Elias Msuya
Senior Member
- Dec 23, 2011
- 173
- 671
Chama Cha Wananchi (CUF) kimesisitiza kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka huu, huku kikiwaalika makada wa Chadema waliounda kundi la G-55, kujiunga nao ili wagombee kupitia chama hicho.
G55 linahusisha makada wa Chadema waliotoa waraka wakiushauri uongozi wa Chadema kushiriki uchaguzi licha ya kuwepo kwa kampeni ya kutaka mabadiliko kabla ya uchaguzi maarufu No Reforms No Election.
Soma kuhusu G-55
Kupitia kampeni hiyo, Chadema wamesema hawatasusa uchaguzi ila watazuia usifanyike, jambo linalopingwa na G-55.
Taarifa iliyotolewa leo Aprili 21 na Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma wa chama hicho, Mohamed Ngulangwa imewaalika wananchi kujiunga na chama hicho ili kishiriki uchaguzi.
"Kwa uzito wa kipekee, tunatoa wito kwa wanachama wa Chadema hususan wale wa G-55 na wengine wanaoamini kwamba kushiriki Uchaguzi ni bora kuliko kususia, waje CUF- Chama Cha Wananchi ili tuendeleze mapambano," amesema Ngulangwa.
Ngulangwa amesema chama hicho kitashiriki uchaguzi huo licha ya kutambua upungufu wa kisheria na kikatiba katika Tume Huru ya Uchaguzi licha ya kufanyika mabadiliko madogo waliyosema yanayofanana na kuibadilishia chupa juisi iliyoharibika.
"Tumefanya tafakuri ya kina na kubaini kwamba yale mapambano ambayo vyama vya upinzani viliyafanya vikiwa ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano na Baraza la Wawakilishi yalikuwa na tija kubwa zaidi kwa taifa kuliko tulipobaki nje.
"Hivyo, msimamo wetu mpaka sasa ni wa Kushiriki Uchaguzi Mkuu wa 2025 na kulinda kura zetu kwa jasho na damu, ikilazimu.
"Tunaendelea kujiandaa kuukabili Uchaguzi kwa mazingira yaliyopo huku tukiendelea kutoa wito kwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kukaa chini na vyama vya Siasa kuangalia namna ya kuhakikisha Uchaguzi Mkuu unakuwa huru na wa haki, kama njia pekee ya uhakika ya kulinusuru Taifa kuingia kwenye machafuko likiwa mikononi mwake," amesema Ngulangwa.
Hata hivyo, amesema wanachama wao wenye nia ya kugombea urais, ubunge na udiwani katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, watalazimika kusubiri kalenda itakayotolewa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa (BKUT) litakaloketi hivi karibuni.
"CUF ni Taasisi inayoongozwa na Vyombo Mahususi vya Kikatiba. Baraza Kuu la Uongozi la Taifa (BKUT) kwenye Kikao kijacho kinatarajiwa kuweka Kalenda na Utaratibu mzima wa kuwapata wagombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano; Urais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar; Ubunge; Uwakilishi na Udiwani," amesema.