chuoni hapo akitokea Nyegezi Mwanza.

“Anha! Kumbe na wewe ni msukuma? Mimi ni mwenzio bwana, naitwa Moses” akalikumbuka Tabasamu lililoacha uchi kinywa chake na kuonesha meno yaliyojipanga na kufanya mpangilio sahihi katika kinywa cha Bertha. Kwa mara ya kwanza Moses alikiri kuushika mkono wa malaika ‘laivu’ waliposalimiana kwa kushikana mikono.

Ila Bertha sasa si Bertha tena. Ingefaa utangulize jina jipya, kabla hujaamua kumuita Bertha. Bertha kwa sasa aliitwa marehemu. Maiti yake yalifichwa na Moses ndani ya chumba chake mwenyewe Bertha. Chini ya kitanda na kuhifadhiwa kwa kuviringishwa ndani ya mkeka.

Hakika aliuwawa kinyama. Moses alifanya unyama zaidi ya mnyama. Unyama aliomfanyia binadamu mwenzake. Shingo yake Bertha haikutenganishwa na kiwili wili wakati alipochinjwa kama kuku na kisu kilichopoteza makali kwa kukatiwa nyanya na vitunguu; mpaka Moses alipohakikisha kumlisha masoksi machafu mdomoni ili Bertha asitoe sauti. Japo si Bertha pekee aliyekuwa maiti ndani ya nyumba yake. Rafiki yake Pamela pia, alipoteza roho yake kwa kutaka kutoa ushahidi polisi.

Yeye aliuwawa kikawaida kwa sumu aliyoinywa ndani ya maji ya baridi. Ilikuwa ni sumu kali sana. Nyongo ya mamba waliovuliwa kutoka katika ziwa Tanganyika. Ilisagwa na kuwa unga baada ya kukaushwa sana. Pamela aliipoteza roho yake kwa kiu ya maji ndani ya dakika kumi tu.

Baada ya kufanya yote hayo, Moses alikumbuka kufanya jambo. Alikaa uelekeo ambao mwanga wa taa ulimpiga na kutumia kamera yake aina ya Kodak, kukipiga kivuli chake mwenyewe. Baada ya kuridhika na picha aliyoipata, akatumia mashine ndogo ya kusafishia picha hiyo, picha ikatoka vile alivyotaka.

Akatabsamu kwa kebehi, kisha nyuma ya picha hiyo akaandika maandishi haya ‘KIVULI CHEUSI’ akaiweka picha hiyo pembeni ya kichwa cha Bertha, alichokiweka ndani ya friji.

ITAENDELEA...............
 
Hizi hadithi zenu ni nzuri, na tunashukuru kwa michango yenu ila inaudhi pale mnapotuacha hewani...ni kama kumwandaa mwenza kimapenzi kisha kumwacha! Kwani ni lazima kusimulia kwa namna ya mwendelezo?
 
Wakuu;

Naomba msiandamane. Kwa heshima na taadhima naongeza kipande kingine hapa. Labda mtanisamehe........
 
TULIPOISHIA SEHEMU YA KWANZA:

Rafiki yake Pamela pia, alipoteza roho yake kwa kutaka kutoa ushahidi polisi. Yeye aliuwawa kikawaida kwa sumu aliyoinywa ndani ya maji ya baridi. Ilikuwa ni sumu kali sana. Nyongo ya mamba waliovuliwa kutoka katika ziwa Tanganyika. Ilisagwa na kuwa unga baada ya kukaushwa sana. Pamela aliipoteza roho yake kwa kiu ya maji ndani ya dakika kumi tu. Baada ya kufanya yote hayo, Moses alikumbuka kufanya jambo. Alikaa uelekeo ambao mwanga wa taa ulimpiga na kutumia kamera yake aina ya Kodak, kukipiga kivuli chake mwenyewe. Baada ya kuridhika na picha aliyoipata, akatumia mashine ndogo ya kusafishia picha hiyo, picha ikatoka vile alivyotaka. Akatabsamu kwa kebehi, kisha nyuma ya picha hiyo akaandika maandishi haya ‘KIVULI CHEUSI' akaiweka picha hiyo pembeni ya kichwa cha Bertha, alichokiweka ndani ya friji.


ENDELEA..........

"si kawaida ya Bertha kuchelewa kufungua mlango" alijinong'oneza, baada ya kusonya muda mfupi uliopita. Pamela aligonga mlango muda mrefu, bila dalili yoyote ya kuja kufunguliwa. Alijishauri aondoke, lakini alikumbuka kuwa Bertha alimtumia ujumbe kuwa, anamualika katika sherehe. Sherehe yake ya kuvalishwa pete ya uchumba na mpenzi wake, Moses. Hivyo aliamua kujikaribisha, baada ya kuona kuwa; mlango ulikuwa wazi.

Mara tu alipoingia ndani, alipigwa na butwaa. Butwaa ya nini kimetokea kwa Bertha. Alilakiwa na damu nzito, iliyoanza kuganda pale sebuleni. Alihisi miguu ikikosa nguvu ya kukibeba kiwiliwili chake. Kizunguzungu kikampepesua, akastahimili kiukakamavu asidondoke.

Mapaja yakalowana kwa mkojo uliomchuruzika kiuwoga. Hakika hali ya sebule ilitisha. Macho yakavutwa na matone ya damu, yaliyodondoka mpaka kwenye friji. Alijikokota taratibu kwa mwendo wa kuvizia, mpaka kwenye friji hilo. Alipolifungua friji, hakuamini alichokiona. Kilikuwa ni kichwa cha rafiki yake, Bertha. Mdomoni akiwa na matambara machafu. Wakati huo ndipo, kile kitu alichokuwa akikizuia kwa muda mrefu, kikampiga mtama. Alianguka bila kupenda, Pamela akazimia.

Zilipita dakika nyingi, mpaka alipoanza kuhisi kichwa kikimuuma kupita kiasi. Hakujuwa amezimia kwa muda gani na pia alikwisha sahau, kilichomfanya ajikute kaibusu sakafu kama anayekisujudia kichwa cha rafiki yake mrembo, Bertha. Friji lilikuwa wazi hivyo kichwa cha Bertha kilikuwa juu kikionekana. Ulikuwa ni usiku mzito uliomuogopesha kuendelea kutazama hali ya nyumba ya rafiki yake. Alipiga simu katika kituo cha polisi kwa kutumia zile namba, zilizotolewa kwa ajili ya usalama wa raia. Kwa kuwa simu yake haikuwa na salio aliamua kutumia simu ya Bertha.

"habari yako?"

ilijibu sauti ya upande wa pili, baada ya kuita kwa muda mrefu bila kupokelewa. Pamela aliongea kwa pupa, bila mpangilio wa mtu wa pili kumuelewa vizuri.

"anti embu tulia!"

ilikoroma sauti ile, Pamela akatii. kisha sauti ya upande wa pili ilivuta tafakuri na ilipopata uhai, ikasema "unasema mauaji?"

kabla sauti ile haijamaliza, Pamela alidakia tena "rafiki yangu Bertha, wamemuua kinyama. Kichwa chake" sauti ile, ambayo Pamela aliifahamu vizuri, ikapata tena uhai. Pamela hakuweza kuigundua, kutokana na papara zake na kuchanganyikiwa.

"unasema mauaji yametokea hapo nyumbani kwa rafiki yako?"

Pamela akajibu kiutulivu huku akiwa analia "ndiyo afande" Pamela alichukuwa jukumu la kumuelekeza mtu aliyekuwa akiongea naye, bila kuulizwa.

"sawa usimueleze mtu yeyote mpaka tutakapofika hapo"

Pamela alipoitikia, sauti ile ilitoa onyo la mwisho "kumbuka usimwambie mtu yeyote mpaka tutakapofika hapo. Hata wazazi wake wala mtu wake yeyote wa karibu usimwambie, hiyo ni kutokana na usalama wako. Pia usiende popote" kisha alikata simu.

Pamela aliendelea kusubiri kwa dakika arobaini na tano zaidi. Muda wote hakuwasha taa wala kujigusa. Alitetemeka kiasi cha kuhisi joto kali, licha ya kiyoyozi kilichokuwa kikibadilisha hali ya hewa kwa fujo, kikifanya kazi yake kiufasaha. Alikwisha jikojolea mara mbili kwenye kochi alilokalia akakauka. Choo kilikuwa ni cha ndani, vipi aingie akutane na muuaji kajibanza?

Alijiuliza.

Akiwa katika lindi la mawazo, ndipo aliposikia kitasa kikishikwa na mlango kufunguliwa. Kutokana na giza totoro, hakuweza kumuona aliyeingia. Mapigo ya moyo yalimuenda mbio sana, jasho likamtiririka kwa wingi. Kivuli kile cheusi, kilichojitoma ndani ya nyumba bila hodi, kikawasha taa. Macho ya Pamela yakamtoka pima baada ya kumuona aliyeingia.

Alikuwa ni Moses.

"shemeji" kilio kikaanza upya "wamemuua rafiki yangu, amewakosea nini jamani"
Moses alimkumbatia Pamela na kumliwaza kinafki. Walikaa kwenye kochi, huku Pamela akimuhadithia Moses yote tangu Bertha alipomtumia ujumbe uliomfanya yeye kuja hapo.

"aliniambia upo naye, leo ulikuwa ukimvisha pete ya chumba" Pamela alimshitua Moses. Moses akamtusi Bertha kimoyomoyo. Pamela akaendelea kumueleza mpaka alipopoteza fahamu baada ya kukiona kichwa cha Bertha ndani ya friji. Moses hakuoneshwa kushitushwa na hadithi hizo zote zilizosindikizwa na kilio. Alinyanyuka na kuelekea jikoni. Pamela alikuwa huru kwa kuwa aliaamini sasa ana mtu wa kumlinda. Lakini laiti angejua, asingethubutu kuiuza roho yake kwa mkopo. Alimwambia Moses

"nimewataarifu polisi, lakini naona wanachelewa"

sauti ilimfikia Moses jikoni, naye akajibu "umefanya vizuri"

Moses alikuja na bilauri ya maji ya baridi yaliyotoka kwenye friji ya jikoni. "ahsante shemeji umejuaje nilikuwa na kiu? Yaani sijatoka kwenda popote kwa uoga" aliyafakamia maji hayo, bila kujua hila za Moses. Moses alimtazama huku akimcheka kimoyo moyo. Alijiambia

"kufa Malaya wewe, kamsalimie mbwa mwenzio" dakika tano zilikuwa nyingi. Tumbo lilianza kumsokota Pamela. Pamela alilia kwa uchungu huku akimtazama Moses aliyekuwa akitabasamu. Pamela Akagundua kuwa maji aliyoyanywa yaliwekwa sumu. Alijuwa kuwa, Moses alipanga kummaliza ili ushahidi upotee. Akiwa katika kuugulia, alimwambia Moses

"kwa nini unatuua Moses? Kumbe ni wewe ndiye uliyepokea simu yangu? Kwanini Moses unafanya hivi? Tumekukosea nini?"

Moses alicheka kifedhuli, akamwambia neno moja ambalo liliisindikiza roho ya Pamela katika umauti "Pole Pamela, ni ujinga wako ndiyo umekuponza. haukuwa katika njama hizi, lakini ni upuuzi wako. Nililazimika kuidaiveti namba ya Bertha ila nikupate muda utakaokuja. Sikujuwa kama utaitumia simu yake kuwapigia polisi, ila nilifahamu utanipigia kuniuliza nilipo na kunipa taarifa ya msiba. Lakni harakati hizi haziishii hapa naapa kukiangamiza kizazi chake chote, na umsalimie kuzimu uendako" si maneno yote ambayo Pamela aliyasikia, kwa sababu tayari alikwisha funga macho na roho kuiacha mwili.

Moses alicheka kwa kejeli baada ya kuzikusanya simu zote mbili, simu ya Pamela na Bertha kisha kutokomea nazo baada ya kuacha picha yenye ujumbe wa kivuli cheusi nyuma ya picha aliyojipiga mwenyewe.
*****

ITAENDELEA.................
 
HADITHI: KIVULI CHEUSI


SEHEMU YA TATU


TULIPOISHIA

"Pole Pamela, ni ujinga wako ndiyo umekuponza. haukuwa katika njama hizi, lakini ni upuuzi wako. Nililazimika kuidaiveti namba ya Bertha ila nimpate ninayemkusudia. Sikujuwa kama wewe ungekuwa wa kwanza kukiona kifo cha Bertha na harakati hizi haziishii hapa naapa kukiangamiza kizazi chake chote, na umsalimie kuzimu uendako" si maneno yote ambayo Pamela aliyasikia, kwa sababu tayari alikwisha funga macho na roho kuiacha mwili. Moses alicheka kwa kejeli baada ya kuzikusanya simu zote mbili, simu ya Pamela na Bertha kisha kutokomea nazo baada ya kuacha picha ile yenye ujumbe wa kivul
i cheusi nyuma ya picha aliyojipiga mwenyewe.

ENDELEA NAYO..............


Bertha alipendelea sana kunywa supu wakati ambao anaamka, hakuna mtu ambaye alikuwa halifahamu hilo. Ndio maana aliweka oda ya kutengenezewa supu ya ulimi na chapati mbili, katika pub iliyo jirani na nyumbanin kwake. Hicho ndio kilikuwa kifungua kinywa chake mara kwa mara. Ilikuwa ni baada ya oda aliyoiacha jana alipoitembelea Pub hiyo, akiwa na Moses. Pub inayojulikana kama GQ.

Wapishi na wahudumu wa pub hiyo, walikwishazoea kumpelekea mpaka nyumbani kwake. Walimthamini kutokana na kuwa mteja wao mkubwa na kumfanya wa muhimu kwao. Leo ikawa zamu ya Eva kupeleka supu.

"mwambie atusamehe sana, tulikosa ndimu" mpishi mkuu wa jiko, alisikika kwa mbali. Eva alijibu huku akiendelea kutembea

"huo ni uzembe jamani, kila inapofika zamu yangu hamkamilishi breakfast yake, Mimi namuogopa jamani"

Eva akazipita nyumba tatu, ndipo akaifikia ya Bertha. Hakushangaa kukuta geti lipo wazi, lakini alistaajabu kukuta mlango ukimzomea na nzi wengi wakimlaki kwa shangwe. Alibisha hodi mara tatu kana kwamba aliukuta mlango ulikuwa umefungwa. Ukimya ukamfanya kujikaribisha ndani huku akiwa ananyata akiendelea kuita

"Dada Bertha nimekuletea…." Mdomo wake ukakosa stamina na kuropoka neno "mamaaaaa!!!!!" baada ya kuangusha sahani iliyobeba bakuli la supu na chapati. Hakuingia zaidi ndani kwa kile alichokiona. Akatoka mbio bila kutazama alipokuwa akienda.

Alikwisha jikwaa mara tatu na kupiga yowe, alipokuwa akikimbilia getini huku akitazama nyuma GQ alipaona mbali. Hakika Eva alipendeza kuwa mwanariadha, Kisigino kilibaki sentimita chache kigonge kisogo kwa kukimbia.

Alienda mpaka kwa mpishi mkuu bila kujali hasara aliyosababisha ya kulikwapua sinia lililojaa maini na chapati za mteja.

"Mungu wangu…. "muhudumu mwenzie alibwatuka, baada ya kushindwa kulizuia sinia lisianguke akahamanika kwa fadhaha "..Eva!!". Aliye angusha sinia alimfuata Eva mpaka jikoni akipokimbilia.
"Amekufa?" mzee huyo wa jikoni alibwatuka kwa butwaa. Hata Yule aliyekuwa akimjia kwa jazba naye aliuliza kwa kuhamanika "Bertha amekufa?" Eva alionekana kuchanganyikiwa kupitiliza
"Mimi jamani sifahamu ila nyumba yake haitamaniki, Kila sehemu damu na nilimuona amejilaza chini niliogopa kutazama kama ameshakufa au lah!"

Eva hakujuwa kuwa Yule aliyemuona ndani ya nyumba ya Bertha, hakuwa Bertha bali ni Pamela. Mpishi mkuu wa jikoni alimuamuru Bosco yule mhudumu wa vinywaji, akaangalie nini kimemkuta Bertha. Kama kuna msaada wowote unahitajika, inabidi waitaharifu polisi.

"sawa babu bonge"

Bosco alijibu huku akitoka yeye na Eva mpaka nyumbani kwa Bertha. Bosco hakuamini alichokikuta kwa Bertha. Ilikuwa ni harufu ya uvundo wa damu, iliyoanza kunuka. Aliziba pua yake na kuingia ndani. Alimuacha Eva nje, akitetemeka kwa uoga.

Mwili wa Pamela uliojilaza sakafuni haukuwa na damu zaidi ya mapovu yaliyomtoka, kutoka mdomoni. Bosco hakuitaji ushaidi wa daktari, kumuhakikishia kuwa aliugusa mwili tu, roho haikuwepo tena ndani yake
"Huyu siyo Bertha" Bosco akasema kwa nguvu.

"Sasa atakuwa nani bwana?" Eva alisema huku akichezesha chezesha miguu yake kwa uoga.

"Sijuhi ni nani? Na hizi damu ni za nani? Maana huu mwili hauna jeraha lolote" alisema Bosco. Jambo lililomvuta Eva kuingia ndani na kuangalia alichokuwa akikisema Bosco. Bosco yeye alikwisha ona damu zilizochuruzika mpaka kwenye friji, hivyo wakati Eva anaingia na yeye alikuwa amekwisha fungua mlango wa friji na kukiona kichwa cha Bertha kilichong'ata matambara machafu.

Damu zilizoanza kuganda shingoni mwake, miguu ikamkosea adabu Bosco, akadondoka kama mtoto aliyeanza kujifunza kutembea. Ilikuwa ni hali inayotisha. Eva alishitushwa na kuzimia huko kwa Bosco, akavutwa kukitazama kilichomfanya Bosco adondoke. Alipoona! yeye akatapika, alitapika sana mpaka akaitapika nyongo. Mkojo ulimtoka na machozi kumchuruzika asijue ni hatua ipi ya kuichukuwa. "Berthaaa" alipiga mwereka alipotaka kukimbia, kumbe alimkanyaga Bosco aliyedondoka. Alijiinua na kukimbia hovyo kurudi GQ.


ITAENDELEA....................
 
HADITHI: KIVULI CHEUSI


SEHEMU YA NNE

TULIPOISHIA......

Jambo lililomvuta Eva kuingia ndani na kuangalia alichokuwa akikisema Bosco. Bosco yeye alikwisha ona damu zilizochuruzika mpaka kwenye friji, hivyo wakati Eva anaingia na yeye alikuwa amekwisha fungua mlango wa friji na kukiona kichwa cha Bertha, kilichong'ata matambara machafu. Miguu ikamkosea adabu, Bosco akadondoka kama mtoto aliyeanza kujifunza kutembea. Ilikuwa ni hali inayotisha. Eva alishitushwa na kuzimia huko kwa Bosco, akavutwa kukitazama kilichomfanya Bosco adondoke. Yeye alitapika , alitapika sana mpaka akaitapika nyongo. Mkojo ulimtoka na machozi kumchuruzika asijue ni hatua ipi ya kuichukuwa. "Berthaaa" alipiga mwereka alipotaka kukimbia, kumbe alimkanyaga Bosco aliyedondoka. Alijiinua na kukimbia hovyo kurudi GQ.

ENDELEA.................


Yeye Moses aliirudia taswira yake ile ile aliyokuja nayo jana. Kofia ya kizee vijana wakaiita pama, miwani mikubwa iliyobebwa na mashavu yake pamoja na jino moja la dhahabu. Taswira iliyomfanya aonekane mzee kwa kuvaa midabwada na mandevu ya bandia yaliyochafua kidevu chake. Alipanga hila za kutoka katika Guest hiyo ya vichochoroni, asigundulike na mtu wapi aelekeako.

Ni Yule kijana mroho wa mapokezi ndiye aliufahamu ugeni wa Mzee huyo aliyejiandikisha katika kitabu cha wageni kwa jina la Mussoline. Mzee aliyenuka umasikini lakini mwenye pesa nyingi. Alijisemea hivyo Yule kijana. Moses alipopita pale mapokezi akiwa katika mwendo wake ule ule wa kuchechemea, Yule kijana alimsimamisha. "mzee umedondosha kitambulisho chako" Moses alikuwa ameshampita pale alipokuwa anafagia. Yule kijana alikuwa ameshakisoma kile kitambulisho na kuitazama picha ya muhusika.

Hakuwa "mzee mussoline" alijisemea yeye. Moses alimshukuru na kumuondoa wasiwasi "nashukuru sana kijana wangu. Hiki ni kitambulisho muhimu sana" Moses hakujuwa Yule kijana alikwisha kisoma. Alimuuliza "sasa babu, huyo pichani ni nani?" Moses alishituka lakini hakumuonesha wasiwasi. Alimjibu kwa hekima, baada ya kikohozi kifupi kumpitia "mwanangu, mwanangu mpendwa na wa pekee Fredy.

Amekufa katika kifo cha kusikitisha sana. Ndio maana nimekueleza ni kitambulisho cha muhimu kwa kuwa ni ukumbusho wa pekee unaonifanya nihisi ninaishi naye mpaka sasa" Moses aliongeza hila zake kwa kujifanya akivuta kamasi na kuyafuta machozi ya uongo na kweli kwa kitambaa. Alimuuliza "kijana, unaitwa nani tena?" yeye akajibu "pole sana mzee, mimi naitwa Omary au alimarufu kama Kibanga" Moses na Omary wakaagana kuwa wangeonana jioni wazungumze megi.

Safari ya Moses ilikuwa ni kwenda katika ofisi za baba yake Bertha, akiwa katika Taswira ile ile. Kabla ya kwenda aliingia katika kibanda kimoja cha TTCL na kutumbukiza sarafu kadhaa na kuzungusha nambari za Mzee Raymond baba yake Bertha. Alizifahamu. "Raymond Chilambo nikusaidie nini?" sauti katika spika ilikoroma baada ya kuita kidogo tu. Moses alicheka kimoyo moyo baada ya kusikia sauti iliyopwaya kutoka upande wa Raymond. Yeye alijibu "hiki ni kivuli cheusi, ninakuja kuichukuwa roho yako" kisha alikata simu

Bosco ndiye alipewa jukumu la kuitaarifu polisi. Alipiga simu ya mkuu wa kituo cha Osterbye, inspekta Nyaluto. "tupo njiani, ahsante kwa taarifa"

Nyaluto hakuwa mwenye maneno mengi. Aliikata simu baada ya kuelekezwa eneo lilipotokea mauaji hayo. Kifo cha Bertha kikawa gumzo katika maeneo yote ya Kijitonyama. Hata wasiomjua walipozisikia habari za kifo cha kinyama alichofanyiwa mrembo huyo, wakinamama kanga ziliwavuka kuelekea alipokuwa akiishi Bertha. Huyu akasikitika, Yule vinyweleo vikamsimama wengine walishika midomo yao. Kuna walioshindwa kuyazuia machozi yasiwaadhiri, kwa huruma waliyolaaniwa nayo wanawake, hata yakawadondoka.

Ni nani ambaye asingeshituka kusikia "kichwa chake kimekutwa ndani ya friji, kikiwa kimetafuna soksi?" ilikuwa ni habari ya kusikitisha, iliyowavuta pia na waandishi wa habari. Waandishi wakataka kufahamu kuhusu maiti nyingine iliyopatikana ndani ya nyumba hiyo. Maiti iliyoonekana kuwa na kichwa chake, isiyo na jeraha lolote lililovuja damu. Kikawa kitendawili kwao Betha ni yupi na huyu ni nani?

Hakuna ambaye aliifahamu familia ya Bertha, hivyo hakuna ambaye alitoa wazo la kumtaarifu ndugu au jamaa yeyote wa karibu na Bertha. Jeshi la polisi lilikuwa eneo la tukio, kupima hiki na kukiokota kile. Mwili wa Pamela uliwekwa ndani ya mfuko maalumu baada ya kupigwa picha kadhaa. Inspekta Nyaluto alikuwa karibu na Bosco kumuuliza ile na lile
"sasa huyu ndiye Bertha?"

Bosco akajibu "hapana, ila kichwa mlichokikuta kwenye friji ndiyo cha Bertha"

"kiwiliwili cha Bertha kiko wapi sasa?"

Ukimya wa Bosco ukamsuta Inspekta Nyaluto, akajuwa kuwa, Bosco hakuwa akijuwa lolote. Punde askari mmoja alisikia akipiga yowe kutokea katika chumba cha Bertha baada ya Harufu iliyomvuta kudadisi kulikuwa na nini dani ya mkeka uliofungwa kwa nyaya za umeme. Mkeka huo aliutoa kutoka chini ya uvungu.

"kiwiliwili chake nimekitoa kutoka kutoka chini ya uvungu" alisikika akisema hivyo.

Askari walifanya kazi hiyo pamoja na mpelelezi aliyeaminika sana katika kutatua matatizo mbalimbali yaliyowashinda makamanda hata wale wa jeshi. Yeye alijulikana kama Vanessa. Ni nani aliyesahau kuwa huyu ndiye mwanamke shujaa mwenye hekima, hata akakitoa kitanzi katika shingo ya Ramon? Ramon aliyezua gumzo katika jiji la Dar es salaam baada ya kuonekana kuwa amemuuwa mpenzi wake.

Beatrice mtoto wa kigogo kutoka umoja wa mataifa, kama kesi hii ilivyo? Ditektivu Jafari Hiza alimnong'oneza Vanessa "hizi kesi za mpenzi kumuuwa mpenzi zinaelekea kukuandama sana Vanessa" kama kawaida yake, tabasamu likamponyoka. Muda mwingine unaweza usielewe alitabasamu nini.


Vanessa alimtafuta mtu wa kwanza kugundua mauaji, ndani ya nyumba ya Bertha. Haikumchukua muda mrefu, kuletewa Eva aliyekuwa hajiwezi kwa kulia. Alimtazama kwa tuo kabla ya kumpatia leso ya kujifuta machozi.

"naitwa Vanessa" alijitambulisha

"naitwa Eva" kilio kikapamba moto

"naomba unyamaze nina maswali machache ninataa kukuuliza"

"lakini afande mimi sijaua" Maneno hayo ya kiudhaifu yakamponyoka Eva. Vanessa alicheka kwa huruma na kumwambia "usiogope, mimi sio afande ndio maana sijajitambulisha kama Afande Vanessa. Naomba uwe huru kuzungumza na mimi" alimpa moyo kisha aliendelea "naomba nifahamu wewe unamfahamu vipi Bertha"

jina lake alikwisha ambiwa na wakazi wawili, watatu wambea walioponyokwa na maneno wasiyoulizwa na mtu ambaye hawamfahamu. Ili mradi ilikuwa ni siku ya majonzi, kila mtu alizungumza lake analolijua kumuhusu Bertha. ‘alikuwa mpole, masikini dada wa watu' alimsikia mmoja akisema .

huyu naye "aliongea na kumchangamkia kila mtu" wa mwisho kabla hajamuita Eva ndiye akalitaja jina la Bertha "halafu Bertha ni mgeni, hapa hana hata wiki tatu. Yule jamaa yake aliyekuwa naye jana hapo GQ simuoni hapa? ina maana hana taarifa" pia habari hiyo ilimsukuma haswa afanye mahojiano na Eva.

*****

ITAENDELEA.....
 
Aisee, ni nzuri though inatisha, nataka kumjua moses na kwanini ameamua kufanya haya mauaji na yuko wapi mchumba wa beatha Yesaya mizambwa


Haya majibu yake yote yatapatikana tukikaribia mwisho wa hadithi
 
Last edited by a moderator:
Back
Top Bottom