Corona ni nani?

Mohamed Ismail

JF-Expert Member
Mar 16, 2014
214
229
CORONA NI NANI?
___________________
Corona wewe ni nani?
Corona umetoka wapi?
Una sura gani?

Mlimwengu mimi siwezi kukaa kimya juu yako. Mara ya kwanza tuliposikia jina lako kila mtu alitamani kukujua wewe ni nani?, lakini kadri zilivyosonga tukaijua rangi yako halisi tukaona unamsaidia kazi Ibilisi ya kupunguza ndugu zetu. Tukahisi umezaliwa Wuhan China ila tukaamini na umauti utakukutia hapo.

Ukatutengenezea uadui na ndugu zetu walioko huko wakaamini hatuwapendi kumbe tunaogopa kusambaza uzao wako nchini mwetu.

Mataifa mengi yakatangaza kuwa hawahitaji wageni kwa ajili yako wengine ikafikia hatua ya kurushiana mpira juu ya ujio wako. Ile ya karibu mgeni mwenyeji apone sasahivi imebaki kuwa nadharia tu.

Ulivyo na roho mbaya ukawapoteza ndugu zetu wa china ukaona usiishie hapo ukajipenyeza penyeza kwenye vyombo vya usafiri na kuyafikia mataifa mbalimbali.

Mara Paap ukaja kwenye nchi yangu mama Tanzania nchi ya amani na upendo. Ukatujengea taharuki uzuri ukakuta taifa letu tuna baba anayejiamini akatupa nguvu na kutuaminisha kuwa tukimtanguliza Mungu pamoja na tahadhari ya kutosha hutaweza kudumu tutakusahau kama tulivyosahau habari ya nzige na utajiri wa Dr Shika.

Tunasikia kila siku unavyotenganisha viwiliwili na roho za watu kwa huko Italy, Spain, France na nchi nyingine lakini tunaamini hili ni funzo kwetu. Tulizoea watu wa Marekani wasaidie mambo kama haya ila na wao wanapambania kuendelea kuivuta oksijeni.

Umesababisha kuturudisha enzi za utumwa watu wanapigwa viboko matakoni kisa wewe, tuliona picha hizo kwenye vitabu vya kihistoria leo tunaangalia kwenye Tecno zetu. Achana na habari za mvua na jua bora nini ? Sasa hivi ajenda ni njaa na corona bora nini?

Corona wewe ni muuaji kama wauuaji wengine, wewe ni laana kama laana nyingine, wewe ni janga kama majanga mengine na hufai kuchekewa na mtu yeyote mwenye kujipenda na kuipenda nchi yake. Na jua kwamba hakuna jambo linaloshindikana chini ya hili jua walikuja ebola, kipindupindu, ukimwi na wengine wakaondoka na kutulia tuli kama maji mtungini.

Jamani ndugu zangu tusidharau vitu vidogovidogo tuendelee kusikiliza kwa umakini maelekezo tunayopewa na taasisi husika dhidi ya kudhibiti huyu corona. Miluzi mingi humpoteza mbwa maana najua huko kwetu kila mtu huwa ni mjuaji. Wazungu wanasema prevention is better than cure.

Leo ni weekend najua walimwengu wengine imeisha kinyonge maana tulitegemea tuwe na wenza ila tunaiepuka corona. Tutumie tu mitandao vizuri kujielimisha na kuchambua taarifa nzuri. Serikali yetu iko makini lakini na sisi ni sehemu ya serikali hivyo inabidi tusiiangushe serikali yetu. Na nyie roho mbaya haijengi kujifanya kupandisha gharama za vifaa vya kinga dhidi ya corona. Je, mnapandisha mnapata faida kubwa na sisi tunakufa na nyie mnakufa mtakuwa mmefanya nini? Huu ni muda ambao inabidi tushikane mikono na tuongozwe na upendo wa hali ya juu.

Mlimwengu mimi kwa leo naishia hapa. Tuzidi tu kulikemea hili pepo chafu kama mapepo mengine tu.

#mlimwengumimi

30/03/2020
 
Back
Top Bottom