Dkt. Mkenda azindua mradi wa HEET utakaonufaisha vyuo 14 Mradi una thamani ya Tsh. Bilioni 972. Sasa Elimu ya Tanzania kuwa bora

JanguKamaJangu

JF-Expert Member
Feb 7, 2022
2,309
5,464
e0a1f7ff-fe3c-4ab9-8de4-d1e59ac2941e.jpg

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda akizindua Mradi wa HEET wa miaka mitano uliolenga kuboresha elimu na kunufaisha vyuo 14, uzinduzi umefanyika leo Septemba 13, 2022, Dar es Salaam.

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema Serikali itahakikisha inawasomesha Wahadhiri wa Vyuo Vikuu nje ya nchi Ili kusaidia kutoa elimu ujuzi yenye kiwango bora kuendana na soko la ajira kimataifa.

Akizungumza leo Septemba 13,2022 Jijini Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi wa Mradi wa HEET wa miaka mitano uliolenga kuboresha elimu na kunufaisha vyuo 14 ambapo amesema kupitia mradio pia unakwenda kusaidia Wahadhiri kwenda kusoma katika nchi mbalimbali ikiwemo Denmark,Ufaransa,Ubelgiji, Ili kusaidia kuongeza ubora wa Elimu na lazima ianzie juu ndipo ishuke sekondari hadi shule za msingi kwani dunia Sasa hivi imebadikika kinachohitajika ni ujuzi zaidi.

"Duniani kote wanazungumzia suala la elimu hii inatokana na changamoto ya kuwa na wahitimu wengi lakini wanaoshindwa kujiajiri kutokana na kutokuwa na ujuzi ukitazama vyeti wanavyo lakini digree za kutosha lakini mwanafunzi inashindikana kuajiajiri hivyo Wahadhiri waliopata fursa kwenda kusoma njee wakihitimu wanaokuja kubadilisha mtazamo"amesema Waziri

WhatsApp-Image-2022-09-13-at-1.15.13-PM-3.jpg

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Mradi wa HEET wa miaka mitano uliolenga kuboresha elimu na kunufaisha vyuo 14 uliyofanyika leo Septemba 13, 2022, Dar es Salaam.

Sanjari na hayo Waziri amesema Mradi huo ni mkubwa na ni wa kipekee ambao umekuja kutoa hamasa na kusukuma Tanzania katika suala zima la elimu ikiwa ni pamoja na uboreshajiwa miundombinu ya vyuo ikiwemo mitaala.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Francis Michael amewataka wasimamizi wa mradi kuhakikisha fedha zikizotolewa za mradi zinatumika katika mlengo uliokusudiwa kwani ikibainika kuna ujanja ujanja watakaohusika watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Amebainisha kuwa fedha zikizotolewa jumla ya Milion 425 sawa na Bilioni 972 zimetolewa na Benki ya dunia ikiwa ni mkopo wa masharti nafuu Kwa lengo la kuboresha elimu ya juu.

"Bado Vyuo vikuu havijafikia kiwango kilichowekwa kwa wahitimu wa elimu ya juu kwani mpaka sasa ni asilimia 3.5 ambapo lengo ni kufikia asilimia 12. naitaka kamati ya wasimamizi wa mradi huu kutosita kutoa taarifa ya changamoto yeyote itakayowakabili ili kuenda sambamba na kasi ya utekelezaji "amesema Mkenda.

Naye Mwakilishi kutoka benki ya Dunia Preeti Arora ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuwa na mtazamo chanya wa kuboresha elimu Ili kuendana na mahitaji ya Soko la ajira la kimataifa hivyo watahakikisha wanashirikiana nao began kwa bega pale watakapohitajika.
====

Hotuba ya Dkt. Francis Michael, Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Francis Michael, Katika Hafla ya Uzinduzi wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi Tarehe 13 Septemba, 2022, Katika Ukumbi Wa Golden Jubilee, Jijini Dar es Salaam.

WhatsApp-Image-2022-09-13-at-1.15.13-PM-2.jpg

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Francis Michael akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Mradi wa HEET wa miaka mitano uliolenga kuboresha elimu na kunufaisha vyuo 14 uliyofanyika leo Septemba 13, 2022 Dar es Salaam.


Awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema kwa kutujalia afya njema na kutukutanisha katika hafla hii ya uzinduzi wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (Higher Education for Economic Transformation-HEET).

Ninakushukuru sana wewe binafsi kwa kuridhia kuwa Mgeni Rasmi katika hafla hii na ushirikiano tunaoupata kutoka kwako tangu ulipoteuliwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mama Samia Suluhu Hassan kusimamia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Sote ni mashahidi kuwa umejitoa kwa moyo wote katika kuona elimu inayotolewa kwa ngazi zote inakidhi mahitaji mapana ya wanayoipata na hususani mahitaji ya soko la ajira. Ndio maana pamoja na kuwa na majukumu mengi muhimu ya Wizara, umeona vema kuwa nasi leo kama Mgeni rasmi ili uweze kuzindua rasmi mradi wa Elimu ya Juu kuashiria kuanza rasmi utekelezaji wake.

Aidha, ninatoa shukrani nyingi kwa Benki ya Dunia kwa kuridhia kutoa mikopo ya masharti nafuu kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi huu na Miradi mingine nchini. Ninawashukuru pia kwa kuungana nasi leo katika hafla ya uzinduzi wa Mradi huu; Asanteni sana! Aidha, ninawashukuru nyote mlioungana nasi leo katika uzinduzi wa mradi huu.
2fec25ed-ef6d-41ba-8045-2f89c2b07fcd.jpg

Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi ni mradi wenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 425.0 sawa na wastani wa shilingi za Tanzania bilioni 972.0. Fedha hizi ni Mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mradi huu unatarajiwa kutekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia 2021 hadi 2026.

Mradi wa HEET unatekelezwa kupitia Vyuo Vikuu 14, Taasisi Tatu (3) ambazo ni Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTEC), pamoja na Taasisi Tano (5) za Wizara ya Fedha na Mipango. Aidha, kupitia Mradi huu Serikali itatoa ruzuku kwa Vyuo Vikuu Binafsi kwa ajili ya kusomesha wahadhiri katika masuala ya afya na tiba kutokana na mahitaji mkubwa ya wataalam katika sekta hiyo, lakini pia kama sehemu ya mkakati wa serikali wa kushirikisha Vyuo Vikuu binafsi katika kuendeleza sekta ya Elimu ya Juu nchini.

Kupitia utekelezaji wa mradi wa HEET, Serikali itaboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika Vyuo Vikuu na Taasisi nufaika kwa kutekeleza mambo mbalimbali; kwa ruhusa yako ninaomba kutoa ufafanuzi kwenye maeneo machache:
  • Ujenzi na ukarabati wa miundombinu kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya Kitaaluma na Kiutawala.
  • Mheshimwa Mgeni Rasmi, kiasi cha Dola za Marekani milioni 329, sawa na wastani wa shilingi bilioni 752.50, zitatumika kujenga miundombinu mipya na kukarabati iliyopo ikiwemo kumbi za mihadhara na madarasa (130), maabara na karakana (108), mabweni (34), ofisi (23) na miundombinu ya mashambani na vituo atamizi (10) pamoja na kuweka vifaa vya kisasa vya TEHAMA katika Vyuo Vikuu na Taasisi nufaika wa Mradi. Uboreshaji huu utaongeza udahili katika program za kipaumbele kutoka wanafunzi 40,000 mwaka 2020 hadi kufikia 106,000 mwaka 2026.
Sambamba na kuboresha na kujenga miundombinu mbambali katika kampasi kuu za Vyuo Vikuu/Taasisi nufaika, Serikali itajenga kampasi mpya 14 katika Mikoa mbalimbali nchini ikiwemo Lindi, Katavi, Rukwa, Mwanza, Tanga, Shinyanga, Kigoma, Simiyu, Ruvuma, Singida, Tabora, Manyara, Kagera na Dodoma. Kwa mkoa wa Dodoma, Serikali itajenga Chuo Kikuu cha kisasa cha TEHAMA. Bila shaka mtakumbuka kwamba ujenzi wa Chuo Kikuu hiki ni sehemu ya ahadi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Aidha, kampasi hizi mpya zitajikita katika kutoa ujuzi katika maeneo ya kimkakati.

Uboreshaji wa baadhi ya mitaala iliyopo na Uandaaji wa Mitaala mipya ya programu za kipaumbele ili iendane na mahitaji ya soko la ajira

Kiasi cha Dola za Marekani milioni 7.97, sawa na wastani wa shilingi bilioni 18.23, zitatumika kuhuisha na kuandaa mitaala mipya zaidi ya 290 ili kuhakikisha kwamba elimu inayotolewa inaendana na kujibu mahitaji ya soko la ajira ndani na nje ya nchi. Aidha, Serikali itatumia kiasi cha Dola za Marekani milioni 7.79, sawa na shilingi bilioni 17.83, kuboresha mazingira ya kubuni na kuunda teknolojia na kuziendeleza hasa zile zinazolenga kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi. Ni dhahiri kwamba elimu ya namna hii itaongeza uwezo wa kujiajiri kwa wahitimu.

Kusomesha wanataaluma kuanzia ngazi ya shahada ya umahiri hadi uzamivu sambamba na kutoa mafunzo kazini kwa watumishi

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

Mradi huu unalenga kusomesha takribani wahadhiri 1,100, ambapo Wahadhiri 623 katika shahada za uzamivu (PhD) (wanaume 355 na wanawake 268), na Wahadhiri 477 katika shahada ya umahiri (MSc) (wanawake 197, wanaume 280). Halikadhalika, wahadhiri na wafanyakazi wengine katika Vyuo Vikuu, Wizara na Taasisi nyingine watanufaika wa Mradi huu, watapata fursa ya mafunzo ya muda mfupi na ya viwandani ndani na nje ya nchi. Aidha, kama nilivyosema awali, katika kutambua mchango wa sekta binafsi katika Elimu ya Juu, Serikali itatumia sehemu ya fedha za mradi kufadhili masomo kwa wahadhiri wa Vyuo Vikuu Binafsi vinavyotoa mafunzo katika fani za Afya na Tiba.
e0a1f7ff-fe3c-4ab9-8de4-d1e59ac2941e.jpg

Kuimarisha ushirikiano na Sekta Binafsi na viwanda katika kundaa mitaala, ufundishaji, mafunzo kwa vitendo na ubiasharishaji wa matokeo ya utafiti na ubunifu.

Sehemu ya fedha za Mradi huu pia zitatumika kuwezesha Taasisi za Elimu ya Juu kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi kwa ujumla ikiwemo sekta ya viwanda ili kuhakikisha kwamba wahitimu wanapata maarifa na ujuzi unaohitajika na unaoendana na soko la ajira. Vilevile, kupitia ushirikiano huo matokeo ya tafiti yatabiasharishwa na hivyo kutumika kutatua changamoto mbalimbali katika jamii.
  • Mheshimiwa Mgeni Rasmi, vilevile mradi wa HEET umelenga katika kuimarisha mifumo ya usimamizi wa Elimu ya Juu kwa kuimarisha uratibu na usimamizi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia na ubunifu kwa kuzijengea uwezo Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia: Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH); Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB); na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na kufanya mapitio ya sheria, kanuni na miongozo mbalimbali ya Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia na Ubunifu

  • Mheshimiwa Mgeni Rasmi, baada ya kuelezea shughuli muhimu zitakazotekelezwa na mradi ninaomba kuhitimisha kwa kukuhakikishia kwamba Wizara na Taasisi nufaika zote za Mradi huu tumejipanga kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yanatekelezwa kwa tija na kwa wakati.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi, Mabibi na Mabwana, baada ya hotuba yangu fupi ninaomba niwashukuru kwa kunisikiliza na nichukue fursa hii sasa kukukaribisha uongee na hadhira hii na kisha uzindue Mradi huu rasmi.
 
Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi ni mradi wenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 425.0 sawa na wastani wa shilingi za Tanzania bilioni 972.0. Fedha hizi ni Mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mradi huu unatarajiwa kutekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia 2021 hadi 2026.
Haya mageuzi yanaimbwa miaka nenda rudi hatuoni mabadiliko kwa vijana wanaomaliza vyuo
 
Back
Top Bottom