ELON MUSK; Binadamu 'Kutoka Mars' Mwenye akili zaidi katika Karne ya 21

Hashpower7113

JF-Expert Member
Sep 26, 2011
1,353
2,137
musk 1.jpg

Imeandikwa na Hash Power kwa Msaada wa Mitandao.

Mei 30, 2020 ilikuwa ni siku ya kukumbukwa katika historia ya sayansi ya anga, astronomy duniani kote na hiyo ilikuwa ni baada ya kufanikiwa kwa chombo maalum kiitwacho Falcon 9 kufanikiwa kuwapeleka salama wanasayansi wawili, Doug Hurley na Bob Behnken kwenda kwenye kituo cha anga cha kimataifa, International Space Station.

Hii ilikuwa ndiyo safari ya kwanza kufanywa na kampuni binafsi, kuwasafirisha kwa mafanikio binadamu kwenda nje ya dunia mpaka ISS (International Space Station), ikumbukwe kwamba safari zote za awali zilikuwa zikifanywa na Shirika la Utafiti wa Anga la Marekani, Nasa.

Waliowezesha safari hiyo ya kihistoria, ni kampuni ya Space X, inayomilikiwa na binadamu kutoka sayari nyingine, Elon Musk! Ndiyo, Elon Musk, mfalme wa sayansi ya kizazi kipya ni binadamu kutoka sayari nyingine.

Unaweza kushangaa kwa nini Elon Musk anatukuzwa kama mfalme wa sayansi ya kizazi kipya na binadamu kutoka sayari nyingine? Kwa nini wengine wanampachika nadharia ya utani kwamba anatafuta njia ya kurudi kwenye sayari ya Mars iliko asili yake?

Kwa taarifa yako, jamaa anatisha kwelikweli kwenye ubunifu wa hali ya juu wa kisayansi, pengine kuliko binadamu mwingine yeyote aliyewahi kuishi duniani. Falsafa kuu ambayo imekuwa ikimuongoza, ni kuibadili dunia na hiyo imemfanya kutajwa kuwa miongoni mwa watu wachache wenye akili zaidi kuliko wote, wanaoishi katika karne ya 21.

Unaweza kujiuliza, huyu Ellon Musk ni nani? Ametokea wapi? Ni mambo gani makubwa anayoyafanya mpaka kumfanya awe mtu anayeheshimika kiasi hiki duniani kote kwenye masuala ya sayansi na teknolojia?

Twende pamoja!

ELON MUSK NI NANI?
Alipozaliwa Juni 28, 1971 kutoka kwa baba yake, Errol Musk, mhandisi na tajiri mkubwa kwa wakati huo, raia wa Afrika Kusini na mama Maye Musk, mwanamitindo mwenye asili ya Canada, alipewa jina la Elon Reev Musk FSR.

Hiyo ilikuwa ni Pretoria, Afrika Kusini, ambako baba yake alikuwa akifanya shughuli za uhandisi wa vifaa vya kielektroniki, rubani na nahodha. Hapo ndipo safari ya maisha ya Musk ilipoanza, akilelewa pamoja na kaka yake, Kimbal na dada yake Tosca.

Katika umri wake wa utoto, inaelezwa kwamba Musk alikuwa akipenda kucheza peke yake, akiwa kimya kabisa kiasi kwamba kuna wakati wazazi wake walihisi kwamba pengine alikuwa na matatizo ya kusikia, akapelekwa kwa daktari kufanyiwa uchunguzi lakini hakubainika kuwa na tatizo lolote.

Alianza shule lakini huko akakutana na changamoto nyingine! Licha ya uwezo wake mkubwa darasani, Musk alikuwa na umbo dogo kuliko watoto wengine wa umri wake, alikuwa mkimya na alipenda sana kujisomea vitabu, jambo lililosababisha awe anaonewa sana na wenzake.

Inaelezwa kwamba wakati fulani amewahi kupigwa na kundi la watoto wenzake, wakamsukumia kwenye ngazi alikoporomoka na baadaye kupoteza fahamu,

“Watoto wenzake walikuwa wakimpa wakati mgumu sana, unajua kabisa unaonewa lakini kesho ni lazima tena uende shuleni kukutana na walewale waliokuonea, ilikuwa ikimsumbua sana kichwa chake lakini nashukuru alifanikiwa kusonga mbele,” hayo ni maneno ya kaka yake, Kimbal wakati akizungumza na gazeti la Business Insider kuhusu maisha ya mdogo wake huyo.

Hali hiyo ilizidi kumfanya awe anajitenga muda mwingi huku akionesha kuwa na shauku kubwa ya kuvumbua vitu mbalimbali.

Alipofikisha umri wa miaka 10, wazazi wake walipeana talaka, akachukuliwa na mama yake na kwenda nchini Canada, maisha yakaendelea.

Ni katika kipindi hicho, alianza kuonesha mapenzi makubwa kwenye elimu ya kompyuta, akawa anajifunza mwenyewe mambo mbalimbali ikiwemo programming na alipofikisha umri wa miaka 12, tayari alikuwa na uwezo wa kutengeneza program mbalimbali za kompyuta.

Akafanikiwa kutengeneza ‘gemu’ akiwa na umri wa miaka 12 na kuvunja rekodi ya mtaalamu wa kompyuta mwenye umri mdogo zaidi baada ya kugundua video game iliyopewa jina la Blastar.

Alipofikisha umri wa miaka 15, alichoshwa na uonevu wa wanafunzi wenzake, akaamua kuanza kujifunza mafunzo ya karate na miereka, sasa akaanza kuwa tishio miongoni mwa waliokuwa wakimuonea awali.

Inaelezwa kwamba baada ya kuachana na baba yake Musk, mama yake alikuwa akifanya kazi mpaka tano tofauti kwa wakati mmoja ili kuitunza familia ya watoto watatu aliozaa na mumewe huyo. Mama yake pia alikuwa mtaalamu wa masuala ya lishe.

Baada ya kuhamia nchini Canada, aliendelea na masomo yake na baadaye akajiunga na Chuo Kikuu cha Queen’s University. Miaka mitatu baadaye, alihamia nchini Marekani alikoenda kujiunga na Chuo Kikuu cha Pennsylvania ambako alifanikiwa kuhitimu masomo ya Fizikia (Physics) na biashara.

Hizo ndizo zilizokuwa ndoto za Musk, kwenda kusoma nchini Marekani na inaelezwa kwamba aliwahi kugombana sana na baba yake, ambaye alimtaka abaki Afrika Kusini baada ya kupeana talaka na mama yake, lakini mwenyewe akang’ang’ania kwenda Canada.

Hakung’ang’ania kwa sababu anakupenda Canada, la hasha! Ndoto zake zilikuwa ni kuja kusoma nchini Marekani na aliamini itakuwa rahisi zaidi kwake kutimiza ndoto zake akitokea Canada na hicho ndicho kilichotokea.

Baada ya kuhitimu katika Chuo Kikuu cha Pennsylvania, alijiunga na Chuo Kikuu cha Stanford, nacho cha Marekani lakini baadaye aliamua kuachana na masomo ya chuo! Ndiyo, aliamua kukacha masomo ili atimize ndoto kubwa zaidi maishani mwake.

Inaelezwa kwamba kipindi anaacha chuo, tayari alikuwa amefungua kampuni yake ya Zip2 Corporation kwa kushirikiana na kaka yake na hakuacha chuo ili akazurure mitaani, la hasha! Aliacha ili apate muda wa kutosha wa kuisimamia kampuni hiyo.

SAFARI YA MAFANIKIO

Kampuni aliyoifungua na kaka yake, Zip2 Corporation, ilikuwa ni maalum kwa ajili ya kuwezesha malipo ya kimtandao! Naam, ni katika kipindi hicho cha mwishoni mwa miaka ya tisini, ndipo matumizi ya kompyuta yalipoongezeka kwa kasi duniani kote!

Bado kulikuwa na tatizo mahali, watu wengi walikuwa wakitaka kununua vitu online na hakukuwa na mfumo wowote ambao ungerahisisha kazi hiyo, mambo yakawa magumu lakini kwa Elon Musk na kaka yake, hiyo ilikuwa ni fursa ya kupiga hela ndefu!

Hilo lilifanikiwa kwa sababu sasa, Kampuni ya Zip2 iliwezesha wateja kuwa na uwezo wa kulipia bidhaa mbalimbali ‘online’, jamaa wakaanza kuogelea kwenye utajiri mkubwa ndani ya muda mfupi sana.

Baadaye Elon Musk aliamua kuuza shea zake katika Kampuni ya Zip2, pesa alizozipata akaanzisha kampuni nyingine ambayo pia ilikuwa ikihusika na kufanya miamala ya kielektroniki, X.com ambayo ilianzishwa mwaka 1999.

Ni kampuni hii ndiyo baadaye, ilikuja kubadilisha mfumo wa utendaji kazi wake na jina, na hapo ndipo ilipozaliwa PayPal, mtandao mashuhuri duniani kote kwa ajili ya kufanyia manunuzi.

Jamaa aliendelea kutengeneza pesa ndefu, baadaye akaja kuiuza PayPal kwa kampuni nyingine kubwa, eBay kwa gharama ya dola za Kimarekani, bilioni 1.5! narudia tena, dola bilioni 1.5! Unajua Kibongobongo ni shilingi ngapi hizi? Ni trilioni 3.5. Usifanye masihara.

Inaelezwa kwamba mkwanja huo sasa ulimpa nguvu Musk ya kuibadili dunia kadiri awezavyo na hapo ndipo mamiradi makubwa ya mabilioni ya fedha yalipoanza kutekelezwa, ikiwemo kutengeneza roketi, kurisha satelite, kutengeneza magari ya umeme na mbwembwe nyingine nyingi anazoendelea kuzifanya mpaka leo!

Mwaka 2002, Elon alianzisha kampuni nyingine ya SpaceX, ambayo mwanzo wa makala haya nimekueleza kwamba ndiyo iliyofanikisha safari ya kwanza binafsi kwenda kwenye kituo cha anga za juu cha kimataifa, International Space Station, wiki chache zilizopita.

Lakini pia, mwaka 2003, Musk alianzisha kampuni nyingine ya Tesla Motors ambayo baadaye ilibadilishwa na kuwa Tesla Inc. Kwa taarifa yako, kampuni hii ni miongoni mwa kampuni zinazoongoza kwa ugunduzi wa teknolojia mpya duniani kote.

Tesla ndiyo waliogundua magari ya kisasa yanayotumia umeme, Tesla ndiyo waliogundua magari yanayojiendesha bila dereva, Tesla ndiyo waliogundua treni yenye kasi ya ajabu, Hyperloop na kadhalika!

Ni Elon Musk huyu ndiye ambaye baada ya kuchoshwa na foleni za magari kwenye miji mikubwa duniani, alikuja na wazo jipya, la kutengeneza barabara za chini ya ardhi, kupitia kwa kampuni yake ya The Boring Company.

Kinachofanyika ni kwamba, kampuni hii inaingia mkataba na serikali na kwa kuanzia, tayari majimbo kadhaa nchini Marekani yameingia mkataba na kampuni yake, kisha baada ya hapo zinachimbwa barabara za chini ya ardhi.

Yaani huku juu shughuli zinaendelea kama kawaida lakini mita kadhaa chini ya ardhi ujenzi unaendelea! Barabara kubwa na za kiwango cha kimataifa zinajengwa, lengo likiwa ni kuhakikisha kunakuwa na njia ya haraka ya kumfanya mtu afike mahali fulani bila kulazimika kukaa foleni!

Dhamira yake ilikuwa ni kuibadili dunia na hakika ameweza! Amewezesha mabadiliko makubwa kwenye masuala mbalimbali, kuanzia kwenye mawasiliano mpaka teknolojia na kama bado huamini kama jamaa anaubadilisha ulimwengu, sikia hii.

Kampuni ya Space X inayomilikiwa na Elon Musk, ipo kwenye majaribio ya mwishomwisho ya mradi wake mkubwa wa kusambaza intaneti ya bure dunia nzima, kwa kutumia satalite maalum ziitwazo SpaceX Starlink ambazo tayari zimerushwa nje ya dunia na kukaa kwenye mzingo wake!

Kwa majaribio zimerushwa satelite 60 lakini malengo ni kurusha satelite 12,000 ambazo zitakuwa na uwezo wa kufanya watu wote duniani kuwa na uwezo wa kupata intaneti, buree kabisa!

Sasa vita iliyopo, ni kati ya wasambazaji wa intaneti na data ambao kwa kipindi kirefu wamekuwa wakijipatia faida kubwa kwa biashara hiyo, itakuwaje kama ukiwasha data kwenye simu yako tu, mambo yanaenda fresh kabisa bila kulipia bando la intaneti?

Bila shaka sasa umeanza kumuelewa Elon Musk lakini hiyo ni kama tone tu ndani ya bahari, ipo miradi mingine mikubwa ambayo hakika inakwenda kuibadili kabisa dunia.

Miaka michache baadaye, itakuwa ni kitu cha kawaida kukutana na gari likiwa linajiendesha lenyewe bila dereva! Hiyo ni akili ya Musk na tayari katika nchi zilizoendelea magari ya aina hii yapo, yakiwa yanatengenezwa na Kampuni ya Tesla ambayo ni miongoni mwa kampuni kibao zinazomilikiwa na binadamu huyu wa aina yake.

Miaka michache baadaye, itakuwa pia ni kitu cha kawaida kuwa na treni zinazopita chini ya bahari, tena kwa kasi kubwa zaidi ya ile ya sauti, wataalam wanaiita supersonic! Yaani huko tunakokwenda, haitakuwa ajabu tena mtu aliyepanda treni ya umeme, Hyperloop, kuwahi kufika safari yake kabla ya mtu aliyepanda ndege!

Tukija kwenye suala la usafiri wa anga za mbali, baada ya kufanikisha safari ya kwanza ya chombo cha Falcon 9, Musk na vijana wake wapo bize kuumiza vichwa, na sasa wapo kwenye project ya kutengeneza roketi kubwa yenye uwezo wa kubeba mzigo mzito kuliko roketi zote duniani.

Lengo la project hiyo ni kufanikisha kusafirisha mizigo mikubwa na mizito zaidi kutoka duniani kwenda kwenye sayari nyingine na kwenye kituo cha kimataifa cha anga za juu na kurudi duniani! Usije kushangaa siku jamaa akavumbua teknolojia ya kulifanya jua liwe linachomoza Magharibi na kuzama Mashariki! Ni utani tu!

Huyo ndiyo Elon Musk, mchawi wa teknolojia na binadamu mwenye akili zaidi katika karne ya 21.

Hash Power!
 
Duniani kuna vichwa aisee, huku sisi wengine tukiwa tunaumiza kichwa kuhakikisha tunapata milo mitatu ya familia wenzetu hawa washasahau habari hizo ndio maana akili zao sasa zinawaza extra miles na kufanikiwa kupata mavumbuzi mapya yanayoitikisa dunia. Taratibu tu, tutafika na sisi hata kama ni kwa kuchelewa sana.
 
Shukrani sana ndugu mleta uzi kwa maelezo adhimu kumuhusu huyu "Genius" wa kizazi hiki, zipo hisia kichwani mwangu juu ya uhusika wa huyu bwana, miradi yake na so called "deep state" natamani sana mkuu Habibu B. Anga kama siku ikikupendeza utuletee nondo kuhusiana na hili, asante!

Let's meet at the top, cheers 🥂
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom