Cheka, Simulia, Lakini Usiombe Yakukute - 9
Sasa, kwa bahati mbaya, mbio zake za kumkimbiza bosi meneja zilionekana kumgadhibisha vibaya baba yake, ambaye hapo awali alikuwa ameanza kutulia. Kwani, badala ya naye kumkimbiza bosi meneja au basi walau asimzuie Grego kwenye mbio zake, baba alinyakua mkongojo wa kutembelea wa bosi meneja aliokuwa ameutelekeza pamoja na kofia na koti lililokuwa kwenye kiti.
Kwa kutumia mkono wake wa kushoto, Baba Grego alichukua gazeti kubwa kutoka mezani, na akikanyaga mguu kama apigaye kwata, alienda kumswaga Grego arudi chumbani kwake, akipunga mkongojo na gazeti kumtishia.
Maombi yoyote kutoka kwa Grego hayangefaa kitu; hakuna maombi ambayo hata yangeeleweka. Bila kujali utayari aliokuwa nao Grego kugeuza kichwa chake kwa hishma, baba yake aliendelea tu kukanyaga sakafu kwa nguvu zaidi.
Upande wa pili wa sebule, Mama Grego alikuwa amefungua dirisha, bila kujali hali ya hewa ya baridi iliyokuwako, na kutoa kichwa nje kabisa ya dirisha, mikono ikiwa mashavuni.
Kati ya uchochoro na ngazi, ulipita upepo mkali, na mapazia ya dirisha yakasukwasukwa huku na kule, na magazeti mezani yakapeperuka, kurasa mbalimbali zikitapakaa sakafuni.
Baba Grego akaendelea mbele bila kurudisha nyuma majeshi, akinguruma mithili ya chizi.
Hapo, Grego hakuwa amejizoesha kujongea kinyumenyume; alikuwa anarejea polepole sana. Yaani kama angempatia fursa ya kugeuka nyuma mzimamzima, angekuwa keshafika chumbani kwake zamani. Lakini alihofia kumchokoza baba yake kwa kujaribu kugeuka nyuma, mchakato ambao ungetumia muda mwingi sana.
Kila sekunde ipitayo, alikuwa kwenye hatari ya kupata pigo mgongoni au kichwani linaloweza kumuua, kutoka kwenye ule mkongojo uliokuwa mkononi mwa Baba Grego.
Mwishowe Grego hakuwa na uchaguzi mwingine, kwani alitishika sana alipobaini kwamba hajajimudu kudhibiti uelekeo arudipo kinyumenyume.
Hivyo alianza, huku akimwangalia mara kwa mara kwa chati uelekeo wa baba yake, ili aweze kujigeuza haraka sana (ingawa kiukweli hii ilikuwa ni polepole sana)
baba yake alibaini nia yake njema, kwani hakumbughudhi Grego alipokuwa akijongea, bali hapa na pale hata alitumia ncha ya mkongojo kwa mbali kumswaga Grego ageuke vizuri.
Laiti pasingekuwa na mguno usiovumilika wa Baba Grego! Kwa sababu ya huo Grego alipoteza kabisa utulivu wake. Alikuwa karibu kabisa kukamilisha kugeuka, wakati ambapo kelele za mguno sikioni mwake, alipofanya kosa na kugeuka nyuma kidogo. Lakini hatimaye alipofanikiwa kuweka kichwa chake sawa, alibaini kwamba mwili wake ulikuwa mkubwa kuliko uwazi wa mlango uliokuwako, na hangeweza kuendelea kujongea mbele zaidi.
Kama inavyotarajiwa, kwa hali baba yake aliyokuwa nayo kichwani mwake, hakujiwa na wazo la kuufungua zaidi mlango ili kumsaidia Grego aweze kupita. Na hangeweza kuvumilia maandalizi marefu yaliyohitajika ili Grego aweze kubabatiza kupenya kwenye kanafasi kalioko.
Nyuma ya Grego, ile sauti ya mguno sasa ilikuwa si tena sauti ya baba mmoja. Sasa ilikuwa si masikhara tena, na Grego alijishurutisha, lolote na liwe, kupita hivyohivyo mlangoni.
Upande mmoja wa mwili wake ulikuwa umeinuka juu. Alikuwa kwenye mlalo wenye nyuzi kadhaa kulinganisha na uwazi wa mlango. Upande wake wa pili ulikuwa unauma kutokana na kujiburuza.
Kwenye ule mlango mweupe, madoa ya kuchukiza yalibakia.
Punde, alikwama mlangoni na hakuweza tena kujongea yeye mwenyewe peke yake. Tuvigulu twake vikining’inia na kujirusharusha juu hewani, na upande wa pili ukiburuzika kwa maumivu sakafuni. Ndipo baba yake alipomsukuma kwa nguvu moja kubwa iliyomkwamua Grego, na ambaye alijikongoja, akitokwa sana na damu, mpaka ndani kabisa chumbani kwake.
Mlango ulifungwa, ukibamizwa kwa kusukumwa na mkongojo, na hapo kukawa hatimaye kimya.
Inaendelea Sehemu ya 10