SEHEMU YA 71
Hiyo ilitosha kabisa kuandika habari hiyo iliyosisimua. Kesho, magazeti yakawa na taarifa ya kifo cha Balozi Mapoto. Watu hawakuamini, kitu cha kwanza kabisa walichohisi ni kwamba serikali ilihusika katika kifo chake lakini baada ya kuambiwa kilichotokea, jinsi kifo kilivyokuwa, wakagundua kwamba ilikuwa ni ajali tu, kitu ambacho hakukuwa na mtu wa kupewa lawama.
“Ni ajali! Ila nasikia ilikuwa mbaya sana,” alisema mwanaume mmoja.
“Wacha weee….”
Katika kipindi hicho cha mwaka 2002, mitandao ya kijamii iliyokuwepo kama Yahoo na Bearshare haikuwa na nguvu hivyo ilikuwa ni vigumu kupata taarifa kutoka katika mitandao ya kijamii, kila mmoja alitegemea magazeti na televisheni.
Tanzania ikanyamaza, ikaomboleza, kifo cha Balozi Mapoto kilimsisimua kila mmoja. Vilio vilitawala kila kona, hakukuwa na mtu aliyekuwa na furaha kwani mtu ambaye alikuwa amekufa alikuwa mtu wa watu, tumaini jipya kwa Watanzania, mtu ambaye alikuwa mabadiliko sahihi kwa Watanzania wote.
Rosemary hakutaka kubaki nchini Tanzania, akapanga kuondoka na kuelekea nchini Marekani, alitaka kwenda kuuona mwili wa mume wake hospitalini lakini hata kabla hajafanya hivyo, akapigiwa simu na rais na kuanza kuzungumza naye.
Kwanza akampa pole kwa kile kilichotokea, akamfariji katika kipindi kigumu alichokuwa akipitia lakini pia alimwambia kwamba serikali yake ingefanya kila liwezekanalo kuupeleka mwili wa Balozi Mapoto nchini Tanzania.
Hilo ndilo lililofanyika, siku mbili baadaye, mwili wa mwanaume huyo ukaingia nchini Tanzania.
Uwanja wa ndege watu walijaza kupita kawaida, wengi hawakuamini kama kweli mwanaume huyo alikufa nchini Marekani, walitaka kujionea wenyewe, walitaka kuona kama kweli aliyekufa alikuwa Balozi Mapoto waliyekuwa wakimpenda au mtu mwingine.
“Inauma sana, ni bora angekufa ndugu yangu yeyote yule kuliko Mapoto,” alisema mwanaume mmoja, alionekana kuguswa sana na msiba wa Mapoto.