Dunia haina usawa

Dunia haina usawa

SEHEMU YA 81

Alikuwa na mawazo tele, ubongo wake ulikuwa ukifikiria kupita kawaida. Alipewa muda wa mwezi mmoja kukamilisha deni alilokuwa akidaiwa, hakujua ni mahali gani ambapo angepata kiasi kikubwa namna hiyo na kukilipa.

Alijaribu kuwasiliana na ndugu zake wengine, wote walipogundua tatizo alilokuwa nalo, hata simu hawakuwa wakipokea. Hakuchoka, aliendelea kuwatafuta lakini majibu yalikuwa yaleyale.

Wakati zikiwa zimebaki siku kumi, akajaribu kumpigia simu Edward kwa ajili ya kumuomba msaada wa kisheria zaidi lakini kitu cha ajabu kabisa, mwanaume huyo hakuwa anapokea simu zake na hata alipokuwa akimtafuta ofisini kwake, mwanaume huyo alijifanya kuwa bize na kutokuwa na muda wa kuzungumza na mtu yeyote yule.

Hilo lilimuuma mno moyoni mwake. Edward, mwanaume ambaye kila siku alimwambia kwamba angepigana naye kwa moyo mmoja leo hii hakutaka kupokea simu zake na mbaya zaidi hata alipokwenda kumuona ofisini kwake, hakutaka kabisa kuonana naye.
Hakujua cha kufanya, akarudi nyumbani kwake na kutulia sebuleni. Kila alipokuwa akiwaona watoto wake, mawazo yake yalikuwa ni juu ya maisha ambayo wangeishi baada ya nyumba hiyo kupigwa mnada.

Alikitegemea kiasi cha shilingi milioni mia mbili kilichokuwa kwenye akaunti yake, akahisi kwamba hicho kingemsaidia kuyaendeleza maisha yake, angenunua nyumba ya kawaida kuendelea na maisha yake na watoto wake.
“Mama nimerudi tena!” alisema mwanaume mmoja aliyemfuata nyumbani kwake.

“Eeh! Jamani! Kuna nini tena?”
“Nimekuletea barua!”
“Nyingine?” aliuliza huku akionekana kushangaa.
“Ndiyo! Hii hapa!”

Mwanaume yule akampa barua hiyo. Rosemary alibaki akitetemeka, hakujua ni kitu gani ambacho angekutana nacho katika barua ile. Alipoifungua, maneno ya kwanza aliyokutana nayo ni kuhusu kufungwa kwa akaunti yake ya benki ya mume wake.

“Nini? Wanafunga akaunti?” alijiuliza huku akishtuka kupita kawaida.
Akasoma maelezo kwa kirefu. Benki hiyo iliyokuwa ikimdai mumewe ilieleza kwamba kwa kiasi cha shilingi milioni mia mbili kilichokuwa benki kilitakiwa kuchukuliwa chote na kisha nyumba hiyo kuuzwa kwa bei ya kawaida kwa ajili ya kupata hata nusu ya fedha walizokuwa wakimdai.
 
SEHEMU YA 82

“Mungu wangu! Kwa nini wananifanyia hivi? Nimewakosa nini?” aliuliza Rosemary na kuanza kulia.
Hakupata faraja, siku hiyo ndiyo iliyomuumiza mno, maisha yake yalikuwa ni sawa na karatasi nyeupe ambayo haikuandikwa kitu chochote kile, hakujua angeanzia wapi, hakujua angefanya nini ili kupata haki zake za msingi.

Alijua kwamba kulikuwa na mchezo mchafu uliokuwa ukichezwa na serikali, alijua kabisa kwamba serikali hiyo iliamua kufanya hayo yote kwa kuwa tu mumewe alionyesha upinzani mkubwa hivyo walifanya hayo yote kama kuipoza mioyo yao kwa majeraha makubwa waliyokuwa wameyapata.

Akawashirikisha walimu wenzake ambao aliamini kwamba ndiyo walikuwa watu pekee ambao wangeweza kumfariji. Walimu hao wakamshauri kwamba lingekuwa jambo jema kama angewasiliana na Rais Bokasa na kumwambia kilichokuwa kikiendelea.
“Mmh! Itawezekana kweli?” aliuliza Rosemary.

“Jaribu! Tunaamini kwamba anaweza kukusaidia,” alisema mwalimu mwenzake.
“Lakini nahisi serikali inahusika, sasa kama inahusika, itakuwaje rais kunisaidia?” aliuliza.
“Hebu kwanza wasiliana naye. Usitake kuingiza hofu na wakati bado hujawasiliana naye. Akikataa, basi jua kwamba umeshindwa,” alisema mwalimu mwingine.

Hakutaka kusubiri, siku zilikuwa zimekwenda sana hivyo akatafuta mawasiliano ya Rais Bokasa na kumpigia. Alipoisikia sauti ya mwanaume huyo tu, Rosemary akaanza kulia, moyo wake ulimchoma kupita kawaida, alijua kwamba mtu huyo ndiye alikuwa wa mwisho kumsaidia na kusingekuwa na mtu yeyote ambaye angeweza kumsaidia.
 
SEHEMU YA 83

Akamwambia Rais Bokasa kila kitu kilichokuwa kimetokea. Rais huyo alihuzunika mno, hakuamini kama benki hiyo ingeweza kumfanyia mwanamke huyo mambo ya kijinga kama hayo. Akamwambia kwamba angemsaidia kwa hali na mali.

“Nitakusaidia, nitazungumza nao, ila jua utashinda tu,” alisema Rais Bokasa maneno yaliyomfanya Rosemary kushukuru sana.
Moyo wake ukarudisha tumaini, akafarijika na kuwaambia walimu wenzake kwamba rais huyo aliahidi kumsaidia na hivyo alitakiwa kusubiri. Siku ya kuondolewa ndani ya nyumba hiyo, hakuondolewa kitu kilichompa uhakika kwamba tayari rais huyo alizungumza nao na kumalizana.

Siku ziliendelea kukatika, baada ya wiki mbili kupita baada ya siku ile ya kuondolewa ndani ya nyumba, akashangaa akipigiwa simu kwa namba ngeni wakati akiwa shuleni na kuambiwa aende nyumbani kwake kwani kuna watu walifika na kuanza kuipiga mnada nyumba hiyo.

“Wanaipiga mnada? Kivipi? Mimi ndiye nina hati ya nyumba!” alisema Rosemary huku akionekana kuchanganyikiwa.
“Sidhani kama unayo! Wahi kuja hapa, vinginevyo utakuta mtu kaipandia dau,” ilisikika sauti ya mwanaume aliyempigia simu. Rosemary hakutaka kufanya kitu chochote, akaingia ndani ya gari lake, akaliwasha na kuondoka shuleni hapo kwa mwendo wa kasi, hata kuaga akasahau, wanafunzi na walimu wote wakabaki wakimshangaa.

Je, nini kiliendelea?
Tukutane tena kesho....
 
Dada angu umeanza jamani yaan kwa ninavyokujua utakuwa umesoma kwa rosemary tu ni alikuwa mke wa marehemu mgombea uraisi wa upinzani sasa bada ya mumewe kufa ghafla tu imekuja bank ghafla inataka kumfirisi kuwa mumewe alikopa mill 500
Khaaaa
Million zote hizo akapeleka wapi
 
Dada angu umeanza jamani yaan kwa ninavyokujua utakuwa umesoma kwa rosemary tu ni alikuwa mke wa marehemu mgombea uraisi wa upinzani sasa bada ya mumewe kufa ghafla tu imekuja bank ghafla inataka kumfirisi kuwa mumewe alikopa mill 500
Khaaaa
Million zote hizo akapeleka wapi
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom