DK. awindwa

Selous

JF-Expert Member
Jan 13, 2008
1,325
143
na Mwandishi Wetu, Dodoma

Source:http://www.freemedia.co.tz/daima/2008/6/29/habari2.php

KATIKA hali inayoonyesha kuelemewa na mzigo wa kashfa, serikali imeanza kujipanga kuwashughulikia wale wote wanaoiumbua.

Mkakati huo wa kuwashughulikia wanaoikosoa na kuanika dhambi za serikali hadharani, unatarajiwa kuanzia bungeni na mlengwa wa kwanza ni Mbunge wa Karatu, Dk. Willibrod Slaa (CHADEMA).

Tayari Dk. Slaa anayeonekana kuwa mlengwa mahsusi wa mkakati huo, amekwishaonywa kuwa utumiaji wake wa nyaraka za serikali zinazotajwa kwamba ni siri za serikali, kila anapoirushia makombora, unaweza kumtokea puani.

Dalili kwamba serikali imeamua kupambana na watu wanaoirushia tuhuma ambazo zimekuwa zikiitesa na hata kusababisha baadhi ya viongozi kulazimika kuachia nyadhifa zao, ni kauli ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Uratibu na Bunge, Philip Marmo aliyoitoa bungeni Alhamisi iliyopita, aliposimama na kutaka mwongozo wa Spika, kuhusu wabunge wanaopata nyaraka za siri za serikali na kuzitumia kuirushia tuhuma.

Katika ombi lake hilo, Marmo alisema kuwa ipo sheria inayobainisha kuwa ni kosa la jinai kwa mtu kukutwa na nyaraka za siri za serikali, na alimtaja Dk. Slaa kama mmoja wa watu wanaozipata nyaraka hizo.

“Sehemu zote duniani, kila waziri anapo-declare (anapotangaza) kuwa hii ni classified document (nyaraka ya siri) huwa haijadiliwi bungeni. Hata ukikutwa unatembea na nyaraka hizo, ukikamatwa nazo ni kosa la jinai. Hivi hawa wenzetu wanazipata wapi? Ni kwamba hapa kwetu vyombo vya dola vinafumba macho tu, vikiamua kupambana nao itakuwaje?” alihoji Marmo.

Naibu Spika, Anna Makinda ambaye alikuwa akiendesha kikao hicho, alitoa mwongozo wake kwa kueleza kuwa mbunge yeyote anapokuwa na nyaraka ambayo anataka kuinukuu wakati anachangia, kama vile kitabu au gazeti, anapaswa kwanza kukieleza kiti.

Alisema hata kama mbunge anataka kuinukuu sehemu ya hotuba ya bajeti anayochangia, anapaswa kuomba ruhusa kwa anayeongoza kikao, na atainukuu tu atakaporuhusiwa kufanya hivyo.

Makinda alikwenda mbali zaidi kwa kuonya kuwa, katika sheria ya haki na wajibu wa wabunge, kipo kipengele kinachosema kuwa nyaraka ambazo ni za siri za serikali, haziruhusiwi kujadiliwa bungeni isipokuwa kwa kibali cha maandishi cha rais.

“Najua wabunge wanajua kuwa wana kinga humu ndani, lakini ukikamatwa huko nje na nyaraka hizo shauri yako,” alisema Makinda.

Siku moja baada ya Makinda, kutoa onyo hilo, Dk. Slaa alieleza msimamo wake kuwa yupo tayari kukamatwa na kufungwa gerezani kwa kutumia nyaraka ambazo serikali inasema kuwa za siri, lakini zinazoficha ubadhirifu, wizi na hujuma dhidi ya Watanzania.

Dk. Slaa alieleza msimamo wake huo Ijumaa wakati Bunge lilipokaa kama kamati kupitia bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, alipohoji kauli ya Waziri Marmo baada ya kushindwa Alhamisi kwa kubanwa na kanuni.

Dk. Slaa alimuhoji Marmo kuwa kinachoitwa siri za serikali kina mipaka gani? Alibainisha kuwa zipo nyaraka zinaonyesha kuwepo kwa ubadhirifu wa mali ya umma, na kusisitiza kuwa yeye hawezi kuzihesabu nyaraka hizo kuwa za siri.

Alisema kuzifanya nyaraka za aina hiyo kuwa siri za serikali, ni kuendelea kuficha maovu, jambo ambalo ni kinyume cha utawala bora ambao serikali inapaswa kuusisitiza na kuusimamia.

“Hivi kweli Marmo anataka kama kuna nyaraka za wizi na ubadhirifu tufiche? Wizi na ubadhirifu hauwezi kufichwa kwa siri za serikali,” alisema Dk. Slaa.

Aidha, mbunge huyo ambaye ni maarufu kwa kuibua kashfa kadhaa dhidi ya viongozi wa serikali, alikiri kuwa yeye anazo hizo zinazoitwa nyaraka za siri, na baadhi yake amezikabidhi kwa Marmo.

Alisema kuwa ataendelea kuzitafuta nyaraka hizo kwa njia anazozifahamu yeye, kwa sababu jitihada zake za kuzitafuta kwa njia halali zimeshindwa.

Aliitaka serikali isiendelee kujidanganya kuwa inaweza kuficha kila kitu katika dunia ya sasa, kwani wapo Watanzania wazalendo walio tayari kutoa msaada unaohitajika ili kuhakikisha kuwa mambo mabaya serikalini yanafichuliwa.

Akitoa mfano, Dk. Slaa alisema kuwa alifanikiwa kupata nakala ya kikao cha Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Kuu, kilichofanyika mapema mwezi huu, ambayo alilazimika kuitafuta kwa kutumia mbinu zake baada ya kubaini kuwa timu ya kuchunguza upotevu wa fedha kupitia Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), iliyoundwa na Rais Kikwete alipaswa kuona taarifa ya kikao hicho, lakini nyaraka hiyo haikukabidhibwa katika timu hiyo, licha ya kikao hicho kuzungumzia masuala hayo hayo.

Marmo alikiri kupokea baadhi ya nyaraka za siri za serikali kutoka kwa Dk. Slaa ikiwemo hiyo ya taarifa ya kikao cha Bodi ya Wakurugenzi wa BoT, lakini alisema mwanasiasa huyo ni mjanja sana kwa sababu amemkabidhi akiwa ameondoa sehemu zote zinazoweza kuonyesha mahala nyaraka hiyo ilikotokea.

“Amemwandikia aliyempelekea nyaraka hii kuwa ‘Nimeondoa jina la source (chanzo), ili kuwalinda maofisa wetu’…ina maana hawa wenzetu wana maofisa wao ndani ya serikali!”

Akizungumzia suala hilo baadaye, Makinda alisema katika mfumo wa vyama vingi, kuna kamati tatu zinaongozwa na wapinzani makusudi kwa ajili ya kuhakikisha ufuatiliaji mpana zaidi kwa masuala yanayofanywa na serikali.

Hata hivyo, alisema kuwa kuna taratibu za kufuatwa iwapo mbunge atataka kupatiwa nyaraka za serikali, lakini inaonekana kuna matatizo ndani ya serikali, na kwamba suala hilo halipaswi kuifanya serikali kuanza kuwatisha watu.
 
Sasa wanatibu nini hawa SIRIKALI? Wajaribu tu kumkamata, ndo itakuwa mwisho wa CHICHIEM
 
Kumbe wizi na UFISADI ni nyara za serikali?

Kumbe watu wanapotwambia kuwa tuwapelekee tarifa za uhalifu wanakuwa na maana gani?

Basi mwaka huu tutajua mengi.
 
Kuna haja ya kumtafutia INTERNET huyu Dr kama hana. Akifika Bungeni ana-DOWNLOAD hizo habari na akimaliza Bunge anazifuta na hapo hakuna ushahidi tena kuwa alikuwa na NYARAKA za KIFISADI za serikali. Hizi zinaweza kuwa hata JF ili wengi tufaidi :).
 
Why are people not ashamed of the things they do? Kuna vitu vingine hata kabla sijafungua mdomo wangu au kutenda najiuliza jamii itanifikiriaje? Mtu anasema uongo mtupu, mtu anasifia madhambi na huku wengine wanampigia makofi lakini haoni hata aibu nafanaya hivyo kila siku ijayo kwa Mungu. Dhamira haziwasuti au ndio tuseme hawana dhamira.
 
Huyu Slaa ajiandae kukamatwa tu kwa kuwa na nyaraka za siri za serikali. Unajua kuna watu wanadhani kuwa serikali imelala kumbe hawajui kuwa Mheshimiwa Kikwete anawatafutia tu muda maalumu wa kuwakamata kwa kuwa na nyaraka za siri za taifa na kuingilia mambo ya usalama wa taifa.

Subirini tu
 
Huyu Slaa ajiandae kukamatwa tu kwa kuwa na nyaraka za siri za serikali. Unajua kuna watu wanadhani kuwa serikali imelala kumbe hawajui kuwa Mheshimiwa Kikwete anawatafutia tu muda maalumu wa kuwakamata kwa kuwa na nyaraka za siri za taifa na kuingilia mambo ya usalama wa taifa.

Hatuna usalama wa Taifa tuna usalama wa ikulu tu kwa mtazamo wangu. 1. Kama Usalama wa taifa ungekuwepo tusingehangaika kuunda Tume kila kukicha kwaajili ya kufanya uchunguzi? 2. Hiyo mikataba mibovu na document za kufoji wizi kama wa EPA ndio unaita siri za serikali??
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom