Familia yagoma kumzika ndugu anayedaiwa kuuawa kwa kipigo

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,376
8,118
Mwili wa Ibrahim Shakiru (16) utaendelea kusalia katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Bugando mpaka pale familia ya mtoto huyo itakapoelezwa hatua zilizochukiliwa dhidi ya watu waliomshambulia na kusababisha kifo cha mtoto wao.

Ibrahim anadaiwa kufariki Jumatano Oktoba 26, katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando alikokuwa akitibiwa majeraha aliyoyapata kwa kipigo kutoka kwa askari wa ulinzi shirikishi (mgambo) wakishirikiana na walimu wa Shule ya Sekondari Kirumba.

Inadaiwa kuwa mgambo na walimu hao walimkamata Ibrahim Jumamosi Oktoba 22, akiwa na panga jirani na ukumbi wa Shule ya Sekondari Kirumba yalipokuwa yanafanyika mahafali ya kidato cha nne.

Mwili wa Ibrahim, ambaye ni mkazi wa Mtaa wa Songambele kata ya Kirumba wilayani Ilemela mkoani Mwanza umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Bugando wakati familia ikisubiri hatua walizochukuliwa waliohusika na tukio hilo.

Alivyoshambuliwa

Shuhuda wa tukio hilo, Juma Athuman (siyo jina halisi) aliieleza Mwananchi kuwa siku hiyo alishuhudia mwalimu anayemtambua kwa jina la Mtaki na mwingine hamjui jina lake na mgambo wawili, Omera na Kodo wakimpiga rafiki yake.

“Mwingine alikuwa ameshika mpini wa jembe akimpiga nao kichwani na virungu, sasa wakati wanampiga nikawa nawauliza kwani Ibrahim amefanyaje mpaka mnampiga hivi? Nikaambiwa wamemkuta ametunza panga,” alisema Juma.

Juma alisema anafahamu kuwa Ibrahim alikuwa na panga ambalo hulitumia katika shughuli ya kuparua na kukata samaki katika Soko la Mwaloni Kirumba wilayani Ilemela mkoani hapa.

Alisema baada ya watu hao kumuingiza katika chumba kilichopo shuleni hapo, waliendelea kumpiga hadi alipopoteza fahamu kisha kumpakiza kwenye bajaji na kutokomea naye sehemu ambayo hakuitambua.

“Kama kosa lake ni kukutwa na panga kwa nini walijichukulia sheria mkononi badala ya kumpeleka kituoni akasikilizwe. Ninavyomjua Ibrahim hakuwa mwizi, alikuwa anatafuta hela zake mwenyewe hapo sokoni ndiyo anamhudumia bibi yake,” alisema.

Kaka wa marehemu, Fadhiri Kachwamba aliieleza Mwananchi kuwa alipigiwa simu Jumamosi saa 11:30 jioni na rafiki yake Ibrahim, akimtaarifu kuwa ndugu yake amepelekwa katika Kituo cha Polisi Kirumba baada ya kupigwa na watu aliowataja kuwa ni walimu na mgambo.

Anasema Jumapili ya Oktoba 23, alikwenda kituoni hapo, lakini hakumkuta huku akielezwa kuwa ndugu yake amepelekwa katika Hospitali ya Mkoa Sekou Toure kutibiwa majeraha aliyoyapata kutokana na kipigo hicho.

“Nikiwa na rafiki zake wawili wa kike tulikimbia hadi Sekou Toure tukamkuta amelazwa akipumua kwa usaidizi wa mipira maalumu, ilipofika Jumatatu wakasema wanamhamishia Hospitali ya Bugando, ambapo alibebwa kwenye gari la wagonjwa kuelekea Bugando ambako alilazwa wodi namba sita chumba namba tatu,” alisema Kachwamba.

Alisema ilipofika Jumanne madaktari waliwataka wawe na subira ili damu ianze kutembea kichwani ili afanyiwe kipimo cha X-ray, jambo ambalo halikufanikiwa, badala yake alipewa taarifa ya kifo cha Ibrahim Jumatano ya Oktoba 26.

Hata hivyo, mwandishi wa gazeti hili apofika hospitalini hapo kujua daktari alibaini nini kwenye vipimo vya Ibrahim, hakupata ushirikiano.

Alipotafutwa Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk Fabian Massaga alisema kutokana na unyeti wa taarifa hizo hawezi kuzisema kwenye simu, anayezitaka afike hospitalini kwa sababu hajui kuhusu kuwepo au kutokuwapo kwa kijana huyo hospitalini hapo.

Danadana polisi

Fadhiri anadai pamoja na kuugulia maumivu ya kumpoteza Ibrahim, hawajapata majibu ya hatua ambazo zimechukuliwa dhidi ya watu wanaodaiwa kusababisha kifo cha mpendwa wao.

Alisema taarifa ya fomu namba tatu (PF3) iliyosainiwa katika kituo cha Polisi Kirumba na G.2473 Koplo Mussa yenye namba ya faili MZA/RB/10960/2022 imeonyesha kuwa Ibrahim alishambuliwa na wananchi ambao hawakutajwa majina yao.

“Kila tukienda kituoni pale tunaambiwa huyu mdogo wako alikuwa na wenzake wameenda kuvamia shuleni wakiwa na mapanga tukabahatika kumkamata, wenzake wakakimbia na panga lake liko kituoni,” alisema.

“Wanaodaiwa kutenda unyama huu wanatambulika kuwa ni askari wa polisi jamii na walimu wa Sekondari ya Kirumba, kwa nini wasiende kufuatilia, badala yake wananiambia nikawalete watu wanaosema wameshuhudia tukio hilo,” alihoji.

Kijana huyo ambaye pia alikuwa anafanya kazi ya kuparua samaki na Ibrahim, aliiomba Serikali kuingilia kati suala hilo ili haki itendeke na waliokatisha maisha ya ndugu yake wachukuliwe hatua za kisheria.

Kauli za bibi

Kifo cha mtoto huyo kimeacha simanzi kwa bibi yake, Nyamisi Masinye (73) ambaye anadai taa iliyokuwa ikiangaza maisha yake imezima, kwani alikuwa akitegemea kipato cha mjukuu wake kuishi. Nyamisi, ambaye ni mama mlezi wa Ibrahim alisema mjukuu wake alisoma hadi kidato cha pili na kulazimika kukatisha masomo 2020 ili kutafuta kazi ya kuihudumia familia yake.

“Mimi ndiyo nilikuwa mama, baba, bibi na babu wa huyu mtoto, nimeteseka mno kumlea hadi amekuwa mtu mzima, alikuwa anafanya kazi zake za kuparua na kukata kata samaki tunapata hela ya kuendesha familia yetu, sasa wamemuua nitaishije...,” alisema.

Alisema jambo linaloumiza ni kuona hakuna taarifa za kukamatwa kwa watu waliomshambulia. “Nasisitiza familia haitazika mwili wa mjukuu wangu hadi pale hatua za kisheria zitakapochukuliwa dhidi ya waliotekeleza unyama huo.

“Mpaka sasa nikienda kituoni Kirumba wananiambia niwapeleke watu walioshuhudia, hivi kwa uzee huu nitaweza kweli? Jana (Jumamosi) nimekwenda kumuona RPC sikumkuta, wasaidizi wake wamenirudisha tena kwenye kituo cha Kirumba ambako naishia kuzungushwa tu,” alisema.

Kauli ya DC, polisi

Akijibu swali aliloulizwa kuhusu tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masala alisema taarifa ya kifo cha mtoto huyo hazijafika ofisini kwake, huku akimtaka mwandishi awasiliane na maofisa wa polisi kwa taarifa za uhakika.

Alipotafutwa kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi (RPC) Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa alisema bado hajaripoti kazini.

Baada ya kumtafuta Afande Gideon Msuya ambaye huwa anakaimu nafasi hiyo, alidai yuko nje ya ofisi na nafasi hiyo inakaimiwa na afande Mairi Makori, ambaye simu yake ya mkononi haikupatikana na ya ofisini haikupokelewa.

MWANANCHI
 
Sasa watu wapo kwenye mahafali ww unakuja Na panga aisee!! Ila mm sidhani kama hao walimu waliamua kumpiga bila sababu lazima Kuna jambo Dogo alifanya japo Sio tiketi YA kumpeleka kuzimu.
 
Kwahiyo ilikuwa ni bora ajeruhi wanafunzi na panga lake kuliko yeye kujeruhiwa. Ni vyema wazazi wawe wanafatilia watoto wao kabla hayajawakuta haya ili kuepuka mabalaa.

Niliwahi toa shuhuda humu.

2019 usiku mmoja nilivamiwa na vijana wawili wa rika la huyo dogo kwakweli walinipa kipondo cha kutosha almanusra wanitoe roho kwa roba niliyopigwa ilibidi nijiokoe kwa kuwatandika visu maeneo mbalimbali.

Kimbembe kilianza baada ya kukamatwa, nilisota mahabusu miezi miwili eti mpaka wapone. Nashukuru nilishinda kesi baadae. Wazazi wao walichachamaa eti vijana wao hawana tabia ya wizi kama huyo bibi anavyodai.

Niliumia na kufadhaika sana na jambo Hilo.
 
Sasa watu wapo kwenye mahafali ww unakuja Na panga aisee!! Ila mm sidhani kama hao walimu waliamua kumpiga bila sababu lazima Kuna jambo Dogo alifanya japo Sio tiketi YA kumpeleka kuzimu.
Hata kama kuna sababu ndo mmpige? Kwanini msimpeleke kituo cha polisi?
 
Hao madogo ndo Huwa wanaanzisha fujo kwenye sherehe, kwenye sherehe ya shule unaend na panga la nini? Je ikitokea ukapata ukichaa ghafla?
 
Back
Top Bottom