Mag3
Platinum Member
- May 31, 2008
- 13,064
- 22,757
Dk Slaa, NEC wamshukia Tendwa
Boniface Meena, Rombo na Salim Said Dar - Mwananchi
Boniface Meena, Rombo na Salim Said Dar - Mwananchi
TUME ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) imemshukia Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, ikibainisha kuwa msajili huyo amevuka mipaka kutokana na kitendo chake cha kutetea baadhi ya wagombea kufanya kampeni hadi nje ya muda uliopangwa kisheria wa saa 12 jioni.
Juzi Tendwa alitetea hatua ya mgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete, kufanya kampeni hadi hadi saa 1:00 usiku badala ya saa 12:00 jioni ulioidhinishwa na Nec.
Nec imeeleza hayo jana ikiwa ni siku moja tu baada ya Tendwa kueleza kuwa kuanzia sasa wamekubaliana kuwa mwisho wa mikutano ya kampeni ni saa moja usiku badala ya saa 12 jioni.
Akitoa tathimini ya mzunguko wa kwanza wa kampeni mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Slaam jana, Mwenyekiti wa Nec, Jaji Lewis Makame alisema Tendwa amevuka mipaka kwa sababu ameingilia majukumu yasiyokuwa ya kwake.
"Msajili wa Vyama amevuka mipaka kwa kutetea baadhi ya wagombea kupiga kampeni hadi saa 1:00 usiku jambo ambalo ni kinyume cha sheria," alisema Jaji Makame.
Jaji Makame aliongeza kuwa: "Kazi ya kupanga ratiba ya mikutano ya kampeni na uchaguzi ni ya Nec na sio ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa."
Jaji Makame alikemea vikali ukiukwaji wa kanuni na taratibu zilizowekwa na Nec kuhusu mikutano ya kampeni na kwamba, Tume haitosita kuchukua hatua kali zaidi kama ambavyo zimeainishwa katika maadili ya uchaguzi.
"Hatua hizo ni pamoja na kusimamisha kampeni za chama au mgombea atakayeendelea kukiuka sheria na maadili ya uchaguzi," alisema Jaji Makame.
Wakati Tendwa akisema muda wa kampeni umeongezwa hadi saa 1:00 kuanzia sasa kutokana na sababu za kijiographia, Jaji Makame huku akinukuu kanuni za sheria na maadili ya vyama vya siasa alisema muda wa kampeni uliokubaliwa kisheria, ni kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni.
"Tume inapenda kusisitiza kwamba ni muhimu kwa vyama na wagombea wao, kuendesha kampeni kwa njia ya busara na kuheshimiana," alisema Jaji Makame na kuongeza:
"Kampeni za uchaguzi zifanyike katika muda unaoruhusiwa kisheria ambao ni kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 12:00 jioni."
Tofauti na Tendwa ambaye kisheria hana mamlaka ya kuratibu mikutano ya kampeni, Jaji Makame alisema hakuna mabadiliko yoyote ya muda wa mikutano ya kampeni yaliyofanywa na kwamba vyama na wagombea waheshimu muda na ratiba iliyopangwa na Nec na sio msajili.
Akitoa tathmini ya awamu ya mzunguko wa kwanza wa kampeni hizo, Jaji Makame alisema kiujumla kampeni zimekuwa zikienda vizuri katika maeneo mengi nchini.
Hata hivyo, alisema ofisi yake imebaini mapungufu nane ambayo yameonekana waziwazi katika mzunguko huo wa awali katika kampeni za kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31 mwaka huu.
Aliyataja mapungufu hayo kuwa ni pamoja na baadhi ya wafuasi wa vyama kuingilia mikutano ya kampeni ya vyama vingine na kusababisha fujo, baadhi ya vyama na wagombea kufanya mikutano ya kampeni nje ya muda unaoruhusiwa na baadhi ya wagombea kutumia lugha za kejeli na matusi kushambulia wagombea wengine.
"Jazba kwa wafuasi wa baadhi ya vyama na kuchana bendera na mabango ya wagombea wengine, baadhi ya wagombea kutumia lugha za kienyeji (kikabila) badala ya Kiswahili na wafuasi wa baadhi ya vyama kuwabuguzi waandishi wa habari na kulazimisha kuvaa sare za vyama vyao," alisema Jaji Makame.
Alisema mapungufu mingine ni pamoja na baadhi ya vyama kutumia mabango yasiyoidhinishwa na Tume na baadhi ya vyombo vya habari kushindwa kutoa taarifa sahihi na zisizoegemea upande wowote na hivyo kukiuka maadili ya habari kuhusu usawa wa kuripoti.
Alisema kufuatia mapungufu hayo, Tume kupitia wasimamizi wake wa uchaguzi na makao makuu imeweza kushugulikia malalamiko na rufaa kadhaa zilizofikishwa ofisini kwao.
Alisema vitendo hivyo vikiachiwa kuendelea vinaweza kusababisha uvunjifu wa amani na utulivu wa nchi, huku akivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha wanaimarisha ulinzi sehemu za mikutano.
Alisema kampeni sheria imeruhusu kampeni za nyumba kwa nyumba, lakini mambo ya kitanda kwa kitanda, kichwa kwa kichwa ni tafsiri za wanasiasa tu.
Wakati hayo yakiendelea Chadema, kimemshukia Tendwa kwa kusema kuwa hakina imani naye tena kwa kuwa ameonyesha kuisaidia CCM baada ya kuongeza muda wa kampeni kinyume cha sheria.
Akihutubia wananchi wa Tarakea katika Jimbo la Rombo mgombea urais wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa alisema kuwa Tendwa ameamua kufanya hivyo baada ya mgombea wa CCM, Kikwete kufanya kampeni zaidi ya muda uliopangwa kinyume na maadili waliyokubaliana.
"Kikwete amekuwa akihutubia zaidi ya muda uliopangwa wa saa 12 kamili, kwa mfano alipokuwa Arusha, Babati na Mbulu amehutubia zaidi ya muda huo na hakuna hatua alizochukuliwa na ndiyo maana Tendwa ameamua kufanya hivyo,"alisema Dk Slaa.
Dk Slaa alitaka Tendwa ajiuzulu baada ya kauli ya NEC kusema kuwa haitambui alichokifanya na kama hatajiuzulu Rais Kikwete amfukuze kazi kwa kuwa anaweza kuleta vurugu katika Uchaguzi Mkuu.
Dk Slaa alisema kuwa wanasheria wa Chadema wanalishughulikia suala hilo kwa kuwa Tendwa haaminiki.
"Mimi siogopi kufa, niko tayari kupigwa risasi kwa kutetea Watanzania masikini na Tendwa ajue wananchi wamechoka na mizengwe wanayofanya kumlinda Kikwete ambaye amevunja sheria tangu alipoanza kampeni kwa kutoa ahadi lukuki kitu ambacho sheria inakataza,"alisema.
Katika hatua nyingine, Dk Slaa aliwataka wakazi wa Jimbo la Rombo kutokumchagua Basil Mramba kuwa mbunge kwa kuwa ni mtuhumiwa na jimbo hilo halina sababu ya kuongozwa na mtuhumiwa ambaye ana kesi mahakamani.
"Mramba apumzike kwa kuwa anahitaji kupunguza aibu aliyoipata, kwani asipofanya hivyo aibu hiyo itaongezeka. Ninaishangaa CCM kumpitisha mtuhumiwa kitu ambacho ni cha kuwazalilisha wananchi wa Rombo,"alisema Dk Slaa.
Hata hivyo, Tendwa alipotafutwa na gazeti hili kwa ajili ya kuzungumzia suala hilo hakuwa tayari kusema chochote kutokana na kile alichosema ana uchovu mkubwa.
"Nemechoka sana, ndio kwanza nimemaliza safari ndefu ya kutoka Arusha kuja Mwanza, kwa hiyo unaonaje kama tukizungumza kesho," alisema Tendwa.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema kuwa chama chake kilisoma alama za nyakati kilipoamua kumteua Dk Slaa kugombea urais na ndiyo maana CCM imechanganyikiwa.
Alisema Chadema iliamua kufanya hivyo baada ya kusoma alama hizo kwa kuwa Dk Slaa anauzika kutokana na kazi nzuri aliyoifanya bungeni kwa muda wa miaka 15 iliyopita.
Mbowe alisema chama kilifanya siri uteuzi wa Dk Slaa kwa kuwa CCM walijua yeye ndiye atakayegombea hivyo walijua njia ya kuwamaliza ni kuwapa Dk Slaa wapambane naye.
Mbowe alisema kuwa Slaa anawachanganya CCM na ndiyo maana mgombdea wa CCM, Kikwete hivi sasa anahaha kuhutubia hadi usiku na kuvunja sheria ya uchaguzi ambayo aliisaini mwenyewe.
"Kikwete roho yake itamtoka kutokana na sheria ya uchaguzi aliyoisaini mwenyewe, nadhani hakuisoma sheria hiyo vizuri na sasa hivi anayaona maumivu yake,"alisema Mbowe.
Alisema kuwa hivi sasa maji yako shingoni kwa Kikwete na ndiyo maana huwa anafanya mikutano mijini na kuacha wananchi wa vijijini kutokana na kutokujua afanye nini Dk Slaa asimdondoshe.
Akizungumzia kuhusu nafasi yake ya kugombea ubunge katika Jimbo la Hai dhidi ya mgombea wa CCM, Fuya Kimbita, Mbowe alisema kuwa Kimbita akimshinda katika kinyang'anyiro hicho ataachana na siasa moja kwa moja.
"Fuya akinishinda naachana na siasa, amekuwa akifanya mikutano usiku na mchana wakati mimi sijafanya hata mmoja mpaka alipofika Dk Slaa ndiyo nikazunguka naye," alisema Mbowe.
Hivi Tendwa anajua hata mipaka ya utendaji wa Ofisi yake ?