Nchi hii tunacheza michezo ya hatari kweli. Hainiingii akilini kama tunaweza kuthubutu kushabikia kitendo cha mtu kuiba nyaraka ya serikali wenyewe tunasema 'akamata'. Kuiba nyaraka ya serikali ni jambo la hatari kwa uhai wa taifa lolote haijalishupi umefanywa na nani? Leo Dr. Slaa anaiba nyaraka ya Serikali na tunamshangilia.
Mbinu hii itatumika dhidi ya Serikali ya CHADEMA siku itakapojaaliwa kuingia madarakani. Mchezo huu ukiendelea, hakuna Serikali itakayotawala. Kitendo hiki kinadhoofisha Serikali na sio kitendo ch kushabikia hata kidogo, na ndio maana kuna sheria ya bunge dhidi ya kitendo hicho. Bahati nzuri Serikali yenyewe in huruma huruma hivi.
Lakini la pili ni kuwa, tunataka sasa kuhalalisha ushiriki wa watumishi wa umma kwenye siasa. Hii ni hatari nyingine. Kitendo cha kunajisi utumishi wa umma na siasa, aidha kusaidia Chama Tawala au Chama cha Upinzani ni kitendo cha hatari na kukemea. Watumishi wa umma wakifanya kazi kisiasa hakuna maendeleo yatakayopatikana na hatari ya hujuma aidha dhidi ya wapinzani au serikali inaweza kuwa kitu cha kawaida.
Sioni tatizo lolote kuhusu Waraka huo wa kukataza watumishi wa umma kutoshiriki shughuli za siasa. Waraka haukatazi mtumishi wa umma kuwa mwanachama, kinachokatazwa ni kuwa kiongozi wa chama au kufanya shughuli za chama cha siasa mahala pa kazi. Waraka huu unawasaidia pia CHADEMA kuliko tunavyotaka kuaminishwa.
Watumishi wa Umma wakiamua kutumika dhidi ya CHADEMA ustawi wa Chama hicho utakuwa mashakani. Inawezekana walioko kwenye utumishi wa umma wakawa CCM wengi kuliko CHADEMA kama ambavyo inawezekana pia wakawa CHADEMA wengi kuliko CCM. Lengo la Waraka huu ni kulinda maslahi ya umma wote na haki yao ya kupata haki na huduma kutoka katika utumishi wa umma bila kujali itikadi.
Pengine nielezwe humu ni nchi gani na wapi ambapo utumishi wa umma wanaruhusiwa kujihusisha na siasa za vyama mahala na wakati wa kazi? Kwa nini sisi tuwe wa kwanza?
Tusikubali kutumiwa kuhalalisha mbinu haramu kwa sababu tu ya kutaka kufikia maslahi yetu ya kisiasa. CHADEMA wakumbuke, mbinu hizo hizo zitatumika dhidi yao wakiwa madarakani.