Elimu kwa Umma: Faida za Kusafiri na Kitabu (Richard Mabala)

Bonheur Travels Tanzania

Verified Member
Dec 29, 2020
168
500
Ndugu WanaJF,

Tunaendelea na 'misheni' yetu ya kutoa elimu kwa umma hapa JamiiForums kuhusiana na masuala mbalimbali ya safari za ndege, utalii na mambo yanayoshabihiana na hayo.

Kupitia thread hii, utajifunza faida zipatikanazo wakati unasafiri na namna ya kufanya #UtaliiNaKitabu hasa katika kipindi hiki cha sintofahamu ya janga la corona.

Tutakuwa LIVE hapa JF kukuletea updates za uchambuzi wa kitabu cha riwaya ya malezi kiitwacho #LoveBombs kilichotungwa na Mwalimu Richard Mabala (maarufu Mabala The Farmer).

IMG-20210219-WA0046.jpg


Uchambuzi huu utarushwa MUBASHARA pia kupitia televisheni ya ITV kesho Jumamosi tarehe 20 Februari 2021. Muda ni kuanzia saa 3 asubuhi.

Tunashirikina na Mwalimu Mabala kukuletea uchambuzi huu kupitia kampeni yetu ya #SafiriNaKitabu tutakayoitangaza rasmi hivi karibuni!

Endelea kuwa nasi..
----

UPDATES:

Muda wowote kutoka sasa tutakuletea mahojiano ya moja kwa moja kutoka studio za ITV/Mikocheni, ambapo Mwalimu Richard Mabala kupitia kipindi cha Watoto Wetu, atatoa elimu ya malezi inayopatikana kwenye kitabu chake cha #LoveBombs.

Ikumbukwe kuwa hii ni sehemu ya mfululizo wa dhamira yetu ya kutoa Elimu kwa Umma juu ya Usafiri wa Anga, Utalii, Safari na mengineyo kuelekea katika uzinduzi wa programu ya #SafiriNaKitabu #TaliiNaKitabu #KitabuNiZawadi ambayo tutawashirikisha rasmi hivi karibuni.

Kama upo karibu na TV basi wakati ndio huu, unaweza kuweka ITV kufuatilia moja kwa moja yanayoendelea studio au endelea kuungana nasi kwenye uzi huu tutakuletea moja kwa moja yanayojiri..


Video: Mahojiano ITV na Mwandishi Mabala
-----

UPDATES:

Swali: Karibu sana katika studio za ITV ndugu Richard Mabala. Unaweza kutueleza historia ya hii kazi yako japo kwa ufupi na sasa hivi unafanya nini?

Mabala: Kwa sasa mimi ni mstaafu.. Miaka mingi nilikuwa nimejikita zaidi kwenye kutoa mafunzo kwa vijana hasa kuhusu ujinsia na kujitambua.. Ninachofanya kwa sasa ni kuendelea na kazi ninayoipenda ya kuandika vitabu.

Mabala: Safari yangu ya uandishi wa vitabu ilianzia kwenye utunzi wa mashairi. Namkumbuka mwandishi anaitwa Kajube. Alikuwa mwandishi mzuri sana wa mashairi (siku hizi ameacha). Miongoni mwa vitabu vyangu maarufu ambavyo naye yumo ni "Summons". Watu walikuwa wakinisifia kuandika story nzuri za Afrika.

Baadae nikaja kuingia kwenye riwaya.

Pia niliwahi kupitia kitabu cha Three Suitors One Husband mpaka baadhi ya watu wakadhani mimi ndiye mwandishi.

Mabala: Vitabu vya Hawa the bus driver na Mabala the farmer sikutaka viingie kwenye kufanyiwa mitihani. Nilitaka tu kuandika watu wasome wafurahi na wajifunze.

Mabala: Baada ya vitabu hivyo kufanya vizuri baadae nikaona niingie kwenye uandishi wa vitabu vya watoto, Niliandika vitabu vingi kikiwemo cha kitabu cha Hadithi ya Sara, Kurwa na Doto na vingine.

Mabala: Mwanafunzi wangu mmoja aliwahi kuniambia, mwalimu mimi napenda sana kitabu cha Mabala the farmer, lakini kwanini usituandikie na riwaya badala ya kusoma za waandishi kutoka Nigeria, Ghana na Kenya? Ndipo nikaanza hayo mawazo ya uandishi wa riwaya..

Kitabu cha riwaya ambacho nimekiandika na kukichapisha tayari ni hiki cha Love Bombs.

Mabala: Wazo la Love Bombs nililipata baada ya kuona kuna mtoto kila mara alikuwa na tabia ya kumwambia mama yake; kwanini kila kitu mpaka tugombane? Huyu hakuwa mwanangu lakini nilipata kitu cha kuandika kupitia mgogoro huo.

(Endelea kusoma zaidi kwenye post zinazofuata)..
 

Bonheur Travels Tanzania

Verified Member
Dec 29, 2020
168
500
Mabala: Riwaya ya Love Bombs kimsingi inahusu malezi. Kwa mfano utakutana na maneno ya mtoto Marietta akiwahoji wazazi wake; kwanini kila siku mnalalamika kuhusu watoto wa siku hizi bila kufikiri? Watoto wa siku hizi hivi, watoto wa siku hizi vile! Badala ya kushangaa watoto wa siku hizi, kwanini msishangae kuhusu wazazi wa siku hizi? Sisi tupo tulivyo kwa sababu ya ninyi mlivyo".

Ujumbe mkubwa niliotaka kuufikisha kupitia riwaya hii ni kuwakumbusha wazazi/walezi kuwa maneno wanayosema na vitendo wanavyofanya kwa kiasi kikubwa vinawaathiri watoto.

Mabala: Watoto wengi ukiwauliza wanataka nini kwa wazazi wanasema wanataka kukaa nao wazungumze, wawasikilize, kupewa nafasi na kupendwa. Sio kununuliwa iphone, ipads na kutimiziwa mahitaji yao pekee.
 

Bonheur Travels Tanzania

Verified Member
Dec 29, 2020
168
500
Kwa wasiomfahamu vizuri Richard Mabala:

Richard Mabala ni mtunzi wa vitabu maarufu vya fasihi vya “Mabala The Farmer" na “Hawa the Bus Driver” vinavyotumika katika shule za sekondari nchini.

Pia ni mtunzi wa mashairi ya Kiingereza yaliyomo kwenye vitabu vya “Summons: Poems From Tanzania” na “Selected Poems”.

Mabala ni mwanafasihi, mkereketwa wa elimu ya Tanzania, mhamasishaji wa matumizi ya lugha ya Kiswahili kama lugha rasmi ya kufundishia nchini, mwanasafu kwenye magazeti mbalimbali na mwanaharakati.

Wasifu wake kamili uko hapa > Mambo 10 usiyoyajua kuhusu richard mabala
 

Bonheur Travels Tanzania

Verified Member
Dec 29, 2020
168
500
UPDATE: Muda wa maswali na majibu

Swali: Usemi wa ukitaka kumficha jambo Mwafrika liweke kwenye kitabu. Je unakubaliana nao? Wewe kama mwandishi unafanyaje kuvutia watu kusoma?

Mabala: Mimi sikubaliani na usemi huo. Tabia ya usomaji vitabu sio tatizo la Mwafrika pekee. Linaweza kuwepo hata nchi za Ulaya. Tabia ya kusoma vitabu huanzia utotoni. Watoto wote (bila kujali wanatoka wapi) wakijengewa tabia ya kusoma, watasoma tu hadi ukubwani.
 

Bonheur Travels Tanzania

Verified Member
Dec 29, 2020
168
500
Swali (kutoka Geita): Vitabu vingi vya kihistoria vimeandikwa zaidi historia ya nje. Je, Mabala haoni umuhimu wa kushiriki kutoa mawazo yake na ikibidi kuandika kuhusu historia ya Tanzania ili isomwe kwa wingi hasa mashujaa wetu na mazuri yetu?

Mabala: Ni kweli kuna umuhimu wa kusoma zaidi historia ya Tanzania. Mimi pia ni mwalimu mzuri wa Historia na nakubaliana na wazo hilo. Kwa mtazamo wangu, kuna watu watu wengi walichangia Uhuru wa Tanganyika hawajaelezwa vizuri. Mfano watu waliompokea na kumsaidia Mwalimu Nyerere kwenye harakati za Uhuru, Muungano, Mapinduzi ya Zanzibar na mengine. Haya yakiandikwa vizuri kwa kina watu wakajifunza na kujadiliana, itakuwa ni jambo zuri.
 

Bonheur Travels Tanzania

Verified Member
Dec 29, 2020
168
500
Swali: Mzee Mabala ulisema umeingia Tanzania mwaka 1973. Bila shaka unafahamu mambo mengi yaliyotokea Tanzania. Kama ilivyoelezwa, wanaoandika Historia ya Tanzania wengi hawakuwepo hapa, wewe ambaye ulikuwa hapa na ni Mwandishi, unaonaje ukiandika?

Mabala: Pale Chuo Kikuu Dar es Salaam kuna kitivo cha Histor.... (anakatishwa).

Swali: Kwanini Mabala haandiki kuhusu tatizo la wazazi walevi?

Mabala: Hahaha, ndio changamoto ya kuwa mwandishi. Kila mtu atataka uandike kuhusu kila kitu. Mimi sipendezwi na jinsi watu wanavyoandika au kutunga hadithi wakielezea ulevi, kuwataja kina Baba ndio walevi. Hawaelezi kuhusu wakina mama.

Pia si kweli kwamba matatizo yote ya kifamilia chanzo chake ni ulevi, wapo wanaume/baba wengi sio walevi na wanalea familia zao vizuri tu japo wana madhaifu yao mengine.
 

Bonheur Travels Tanzania

Verified Member
Dec 29, 2020
168
500
Swali: Ukilinganisha ubora wa elimu ya miaka ya zamani na sasa, unadhani ubora wa elimu umeongezeka au umepungua? Kwa sababu tunasikia tu ufaulu umeongezeka lakini ukiangalia maswali kwenye mitihani siku hizi ni rahisi sana.


Mabala: Zamani kulikuwa na mchujo mkali sana. Mimi nimefundisha sekondari pia. Nakumbuka kulikuwa na sekondari saba tu zinazofundisha kiingereza form 6. Ni ngumu kufananisha ubora na zama za sasa ambapo mambo yamepanuliwa sana. Shule zimekuwa nyingi na wanafunzi ni malaki - huwezi kuwasimamia na kuwachuja wote ukapata kilicho bora.

Mimi nafikiri miundombinu na maandalizi hayapo ya kutosha. Kuanzia walimu, nyenzo za kujifunzia na mengine. Pia tabia ya kufundisha watoto kwa lugha ya kiingereza sio sawa. Nchi nyingi zinafundisha watoto wao kwa lugha zao.

Kwa hapa Tanzania watoto wafundishwe kwa Kiswahili waelewe mambo kwa lugha yao. Ukimfundisha mtoto jiografia kwa lugha yake ataelewa vizuri jiografia. Ukimfundisha historia kwa lugha yake ataijua vizuri historia. Somo la Kiingereza libaki kuwa somo na lifundishwe vizuri.
 

Bonheur Travels Tanzania

Verified Member
Dec 29, 2020
168
500
Swali (mwandishi): Muda sio rafiki.. Natamani hata kuongezwa muda vile kuna mengi ya kujifunza kutoka kwako. Ni sawa na samaki ana mengi ya kusema lakini tatizo mdomoni ana maji. Mtu akitaka kukupata kwa haraka mzee Mabala anakupataje?

Mabala: Asante sana. Kunipata zaidi ni kwenye Twitter kwa jina la @mabalamakengeza

(Maelezo ya kufunga kipindi).
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom