DJ wa Uswazi ndani ya harusi ya kishua

Mar 4, 2015
13
12
Dahh nimeamka kichwa kinagonga, masikio yameziba halafu nimekasirika sana. Na wala sio malaria inayonisumbua, tatizo limetokana na ishu ya kupeana tenda kirafiki bila kupimana ujuzi. Unajua kila kazi ina ujuzi wake, usidhani kwa kuwa kila anaejua kupaka rangi kuta za nyumba ni mchoraji, ukataka kumpa tenda ya kuchora mabango, kitakachotokea ni kichekesho kitupu. Haya mambo ya kupeana tenda kirafiki yanaleta hasara sana, na ndio maana nimeamka naumwa leo.

Ishu nzima ilikuwa hivi. Tulikuwa kwenye kamati ya harusi ya jamaa yetu fulani tunapanga hiki na kile, ukumbi uwe wapi, usafiri na kila kipengele cha sherehe. Hatimae kila kitu kilikuwa katika maandishi na kulipiwa, mwanakamati mmoja akaomba aachiwe kipengele cha MC na muziki, akatuambia kuna jamaa yake ni bonge ya MC na pia ana muziki mnene, na bei yake ndogo, watu wakapiga makofi na kumruhusu aje nae.

Hakika tulipoingia kwenye ukumbi jana tukakuta maspika makubwa yamepangwa, MC tukamkuta kashavaa suti yake safi, tukajua mambo yatakuwa mswano.
Muda ulipofika tukaomba muziki taratibu uanze, muziki ukaanza, ukumbi ulikuwa bado mtupu, lakini muziki ukaanza kwa kelele sana, ikalazimu mwanakamati mmoja amuombe DJ kupunguza, Dj akapunguza kidogo tu, kelele bado ikawa juu.

Akafwata MC ili amtaarifu DJ apunguze sauti, haikusaidia. Wageni waliokuwa wamewasili kidogo walionekana kutokuwa na raha kukaa ukumbini kwani ilikuwa kelele tupu. Baada ya kubembelezana sana hatimae DJ akaombwa azime kwanza muziki. Mwanakamati aliyekuwa akishughulikia muziki akaitwa kando tukaanza kumhoji kuhusu DJ wake? Tukagundua kuwa kumbe ni DJ wa Uswazi, DJ wa Uswazi sifa yake ni kufungulia muziki kwa nguvu, ila hata mtaa wa tatu wajue ana maspika yenye nguvu.

DJ wa Uswazi ukitaka apunguze sauti kesi mpaka ifike kwa mjumbe kwanza au aiitiwe polisi. DJ wa Uswazi ukimleta kwenye harusi au hafla kwenye ukumbi, unamchanganya maana huwa hajui muziki gani upigwe saa ngapi, na yeye kazoea kupanga spika barabarani na kutwanga wimbo anaotaka yeye na masela wenzie. Na DJ wa Uswazi saa yoyote ukimuona kaenda chooni ujue kaenda kuongeza stim akirudi anaona kama spika hazilii anaongeza sauti.

Basi harusi ya jana tulikumbana na DJ wa Uswazi masikio bado yameziba…
 
Duh pole muungwana, hilo jipu mmechelewa kulitumbua, angalau mulisafishe wakati wa kuvunja kamati.
 
Back
Top Bottom