Dunia haina usawa

Dunia haina usawa

SEHEMU YA 84

Rosemary alichanganyikiwa, aliendesha gari kwa mwendo wa kasi ili kuiwahi nyumba yake hata kabla haijapigwa mnada. Hakujua ni kitu gani kilikuwa kimeendelea kwani alizungumza na Rais Bokasa na kumwambia kwamba angezungumza na benki hiyo ili nyumba yake isipigwe mnada na hata kiasi cha fedha alichotakiwa kutoa kama malipo ya mkopo ambao aliuchukua mumewe kisichukuliwe.

Aliendesha gari huku akilia, akaanza kuyafikiria maisha yake bila kuwa na fedha, watoto wake walimuumiza kichwa na hakujua ni kwa jinsi gani wangeweza kuishi bila kuwa na pesa hata kidogo.
Kama angefilisiwa kila kitu alichokuwa nacho inamaanisha kwamba angekwenda kuishi mitaani huku watoto wake wakiachishwa shule ile ya watoto wa matajiri na kwenda katika shule nyingine za kawaida kitu ambacho hakutaka kabisa kuona kikitokea.

Foleni zilimchelewesha, zilikuwa nyingi na alitumia muda mwingi kukaa katika foleni hizo. Mpaka anafika nyumbani kwake, alichukua saa moja, akafika mahali hapo, idadi kubwa ya watu iliyokuwa mahali hapo ilionyesha kabisa kwamba kulikuwa na kitu kinaendelea.

“Mbona mnaipiga mnada nyumba yangu? Kwa nini?” aliuliza Rosemary huku machozi yakiendelea kumtiririka mashavuni mwake, alikuwa akizungumza na kijana mmoja aliyevaa shati jeupe na tai nyekundu.

“Kamuulize bosi!”
“Yupo wapi?”
“Yule pale,” alisema kijana huyo huku akimnyooshea mwanaume aliyesimama pembeni kabisa huku akiwa na makaratasi mikononi mwake.

Akamfuata mwanaume huyo na kumuuliza swali lilelile, akamwambia wazi kwamba alishindwa kulipa fedha walizokuwa wakidaiwa na ndiyo maana nyumba ilikuwa ikipigwa mnada na hata pesa zilizokuwa kwenye akaunti ya mumewe, zilizuiliwa.

“Ila niliongea na rais,” alisema Rosemary.
“Kwani sisi tulimkopa rais? Hoja yako haina mashiko mama!” alisema mwanaume huyo, kwa kumwangalia tu, uso wake ulitosha kuonyesha ni kwa jinsi gani alikuwa na chuki kali dhidi ya Rosemary.

Rosemary hakutaka kukubali, hapohapo akachukua simu yake kwa lengo la kumpigia rais lakini sipo ilipopokelea, akaambiwa kwamba rais alikuwa safarini kuelekea nchini Ujerumani.
 
SEHEMU YA 85

Moyo wake ulimuuma, ulimchoma kupita kawaida. Akashindwa kujizuia, akakaa chini na kuendelea kulia kama kawaida. Kila mtu aliyemwangalia alimuonea huruma, alionekana kuwa mtu aliyekuwa akipitia matatizo makubwa mno, kwa jinsi mume wake alivyokuwa kipenzi cha watu, kwa jinsi alivyokuwa akipendwa kila siku, hakustahili kuwa katika hali aliyokuwa nayo kipindi hicho.

Rosemary akakumbuka kwamba alikuwa na hati ya nyumba, haraka sana akasimama na kuelekea ndani, alipofika, akafungua kidroo cha kitanda kwa ajili ya kuangalia hati ya nyumba, akaikuta lakini alichokishangaa, haikuwa hati ya nyumba orijino, ilikuwa ni nyingine kabisa ambayo hata sahihi zilizokuwa zimeandikwa, hazikuwa zake na za mumewe.

“Haiwezekanai!”
Akatoka chumbani huku akiwa amechanganyikiwa, akaelekea nje na kumfuata mwanaume yule huku akiwa ameshika ile hati ya nyumba ambayo ilikuwa feki. Alimwambia mwanaume huyo kwamba kulikuwa na mchezo umechezwa, kulikuwa na mtu aliingia chumbani kwake na kuchukua hati orijino na kumuachia feki.

“Mama! Ulishaambiwa kabla kwamba mumeo alichukua mkopo benki, unadhani angepewa bila kuwa na hati ya nyumba ambayo aliiweka kama bondi?’ aliuliza mwanaume huyo huku akimwangalia Rosemary.

“Lakini ilikuwepo mpaka jana nimeangalia, ilikuwepo,” alisema Rosemary.
“Utakuwa umechanganyikiwa mama! Nenda kwanza kapumzike tufanye yetu,” alisema mwanaume huyo, akageuka upande wa pili na kuendelea na kazi yake.

Rosemary akashindwa kuzuiia, siku hiyo nyumba yake ikapigwa mnada. Yalikuwa ni maumivu makali moyoni mwake, hakuamini kama angeweza kupoteza nyumba hiyo, na mbaya zaidi hata kwenye akaunti ya mumewe, fedha zote zilizokuwepo humo, zikachukuliwa kama kukamilisha malipo ya fedha aliyokuwa akidaiwa mumewe.

*** Miongoni mwa matajiri waliojitolea kukisaidia Chama cha Tanzania National Party alikuwa bilionea Adam Matiku. Huyu alikuwa miongoni mwa mabilionea wakubwa nchini Tanzania. Alimiliki kiasi kikubwa cha fedha, alikuwa na kampuni nyingi za usafirishaji, migodi ya dhahabu iliyokuwa Shinyanga na Mererani mkoani Arusha.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom