Cheka, simulia, lakini usiombe yakukute

Umesoma hadithi hii mwanzo hadi mwisho?

  • Ndio

    Votes: 3 50.0%
  • Hapana

    Votes: 3 50.0%

  • Total voters
    6
Lakini mbona hiki ni kiswahili kabisa jamani au nimepatwa na shida ya uelewa?
 
Cheka, Simulia, Lakini Usiombe Yakukute - 4
“Nakuja sasa hivi,” alisema Grego polepole na kwa kukusudia na hakujongea, kusudi asipoteze hata neno moja la mazungumzo.
“Mama mpendwa, siwezi kujieleza kwa namna yoyote nyingine,” alisema bosi meneja; “Natarajia itakuwa sio kitu kikubwa. Kwa upande mwingine, ni lazima niseme sisi watu wa kazi, kwa bahati nzuri au mbaya, vyovyote vile uangaliavyo, aghalabu hulazimika kuzishinda changamoto ndogondogo kwa sababu ya kazi.”

“Kwa hiyo Bosi Meneja anaweza kuingia kuja kukuona sasa” aliuliza baba, uvumilivu ukimshinda huku akigonga tena mlango.
“Hapana,” alisema Grego.
Kwenye chumba jirani cha upande wa kulia, dada alianza kulia.
Kwa nini dada yake hakuenda waliko wenzie? Pengine alikuwa ndio ameamka kitandani sasa na hata hajaanza kuvaa.
Kwa nini sasa alikuwa akilia? Kwa sababu kaka yake hakuwa ameamka na alikuwa hamfungulii mlango bosi meneja; kwa sababu alikuwa hatarini kupoteza ajira yake, na kwa sababu bosi wake atawasumbua wazazi wake kwa madai yake ya zamani?

Hayo huenda yalikuwa ni mashaka yasiyo mahali pake kwa sasa. Grego alikuwa bado yuko hapahapa na hakufikiria aslan kutelekeza familia yake. Kwa saasa alikuwa amejilaza palepale kwenye zulia, na hakuna mtu ambaye kama angejua hali aliyokuwa nayo angemlazimisha amfungulie bosi meneja.

Lakini Grego hangeweza kutimuliwa ajira papohapo kwa sababu tu ya katatizo hako ka kutomfungulia bosi meneja, kwani angetafuta sababu rahisi na ya kukubalika hapo baadaye. Grego alionelea kwamba ingekuwa ni busara zaidi kutojishughulisha na bosi meneja kwa sasa, badala ya kumghasi kwa mazungumzo na kilio.

Lakini ni hali hiyo ya sintofahamu ambayo iliwapa taabu wengine na kuwaathiri watendayo.

“Bwana Samsa,” bosi meneja sasa alikuwa anapayuka, sauti kubwa, “nini tatizo? Umejifungia chumbani, unajibu tu ‘ndio’ na ‘hapana’, unawatafutia matatizo makubwa wazazi wako bila sababu ya msingi, na kutelekeza (nataja hili kama mengineyo) majukumu yako ya kazi kwa namna ambayo haikuwahi kutokea. Nazungumza hapa kwa jina la wazazi wako na jina la mwajiri wako, na ninakusihi kwa uzito mkubwa utoe maelezo fasaha mara moja. Nastaajabu. Nashangaa. Nilidhani nakufahamu kama mtu mpole, mstaarabu, na sasa waonekana wataka kuanza kuonyesha tabia za ajabu. Bosi Kubwa aliashiria mapema leo hiihi inayoweza kuwa sababu ya mapuuza yako -- inahusika na makusanyo ya pesa taslimu uliyoaminiwa kuyakusanya muda mchache uliopita -- lakini kiukweli bado kidogo nikutetee kwamba maelezo hayawezekani kuwa sahihi.

Lakini, sasa naona hapa ukichwa-maji wako, na ninapoteza hamasa yoyote ya kukutetea hata kidogo. Na nafasi uliyonayo imeandikwa kwa penseli. Mwanzoni nilikusudia kukuambia haya kwa faragha, lakini kwa kuwa unanipotezea muda wangu hapa kizembe, sioni kwa nini suala hili lisiwafikie wazazi wako. Tija yako kadhalika imekuwa hairidhishi kabisa. Sawa, huu sio msimu wa biashara kubwa, tunatambua hilo, lakini msimu wa kutofanya biashara kabisa, hakuna kitu kama hicho, Bwana Samsa, na kitu kama hicho lazima kisiwepo kamwe.”

“Lakini Bosi Meneja,” alisema Grego, ameghadhibika, na kutokana na mhemko wake akajisahau kila kitu.

Inaendelea Sehemu ya 5
 
Cheka, Simulia, Lakini Usiombe Yakukute - 5

“Nafungua mlango sasa hivi, pasi na kuchelewa. Kiugonjwa kidoogo, kizunguzungu, kilinizuia nisiamke. Bado niko kitandani sasa. Lakini sasa najisikia ni mwenye nguvu tena. Niko kwenye mchakato wa kuamka. Endeleeni kuvuta subira muda kidogo! Mambo hayaendi sawa kama nilivyotegemea. Lakini mambo yote sawa. Ugonjwa huingia haraka! Jana tu jioni nilikuwa buheri wa afya. Wazazi wangu wanatambua hilo pasi na shaka. Yaani, jana tu jioni machale yalinicheza. Waliokuwepo watakuwa walibaini hivyo.

Kwa nini sijaripoti ofisini! Lakini watu siku zote hufikiri kwamba wanaweza kupona bila kupumzika nyumbani. Bosi Meneja! Usiwasumbue wazazi wangu! Hakuna msingi wowote wa shutuma unazozitoa sasa dhidi yangu, na kiukweli hakuna mtu yeyote aliyesema chochote kuhusu mimi. Pengine hujazisoma oda nilizozituma hivi karibuni.

Juu ya hayo, najipanga kuondoka na treni la saa mbili kamili asubuhi; mapumziko haya mafupi yamenipa nguvu. Bosi Meneja, ondoka. Nitakuja mwenyewe ofisini hivi punde. Tafadhali nifanyie hisani kumtaarifu hayo Bosi Kubwa.”

Wakati Grego akibwatuka kwa haraka yote hayo, asielewe anachokiongea, alikuwa ameshasogea kirahisi karibu na kabati, pengine urahisi uliotokana na mazoezi aliyokuwa ameyafanya kitandani, na sasa alijaribu kujiinua pale kabatini.

Alitaka hasa kufungua mlango; alitaka haswa aonwe na kuongea na bosi meneja. Alitaka kuona hao wanaomsumbua kutaka kumuona, watakuwaje wamuonapo.

Wakistuka, basi Grego hatakuwa na wajibu wowote tena na atatulia tu. Lakini wakipokea kila kitu kimyakimya na, wakimwambia aendelee na majukumu, basi ataiwahi treni ya saa mbili kamili.

Mwanzoni aliteleza mara mbili tatu kutoka kabatini. Lakini hatimaye alijitutumua na kusimama wima hapo. Hakukumbuka tena maumivu sehemu ya chini ya mwili wake, licha ya kumchomachoma vikali. Kisha akajiangushia kwenye kiti jirani, akijishikilia kwa vigulu vyake vidogo. Kwa kufanya hivi aliweza kujidhibiti na kukaa kimya, kwani sasa aliweza kumsikia bosi meneja.

“Mlielewa hata neno moja?” Bosi Meneja aliwauliza wazazi, “Anatuchezea shere siye kama majuha?”

“Toba yarabi,” mama alipiga kelele, machozi yakimtoka, “pengine yuaumwa sana na tunazidi kumsumbua. Grete! Grete!” sasa alipiga mayowe.

“Mama?” dada aliita kutokea upande wa pili. Sauti zao zilipitia chumbani kwa Grego.

“Nenda kwa dokta sasa hivi. Grego ni mgonjwa. Wahi kwa dokta. Umemsikia Grego akiongea?”

“Hiyo ilikuwa ni sauti ya mnyama,” alisema bosi meneja, taratibu kama ungelinganisha na vilio vya mama.

“Anna! Anna!” baba alipiga kelele kutoka sebuleni hadi jikoni, akipiga makofi, “kamlete fundi wa makufuli sasa hivi!”

Mabinti wadogo wawili hao walikuwa tayari wakikimbia ukumbini, sketi zao zikiyumba huku na kule (dada kawezaje kuvaa haraka hivyo?) na kufungua milango ya nyumba yao. Sauti ya milango kufungwa haikusikikia aslani. Huenda waliiacha milango wazi, kama ulivyo utamaduni kwenye nyumba iliyofikwa na msiba.

Hata hivyo, Grego alikuwa ametulia zaidi. Sawa, watu hawaelewi maneno yake tena, ingawa kwake yeye aliyaona ni wazi kabisa, pengine kwa sababu masikio yalishayazoea. Lakini walau sasa watu walianza kuelewa mambo yake si shwari na walikuwa wakijiandaa kumsaidia. Imani na uhakika vilivyotumika kupangilia mipango hiyo kulimfanya ajihisi vema. Alijiona amerudishwa kundini mwa binadamu, na alikuwa na matarajio makubwa kwa daktari na fundi wa makufuli, bila kuwatofautisha vizuri nini kazi zao, kwamba wangeleta matokeo makubwa.

Ili kutoa sauti safi inavyowezekana kwa mazungumzo yatakayojitokeza punde, alikohoa kidogo, akifinya sauti isije ikasikika, kwani inawezekana hata sauti ya kikohozi ingesikika tofauti na kikohozi cha kibinadamu. Hakujiamini kufanya maamuzi tena.

Inaendelea Sehemu ya 6
 
Dah Basi Mimi zamani nilifikiria wadudu hawana akili.
Lakini leo hii nagundua kwamba wadudu kumbe Wana akili ya kuangalia picha za mwanamke ukutani,wanaangalia nguo zilizotundikwa,kujipima urefu wake na blanketi.
Hongera zake mdudu.
 
Cheka, Simulia, Lakini Usiombe Yakukute - 6

Wakati huohuo, kule kwenye chumba jirani kulikuwa kimya kweli. Pengine wazazi wake walikuwa wamekaa na bosi meneja mezani na walikuwa wakinong’ona; pengine wote walikuwa wameegemea mlango wakisikilizia. Grego alijisogeza polepole kuelekea mlangoni, kwa msaada wa kiti cha uvivu, akakisukumia mbali, akijirusha mlangoni, akiuegemea akiwa wima (vivimbe miguuni mwake vilikuwa vina vitu vinavyonata), na akapumzika kidogo baada ya jitihada hizo.

Kisha akafanya juhudi kutumia kinywa chake kuzungusha ufunguo ulioko mlangoni. Kwa bahati mbaya, inaonekana mdomo wake haukuwa na meno ya ukweli. Sasa atawezaje kweli kuushikilia ufunguo?

Lakini kama vile kufidia mapungufu hayo, taya lake lilikuwa imara hasa; kwa msaada wa hayo aliweza kuzungusha ufunguo, na hakutanabahi kwamba ni wazi kwamba alikuwa akijijeruhi mwenyewe, kwani ugiligili wa rangi ya kahawia ulitiririka toka kinywani mwake, ukapita juu ya ufunguo, na kudondokea sakafuni.

“Sikiliza kwa makini,” alisema bosi meneja aliyekuwa chumba jirani, “anazungusha ufunguo kufungua mlango.”

Kwa Grego hayo yalikuwa ni maneno ya kutia moyo sana. Lakini wote walitakiwa wamsemeshe, hii ikiwa ni pamoja na baba na mama yake, “Hivyohivyo, Grego,” wangepiga kelele, “endelea, endelea kufungua kitasa.”

Akitafakari kwamba jitihada zake zote zilikuwa zinapokewa na sintofahamu, aliung’ata ufunguo kwa hamasa akitumia nguvu zote alizoweza kuzikusanya. Na kadiri ufunguo ulivyofunguka zaidi, ndivyo alivyozidi kucheza karibu na kitasa. Sasa alikuwa anajishikilia wima mlangoni kwa kinywa chake tu, na ilimbidi kujishikilia kwenye ufunguo au baadae kuusukuma chini kwa kutumia uzito wake wote, kama ilivyohitajika.

Mlio wa kitasa hatimaye kufunguka ulimrejeshea Grego fahamu zake vizuri.

Akivuta pumzi ndefu alijiambia, “Kwa hiyo sikumhitaji fundi wa makufuli,” na akapeleka kichwa chake kwenye hendeli ya kufungulia mlango ili kuufungua mlango uwe wazi kabisa.

Na kwa kuwa aliufungua mlango kwa mbinu hizi, mlango ulikuwa tayari wazi kabisa pasi na yeye kuwa anaonekana.

Kwanza ilimbidi ajigeuze polepole nyuma ya mlango alikokuwa, polepole kabisa, bila shaka, kwani hakutaka kudondokea kizembe mgongo wake pale mlangoni. Alikuwa bado anajihangaisha na jukumu hili zito la kujijongeza na hakuweza kuzingatia kitu chochote kingine, wakati alipomsikia bosi akipiga kelele “Oooo!” (Ilisikika kama mvumo wa upepo), na sasa alimuona bosi meneja, karibu naye kabisa mlangoni, akifunika mdomo wake kwa mdomo wake uliobakia wazi na kurudi kinyumenyume polepole, kana kwamba kani isiyoonekana ilikuwa inamsukumiza.

Mama yake (licha ya uwepo wa bosi meneja alikuwa naye amesimama pale, nywele zake zimevurugika kwa vile hazikutanwa toka usiku) mikono yake imekunjwa akimtazama baba yake; kisha akapiga hatua mbili kumwelekea Grego na kuzirai, huku sketi yake ikimfunika kumzunguka, uso wake umeangukia katikati ya kifua chake, umefunikwa kabisa.

Baba yake alikunja ngumi akiwa amekunja sura kikatili, kana kwamba anataka kumsukuma Grego arudi chumbani kwake, kisha akaangalia kwa mashaka kuzunguka sebule, akafunika macho yake kwa viganja vyake, akaangua kilio mpaka kifua chake kikubwa kikawa kinatikisika.

Mpaka hapo Grego hakupiga hatua hata moja kwenda sebuleni, lakini aliegamisha mwili wake kwenye kizingiti cha mlango, kiasi kwamba ni nusu tu ya mwili wake ulikuwa unaonekana, pamoja na kichwa chake, kimeelekea upande, ambacho kwacho alikitumia kuwachungulia wenzie.

Wakati huohuo, palikuwa pameshakucha. Ikisimama bayana upande wa pili wa mtaa ilikuwa ni sehemu ya nyumba ndefu ya rangi ya kijivu-nyeusi iliyokuwa mkabala na nyumba yao (ilikuwa ni hospitali) ambayo madirisha yake yalikuwa yakielekea kiambazani.

Mvua ilikuwa bado inanyesha, lakini kwa matone makubwamakubwa, kila tone likionekana ladondoka chini ya lenzie, moja baada ya jingine kwenda ardhini.

Vyombo vya chai ya asubuhi vilikuwa vimerundikana mezani, kwa vile chai ya asubuhi ndio ulikuwa mlo muhimu kuliko yote kwa baba, aliyezoea kuirefusha kwa masaa kwa kusoma magazeti mbalimbali huku akiinywa.

Moja kwa moja upande wa pili wa ukuta palikuwa na picha ya Grego ya toka enzi yuko JKT; ilikuwa ni picha yake kama luteni, akitabasamu, bila shaka yoyote, mkononi mwake ameshika sime, akitaka heshima kwa vile alivyo na kwa sare alizovaa.

Mlango kwenda ukumbini ulikuwa wazi, na kwa vile mlango wa nje ulikuwa wazi pia, mtu angeweza kuona kibaraza na ngazi za kushuka chini.

Inaendelea Sehemu ya 7
 
Cheka, Simulia, Lakini Usiombe Yakukute - 7

“Sasa,” alisema Grego, akifahamu fika kwamba ni yeye pekee aliyebaki ametulia. “Nitavaa nguo sasa hivi, nitapakia mkusanyiko wa sampuli za bidhaa, na kuondoka zangu. Utaniruhusu niende, au sio? Unaona, Bosi Meneja, mimi siyo juha, na ninapenda kuchapa kazi. Kusafiri kunachosha, lakini singeweza kuishi bila safari. Waenda wapi, Bosi Meneja? Ofisini? Kweli? Utaripoti kila kitu kiukweli? Mtu anaweza kukwama kufanya kazi kwa muda mfupi, lakini huo ndio muda bora kabisa wa kukumbuka fanaka za awali na kuzingatia kwamba baadae, baada ya vikwazo kuwa vimeondolewa mbali, mtu huyo atachapa kazi kwa juhudi zaidi na maarifa zaidi.

Ninawiwa sana kwa Bosi Kubwa -- wafahamu hayo vema kabisa. Kwa upande mwingine, ninahofia kuhusu wazazi wangu na dada yangu. Yamenikuta, lakini nitapambana mpaka nitoke tena. Usikuze mambo kuliko hivi yalivyo.

Ongea vema kwa niaba yangu ofisini! Watu hawatupendi sisi watumishi wa idara ya mauzo tusafirio sana. Nafahamu hayo. Watu wanadhani tunapata vitita vya fwedha na hivyo kula maisha. Watu hawana hata sababu ya maana kutafakari kuhusu fikra-potofu zao. Lakini wewe, Bosi Meneja, wewe una mtazamo mzuri na mitandao mikubwa kuliko watu hao wengine, hata, nakuambia kwa kujiamini kabisa, kumzidi Bosi Kubwa mwenyewe, ambaye kwa nafasi yake kama mwajiri, anaweza kufanya makosa madogo yenye athari kwa mtumishi fulani. Wafahamu vema sana kwamba wafanyakazi tusafirio wa idara ya mauzo huwa nje ya ofisi takriban mwaka mzima na hivyo ni vyepesi kuwa wahanga wa udaku, matukio yasiyokusudiwa, malalamishi yasiyo na msingi, ambayo kwake ni vigumu kujitetea, kwa vile kwa sehemu kubwa mtumishi hayasikii kabisa na ni pale tu anapokuwa amechoka taaban baada ya kukamilisha safari, apatapo nafasi ya kujisikilizia mwili wake nyumbani kwake mwenyewe, kukutwa na masaibu ambayo hayawezi kuchunguzwa mpaka kufahamika chanzo chake.

Bosi Meneja, usiondoke bila kusema neno kuniambia kwamba walau utakubaliana nami kwamba nasema maneno yenye mantiki ngaa kidogo!”

Lakini wakati maneno ya Grego ya mwanzo yalipoanza kumtoka, bosi meneja alikuwa tayari keshageuka, na sasa alikuwa akimtazama Grego huku akiwa amegeuza shingo yake, na mdomo ameufunga. Wakati wa risala ya Grego, hakuwa ametulia tuli hata kwa sekunde, bali alikuwa akijongea uelekeo wa mlango, macho yake muda wote yako kwa Grego, lakini polepole, kana kwamba palikuwa na katazo la siri la kuzuia kuondoka mle chumbani.

Tayari alikuwa ameshafika sebuleni, na baada ya kugeuka haraka na kuutoa mguu wake sebuleni, mtu angeweza kudhani kwamba ameungua unyayo wake. Kule ukumbini, hata hivyo, aliunyoosha mkono wake wa kuume kuzielekea ngazi, kana kwamba huko nje kulikuwa na pumziko la miujiza lililokuwa likimngojea huko.

Grego alitambua kwamba kwa vyevyote vile, ni lazima ahakikishe meneja haondoki akiwa na mawazo haya, hususan iwapo anataka nafasi yake ya ajira isiwekwe kwenye hatari kubwa.

Wazazi wake walikuwa hawakulitambua hili vema. Kwa miaka mingi, walijijengea imani kwamba Grego amejipatia ajira ya kudumu maisha yake yote, na kwamba, walizingwa kabisa na matatizo yaliyoko kiasi kwamba maono ya mambo yajayo yalikuwa ni vitu vya kigeni kwao.

Lakini Grego alikuwa na maono. Meneja lazima azuiwe, atulizwe, ashawishiwe, na hatimaye awe upande wetu. Maisha yajayo ya Grego na familia yake hakika yalilitegemea hilo!

Laiti dada yake angekuwepo! Alikuwa mwerevu. Tayari alishakuwa ameangua kilio wakati ule Grego akiwa amelala chali. Na bosi meneja, mtu rafiki kwa warembo, bila shaka angeweza kumsikiliza dada yake.

Angeweza kufunga mlango wa nyumba na kuongea naye sebuleni maneno ya kumtuliza hofu aliyokuwa nayo.

Lakini dada yake wala hata hakuwapo hapo. Grego inabidi tu apambane na hali yake yeye mwenyewe.

Bila kufikiri kwamba mpaka hapo alikuwa hafahamu chochote kuhusu uwezo wake wa sasa wa kujongea na bila kufikiri kwamba, huenda (tuseme labda kutokana na) namna ulivyo uwezo wake wa sasa wa kuongea, kwa mara nyingine tena hakueleweka, Grego aliondoka nyuma ya mlango, akapita mlangoni, na akataka kumfuata bosi meneja, ambaye wakati huu alikuwa kajishikilia vizuri kwenye vishikilio vya kwenye ngazi kwa mikono yake miwili kwa namna ya kuchekesha pale kiambazani.

Lakini wakati Grego akitafuta kitu cha kujishikilia nacho, alidondoka akipiga kijiyowe, akitanguliza tuvigulu vyake chini.

Punde baada ya hayo kutukia, ndipo kwa mara ya kwanza kwa asubuhi ile aliweza kujitathmini hali yake ya afya kwa ujumla.

Vigulu vyake vidogo, vingi, viliikamata sakafu iliyokuwa chini yake sawia; vilimtii ipasavyo, kama alivyobaini kwa furaha, na kujitahidi kumpeleka uelekeo alioutaka.

Bila kuchelewa aliamini kwamba madhila yake yote yanafikia mwisho hivi punde.

Inaendelea Sehemu ya 8
 
Cheka, Simulia, Lakini Usiombe Yakukute - 8

Lakini muda uleule aliokuwa ametua sakafuni, akitikisika kwa namna ya kujizuia karibu kabisa na mkabala kabisa na mamaye (akionekana dhof’li-hal) ghafla mamaye aliamka, akasimama wima, mikono yake imeinuliwa mbali na vidole vyake vimekunjuliwa, na kuanza kupiga mayowe.

“Msaada, tumwogope Mungu, msaada!” aliinamisha kichwa chini, kana kwamba alitaka kumwangalia Grego vema, lakini alitimua mbio kurudi nyuma, tofauti na mwonekano ulivyokuwa unaashiria. Alisahau kwamba palikuwa na meza iliyokwisha kuandaliwa madikodiko.

Alipofika mezani, aliikalia bila kuangalia, kana kwamba ni mtu aliyechanganyikiwa, na hakuelekea kuwa ametambua kwamba kando yake kahawa ilikuwa inatiririka chini kwenye zulia, ikitokea kwenye chombo kikubwa kilichobinuka mezani.

“Mama, mama,” alisema Grego kimya kimya, na akimtizama mama yake.

Bosi meneja alikuwa kwa muda huo hayuko mawazoni kabisa, kwani, badala yake, Grego hakuweza kujizuia kutinga taya lake hewani mara kadhaa.

Mama Grego alipoona hayo, alipiga mayowe upya, akaharakia kuondoka mezani, na kuangukia mikononi mwa Baba Grego, ambaye alikuwa akimkimbilia.

Lakini Grego hakuwa na muda wowote wa kuupoteza sasa hivi kwa ajili ya wazazi wake: Bosi Meneja alikuwa tayari kwenye ngazi.

Kidevu chake kikiwa usawa wa kijiukuta cha ngazi, Bosi Meneja aliangalia nyuma kwa mara moja ya mwisho. Grego aliruka ili kumkaribia bosi wake kama angeweza. Lakini Bosi Meneja lazima machale yatakuwa yalimcheza, kwani naye aliziruka ngazi kadhaa na kutokomea, huku akali akipiga kelele za “Hee!”. Sauti hiyo ilirindima kwa mwangwi uliosambaa eneo lote la kwenye ngazi.

Inaendelea Sehemu ya 9
 
Cheka, Simulia, Lakini Usiombe Yakukute - 9

Sasa, kwa bahati mbaya, mbio zake za kumkimbiza bosi meneja zilionekana kumgadhibisha vibaya baba yake, ambaye hapo awali alikuwa ameanza kutulia. Kwani, badala ya naye kumkimbiza bosi meneja au basi walau asimzuie Grego kwenye mbio zake, baba alinyakua mkongojo wa kutembelea wa bosi meneja aliokuwa ameutelekeza pamoja na kofia na koti lililokuwa kwenye kiti.

Kwa kutumia mkono wake wa kushoto, Baba Grego alichukua gazeti kubwa kutoka mezani, na akikanyaga mguu kama apigaye kwata, alienda kumswaga Grego arudi chumbani kwake, akipunga mkongojo na gazeti kumtishia.

Maombi yoyote kutoka kwa Grego hayangefaa kitu; hakuna maombi ambayo hata yangeeleweka. Bila kujali utayari aliokuwa nao Grego kugeuza kichwa chake kwa hishma, baba yake aliendelea tu kukanyaga sakafu kwa nguvu zaidi.

Upande wa pili wa sebule, Mama Grego alikuwa amefungua dirisha, bila kujali hali ya hewa ya baridi iliyokuwako, na kutoa kichwa nje kabisa ya dirisha, mikono ikiwa mashavuni.

Kati ya uchochoro na ngazi, ulipita upepo mkali, na mapazia ya dirisha yakasukwasukwa huku na kule, na magazeti mezani yakapeperuka, kurasa mbalimbali zikitapakaa sakafuni.

Baba Grego akaendelea mbele bila kurudisha nyuma majeshi, akinguruma mithili ya chizi.

Hapo, Grego hakuwa amejizoesha kujongea kinyumenyume; alikuwa anarejea polepole sana. Yaani kama angempatia fursa ya kugeuka nyuma mzimamzima, angekuwa keshafika chumbani kwake zamani. Lakini alihofia kumchokoza baba yake kwa kujaribu kugeuka nyuma, mchakato ambao ungetumia muda mwingi sana.

Kila sekunde ipitayo, alikuwa kwenye hatari ya kupata pigo mgongoni au kichwani linaloweza kumuua, kutoka kwenye ule mkongojo uliokuwa mkononi mwa Baba Grego.

Mwishowe Grego hakuwa na uchaguzi mwingine, kwani alitishika sana alipobaini kwamba hajajimudu kudhibiti uelekeo arudipo kinyumenyume.

Hivyo alianza, huku akimwangalia mara kwa mara kwa chati uelekeo wa baba yake, ili aweze kujigeuza haraka sana (ingawa kiukweli hii ilikuwa ni polepole sana)

baba yake alibaini nia yake njema, kwani hakumbughudhi Grego alipokuwa akijongea, bali hapa na pale hata alitumia ncha ya mkongojo kwa mbali kumswaga Grego ageuke vizuri.

Laiti pasingekuwa na mguno usiovumilika wa Baba Grego! Kwa sababu ya huo Grego alipoteza kabisa utulivu wake. Alikuwa karibu kabisa kukamilisha kugeuka, wakati ambapo kelele za mguno sikioni mwake, alipofanya kosa na kugeuka nyuma kidogo. Lakini hatimaye alipofanikiwa kuweka kichwa chake sawa, alibaini kwamba mwili wake ulikuwa mkubwa kuliko uwazi wa mlango uliokuwako, na hangeweza kuendelea kujongea mbele zaidi.

Kama inavyotarajiwa, kwa hali baba yake aliyokuwa nayo kichwani mwake, hakujiwa na wazo la kuufungua zaidi mlango ili kumsaidia Grego aweze kupita. Na hangeweza kuvumilia maandalizi marefu yaliyohitajika ili Grego aweze kubabatiza kupenya kwenye kanafasi kalioko.

Nyuma ya Grego, ile sauti ya mguno sasa ilikuwa si tena sauti ya baba mmoja. Sasa ilikuwa si masikhara tena, na Grego alijishurutisha, lolote na liwe, kupita hivyohivyo mlangoni.

Upande mmoja wa mwili wake ulikuwa umeinuka juu. Alikuwa kwenye mlalo wenye nyuzi kadhaa kulinganisha na uwazi wa mlango. Upande wake wa pili ulikuwa unauma kutokana na kujiburuza.

Kwenye ule mlango mweupe, madoa ya kuchukiza yalibakia.

Punde, alikwama mlangoni na hakuweza tena kujongea yeye mwenyewe peke yake. Tuvigulu twake vikining’inia na kujirusharusha juu hewani, na upande wa pili ukiburuzika kwa maumivu sakafuni. Ndipo baba yake alipomsukuma kwa nguvu moja kubwa iliyomkwamua Grego, na ambaye alijikongoja, akitokwa sana na damu, mpaka ndani kabisa chumbani kwake.

Mlango ulifungwa, ukibamizwa kwa kusukumwa na mkongojo, na hapo kukawa hatimaye kimya.

Inaendelea Sehemu ya 10
 
Cheka, Simulia, Lakini Usiombe Yakukute - 10

kava.png


Grego alipoamka kutoka kwenye usingizi wake mzito wa pono ilikuwa ni mida ya magharibi. Bila shaka angeweza kuendelea kuuchapa usingizi kidogo zaidi, kwani alikuwa anajisikia ni aliyepumzika vya kutosha na hana usingizi, japokuwa alihisi kana kwamba sauti za mtu atembeaye kwa haraka na za kufungwa mlango wa sebuleni kwa uangalifu ndizo zilizomuamsha.

Mwanga wa taa za umeme barabarani zilimulika kiaina kwenye singibodi na kwenye maeneo ya juu ya samani, lakini maeneo ya chini alikokuwa Grego yalikuwa na giza.

Alisonga polepole kuelekea mlangoni, akipapasa huku na kule kwa kutumia udevu huu na ule, ambayo sasa kwa mara ya kwanza alikuwa ametambua umuhimu wake, ili aweze kubaini kilichokuwa kinaendelea kule sebuleni.

Inaendelea Sehemu ya 11
 
Cheka, Simulia, Lakini Usiombe Yakukute - 11

Upande wake wa kushoto ulikuwa ni kama kovu moja refu la kuchukiza, na ilimlazimu kuchechemea kwenye jozi mbili za miguu. Na kama nyongeza, kigulu kimoja kidogo kilikuwa kimejeruhiwa vibaya wakati wa timbwili la asubuhi (yaani ni kama muujiza kwamba ni kiguu kimoja tu kilichojeruhiwa) na alikikikongoja na kukiburuta kama kilichokufa.

Mlangoni ndipo alipobaini ni nini hasa kilichomrairai ajongee hapo: ilikuwa ni harufu ya kitu cha kula. Kwani hapo palikuwa na bakuli lililojaa maziwa yaliyoongezewa sukari, na ambamo muliogelea tuvipande tudogo twa mikate.

Almanusura aangue kicheko kwa furaha, kwani sasa alijihisi njaa kali kuliko ilivyokuwa asubuhi, na mara moja alidumbukiza kichwa chake mpaka karibu na yaliko na hata kuzidi usawa wa macho yake kwenye maziwa.

Lakini mara moja alikiondoa akikirihika, siyo tu kwa sababu ya ugumu uliotokana na hali iliyokuwa nayo upande wake wa kushoto (angeweza tu kula kama mwili wake uliokuwa ukipwita ungekuwa na wote unashirikiana), bali pia kwa sababu maziwa, ambayo kwa kawaida yalikuwa ndio kinywaji chake pendwa na ambayo dada yake bila shaka aliyaleta kwa sababu hiyo, hayakumvutia aslan. Aligeuka kuondoka kwenye bakuli akiwa amekereka fulani hivi na kutambaa mpaka katikati ya chumba.



Kule sebuleni, kama ambavyo Grego aliweza kuona kupitia ufa wa mlangoni, taa ilikuwa imewashwa, lakini japo kwa kawaida inavyokuwa mara zengine mida hii baba alijizoeza kusoma magazeti kwa sauti ili mama asikie au kwa wakati mwingine dada asikie, kwa wakati huu hapakuwa hata na kasauti kalikosikika.

Sasa, pengine huu utaratibu wa kusomeana kwa sauti, ambao dada siku zote aliongea na kumwandikia, siku hizi ulikuwa umepotea kwenye mazoea. Lakini palikuwa kimya, licha ya ukweli kwamba nyumba haikuwa tupu.

“Maisha yamekuwa kimya kweli kwenye kaya hii”, alijiambia Grego, huku akikodoa macho kizani, alijivunia sana kwamba aliweza kuwezesha maisha mazuri kwenye nyumba nzuri kama hii kwa wazazi wake na dada yake.

Lakini nini kitajiri iwapo utulivu wote huu, fanaka yote hii, kuridhika kote huku kutakapofikia mwisho fulani mbaya? Ili asivurugwe na mawazo yote hayo, Grego aliamua kuanza kujongea na kutambaa huku na kule chumbani.

Mara moja wakati huo wa jioni ndefu, upande mmoja wa mlango na kisha mlango mwingine ulifunguliwa kiduchu tu na kisha kufungwa haraka. Mtu fulani yaonekana alihitaji kuingia chumbani lakini akabadili mawazo.

Grego mara moja akajongea kwenye mlango unaoelekea sebuleni, akidhamiria kumkaribisha mgeni yule mwenye kusitasita au mwingine au walau kubaini ni nani. Lakini mlango haukufunguliwa tena, na Grego alisubiri bila mafanikio.

Pale mwanzoni, wakati mlango ulipokuwa umefungwa, wote walikuwa wanataka kuingia chumbani kwake; sasa, baada ya kuwafungulia mlango mmoja na milango mingine bila shaka ilikuwa imefunguliwa wakati wa mchana, hakuna yeyote aliyekuja hata mara moja, na funguo zilifungwa kwa nje.

Taa ya sebuleni ilizimwa pale ilipokuwa usiku sana, na hivyo ilikuwa rahisi kutambua ya kwamba wazazi wake na dada yake walikuwa macho muda wote huu, kwani mtu angeweza kuwasikia wazi kabisa wakati wote watatu wakiondoka kwa kunyatanyata.

Sasa ilikuwa ni wazi kwamba hakuna mtu angekuja chumbani kwa Grego mpaka kukuche. Kwa hiyo, alikuwa na muda mrefu wa kutafakari bila kubughudhiwa juu ya namna gani ayaanze maisha yake upya.

Lakini chumba hicho, kilichokuwa wazi, ambacho alilazimika kulala kifudifudi sakafuni, kilimfanya ahamanike, bila kutanabahi sababu, kwani ni miaka mitano amekuwa akiishi katika chumba hichohicho.

Akigeuka bila kufikiri sana na kwa kaaibu kidogo, alijisogeza chini ya kochi, mahali ambako, licha ya ukweli kwamba mgongo wake ulikuwa umebanwa kidogo, na hakuweza kuinua kichwa chake, alijihisi yuko vizuri na alisikitika tu kubaini kwamba mwili wake ulikuwa mpana kiasi cha kumzuia asizame mzima chini ya kochi.

Inaendelea Sehemu ya 12
 
Cheka, Simulia, Lakini Usiombe Yakukute - 12

Hapo ndipo alipobakia kwa usiku mzima, ambao kwa sehemu aliutumia kwa usingizi wa mang’amung’amu, uliokatizwakatizwa na njaa, lakini kwa sehemu akiwa katika hali ya hofu na matumaini hafifu, ambavyo vyote vilipelekea hitimisho moja kwamba kwa muda huu angelazimika kutulia na kuwa na subra na kuwajali sana familia yake inayopitia zahma ambayo hali yake hii aliyonayo inamlazimu kuwasababishia.

Tayari mapema asubuhi (ilikuwa takriban bado usiku) Grego alikuwa na muda wa kupima uimara wa maamuzi aliyokuwa ameyafikia, kwani dada yake, akiwa karibu na kuwa amevalia rasmi, alifungua mlango wa chumba chake unaoelekea sebuleni, na akaangalia ndani kwa shauku. Hakumuona mara moja, lakini pale alipombaini chini ya kochi (Yaani, lazima angekuwepo tu mahali hapa au pale; kwani hakuwa na mabawa ya kuruka) alipata mshituko mkubwa kiasi kwamba, bila kuweza kujizuia, alibamiza mlango kuufunga akiwa kulekule nje.

Lakini, kana kwamba alijutia aliyoyatenda, dada yake aliufungua tena mlango na kuingia akinyata, kana kwamba alikuwa mahali palipokuwa na mgonjwa mahututi au mgeni asiyejulikana.

Grego alikuwa amesogeza kichwa chake mbele kidogo mpaka mwisho wa mguu wa kochi na alikuwa akimwangalia dada yake.

Dada yake angeweza kubaini kwamba aliyaacha maziwa kama yalivyo, na siyo kwa sababu hakuwa na njaa, na angemletea kitu kingine cha kula kinachomfaa Grego?

Kama hangefanya hivyo dada mwenyewe, basi Grego alikuwa radhi kufa kwa njaa kuliko kuchukua hatua za kumwambia dada yake, japo alitamani sana atoke chini ya kochi na kujitupa miguuni pa dada yake, akimuomba ampatie chakula hiki au kile kizuri kwa kula.

Lakini dada yake alibaini mara moja, kwa mshituko, kwamba bakuli lilikuwa bado limejaa, isipokuwa maziwa kidogo yaliyomwagika kulizunguka.

Aliliinua (japo siyo kwa mikono mitupu, bali kwa kulishika na dekio), na kuliondoa chumbani.

Grego alikuwa na shauku kubwa kujua ni nini dada yake ataleta kama mbadala, na akajiwekea taswira anuai kuhusu hayo. Lakini hangeweza kubashiri kile ambacho dada yake, kwa moyo wake mwema, hasa alichokileta.

Alimletea, ili kupima kipi anaweza kula, vyakula anuai vilivyotapakaa juu ya gazeti la zamani. Palikuwa na mbogamboga zilizoanza kuoza, mifupa masalia ya chakula cha jana jioni, iliyofunikwa na mchuzi mweupe ambao bado kidogo uwe umeganda kabisa, zabibu na mlozi, jibini, ambayo siku mbili tu zilizopita Grego alisema hailiki, kipande kikavu cha mkate, kipande cha mkate wenye chumvi kilichopakwa siagi.

Kuongezea, aliweka chini bakuli (bila shaka bakuli hili litakuwa likitumiwa na Grego tu) ambamo ndani yake alimimina maji. Na kwa moyo wake mwema, kwa vile alijua Grego hatakula akiwepo, dada yake aliondoka chumbani haraka sana na hata kuufunga mlango kwa funguo, ili Grego atambue anaweza kujinafasi apendavyo.

Inaendelea Sehemu ya 13
 

Similar Discussions

2 Reactions
Reply
Back
Top Bottom