SoC02 Fumbo na jawabu la Utawala Bora

Stories of Change - 2022 Competition

Lidafo

JF-Expert Member
Sep 26, 2019
551
748
Kwanza kabisa nipende kumshukuru mungu kwa nafasi hii, Natumai sote tuwazima. Wenye maradhi na shida mbalimbali mungu awaongoze na awasaidie.


UTANGULIZI .

Nini maana ya utawala ?
Utawala ni Hali ya kuwa na mamlaka na haki ya kuongoza. Dhana hii ya utawala ndio itakae tupeleka katika dhana nyingine ya utawala Bora.

Utawala Bora ni utawala unaotoa miongozo ya jinsi gani mtawala anatakiwa kuongoza, kuwajibika na kuwajibishwa kulingana na misingi ya Sheria.

Kwa ufupi ni kwamba ili utawala uwe Bora una misingi na sifa zake sifa hizo ndio zinatumika kupima ubora wa utawala. Kupatikana na kufuatwa kikamilifu kwa sifa hizi ni ishara ya moja kwa moja kwamba nchi husika ama jamii husika ina utawala bora na kinyume chake ni ishara ya wazi kabisa kuwa hakuna utawala Bora katika jamii au nchi husika.


Misingi na sifa za utawala bora.

Miongoni mwa sifa za utawala Bora ni pamoja na uwazi, ushirikishwaji wa wananchi, utawala wa Sheria, uwajibikaji,usikivi na usawa.

Ni vizuri tufahamu kwamba utawala Bora unaanza katika ngazi za juu kabisa za uongozi yaani serikali kuu mpaka ngazi za chini kabisa yaani serikali za mitaa.


Hapa tuangalie Mambo machache juu ya sifa za utawala Bora .

Uwazi, Katika jamii zetu tumekuwa tukiona jinsi ambavyo Kuna kugongana kwa taarifa katika baadhi ya mamlaka , Si ajabu leo hii kukuta kuna ukinzani wa taarifa baina ya mamlaka tofauti ambazo zote zinafanya kazi katika serikali moja.

Hii ni dalili kubwa ya kwamba hakuna uwazi wa taarifa katika tawala zetu, Jambo linalohamsha fikra hasi kwa wananchi . kwamba Kama Jambo dogo la uwazi wa taarifa na maagizo mbalimbali yanakinzana vipi weledi na uwazi juu ya mikataba na taarifa muhimu kuhusu nchi.

Pili, Utawala wa Sheria. Sheria katika jamii zetu zipo na zimebainishwa wazi katika katiba yetu.
Hapa swala la misingi ni je utawala katika jamii zetu unafuata Sheria? Kama jibu ndio je Sheria zinafuatwa kwa kiwango gani? Kama jibu ni hapana je viongozi wetu na jamii kwa ujumla hawaoni huu ni ukiukwaji wa wazi kabisa wa misingi ya utawala Bora.

Hata hivyo ukilitazama Jambo hili kwa jicho la tafakari utagundua kinachoiumiza jamii sio ubovu wa Sheria tu, Bali ni hata Sheria zilizopo hazifuatwi kwa weledi. Hapa tunapata swali lingine la msingi ikiwa wanaotakiwa kuwajibisha viongozi kwa mujibu wa Sheria wao hawafuati Sheria je ni nani Basi wakuwawajibisha viongozi ?
Hata hivyo katika andiko hili nitajitahidi kujibu baadhi ya maswali ili kuleta chachu ya mabadiliko katika nchi yetu na ustawi mzuri wa jamii.

Tatu ni ushirikishwaji wa wananchi,usikivi, uwajibikaji na usawa. Mambo yote haya ni sifa za utawala Bora, Kumekuwa na Tabia ya viongozi kuhimiza wananchi kushiriki katika upigaji wa Kura lakini baada ya chaguzi mawazo ya wananchi na ushauri wao hauzingatiwi.

Hii ni kusema kwamba kasi ya watawala katika jamii haiendani na matarajio ya raia. Usikivu na usawa wa utekelezaji wa mahitajio ya wananchi umekuwa haupewi kipaumbele na watawala wengi.

Baada ya kuona misingi na sifa za utawala bora japo kwa kifupi sasa sote tujiulize je jamii tuliyonayo na serikali zetu zinafuata misingi ya utawala bora?


Faida za utawala bora

Ikiwa nchi itafuata misingi ya utawala Bora faida zifuatazo zitapatikana
  • Utawala Bora huleta ustawi wa wananchi​
  • Kuwepo kwa matumizi mazuri ya rasilimali na matumizi mazuri ya Mali za umma.​
  • Huduma nzuri na Bora kwa jamii na kuheshimiwa kwa haki za binadamu.​
  • Utatuzi wa migogoro kwa haki na kwa mujibu wa sheria.​
Faida tajwa hapo juu ni matunda yatokanayo na utawala Bora. Hivyo kukosekana kwa faida hizi ni ishara ya wazi kuwa hakuna utawala Bora .

Sasa tujiulize tena katika jamii zetu je Kuna matumizi mazuri ya rasilimali?, Kuna huduma nzuri za kijamii vipi kuhusu huduma za afya, Elimu, Mafao, Bima na huduma nyengine nyingi za serikali, Vipi kuhusu rushwa na ufuataji wa Sheria rejea sakata la ESCROW na RICHMOND hiyo ni mifano michache ya kuamsha fikra zetu.


Kipi kifanyike kuupata utawala Bora.

Hapa nitaeleza ni vitu gani vifanyike ili kuupata utawala Bora
  • kuchagua kiongozi Bora na mwenye maono
Kama Kuna sababu ya msingi ya kufikia utawala Bora ni kupata kiongozi mwenye maono ,Kiongozi Bora ataweza kuweka misingi Bora na kuteua viongozi Bora wakumsaidia hapa ni lazima ieleweke kuwa siku zote uongozi wa juu ukiwa imara unaleta athari kwa uongozi wa chini kinyume chake ni kwamba uongozi wa juu ukiwa mbovu tutegemee maumivu.

Hili ni suala la Kila mwananchi kutambua kuwa utawala bora unaanza kujengwa na Mimi na wewe hivyo ni jukumu la Kila mtanzania kuwapima viongozi katika chaguzi mbalimbali ni muhimu tutambue kuwa haitatokea siku tumeamka tukakuta tayari tuna utawala bora. Hapa ni muhimu kuweka tanbihi.

Suala la kiongozi Bora na mwenye maono haliaangalii itikadi zetu za dini, uchama Wala ukabila hivyo ni muhimu kuepuka Mambo hayo katika mchakato wa kumpata kiongozi bora.
  • Kutoa elimu kwa wananchi juu ya utawala Bora
Hili ni suala la Kila mwenye uelewa juu ya utawala Bora kufundisha angalau watu wawili mpaka kumi juu ya utawala Bora lakini pia asasi zisizo za serikali ,vyombo vya habari na serikali kwa ujumla viwajibike kutoa elimu katika jamii
  • Kuipa nguvu wizara ya menejimenti ya utumishi wa umma na utawala Bora
Serikali kupitia wizara ya menejimenti ya utumishi wa umma na utawala Bora inalojukumu la kuhakikisha jamii inayouelewa juu ya dhana ya utawala bora hivyo ni muhimu pia kuipa nguvu wizara hii ili iweze kuwajibika ipasavyo .Hivyo ni wakati sasa wa wizara chini ya MHE.JENISTA .J. MHAGAMA kujitafari, Je elimu inayotolewa inakidhi na kutosha kujenga uelewa wa kutosha kwa jamii juu ya utawala bora.

HITIMISHO
Suala la utawala Bora ni suala mtambuka lenye maelezo marefu lakini kwa ufupi ni jukumu la serikali na viongozi wenye mamlaka sasa kuchukua hatua madhubuti katika kuendea utawala bora hili litafikiwa na msukumo tutakao utoa wananchi ikiwemo kuwawajibisha viongozi na kushauri serikali yetu kuanzia ngazi ya taifa mpka mtaa tusipo fanya hivi tutajikuta katika jamii ambayo hata "mgaagaa na upwa atakula wali mkavu".

Karibuni kwa maoni

Mwandishi: Shafii .R. Bakari

ASANTENI.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom