Dunia haina usawa

Dunia haina usawa

SEHEMU YA 90

Juma hakunyamaza, aliendelea kuomba msamaha, hakuwajua watu hao walikuwa wakina nani, hakujua walikuwa wakihitaji nini kutoka kwake. Alitetemeka, alilia kama mtoto mdogo huku akiwaambia watu hao wasimuue kwani alikuwa na familia iliyokuwa ikimtegemea.

Wanaume hao ni kama hawakuwa wakimsikiliza, walikuwa wakiendelea kuzungumza huku katika mazungumzo hayo wakijadili ni kwa namna gani walitakiwa kumuua Juma baada ya kuliegesha gari sehemu husika.

Gari lilizidi kusonga mbele, mwendo wao ulikuwa wa kawaida sana, walipofika Kawe karibu na Uwanja wa Tanganyika Parkers, wakaliingiza gari hilo humo na kwenda kulificha nyuma ya jengo moja ambalo zamani lilitumika kama kiwanda cha nyama.

Japokuwa kulikuwa na watu wengi waliloliona gari hilo lakini hakukuwa na mtu aliyekuwa na wasiwasi nalo. Hiyo haikuwa mara ya kwanza magari kufika mahali hapo, kulikuwa na magari mengi yaliyokuwa yakiingia katika uwanja huo, hasa magari ya wachezaji mpira na watu waliokuwa wakienda kutazama mechi mbalimbali.

“Hapa panatosha,” alisema mwanaume mmoja.
“Jamani naomba mnisamehe! Sijafanya lolote lile,” alisema Juma huku akivikutanisha viganja vyake kama ishara ya kuomba msamaha.

“Sawa. Tutakuacha kama tu utatuambia ukweli!” alisema mwanaume mwingine.
“Hakuna shida mkuu! Nitawaambia kila kitu. Haki ya Mungu nitawaambia kila kitu!” alisema Juma huku akitetemeka.
“Ni nani amekutuma ndani ya nyumba ile kuzungumza na yule mwanamke?” aliuliza jamaa mmoja huku akiwa na bastola mkononi mwake.

“Nimetumwa na bosi wangu!”
“Hana jina?”
“Matiku. Adam Matiku!”
“Alivyokutuma alikwambiaje?”
“Aliniambia kwamba nimwambie mwanamke yule kwamba amemtuma mtu anunue ile nyumba halafu atamsaidia kwa kila kitu,” alisema Juma.

“Nadhani unatuchezea mpaka unatudanganya,”alisema mwanaume mmoja kwa lengo la kuambiwa zaidi.
“Haki ya Mungu tena! Siwadanganyi! Naapia, wallahi tena,” alisema Juma.
“Kingine?”
“Ni hayo tu!”
“Sawa.”

Mwanaume mmoja akateremka kutoka ndani ya gari na kupiga simu sehemu fulani, ndani ya sekunde kadhaa akawa anazungumza na mwanaume mmoja kutoka kutoka upande wa pili na kumwambia kila kitu ambacho Juma aliwaambia baada ya kumteka.
 
SEHEMU YA 91

“Kumbe ndiyo hivyo! Sawa. Sasa fanyeni kitu kimoja,” alisikika mwanaume huyo.
“Ndiyo bosi!”
“Muueni na muuache mwili wake hapohapo,” alisikika mwanaume huyo.
“Sawa. Hakuna tatizo!”

Jamaa yule akarudi ndani ya gari na kuwapa ishara wenzake juu ya kile kilichotakiwa kufanywa. Juma hakujua lakini kwa namna wanaume wale walivyokuwa wamebadili mikao yao akajua tu kwamba kulikuwa na kitu kinataka kutokea.

“Jamani! Nimewaambia ukweli! Naomba mniruhusu niondoke,” alisema Juma.
“Boka! Kazi kwako!” alisema mwanaume mmoja, mwenzake aliyeitwa Boka akatoa kitambaa kutoka mfukoni mwake na kumkamata Juma na kumziba pua na mdomo kwa kutumia kitambaa kile.

*** Moyo wa Rosemary ukawa na amani tena, alifurahia lakini kilichokuwa kikimsumbua ni juu ya mwanaume huyo aliyekuwa ameahidi kumsaidia, hakumfahamu, hakujua alikuwa nani lakini kwa mawazo yake, akagundua kwamba alikuwa Rais Bokasa ambaye hakutaka kugundulika kama alikuwa akimsaidia.

Hakuacha kumpigia simu, alipoona haipatikani, akamtumia ujumbe mfupi wa kumshukuru kwa kile alichokuwa amemfanyia kwani alikata tamaa na kuamini kama ndiyo ungekuwa mwisho wake lakini kwa kutumia fedha zake aliweza kumsaidia kulimaliza suala la nyumba.

Kila siku alikuwa akitumiwa kiasi cha fedha, hakujua kilipotoka lakini kila alipokuwa akiangalia kwenye akaunti yake benki, aliona akiwa ameingiziwa kiasi kikubwa cha fedha.

Hicho ndicho kilichoyaendeleza maisha yake, hakutaka kuona watoto wake wakipata tabu, alitaka kuona wakiendelea kusoma katika shule nzuri na za gharama kwa kuwa tu alikuwa na fedha ambazo aliamini kwamba zilitoka kwa Rais Bokasa.

Siku zikaendelea kukatika, baada ya miezi miwili ya msaada wa kifedha, ghafla msaada huo ukakatika, hakukuwa na fedha zilizoingizwa katika akaunti yake. Hakujua sababu iliyomfanya Rais Bokasa kuchukua uamuzi huo, akajipa moyo kwamba labda kulikuwa na vitu vimeingilia hivyo kusubiri na kusubiri lakini hali haikubadilika, hakikuingia kiasi chochote cha fedha katika akaunti yake.
 
SEHEMU YA 92

Hilo likamtia hofu, hakujua ni kitu gani kilikuwa kimetokea na wakati huku akiendelea kusubiri kuona nini kingeendelea, kapokea notisi ya kuhama ndani ya nyumba hiyo.
“Nihame? Nihamie wapi? Ila si niliambiwa nitakaa miaka yote?” alijiuliza pasipo kupata jibu.

Hakutaka kuondoka, alitaka kupata jibu la mtu aliyekuwa amemuagiza kukaa ndani ya nyumba hiyo. Hakuondoka, baada ya wiki moja, wanaume wawili wakafika nyumbani hapo huku wakiwa wameongozana na polisi na kumwambia kwamba siku hiyohiyo alitakiwa kuondoka ndani ya nyumba hiyo.

“Niende wapi?”
“Hiyo haituhusu! Unachotakiwa ni kuondoka humu,” alisema mwanaume mmoja.
“Hapana! Sina pa kwenda, nitakuwa mgeni wa nani mimi?” aliuliza Rosemary.
“Hilo nalo halituhusu! Chukua kila kitu kilichokuwa chako. Tukifunga milango, hutoingia tena ndani ya nyumba hii,” alisema mwanaume mwingine huku akionekana kumaanisha.

“Hapana!”
“Mama! Fanya kama unavyoambiwa, utajuta!” alisema polisi, kidogo Rosemary akaona kwamba watu hao hawakuwa na utani hata kidogo.

Kwa mwendo wa taratibu akaingia ndani ya nyumba yake, akachukua baadhi ya vitu na kutoka nje ambapo watu wale wakafunga milango ya nyumba ile. Hakuamini macho yake, nyumba ambayo aliijenga na mumewe, leo hii ilikuwa ikiondoka mikononi mwake.

Alilia na kulia, hakuondoka mahali hapo, akabaki kibarazani akiwasubiria watoto wake, Godwin na Irene ambao walikuwa shuleni kipindi hicho. Waliporudi, wakashangaa kumuona mama yao akiwa nje ya nyumba ile akilia.

“Mom! Why are you crying?” (mama! Kwa nini unalia?) aliuliza Godwin.
“We have to leave?” (tunatakiwa tuondoke)

“Where to?” (kwenda wapi?) aliuliza Irene huku akionekana kushangaa.
“I don’t know but we have to,” (sifahamu ila tunatakiwa kuondoka) alijibu mwanamke huyo huku akilia kama mtoto.
 
SEHEMU YA 93

Shughuli zilikuwa zikiendelea katika Uwanja wa Tanganyika Parkers kama kawaida. Hakukuwa na mtu aliyejua kama kulikuwa na tukio la kutisha lilitokea katika jengo bovu lililokuwa mahali hapo.

Waliokuwa wakicheza mpira, kama kawaida waliendelea, waliokuwa wakifanya shughuli zingine, nao waliendelea kama kawaida.
Baada ya siku mbili kupita ndipo watu wakahisi kitu cha tofauti, pua zao zikaanza kuhisi harufu mbaya na kali ya mzoga ambapo mara ya kwanza walihisi kwamba alikuwa paka au mbwa lakini kadiri muda ulivyokwenda, harufu hiyo ilikuwa kali tofauti na harufu za mizoga ya wanyama hao.

Kila mmoja akawa na wasiwasi, wengi wakahisi kwamba huo ulikuwa ni zaidi ya mzoga wa wanyama hao hivyo walichokifanya ni kuanza kutafuta ni kitu gani kilikuwa kimesababisha harufu kali namna hiyo.

“Harufu inatokea kwenye jumba,” alisema mwanaume mmoja.
“Twendeni!”
Wakaacha kucheza mpira na kuelekea huko, kila mmoja alitaka kuona ni kitu gani kilichokuwa kimesababisha harufu kali namna hiyo. Walipoingia ndani ya jumba hilo, harufu ikaongezeka zaidi, wakaziba pua zao na kusonga mbele na baada ya kwenda katika pembe moja ya jumba hilo, wakashtuka baada ya kuiona maiti ya mtu ikiwa chini huku imeharibika vibaya.

Wakashtuka, hawakuamini walichokuwa wakikiona, hawakutaka kuchelewa, wakapiga simu katika Kituo cha Polisi cha Kawe ambacho hakikuwa mbali kutoka mahali hapo na kufika katika uwanja huo kwa lengo la kuuchukua mwili huo.
“Imekuwaje?” aliuliza polisi mmoja.

“Tumeshtukia kuiona maiti! Hatujui kitu chochote mkuu!” alijibu mwanaume mmoja huku akiwaangalia polisi waliofika mahali hapo.
“Hakuna watu waliokuja kuitupa hii maiti?” “Hakuna mkuu! Kuna magari mengi huwa yanakuja na kuondoka, hatujui chochote kile,” alijibu jamaa mmoja.

Polisi hao waliwauliza maswali kadhaa watu waliokuwa mahali hapo, walipomaliza, wakaondoka na mwili wa Juma. Nyuma wakaacha minong’ono ya watu, kila mmoja alikuwa akilizungumzia tukio hilo.
 
SEHEMU YA 94

Walishangaa, ilikuwaje mwili ukae siku zote hizo mpaka kuharibika halafu kusiwe na mtu yeyote aliyegundua kama kuna mtu aliuawa? Hakukuwa na mtu aliyemfahamu mtu aliyeuawa kwani mwili ulikuwa umeharibika kupita kawaida.

Taarifa hizo zikawafikia waandishi wa habari ambapo kituo cha taifa kikaitangaza taarifa hiyo kitu kilichomfanya Bilionea Matiku kuhisi kwamba maiti iliyokuwa imeokotwa ilikuwa ya kijana wake, Juma.
Akaifuatilia, aliyakumbuka mavazi aliyokuwa amevaa, saa ya gharama aliyomnunulia, alipofika huko hospitalini ilipohifadhiwa maiti ile, akaomba kuiona.
“Hakuna shida mkuu!”

Akaelekea katika chumba cha kuhifadhia maiti ambapo akaanza kufunguliwa kila droo iliyokuwa na maiti kwa ndani. Akaanza kuziangalia, aliangalia moja baada ya nyingine na alipoona kulikuwa na ugumu wa kuiona maiti ya Juma, akawaambia mahali ilipokuwa imetolewa.
“Kumbe yule aliyeuawa Tanganyika Parkers?”
“Ndiyo!”

Akachukuliwa na kupelekwa katika droo za mwisho kabisa ambapo zikaanza kufunguliwa na kuiona maiti ya Juma. Hakukuwa na ugumu wa kuitambua japokuwa ilikuwa imeharibika vibaya, alipoziona nguo tu, akagundua kwamba alikuwa yeye.

“Polisi wa kituo gani walimleta mahali hapa?” aliuliza Matiku huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Sijajua! Ila kama aliokotwa Kawe, basi ni polisi wa huko ndiyo waliomleta,” alijibu kijana aliyekuwa na jukumu la kuzipokea maiti na kuzihifadhi hapo mochwari.

Matiku akaondoka hospitalini hapo, alitaka kujua kitu kilichokuwa kimetokea Juma, alijua kwamba kulikuwa na watu walimuua, alitaka kuwajua watu hao kwani mara baada ya kumteka, walionyesha kabisa kwamba hawakutaka kitu chochote kutoka kwake zaidi ya roho yake.

Alichukua dakika thelathini mpaka kufika katika Kituo cha Polisi cha Kawe ambapo akahitaji msaada wa ripoti kuhusu maiti iliyokuwa imeokotwa na polisi kumwambia kila kitu kilichokuwa kimetokea.

Hakuridhika, alitaka kumjua mtu aliyefanya mauaji hayo. Ilimuuma moyoni mwake kwani Juma alikuwa mtu muhimu kwake, dereva aliyemwamini kwa kila kitu na wakati mwingine kumpa siri zake nyingi kuhusu wanawake aliokuwa akitembea nao.
 
shunie........nataman kama unisomee niwe naskiliza tu mana nna usingizi balaa..
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom