Hakuna kitu kibaya sana kama ujengaji hoja wenye makosa (fallacious argumentation). Ukishakosea kwenye msingi wa hoja (proposition) ni lazima utajikuta unakosea kwenye hitimisho (conclusion). Ritz ameandika kitu ambacho kwa mtu asiyejua makosa ya mantiki (illogical arguments) ni rahisi kuamini kuwa ndugu yetu Ritz ameonesha kuwa Dr. Slaa ana njama ya kulipa kodi. Unapojenga hoja ni lazima hoja yako ikubaliane na mantiki; na ile inayotoa madai (kama hii) ni lazima iwe ne msingi wa ushahidi (credibility). Hebu tuangalie mtiririko huu wahoja (flow of argument)
Kwanza:
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na maendeleo Chadema, Dr. Slaa anapenda sana kujinasibisha kwamba yeye ni mzalendo wa kupindukia, anayechukia vitendo vya ufisadi na anayeionea huruma nchi yetu.
Kimsingi, hoja nzima ya Ritz imejibanza hapa kwamba kwa vile A - Dr. Salaa anajinasibisha kwamba ni mzalendo..... na anaionea huruma nchi basi - B.
Pili (B):
Taarifa za uhakika kabisa zinathibitisha kwamba mwishoni wa mwezi Juni, mwaka 2013 Dr.Slaa na Mchumba wake walitembelewa na kundi la Wapani wapatao 20 nyumbani kwao Mbweni, Kinondoni ambapo wote kwa pamoja walikula cha jioni.
Dhumuni la ugeni huo wa Wajapani, ilikuwa ni kuthibitisha kama kweli Chadema kina mpango wa kujenga hospitali kubwa ya kisasa katika eneo la Mlalakuwa Dar es Salaam, Wajapani hao ndiyo walipangwa au kuteuliwa kujenga hospitali hiyo,
Sasa, hili hapa linaweza kuvutia hisia tu kuwa watu wanajua hadi wageni wa Dr. Slaa nyumbani kwake lakini halihusiani kabisa na hoja iliyopo; kwani wageni hawa - kama kweli walikuwepo - hawakuhitaji kwenda kula chakula cha jioni ili kujadili jambo hili. Kama watu wamefika hadi nchini ni wazi watakuwa wameshafanya mazungumzo ya kina kuhusiana na mradi na mtu kuwakaribisha wageni nyumbani basi inaweza kuwa ni kuwakirimu wageni. Hivi ni watu wangapi wanakaribisha wageni wao wa kibiashara nyumbani wakala chakula - kwa wanaojua haya mambo hakuna mahali ambapo deals zinaweza kuingiwa nzuri kama katika informal settings. Tukubaliane tu kwa muda huu kuwa kweli wageni walikuja na kula chakula cha jioni na kufanya mazungumzo ya kibiashara hapo - kulikuwa na kosa? NONE.
Wengine wanaita kitu kama hicho ni kama nafasi ya ku 'seal the deal'!
Tatu:
wameakikishiwa pamoja na mambo mengine ya kimaslahi yao makampuni yao mengine, kwamba msimamizi wa hospitali hiyo ndiyo atakayekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2015, kwa maana ya Dr. Slaa.
Hii nayo ni hoja ndani ya hoja lakini ni hoja yenye makosa (fallacious argument) ndani ya hoja yenye makosa! Hivi kweli Ritz na watu waliokubali hoja yake hii wanaamini kabisa mtu anaweza kwenda "kuwahakikishia" watu wenye akili na wafanyabiashara kuwa matokeo ya uchaguzi ya 2015 yatakuwa ya kuipendelea CHADEMA? Watu kama Wajapan ambao ni wasomi, wana nchi ya kidemokrasia wataweza kuuliza swali moja tu - mnajuaje kuwa Dr. Slaa atashinda urais? Well, hakuna anayejua na hakuna guarantee inayoweza kutolewa kumfanya mtu mwenye akili timamu aamue kuingiza mabilioni ya hela kwa ahadi ya matokeo ya uchaguzi ambao haujapigwa na bado kuna muda mrefu.
Jambo hili hata hivyo ni rahisi kufanywa na watu walio madarakani tu! Mtu asiye madarakani atakuwa na wazimu kutoa ahadi ya matokeo ya uchaguzi. Rais Kikwete alijua atagombea 2005 na atashinda; mifumo yote ilikuwa imeandaliwa ili ashinde na hivyo aliingia ahadi na watu mbalimbali akiwemo Brig. Gen Al Adawi na wengine kutoka Oman ili wamchangie fedha wakijua kuwa akiingia madarakani (siyo kama akiingia) basi na wao watakumbukwa na kweli ikawa hivyo! Sasa hivi kuna mtu mwingine ndani ya CCM ambaye anaamini kabisa kuwa mifumo imemuandalia ikulu na tayari anatoa ahadi na anapata ufadhili wa mabilioni kutoka kwa 'marafiki' kwani wanajua na yeye akiingia madarakani atawakumbuka. Chama chake kimemlinda na kinamuandalia hivyo! Hawa wanaweza lakini chama cha upinzani ambacho hakina hata majority Bungeni kitoe ahadi ya namna hiyo kwa wafanyabiashara wa kimataifa?
Nne -
Mipango yote ya kujenga hospitali hiyo, inaratibiwa na Askofu mmoja anayemiliki Kanisa lake maeneo ya Kawe, Dar es Salaam, Askofu huyo amekuwa akifanya safari za Japani akiwa ameandamana na mchumba wa Dr. Slaa, Josephine, mpango unafanyanyika vifaa vyote vitakavyoingizwa kutoka Japani vipitie mikononi mwa Kanisa ili tu visitozwe kodi na serikali.
Kwanza, hakuna tatizo lolote la ushirikiano wa taasisi au watu binafsi katika kufanya biashara au mipango fulani ya kibiashara. Ni sehemu ya kawaida ya biashara. Unless, kama Ritz anataka kusema kuwa Askofu huyo anafanya mambo hayo kwa siri na kanisa lake halijui na ama yanafanywa kwa siri na kina Slaa. Lakini hata kama ni kwa siri bado hoja inaweza kujengwa kuwa ni katika kulinda maslahi yao ya biashara (trade secrets). Lakini tukubali tu kuwa ni kweli wanafanya hivyo ili wasibebe mzigo mkubwa wa kodi swali linakuja je ni kosa? Je ni kosa kwa taasisi ya kibiashara au yoyote ile ambayo inaona kodi inaweza kuwa kubwa sana kutafuta unafuu wa kodi?
Well, jibu ni kuwa hakuna tatizo. Waliotengeneza mfumo wa kodi nchini ni serikali ya chama cha mapinduzi; unafuu wa kodi na mianya ya kodi (tax loopholes) zimetengenezwa na sheria zilizotungwa na wana CCM na kupitishwa na Bunge lao na kutiwa sahihi na RAis (ambaye ni mwenyekiti wa CCM). Kama hili ni kweli ni wazi kuwa hawakuwa wanamfikiria Slaa walikuwa wanawafikiria watu wengine; makampuni makubwa ya simu, ya madini ya nishati n.k ambayo yanatumia mianya mingi ya kodi ambayo imeshawahi kuwekwa bayana na watu kama kina Zitto.
Sasa kama kweli CCM wanaona Dr. Slaa kutumia sheria ambazo wao wamekuwa wakizitumia kwa muda mrefu ni makosa kwake basi wazibe mianya ya kodi; wabadilishe sheria ili ziwabane watu wote. Kama kweli wanataka watu walipe kodi na wasitafute unafuu wa kodi (itakuwa nchi pekee ambayo itaondoa kabisa unafuu wa kodi) basi wafute mianya hii au waizibe kabisa. Hapo ndio tutajua kweli wanataka uzalendo.
Lakini labda swali lililojifisha kwenye hoja hii ni hili:
Kama Dr. Slaa na washirika wanataka kujenga hospitali ambayo itahudumia wananchi wa Tanzania na kama wamegundua kuwa ili kupunguza gharama za ujenzi na uendeshaji wa hospitali hiyo ni bora kutumia sheria ya kodi kutafuta unafuu (kushirikiana na Kanisa) ili wananchi nao wapate unafuu au gharama za hospitali zisiwe za juu mno kwa wananchi je kama huu siyo uzalendo uzalendo ni nini basi? Ni kuwabambikizia mzigo wa kodi na gharama za juu wananchi bila kuwapa ahueni yoyote?
Binafsi ningependa kusikia watu wengine nao wanafanya hivi hivi ili kusogeza huduma za kijamii nyingi zaidi kwa wananchi na katika unafuu unaowezekana. Nilitarajia Ritz angetoa pongezi kwa Dr. Slaa na wageni wake kwa kubuni njia nzuri zaidi ya kupunguza gharama za ujenzi wa hospitali!
Hata mimi nilipochapisha kitabu changu cha kwanza hapo nyumbani nilijaribu kutafuta mianya ya kodi (VAT). Kulipa asilimia karibu 18 kwa kitabu niliona ni mzigo mkubwa kwani ungenilazimisha kuweka bei ya kitabu juu mno. Matokeo yake kodi ilipobadilishwa na mimi nikajaribu kutafuta ahueni au hata kuchapisha vitabu vyangu nje! Na hata kama ningetaka kujenga kadispensari hapo Nyamaswa basi ningejiuliza je kwenye kodi naweza vipi kupata unafuu?