Dunia haina usawa

Dunia haina usawa

SEHEMU YA 108

“Mungu hakutuumba kwa ajili ya kuwa watoto wa mitaani, hakutuumba ili tuwe ombaomba mitaani, kuna mtu au watu ambao wamesababisha sisi kuwa katika hali hii! Ni lazima tupambane na tutoke huku! Ni lazima turudi kule tulipokuwa,” alisema Irene.

Wakati wakizungumza hayo walikuwa katika Barabara ya Ali Hassani Mwinyi wakiomba. Hakukuwa na mtu ambaye aliwagundua, wakati baba yao alipokuwa na jina kubwa nchini Tanzania, walikuwa wadogo sana. Waliokuwa na pesa waliwasaidia lakini wala ambao hawakuwa na kiasi chochote kile, waliwapita kama hawakuwaona.

“Jamani! Kwa nini hampo darasani?” aliuliza mwanamke mmoja, alikuwa akizungumza na Irene.
“Sisi ni masikini mama!”

“Mbona mnaonekana wakubwa hivyo! Wazazi wenu wapo wapi?” aliuliza mwanamke huyo, alikuwa kwenye gari lake, Land Cruiser nyeusi.

“Baba alikufa! Mama yetu masikini! Hana pesa ndiyo maana tunaomba kumsaidia,” alijibu Irene huku akimwangalia mwanamke huyo usoni.
“Sawa.”

Mwanamke huyo aliwaonea huruma, alimwangalia Irene, akamwangalia Godwin, walikuwa watoto wazuri walioonekana kuwa na akili sana.

Alitamani kuwasaidia, si pesa tu, alitamani kuwapa maisha mazuri lakini kitu pekee alichokuwa akikihitaji ni kuonana na mzazi wa watoto hao.
“Ninahitaji kuwasaidia, huwa mnapatikana wapi?” aliuliza mwanamke huyo.

“Hapahapa!”
“Sawa. Wiki ijayo nitakuja kuzungumza nayi kwa kirefu. Mmesikia?” aliuliza mwanamke huyo.
“Ndiyo mama!”

Mwanamke huyo akaingiza gia na kuondoka mahali hapo. Kichwa chake kilichanganyikiwa. Aliolewa na mumewe, aliishi katika ndoa kwa miaka kumi na tano na hakubahatika kupata watoto.

Kitendo cha kuwaona watoto hao kilimfanya kujisikia huruma mno moyoni mwake. Alitamani nyumbani kwake kuwe na watoto, alitamani sana kuwachukua watoto wa ndugu zake na kuishi nao lakini ndugu haohao ndiyo waliokuwa na gubu, kumsema kila siku hiyo kuachana na watoto wao.
 
SEHEMU YA 109

Moyo wake ukatua kwa Godwin na Irene, akajiwekea nadhiri moyoni mwake kwamba ni lazima awasaidie watoto hao kama watoto wake.

Alitaka kufanya hivyo baada ya kumshauri mumewe, alijua jinsi mwanaume huyo alivyokuwa na kiu ya kuwa na watoto ndani ya nyumba yake, aliamini kabisa kwamba kama angemshirikisha, hakika asingekataa.

*** “Huyu chizi vipi?” aliuliza jamaa mmoja, alikuwa muuza duka katika mtaa wa Mikocheni.
“Hata mimi nashangaa! Halafu amekuja kuweka makazi hapa! Kweli huu ni mtaa wa machizi jamani?” aliuliza jamaa mwingine.

Macho yao yalikuwa yakimwangalia mwanaume asiyekuwa na akili ambaye alikuwa akitangatanga katika Mtaa wa Mbuni, Mikocheni. Kila mmoja alishangaa, huo waliuita mtaa wa matajiri, hawakuwa na historia ya kumuona kichaa akirandaranda mitaani, hawakujua kichaa huyo alitoka wapi kwani hata kumsogelea waliogopa kwa kuwa mkononi mwake alikuwa na fimbo ndefu.

Kila mmoja alitamani kumfuata kichaa huyo na kumfukuza lakini hakukuwa na mtu aliyethubutu kumfuata. Hawakumpenda, walimjadili kila siku lakini hawakupata jibu juu ya kitu gani walitakiwa kumfanya.

Mbali na kichaa huyo pia waliwaangalia Rosemary na watoto wake, kama ilivyokuwa kwa kichaa yule, hata mwanamke huyo hawakupenda kumuona mahali hapo. Hiyo haikuwa sehemu ya kuwaweka ombaomba wa mitaani wala vichaa lakini walishindwa kujua wafanye nini.

“Tuanze na kichaa au huyu mwanamke?” aliuliza jamaa mmoja.
“Kichaa kwanza! Yule mwanamke na watoto wake tuachane nao, wanatafuta maisha, ni masikini. Ila huyu kichaa tumtoeni mtaani kwetu,” alisema jamaa mwingine.

Hawakujua sababu ya kichaa yule kuwa mahali hapo, hawakujua alitoka wapi, walichokiangalia ni kuona kichaa huyo akiondolewa mahali hapo mara moja.

Wakaitana vijana wote wa mtaani, wakaweka nguvu za kutaka kuhakikisha mtu huyo anaondolewa mahali hapo pasipo kujua kwamba kichaa huyo alikuwa ni ofisa wa Usalama wa Taifa ambaye alifika hapo kwa kazi maalumu ambayo hawakuijua.

Je, nini kitaendelea?
 
DUNIA HAINA USAWA

“Huyu chizi vipi?” aliuliza jamaa mmoja, alikuwa muuza duka katika mtaa wa Mikocheni.
“Hata mimi nashangaa! Halafu amekuja kuweka makazi hapa! Kweli huu ni mtaa wa machizi jamani?” aliuliza jamaa mwingine.
Macho yao yalikuwa yakimwangalia mwanaume asiyekuwa na akili ambaye alikuwa akitangatanga katika Mtaa wa Mbuni, Mikocheni. Kila mmoja alishangaa, huo waliuita mtaa wa matajiri, hawakuwa na historia ya kumuona kichaa akirandaranda mitaani, hawakujua kichaa huyo alitoka wapi kwani hata kumsogelea waliogopa kwa kuwa mkononi mwake alikuwa na fimbo ndefu.
Kila mmoja alitamani kumfuata kichaa huyo na kumfukuza lakini hakukuwa na mtu aliyethubutu kumfuata. Hawakumpenda, walimjadili kila siku lakini hawakupata jibu juu ya kitu gani walitakiwa kumfanya.
Mbali na kichaa huyo pia waliwaangalia Rosemary na watoto wake, kama ilivyokuwa kwa kichaa yule, hata mwanamke huyo hawakupenda kumuona mahali hapo. Hiyo haikuwa sehemu ya kuwaweka ombaomba wa mitaani wala vichaa lakini walishindwa kujua wafanye nini.
“Tuanze na kichaa au huyu mwanamke?” aliuliza jamaa mmoja.
“Kichaa kwanza! Yule mwanamke na watoto wake tuachane nao, wanatafuta maisha, ni masikini. Ila huyu kichaa tumtoeni mtaani kwetu,” alisema jamaa mwingine.
Hawakujua sababu ya kichaa yule kuwa mahali hapo, hawakujua alitoka wapi, walichokiangalia ni kuona kichaa huyo akiondolewa mahali hapo mara moja.
Wakaitana vijana wote wa mtaani, wakaweka nguvu za kutaka kuhakikisha mtu huyo anaondolewa mahali hapo pasipo kujua kwamba kichaa huyo alikuwa ni ofisa wa Usalama wa Taifa ambaye alifika hapo kwa kazi maalumu ambayo hawakuijua.
***
“Kuna taarifa gani kuhusu yule mwanamke?” ilisikika sauti kutoka upande wa pili.
“Kila kitu kipo kama kilivyopangwa. Anapigwa na maisha!”
“Safi sana! Inatakiwa tufuatilie kila kitu kitakachoendelea katika maisha yake. Ninahitaji vijana zaidi wamfuatilie kila hatua, hatakiwi kuyafurahia maisha, ninataka ale matunda ya kazi aliyoifanya mumewe,” iliendelea kusikika sauti ya mwanaume huyo.
Huo ndiyo ulikuwa mpango uliopangwa, ilikuwa ni lazima kuhakikisha kwamba Rosemary na watoto wake wanaishi kwenye maisha ya tabu kwa kuwa hawakustahili kuishi maisha ya raha hata siku moja.
Hilo ndilo lililofanyika, vijana wakaandaliwa na kuanza kufanya kazi waliyotumwa. Rosemary na familia yake walipokuwa Tandale, vijana hao nao wakaenda huko, wakapanga vyumba na kutulia huko.
Walitakiwa kupeleka ripoti kila baada ya siku mbili ili wakubwa wajue ni kitu gani kilichokuwa kikiendelea. Wakati mwingine vijana hao waliwaonea huruma lakini hawakutakiwa kujali, ilikuwa ni lazima kuhakikisha anaishi maisha ya tabu kwa sababu tu walipewa maagizo ya kufanya hivyo.
Walikuwa nao hatua kwa hatua, walipohama Tandale na kuhamia mtaani huko Mikocheni, hawakuweza kuwafuatilia bali walipeleka ripoti kwamba mwanamke huyo na familia yake walihamia huko na hivyo kulitakiwa kupelekwa mtu wa kuendelea kuwafuatilia.
Waliamini kwamba kama wangewaweka vijana wa kawaida, basi watu waliokuwa wakiishi mahali hapo wangeweza kuwashtukia hivyo walichokifanya ni kumuweka kijana aliyeonekana kuwa kama kichaa kwa ajili ya kuendelea kumfuatilia mwanamke huyo na familia yake.
Hilo halikuwa tatizo, baada ya siku kadhaa, mwanaume mmoja, mwendawazimu akaanza kuonekana mtaani hapo. Kila mmoja alihisi kwamba alikuja na kuondoka lakini kilichowashangaza ni kwamba maisha yake yakaanzia hapo, wakati Rosemary akiwa na familia yake upande mmoja, mwenyewe aliweka kijiwe chake upande mwingine.
Ilikuwa ni vigumu kugundua kama mwanaume huyo alikuwa na akili timamu, muonekano wake ulikuwa kama kichaa, alitembea na fimbo na alionekana kuwa mkali hasa.
Pembeni yake kulikuwa na mifuko kadhaa, ilionekana kama takataka, alivaa nguo za kuchakaa lakini kiunoni alikuwa na bastola yake ya kujilindia kama kungekuwa na tatizo lolote lile.
Wakati vijana wa mtaa huo wakijiandaa kumfuata kwa ajili ya kumuondoa mahali hapo, aliwaona, alitulia, akachukua fimbo yake na kusimama, akawaangalia watu hao ambao walionekana kuwa na dhamira ya kutaka kumuondoa mahali hapo.
“Vipi sasa?” aliuliza jamaa mmoja, alionekana kuogopa kwani kwa jinsi kichaa yule alivyosimama na fimbo yake, aligundua kabisa kwamba kungekuwa na hatari mahali hapo.
“Tumsogeleeni!”
“Mmh! Tutamuweza jamani?” aliuliza jamaa mwingine.
Walikuwa wakijiuliza, kumuondoa kichaa huyo mtaani kwao likaonekana kuwa zoezi kubwa na gumu ambalo kulifanya ilihitajika nguvu za ziada. Walimwangalia, naye alikuwa imara akiwaangalia kwa hasira kubwa.
Waliogopa, hawakuwa radhi kuumia hivyo walichokifanya ni kupiga hatua kurudi nyuma na kumwacha akiendelea na mambo yake. Alionekana kuwa kero lakini hawakuwa na la kufanya, waliwasiliana na serikali ya mtaa lakini nao walishindwa kumtoa kichaa huyo mahali hapo.
Rosemary hakujua kama alikuwa akifuatilia yeye na familia yake. Maisha yake yaliendelea na kila siku alikuwa akiteseka. Hakuwa na muda wa kwenda kutafuta pesa, alijulikana na watu wengi hivyo kuhisi kwamba kama angekwenda huko angeweza kuonekana na waandishi wa habari na kumripoti katika vyombo vyao vya habari.
Watoto wake ndiyo walikuwa kila kitu kwake. Walipokuwa wakirudi nyumbani, walimgawia kiasi cha fedha ambacho walikipata mitaani na maisha kusonga mbele.
“Tumekutana na mwanamke mmoja hivi,” alisema Irene huku akimwangalia mama yake, alikuwa na shauku kubwa ya kumwambia kuhusu mwanamke waliyekutana naye.
“Nani?”
“Sijui! Ila amesema kwamba anataka kutusaidia!” alisema Irene.
“Kuwasaidia? Kivipi?”
Irene akaanza kumuhadithia kila kitu kilichotokea barabarani, jinsi mwanamke huyo alivyowaona na kuwaonea huruma kwa hali waliyokuwa nayo. Rosemary alimsikiliza kwa makini, hakumfahamu mwanamke huyo lakini kitendo cha kusema kwamba awachukue watoto hao na kuondoka kwenda kuishi nao lilionekana kuwa jambo gumu mno.
“Haiwezekani!” alisema Rosemary.
“Mama! She is a good woman!” (mama! Ni mwanamke mwema.)
“No! You can’t leave me here? I just want to live with you both,” (hapa! Hamuwezi kuniacha! Ninataka kuishi na nyie wote wawili).
Huo ndiyo ukweli, hao walikuwa watoto wake, kwake, walikuwa kila kitu katika maisha yake. Hakutaka mtu yeyote aje na kuwachukua, aliwapenda, japokuwa hakuwa na kitu, japokuwa alikuwa masikini mkubwa sana lakini suala la kuwaacha watoto wake lilikuwa gumu mno.
Hakutaka kumwamini mtu yeyote katika maisha yake, hakumjua mbaya wake alikuwa nani, alihisi kwamba inawezekana huyo mbaya wake alikuwa akimfuatilia, aliamini kwamba kama angeruhusu watoto wake waondoke mikononi mwake basi wasingekuwa salama.
Alitaka kuendelea kuishi nao ili hata kama ingetokea kufa basi afe akiwa mikononi mwao. Kukataa kwa mama yao kuliwaumiza mno mioyoni mwao. Hakukuwa na kitu walichokitamani wakati huo kama kusoma, waliamini kwamba kama wangekwenda kwa mwanamke huyo ilikuwa ni lazima kuwasomesha kama walivyokuwa wakifanya zamani.
Walihuzunika lakini hawakutaka kumuonyeshea mama yao huzuni zao. Walitamani kumuona akiwa na furaha muda wote, walitamani kumuona akisahau kila kitu kilichokuwa kimetokea na kuishi maisha ya kawaida.
Siku iliyofuata, kama kawaida wakaamka asubuhi na mapema na kuelekea mitaani kama kawaida. Hayo yalikuwa maisha yao ya kila siku na jioni walipokuwa wakirudi walikuwa na kiasi cha fedha cha kutosha ambacho walimpa mama yao.
Baada ya wiki moja, wakafanikiwa kukutana na mwanamke yule ambaye alijitambulisha kwa jina la Angelina, ila alipenda sana kuitwa kwa jina la Madam Angelina. Akawaambia kwamba alitaka kuonana na mama yao kwa ajili ya kuzungumza mawili matatu kwani bado mpango wa kwenda kuishi nao.
“Ila mama alikataa!” alisema Irene, wakati huo Godwin alikuwa kimya kabisa.
“Wala usijali! Nina uhakika atakubali! Nitazungumza naye tu,” alisema mwanamke huyo.
Akawaambia waingie ndani ya gari, wakafanya hivyo na kuondoka mahali hapo. Kitendo cha kuwa humo tu, mawazo yao yalianza kukumbuka mbali, siku ambayo baba yao alikuwa akiwafuata shuleni na kuwachukua kisha kuondoka nao.
Mule garini, walikuwa wakitokwa na machozi kwani hawakukumbuka mara ya mwisho kupanda gari ilikuwa lini. Madam Angelina aliwaonea huruma, kila alipowaangalia, walikuwa watoto wazuri ambao walistahili kupewa maisha mazuri, hawakutakiwa kuwa mitaani, walitakiwa kuwa shuleni wakisoma.
Hawakuchukua muda mrefu wakafika mahali walipokuwa wakiishi, wakateremka na kisha kukifuata kibanda chao ambapo mara baada ya kuingia, mwanamke yule akapigwa na mshtuko, hakuamini yule aliyemuona ndani ya kibanda kile, alimfahamu, alikuwa Rosemary, mwanamke mpole, mke wa mwanasiasa mkubwa sana nchini Tanzania.
“Rosemary!” aliita huku akionekana kushtuka.’
“Ndiyo mimi!”
“Nini kimetokea?”
Rosemary hakujibu kitu zaidi ya kulia tu. Moyo wake ulimuuma, swali hilo likaanza kuyarudisha mawazo yake nyuma, tangu siku za kwanza alipoanza kunyanyaswa mpaka kufikia hatua ya kufukuzwa nyumbani kwake.
Moyo wake ulimuuma mno. Madam Angelina akaanza kumbembeleza akimtaka kunyamaza. Baada ya kunyamza akaanza kumuhadithia mwanamke huyo kila kitu kilichokuwa kimetokea kwenye maisha yake.
Madam Angelina aliumia moyoni, yeye mwenyewe akahisi kabisa kwamba kulikuwa na mtu aliyekuwa amehusika katika maisha ya mwanamke huyo, ila alimuahidi kumpa msaada wa hali na mali.
“Nitakusaidia mpaka unapata kila kitu chako,” alisema Madam Angelina huku akimwangalia Rosemary.
“Nitashukuru sana!”
Hata suala lililokuwa limemleta nyumbani hapo hakulizungumzia, alikuwa na maumivu makali hivyo kuondoka. Akaingia ndani ya gari lake, kabla ya kuliwasha, akaegemea usukani na kuanza kulia kama mtoto, maisha ya Rosemary na watoto wake yaliugusa moyo wake vilivyo.
Alikaa kwenye hali hiyo kwa dakika kadhaa, akawasha gari na kuondoka mahali hapo. Wakati akiwa kwenye barabara ya lami maeneo ya Rose Garden, akashtukia magari mawili yakifunga breki mbele yake, wanaume wawili waliokuwa na bunduki wakateremka, watu wakashangaa, wanaume hao wakapiga risasi juu, kila mmoja akakimbia.
Wakalifuata gari lile, wakapiga kioo kwa bastola, kikavunjika, wakaufungua mlango na kumshusha Madam Angelina kisha kuanza kumpeleka lilipokuwa gari lao.
“Naomba msiniue! Nitawapeni kiasi chochote cha fedha,” alisema Madam Angelina huku akilia.
“Hatuhitaji pesa zako! Tunachotaka ni roho yako tu,” alisema mwanaume mmoja na kumuingiza ndani.
Kila kilichokuwa kikiendelea, watu walikuwa wakishuhudia kwa kujificha. Ilionekana kama muvi fulani ya mapigano ya Kimarekani.
***
Kazi waliyokuwa wametumwa waliifanikisha kwa asilimia sabini. Waliambiwa wamteke Madam Angelina kwa kuwa alikuwa kimbelembele kumsaidia Rosemary ambaye hakutakiwa kupata faraja yoyote ile, hakutakiwa kusaidiwa kwa kitu chochote.
Mawasiliano yakafanyika na kuwaambia watu waliowatuma kwamba tayari mwanamke huyo alikuwa mikononi mwao na walisubiri kuambiwa ni kitu gani walitakiwa kufanya wafanye.
Mtu kutoka upande wa pili akawaambia kwamba mwanamke huyo alitakiwa kufa, hakutakiwa kuachwa kwani kwa kile alichokuwa amekifanya kiliwachanganya mabosi na hakutakiwa kuachwa hai hata mara moja.
“Sawa mkuu!”
Safari ilikuwa ikiendelea, Madam Angelina alikuwa akilia ndani ya gari, hakujua ni kitu gani alikuwa amekifanya, alihisi watu hao walikuwa majambazi, walimteka kwa sababu walihitaji pesa lakini alipowaambia suala la kuwapa pesa, wakakataa na kumwambia kwamba walichokihitaji kilikuwa ni roho yake tu.
Alikiona kifo, bastola walizokuwa wamezishika wanaume wale ziliwaogopesha na kuona kwamba mwisho wake ulikuwa umekaribia. Alitamani kumpigia simu mumewe na kumwambia kile kilichomtokea lakini alishindwa kufanya hivyo kwani simu yake ilikuwa ndani ya gari lake.
“Naomba msiniue…naomba msiniue,” alisema Madam Angelina huku akilia kama mtoto.
“Tumesema tuna kazi na roho yako! Hata ulie machozi ya damu jua kwamba wewe kuiona kesho ni vigumu sana,” alisema mwanaume mmoja kwa jeuri huku akimwangalia Madam Angelina.
Kilio chake hakikusaidia kitu, wanaume wale walikuwa na lengo moja tu, kumuua na kuutelekeza mwili wake. Safari iliendelea mpaka walipokaribia katika Msitu wa Pande.
Kilio cha Madam Angelina kiliongezeka zaidi, aliufahamu msitu huo, kulikuwa na watu wengi waliokuwa wakiuawa huko na miili yao kutelekezwa, akajua kwamba huo ndiyo ulikuwa mwisho wake na wanaume wale walipomwambia kwamba lazima afe walimaanisha na walichokuwa wakikisema.
Gari likakata kona kulia, likatoka katika barabara ya lami na kuingia katika msitu wa Pande. Madam Angelina aliendelea kulia, alivikutanisha viganja vyake na kuanza kusali kwani hakuona kama kungekuwa na dalili za kuachwa salama humo.
Gari lilipita msituni, liliendelea mbele mpaka lilipofika sehemu kulipokuwa na nyasi nyingi, likasimama na kisha kumteremsha na kumuweka chini. Mwanaume mmoja akachukua bastola yake na kuikoki tayari kwa kumfyatulia Madam Angelina risasi.
“Yule wa siku ile kule Tanganyika Parkers ulimuua wewe, leo huyu wangu,” alisema mwanaume huyo.
“Haina shida. Ua fasta tusepe!”
“Na mwili wake?”
“Tuuacheni hukuhuku!”
“Tukiwa tumeuzika?”
“Tuuzike? Tunauzikaje kwa mfano? Ndege watakula wapi? Ni dhambi kuua ila ni thawabu kuwapa ndege chakula chao,” alisema jamaa mmoja.
“Sawa. Let me kill her,” (sawa. Acha nimuue) alisema jamaa huyo ambapo akachukua bastola yake na kumnyooshea Madam Angelina na kumuua kama walivyofanya kwa Juma.
****
Matumaini yalianza kurudi tena, kila mmoja akaona kabisa kwamba siku chache zijazo maisha yangekuwa nafuu, kusingekuwa na harakati zao za kuombaomba mitaani. Walimwamini Madam Angelina, kwa jinsi alivyokuwa ameongee nao, walikuwa na uhakika wa kupata maisha mazuri.
Walikumbuka shule, walitamani kurudi darasani na kusoma kama ilivyokuwa zamani, hawakutaka kuendelea kuishi mitaani kwani waliamini kwamba kwa staili yoyote ile ilikuwa ni lazima kurudi darasani na kuendelea kusoma, kwa jinsi maisha yao yalivyokuwa, hawakuona kama walistahili kuwa mitaani kama walivyokuwa.
Walimsubiri Madam Angelina, siku ya kwanza ikakatika, ya pili ikaingia na kukatika lakini bado hawakupata mawasiliano kutoka kwa mwanamke huyo. Hilo hawakuwa na hofu nalo, hawakujua kama kulikuwa na kitu kibaya kilitokea, kitu pekee ambacho walikiamini ni kwamba alikuwa akijiandaa kuwasaidia, na kama hakuwa akionekana basi alikuwa akifuatilia shule ambazo walitakiwa kwenda kusoma.
Wiki ya kwanza ikakatika, hawakupata taarifa zozote kutoka kwa mwanamke huyo, hawakukata tamaa, kwa jinsi Madam Angelina alivyojitolea kuwasaidia, alivyowaambia maneno matamu ya matumaini walikuwa na uhakika kwamba angerudi tena.
Wiki ya pili ilipoingia ndipo wakagundua kwamba mwanamke huyo asingeweza kurudi tena. Walimsubiri, kama kweli alikuwa na lengo la kuwasaidia ilikuwa ni lazima kuwarudia na kuwapa kila kitu alichowaambia kabla.
“Will she come back?” (atarudi?) aliuliza Irene huku akimwangalia mama yake, macho yake tu yalionyesha jinsi alivyochoka kusubiri.
“I don’t know! We have to wait!” (sijajua! Tunapaswa kusubiri) alijibu mama yake.
Hawakuchoka kusubiri, hawakuwa na msaada wowote kutoka sehemu yoyote ile zaidi ya kwa Madam Angelina ambaye hawakujua alikuwa wapi. Walikuwa wavumilivu na mpaka mwezi unakatika, mwanamke huyo hakutokea, na si hivyo tu bali hata dalili za kutokea tena hazikuwepo.
****
Mawasiliano yalikuwa yamefanyika kwamba Madam Angelina alitakiwa kuuawa haraka iwezekanavyo. Hakutakiwa kuachwa hai, kitendo cha kutaka kumsaidia Rosemary na familia yake tayari alijiwekea uadui kati yake na watu waliokuwa wamesababisha mwanamke huyo kuwa kwenye hali hiyo.
Vijana waliowatuma walifanya kazi, walifanikisha mpango wa kumteka na muda huo walikuwa safarini kuelekea msituni ambapo ndipo wangefanya mauaji hayo.
Baada ya dakika kadhaa, mwanaume mmoja akapiga simu na kuanza kuzungumza na mtu aliyekuwa Masaki ambaye kazi yake ilikuwa ni kuchukua maelekezo na kuwapa vijana wale.
“Wamefikia wapi?” aliuliza mwanaume huyo kwa sauti nzito.
“Ndiyo wapo njiani kwenda kummaliza,” alijibu huku siku ikiwa sikioni.
“Nimebadili mawazo!”
“Yapi hayo!”
“Asiuawe kama ilivyotakiwa bali anatakiwa kupewa onyo kali!” alisema mwanaume huyo.
“Lakini tutakuwa tumechelewa, nahisi tayari watakuwa wamemuua!” alisema mwanaume huyo.
“Wasiliana nao! Kama bado, waambie waache kufanya hivyo, ila wamwambie akae mbali na familia hiyo, kama ataonekana tena, tutammaliza,” aliikika mwanaume huyo.
Baada ya kukata simu, haraka sana simu nyingine ikapigwa kwenda kwa wale vijana kwa ajili ya kuwapa maagizo aliyokuwa amepewa na mtu aliyemzidi cheo.
Wakati huo ambao simu ilikuwa ikiita ndiyo kipindi ambacho wanaume hao walikuwa msituni na mmoja alishikilia bastola kwa ajili ya kumuua Madam Angelina.
Mwanamke huyo alilia, alisali sala yake ya mwisho, hakuona dalili za kunusurika kifo mahali hapo. Wakati akiwa anamalizia sala ya Baba Yetu, mara simu ya mwanaume aliyeshika bastola ikaanza kulia.
“Halo mkuu!” aliita.
“Umekwishafanya nilichokuagiza?”
“Ndiyo nataka nimuue hapa!”
“Ila bado?”
“Ndiyo!”
“Sasa kuna maagizo mapya!”
“Yapi? Tumchinje kama mbuzi chang’ombe?” aliuliza.
“Hapana! Muacheni ila mumpe masharti kwamba hatakiwi kuisogelea familia ile, vinginevyo, atauawa,” alisema mwanaume huyo na simu kukatwa.
Yule jamaa akabaki akimwangalia Madam Angelina, hakuamini kama alinusurika kuuawa na wakati tayari kila kitu kiliandaliwa na kilichobaki kilikuwa ni kubonyeza kitufe cha kuruhusu risasi itoke.
Akamshika mkono na kumuinua, akamwambia aingie ndani ya gari kitendo ambacho wenzake wote walibaki wakishangaa kwani hayo hayakuwa maagizo waliyokuwa wamepewa, hawakusikia maagizo hayo mapya.
“Vipi tena?” aliuliza jamaa mwingine huku akionekana kushangaa.
“Huyu mwanamke inabidi aende kusali! Tena akasali mpaka ibada za katikati ya wiki. Amepona! Kweli ana Mungu,” alisema jamaa huyo.
“Kwani imekuwaje?”
“Nimepigiwa simu na kuambiwa tumuache huru, aondoke, ila kuna mambo nataka nimwambie,” alisema yule jamaa na kumwangalia Madam Angelina aliyekuwa akilia, hakuamini kama alinusurika.
Alimwambia kama aliyoambiwa kwamba hakutakiwa kujihusisha na familia hiyo, hakutakiwa kujifanya kuwa msamaria mwema kwa familia hiyo, hilo lilikuwa onyo kali na kama angeendelea kuwasaidia basi mwisho wake ungekuwa mbaya, ni lazima angerudishwa tena msituni pale kuuawa.
“Ahsanteni! Ahsanteni!” alisema Madam Angelina.
“Na kilichotokea huku hutakiwi kumwambia mtu yeyote, hata ukimwambia mumeo na tukajua, bado tutakutafuta na kukuua! Umesikia?” alisema mwanaume huyo.
“Ndiyo!”
“Sawa. Ila una Mungu sana! Hudhuria kanisani kila siku! Kupona kwako ni mpango wa Mungu tu,” alisema jamaa huyo na safari ya kurudi mjini kuanza huku Madam Angelina akiwa haamini kama kweli alinusurika kuuawa msituni.
***
Madam Angelina aliogopa, hakuamini kama alinusurika kufa kutoka katika mikono ya watu asiowafahamu ambao walitumwa kwa ajili ya kummaliza. Kila wakati aliikutanisha mikono yake na kuanza kumshuruku Mungu kwa muujiza aliomtendea.
Gari lilirudi mpaka Sayansi, Kijitonyama na kuambiwa kwamba gari lake lilikuwa katika Kituo cha Polisi cha Mabatini. Akateremka, akachukua bodaboda huku akionekana kuhofia mno, hakujiona kama alikuwa salama, hakuona kama alitakiwa kumwambia mumewe kwani aliamini kuwa watu wale wangeweza kumfuata muda wowote ule.
Wakati safari ya kwenda kituoni ikiendelea kichwa chake kilikuwa na mawazo mengi, alikuwa akijiuliza kuhusu wale watu, walitoka wapi na kwa nini hawakutaka kuona akimsaidia Rosemary na watoto wake.
Moyo wake ukauma, ukachoma kupita kawaida. Aliikumbuka familia ile, ilikuwa moja ya familia masikini kuliko za watu wote aliokuwa akiwafahamu. Walishuka kwa kasi kubwa kwenda chini, yeye na mumewe walipanga kuwasaidia lakini mwisho wa siku akatekwa na kupelekwa polisi mpaka simu ilipopigwa na vijana wale kupewa maagizo kwamba hawakutakiwa kumuua.
“Ni nani yupo nyuma ya mpango huu? Na kwa nini hawataki nimsaidie Rosemary na familia yake?” alijiuliza Madam Angelina.
Safari haikuwa ndefu sana wakafika katika Kituo cha Polisi cha Mabatini. Kwa mbali, akaliona gari lake, akamshukuru Mungu, akateremka na kuanza kuelekea ndani ya kituo hicho mpaka kaunta ambapo akawahadithia polisi aliowakuta kila kitu kilichotokea.
Polisi walikuwa kimya wakimwangalia na kumsikiliza. Madam Angelina alisimulia huku akionekana kuumia moyoni, machozi yalikuwa yakimtiririka mashavuni mwake kiasi kwamba polisi wote waliokuwa kituoni hapo wakamuonea huruma.
“Pole sana mama! Ila watu wanapotea sana sasa hivi, nafikiri kuna kitu,” alisema polisi mmoja aliyekuwa na muonekano wa kikakamavu, hata mwili wake ulikuwa na misuli mingi.
“Sisi kama jeshi la polisi ni lazima tupambane kwa ajili ya wananchi wetu, hatutaruhusu kuona jina la nchi yetu likichafuliwa,” alisema polisi mwingine maneno yaliyoungwa mkono na kila mmoja.
Akaandikisha maelezo yote yaliyotakiwa kituoni hapo na polisi walipojiridhisha, wakamruhusu kuondoka na gari lake ambapo breki yake ya kwanza ilikuwa nyumbani kwake.
Alimkuta mumewe akiwa na wasiwasi tele, muda mwingi alijaribu kumpigia simu, haikuwa ikipokelewa mpaka kikafika kipindi simu ikazima chaji na kutokupatikana kabisa.
Alikuwa na hofu, alihisi kwamba kulikuwa na jambo baya lilikuwa limetokea, aliwasiliana na ndugu zake wengine kumuulizia, hakumpata, akawasiliana na marafiki zake lakini kote huko aliambulia patupu mpaka pale ambapo alimuona akiingia ndani ya nyumba hiyo.
Muonekano wake tu ulionyesha kulikuwa na kitu kibaya kimetokea, alizoea kumuona mkewe akiwa kwenye hali ya furaha hata kama kulikuwa na jambo baya, hakuonekana kuwa mwanamke mwenye kuonyesha huzuni zake lakini kwa siku hiyo, Madam Angelina alishindwa kabisa, mumewe aliposimama na kumsogelea tu, akaanza kulia.
“Kuna nini? Kuna nini mke wangu?” aliuliza mumewe, Mzee Paul Semenya.
“Nilitekwa!”
“Ulitekwa? Kivipi? Ilikuwaje?” aliuliza mumewe maswali mawili mfululizo.
Madam Angelina akaanza kumuhadithia kila kitu kilichotokea. Mzee Semenya alikuwa kimya akimsikiliza mkewe, moyo wake ulimuuma kwani suala la kutekwa aliwahi kulisikia sehemu nyingi na hakuamini kama kuna siku hata mke wake angetekwa kama watu wengine.
Huo ndiyo ukawa mwisho wa kuisaidia familia hiyo. Kwa tukio lililotokea waliamini kwamba kulikuwa na watu wabaya ambao walikuwa wakiwafuatilia kwa kila kitu kilichokuwa kikitokea.
Madam Angelina hakutaka kuzungumza na watoto wa Rosemary, kila alipokuwa akielekea kazini, barabarani alikuwa akiwaona, aliumia, maisha yao yalimuumiza moyo wake lakini hakuwa na jinsi, alikuwa akiwapita kama hawaoni kwani alijua kuwa endapo angethubutu kutoa kiasi chochote na kuwasaida, angeweza kutekwa kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma.
***
Maisha hayakuwa na afadhali hata siku moja, waliendelea kuteseka mitaani, pale walipokuwa wakiishi hapakuwa salama hata mara moja, hawakuwa na nyumba, kilikuwa ni kibanda kidogo sana ambacho kila walipokuwa wakilala kipindi cha mvua na kunyesha, walilowa na hivyo kukesha macho usiku mzima.
Hawakuyapenda maisha hayo ila hawakuwa na jinsi kwani mtu ambaye waliamini kwamba angewasaidia alikuwa Madam Angelina ambaye mpaka kipindi hicho hakujua alikuwa wapi kwani aliwaahidi kwamba angewarudia tena na kuwasaidia lakini, hakuonekana.
“Mama! Mbona Madam Angelina harudi?” aliuliza Godwin huku akimwangalia mama yake.
“Atarudi tu! Labda amepata matatizo! Ila atarudi tu,” alijibu Rosemary huku akimwangalia Godwin, japokuwa alimtia moyo lakini alijua kabisa kwamba ilikuwa ni vigumu kwa mwanamke huyo kurudi tena mahali hapo.
“Kwa hiyo tumsubiri tu?” aliuliza Irene.
“Ndiyo! Tuendelee kumsubiri! Atarudi na nyie mtakwenda shuleni tena,” alisema Rosemary.
“Sawa mama!”
Mama yao aliwaambia kwamba Madam Angelina angerudi tena, walimwamini mama yao, hawakuwahi kumsikia akiwadanganya na kila siku alikuwa mkweli na kila kitu ambacho aliwaambia, haikuchukua muda mwingi, kilitokea.
Walikuwa wavumilivu, waliendelea kusubiri, maisha yaliwapiga lakini mioyo yao iliendelea kuwaambia kwamba Madam Angelina angerudi tena na kuwasaidia kama alivyowaahidi kipindi cha nyuma.
Mwezi wa pili ulipoingia na kukatika tangu mara ya mwisho kuonana nao, wakajua kabisa mwanamke huyo asingeweza kurudi tena nyumbani hapo. Hawakujua ni kitu gani kilitokea, kwa jinsi alivyokuwa akizungumza nao kipindi cha nyuma, aliwaonyeshea kila dalili kwamba angerudi tena na kuwasaidia kama alivyokuwa amewaambia.
“Mama! Ndiyo basi tena! Madam hatoweza kurudi tena,” alisema Godwin huku akionekana kuumia mno. Alitamani sana kurudi shuleni, mwanamke huyo aliwaahidi mambo mengi likiwemo suala la kurudi shuleni na kusoma lakini mwisho wa siku, hakurudi, hata kuonekana mbele ya macho yao hakuweza kuonekana tena.
“Tuendelee kusubiri! Naamini kwamba kuna siku atarudi tena. Godwin! Mchungaji huwa anasemaje kuhusu maisha yetu?” aliuliza Roseemary.
“Kuwa na imani!”
“Unaamini kama atarudi tena?”
“Mama! Lakini….”
“Amini mwanangu. Atarudi tena na mtakwenda shuleni kwa mara nyingine. Hili ni jaribu na lazima mkumbuke kwamba kwenye kila jaribu, Mungu ameweka mlango wa kutokea,” alisema Rosemary maneno ambayo kidogo yakawatia nguvu watoto wake na kukubaliana naye kwamba ipo siku Madam Angelina angerudi tena, hawakujua kile kilichokuwa kimemtokea mwanamke huyo.
****
“Mkuu! Kuna simu imepigwa,” alisikika mwanaume mmoja akimwambia kiongozi wake.
“Kutoka wapi?”
“Makao makuu!”
“Inasemaje?”
“Nimepewa maelezo kwamba yule mwanamke anatakiwa kuuawa,” alisema mwanaume huyo.
“Mwanamke gani?”
“Rosemary!”
“Kwa nini umekuwa ni uamuzi wa ghafla namna hiyo?” aliuliza mwanaume aliyepewa ujumbe huo.
“Sijajua! Ila hilo ni agizo!”
“Sawa.”
Hakukuwa na mtu aliyebisha, hayo yalikuwa maagizo kutoka makao makuu kwamba Rosemary alitakiwa kuuawa wakati wowote ule. Watu ambao walisababisha kuwa mahali hapo hawakutaka kumuona akiendelea kuishi, walitaka kummaliza kwani uwepo wake ungeweza kuwasababishia gharama kubwa kwa ajili ya kuwalipa watu ambao kila siku walitakiwa kumfuatilia alikula nini na alifanya nini.
Mikakati kabambe ikaanza kupangwa, kila mmoja alitakiwa kumwambia mwenzake hatua ambayo walitakiwa kuichukua haraka iwezekanavyo. Kikao cha siri cha watu watatu kikawekwa ndani ya chumba kimoja kikubwa kilichokuwa na meza ndogo na viti vitatu.
Wanaume hao waliovalia suti walikaa huku wakiwa na karatasi zao, walikuwa na kalamu kwa ajili ya kuchora ramani ya mauaji ambapo kusingekuwa na mtu yeyote ambaye angegundua kitu chochote kile.
Walikubaliana kwamba wamuue kwa kumuwekea sumu kwenye chakula ila baada ya kufikiria kama kungekuwa na urahisi wa kumpa chakula, wakaona lingekuwa jambo gumu sana hivyo wakakubaliana kumuua kwa kumpiga risasi.
“Lakini ni lazima isionekane kama ameuawa,” alisema mwanaume mmoja.
“Ndiyo!”
“Sasa hamuoni kama tukimuua kwa kumpiga risasi itagundulika kama ameuawa?” aliuliza jamaa mmoja.
“Hilo nalo neno! Kweli kabisa. Sasa kifo gani?”
“Tumgonge na gari! Tuna sababu ya kusingizia kwamba gari lilikatika breki! Halafu hata kama tukiomgonga na kusepa, nani atagundua kama ameuawa? Mbona kuna madereva wengi wanaua na kusepa! Nadhani hakuna tatizo,” alisema mwanaume mwingine.
Wakakubaliana kwamba Rosemary alitakiwa kuuawa kwa kugongwa kwa gari hivyo walitakiwa kupanga vijana kwa ajili ya kuifanya kazi hiyo haraka iwezekanavyo.
“Sawa. Wapigie simu vijana. Mpaka kesho mchana tupewe taarifa ya kifo chake,” alisema mwanaume mmoja.
“Hakuna tatizo!”
Wakakubaliana na kikao kufungwa, kilichobaki kilikuwa ni utekelezaji tu.

Je, nini kitaendelea?
Tukutane wiki ijayo hapahapa.
 
Halaf Davet akiketa hadithi haiwi nzuri
Mwambie hatumtaki
Uwe unaleta mwenyewe tu
Uwiiiii kaka angu jamani usiseme hivyo atasikia ungejua kazi ninayopata kumwambia apost story mm huwa nawaonea huruma jamani kama sijaingia na arosto ndio naanza kubembelezana nae sasa awatumie
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom