Cheka, Simulia, Lakini Usiombe Yakukute - 22
Tokea yamkute, hayo ndiyo yaliyokuwa maneno ya kwanza ambayo dada yake alimwambia Grego moja kwa moja.
Dada alikimbilia chumba jirani ili kuleta spiriti au chochote ambacho kingesaidia kumzindua mama yake kutoka kwenye kuzirai kwake.
Grego alitaka kusaidia pia (pangebaki bado muda wa kutosha kuilinda picha ile) , lakini alikuwa ameganda kwenye kioo na ilibidi ajikwamue kwa kutumia nguvu.
Kisha naye akakimbilia chumba jirani, kama ambaye angeweza kumpa dada yake ushauri hivi, kama ilivyokuwa kwenye maisha yake ya awali, lakini ikamlazimu kusimama vivi hivi tu nyuma yake, wakati dada akipekua huku na kule miongoni mwa vyupa vingi vidogodinyo.
Hata hivyo, dada alistushwa sana alipogeuka. Chupa moja ikadondoka chini na kupasuka vipandevipande. Kipande cha chupa kikamjeruhi Grego usoni, huku dawa au nini sijui ilikuwa iumizayo ikitiririka juu yake.
Ndipo, bila kusita zaidi, Grete alichukua vyupa vingi kadiri alivyoweza kuvibeba na kukimbia navyo kwa mama yake. Akafunga mlango kwa mguu wake. Grego sasa alikuwa amefungiwa nje mbali na mama yake, ambaye pengine alikuwa karibu ya kufa, yote hayo shauri ya Grego.
Hakuweza kuufungua mlango, na hakutaka kumfukuza dada yake ambaye ilimbidi abaki na mama yake.
Kwa wakati huu hakuwa na lolote la kufanya zaidi ya kusubiri, na akiwa amezidiwa na majuto na wasiwasi, alianza kujongea na kutambaa juu ya kila kitu: kuta, fenicha, na dari. Hatimaye, katika sintofahamu yake, kadiri alivyokuwa akiona chumba chote kinaanza kumzunguka, alidondoka katikati ya meza kuu.
Muda mfupi ulipita. Grego alilala pale kilegelege. Kila kitu kumzunguka kilikuwa kimetulia. Pengine hiyo ilikuwa ni ishara njema.
Kisha kengele ya mlangoni ikalia.
Yule dada wa kazi alikuwa amejifungia jikoni kama ilivyo desturi, na ilimlazimu Grete kwenda kufungua mlango.
Baba alikuwa amerudi.
“Nini kimetukia,” yalikuwa ndio maneno yake ya kwanza. Muonekano wa Grete ulimwambia kila kitu.
Grete alimjibu kwa sauti chovu; wazi kabisa kichwa chake kilikuwa kifuani mwa baba:
“Mama alizimia, lakini sasa anaanza kuendelea vizuri. Grego ametoroka chumbani.”
“Ndio, niliyategemea hayo,” alisema baba, “Siku zote nawaambieni, lakini ninyi wanawake hamtaki kusikiliza.”
Ilikuwa ni wazi kwa Grego kwamba baba yake ameelewa vibaya ujumbe mfupi wa Grete na sasa alikuwa anadhani kwamba Grego amefanya jinai hii au ile ya kutumia nguvu. Hivyo Grego sasa ilimbidi atafute namna ya kumpoza baba yake, kwani hakuwa na muda wala fursa ya kumfafanulia baba yake hali halisi ilivyo.
Na hivyo alikimbilia mlango wa chumba chake na kuuegemea, ili kwamba baba yake aweze kuona moja kwa moja pale aingiapo kwamba Grego ana makusudi mazima ya kurudi chumbani mwake mara moja, kwamba haikuhitaji kumswaga ili arejee chumbani, bali ilichohitajika ni kumfungulia tu
mlango naye atatokomea ndani papo hapo.
Lakini baba yake hakuwa kwenye hali ya kuweza kubaini wema wote huo.
“Ah,” alipiga kelele mara tu alipoingia, kwa sauti inayoashiria kwamba alikuwa kwa wakati mmoja amekasirika na kufurahi.
Grego alikiondoa kichwa chake kutoka mlangoni na kukiinua uelekeo alikokuwa baba yake. Hakuwahi kwa kweli kumfikiria alivyo baba yake kama alivyokuwa amesimama pale.
Ndio, kwa mbinu yake mpya ya kutambaa huku na kule, alikuwa ameacha kuzingatia yanayoendelea mle nyumbani, kama ambavyo alikuwa anafanya awali, na kwa kweli impasa kutarajia ukweli kwamba atakuana na hali tofauti.
Hata hivyo, pamoja na hayo, yule kweli alikuwa ndiye baba yake yuleyule? Alikuwa mtu yuleyule ambaye alilala hoi amejitupa kitandani siku za mwanzo wakati Grego akifunga safari za kibiashara, ambaye alimpokea mida ya jioni siku arudipo akiwa amevaa nguo za kulalia na amekaa kwenye kiti cha uvivu, asiyeweza kabisa kuinuka, ambaye aliweza tu kuinua mkono kama alama ya kufurahi, na ambaye alienda kutembea Jumapili chache katika mwaka na kwenye sikukuu muhimu alijongea polepole baina ya Grego na mama yake (ambao nao walijongea poleple), mara zote akiwa polepole zaidi yao, akiwa amejifunika koti lake la zamani, muda wote akitumia mkongojo wake kwa makini, na ambaye, pale ambapo alitaka kusema kitu, karibu mara zote alisimama tuli na kuwakusanya wanafamilia waliomzunguka?
Lakini sasa alikuwa amesimama wima hasa, amevaa ovaroli la bluu lililomkaa vizuri, lenye vifungo vya rangi ya dhahabu, kama vile watumishi wa benki wavivaavyo.
Juu ya kola ngumu ya jaketi lake videvu vyake dabali vilijitokeza vikiwa imara kabisa, chini ya nyusi zake nyingi macho yake yalijaa nuru yakiwa imara kabisa, na nywele zake nyeupe ambazo alizoea kuziona zikiwa zimevurugika zilikuwa zimetanwa vema kuwa zing’arazo.
Baba alitupa kule kofia yake, ambayo ilikuwa na maandishi ya dhahabu (huenda yakiwa ni alama za benki), mpaka ilipotua kwenye kochi lililokuwa upande wa mwisho wa chumba, akajongea, huku pindo za koti lake refu la sare ya ofisi zikisukwasukwa huku na kule, mikono yake ikiwa kwenye mifuko ya suruali, uso wake ukiwa na sura ya kazi, mpaka alipomfikia Grego.
ITAENDELEA