Hadithi: Jini Mweusi

Hadithi: Jini Mweusi

SEHEMU YA 61

Hali ya sintofahamu inazuka jijini Dar es Salaam, machangudoa wengi wanaanza kuuawa katika mazingira ya kutatanisha. Hakuna anayemjua muuaji, kila changudoa anayenunuliwa na mwanaume aliyekuwa kwenye gari aina ya Volkswagen nyeusi, anauawa kikatili.

Kila mmoja anaogopa, machangudoa wengine wanaacha kujiuza, wanajifungia vyumbani mwao, ila kwa wengine ambao hawakuweza kuishi bila kufanya biashara hiyo, wanakwenda huko, bado wengine wanaendelea kuuawa.

Aliyekuwa akiwaua wanawake hao ni Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam, Dickson. Aliwaua kwa siri lakini baada ya kipindi fulani kupita, akagundulika na hivyo kuanza kutafutwa.

Kwa sasa amehamishia fedha zake zote katika akaunti yake ya siri, hakuna aliyejua fedha zimehamishwaje kwani aliyefanya kazi hiyo ni mtaalamu sana katika mambo ya kompyuta, anachokifanya ni kuanza safari ya kuelekea Mwanza.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

“Hivi kuna sehemu ya kupumzika humu?” aliuliza Dickson huku akimwangalia dereva aliyekuwa amempakiza.

“Unamaanisha sehemu ya kulala?”

“Ndiyo!”

“Ingia hapo nyuma, wewe tulia, pumzika kwanza, nahisi umechoka na una safari ndefu sana,” alisema dereva huku akimuonesha Dickson sehemu ambayo alitakiwa kuingia na kutulia.

“Nasikia kichwa kinauma sana, nataka nilale, nahisi kufa-kufa..” alisema Dickson huku akiingia sehemu aliyokuwa ameelekezwa ambayo ilikuwa na godoro, akatulia huko.

Hakuwa na amani hata kidogo, kijasho chembamba kilikuwa kikimtoka, mwili ulitetemeka mno kwani alihisi siku hiyo, tena katika usiku huohuo ndiyo ilikuwa siku ya kukamatwa kwake.

Moyo wake ulisikitika mno, alipania kuondoka jijini Dar es Salaam na kuingia jijini Mwanza ambapo huko angechukua boti ambayo ingempeleka mpaka katika Kisiwa cha Ukerewe ambacho ndicho angekitumia katika kujificha kwake.

Hata kabla theluthi ya safari haijakamilika, tayari polisi walikuwa njiani, walilisimamisha gari alilopanda ambapo aliamini kama kweli polisi hao wangelipekua, basi ingekuwa rahisi sana kukamatwa.

“Unakwenda wapi babu?” aliuliza polisi aliyelisimamisha gari lile kwa kulitaka lisogee pembeni kabisa, mkononi alikuwa na bunduki yake.

“Nakwenda Singida mkuu!”

“Kufanya nini?”

“Kuna mizigo napeleka, si unaona huko nyuma…” alijibu mzee huyo.

“Upo na nani?” aliuliza polisi huyo. Dickson alilisikia swali hilo, alitamani mzee huyo ajibu kwamba alikuwa peke yake.

“Nipo na mwenzangu…”

“Yupo wapi?”

“Huyu huku amelala!” alijibu mzee huyo.

“Hebu teremka kwanza…” alisema polisi yule na mzee huyo kufanya hivyo.

Kila polisi mahali hapo alikuwa bize akiyakagua magari yaliyokuwa yakiendelea kupita mahali hapo. Hakukuwa na nafasi ya polisi wawili kulipekua gari moja kwani magari yalionekana kuwa mengi hata zaidi ya wao wenyewe.

Alichokifanya dereva yule ni kuteremka, polisi yule akapanda na kuingia ndani. Moja kwa moja macho yake yakatua kwa Dickson ambaye alikuwa amejifunika shuka pasipo kuacha sehemu yoyote ya mwili wake kuonekana.

Polisi huyo akamsogelea pale alipokuwa na kumgusa kwa bunduki yake, alitaka aamke na kumwangalia ili aone kama alikuwa mtu waliyekuwa wakimtafuta au la.

Dickson alitulia, alijifanya kukoroma na wakati alikuwa macho kabisa, tena alimsikia polisi huyo tangu akiwa nje ya gari akiongea na yule mzee. Kujitetea lilikuwa ni jukumu lake, hakukuwa na kitu ambacho kingemfanya kuinusuru nafsi yake tofauti na kufanya kitu kingine ambacho kingemfanya kuwa huru.

“Wewe bwana funua shuka nikuone…” alisema polisi yule huku akiendelea kumgusa Dickson na bunduki yake ile.

“Wewe bwana unanisikia au hunisikii? Funua shuka nikuone…” alisema polisi yule kwa sauti yenye msisitizo, Dickson akazidi kuogopa, mapigo ya moyo wake yakazidi kudunda kwa kasi, alichanganyikiwa, hakujua nini cha kufanya, hakujua ni kwa namna gani angeweza kujiokoa kutoka kwa polisi huyo.

“Funua shuka….” alisema polisi yule wakati Dickson alipoanza kujigeuzageuza katika godoro lile.

Wazo lililomjia Dickson ni kupambana tu, hakuwa na kitu kingine alichotakiwa kufanya zaidi ya kuonesha umwamba wake na mtu wa kwanza kabisa kupambana naye alikuwa huyo polisi aliyeona kama amejipendekeza kuingia ndani ya gari hilo.

Wakati anaguswa na bunduki ile, akafunua shuka lake na kumwangalia polisi yule ambaye hakuwa ameuona sura vizuri hali iliyomfanya kutaka kuwasha tochi yake ili amtazame usoni, hata kabla hajawasha tochi hiyo, akashtukia akivutwa chini, akazibwa mdomo na kupewa kabali moja matata.

Polisi yule akabaki akikukuruka ili ajinasue kutoka katika mkono wa Dickson, alijitahidi kwenda huku na kule lakini kabali ile iliendelea kama kawaida. Alitamani kupiga kelele lakini kitendo cha kuzibwa mdomo wake ikilimfanya kushindwa kabisa kufanya hivyo.

Baada ya sekunde thelathini tu, polisi yule akaanza kulegea, mapovu yalianza kumtoka mdomoni, sekunde chache zilizofuata, mwili ukalegea na kutulia kimya.

“Kwisha habari yake…” alijisemea huku akiuchukua mwili wa polisi yule na kuuweka pembeni kwa kuuficha kisha akaenda katika kiti cha mbele na kumuita dereva aliyekuwa amesimama nje ya gari lile.

“Tuondoke…” alimwambia.

“Kivipi? Polisi yupo wapi?”

“Ametokea mlango huu mwingine, kwani hakukwambia?”

“Hapana! Ila ilitakiwa atokee mlango huu! Hawa polisi wa Tanzania bwana, huwa hawaeleweki,” alisema dereva kwa mashaka huku akipanda ndani ya gari tayari kwa kuanza safari.

Dereva hakujua kilichoendelea, alidanganywa kidogo sana na aliukubali uongo huo hivyo kuwasha gari kwa lengo la kuondoka mahali hapo. Polisi wengine walionekana kuwa bize na hawakuwa na habari kabisa kama mwenzao aliuawa ndani ya gari hilo.

Kwa kuwa walimuona wakati anaingia, hata gari hilo lilipoanza kuondoka, hawakulisimamisha, wakaliruhusu lipite pasipo kugundua kwamba hata yule mtu aliyewafanya kuwa mahali hapo usiku huo, alikuwa ndani ya gari waliloliruhusu kuendelea na safari.

Safari iliendelea ndani ya gari kulikuwa kimya, muda wote dereva alikuwa akijiuliza maswali mengi kichwani mwake, kitu ambacho kilimtatiza ni kwa namna gani polisi yule aliteremka ndani ya gari kwa kutumia mlango tofauti na ule aliopitia? Kila alichojiuliza alikosa jibu kabisa.

“Tukiwa tunakaribia kufika Mlandizi niambie…” alisema Dickson.

“Kuna ndugu yangu nataka nimshtue ili twende wote kijijini…” alijibu.

“Sawa! Sasa ungemwambia akae barabarani kabisa…”

“Sawa!”

Baada ya dakika kadhaa, tayari walikuwa wakikaribia Mlandizi ambapo Dickson alimwambia dereva asimamishe gari kwa ajili ya kumwangalia huyo mtu aliyemuita ndugu yake.

“Mbona porini?”

“Ndipo hapahapa aliposema…subiri nishuke, nikamfuate, kama ikichukua zaidi ya dakika kumi, wewe endelea na safari yako,” alisema Dickson.

“Sawa…”

Alichokifanya ni kuteremka na kuanza kuondoka mahali hapo. Kwenda Mwanza kwa kutumia usafiri wa gari hakukuwa na amani kabisa, roho mkononi na muda wote ule alihisi angekamatwa, alichokiona, kama kwenda Mwanza basi aende kwa miguu, pori kwa pori, msitu kwa msitu mpaka kufika huko. Hata ile maiti ndani ya gari, akaitelekeza.


Je, nini kitatokea mara yule dereva atakapogundua ndani ya gari nyuma ya siti kuna mwili wa askari polisi?
 
SEHEMU YA 62

Hali ya sintofahamu inazuka jijini Dar es Salaam, machangudoa wengi wanaanza kuuawa katika mazingira ya kutatanisha. Hakuna anayemjua muuaji, kila changudoa anayenunuliwa na mwanaume aliyekuwa kwenye gari aina ya Volkswagen nyeusi, anauawa kikatili.

Kila mmoja anaogopa, machangudoa wengine wanaacha kujiuza, wanajifungia vyumbani mwao, ila kwa wengine ambao hawakuweza kuishi bila kufanya biashara hiyo, wanakwenda huko, bado wengine wanaendelea kuuawa.

Aliyekuwa akiua wanawake hao ni Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam, Dickson. Aliwaua kwa siri lakini baada ya kipindi fulani kupita, akagundulika na hivyo kuanza kutafutwa.

Kwa sasa amehamishia fedha zake zote katika akaunti yake ya siri, hakuna aliyejua fedha zimehamishwaje kwani aliyefanya kazi hiyo ni mtaalam sana katika mambo ya kompyuta, anachokifanya ni kuanza safari ya kuelekea Mwanza.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Mzee yule hakutaka kuondoka, bado akili yake ilimwambia kwamba mtu yule aliyemsaidia ni kweli alifiwa na hivyo kuondoka mahali hapo na kumuacha na wakati alikuwa na tatizo, halikuwa jambo la busara.

Aliambiwa kwamba kama zingepita dakika kumi na kuona kimya, basi aondoke zake lakini hakufanya hivyo, alikaa mpaka dakika arobaini, Dickson hakutokea hali iliyomfanya ahisi kulikuwa na tatizo.

“Mmh! Isije ikawa amepata tatizo!” alijisemea.

Alichokifanya ni kuvuta subira. Sekunde ziliendelea kwenda mbele, dakika zikakatika mpaka kutimia saa moja, bado Dickson hakutokea. Hakutaka kusubiri zaidi, kama kujitoa, alijitoa sana, alichokifanya ni kuwasha gari lake na kuanza kuondoka huku moyo wake ukiwa na huruma nyingi juu ya Dickson.

“Atanisamehe tu, nimesubiri sana,” alijisemea huku akipiga gia na safari yake kuendelea.

Safari iliendelea, mzee yule hakujua kama ndani ya gari lake kulikuwa na maiti ya polisi, hakuwa na wasiwasi kabisa, kitu alichofikiria ni kufika mkoani Dodoma salama na kufanya mambo yake.

Baada ya dakika kadhaa, akawa anaingia maeneo ya Chalinze, mbele yake aliona magari mengi yakiwa yamepaki pembeni huku mbele kabisa kukiwa na magari ya polisi waliokuwa wakifanya msako wa kumtafuta Dickson ambaye mpaka wakati huo hawakujua alikuwa wapi, ila pamoja na hayo, walijua kwamba inawezekana angekimbilia nje ya Jiji la Dar es Salaam.

Alichokifanya mzee yule naye ni kupanga foleni huku polisi wakiendelea na kazi yao kama kawaida. Foleni ilisogea na baada ya dakika thelathini, gari lake likawa mbele kabisa.

“Naomba uteremke mzee,” alisema polisi mmoja huku akimmulika kwa tochi usoni, mzee akateremka.

“Unakwenda wapi?” aliuliza polisi mmoja.

“Dodoma…”

“Kufanya nini?”

“Napeleka mzigo mkuu!”

“Sawa! Huogopi kutembea usiku sana?”

“Hapana! Nimeshazoea, namshukuru Mungu kwa miaka ishirini niliyofanya kazi hii, sijawahi kukutwa na balaa,” alijibu mzee huyo huku akionesha tabasamu pana.

“Upo na nani ndani ya gari?”

“Peke yangu!”

“Una uhakika?”

“Asilimia mia moja!”

“Basi sawa, naomba tufanye upekuzi kidogo, kuna mtu tunamtafuta,” alisema polisi huyo.

“Sawa! Hakuna tatizo.”

Hakuwa na wasiwasi hata kidogo, alikuwa na uhakika kwamba ndani ya gari hakukuwa na mtu yeyote yule zaidi yake, hakujua kuhusu maiti ile ya polisi iliyokuwemo na hata yule mtu aliyempa lifti alionekana kuwa mtu mzuri kitu ambacho hakikuwa sahihi kabisa.

Polisi mmoja mwenye tochi akaanza kuimulika mizigo ile. Zilikuwa mbao nyingi ambapo polisi hao wala hawakuwa na wasiwasi kwani kama kungekuwa na mtu aliyejificha, asingeweza kukaa kwenye mbao.

Walipoona kwamba hakukuwa na mtu yeyote katika mbao zile ndipo polisi mmoja akaufungua mlango na kuingia ndani. Muda wote mzee yule alikuwa akiwaangalia polisi wale, hakuwa na hofu hata kidogo ndiyo kwanza alisogea pembeni, akatoa sigara yake na kuanza kuvuta taratibu.

Ghafla, yule polisi aliyeingia ndani ya gari akatoka, alionekana kubadilika, alipofika chini tu, akatoa bunduki yake na kumuweka yule mzee chini ya ulinzi. Polisi wengine hawakujua kitu gani kilitokea, ila nao wakatoa bunduki zao na kumuweka chini ya ulinzi.

“Upo chini ya ulinzi…” alisema polisi yule.

“Chini ya ulinzi? Nimefanya nini?”

“Kwa mauaji!”

“Mauaji ya nani tena jamani?” aliuliza mzee yule huku akionekana kupigwa na mshangao.

Hata kabla hajapewa jibu, akaamrishwa alale chini na kuweka mikono yake kichwani, hakuwa mbishi, akafanya hivyo ndipo polisi yule alipoanza kuwaambia wenzake juu ya kile alichokiona ndani ya gari.

“Hapana! Sijamuua yeyote yule,” alisema mzee yule wakati maiti ya polisi yule ikitolewa ndani ya gari.

“Nyie wauaji huwa hamsemi ukweli, utakwenda selo sasa hivi,” alisema polisi mwingine huku akionekana kuwa na hasira.

Pingu ikatolewa na hapohapo akafungwa. Muda wote mzee huyo alikuwa akijitetea kwamba hakuwa amemuua mtu yeyote yule na hakujua maiti ile ilifikaje ndani ya gari lake.

Huo haukuwa muda wa kumsikiliza tena, walijua kwamba kwa jinsi tukio hilo lilivyotokea, angeweza kusema neno lolote ili kujitetea, walichokifanya ni kumpakiza ndani ya gari na kuanza kuondoka naye huku polisi wengine wakibaki mahali pale kuendelea na msako.

“Sijamuua mtu yeyote jamani, haki ya Mungu sijamuua mtu yeyote yule,” alijitetea mzee huyo huku machozi yakimtoka.

“Utasema ukweli tu.”

Baada ya dakika kadhaa, wakafika katika kituo cha polisi ambapo mzee huyo akaanza kuhojiwa maswali kadhaa. Akatoa maelezo yake juu ya safari yake ilipoanza mpaka pale alipofika Chalinze ambapo alikamatwa.

“Unasema ulimpakiza mtu?”

“Ndiyo!”

“Unasema alikuwa na kofia kama ya Marlboro?”

“Ndiyo! Alishuka Mlandizi, nilishangaa kuona anaelekea porini, sikuuliza sana, sikujali, baadaye nikaondoka,” alisema mzee huyo.

“Na ulimzungumzia polisi, ulisema alivyoingia garini, hukumuona akitoka na ulipomuuliza, alisema alitokea upande wa pili?”

“Ndiyo!”

“Huyo atakuwa Dickson…. atakuwa Dickson huyo tu,” alisema mkuu wa kituo.

Hawakutaka kuendelea kubaki kituoni hapo, tayari walikuwa na uhakika kwamba mtu huyo alikuwa ni Dickson kwani hata maelezo ya mzee huyo yalionesha kwamba muuaji huyo alikuwa yeye. Walichokifanya ni kuingia ndani ya gari na mzee huyo, wakawachukua mbwa wao, bunduki zao na kuanza kuelekea kule aliposhukia Dickson, yaani piga ua hata kama angekuwa amekwenda wapi, ilikuwa ni lazima atafutwe na kukamatwa usiku huohuo.

“Tumefika…alielekea huku,” alisema mzee yule mara baada ya kufika eneo husika, wote wakateremka, bunduki mikononi na kuanza kuelekea kule alipoelekea Dickson, walikuwa na uhakika kwamba hakuwa amefika mbali.

Umbali kama hatua ishirini, wakaona mbwa wao wakibweka sana na kutaka kusonga mbele, hapo walikuwa na uhakika kwamba hawakuwa mbali na mtu huyo, hivyo wakaongeza kasi kwani kadiri sekunde zilivyokatika, mbwa walizidi kubweka.

Dickson alisonga mbele, hakutaka kusimama, hakutaka kurudi alipotoka, alitaka kufanya kila liwezekanalo mwisho wa siku afike Mwanza. Alitembea kwa mwendo wa kasi lakini baada ya umbali fulani, akahisi kuchoka hivyo kukaa chini ya mti na kupumzika.

Hapo ndipo kumbukumbu za maisha yake ya nyuma zilipomjia kichwani, alikumbuka mambo mengi mpaka kupitiwa na usingizi. Baada ya saa moja, akashtuka, kwa mbali akaanza kusikia sauti za mbwa wakibweka, hiyo ilikuwa saa nane usiku.

Hakutaka kuwa na wasiwasi, alichokifanya kwa sababu ya kuchoka sana, akajigeuza upande wa pili na kuanza kuuvuta usingizi, akili yake ilimwambia kwamba mbwa hao walikuwa ni wa wawindaji waliokuwa wakiwinda kenge, hivyo hakutaka kujali.

Usingizi ukaanza kumjia tena pasipo kugundua kwamba mbwa wale walikuwa ni wa polisi waliokuwa wakimsaka kufuatia mauaji aliyoyafanya.


Je nini kitaendelea? Au Dickson atakamatwa?
 
SEHEMU YA 63

Hali ya sintofahamu inazuka jijini Dar es Salaam, machangudoa wengi wanaanza kuuawa katika mazingira ya kutatanisha. Hakuna anayemjua muuaji, kila changudoa anayenunuliwa na mwanaume aliyekuwa kwenye gari aina ya Volkswagen nyeusi, anauawa kikatili.

Kila mmoja anaogopa, machangudoa wengine wanaacha kujiuza, wanajifungia vyumbani mwao, ila kwa wengine ambao hawakuweza kuishi bila kufanya biashara hiyo, wanakwenda huko, bado wengine wanaendelea kuuawa.

Aliyekuwa akiwaua wanawake hao ni Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam, Dickson. Aliwaua kwa siri lakini baada ya kipindi fulani kupita, akagundulika na hivyo kuanza kutafutwa.

Kwa sasa yupo Mlandizi, baada ya kuona msako umekuwa mkubwa barabarani anaamua kwenda Mwanza kwa miguu kupitia Mlandizi. Anapofika porini, anaamua kujipumzisha huku polisi wenye mbwa wakiendelea kusogea kule alipokuwa.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Usingizi ulikuwa ukimnyemelea, alichokitaka kwa wakati huo ni kulala tu kwani muda ulikwenda sana na hakujisikia kuendelea na safari yake. Sauti za mbwa ziliendelea kusikika masikioni mwake, hakutaka kujali sana kwani bado akili yake ilimwambia kuwa mbwa waliokuwa wakija hawakuwa na madhara yoyote kwake kwani watakuwa ni mbwa wa wawinda kenge ambao mara kwa mara walikwenda porini na hata pembezoni mwa mito kuwinda wadudu hao.

Wakati akiwa amekwishajiachia huku akiuvuta usingizi, akahisi mwili wake ukianza kusisimka mno. Haikuwa kawaida yake hata kidogo, alihisi labda kulikuwa na tatizo, akayafumbua macho yake na kuangalia huku na kule kuona kama kulikuwa na hatari ya kiumbe chochote mbele yake, hakukuwa na kitu chochote.

Usingizi haukuja tena, alijitahidi kuuvuta lakini mwili wake haukukubali hata kidogo. Alipitia mafunzo, aliujua mwili wa binadamu ulivyo, hakutaka kubishana nao, alihisi kwamba kulikuwa na tatizo na kama asingefanya lolote liwezekanalo basi angeweza kukutwa na hatari.

Alichokifanya ni kusimama, akaanza kuyapeleka macho yake huku na kule. Kwa mbali, aliweza kusikia sauti kadhaa za watu wakija kule walipokuwa, maneno aliyoyasikia, hayakuwa ya kawaida, yalikuwa ni koplo, kamanda na mengine, japokuwa aliyasikia kwa mbali, alihisi kwamba hao walikuwa polisi.

Kutoka hapo aliposimama mpaka sehemu ambapo polisi wale walifika, ilikuwa ni kama hatua mia moja, na sauti zile alizisikia vizuri ingawa ilikuwa na umbali mkubwa kutokana na ukimya uliokuwepo usiku, hakukuwa na haja ya kusubiria mahali hapo, alichokifanya ni kukimbia zake.

Hakutaka kusimama sehemu yoyote ile, aliendelea kusonga mbele, milio ya mbwa wakibweka haikuacha kusikika masikioni mwake, iliendelea kusikika zaidi hivyo kuongeza kasi kuelekea mbele zaidi.

Kulikuwa na giza, hakuanguka, kulikuwa na miba lakini hakujichoma, wakati mwingine alipita mpaka sehemu zilizokuwa na upupu, cha kushangaza hakuweza hata kuwashwa.

“Ni lazima nijiokoe, siwezi kukamatwa kizembe hivi,” alijisemea.

Alikimbia hadi alipofika sehemu ambapo kulikuwa na uwazi mkubwa, haikumpa tabu kugundua kwamba sehemu ile ilikuwa shambani. Hakukuwa na mtu yeyote mahali hapo, alijaribu kuangalia vizuri, shamba hilo lilikuwa ni la mpunga.

Hakutaka kusubiri, hakutaka kujiuliza, alichokifanya ni kuingia shambani humo huku akiendelea kukimbia. Shamba hilo lilikuwa kubwa, aliharibu mpunga lakini hakutaka kusimama, alisonga mbele zaidi huku akihema kama mbwa.

“Yule kule, kamata huyo mwiziiiii….kamata mwizi huyooooo….” alisikia sauti nyuma yake, alipogeuka, akawaona watu watano wakiwa wanamkimbiza kwa kasi kubwa.

Akili yake ikamwambia kwamba watu hao walikuwa polisi, akazidi kukimbia, tayari alijiona kukamatwa kama tu asingefanya juhudi za kukimbia na kuwaacha. Ila pamoja na hayo yote, kilichomtatiza ni juu ya mbwa.

Katika kipindi alichokuwa kule chini ya mti, alisikia watu wakija huku wakiwa na mbwa, alijua kabisa kwamba watu hao walikuwa polisi kutokana na majina waliyokuwa wakiita. Sasa hawa waliokuwa wakimkimbiza, ambao alihisi kwamba walikuwa polisi, hawakuwa na mbwa, walikuwa wao kama wao.

“Simama, tutakupiga mishale,” alisema mwanaume mmoja, naye alikuwa kasi kama wenzake.

“Aisee Iddi! Mfyatulie mmoja kwanza, piga wa mgongoni,” alisikika jamaa mwingine akimwambia mwenzake.

Iddi, mwanaume aliyejulikana kuwa na shabaha akaanza kumrushia mishale. Dickson alijua kilichokuwa kinaendelea hivyo naye kitu alichokifanya ni kukimbia kwa staili ya zigizaga, yaani kushoto kulia, kulia kushoto, yote ikiwa ni harakati za kukwepa mishale ile.

Wakati akiwa amebakiza kama hatua ishirini kumaliza shamba lile na kutoka nje, akashtukia akipigwa na mshale katika mguu wake, maumivu aliyoyasikia yalikuwa makubwa mno, akadondoka chini lakini hakutaka kutulia, akasimama na kuendelea kuukimbia huku akichechemea, damu zilimtoka mguuni lakini hakujali.

“Simama….tunasema simama utatuletea kesi ya mauaji…” alisema mwanaume mmoja kwa sauti ya juu.

Dickson hakuwa radhi kusimama, alijua kitendo cha kufanya hivyo matokeo yake ni kifo. Alipambana, alizidi kusogea mbele zaidi huku akichechemea, alipolimaliza lile shamba tu, hakuweza kupiga hatua, akajikuta akianguka chini, watu hao wakamfikia.

“Wewe ni nani?” aliuliza mwanaume mmoja kwa sauti ya juu huku akiwa amemuelekezea mshale mwingine usoni.

“Nao..mba mn..isa..meh..e..” alisema Dickson huku akihema kwa nguvu.

“Wewe ni nani?”

“Mbona unamuuliza maswali mengi Iddi, kama vipi mtawanye ubongo wake tu! Halafu nashangaa siku hizi una huruma sana aisee…” alisema jamaa mwingine huku akimwangalia swahiba wake ambaye alimuelekezea mshale Dickson.

“Haina noma, ngoja tuue fastafasta halafu tukamtupe porini,” alisema Iddi kisha kujiandaa kuachia mshale usoni mwa Dickson.

* * * *

Polisi waliendelea kusogea mbele, kadiri walivyozidi kusogea ndivyo ambavyo mbwa walivyozidi kubweka kuon esha kwamba mtu waliyekuwa wakimtafuta hakuwa mbali kutoka hapo walipokuwa.

Baada ya sekunde kadhaa wakafika katika ule mti alipokuwa amepumzika Dickson, mbwa wakausogelea, wakanusanusa sehemu ile na kusonga mbele zaidi.

Polisi walikuwa na uhakika kwamba hatimaye wangeweza kumpata Dickson, hawakukata tamaa, walizidi kusonga mbele na baada ya dakika kadhaa, wakafika katika eneo moja kubwa, lilikuwa shamba, hakuna walichojiuliza, walichokifanya ni kuingia shambani na kusonga mbele, kama kawaida mbwa waliendelea kubweka.

Je, nini kitaendelea?
 
SEHEMU YA 64

Hali ya sintofahamu inazuka jijini Dar es Salaam, machangudoa wengi wanaanza kuuawa katika mazingira ya kutatanisha. Hakuna anayemjua muuaji, kila changudoa anayenunuliwa na mwanaume aliyekuwa kwenye gari aina ya Volkswagen nyeusi, anauawa kikatili.

Kila mmoja anaogopa, machangudoa wengine wanaacha kujiuza, wanajifungia vyumbani mwao, ila kwa wengine ambao hawakuweza kuishi bila kufanya biashara hiyo, wanakwenda huko, bado wengine wanaendelea kuuawa.

Aliyekuwa akiua wanawake hao ni Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam, Dickson. Aliwaua kwa siri lakini baada ya kipindi fulani kupita, akagundulika na hivyo kuanza kutafutwa.

Kwa sasa yupo Mlandizi, baada ya kuona msako umekuwa mkubwa barabarani anaamua kwenda Mwanza kwa miguu kupitia Mlandizi. Anapofika porini, anaamua kujipumzisha huku polisi wenye mbwa wakiendelea kusogea kule alipokuwa.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Watu wengine waliwaona polisi kuwa wazembe mno, hawakuamini kama katika kipindi chote hicho hawakufanikiwa kumpata Dickson. Aliwakimbia katika mazingira ya kutatanisha sana hali iliyomfanya IGP Mayala kukasirika mno.

Alichokiona kwa polisi wake ni kwamba walikuwa wazembe, aliwaamini, alijua kwamba walikuwa wachapakazi wakubwa lakini swali likaja ni kwa namna gani huyo Dickson aliweza kuwatoroka, yaani kutoka ndani ya Jiji la Dar es Salaam pasipo kugundulika?

Hilo ndilo lililomfanya kuzungumza na kitengo cha upelelezi na kumhitaji mpelelezi mmoja, mwenye uwezo mkubwa ambaye angekula sahani moja na Dickson mpaka kuhakikisha mtu huyo anakamatwa.

Walijua ni mtu gani waliyekuwa wakishughulika naye, hakuwa mtu mzuri hata kidogo, kama kupambana, hata kama ungemuwekea watu watano, angeweza kupambana nao na kuwapiga wote hivyo hata mpelelezi ambaye alitakiwa kutumwa kwenda kumtafuta, alitakiwa kujua jinsi ya kupambana ili iwe rahisi kumtia nguvuni.

“Tumchukue James Malope…” alisema polisi mmoja.

“Unahisi ataweza?” aliuliza IGP Mayala.

“Nadhani…”

“Hatua tuliyofikia sasa hivi si ya kudhani, tunahitaji watu wenye uhakika, unahisi ataweza?” aliuliza IGP Mayala.

“Ataweza tu.”

“Hapana! Bado sijafikiri hilo, nadhani Fredrick Limao atafaa zaidi kwa kuwa ndiye mtu mwenye uwezo mkubwa katika masuala ya upelelezi,” alisema IGP huku akionekana kuwa na uhakika na kile alichokuwa akikisema.

“Hakuna tatizo mkuu,”

Fredrick Limao alikuwa mpelelezi kutoka TISS ambaye kwa kipindi hicho alikuwa ametoka nchini Urusi alikopelekwa kwa ajili ya kumtafuta mtu aliyejulikana kwa jina la Mirkovic Ilalatovic.

Huyo alikuwa mfanyabisahara mkubwa wa madawa ya kulevya. Aliua watu na kujificha huku nyuma yake kukiwa na ulinzi madhubuti. Hakupatikana kirahisi, Wamarekani na watu wao wa upepelezi wa kimataifa, CIA walijaribu kumtafuta kwa kipindi cha miaka mitano, hawakufanikiwa kumpata.

Tofauti na CIA, hata shirika la Kijasusi la Urusi, KBG nalo lilijaribu kumtafuta kila kona lakini halikufanikiwa. Mara baada ya kuhangaika sana, walichokifanya KGB ni kuomba msaada kutoka Afrika Kusini ambapo ikatuma wapelelezi wake waliokaa huko kwa muda wa miaka miwili lakini waliambulia patupu.

Mirkovic aliendelea kuwa gumzo, bado watu wengi walikuwa wakiuawa kila siku. Madawa ya kulevya yalisafirishwa, hongo ilitapakaa kwa kila polisi aliyekuwa akiwakamata wasafirishaji wa madawa hayo, kwa wale waliokataa kupokea hongo hiyo, waliuawa wao na familia zao.

Hofu kubwa ikatanda na hawakujua ni kwa jinsi gani wangeweza kumpata mtu huyo. Baada ya miaka kadhaa kukatika, hatimaye akatumwa mtu mmoja, aliyepokea mafunzo ya kijasusi kutoka nchini Cuba, huyo alikuwa Fredrick Limao.

Kwa watu wengi walihisi kwamba hiyo ingekuwa kazi kubwa sana ila moyoni mwake, kazi hiyo ilionekana kuwa nyepesi mno na wala isingemchukulia muda wake mwingi.

Alipofika nchini Urusi, kitu cha kwanza kabisa akajifanya mwanachuo katika Chuo Kikuu cha Moscow, hakukuwa na mtu aliyeelewa kilichokuwa nyuma ya pazia.

Huko chuoni, akakutana na kijana aliyeitwa Paul Mirkovic, akalazimisha urafiki na kwa sababu alikuwa na akili sana, hatimaye akafanikiwa, wakawa marafiki wakubwa, wakaaminiana na hatimaye kuanza kuambiana mambo yao ya siri.

“Wewe ni rafiki yangu mkubwa sana Limao…” alisema Paul huku akimwangalia Fredrick.

“Najua hilo!”

“Kuna kitu nataka kukwambia..”

“Kipi?”

“Unaweza kutunza siri?”

“Naweza, kwa nini nisiweze…”

“Basi sawa! Baba yangu ni miongoni mwa watu wenye fedha nyingi hapa Urusi. Kutokana na fedha hizo ana mali kibao na kuheshimiwa sana,” alisema Paulo.

“Hongera kwa kuwa na baba mwenye fedha nyingi, nini chanzo cha fedha hizo?” Fredrick alimwuliza.

Paulo alipoulizwa hivyo, alicheka na kumwambia siku zote mjini ni mipango.

“Unaposema mjini ni mipango nashindwa kuelewa, au biashara zake hazieleweki?” Fredrick alimwuliza.

“Wewe elewa ana ishu kubwa zinazomwingizia fedha usiku na mchana, huwa nakutana naye kila siku ya Jumamosi katika klabu ya Amazon…” alisema Paul.

“Baba yako nani? Mzee Mirkovic?”

“Ndiyo!”

“Mmh! Mimi mbona simjui!”

“Ni mtu maarufu sana hapa Urusi, huyo ndiye ninayekutana naye, kuna siku utamuona tu,” alisema Paul.

Kazi kubwa aliyokuwa nayo, ikarahisishwa, hakuamini kama ingekuwa nyepesi kiasi hicho. Alichokifanya baada ya mwezi mmoja ni kuwataarifu polisi kisha mtu huyo hatari kukamatwa.

Baada ya kufanya kazi hiyo na nyingine nyingi za hatari, hatimaye akaamua kurudi nchini Tanzania huku akiwa na heshima kubwa. Alipofika, hakukaa sana akaambiwa kulikuwa na kazi ya kufanya, kumtafuta mtu aitwaye Dickson aliyekuwa Kamanda Mkuu wa Polisi Kanda ya Dar es Salaam.

Alipoambiwa, kwake haikuwa kazi kubwa. Kama aliweza kupambana na Wazungu, wenye uwezo mkubwa angeshindwa vipi kwa Mtanzania, tena kwa mtu kama Dickson? Kila alipojifikiria, kwake, kumtafuta mtu huyo ilikuwa kazi nyepesi kabisa, yaani ni kama kumsukuma mlevi kwenye mremko wa mlima. Akakubali, akajipanga na kuanza kazi ya kumtafuta mtu huyo hatari.


Je, nini kitaendelea?
 
SEHEMU YA 65

Hali ya sintofahamu inazuka jijini Dar es Salaam, machangudoa wengi wanaanza kuuawa katika mazingira ya kutatanisha. Hakuna anayemjua muuaji, kila changudoa anayenunuliwa na mwanaume aliyekuwa kwenye gari aina ya Volkswagen nyeusi, anauawa kikatili.

Kila mmoja anaogopa, machangudoa wengine wanaacha kujiuza, wanajifungia vyumbani mwao, ila kwa wengine ambao hawakuweza kuishi bila kufanya biashara hiyo, wanakwenda huko, bado wengine wanaendelea kuuawa. Aliyekuwa akiwaua wanawake hao ni Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam, Dickson. Aliwaua kwa siri lakini baada ya kipindi fulani kupita, akagundulika na hivyo kuanza kutafutwa. Kwa sasa yupo Mlandizi, baada ya kuona msako umekuwa mkubwa barabarani anaamua kwenda Mwanza kwa miguu kupitia Mlandizi. Anapofika porini, anaamua kujipumzisha huku polisi wenye mbwa wakiendelea kusogea kule alipokuwa.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Ilikuwa ni lazima kupambana na watu hao. Aliwahesabu, aliangalia silaha walizokuwa nazo, hazikuwa na uwezo wa kumfanya kutofanikiwa kufanya kile alichotaka kufanya. Mtu wa kwanza kabisa ambaye aliona kama angeweza kumkabili na kuwashinda wengine, alikuwa Iddi. Huku mwanaume huyo akiwa amemsogelea kwa ajili ya kumfunga kamba, alichokifanya Dickson ni kukunja ngumi yake nzito na kumpiga Iddi ngumi ya shingo iliyomfanya kupiga uyowe mara moja tu, akaanguka chini.

Wale wengine walipoona hivyo, hawakutaka kukubali, hicho ndicho alichokitaka Dickson, wa kwanza alipomsogelea, akamdaka kwa mkono mmoja, akampiga kichwa kimoja kitakatifu usoni, jamaa akaanza kuona mawenge, hata alipoachwa na kutaka kukimbia, akapepesuka akashindwa, kuendelea mbele, akalala chini na kuanza kupiga kelele.
Walibaki wawili, wakabaki wakiangaliana tu, mapigo mawili aliyowapiga wenzao yaliwachanganya hata wao wenyewe. Hawakujua kama huyo mtu alikuwa wa kawaida au mzimu, hawakutaka kubaki mahali hapo, waliogopa, hawakutaka kufa, waliyapenda maisha, kilichofuata ni kukimbia.

Dickson alitisha, mapigo aliyowapiga watu wale yalikuwa mawili, kila mmoja moja lakini yalikuwa ya maana yaliyoonesha kwamba kama angewapiga kwa mapigo matatu au zaidi, wangeweza kufa. Ndani ya sekunde chache, Dickson akabaki peke yake, hakutaka kubaki mahali hapo, bado alikuwa na safari ndefu na ilikuwa ni lazima kusonga mbele kwani asingeweza kurudi nyuma. Akaondoka zake. Mpaka alfajiri inaingia, bado Dickson alikuwa akielekea mbele, hakujua mahali alipokuwa akielekea palikuwa wapi, kitu pekee kilichomjia kichwani mwake ni kwamba alikuwa akikimbia kuepuka mkono wa sheria.

Alikimbia mpaka alipofika sehemu iliyokuwa na mto mdogo ambao maji yake yalikuwa yametulia. Hakutaka kuvuka, kitu cha kwanza kabisa akasimama pembeni na kuanza kunawa uso wake. Njaa kali ilianza kumuuma, alikuwa na fedha za kutosha mifukoni mwake lakini hazikuwa na thamani kipindi hicho, hakuwa na pa kuzitumia, alibaki nazo mifukoni kama mtu aliyekuwa na makaratasi yasiyokuwa na umuhimu wowote ule.

Ilikuwa ni lazima avuke kuelekea upande wa pili wa mto ule, hakujua angevuka vipi lakini ilikuwa ni lazima afanye hivyo. Mtoni, hakukuwa na mtumbwi wowote ule, kuna kipindi alifikiria kuogelea mpaka upande wa pili lakini wakati mwingine akahisi kufanya hivyo si vizuri kwani hakujua ndani ya mto ule kulikuwa na nini. Alichokifanya ni kwenda pembeni na kupumzika. Hapo ndipo mawazo yake yalipoanza kurudi nyuma, tangu siku ya kwanza alipoanza kufanya kazi ya upolisi, alipokutana na msichana Pamela mpaka siku hiyo. Kwenye kila kitu alichokuwa akikifikiria, kilimuumiza, hakuamini kwamba yeye huyohuyo, leo hii ndiye angekuwa akitafutwa Tanzania nzima. Pale alipojipumzisha, akajikuta akipitiwa na usingizi na baada ya dakika kadhaa, akaamshwa na sauti za watu waliokuwa mtoni.

Haraka akasimama, akayatupia macho yake mtoni, wavuvi waliokuwa na mtumbwi walikuwa wakipiga kasia.
Huo ndiyo ulikuwa msaada wake mkubwa wa kumvusha mahali hapo, alichokifanya ni kuanza kuwaita kwa kuwapigia mluzi. Wale wavuvi waliposikia, wakageuza mtumbwi wao na kuanza kumfuata.

“Mbona upo hapa?” aliuliza mvuvi mmoja.
“Nilikuwa nasubiri msaada wa kunivusha kule ng’ambo,” alijibu Dickson.
“Haujakutana na kitu chochote kibaya?”
“Hapana! Kwani kuna nini?” aliuliza Dickson, kauli za mzee yule zikamfanya kuhisi kitu.
“Basi tu.”

Hakutaka kuuliza swali jingine, alichokihitaji ni msaada tu na wavuvi wale wakaanza kufanya kama alivyoomba. Muda wote macho yao yalikuwa kwenye maji, Dickson hakujua walikuwa wakitafuta nini, akaona bora aulize.
“Kuna mamba wengi sana, huwa wanatumaliza sana wanakijiji,” alijibu mvuvi mmoja baada ya kumuuliza kuhusu utazamaji wao wa makini mtoni.
“Kuna mamba? Mto huu una mamba?” aliuliza Dickson.
“Ndiyo! Tena mamba hatari sana. Umeshawahi kusikia kuhusu Malupupu?” aliuliza mvuvi mmoja.
“Hapana! Ndiyo nini?”
“Ni aina ya mamba wanaopatikana katika mto huu ni hatari sana,” alijibu mvuvi mwingine.
Walibaki wakizungumza mpaka walipofika ng’ambo ambapo Dickson akateremka na kutaka kuwalipa lakini wazee wale walikataa katakataka kwa kumwambia kwamba walimsaidia tu, Hakutaka kujali, alichokifanya ni kusonga mbele zaidi. Baada ya dakika kadhaa, akafika katika kijiji kimoja kikubwa, kilichokuwa na nyumba nyingi za nyasi, kijiji hiki kiliitwa Mzenga, Kusini mwa Mkoa wa Morogoro ambapo kulikuwa na kanisa kubwa lililojengwa na Wamishenari miaka ya nyuma.

Wanakijiji waliomuona Dickson, wengi wakaanza kukimbia. Walimuogopa, Dickson hakujua kitu gani kilikuwa kimesababisha mpaka watu hao kuanza kumkimbia. Wakati akijiuliza hilo, mara mbele yake akasimama kijana mmoja aliyeonekana kuwa mtanashati.

Alikuwa tofauti na wanakijiji wengine, kwa jinsi alivyovaa wala isingekupa wakati mgumu kugundua kwamba mtu huyo alitoka mjini siku za hivi karibuni. Wakabaki wakiangaliana tu. “Kwa nini umekuja katika kijiji chetu?” aliuliza jamaa huyo, alionekana kumfahamu Dickson kwa sura, hata alipomwangalia, sura ya mwanaume huyo haikuwa ngeni kabisa, alimfahamu. Wakati Dickson akibaki na maswali mengi, hapo ndipo alipogundua kwamba kijana yule aliyesimama alikuwa na karatasi yenye picha, alipoiangalia vizuri karatasi ile, akaiona ikiwa na picha yake, moyo wake ukapiga paaaaa.

Je, nini kitaendelea?
 
SEHEMU YA 66

Hali ya sintofahamu inazuka jijini Dar es Salaam, machangudoa wengi wanaanza kuuawa katika mazingira ya kutatanisha. Hakuna anayemjua muuaji, kila changudoa anayenunuliwa na mwanaume aliyekuwa kwenye gari aina ya Volkswagen nyeusi, anauawa kikatili.

Kila mmoja anaogopa, machangudoa wengine wanaacha kujiuza, wanajifungia vyumbani mwao, ila kwa wengine ambao hawakuweza kuishi bila kufanya biashara hiyo, wanakwenda huko, bado wengine wanaendelea kuuawa.
Aliyekuwa akiwaua wanawake hao ni Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam, Dickson. Aliwaua kwa siri lakini baada ya kipindi fulani kupita, akagundulika na hivyo kuanza kutafutwa. Aliamua kukimbia kupitia Mlandizi, huko, akapitia misukosuko mingi na mwisho wa siku akajikuta kwenye kijiji kimoja ambapo baada ya wanakijiji kumuona, wakaanza kujificha. Huku akijiuliza nini kinaendelea, akatokea kijana aliyekuwa na picha yake mkononi, Dickson akashtuka.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Kazi iliyokuwa mbele yake ilikuwa kubwa lakini hakutaka kuliona hilo. Alikuwa amefanya kazi ya upelelezi katika nchi nyingi, tena kwa watu waliokuwa na mtandao mkubwa, wauza madawa ya kulevya lakini kote huko alifanikiwa kwa asilimia zote. Hiyo kazi iliyokuwa mbele yake, Fredrick aliiona kuwa ndogo sana, haikuwa kubwa, kumkamata mtu kama Dickson ambaye hakuwa akilindwa, hakuwa na mtandao wowote ilionekana kuwa kazi nyepesi, kama kumsukuma mlevi kwenye mteremko wa mlima.

Mara baada ya kuiona picha ya Dickson, akaondoka. Hakutaka kufanya kazi ya kwenda sehemu nyingine yoyote ile zaidi ya Mlandizi ambapo huko, kitu cha kwanza kabisa akaonana na polisi waliokuwa wamemfuatilia Dickson na mbwa wao lakini hawakufanikiwa.

“Tulimfuatilia lakini tulimkosa,” alisema mkuu wa kituo.
“Mlihisi anakwenda wapi?” aliuliza Fredrick.
“Hatujui kwa kweli, ila ni pori kwa pori, nahisi kuna sehemu anakwenda,” alijibu huku akimwangalia Fredrick usoni, alionekana kutokuwa mtu wa masihara hata mara moja.
Alichokitaka ni kupelekwa katika njia ile aliyoingia Dickson, hilo halikuwa tatizo, akachukuliwa na kupelekwa huko kisha kuachwa, sasa kazi ikawa kwake, kufuatilia hatua kwa hatua mpaka kuhakikisha huyo Dickson anapatikana.

Alikuwa na silaha zake, bunduki ndogo aina ya 45 Automatic upande wa kushoto kiunoni lakini katika soksi zake alikuwa na bunduki nyingine ndogo aina ya Revolver tena zote hizo zikiwa zimejaa risasi. Alijitahidi kwenda mbele, alitembea mchana na usiku, alipita sehemu zilizokuwa na miti mingi, mabonde lakini aliendelea kusonga mbele. Chakula chake kikubwa huko njiani kilikuwa ni matunda mbalimbali ya miti.

Usiku wa siku hiyo alipolala na kuamka asubuhi, akaendelea na safari yake mpaka alipofika sehemu iliyokuwa na uwazi mkubwa, kulikuwa na shamba kubwa la mpunga, shamba lilelile alilopita Dickson kipindi cha nyuma. Kabla ya kuingia ndani ya shamba hilo, akasimama na kuliangalia kwa makini. Kwa mtu kama yeye, mpelelezi aliyepitia mafunzo, hakutakiwa kufanya mambo kiholela, kila kitu alichotakiwa kufanya ilikuwa ni lazima kusubiri kwa muda. Ardhini kuulionekana kuwa na alama za miguu ya watu, hiyo ikampa uhakika kwamba kulikuwa na watu mahali hapo kwani hata zile alama za miguu hazikuonesha kama watu hao walipita muda mrefu uliopita.

Akaanza kutembea pembeni ya shamba lile huku akionekana kuwa na wasiwasi, hisia zake zilimwambia kabisa kwamba kulikuwa na watu waliokuwa wakimwangalia. Alikuwa na bastola hakutaka kuzitoa kwani aliamini kama kulikuwa na watu, wasingekuwa na bastola, silaha zao zingekuwa za jadi kitu ambacho kingemfanya kupambana nao vilivyo.
Wakati akiwa ametembea kama hatua hamsini, akahisi nyuma yake kulikuwa na mtu akimsogelea, alichokifanya ni kupiga hatua ndefu mbili mbele kisha akageuka na teke moja la ghafla, alichokisikia nyuma yake ni uyowe mkubwa.
“Unaniuaaaaaa….” alisema mwanaume mmoja, alikuwa chini, teke lile lililopigwa, lilimpiga vilivyo kichwani.
Ghafla, wanaume watatu wakatokea mahali hapo, walikuwa na mikuki, wakamnyooshea Fredrick ambaye hakuonesha wasiwasi wowote, alibaki akiwaangalia.

“Mikono juu!” alisema mwanaume mmoja.
“Na miguu je?” alijibu Fredrick kijeuri, tena huku akiwaangalia watu hao, hakuonekana kuwa na hofu hata kidogo.
“Tumesema nyosha mikono juu!”
“Hebu acheni upuuzi, nipo safarini, mnanichelewesha, mmemuona mwanaume mmoja mwenye sura mbaya akipita huku?” aliuliza Fredrick huku akiwaangalia wanaume hao.
“Mikono inauma, siwezi kufanya hivyo!”
“Nimesema nyosha mikono juu!”
* * *
“Kwa nini umekuja kijijini kwetu?” Kijana yule alirudia swali lake. Dickson akabaki akimwangalia, kilichomtia hofu ni ile picha aliyokuwa ameishika kijana yule. Japokuwa ilikuwa ni kijijini alijua kwamba kijana huyo ndiye aliyepeleka picha na mwisho wa siku wanakijiji kuanza kumkimbia kwa kuwa walimuogopa.
“Unahitaji nini kutoka kwangu?” aliuliza Dickson huku akimwangalia kijana yule.
“Sihitaji chochote kile, ninataka uondoke kabla polisi hawajafika,” alisema kijana yule.
Dickson hakutaka kuzungumza kitu, alichokifanya ni kuendelea na safari yake. Alikuwa amechoka na alitegemea angepumzika kijijini hapo lakini hilo likashindikana, hivyo akaondoka zake.

Mguu ulikuwa ukimuuma lakini hakusimama, kidonda kilizidi kuongezeka, kilichimbika na kitu pekee alichokihitaji kilikuwa ni dawa tu, ila kijijini hapo, hakukuwa na msaada wowote ule, hivyo akaondoka. Wanakijiji ambao walikuwa wamejificha walibaki wakimwangalia, hata kutoka huko walipokuwa hawakuthubutu kwani habari ambazo kijana yule alizileta kijijini pale, aliziongezea chumvi kwa kusema kwamba Dickson alikuwa na uwezo wa kulipua sehemu yoyote ile kwani kila alipotembea, alitembea na mabomu.

Njia nzima alikuwa na mawazo tele, hakutaka kurudi nyuma, japokuwa mbele yake kulikuwa na safari ndefu ya kuelekea Mwanza lakini ilikuwa ni lazima afike huko kwa kupita pori mpaka pori. Baada ya mwendo kama wa kilometa mbili, akaanza kusikia sauti za watu kutoka porini. Kwanza kitu alichokijua ni wanakijiji tu ambao kazi yao ilikuwa ni kushinda mashambani mwao. Hakutaka kuogopa, alijiamini sana, alichokifanya ni kusimama wima ili kuwaona hao watu ambao walikuwa porini kuja mahali pale aliposimama.


Ghafla, wanaume watatu walioshiba, waliokuwa na bunduki nzito mikononi mwao wakatokea mahali hapo, Dickson akashtuka, alipomwangalia mmoja wapo, huyu alikuwa Savimbi, mmoja wa wanaume walioshiba ambao kazi yao kubwa ilikuwa ni kuteka mabasi yaendayo mikoani. Alipomuona, akashtuka, wote wakaangaliana, walifahamiana, vijana wengi wa Savimbi ambao walikuwa wakielekea benki jijini Dar es Salaam kuiba fedha waliuawa na mwanaume huyo alipokuwa polisi.

Alimfahamu, aliujua uwezo wake, wakabaki wakiangalia, umbali uliokuwepo kati yao, kama miguu ishirini hivi.
Alichokifanya Savimbi ni kuikoki bunduki yake na wale vijana wake, mtu aliyesimama mbele yake, alikuwa akimchukia mno, ilikuwa bora kumpenda shetani lakini si huyo Dickson, leo aliingia kwenye kumi na nane zake, ilikuwa ni lazima amuue. Dickson akabaki akitetemeka.


Je, nini kitaendelea?
 
SEHEMU YA 67

Hali ya sintofahamu inazuka jijini Dar es Salaam, machangudoa wengi wanaanza kuuawa katika mazingira ya kutatanisha. Hakuna anayemjua muuaji, kila changudoa anayenunuliwa na mwanaume aliyekuwa kwenye gari aina ya Volkswagen nyeusi, anauawa kikatili.

Kila mmoja anaogopa, machangudoa wengine wanaacha kujiuza, wanajifungia vyumbani mwao, ila kwa wengine ambao hawakuweza kuishi bila kufanya biashara hiyo, wanakwenda huko, bado wengine wanaendelea kuuawa.
Aliyekuwa akiwaua wanawake hao ni Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam, Dickson. Aliwaua kwa siri lakini baada ya kipindi fulani kupita, akagundulika na hivyo kuanza kutafutwa.

Aliamua kukimbia kupitia Mlandizi, huko, akapitia misukosuko mingi na mwisho wa siku akajikuta kwenye kijiji kimoja ambapo baada ya wanakijiji kumuona, wakaanza kujificha. Huku akijiuliza nini kinaendelea, akatokea kijana aliyekuwa na picha yake mkononi, Dickson akashtuka.

Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Walibaki wakiangaliana, walifahamiana, Savimbi alikuwa mtu hatari, jambazi ambaye kila siku alikuwa akikiongoza kikosi cha porini kuteka mabasi na kuwafanyisha abiria vitendo vya kinyama. Hata na yeye alipomwangalia Dickson, alimfahamu vilivyo, alikuwa miongoni mwa askari hatari sana, wenye mafunzo makubwa, aliwasumbua vijana wake kwa kipindi kirefu, leo hii alikutana naye porini.

Watu hao walikuwa na silaha mikono mwao na Dickson hakuwa na kitu chochote kile. Kila alipowaangalia, aliona kabisa kwamba kifo kipo mbele yake, hakutaka kujiuliza nini cha kufanya, hapohapo akaanza kukimbia. Savimbi na vijana wake wakaanza kumkimbiza huku wakimrushia risasi. Mbali na kupambana, Dickson alikuwa mtu hatari katika kukwepa, hakukimbia moja kwa moja, alikimbia kwa staili ya zigzag tena katika miti iliyokuwemo mle porini.

Risasi zote alizokuwa akirushiwa alizikwepa vyema na kupiga kwenye miti. Mahali hapo kulikuwa na pori kubwa, alijitahidi kukimbia kwa tahadhali, japokuwa mguu wake mmoja ulikuwa na kidonda kikubwa lakini hakujali, hakutaka kusimama, aliendelea mbele huku akiruka kila kizuizi alichokutana nacho njiani. Savimbi na vijana wake hawakutaka kukata tamaa, waliendelea kumkimbiza Dickson lakini mwanaume huyo alikuwa na kasi kubwa hivyo kuona wakiachwa taratibu na baada ya dakika chache, Dickson akawapotea. “Yupo wapi?” aliuliza Savimbi huku akihema kama mbwa.

Walimtafuta sehemu hiyo lakini hawakumpata, hawakujua kama Dickson aliendelea kukimbia au alijificha sehemu fulani. Walichokifanya kama kumtisha ni kuanza kupiga risasi mfululizo kila upande ili kama amejificha atoke alipokuwa lakini bado kulikuwa na ukimya. “Atakuwa ametuacha, ana bahati sana, ningemuua na kumla nyama, katusumbua sana huyu mtu, katukosesha sana madili,” alisema Savimbi kwa hasira.

Wakati wakiyazungumza hayo, Dickson alikuwa mbali kabisa, aliendelea kukimbia, mguu ulikuwa ukimuuma sana lakini hakutaka kusimama, bado aliendelea mbele huku akichechemea. Hakukuwa na sauti za vitu vingine zilizokuwa zikisikika zaidi ya ndege tu. Aliendelea kwenda mbele huku akichechemea mpaka alipofika sehemu ambayo aliamini kwamba angeweza kupumzika kwani kadiri muda ulivyokuwa ukienda mbele na ndivyo alivyozidi kuchoka na mguu kuuma zaidi.

Akatulia sehemu iliyokuwa na miti mingi iliyotengeneza kama chumba fulani na kukaa hapo. Mguu ulikuwa kwenye maumivu makali, hakuwa na dawa wala kitu chochote kile, alichokifanya ni kuchukua majani kisha kuanza kufuta damu zilizoendelea kutoka katika kidonda. Muda ulikuwa umekwenda sana, ilikuwa ni saa kumi jioni, mwili ulichoka na macho yake yalikuwa mazito mno. Hakutaka kubaki macho, ilikuwa ni lazima apumzike hata kabla ya kuendelea na safari yake. Akajikuta akipitiwa na usingizi mzito.

Mara baada ya saa mbili, Dickson akashtukia akiamshwa hapo alipolala, sauti iliyosikika ikimuamsha haikuwa ya amani hata kidogo, ilikuwa ni sauti iliyojaa amri, akayafumbua macho yake kuangalia ni nani aliyekuwa akimwamsha.
Kitu cha kwanza kabisa kukiona kilikuwa ni mdomo wa bunduki. Dickson akashtuka, akayaona maisha yake kuwa hatarini, hata kabla hajasema kitu chochote, mtu huyo akamkandamiza na mguu wake palepale chini.
“Tulia hivyohivyo, nimekutafuta sana mpumbavu wewe,” alisema mwanaume huyo huku akiwa na hasira, hapohapo akaanza kuikoki bunduki yake tayari kwa kumfyatulia risasi Dickson pale chini alipomkandamiza.
* * *
Kwa kumwangalia usoni tu, Fredrick hakuonekana kuwa mtu wa kawaida, alionekana kuwa mtu hatari aliyekuwa na mafunzo makubwa ya kupambana na watu wengi.
Japokuwa aliambiwa kwamba anyooshe mikono juu lakini hakutaka kufanya hivyo ndiyo kwanza alibaki akiwaangalia watu hao huku uso wake ukionesha kama mtu aliyekuwa akihitaji kitu fulani kutoka kwao.
“Nimewauliza swali, mnanikumbuka?” aliuliza Fredrick, alionekana kuwa mwanaume jeuri.

Wao ndiyo walikuwa na silaha mikononi mwao lakini hawakuonekana kujiamini, walihisi kwamba hata kama watamrushia mishale, mwanaume huyo angeikwepa na kuwafuata. Wakajikuta wakizishusha silaha hizo chini na kumwangalia. Hapohapo Fredrick akaanza kupiga hatua kuwafuata watu hao, alipowafikia, akasimama karibu yao na kuanza kuzungumza nao. “Ninamtafuta mtu mmoja hivi, inasemekana alipita hapa,” alisema Fredrick.

“Nani?”
“Mwanaume mmoja mwenye sura mbaya, mmemuona?” aliuliza. Wanaume hao wakabaki kimya kwanza, walimuona mtu huyo, aliyekuwa akizungumziwa alikuwa Dickson, mwanaume mwenye sura mbaya ambaye naye aliwasulubu baada ya kutaka kumfunga kwenye mti. Kama alivyokuwa huyo mwanaume aliyesimama mbele na ndivyo alivyokuwa Dickson, naye alionekana kuwa mtu wa mapambano ambaye hakutakiwa kufuatwa hovyo.
“Tulimuona ni mtu hatari sana,” alijibu mwanaume mmoja.
“Lini?”
“Siku mbili zilizopita. Tulikuwa watu kama wanne hivi, akatupiga wote, ila tulimjeruhi mguuni kwa mshale,” alisema mwanaume huyo.

“Alielekea wapi baada ya kuondoka?” “Hatujui, alitupiga na kuzimia, hatukujua alielekea wapi,” alijibu mwanaume huyo.
Fredrick alikasirika, alitumia muda wake mwingi kutembea pori kwa pori mpaka kufika mahali hapo na mwisho wa siku kuambiwa kwamba mtu huyo alipita mahali hapo siku mbili zilizopita. Walichokifanya wanakijiji hao ni kumchukua na kumpeleka nyumbani kwao na kumtaka kukaa huko japo kwa saa kadhaa kabla ya kuendelea na safari yake ya kumtafuta huyo mtu aliyekuwa akimtafuta.

Wanakijiji walikuwa na maswali mengi juu ya huyo mtu, alionekana kuwa mgeni mahali hapo lakini wakulima wale walizungumza naye kila wakati kama mtu ambaye walikuwa wakifahamiana naye kwa kipindi kirefu. Ingawa wanakijiji hao walimuuliza sababu za kumtafuta huyo mtu zilikuwa zipi, Fredrick hakujibu, hakutaka mtu yeyote afahamu lolote lile kwa kuhisi kwamba inawezekana Dickson angepata taarifa kwamba nyuma kulikuwa na mtu aliyekuwa akimtafuta.

“Hatakuwa mbali kutoka hapa ni lazima niendelee kumtafuta,” alisema Fredrick, hakutaka kukaa kijijini hapo.
Siku hiyohiyo akaondoka kuendelea na safari yake, mbele yake kulikuwa na kazi kubwa sana ambayo ilikuwa lazima aikamilishe haraka iwezekanavyo.

Je, nini kitaendelea na je Fredrick atafanikiwa kumpata Dickson?
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom