SoC04 Elimu ya Teknolojia ya kisasa iwe kipaumbele mashuleni kuendana na utandawazi na maendeleo ya sayansi duniani

Tanzania Tuitakayo competition threads

Xpertz

Member
May 3, 2024
12
8
UTANGULIZI
Wizara ya elimu imezindua mtaala mpya wa elimu karibuni wenye maboresho mbalimbali ambayo binafsi naona bado hayakidhi matakwa ya kasi ya sasa ya ulimwengu kisayansi na kiteknolojia. Bado tumelenga kuzalisha kundi kubwa la wasomi wasio na uwezo wa kuendana na maendeleo ya sayansi na teknolojia kwenye ulimwengu wa sasa.

Tumejikita kwenye vipaumbele vya sayansi ya Jamii zaidi, historia na kanuni msingi za sayansi kwa maana ya kwamba masomo ya msingi ya sayansi, hakuna kozi bunifu za kuendana na mabadiliko mengi mapya yanayoendelea kutokea katika uga wa sayansi na teknolojia duniani mfano akili mnemba (AI) nk. Tumejikita kwenye masomo ya maadili uzalendo dini nk.

Nini kifanyike kuendana na dunia ya sasa?
1. Nashauri kozi za TEHAMA ziboreshwe na kufundishwa kwa mapana yake. Kipengele cha matumizi ya akili mnemba(Artificial Intelligence) kipewe KIPAUMBELE kikubwa ambapo huko ndio dunia inapoelekeza nguvu kubwa kwa sasa katika sayansi. Mfano kwenye masomo ya kidato cha tano na sita nashauri miunganiko ya masomo(combination) ziangaliwe upya, zilizopitishwa nyingi haziendani na matakwa ya mabadiliko ya kisayansi ulimwenguni.

2. Elimu yetu Upande wa sayansi ijikite katika mazoezi (practical) tofauti na nadharia. Miundombinu ya mashuleni IBORESHWE maabara nyingi zijengwe na kupelekwa vifaa vingi zikiwemo kompyuta. Elimu ya sayansi kwa vitendo ndio suluhisho la kuzalisha wanasayansi wenye uwezo kiushindani kuendana na mabadiliko ya sayansi duniani na utandawazi. Wataalamu wa sayansi pia waajiriwe kwa wingi kwenye mashule kuanzia ngazi ya chini ili kuchochea hamasa ya sayansi kwa watoto wetu. Mfano kwa sasa masomo ya sayansi mashuleni yanaogopwa na wanafunzi wengi wakiamini ni magumu kumbe shida ni miundombinu sio rafiki na Wataalamu hawapo wa kutosha kama ilivyo kwa masomo ya sanaa. Nashauri hata Wataalamu wa sayansi ambao hawajasomea ualimu waajiriwe huko wapitie mafunzo ya msingi (principles of teaching methodology)

3. Ubunifu wa kisayansi uongezewe nguvu na kupewa ufadhili na serikali kifedha. Bado Tanzania tupo nyuma sana kwenye kuzalisha wabunifu wakubwa wa kubadili dunia kisayansi hivyo mkono wa Serikali katika kuwainua, kuwaunga mkono na kuwapa mitaji na ruzuku wabunifu itasaidia kuzalisha Wataalamu wengi na teknolojia nyingi zenye tija nchini kwa maendeleo ya nchi. Bado mifumo ya kuibua wabunifu nchini sio mizuri, pia wabunifu wengi wamekua wakitumia vitendea kazi duni. Nashauri Serikali ije na mipango ya kufadhili bunifu mbalimbali kwa kuzingatia maandiko, kuwapa Wataalamu mitaji kufanya tafiti zao kwa kutumia vifaa vya kisasa badala ya sasa ambapo wamekua wakifanya tafiti zao katika mazingira yasiyo rafiki kwa vifaa duni.

4. Ufadhili wa masomo nje (scholarship) ujikite zaidi kwenye kozi za kimkakati za kisayansi ili kuongeza idadi ya Wataalamu na kupanua wigo wa teknolojia mpya nchini. Bado nchi imeendelea kuwa tegemezi kwa Wataalamu wa nje mfano Sekta ya afya na kutumia fedha nyingi mno wakati tunao uwezo wa kufadhili mamia au maelfu ya vijana wetu watakaoweza kuja kufanya kazi hizo hapa hapa nchini. Serikali iratibu kuwaombea nafasi za ufadhili wanafunzi na Watumishi wa kitanzania nafasi kwenye vyuo bora duniani kwa kozi za kimageuzi katika sayansi ikibidi iwafadhili. Hii itasaidia kupata Wataalamu wengi watakaokuja kuleta mageuzi nchini pia nashauri wakitoka masomoni Serikali ihakikishe wanatumika wasiachwe kufanya mambo tofauti na kupoteza tija yao.

5. Shule za vipaji maalumu zitumike kuzalisha wanamageuzi wa kisayansi nchini. Tumeona bado kuna changamoto kubwa nchini toka shule za vipaji maalumu kama Ilboru, mzumbe nk ziwepo miaka yote hazijaweza kukidhi haja ya nchi kupata wanamageuzi, zinazalisha watu wa kawaida kwenye jamii hakuna jipya. Serikali iweke mkazo kwenye shule hizo wanakopelekwa vijana wenye uwezo mkubwa zaidi kiakili ili waweze kufika mbali na tija yao kwa taifa ikafikie viwango kusudiwa. Humo ndio sehemu sahihi kuzalisha Wataalamu mahiri na wabunifu vinginevyo tutaishia kuwa na wasomi wa kawaida wasio na matokeo ya ajabu kwenye taifa. Inasikitisha Sana kuona kwamba maono ya baba wa taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipoanzisha shule hizo kwa lengo la kuzalisha wanamageuzi hadi leo zaidi ya miaka 60 ya uhuru bado zimekua shule za kawaida kabisa, matokeo ya mitihani yanatangazwa wamefaulu alama juu ila tija yao kwenye jamii kimageuzi haipo, wanaishia mitaani na kuwa kama wasomi wa kawaida kabisa. Hawana maajabu wala ubunifu wowote wa kipekee. Hii inaonesha uendeshaji na usimamizi wa shule hizo haukidhi malengo yaliyokusudiwa.

6. Wawekezaji kwenye Upande wa sayansi na teknolojia wavutiwe na kuondolewa vikwazo vingi. Tumeona wamiliki wa kampuni ya mtandao ya Star Link ikibanwa kwa mashariti mengi yaliyoikwamisha kuwekeza nchini teknolojia yake kwa wakati huku nchi nyingine kama Zambia zikichangamkia fursa hiyo, lazima tutafakari kwa kina je tukiwaruhusu tunapata hasara kubwa kiasi gani na je tija yake ni kiasi gani, hofu inaweza kutuchelewesha bure.

Nawasilisha
 
Kipengele cha matumizi ya akili mnemba(Artificial Intelligence) kipewe KIPAUMBELE kikubwa ambapo huko ndio dunia inapoelekeza nguvu kubwa kwa sasa katika sayansi.
Na tukisema, tuzalishe wataalamu wa hayo masomo mengine wabobevu walio nondo kabisa ili watusaidie data za kuzifundishia hizo akili mnemba??

Elimu yetu Upande wa sayansi ijikite katika mazoezi (practical) tofauti na nadharia. Miundombinu ya mashuleni IBORESHWE maabara nyingi zijengwe na kupelekwa vifaa vingi zikiwemo kompyuta. Elimu ya sayansi kwa vitendo ndio suluhisho la kuzalisha wanasayansi wenye uwezo kiushindani kuendana na mabadiliko ya sayansi duniani na utandawazi
Maboresho pande zote, nadharia na vitendo. Nakubali vitendo, lakini hatuwezinkamwe kumuua mmoja halafu mwingine akabaki hai.
Nashauri Serikali ije na mipango ya kufadhili bunifu mbalimbali kwa kuzingatia maandiko, kuwapa Wataalamu mitaji kufanya tafiti zao kwa kutumia vifaa vya kisasa badala ya sasa ambapo wamekua wakifanya tafiti zao katika mazingira yasiyo rafiki kwa vifaa duni.
Hili wazo zuri kabisa, kuwezesha wabunifu kuzalisha.
 
Back
Top Bottom