Kanungila Karim
JF-Expert Member
- Apr 29, 2016
- 20,744
- 25,444
Mtunzi : Eric J Shigongo
SEHEMU YA 01
Sauti kubwa ya muziki ilikuwa ikisikika, huku watu wengi wakionekana kurandaranda huku na kule katika eneo maarufu la Sinza Afrikasana jijini Dar es Salaam. Japokuwa ilikuwa ni usiku wa manane, mandhari ya mahali hapo ilikuwa imechangamka mno utafikiri mchana.
Taa za rangi mbalimbali zilikuwa zikimulika huku na kule, sauti kubwa ya muziki ikazidi kupachangamsha mahali hapo ambapo kulikuwa na baa kadhaa zilizojipanga ambazo zote zilikuwa zikikesha mpaka asubuhi. Idadi ya wanawake waliokuwa eneo hilo, ilikuwa kubwa ukilinganisha na wanaume. Wanawake wa kila rika, wasichana wadogo, wa makamo na wanawake watu wazima, walikuwa wakizungukazunguka huku na kule, tena wakiwa wamevalia mavazi ambayo yaliacha wazi sehemu kubwa za miili yao.
Kama ndiyo mara yako ya kwanza kufika eneo hilo, ungeweza kudhani zile zama za Sodoma na Gomora zimerejea tena kwani uchafu mkubwa ulikuwa ukifanyika hadharani, huku kukiwa hakuna mtu anayejali, kila mmoja akiendelea na shughuli zake.
“Psii! Psiii! Njoo basi anko, si unaniona nilivyo bomba?” nichukue mimi ukafurahi, hata ukitaka usiku kucha ni wewe tu na roho yako,” msichana mmoja alisikika akiongea kwa sauti ya kilevi, huku akipandisha juu kisketi kifupi alichokuwa amevaa, wakati akizungumza na mwanaume aliyekuwa ndani ya gari dogo, akitafuta sehemu ya kuegesha gari hilo.
Mwanaume huyo aliposimamisha gari lake, wanawake wengine wengi walilizunguka gari lake na kila mmoja akawa anatangaza ‘biashara’ yake. Baada ya majadiliano yaliyochukua dakika chache, mlango ulifunguliwa, mmoja kati ya wale wanawake akaingia kwenye gari kisha likaondoka kwa kasi eneo hilo.
Hali ilikuwa hivyohivyo, magari mengi ya kila aina yakawa yanakuja eneo hilo na kuondoka yakiwa na wanawake hao ambao bila hata kuuliza, ungeweza kugundua kwa urahisi kwamba walikuwa wakifanya biashara haramu ya ngono iliyokuwa inasifika mno katika eneo hilo.
Wale ambao hawakuwa na magari, nao hawakuwa nyuma, walikuwa wakifika eneo hilo kwa teksi za kukodi, Bajaj au bodaboda huku wengine wakitembea kwa miguu. Baada ya makubaliano, kila mtu alikuwa akiondoka na wake. Kadiri muda ulivyokuwa unasonga mbele ndivyo watu walivyokuwa wanazidi kuongezeka eneo hilo huku pilikapilika zikizidi kupamba moto.
Saa tisa na dakika kadhaa za usiku, gari jipya la kisasa aina ya Volkswagen lenye rangi nyeusi liliwasili eneo hilo, kama kawaida akina dada hao walilikimbilia na muda mfupi baadaye, changudoa maarufu wa eneo hilo, Aisha au Ndembendembe kama wengi walivyokuwa wanamfahamu, alipanda kisha gari hilo likaondoka kwa kasi. Pilikapilika ziliendelea mpaka kulipoanza kupambazuka ambapo watu walianza kupungua na ilipofika majira ya saa kumi na mbili za asubuhi, eneo lote lilikuwa kimya kabisa baada ya watu wote kuondoka.
Kulipopambazuka kabisa, watu mbalimbali waliendelea na shughuli za kawaida eneo hilo kiasi kwamba kama ulikuwa mgeni, usingeweza kujua chochote kinachoendelea mahali hapo giza likiingia. Saa ziliyoyoma na hatimaye giza likaanza kuingia tena. Kama kawaida, watu kutoka sehemu mbalimbali wakaanza kumwagika kwa wingi eneo hilo, wanawake wanaofanya biashara haramu ya kuuza miili yao nao wakaingia kazini kama kawaida. Mambo yalianza taratibu lakini kadiri muda ulivyokuwa unakwenda mbele ndivyo eneo hilo lilivyozidi kuchangamka.
“Jamani leo Aisha Ndembendembe mbona hajafika mpaka saa hizi wakati yeye ndiye anayesifika kwa kuwahi?” changudoa mmoja alimuuliza mwenzake lakini hakuna aliyekuwa na jibu. Wakajua huenda kuna sehemu alikuwa amepitia, kila mmoja akaendelea na kazi ya kuwinda wateja mpaka usiku wa manane.
Magari yaliendelea kumiminika kwa wingi kama kawaida na kila lililokuwa linafika eneo hilo, lilikuwa likiondoka na changudoa. Saa tisa juu ya alama, lile gari lililofika eneo hilo siku moja iliyopita, Volkswagen la kisasa kabisa, lenye rangi nyeusi na vioo vyenye ‘tinted’, liliwasili na kuegesha pembeni.
Kama kawaida, wanawake wa kila aina wasiopungua kumi walilizunguka na kuanza kujinadi kwa dereva ambaye alikuwa ameshusha kioo kidogo, mahali palipomtosha kuzungumza na watu wa nje tu ila siyo yeye kuonekana. Baada ya kuridhika na changudoa mmoja, Sikitu ambaye alikuwa akisifika kwa kupenda kupigana na machangudoa wenzake kugombea wanaume, aliingia na kukaa siti ya nyuma. Gari likaondoka kwa kasi na kutokomea kusikojulikana.
Kama ilivyokuwa kwa Aisha Ndembendembe, Sikitu naye hakurejea tena tangu alipochukuliwa usiku huo. Hata hivyo, hakuna aliyetilia maanani sana, wenzao wakawa wanahisi wamepata fedha nyingi hivyo wanaendelea kuzitumia mpaka ziishe kama ilivyokuwa kawaida yake.
Siku ya tatu iliwadia, kama kawaida ya eneo la Sinza Afrikasana, pilikapilika zilianza pale tu giza lilipoingia. Biashara ya ukahaba ikaendelea kufanyika waziwazi usiku kucha. Kama ilivyokuwa kwa siku mbili zilizopita, ilipofika majira ya saa tisa za usiku, Volkswagen nyeusi yenye vioo vya tinted iliwasili eneo hilo na kupaki pembeni.
“Anko leo nichukue mimi, kila siku unanikataa unawachukua wenzangu, kwani mimi siyo mzuri? Cheki nilivyojazia,” alisema changudoa mmoja machachari ambaye wenzake walimbatiza jina la utani la Lily Mcharuko, akaendelea kumfanyia vituko dereva huyo mpaka alipomuoneshea ishara kwamba aingie ndani ya gari.
Akaondoka naye na kutokomea kusikojulikana. Siku iliyofuatia, Lily hakuonekana kabisa wala lile gari halikuonekana kufika eneo hilo. Siku kadhaa baadaye, liliendelea kuja na kuchukua machangudoa wengine ambao baada ya kuchukuliwa, hawakuonekana tena eneo hilo, jambo lililoanza kuzusha hofu kwa wenzao.
“Jamani mbona wenzetu wanapotea kimaajabu na hakuna mwenye taarifa zozote?” aliongea changudoa mmoja katika mkutano ambao haukuwa rasmi usiku mmoja, wakaanza kujadiliana kwani ilionesha dhahiri kuna jambo halikuwa sawa.
“Lile gari jeusi lina nini? Mbona kila anayelipanda harudi tena hapa wala simu yake haipatikani tena?”
“Jamani ee, wasiwasi wa nini? Huenda yule bosi anatoa fedha nyingi mpaka kila anayetoka naye anaamua kuacha kazi ya uchangudoa,” alisema changudoa mmoja na kushambuliwa vikali na wenzake ambao walimtaka kutoleta masihara wakati wenzao walikuwa wakizidi kupukutika.
Mjadala mkali uliendelea na muafaka waliofikia, ilikuwa ni kwenda kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kwani walishindwa kupeleka malalamiko hayo polisi kwani kazi yao haikuwa halali kisheria na mara kwa mara walikuwa wakisumbuana na polisi waliokuwa wanawavamia eneo hilo na kuwakamata. Kutokana na mtandao mpana waliokuwa nao machangudoa hao, habari zilisambaa kwa kasi kubwa.
“Mpaka sasa wenzenu wangapi wamepotea?”
“Wenzetu kumi na moja hawafahamiki walipo, kwa kweli hali ni mbaya sana, tunawaomba nyie waandishi wa habari mtusaidie kufikisha taarifa sehemu husika, tunakwisha jamani,” changudoa mmoja ambaye hakutaka jina lake wala sura vionekane, alikuwa akizungumza na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali ambao walifika eneo hilo baada ya habari kuanza kusambaa.
Habari zilisambaa kama moto wa nyikani kuhusu kupotea kimaajabu kwa machangudoa hao ambao walikuwa wakichukuliwa na mtu aliyekuwa anaendesha gari jeusi aina ya Volkswagen.
Ndugu wa waliopotea walianza kujitokeza ambapo familia mbili kutoka Tandale Kwa Mtogole zilidai kupotelewa na mabinti zao wawili kwa siku mbili tofauti. Familia hizo zilipotoa picha ya watoto wao, machangudoa wenzao waliwatambua kuwa ni wenzao.
“Mungu wangu, kumbe mwanangu alikuwa anafanya uchangudoa?” mwanamke mmoja aliangua kilio kwa nguvu kwenye eneo hilo baada ya machangudoa kadhaa kukiri kumfahamu binti yake na kueleza kuwa alikuwa mwenzao.
“Alikuwa ananiaga anasema anafanya kazi kiwanda cha soda na kila siku anapangiwa shifti za usiku,” aliendelea kueleza mwanamke huyo huku akilia kwa uchungu mno. Mambo mengi yalizidi kufichuka ambapo ndugu wengine waliendelea kujitokeza na kueleza kupotelewa na ndugu zao. Hata hivyo, kati ya waliopotea, ni ndugu wa wasichana wanne tu ndiyo waliojitokeza na kukiri hadharani kupotelewa na ndugu zao.
Utambulisho wa wasichana wengine waliopotea ulikuwa mgumu kwani hakukuwa na taarifa zozote za kina lakini kutokana na habari hiyo kuanza kutawala kwenye vyombo mbalimbali vya habari, ukweli ulizidi kufichuka kila kukicha na kuzidi kuwashangaza wengi kuhusu wanawake waliokuwa wakijihusisha na biashara ya uchangudoa na kilichokuwa kinawapata.
Je, nini kitafuatia? Machangudoa wanaopotea wanakwenda wapi?