Dunia haina usawa

ERIC SHIGONGO
DUNIA HAINA USAWA

Hakukuwa na utulivu nchini Kenya, kila mtu alitaka kujua mahali ndege ya rais wao ilipokuwa. Wabunge wakapata cha kujadili, kila mmoja hakufahamu ukweli, rais wao alisema kwamba Tanzania ilihusika katika upotevu wa ndege hiyo lakini kitu cha ajabu, walipoulizwa Tanzania walisema kwamba hawakuhusika kabisa.
Hilo liliwachanganya, waliwatuma watu wao kuchunguza kila kona lakini hakukuwa na majibu yoyote yale. Hilo likawapa wasiwasi kwamba ndege hiyo ilipotezwa kama ilivyopotea ndege ya Malaysia na hivyo isingeweza kuonekana tena.
Wakati wakijiuliza sana kuhusu ndege hiyo wakapata taarifa kutoka kwenye mtandao wa Instagram katika Akaunti ya Mabadiliko ya Kweli ambayo ilisema kwamba ingetoka taarifa ambayo ingewafanya Kenya kufahamu mahali ndege yao ilipokuwa lakini endapo tu wangekuwa tayari kuambiwa mahali ndege ilipokuwa kwani aliyehusika katika upoteaji wa ndege hiyo alikuwa akijulikana.
Hilo ndilo lililowafanya Wakenya kidogo kuwapenda Watanzania, wakaanza kuiweka taarifa hiyo katika mitandao mbalimbali kwamba Tanzania ilijua mahali ndege ilipokuwa mpaka mtu aliyehusika katika kuipoteza alikuwa akijulikana.
Haraka sana Rais Onyango akampigia simu Ojuku na kuzungumza naye. Kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kumuomba msamaha kwa kila kitu kilichokuwa kimetokea lakini lengo lake kubwa lilikuwa ni kuambiwa mtu aliyekuwa amehusika katika lile lililokuwa limetokea.
“Tumegundua kosa letu, tusameheane tu kwa kuwa wote ni watu wa ukanda mmoja,” alisema Rais Onyango kwa sauti ndogo na ya huruma kabisa.
“Sawa. Haina tatizo! Nikusaidie nini?” aliuliza Ojuku.
“Kujua mahali ndege ilipokuwa. Hata tukimfahamu mtu aliyehusika, litakuwa jambo jema pia,” alisema mwanaume huyo.
“Hakuna shida! Tutazungumza! Utafahamu kila kitu!” alisema Ojuku, yeye mwenyewe hakufahamu ni kitu gani Godwin alitaka kukifanya, ila aliamini kuwa kuna kitu kikubwa sana ambacho Godwin angekifanya na Wakenya kuchanganyikiwa.
***
Godwin alikuwa bize, hakutaka kuzungumza na mtu yeyote, alitulia chumbani kwake huku akiwa na kompyuta yake mapajani mwake. Alitaka kucheza mchezo hatari ambao ungemfanya kila mtu kushangaa na kustaajabu.
Mtu ambaye alitaka kumtumia kipindi hicho alikuwa bilionea Olotu, alichokifanya kwa kutumia simu ya Rais Onyango aliipata simu yake na hatimaye kuanza kuanza kuidukua. Hiyo wala haikuwa kazi kubwa kwake, alifanikiwa na moja kwa moja kutengeneza meseji ambazo zingekuwa ngumu kuonyesha kama zilikuwa zimetengenezwa.
Akaandika ujumbe kwa namba zilezile, ujumbe uonekane kama ulikuwa umetoka katika simu ya Olotu na kwenda kwa mtu aliyejulikana kwa jina la Ibrahim Omeng, Mkenya aliyekuwa nchini Afrika Kusini, mtu ambaye naye alikuwa karibu sana na bilionea huyo.
Akaweka mawasiliano ya siri kwamba wawili hao walikuwa wakiwasiliana kwamba walitaka kucheza mchezo mmoja hatari, kujifanya kama wanamtaka Bokasa lakini lengo kubwa likiwa ni kuipoteza ndege ya rais nchini Kenya.
“Kwa hiyo tufanyeje?” ilikuwa ujumbe ulioonekana kutoka katika simu ya Omeng.
“Nitajifanya namtaka Bokasa, niitumie ndege yake, halafu ikifika huko, itasafirishwa kupelekwa nchini Uganda kisiri, huko itafunguliwa vipandevipande na kwenda kuviuza,” ulisomeka ujumbe kutoka katika simu ya Olotu.
“Hawatotushtukia?”
“Hakuna kitu kama hicho!”
“Halafu huyo Bokasa tumfanye nini?”
“Tukamtupe katika mpaka wa Tanzania na Kenya. Halafu sisi tunaondoka kwani lengo letu litakuwa ni ndege. Nina kisasi moyoni, tukimaliza suala la ndege, tunafanya mikakati ya kuichoma moto ikulu, tutamtumia mtu mmoja wa karibu ambaye ataifanya kazi hiyo kiuaminifu kabisa,” ulisomeka ujumbe.
“Basi sawa. Ndege tukaiuze kiasi gani?”
“Iuzwe kwa dola bilioni mbili. Ni pesa nyingi sana hizo!”
“Haina shida! Ila kuwa makini ili Rais Onyango asijue kama unamtumia kwa ajili ya kuipoteza ndege yake!”
“Hilo usijali!”
Alizitengeneza meseji hizo na kisha kuzipiga picha. Ilikuwa vigumu kugundulika, baada ya hapo akaziweka katika Akaunti ya Mabadiliko ya Kweli na kuandika kwamba ukweli ungekwenda kujulikana kwa mtu aliyeucheza mchezo huo.
Kitendo cha watu kuziona meseji hizo katika akaunti hiyo tena zikiwa zimepigwa picha, kila mtu alishangaa, Wakenya walichanganyikiwa. Walimjua bilionea Olotu, alikuwa mwanaume makini aliyekuwa akifanya vitu vyake kisiri na kila siku alisema kwamba alikuwa akiipenda sana Tanzania.
Wakenya waliendelea kushangazwa, hawakuamini kile walichokiona, kila siku waliilaumu Tanzania kwamba ilihusika katika upoteaji wa ndege ya rais wao kumbe nyuma ya pazia kulikuwa na mtu aliyekuwa amehusika katika mpango mzima.
Godwin hakuishia hapo, alichokifanya ni kuzitumbukiza meseji zile katika simu za watu hao wawili ili zionekane kuwa ndizo walizokuwa wakichati na mbaya zaidi akaziwekea virusi wakati alipokuwa ameviweka ili kama itatokea wawili hao kutaka kuzifuta, zisifutike, ziendelee kubaki humohumo.
Rais Onyango alisikia kile kilichotokea, akapigiwa simu na kuambiwa kwamba mbaya wake haikuwa nchi ya Tanzania bali rafiki wake wa karibu, Olotu ambaye alicheza mchezo mzima kwa kujifanya kumshirikisha kumbe nyuma ya pazia alikuwa akitaka kukamilisha mambo yake.
Hilo lilimhuzunisha mno, hakuamini, akajifungia chumbani na kuanza kulia, aliumia moyoni mwake, hakuamini kwamba moyo wote wa wema aliojaribu kumuonyeshea mwanaume huyo kwa kukubaliana naye kwenda Ubelgiji kumleta Bokasa kumbe ulikuwa ujanja wa kuipoteza ndege yake.
“Kwa nini amefanya hivi?” alijiuliza huku akionekana kustaajabu, kwake, kilichokuwa kimetokea kilionekana kuwa kama kitu cha muujiza sana.
Hakutaka kupoteza muda, alichokifanya ni kuchukua simu yake na kupiga Mombasa kwa kuwataka polisi wamkamate Olotu haraka sana kitu ambacho ndani ya dakika thelathini akaambiwa kwamba mwanaume huyo alikuwa mikononi mwa polisi na alikuwa njiani kwenda kufanyiwa mahojiano.
***
Bilionea Olutu alikuwa ndani ya jumba lake la kifahari, moyo wake ulikuwa na mawazo tele, alikuwa akimfikiria Bokasa ambaye aliambiwa kwamba alikuwa njiani kupelekwa nchini Kenya. Baada ya saa kadhaa akapewa taarifa za kupotea kwa ndege, alichanganyikiwa, hakuamini kirahisi kama ndege inaweza kupotezwa kirahisi kama ilivyokuwa.
Haraka sana akawasiliana na Rais Onyango na kuanza kuzungumza naye, walipanga mikakati kwamba piga ua ilikuwa ni lazima ndege ipatikane na hatimaye kumpata mtu wake aliyekuwa akimtaka kwa kipindi kirefu.
Akaambiwa kwamba bado Usalama wa Taifa walikuwa wakipambana usiku na mchana kuhakikisha kwamba ndege inapatikana, aliendelea kuambiwa kwamba mawasiliano yalikuwa yakifanyika katika nchi moja na nyingine kujua kama ndege ilikuwa huko au la.
Majibu hayakumridhisha, akaliacha jambo hilo mikononi mwa rais huku naye akiendelea kufanya mambo mengine. Baada ya siku moja na saa kumi na nane, akapokea taarifa kutoka kwa vijana wake kwamba kulikuwa na mtu kwenye mitandao alisema kuwa yeye alihusika katika upotevu wa ndege na alifanya hivyo kwa kuwa alitaka kulipa kisaisi kwa Rais Onyango.
Kwanza akashangaa, hakujua sababu ya taarifa hizo kutolewa na wakati hakukuwa na ukweli wenyewe, akataka kuangalia ili aone kama kweli taarifa hizo zilitolewa au la. Alipoingia, kitu cha ajabu kabisa alichokutana nacho ni meseji ambazo zilionekana akiwa anachati na rafiki yake aliyekuwa Afrika Kusini.
“Mmh!” alishangaa.
Alikumbuka kwamba hakuwa amewasiliana na mwanaume huyo kwa meseji kama zile, zilitoka wapi? Wakati akijiuliza zaidi, akasikia akiambiwa kwamba polisi walikuwa wamefika nyumbani kwake na hivyo kutaka kumchukua.
“Nimefanya nini?” aliuliza.
“Wanasema kwamba meseji zilizokuwa zimetuma na kutumiwa katika simu yako,” alijibu mlinzi aliyekwenda kumpa taarifa kuhusu polisi hao.
Polisi wakaingia ndani, waliagizwa kumchukua bilionea huyo, hawakutaka kuchelewa, wakamfunga pingu na kuondoka naye. Njiani alikuwa akishangaa, kila kitu kilichokuwa kimezungumzwa kilikuwa ni uongo mtu na alikuwa na uhakika kwamba hakuwa amewasiliana na mwanaume huyo kwa kupitia namba yake.
Hakutaka kusema kitu, akanyamaza mpaka alipofikishwa katika kituo cha polisi hapo Mombasa ambapo akachukuliwa na kuingizwa sero huku tayari waandishi wa habari wakiwa wamekwishafika katika kituo hicho.
Kitu cha kwanza walichokifanya polisi ni kuanza kupekua katika simu yake ili kuona kama meseji hizo zilikuwepo, walipoifungua sehemu ya kuhifadhi meseji, wakazikuta meseji hizo zikiwa zimetumwa na kuingia katika namba ya jamaa yuleyule aliyekuwa Afrika Kusini.
“Olotu! Hii kesi ngumu sana, kumbe meseji zenyewe hata kufuta hukufuta,” alisema mkuu wa kituo cha polisi huku akimwangalia mwanaume huyo aliyekuwa sero.
“Meseji gani?”
“Zile ulizochati na huyo mwanaume. Zote zipo tena zikielezea mipango kabambe mliotaka kufanya kuhusu kuipoteza ndege,” alijibu mkuu huyo ambaye alikuwa akilipwa pesa kwa ajili ya kumlinda mwanaume huyo.
“Meseji kwenye simu yangu?”
“Ndiyo! Zipo zote, tena zilezile zilizokuwa zimeandikwa katika mitandao ya kijamii!” alijibu.
Olotu hakuamini, akahitaji kuziona meseji hizo, kisiri akaletewa simu yake ambayo hakuwa ameiangalia na kuonyeshewa meseji zile. Hakuamini alichokuwa akikiona, alipigwa butwaa, alikumbuka kwamba hakuwa amechati na mwanaume huyo kuhusu jambo hilo, meseji hizo zilifikaje katika simu yake?
Alipagawa, akajaribu kuingia sehemu ya kuzifuta, hakuwa na uwezo wa kufanya hivyo, zilionyesha kabisa kwamba zilizuiliwa kwa kila kitu. Alibaki akilia kwani ilikuwa ni lazima kesi ifikishwe mahakamani na kitu cha kwanza kabisa kuangalia kilikuwa ni simu yake ili kuona kama kulikuwa na meseji hizo ambazo hazikuweza kufutika.
“Hapana! Sikuwa nimechati na huyu mtu!” alisema huku akiwehuka.
“Sasa hizi meseji aliandika nani?”
“Sijui! Lakini sikuwahi kuchati na huyu mtu!”
“Olotu! Niliahidi kukutetea, lakini umefanya uzembe sana, yaani hata meseji umeshindwa kufuta?”
Alichanganyikiwa mno, meseji hazikuwa zikifutika, ndani ya saa moja, polisi kutoka jijini Nairobi wakafika hapo, wakamchukua na kuanza kwenda naye huko huku wakiwa na simu yake. Njiani, alikuwa akilia kama mtoto, alijitetea kwamba hakukuwa na meseji alizokuwa amechati na mtu huyo bali kulikuwa na mtu aliyefanya jambo hilo.
“Sikuchati na mtu yeyote yule,” alisema kwa sauti akiwa ndani ya gari la polisi.
“Hiyo utakwenda kusema kwa mahakama,” alisema polisi mmoja kwa lafudhi ya Kikenya.

Je, nini kitaendelea?
 
Back
Top Bottom