Dar: Apotea siku 41 familia ikidai Polisi walimchukua na kumpeleka kusikojulikana

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,377
8,121
Wakati familia ya Fred Ngoti (46) ikidai ndugu yao alitoweka baada ya kuchukuliwa na Jeshi la Polisi, lenyewe limejibu si kila anayepotea huwa limemkamata.

Inadaiwa Fred alitoweka tangu Julai 20, mwaka huu baada ya kupigiwa simu na rafiki yake aliyemtaka wakutane Vingunguti, Dar es Salaam kwa ajili ya kazi.

Hata hivyo, rafiki huyo, Abdallah Haji alisema alilazimishwa kufanya hivyo na watu waliomkamata na kujitambulisha kwake kuwa ni askari polisi.

“Walitoa vitambulisho vyao, walikuwa wako sita na kunilazimisha kutoa neno la siri kwenye simu yangu na kuingiza namba za simu walizokuwa nazo ambazo zilitokea jina la Gaspar,” alisema Haji.

Akizungumza na Mwananchi jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alisema sio kila anayekamatwa na anayetoweka huwa amekamatwa na polisi.

Alisema hawezi kulizungumzia zaidi suala la Fred kwa simu na alimtaka mwandishi aende ofisini kwake.

Mwandishi alipomjibu kuwa anakwenda ofisini, Kamanda Muliro alisema hana muda yuko kwenye majukumu mengine, atafutwe leo.

Simulizi ya tukio

Akizungumza ukaribu wake na Fred, ambaye wao wamezoea kumuita Gaspar, rafiki yake huyo (Haji) alisema amefahamiana naye kwenye ufundi wa magari.

Alisema yeye alikuwa akipeleka magari kwenye gereji ya Fred iliyopo Tabata Barakuda.

“Mimi ni fundi magari, ofisi yangu ipo Kisutu lakini naishi Tabata, Gaspar (Fred) ana gereji yake Barakuda, hivyo nikiwa na kazi ya kupaka rangi gari, nampelekea,” alisema Haji.

Alisema Julai 20, mwaka huu alipigiwa simu kwa namba ngeni, mpigaji akitaka Haji akamtengenezee gari lake Tabata.

Alifafanua kwa kuwa alikuwa ameshatoka nyumbani, alimjibu hawezi kwenda muda ule kwa sababu alikuwa ameshafika mjini, akamuomba aende ofisini kwake.

“Saa saba mchana akanipigia tena akasema amefika kwenye viwanja vya Jakaya Kikwete (Mnazi Mmoja), gari imemzimikia nisogee pale, nikachukua spana na kijana wangu mmoja tukaenda eneo alilonielekeza alipokuwa kaliegesha gari hilo,” alisimulia.

Alisema muda mfupi baadaye wakajikuta wamezungukwa na watu sita wakiwaambia wako chini ya ulinzi.

Alisema watu hao waliokuwa wamevaa kiraia, waliwanyang'anya simu na walipowataka watu hao wawaonyeshe vitambulisho kama ni polisi, waliwaonyesha.

“Baada ya muda ikaja Noah nyeusi tukasukumwa kuingia ndani kisha wakaondoka huku magari yote yakiwa yameongozana.

“Yale magari yalielekea karibu na kituo cha Polisi Mchicha (TAZARA) yakaegeshwa kando ya barabara kwenye miti, mimi na yule kijana wangu tukatenganishwa magari, mimi nikabaki na askari mmoja na mwenzangu akaenda kwenye gari lingine na askari mmoja, wengine wakashuka chini wakawa kama wanajadili jambo.

“Waliporudi wakaniambia hawana shida na mimi, lakini kuna mtu naongea naye kwenye simu yangu mara kwa mara ndiyo wanamtaka, wakanipa simu yangu nitoe namba ya siri, nikatii kisha mmoja akaingiza namba alizokuwa nazo, likatokea jina la Gaspar (Fred), wakasema wao wanamtaka huyo mtu,” alisema.

Alisema aliwaambia huyo ni rafiki yake hata siku hiyo (Julai 20) waliwasiliana mara mbili, yuko ofisini kwake Barakuda, wakamwambia huko hawaendi bali ampigie simu na amwambie aende Vingunguti.

"Wakati huo tulishatoka Mchicha, lile gari limesogea hadi nyuma ya kiwanda cha Pepsi ikawa imepaki, nikampigia Gaspar ambaye siku zote nikimpigia anakuja kwa sababu nafanya naye kazi nyingi za magari.

"Kweli baada ya muda alifika, naye akakamatwa tukaunganishwa wote, tukapelekwa hadi maeneo ya Uwanja wa Ndege tukabadilishiwa magari, Gaspar akaingia kwenye Premio, mimi nikabaki kwenye Noah na yule kijana wangu akahamishiwa nilipokuwa mimi.

"Gari alilopandishwa Gaspar likarudi kwenye mataa, sisi tukaingia njia za ndani kwa ndani tukafika sehemu wakapaki kama nusu saa, kisha tukaja kutokea njia ya Maghorofani (Temeke).

"Wale watu hawakunisemesha kitu tangu baada ya Gaspar (Fred) kukamatwa, walikaa na mimi na kijana wangu hadi saa 11 jioni ndipo tukatoka Maghorofani, tukasogea hadi TAZARA darajani wakapaki.

“Tukiwa pale wakatuuliza majina yetu, namba za simu, umri, kazi na tunapoishi.

"Tulipowajibu wakasema wanaelekea Arusha, watushushe wapi? Nikawaambia Buguruni, hatukujua gari aliyopanda Gaspar ilielekea wapi,” alisimulia Haji.

MWANANCHI
 
Mwizi wa magari au mnunuzi wa magari.

Naipongeza serikali, wampoteze yeye na mtandao wake.


Wezi wanaogopa risasi na moto pekee.
 
Back
Top Bottom