DR Mambo Jambo
JF-Expert Member
- May 10, 2012
- 12,622
- 28,459
Wiki hii, tulichangamshwa na habari juu ya kuibuka kwa kundi jipya linalojiita G55 ndani ya chama kikuu cha upinzani nchini, CHADEMA.
Kutambulishwa rasmi kwa kundi hili kulitanguliwa na kuvuja kwa mawasiliano ya kundi la WhatsApp linalojiita G55. Mawasiliano haya yalivuja wakati uongozi wa CHADEMA ukiwa umeitisha kikao na wanachama wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu—huku msimamo rasmi wa chama ukiwa ni #NoReformsNoElection, yaani kususia uchaguzi endapo sheria za uchaguzi hazitaboreshwa.
Katika mawasiliano hayo, aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema, alisikika akihamasisha wenzake kutohudhuria mkutano huo. Alidai kwamba kutoenda kwao kutatoa ujumbe kuwa hawakubaliani na msimamo wa chama, na pia kuwakwepa "kufokewa".
Miongoni mwa waliotajwa kuwa wanachama wa kundi hilo ni aliyekuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Boniface Jacob. Hakuna aliyejitokeza kukana kuhusika na kundi hilo, badala yake baadhi yao waliamua kujitokeza hadharani na kuthibitisha kuwepo kwao ndani ya G55, huku wakitoa msimamo wao.
Lakini kwa nini jina G55?
Historia Inajirudia?
Kundi hili linajifananisha na lile la mwaka 1993, ndani ya CCM, ambapo wabunge 55 walijitokeza kuunga mkono hoja ya mbunge wa Chunya, Njeru Kasaka, aliyependekeza kuundwa kwa Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano. Hoja hiyo iliwasilishwa kufuatia hatua ya Zanzibar kujaribu kujiunga na Jumuiya ya Kiislamu (OIC) bila ridhaa ya Serikali ya Muungano.
Wabunge hao 55 walichachafya serikali ya Rais Ali Hassan Mwinyi, na hoja yao ilitishia uimara wa Muungano. Miongoni mwa wabunge waliokuwa sehemu ya kundi hilo ni
- Edward Oyombe (Rorya),
- Lumuli Kasyupa (Kyela),
- Phares Kabuye,
- Sebastian Kinyondo (Bukoba), na
- Twaha Ulimwengu maarufu kama "Jenerali Ulimwengu" (mbunge wa kuteuliwa).
- Edward Oyombe Ayila – Aliteuliwa kuwa Balozi, akipelekwa kuwakilisha Tanzania katika nchi za Afrika Mashariki.
- Sebastian Rweikiza Kinyondo – Aliteuliwa kuwa Naibu Waziri katika moja ya wizara muhimu.
- Lumuli Kasyupa – Aliteuliwa katika moja ya bodi za taasisi nyeti za serikali.
- Twaha Ulimwengu "Jenerali" – Alishikilia nafasi ya ushauri wa kisera serikalini.
Kuibuka kwa G55 mpya ndani ya CHADEMA kunaibua maswali mengi kuhusu afya ya demokrasia ya vyama vingi nchini. CHADEMA, ambacho kimekuwa kinapigania mabadiliko ya kisiasa kwa miaka mingi, sasa kinakumbwa na changamoto ya msimamo wa ndani.
Je, kundi hili ni dalili ya ukosefu wa maridhiano ya kimkakati ndani ya chama, au ni njia ya kutafuta mwelekeo mpya wa kisiasa?
Katika demokrasia, tofauti za kimtazamo ni sehemu ya ukuaji. Lakini pale tofauti hizo zinapozua migawanyiko mikubwa na kuvuja kwa taarifa za ndani, huashiria kasoro kubwa ya mawasiliano na maelewano ya ndani ya chama. Kama CHADEMA haitadhibiti mvutano huu kwa njia ya kidemokrasia, kuna hatari ya kudhoofika zaidi kuelekea uchaguzi mkuu.
Lakini pia, kama ilivyokuwa kwa G55 ya mwaka 1993, kundi hili linaweza kuwa chachu ya mageuzi ya kweli—kwa chama chenyewe na kwa siasa ya Tanzania kwa ujumla.
Historia imetuonyesha kuwa pale hoja yenye msingi inapowasilishwa kwa nguvu na msimamo wa pamoja, inaweza kuibadilisha nchi. Swali linabaki: Je, G55 ya CHADEMA ni sauti ya mabadiliko au ishara ya mgawanyiko?
Wakati ndio utakaotoa majibu.