Bada ya kufufuka Yuko wapi?
Habari za Yesu kufa na kufufuka zimekaa kimichongo Sana.
Nitkwambia kwanini? Habari za Yesu kuzaliwa, kufariki na kufufuka zinapatikana kwenye Biblia Pekee kana kwamba Yesu alizaliwa katika Dubai yake.
Peke yake isiyokuwa na watu wengine. Biblia ambayo nayo inatiliwa shaka kuhusu taarifa zake.
Yesu anazaliwa anakuta duniani kuna watu, watu walioishi kabla yake habari zao zimeandikwa na kuelezewa na Watu waliokuwepo, waandishi mbali mbali na vyanzo zaidi ya kimoja.
Leo hata picha ya Yesu au hata sanamu lake Tu hakuna, hakuna kumbukumbu alizaliwa lini na siku gani mwaka gani, kumejaa mabishano na Tarehe za kubuni, je Yesu alizawali hakukuta watu?
Tuje sasa wakati anafufuka watu wachache Sana tena wale wale 12 wafusi wake tu ndio walimwona, dunia nzima hakuna mtu Mwingine aliyeshuhudia, Nani atawaamini?
Tukio la kufa na kufufuka ni tukio kubwa sana, lingeandikwa na kusimuliwa kwa ufasaha kwa Vizazi vyoote.
Farida zake ni za kutilia Mashaka sana
Ndugu yangu, kihistoria na kitaaluma, hoja zako hazina mashiko. Haya twende hatua kwa hatua nikujibu kwa kutumia vyanzo vya kihistoria visivyo vya kidini (Secular Historical Sources):
1. Umedai kwamba "Habari za Yesu zinapatikana kwenye Biblia pekee" (HUU NI UONGO MBICHI KABISA WA KIHISTORIA).
My friend, Yesu hakuishi "Dubai yake peke yake." Waandishi na wanahistoria wakubwa wa Kirumi na Kiyahudi wa karne ya kwanza na ya pili, non-Christians, walikuwa maadui wa Ukristo; hata hivyo waliandika kuhusu kuwepo kwa Yesu, kifo chake, na harakati za wafuasi wake baada ya kufa. Vyanzo hivyo ni pamoja na:
- Flavius Josephus (Mwanahistoria wa Kiyahudi, 37–100 BK): Katika kitabu chake Antiquities of the Jews, anamuelezea Yesu kuwa ni mtu mwenye hekima, aliyetenda mambo ya ajabu, akasulubiwa chini ya Pilato, na kwamba wafuasi wake walisema alifufuka.
- Cornelius Tacitus (Mwanahistoria wa Kirumi, 56–120 BK): Huyu ni mmoja wa wanahistoria makini zaidi wa Kirumi. Katika kitabu chake Annals, anaeleza wazi kwamba jina "Wakristo" linatokana na mtu aliyeitwa Christus (Kristo), ambaye aliuawa kwa adhabu ya kifo wakati wa utawala wa Tiberio, chini ya Liwali Pontio Pilato.
- Pliny the Younger na Suetonius: Hao ni waandishi wengine wa Kirumi walioandika barua na kumbukumbu kuhusu jinsi Wakristo walivyokuwa wakimwabudu Kristo kuwa ni Mungu katika karne ya kwanza.
Hakuna mwanahistoria yeyote makini duniani leo (awe wa dini yoyote au asiye na dini) anayebisha kuwa Yesu hakuwepo duniani. Ushahidi wa kuwepo kwake ni mkubwa kuliko hata wa wanafalsafa wengi wa Kigiriki tuliowasoma shuleni. Tuko pamoja? Haya tuendelee..
2. Umeuliza "Mbona hakuna picha au sanamu yake, na tarehe zake zina mabishano?" Kwanza hii inaonyesha hujui hata historia ya camera. Hebu google ujue camera ya kwanza black and white ilitengenezwa lini ndio utajua kwanini hakuna picha ya Yesu. Haya, tukija kwenye sanamu: Kumbuka Yesu alikuwa Myahudi anayeishi katika karne ya kwanza. Katika utamaduni na sheria za Kiyahudi (Amri 10 za Musa), ilikuwa ni dhambi kubwa na marufuku kuchora picha au kuchonga sanamu ya mtu yeyote wa kidini (Sanamu za kuchonga zilionekana kama ushirikina/idolatry). Ndio maana Wayahudi wa kipindi kile hawakuwa na utamaduni wa picha.
Kuhusu Tarehe: Kalenda tunayotumia leo (Gregorian/Julian calendar) ilitengenezwa miaka mingi baada ya Yesu kuondoka, ikimtumia Yesu kama reference point ya muda, ndio sababu tunasema Kabla ya Kristo - KK, na Baada ya Kristo - BK. Kutokujua tarehe halisi haifanyi tukio lisiwepo. Kwani wewe unajua tarehe halisi na saa aliyozaliwa chifu wako wa kale au babu wa babu yako? Je, kutokujua kwako hizo data inamaanisha hawakuwepo?
3. Umesema "Watu wachache tu ndio waliomwona Yesu baada ya kufufuka"
Hiyo kauli inadhihirisha una taarifa pungufu. Kumbukumbu za kale zinaonyesha wazi Yesu baada ya kufufuka hakuonekana kwa siri au kwa mitume peke yao. Alionekana kwanza kwa wanawake (akina Maria Magdalene). Katika utamaduni wa kale wa Kiyahudi na Kirumi, ushahidi wa mwanamke ulikuwa hauna thamani kisheria. Kama tukio hilo la kufufuka kwa Yesu lingekuwa ni hadithi ya mchongo waandishi wasingeweka wanawake kuwa mashahidi wa kwanza, kwa sababu ingeharibu kesi yao. Wangewaweka viongozi wa kiume. Hii inadhihirisha waliuona ukweli.
4. Hebu jiulize, kama ulikuwa mchongo, mbona mitume walikufa kwa ajili yake? Hii ndio hoja kubwa zaidi ya kihistoria. Wanafunzi wa Yesu waliteswa, waliuawa kikatili (kuchomwa moto, kusulubiwa miguu juu, kukatwa vichwa) kwa sababu tu ya msimamo wao kwamba "Tumemwona Yesu amefufuka."
Mtu anaweza kufa kwa ajili ya kitu anachoamini kuwa ni kweli (hata kama ni uongo). Lakini hakuna mtu anayekubali kufa kwa mateso makali kwa ajili ya kitu anachojua kabisa yeye mwenyewe amekitunga tu kwa hila. Kama mitume wangekuwa wamedanganya, mmoja wao angesaliti mchongo huo wakati walipokuwa wanapigwa mijeledi na kusema: "Jamani tusiuane, tuliuficha tu ule mwili!" Lakini wote walikufa wakishuhudia ufufuo wa Yesu Kristo.
5. Umeuliza "Baada ya kufufuka yuko wapi?"
Baada ya kufufuka, Yesu alikaa siku 40 akithibitisha ufufuo wake, kisha alipaa mbinguni (Matendo 1:9). Yuko mbinguni anatuandalia makao na aliahidi atarudi, kama nilivyoeleza katika uzi wa dalili za kurudi kwa Yesu.
Ufufuo wa Yesu sio tukio la kutilia shaka, ni tukio lililobadili kalenda ya dunia, likageuza utawala wa Kirumi uliokuwa ukiwatesa Wakristo na kuwa himaya ya Kikristo, na hadi leo tukio hilo limesimama kama msingi mkuu wa kihistoria.
Bwana Yesu asifiwe. Sema:
"Ameen"
Tumsifu Yesu Kristo Sema
"Milele Amina"