Dora Block: Mateka wa Israel Aliyesahaulika Entebbe

Abtali mwerevu

JF-Expert Member
May 5, 2013
637
432
Jina ni Dora Bloch na siyo Dora Block kama ilivyoandikwa katika kichwa cha habari hapo juu.

Na: Mwalimu Makoba

Mapema tarehe 28 mwezi Juni mwaka 1976, ndege ya Air France ilitekwa na kikundi cha Popular Front for the Liberation of Palestine na kuilazimisha ndege hiyo itue katika uwanja wa Entebbe huko Uganda. Ndege hii-Air France 139, ilianza safari yake Tel Aviv na ilitekwa mapema kabisa mara baada ya kupaa kutoka Anthens; ilikuwa na abiria mia tatu, wengi wao wakiwa Waisrael.

Nduli Idi Amin Dada aliwapokea watekaji na baada ya mazungumzo ya hapa na pale alimpa maagizo waziri wa afya, “Kyemba, Wapalestina wameteka ndege kutoka Israel na wametua Entebbe. Peleka madaktari na manesi ili kutoa msaada wa matibabu endapo utahitajika.” Jambo hili lilikuwa nyeti, Amin alipendekeza muuguzi wa Kinubi na aliagiza atafutwe daktari anayekubalika na Wapalestina. Kyemba aliwasiliana na Daktari Mmisiri, Dkt. Ayad na kumtaka aelekee Entebbe kwa kazi ya dharura.

Katika uwanja wa ndege, baada ya kupita msururu mrefu wa wanajeshi wa Uganda, Waziri wa Afya alikutana na Maofisa wa Palestinian Liberation Organization kutoka ofisi za Kampala. Walimpeleka mpaka katika jengo mojawapo katika uwanja huo wa ndege. Mara kadhaa jengo hili limekuwa likitumika kuhifadhi chai ikisubiri kusafirishwa kwenda Stanstead, Uingereza. Eneo lilikuwa chafu na madirisha yake yalivunjika vioo. mfumo wa maji haukufanya kazi na vyoo havikupatikana. Mateka walifungwa mahali walipokaa, wengine walilalia nguo zao na baadhi walionekana wakinong’ona taratibu. Walikuwa mahali hapo kwa zaidi ya saa kumi na mbili na walipewa chakula cha mchana, wali na nyama, vyakula hivi vilitolewa Entebbe Airport Hotel. Watekaji waliovalia nguo za kiraia, walisheheni bastola, mabomu ya kurusha kwa mkono aina ya ‘grenades’ na walisimama ndani ya jengo.

Ofisa wa Kipalestina alimtambulisha Waziri wa Afya kwa kiongozi wa watekaji, mwanamke jasiri, ambaye baadae alikuja kutambulika kuwa gaidi kutoka Ujerumani Gabriele Kroche-Tiedemann. Alikuwa mwanamke mwenye mvuto, alivalia sketi ya bluu na jaketi, bastola ilining’inia mapajani kwake. Wapalestina walimtambulisha Waziri wa Afya aliyesimama mbele yao naye alifurahia utambulisho huo. Alimanusura ajitambulishe jina lake, lakini alibadili maamuzi na kusema kwa ufupi, “Mimi ni Bi. Mtekaji.” Waziri akajibu, “Vyema, nafurahi kukutana nawe, Bi. Mtekaji.” Bi. Mtekaji alimtambulisha Waziri kwa mateka kwamba alikuwa mahari hapo kutatua changamoto zao. Alizungumza kwa kiingereza, mwanamke mmoja mateka akitumia kipaza sauti aina ya ‘megaphone’ akafasiri kwa lugha ya Kiebrania. Alisikika mtu mmoja akizungumza kwa sauti ya chini, bila shaka alifasiri kwenda lugha ya Kifaransa.

Baadae Waziri wa Afya alielekeza wahudumu wa afya kuendelea na kazi yao, kisha akazungumza na watekaji kwa muda wa dakika chache, akaondoka. Baadae alipewa taarifa kuwa, mateka walikuwa vizuri, walihitaji dawa za kutibu malaria na kutuliza maumivu.

Siku iliyofuata, Jumanne ya Tarehe 29 mwezi Juni, matatizo kadhaa yakaibuka. Wanawake wazee watatu raia wa Ufaransa walikasirishwa na hali ya wao kuwa mateka na wakasisitiza waruhusiwe kuondoka. Mmoja kati yao, alikojoa hadharani, pembezoni kidogo mwa walipokaa mateka na alionekana angeendelea kufanya vitimbwi vipya mpaka aachiwe. Daktari alishauri mabibi hao wapelekwe hospitali. Mwisho mabibi hao watatu waliruhusiwa kwenda katika hospitali ya Entebbe.

Mateka mwingine, naye Mfaransa, aliruhusiwa kwenda Hospitali ya Mulago. Alikuwa Mwanamke mzee ambaye alitiliwa shaka kuwa na tatizo la moyo. Mara baada ya kufanyiwa vipimo Mzee huyo hakukutwa na tatizo lolote. Hata hivyo Idi Amini akalikuza jambo hili. Akatangaza kwamba, mwanamke Mfaransa aliyeshindwa kupata tiba ya ugonjwa wake wa moyo katika hospitali zote duniani, amepata matibabu nchini Uganda na amepona!

Idi Amin aliagiza mara tu wazee wanapopatiwa matibabu warejeshwe katika jengo la uwanja wa ndege. Hata hivyo, wataalamu wakashauri kama mmojawapo angefariki ingeleta matatizo na pengine kuvuruga mipango. Amin alikubaliana na hoja. Haraka, wazee wanne walitolewa hospitali na kukabidhiwa katika ubalozi wa Ufaransa.

Ndani ya jengo, mateka kadhaa walilalamika kuhusu maumivu ya mgongo. Walikuwa na viti vya kukalia na sakafu ya kulalia pekee. Madaktari wakashauri wapewe magodoro na mashuka mazito.

Misheni yote ilikuwa ikiendeshwa na Idi Amin mwenyewe ambaye alifanya kazi kwa ukaribu na Wapalestina waliokuwa na ofisi zao Kampala. Amin alisikika akisema, “Sasa nimewapata watu hawa katika muda ninaotaka. Nimewakamata Waisrael muda huu.” alikuwa ametingwa na shughuli ya kuhakikisha mahitaji ya Wapalestina yanatimizwa ambayo yalitangazwa siku ya Jumanne: ili kuwaachilia mateka, wafungwa wa Kipalestina hamsini na tatu, waliokuwa wakishikiliwa katika magereza mbalimbali duniani waachiliwe huru. sharti hili lilitakiwa kutekelezwa ndani ya siku mbili, siku ya Alhamisi, tarehe moja mwezi Julai, vinginevyo mateka wote wangeuawa.

Inaendelea Kesho...

Soma: Jinsi ya Kuandika CV
 
Idd kanifurahisha hapo " hospitali zote duniani zimeshindwa kumtibu " ila akaponea Uganda tena pale Mulagi hospital ya miaka ya 70 huko😂😂😂
 
2

Muda uliotolewa ulikuwa mgumu kwelikweli. Haukutosha kufanya mawasiliano katika sehemu zote zilizohusika achilia mbali kukubaliana na masharti yenyewe. Siku ya Alhamisi asubuhi, Amin alifika katika jengo la uwanja wa ndege akiwa na mavazi ya kivita na akaeleza mambo yaliyoendelea kwa mateka. Muda wa mwisho ukaongezwa mpaka Jumapili, Julai 4, saa saba usiku. Ratiba hii ilimfaa Amin. Ingempa muda wa kwenda Mauritius ambako mkutano wa Umoja wa Afrika ulikuwa ukifanyika. Endapo asingeenda, ingeonekana kwamba anaogopa kutoka nchini kwake. Pia angetumia nafasi hii kutamba mbele ya viongozi wenzake kwamba anawashikilia mateka Waisrael. Angeweza kurejea siku ya Jumamosi. Ni katika nyongeza hii ya muda ndiyo iliyowapatia Waisrael nafasi ya kupanga namna ya kuwaokoa mateka.

Amini alisafiri siku ya Alhamisi mchana kuelekea Mauritius. Amin hakuwa na lengo la kuwaua mateka, kwake walikuwa na thamani kubwa wakiwa hai.

Kadri muda ulivyozidi kwenda, ripoti zilisema mateka walizidi kuugua, hata hivyo, wengi walidanganya kuumwa ili waweze kuachiliwa. Amin aliagiza kuongeza idadi ya wahudumu wa afya. Alipoambiwa Dr. Ayad kwamba kungeletwa ongezeko la wahudumu wa afya, alishauri jambo hilo halikuwa la lazima. Mbali na hayo, usafi haukuridhisha, mateka wengi waliumwa tumbo na kichwa, pamoja na hayo, Dr. Ayad alishauri hakuna haja ya kuongeza nguvu ya ziada.

Jioni ya Ijumaa, Julai 2, mmojawapo kati ya mateka, Bibi Mzee, Dora Bloch aliyekuwa na uraia pacha wa Israel na Uingereza, alipaliwa na kipande cha nyama hali iliyosababisha apumue kwa shida, haraka akawahishwa hospitali ya Mulago. Baadae ilielezwa kwamba, kipande kile cha nyama kiliondolewa kwa urahisi na daktari mmoja wa kinywa na meno.

Waziri wa Afya alikwenda kumjulia hali bibi huyu saa tano asubuhi. Alilazwa katika wadi VIP (6B) ghorofa ya sita, pamoja na askari aliyesimama mlangoni.

Waziri alisalimia, “Habari, natumaini utapata nafuu punde.”

“Nipo vizuri,” alijibu, “lakini nina hofu kuhusu mwanangu.” (Mwanae alikuwa uwanja wa ndege.)

Waziri alijibu, “Usijali, kila kitu kitakuwa sawa.”

“Natumaini hivyo,” alijibu, “lakini ninaogopeshwa na mlinzi, ananichungulia muda wote dirishani.”

Waziri alikwenda moja kwa moja mpaka kwa mlinzi na kumtaka akae katika kiti na asisogee mara kwa mara dirishani.

“Hutakiwi kumchungulia mara kwa mara,” Waziri alisema, “pia, ni mzee hata kutembea vizuri hawezi.”

Waziri alirejea na kumweleza Bi. Bloch maelekezo aliyomwachia mlinzi. Bibi alishukuru na waziri akaondoka.

Idi Amin alirejea mapema jioni na aliwatembelea mateka 106 (mateka wengine waliachiwa na Wapalestina muda mfupi kabla hajafika). Alimpigia simu Waziri wa Afya saa nne usiku kufuatilia matibabu yaliyokuwa yakitolewa. Waziri alieleza jambo pekee la kutilia mkazo ni vyoo. Pia alitoa taarifa kuhusu Bi. Bloch, akaeleza kwa nini alilazwa Hospitali ya Mlago na akamaliza kwa kusema, Bibi huyo alikuwa mzima wa afya. Amin aliagiza kupanga mipango ya kumrejesha uwanja wa ndege kabla ya saa saba usiku, muda ambao ulitolewa kuwa wa mwisho kwa Waisrael kutimiza amri waliyopewa ili kuachiliwa kwa mateka. Waziri alijibu anafanyia kazi jambo hilo.

Saa sita na nusu usiku, simu ya Waziri wa Afya iliita. Ilitoka Kampala na ilipigwa na mmojawapo wa wasaidizi wa kike wa Idi Amin. Msichana alisema kuwa Idi Amin alimpigia simu kutoka Entebbe akimpasha habari kuwa palikuwa na mapigano katika uwanja wa ndege na hali haikuwa shwari. Uwanja wa ndege ulitekwa na Idi Amin hakufahamu ulitekwa na nani. Amin alieleza kwamba, alikuwa anajiokoa mwenyewe, na alimshauri msaidizi wake atafute namna ya kujiokoa. Alieleza angemtumia gari na akasisitiza aende mafichoni. Lakini mwanamke huyu hakufahamu mahali pa kwenda kujificha ndiyo sababu alimpigia simu Waziri wa Afya ili ampe msaada.

Amin alidhani shambulio lile lilikuwa jaribio la uasi lililosaidiwa na nchi jirani, Kenya au Tanzania. Hakuweza kuufahamu ukweli kwa sababu mapigano yalipoanza, Maofisa wa jeshi lake walitoweka. Muda wa shambulizi, saa tano na dakika arobaini na tano usiku, maofisa wengi waliokuwa uwanja wa ndege, walikuwa wakinywa pombe na kucheza mziki Lake Victoria Hotel karibu na ikulu. Makomandoo wa Israel walipotua, mirindimo ya risasi iliwatawanya maofisa wote ambao walielekea nyumbani kwao kujificha. Walieleza wanafamilia wao kuwa, endapo ingepigwa simu na mtu yeyote waeleze hawakuwa nyumbani. Wangefanya hivyo mpaka ambapo wangefahamu nani alishambulia. Hakuna ofisa aliyetaka kupambana katika upande usio sahihi.

Inaendelea Kesho...

Soma: Jinsi ya Kuandika CV
 
3

Idi Amin naye alikwenda mafichoni, katika nyumba ya dereva mmoja karibu na Ikulu. Alijaribu kuwasiliana na maofisa wa jeshi lake akiwa mafichoni bila mafanikio. Amin alikuwa sahihi kujificha, endapo shambulio hilo lingekuwa ni uasi wa jeshi, Ikulu ingekuwa sehemu ya kwanza kuvamiwa.

Mapigano yalidumu kwa kipindi kisichozidi saa moja. Ndani ya saa moja na nusu, Waisrael walifanikiwa kuondoka na mateka. Nyuma waliacha maiti ishirini za Waganda, saba za watekaji nao waliondoka na maiti mbili za mateka.

Katika hospitali ya Mulago, magari ya jeshi na magari ya wagonjwa yalipishana yakiingiza majeruhi, nao ndugu walisimama pembeni wakilia. Miili ilipelekwa mochwari na zoezi la kuwatambua liliendelea. Waliojeruhiwa vibaya (walipata kuwa kumi) walipelekwa sadaruki (chumba cha wagonjwa mahututi). waliokuwa na majeraha madogo walitibiwa wakaruhusiwa kurejea nyumbani. Askari wa jeshi la Uganda waliwapiga raia walioonyesha kuwacheka kwa fedhesha iliyowakuta.

Pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatwa na jeshi la Israel katika zoezi la uokoaji, walimsahau Dora Bloch aliyekuwa hospitali!

Saa kumi na mbili kamili jioni, Waziri wa Afya alipokea ujumbe kutoka Hospitali uliomweleza kuwa Ofisa Kutoka Ubalozi wa Uingereza, Peter Chandley, alitaka kuonana na Dora Bloch. Watumishi wa hospitali walimuuliza waziri kipi wafanye? Waziri alisema mtu huyo aruhusiwe kuonana na Dora Bloch kwa muda mchache.

Chandley alifika kumjulia hali Bi. Bloch ambaye aliomba apelekewe vyakula fulani alivyozoea kula ulaya. Chandley alielekea nyumbani kuandaa chakula hicho. Muda huohuo, Idi Amin alikuwa akiandaa jambo lako hasa ukizingatia aibu aliyoipata kwa uvamizi uliofanyika.

Punde Chandley alipotoka,wanaume wanne walifika Hospitali ya Mulago. Wawili kati yao, baadae walikuja kufahamika kuwa Meja Farouk Minawa na Kepten Nasur Ondoga. Walivalia mavazi ya kiraia na walikuwa na bastola. Bila shaka walifahamu walikokuwa wakienda na walifahamu waliyemtaka hakuwa na jeuri ya kuwasumbua. Walipiga kelele kwa watumishi wa hospitali wakiwataka wapishe mbali, wakawataka walinzi waondoke, wakaufungua mlango na kumtoa Dora Bloch kitandani. Walimkamata kwenye mikono yake huku na huku wakaanza kumvuta. Nyuma aliacha fimbo, begi, viatu na gauni. Kwa kuwa hakuwa na uwezo wa kutembea, walimburuza na wakati mwingine alinyanyuliwa juujuu. Alilia bila kunyamaza.

Wagonjwa, watumishi wa afya na waliokuja kutembelea wagonjwa walijaa katika milango ya wodi kushuhudia kilichotokea. Hawakuwa na uwezo wa kufanya chochote kumuokoa. Alipelekwa na kuingizwa katika gari ambayo iliondoka kwa kasi katika eneo lile la hospitali. Tukio lote lilidumu kwa dakika tano tu na ilipata saa tatu kamili.

Inaendelea Kesho...

Soma: Jinsi ya Kuandika CV
 
4

Asubuhi iliyofuata, maombi yalianza. Ubalozi wa Uingereza ulitaka kuzungumza na Mrs. Bloch. Walipiga simu hospitali wakiuliza alipokuwa Bloch. Waziri wa Afya alijulishwa kuhusu simu hiyo lakini hakuwa na cha kujibu. Ilipofika saa tatu na dakika kumi, Amin alimpigia simu Waziri wa Afya na akamweleza kwamba kama mtu yeyote angeomba kufahamu alipo Bi. Bloch, alitakiwa kusema kwamba alirejeshwa uwanja wa ndege saa moja kabla makomandoo wa Israel hawajavamia hivyo makomandoo waliondoka naye. Msimamo wa serikali ya Uganda ni kwamba, hawafahamu alipo Bibi huyo.

Waziri alifafanua kwa Amin kwamba kulikuwa na ushahidi wa nyaraka zake hospitali ambao unakwenda kinyume na anachopaswa kueleza, Amin alihitimisha kwa kumweleza abadili taarifa hizo.

Waziri wa Afya alitumia saa moja hospitali akitengeneza nyaraka mpya na kuziondoa zile za zamani. Pia alificha vitu vilivyoachwa na Bi. Bloch.

Amin alilipa kisasi. Bi Bloch aliuawa. Mwili wa Bibi huyu ulitupwa pembezoni mwa barabara kiasi cha maili ishirini kutoka Kampala, barabara kuu ya kuelekea Jinja. Lilifanywa jaribio la kuuchoma moto mwili huu na uliungua kiasi, hata hivyo mvi hazikuguswa. Habari ilisambaa na watu walifika mamia kwa mamia kushuhudia mwili ule. Hata hivyo, serikali iliendelea kutangaza kuwa haifahamu alipo Bi.Bloch.

Mwandishi wa habari Jimmy Parma alipiga picha mwili wa Bi. Bloch. Kwa serikali ya Amin alifanya kosa kubwa, mwili wake ulitambuliwa baadae ukiwa na majeraha ya risasi na visu.

Mpaka inafika mwaka 1977, serikali ya Idi Amin ilifanya siri juu ya ulipo mwili wa Bi. Bloch, serikali yake ilisisitiza haifahamu alipo Dora Bloch kwani alirejeshwa uwanja wa ndege saa moja kabla ya uvamizi.

Mwaka 1979, majeshi ya Tanzania yaliuangusha utawala wa Idi Amin na kumfukuza Uganda.

Majeshi ya Tanzania kwa intelijensia ya hali ya juu na isiyopimika yaligundua ulipozikwa mwili wa Bi. Dora Bloch. Mwili wa bibi huyu ulizikwa katika shamba kubwa la miwa. Kama ilivyoelezwa, ulikuwa umeunguzwa vibaya kwa moto. Wataalamu waliweza kuhakiki kama kweli ulikuwa mwili wake na ilithibitika kuwa kweli ni mwili wa Dora Bloch. Jeshi la Israel nalo lilithibitisha hivyo. Mwili wake ulirejeshwa kwa mwanae aliyekuwa Israel. Ikumbukwe kuwa, wakati Bi. Dora anatekwa, alikuwa na mwanae huyu. Kwa sasa mwili wa Bi. Dora Bloch umezikwa Jerusalem katika makaburi ya Hamenuchot. Heko! Jeshi la Wananchi wa Tanzania.

Mwisho.

Soma: Jinsi ya Kuandika CV
 
Umesema mwaka 1977 Idd aligoma kukiri alipo bi Bloch baada ya kuuawa, ila mwaka 1979 iligundua alipozikwa huyu na mwili ulikuwa umeharibika mno. Ina maana hadi wakati huo huyu bibi alikuwa hajaoza au? Naomba nifahamishwe hapa.

Sent from my SM-A225F using JamiiForums mobile app
 
Umesema mwaka 1977 Idd aligoma kukiri alipo bi Bloch baada ya kuuawa, ila mwaka 1979 iligundua alipozikwa huyu na mwili ulikuwa umeharibika mno. Ina maana hadi wakati huo huyu bibi alikuwa hajaoza au? Naomba nifahamishwe hapa.

Sent from my SM-A225F using JamiiForums mobile app

Maneno yaliotumika ni "umeunguzwa vibaya kwa moto"

Mwili wa bibi huyu ulizikwa katika shamba kubwa la miwa. Kama ilivyoelezwa, ulikuwa umeunguzwa vibaya kwa moto
 
Umesema mwaka 1977 Idd aligoma kukiri alipo bi Bloch baada ya kuuawa, ila mwaka 1979 iligundua alipozikwa huyu na mwili ulikuwa umeharibika mno. Ina maana hadi wakati huo huyu bibi alikuwa hajaoza au? Naomba nifahamishwe hapa.

Sent from my SM-A225F using JamiiForums mobile app
Wataalamu wanaweza kubaini Hali ya mwili ilikuwaje kabla ya mauaji
 
Back
Top Bottom