abdulahsaf
JF-Expert Member
- Aug 31, 2010
- 858
- 130
Na Oscar Samba, AJTC
WAKAAZI wa Muyuni wilaya ya Kusini Unguja wamesema kuwa ni vyema katiba mpya ya Tanzania ikaainisha uwepo wa serikali tatu ili kuondokana na kero za Muungano zilizopo hivi sasa.
Wananchi hao walieleza hao jana huko Muyuni, wakati kamati ndogo ya Tume ya kukusanya maoni ya katiba mpya ilipofika kijijini hapo.
Walisema kuwa kumekuwepo na kero nyingi za Muungano ambazo zimekuwa kilalamikiwa na kila upande, hivyo uwepo wa serikali tatu itazifanya kero hizo ziwe historia kwani kila upande utashughulikia mambo yake na yale ya Muungano kushughulikiwa na serikali hiyo.
Kwa upande wake Pandu Issa Pandu alipendekeza uwepo wa serikali tatu ikiwemo kurudi kwa serikali ya Tanganyika, Zanzibar na serikali ya Muungano ambayo itakuwa ndio msimamizi mkubwa wa Serikali zote mbili.
''Ninapendekeza tuwe na serikali tatu yaani ya serikali ya Tanganyika, Zanzibar na Serikali ya Muungano ambayo itakuwa ndio msimamizi wa serikali zote mbili na hizo mbili ziwe huru na zijitegemee kwenye mambo yake ya ndani'', alisema Pandu Issa Pandu (43).
Kero za Muungano zimekuja na kuongezeka siku hadi siku kutokana na kutoweka kwa Serekali ya Tanganyika yenye kusimamia mambo yake yasio ya Muungano.
Aidha ambali ya kujitokeza maoni hayo pia wapo wananchi wa shehia hiyo waliopendekeza Rais wa Zanzibar awe na madaraka kamili kuliko ilivyo hivi sasa.
Walisema mfumo uliopo hivi sasa unafanya kuonekana Tanzania kuwe na rais mdogo na rais mkubwa, hivyo Rais wa Zanzibar apewe mamlaka kamili.
Wananchi hao pia walitaka mfumo wa mambo ya nje ubadilike utoe nafasi kwa Zanzibar nayo kutambulikana nje, hali inayoifanya kuweza kunufaika zaidi kuliko ilivyo hivi sasa.
Naye Mwalimu Shukuru Ramadhani (28), akitoa maoni yake alisema suala la elimu ya juu lifutwe kwenye mambo ya Muungano kwani Zanzibar hainufaiki nalo.
''Tunataka suali la elimu ya juu lisiwe la Muungano na wizara ya Elimu ya Zanzibar iwe na Baraza lake la Mitihani, kwani tunahisi hatutendewi haki na Baraza la Elimu juu liliopo hivi sasa la Muungano'', alisema Mwalimu Shukuru Ramadhan.
Suali la elimu ya juu pia lilichangiwa na wanafunzi wa skuli ya Muyuni ambapo walitaka suala la elimu lienguliwe kwenye mambo ya Muungano, huku wakieleza kuwa NECTA inawadhulimu.