Cheka, Simulia, Lakini Usiombe Yakukute - 32
“Bwana Samsa,” alimuita baba yule mpangaji wa kati, na kuonyesha kwa kidole chake cha shahada, bila kutamka neno lingine, kumwelekea Grego wakati akijongea mbele polepole.
Zumari lilinyamaa kimya.
Mpangaji wa kati alitabasamu, kwanza akitikisa kichwa chake kwanza kwa rafiki zake, na kisha akimwangalia Grego kwa mara nyingine tena.
Kuliko kumswaga Grego arudi alikotoka, baba alionekana kuona ni la umuhimu mkubwa kuwatuliza wapangaji, japokuwa hawakuwa wamekasirika hata kidogo na Grego alionekana kuwaburudisha zaidi kuliko zumari lililokuwa likipigwa.
Baba aliharakia kuwafuata na kwa mikono iliyonyooshwa akijaribu kuwasukumia chumbani kwao na kwa wakati huohuo kuwazuia kwa kutumia mwili wake wasiendelee kumuona Grego.
Ndipo kwa wakati huu walipokuwa haswa kiaina wamechukizwa, japokuwa mtu hangeweza tena kujua iwapo ilikuwa ni kutokana na aliyoyafanya baba au kutokana na kutambua kwamba walishakuwa, bila kufahamu, na jirani kama Grego.
Walitaka maelezo kutoka kwa baba yake, wakiinua mikono wakati wakisema hayo, walishika ndevu zao kwa hasira, na kwenda polepole kuelekea chumbani kwao.
Wakati huohuo, ule upweke uliomkuta dada baada ya tumbuizo kukatizwa ghafla lilimuelemea sana.
Aliendelea kulishikilia zumari na upinde wa kulipigia kwenye mikono yake iliyolegea kwa muda tu na aliendelea kutizama karatasi ya muziki kama vile ambaye alikuwa akiendelea kupiga zumari.
Kwa mara moja alijitutumua, akaweka chombo cha muziki kwenye mikono ya mama yake (mama alikuwa akali akiketi kwenye kiti chake akivuta pumzi kwa taabu na mapafu yake yakimnyima ushirikiano) na ikambidi kukimbilia chumba jirani, ambacho wapangaji, wakishinikizwa na baba, walikuwa tayari wakizidi kukikaribia.
Mtu angeweza kuona namna chini ya mikono zoefu ya dada mashuka na mito kwenye vitanda ilivyo juu na kupangiliwa vilivyo.
Hata kabla ya wapangaji kufikia chumbani, alikuwa tayari amemaliza kuviandaa vitanda na alikuwa akichomoka mle chumbani.
Baba alionekana amezidiwa sana kwa mara nyingine na ubishi wake mpaka akasahau kuhusu heshima ambayo siku zote aliwapa wapangaji wake. Aliwasukuma zaidi na zaidi, mpaka mlangoni mwa chumba chao yule jamaa wa kati alikanyaga sakafu kwa sauti kubwa na hivyo kumfanya baba asiendelee kwenda.
“Natamka haya kama ifuatavyo,” alisema mpangaji wa kati, akiinua mkono wake na kuwatizama kwa chati wote wawili mama na dada, “kwamba kwa kuzingatia mazingira ya kutia kinyaa yaliyoko kwenye nyumba hii na kwenye familia,” hapo alitema mate kwa kukusudia sakafuni, “Nasitisha kuwa mpangaji. Ni wazi, sitalipa chochote kwa siku zile ambazo nimekaa hapa; kinyume chake nitatafakari iwapo nichukue hatua fulani dhidi yenu au la, kitu ambacho -- mniamini -- kitakuwa chepesi sana kukitekeleza.”
Alikaa kimya na kuangalia mbele yake moja kwa moja, kama vile aliyekuwa akingojea kitu.
Hakika, rafiki zake wawili mara hiyohiyo walijiunga kutoa maoni yao,
“Nasi pia tunatoa notisi mara moja.”
Hapo alishika kitasa cha mlango, akaubamiza mlango kuufunga, na kufunga kwa funguo.
Baba alipapasa njia yake akitetemeka kwenda kwenye kiti chake na akajiachia aangukiemo.
Ilionekana ni kama vile alikuwa akijinyoosha kwa usingizi wake wa kawaida jioni, lakini kutikisa kichwa kulikokithiri (ambacho kilionekana ni kama kimekosa udhibiti) kulidhihirisha hakuwa analala aslan.
Grego alikuwa amejilaza bila kujongea muda wote huo palepale alipokuwa wakati wapangaji walipombaini. Kukatishwa tamaa kutokana na kuharibika kwa mpango wake na pengine pia udhaifu wake uliotokana na njaa yake kali vilifanya isiwezekane kwa yeye kujongea. Alikuwa na hakika kwamba zahma kubwa itamshukia muda wowote na aliisubiri.
Wala hata hakustushwa pale zumari lilipodondoka toka mikononi mwa mama yake, likiachiwa na vidole vya mama vilivyokuwa vikitetemeka, na kutoa mlio uliokuwa ukiakisiwa kuwa mwangwi.
“Wazazi wangu wapendwa,” dada alisema huku akigonga meza kwa mkono wake kama namna ya utambulisho, “mambo hayawezi kuendelea zaidi namna hii. Pengine kama hamtambui hayo, sawa, mimi natambua. Sitatamka jina la kaka yangu mbele ya dubwasha hili, na hivyo nasema kilichobakia ni kwamba lazima tujaribu kuliondolea mbali. Tumejaribu kadiri inavyowezekana kibinadamu kulihudumia na kuwa watulivu. Naamini hakuna atakayetushutumu hata kidogo.”
“Yuko sahihi kwa njia alfu moja,” baba alijiambia mwenyewe.
Mama, ambaye bado hakuwa anaweza kuvuta pumzi sawasawa, alianza kukohoa kimyakimya huku mkono wake umewekwa kinywani na macho yamemtoka pima.
Dada alimkimbilia mama na kulishika paji lake la uso.
Maneno ya dada yalionekana kumpelekea baba kuwa na tafakari fulani.
Alikaa sawa, akichezea kofia yake ya ofisini kwenye sahani, ambazo bado zilikuwapo mezani baada ya mlo wa jioni wa wapangaji, na mara hii au ile alimtizama Grego aliyekuwa ametulia tuli.
“Lazima tujitahidi kuliondoa hili,” dada sasa alimwambia baba kwa hakika, kwa vile mama, katika kukohoa kwake huku, hakuweza kusikiliza chochote,”linawaua wote wawili. Naona kifo kinavyowajia. Wakati watu inabidi kufanya kazi kwa bidii namna hii tufanyayo, hawawezi kustahamili pia mateso ya namna hii yasiyoisha nyumbani. Siwezi kuendelea namna hii hata kidogo". Na aliangua kilio cha namna yake mpaka machozi yake yakawa yanamdondokea mama usoni. Akamfuta mama machozi hayo kwa kujongeza mikono yake bila kufikiri.
“Mtoto,” baba alisema kwa huruma na kwa kutambua vilivyo mchango wake, “kwa hiyo nini tufanye sasa?”
Dada alitikisa tu mabega yake kama ishara ya kushangazwa, ukilinganisha na kujiamini kwake alikokuwa nako, kushangazwa kulikomjia wakati akilia.
“Laiti angekuwa anatuelewa,” baba alisema kama vile aulizaye.
Dada, huku kwikwi zikiendelea, alitikisa mkono wake kwa nguvu kama ishara ya kusema hakuna mantiki kufikiria hayo.
“Laiti angekuwa anatuelewa,” baba alirudia na kwa kufumba macho alipokea imani ya dada juu ya kutowezekana kwa wazo hilo, “basi labda maelewano fulani naye yangewezekana. Lakini kama hali ilivyo...”
“Liondolewe mbali,” dada alipiga kelele; “Hakuna namna nyingine baba. Unatakiwa ujaribu kuondoa fikra kwamba huyu ni Grego. Kwamba tuliamini hivyo kwa muda mrefu hilo ni bahati mbaya sana kwetu. Lakini hili linawezaje kuwa Grego? Kama lingekuwa Grego, lingeshatambua zamani kwamba maisha pamoja na binadamu hayawezekani na linyama la hivyo na lingeshakuwa limejiondokea lenyewe zamani. Hapo tusingekuwa na kaka, lakini tungeweza kuendelea na maisha na kuheshimu kumbukumbu yake. Lakini hili linyama linatutesa. Linafukuza wapangaji, na ni wazi litateka nyumba hii nzima, na kutuacha tulale nje. Baba, we liangalie,” alianza kupiga makelele, “limeshaanza tena.”
Kwa hofu kubwa ambayo haikueleweka kabisa kwa Grego, dada alimuacha hata mama, akijisogeza mbali na kiti chake, kana kwamba alikuwa tayari kumtoa mama kafara kuliko kuwa karibu na Grego, na kukimbilia nyuma ya baba yake ambaye, kwa kuhemshwa na aliyoyafanya dada, pia aliinuka na kuinua nusu mkono wake kama ambaye anamlinda dada.
Lakini Grego hakuwa na wazo lolote la kutamani kuleta matatizo kwa yeyote yule na hususan kwa dada yake. Alikuwa tu ameanza kujigeuza ili atambae kuelekea chumbani kwake, muonekano wa kutatiza, kwani, kama matokeo ya hali yake dhoofu, ilimbidi ajiongoze mwenyewe kwenye zoezi gumu la kugeukia nyuma na kichwa chake, mchakato uliomfanya akiinue na kujigonga sakafuni mara kadhaa.
Alipumzika na kuangalia huku na kule. Nia zake njema zilikuwa ni kama zimetambuliwa. Hofu ilikuwa ni kwa muda tu. Sasa walimtazama kimya na kwa huzuni. Mama yake alikuwa amejilaza kwenye kiti chake, miguu yake ikiwa imenyooshwa na kuwa pamoja; macho yake ni karibu na yamefumbwa kwa uchovu. Baba na dada waliketi karibukaribu. Dada aalikuwa ameweka mkono mmoja shingoni mwa baba.
“Sasa pengine naweza kujigeuza mwenyewe,” aliwaza Grego na kuanza upya zoezi lile. Hakuweza kuacha kutweta kutokana na juhudi zake na ilimlazimu kupumzika mara hii au ile.
Licha ya hayo, hakuna aliyekuwa akimharakisha.
Aliachwa mwenyewe apambane na hali yake. Wakati alipofanikiwa kukamilisha zoezi la kugeuka, mara moja alianza kujongea moja kwa moja chumbani.
Alishangazwa na umbali mkubwa uliomtenganisha na chumba chake na hakuelewa hata kidogo aliwezaje na hali yake dhaifu kutembea umbali wote huo muda mfupi tu uliopita, takriban bila kutambua hilo.
Bila kusita akidhamiria kuendelea kutambaa haraka, ni kama hakuzingatia ukweli kwamba hakuna neno wala kilio kutoka kwenye familia yake lililokatiza safari yake.
Ni pale tu alipokuwa tayari mlangoni ndipo alipogeuza kichwa chake, kiasi tu, kwa vile bado alihisi shingo yake ikizidi kuwa ngumu.
Kwa vyevyote vile bado aliona kwamba nyuma yake hakuna kilichobadilika. Dada tu alikuwa amesimama. Jicho lake la mwisho alilitupa kwa mama yake ambaye sasa alikuwa ameshalala fofofo.
ITAENDELEA