http://www.mwananchi.co.tz/mwananchisite/Mwananchi/Habari/Habari3.asp
Serikali yafunga mgodi wa dhahabu Musoma
Na Mathias Marwa, Musoma
SERIKALI imesitisha shughuli za uzalishaji wa dhahabu kwenye mgodi wa Buhemba Gold Mine (BGM) katika Kata ya Buhemba, Wilaya ya Musoma Vijijini mkoani Mara, kutokana na madini hayo kupungua katika eneo hilo.
Mkuu wa Wilaya za Musoma Mjini na Vijijini, Saveli Maketa, aliwaeleza wafanyakazi 350 wa mgodi huo kuwa serikali imefikia uamuzi huo kutokana na sababu hiyo, lakini kuwahakikishia kuwa hakuna atakayefukuzwa kazi na wataendelea kulipwa mishahara yao kama kawaida.
"Serikali imetenga eneo lingine la kuchimba dhahabu baada ya dhahabu ya hapo kupungua, lakini hakuna mfanyakazi atakayefukuzwa na wote mtalipwa mishahara yenu kwa kipindi chote ambacho mtakuwa hamfanyi kazi," alisema.
Maketa aliwaeleza wafanyakazi hao kuwa mgodi huo wa Buhemba ni mali ya serikali pamoja na mali nyingine, ikiwamo mitambo yake na kwamba hata mishahara wanayolipwa ni ya serikali kupitia kwa mwekezaji kutoka Afrika Kusini.
"Mgodi, samani zote za ofisi, mali zote za hapa mgodini na mishahara yenu ni mali ya serikali ya Tanzania, hivyo ni mali zenu. Hao mnaowaita makaburu hawana chochote hapa bali wao ni mawakala tu wa serikali," alisema Maketa.
Alifafanua kuwa serikali haiwezi kumudu kukaa na wafanyakazi hao wote 350 wakati hakuna uzalishaji, hivyo utaratibu umepangwa wa kuwarejesha baadhi yao kwao ingawa wataendelea kulipwa mishahara yao na wengine watabaki katika eneo hilo kufukia mashimo, kusawazisha eneo hilo na kupanda miti ili kuhifadhi mazingira.
Alisema, wafanyakazi hao hawatapata malipo ya muda wa ziada kwa kuwa hakuna uzalishaji kwa sasa, ila baada ya uzalishaji mpya kuanza kwenye eneo jipya ambalo tayari limeishapangwa.
Mkuu huyo wa Wilaya alisema pia kwamba serikali ina akiba maalum benki inayotokana na mapato ya mgodi huo ambayo iko chini ya Bodi ya Wadhamini wakiongozwa na Gavana wa Benki Kuu (BoT) na kwamba akiba hiyo ndiyo itakayotumika kuwalipa mishahara.
Akijibu maswali ya wafanyakazi hao, Maketa aliwaeleza kuwa serikali itatoa fedha kwa ajili ya eneo lingine jipya la mgodi huo katika eneo hilo la Buhemba, lakini itachukua takriban miezi saba kuanzia sasa.
Kwa mujibu wa DC, mgodi huo umewekeza kiasi cha Sh18 bilioni, ikiwamo mishahara ya wafanyakazi, mitambo na samani zote za ofisi.
Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Migodi, Ujenzi, Nishati na kazi nyinginezo (Tamico) kanda ya ziwa, Stephen Mageta, alisema pamoja na ujumbe mzuri wa DC kwa wafanyakazi hao, lakini wanataka serikali iwahakikishie kwa maandishi kuwa hawatawafukuza kazi na kwamba watalipwa mishahara yao wakati huo wa mpito.
"Wafanyakazi tulikuwa hatuamini kwamba mgodi huu ni mali yetu, sisi tunajua ni mali makaburu kutokana na unyanyasaji, vipigo tunavyopigwa, mishahara midogo na matusi juu," alisema Mwenyekiti wa Tamico tawi la Buhemba, Edward Ng'wenge.
Meneja wa mgodi huo, Jian Duvenage alikataa kuzungumza lolote na waandishi wa habari mgodini hapo na badala yake alimuomba DC aongee naye faragha.
Gazeti hili toleo la Novemba mosi, mwaka huu lilichapisha habari zikimkariri Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono, akiutaka mgodi huo, pamoja na mambo mengine waonyeshe ankara zao na takwimu za mrahaba wanaolipa tangu waanze kuchimba dhahabu.
"Endapo BGM itapuuza, agizo hilo litaliwasilisha bungeni na nikishindwa nitakwenda kuwatetea wananchi mahakamani," alisema Mkono ambaye pia ni wakili.