SEHEMU YA 21
ILIPOISHIA:
“Yaani hela za jana bado hazijalipwa wala samaki hawajachukuliwa, na wewe leo unaambiwa hayo mambo unayakubali! Kwani wewe na mamaako mdogo mna njama gani? Mnataka kuniangusha mtaji si ndiyo?” alisema baba mdogo tukiwa tumesimama nje ya geti huku akionesha kuwa na jazba kubwa ndani yamoyo wake.
“Lakini bamdogo?”
“Lakini nini? Unafikiri sijui mnachokifanya si ndiyo?” alisema kauli iliyosababisha mapigo ya moyo wangu yalipuke na kuanza kunienda mbio kuliko kawaida.
SASA ENDELEA...
Akili ya haraka ilinituma kuamini kwamba kumbe baba mdogo anajua mchezo wote tunaoufanya na mkewe, nikawa natetemeka kwa sababu sasa nilijua za mwizi zimetimia, kama baba mdogo alikuwa anajua kwamba nilikuwa nikitia mkono kwenye kapu lake, unafikiria anaweza kuchagua adhabu gani inayonifaa? Nilijikuta nikitetemeka.
“Najua kila kitu Chande, huwezi kunizidi akili wala huyo mama mdogo wako hawezi kunizidi akili. Siku zote huwa nakwambia kwamba wanawake siyo rafiki zetu wa kudumu, umeshindwa kusimamia kazi iliyokuleta kutoka kijijini na sasa umeanza kushiriki kunihujumu.
“Jana samaki wote mmewaweka kwenye friji, leo pia unakubali kurudia makosa yaleyale, unafikiri mtaji ukianguka utabaki hapa mjini kufanya nini? Itabidi urudi kijijini, huwa sifugi mbwa asiyewinda mimi,” alisema baba mdogo kwa jazba, kidogo nikaanza kupata amani ndani ya moyo wangu kwamba kumbe alichokuwa anakijua ni kwamba tulikuwa tukishirikiana kumhujumu na siyo kwamba nafaidi kilicho halali yake.
“Mimi na wewe tunahitaji kuzungumza kwa kina baadaye, nitakuita,” alisema huku akigeuka na kuondoka, nikashusha pumzi ndefu na kujiinamia. Ilikuwa ni siku ya mkosi kwangu.
Niliingia chumbani kwangu na kujifungia mlango, nikavua nguo zote na kujilaza kitandani, nikawa naendelea kutafakari mambo yote yaliyotokea siku hiyo. Nilimtafakari Mimah, nikakosa majibu kabisa juu yake.
“Kumbe ni mke wa mtu? Kwa nini aliamua kunichuuza kiasi hicho? Au pengine ndiyo maana aliamua kukaa kimya kwa sababu alikuwa anajua mumewe anarudi?”
Nilimfikiria pia yule mpangaji, nikawa najiuliza kama nilichokuwa nakihisi awali ni kweli, kwamba baba mdogo anajua kwamba namlia mali zake, nani anaweza kuwa amemtonya kama siyo yeye?
Nilirudisha mawazo yangu na kuanza kumfikiria ma’mdogo! Nikakosa majibu. Kutokana na uchovu niliokuwa nao, nilijikuta nikipitiwa na usingizi mzito pale kitandani. Kisimu changu kilichokuwa kinaita mfululizo ndicho kilichokuja kunizindua, alikuwa ni mama mdogo.
“Uko wapi?”
“Nipo ndani nimelala.”
“Kimenuka mume wangu.”
“Usiniite hivyo mam’dogo, anaweza kusikia ikawa tatizo zaidi.”
“Ametoka! Vipi kwani amekwambia nini?”
“Ameniambia kwamba anajua kila kitu kinachoendelea kati yangu na yako, kwani amejua?”
“Hahaaaa,” mamdogo alicheka kwa sauti, nikawa sijaelewa kicheko chake kinamaanisha nini.
“Unacheka? Hujui anaweza hata kunichinja?”
‘Siyo hivyo unavyofikiria. Ananilaumu kwamba eti mimi nakufundisha wewe usimtii, mimi na wewe tuna njama za kumuulia mtaji wake. Wala hajui kwamba wewe ni mume mwenzie.”
“Mbona ameniambia anajua kila kitu? Na amesema baadaye anataka tuzungumze?”
“Wala usiogope! Niachie mimi kila kitu.”
“Kwa hiyo akiniuliza nimwambieje? Mimi naona bora nikiri makosa tu na kumuomba msamaha!”
“Wee! Wee! Atatuchinja wote! Hajui chochote na hata hapa kabla hajaondoka nimemtuliza kidogo, anachojua ni kwamba njama zetu ni kumuangusha mtaji wake, basi!”
“Kwa hiyo tutafanyaje sasa?”
“Inabidi hawa samaki tuwakusanye kesho tukatoe msaada kwenye kituo chochote cha watoto yatima kwa sababu akiwaona hapa ndani ndiyo anachanganyikiwa. Nimemdanganya kwamba waliokuwa wametuagiza wamesogeza mbele sherehe yao lakini kesho watatulipa fedha zote.”
“Sasa tutapata wapi hela za kurudishia? Au unaonaje mimi nikiingia mtaani na kuanza kuwauza? Najua leo na kesho tu watakuwa wameisha.”
“Huna haja ya kuteseka mume wangu, kesho kuna hela ya vicoba nitaenda kuchukua halafu tutamdanganya kwamba wametulipa. Wewe tulia kabisa, kazi yote niachie mimi,” alisema mamdogo huku akiongea kwa kujiamini, akakata simu.
Kidogo roho yangu ilitulia, hata hivyo ndani ya moyo wangu nikajiambia kwamba mchezo niliokuwa naucheza ulikuwa wa hatari sana na unaweza kusababisha mtafaruku mkubwa sana siku akigundua kilichokuwa kinaendelea kati yangu na mkewe! Mke anauma bwana.
Nilichoamua ndani ya moyo wangu, ilikuwa ni kuanza kumkwepa mamdogo na kupunguza ukaribu kati yetu kwa sababu tulikuwa tunaelekea sehemu mbaya. Nikawa najiuliza kwamba hata nikisema nipunguze ukaribu na ma’mdogo, nitapata wapi tena pa kutulizia machungu yangu wakati Mimah tayari alikuwa ameshanichuuza?
Wakati nikiendelea kutafakari mambo mengi, ndipo nilipomkumbuka mtu muhimu sana ambaye alishaonesha kama ananielewa hivi, ambaye angeweza kuziba vizuri pengo la Mimah na ma’mdogo.
“Mambo!”
“Poa!”
“Mzima?”
“Mzima ndiyo, nani mwenzangu?”
“Mi Chande bwana, yule muuza samaki uliyekutana naye kwenye daladala.”
“Mh! Yaani wewe? Mpaka nikajilaumu kwa nini sikuchukua namba yako siku ile. Ndiyo nini unachukua namba halafu hata hunipigii?”
“Nisamehe bure mwaya, nilikuwa nimesahau jinsi nilivyokusevu kwenye simu yangu. Vipi naweza kukuona?”
“Umeanza hivyo muuza samaki! Unataka kuniona mimi ili iweje?”
“Tulia mrembo, mambo mazuri hayataki haraka,” nilimjibu kwenye meseji, huku moyoni nikianza kuchekelea kwa sababu ilishaonesha kwamba kazi inaweza kuwa nyepesi zaidi ya kumsukuma mlevi.
“Kwani kesho si unaenda Feri?”
“Mh! Sina uhakika sana, kwani kazini unatoka saa ngapi?”
“Kesho siendi kazini, nitapumzika nyumbani nifanyefanye usafi.”
“Nielekeze basi nikufuate unakoishi?”
“Akuu! Kwangu huwa hawaingii wanaume, unataka kuja kunifanya nini?” ilisomeka meseji yake, nikaona kama ananizingua, nikaamua kumpigia kabisa huku ‘mkuu wa kaya’ akiwa ameshaanza kusisimka kutokana na majibu yake ya kichokozi.
Je, nini kitafuatia?
Sent using
Jamii Forums mobile app