7th November 2010
Jina lake kuishia kamati kuu
Sitta awajibu: Haki itanibeba
Baada ya kura za maoni ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kukivuruga na kusababisha mivutano ya kimakundi ndani ya chama hicho na kukigharimu kupoteza viti vingi vya ubunge wakati wa uchaguzi mkuu uliofanyika Jumapili iliyopita, imeibuka vita nyingine mpya ya kuwania Uspika wa Jamhuri ya Muungano, hali ambayo inaelezwa itazidi kukiweka pabaya.
Vita hiyo inaelezwa kuendeshwa na kundi la watu wanaotuhumiwa kwa ufisadi, ambalo limeanza mikakati mizito kuhakikisha linamwangusha Mbunge wa Urambo Mashariki, Samuel Sitta, ili asiweze kupitishwa na chama kuwania nafasi hiyo kwa mara ya pili..
Sitta ambaye alikuwa ni Spika wa Bunge lililopita, alionyesha msimamo mkali katika bunge hilo la tisa dhidi ya mafisadi, hali ambayo ilimjengea maadui wengi wa kisiasa, ambao wameapa kuhakikisha kuwa hakamati tena nafasi hiyo kwa kipindi kingine cha miaka mitano ijayo.
Sitta, Mbunge Mteule wa Jimbo la Urambo Mashariki, tayari ameshachukua fomu za kutaka kuwania tena nafasi hiyo kwa mara ya pili kupitia CCM, huku akikabiliwa na upinzani kutoka kwa aliyekuwa Naibu wake, Anna Makinda, Mbunge Mteule wa Bariadi Andrew Chenge, Mbunge Mteule wa Kongwa, Job Ndugai, Mwanasiasa mkongwe, Kate Kamba na Mbunge Mteule Viti Maalum (CCM) Anna Abdallah.
Wengine ni Mhasibu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT), Stephen Deya, Mjumbe wa Baraza la Vijana mkoa wa Pwani, Mohamed Nyundo, Luteni Mstaafu Benedict Lukwembe na Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Tambaza, Salum Kingulilo.
Wakati joto la kindumbwe ndumbwe hicho likizidi kuongezeka, duru za kisiasa ndani na nje ya CCM zimedokeza kwamba chama hicho tawala kwa mara nyingine kitaingia katika hatari ya mpasuko mkubwa unaotokana na vita ya makundi yanayotokana na kashfa ya mkataba wa kifisadi wa Richmond.
Vita hiyo mpya inaelezwa inayahusu makundi pinzani ndani ya CCM ambayo kila moja linajaribu kujiwekea mazingira ya ushindi kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Hali hiyo kwa mara nyingine inakiweka chama hicho njiapanda, baada ya hivi karibuni kuadhibiwa na wananchi katika majimbo kwa kupoteza wabunge wengi na mgombea wake wa Urais, Jakaya Kikwete, kupata ushindi wa jasho kutokana na chama kugubikwa na makundi yanayohasimiana.
Habari ambazo NIPASHE Jumapili imezipata, zinasema kundi la watu wanaotuhumiwa kwa ufisadi, linatumia kila aina ya mbinu kuhakikisha jina la Sitta linaishia Kamati Kuu (CC) kutokana na kuhofu linaweza kupenya na kuwasulubu tena bungeni endapo atakuwa Spika.
Genge hilo linalodaiwa kuongozwa na watu wenye fedha chafu, limekuwa likimtumia kiongozi mmoja wa ngazi ya juu wa CCM (jina linahifadhiwa), kuwashawishi wanachama wakongwe na wenye nguvu ndani ya chama hicho ili wagombee, lakini lengo mwisho wa siku waanguke na Sitta kubakia mgombea wao wanayemtaka.
Inaelezwa kuwa mbinu inayotumika ni kuwashawishi baadhi ya wanachama wakongwe kujitokeza kuwania Uspika, lakini baadaye majina yao yatakatwa CC pamoja na la Sitta, ili kuonyesha kuwa kulikuwa hakuna njama zozote za kumhujumu Sitta, utetezi ukiwa hata vigogo wengine wazito nao pia wameanguka.
NIPASHE Jumapili, lilipomuuliza Sitta jana kama anafahamu kuwepo kwa mkakati huo, alikiri kuufahamu na kueleza kuwa unatekelezwa kwa kushirikiana na baadhi ya watendaji wa CCM wasio waadilifu.
"Nalifahamu vizuri sana jambo hilo. Ni mkakati maalum ambao umeandaliwa lakini kwa bahati mbaya unashirikisha watendaji wakuu ndani ya CCM", alisema.
Alifafanua kuwa mpango uliopo ni kuweka majina mengi ya watu watakaowania uspika, lakini baadaye majina hayo yatakatwa likiwemo lake, ili kuonyesha kuwa hata vigogo wengine waliokuwa wakiwania majina yao yamekatwa hivyo hakuna uonevu.
Hata hivyo, alisema atazishinda njama hizo ambazo ameziita kuwa ni ovu, kwani wananchi wanajua utendaji na uadilifu wake katika kulitumikia taifa kwa moyo wake wote.
"Nimepata habari baadhi ya wagombea wenzangu wanajinadi kuwa wameamua kujitosa kuwania uspika baada ya kuelezwa kuwa jina langu litakatwa. Mimi nasema historia inaonyesha magenge ya uhalifu siku zote hayashindi na uamuzi wa mwisho utakuwa ni wa wananchi, wafanye wafanyavyo lakini hawawezi kuishinda nguvu ya wananchi na mwisho wa siku wataumbuka", aliongeza kusema.
Sitta, alisema wabaya wake wamekuwa wakimchafua kuwa ndiye amesababisha nyufa ndani ya CCM kutokana na kuruhusu mijadala huru ndani ya bunge.
"Nazushiwa na kuhusishwa na kuharibika kwa kila kitu kuanzia Mamlaka ya Makao Makuu Dodoma (CDA) wakati nikiiongoza, hivi kweli ningekuwa mtu mbaya baada ya CDA ningeteuliwa kuwa Waziri wa Sheria?" alihoji.
Alisema ameamua kuingia katika kinyang'anyiro hicho akiamini kuwa haki itatendeka, hivyo hahofii njama zinazofanywa ambazo zipo nje ya utaratibu halali wa kumpata mgombea.
Hata hivyo, duru zaidi za kisiasa zinasema, mkakati huo pia unasukwa Zanzibar na kusimamiwa na mmoja wa mawaziri wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Habari hizo zinasema, katika mkutano uliofanyika visiwani humo juzi, mmoja wa vigogo wa CCM, aliweka bayana msimamo huo wa mafisadi akisema Sitta ni mtu hatari hapaswi kurudi.
Mkakati huo unasimamiwa na vigogo watatu, akiwemo waziri mmoja mwanamke, ambao wameapa jina la Sitta halitapita Kamati Kuu.
Tayari waziri huyo mwanamke ambaye mara nyingi amekuwa akitoa kauli tata katika suala la ufisadi na kuzusha mijadala mizito, amekuwa akitamba kwa kuomba ushawishi kuhakikisha wanamshughulikia Sitta.
Tayari kuna mpango wa kumshawishi mwanasiasa mwingine mkongwe kutoka Kanda ya Ziwa ambaye ameshindwa katika kinyang'anyiro cha ubunge Jumapili iliyopita, kuhakikisha naye anachukua fomu na wakati wowote kuanzia kesho kama atakuwa amekubali atafanya hivyo.
Imebainika kwamba, hata mmoja wa waliojitokeza kuwania nafasi hiyo ambaye ni mwanasiasa mkongwe, alipigiwa simu na kiongozi huyo wa ngazi ya juu wa CCM, akiwa mkoani kwake ambako alikuwa akikarabati nyumba yake akilazimishwa kuchukua fomu hiyo.
Vyanzo vyetu hivyo vya habari viliongeza kwamba, awali mwanasiasa huyo alijenga hoja kwamba hawezi, lakini kiongozi huyo wa CCM alimwambia alikuwa akipingana na msimamo wa chama na fomu hiyo ilikuwa tayari.
Mbunge Mteule wa Peramiho, Jenista Mhagama, yeye amejitosa kuwania nafasi ya Naibu Spika iliyokuwa ikishikiliwa na Makinda bunge lililopita.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILi