Chanzo Kilichounganisha wa Zanzibari | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Chanzo Kilichounganisha wa Zanzibari

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by zomba, Dec 10, 2010.

 1. zomba

  zomba JF-Expert Member

  #1
  Dec 10, 2010
  Joined: Nov 27, 2007
  Messages: 17,081
  Likes Received: 49
  Trophy Points: 0
  Author : Prof. Haroub Othman
  Date: Tue 25 jul 2000
  Subject: BARUA YA WAZI KWA MHESHIMIWA AMANI ABEID AMANI KARUME NA
  MAALIM SEIF SHARIFF HAMAD
  [Ufuatao ni ujumbe kutoka kwa Prof. Haroub Othman.
  Someni kwa furaha. HOA.]

  BARUWA YA WAZI KWA MHESHIMIWA AMANI ABEID AMANI KARUME
  NA MAALIM SEIF SHARIFF HAMAD

  Wapendwa Ndugu Amani na Seif,

  Kwanza napenda kukupongezeni kwa vyama vyenu kukuteuweni kuwa wagombea
  wa kiti cha Rais wa Zanzibar. Hii ni imani kubwa ambayo wanachama
  wenzenu wameonyesha kwenu na heshima ambayo lazima muienzi. Matumaini
  ya wazanzibari wenzenu sasa yako kwenu. Lakini kabla hatujafika siku
  ya uchaguzi, ambapo wananchi wenzetu wataamua nani kati yenu aliongoze
  taifa letu katika kipindi cha miaka mitano ijayo, kuna mambo ningeomba
  mkayafikiria na kuyasimamia.

  Sina haja ya kukuelezeeni vipi umoja na mshikamano wa visiwa vyetu
  umeparaganyika. Hakuna haja ya kunyosheana vidole juu ya nani amesababisha
  hali hii, ijapokuwa tuna wajibu wa kujua chimbo lake. Tulianza kubaguwana
  kikabila, kimkoa, kimajimbo, kichama na sasa hata kiukoo. Naliposikia hata
  uraia wa Mzee Abeid Karume unatiliwa mashakani na kizazi kile kile ambacho
  leo kinanufaika na matunda ya ujasiri na uongozi wake, nalijiuliza: Sasa
  tunakwenda wapi? Sidhani kwamba kati yenu, au yeyote kati ya viongozi wa
  juu wa vyama vyenu Zanzibar, alikuwepo pale jengo la Rahaleo mwaka 1957
  wakati Mzee Karume alipokuja kujiandikisha kupiga kura kwenye uchaguzi
  wa mwaka ule. Mimi nalikuwepo, nikichungulia dirishani. Sheikh Ali Ahmed
  alimpinga Mzee Karume kwamba hakuzaliwa Zanzibar, lakini pingamizi hii
  ilishindwa, na mahakama kuthibitisha kwamba Mzee Karume ni mzaliwa wa
  Zanzibar. Leo, miaka 43 baadae, suala hili kuletwa tena ni kuthibitisha
  tumerejea nyuma kiasi gani.

  Kwa hivyo suala la kwanza ni kurejesha imani ya Wazanzibari katika umoja
  na uzalendo wao. Njia ambayo nyinyi mnaweza kusaidia ni katika kampeni
  zenu kuhimiza wajibu, haki na heshima ya kila Mzanzibari bila ya kujali
  rangi, kabila au sehemu atokayo mtu. Tukubali na tukiri kwamba historia ya
  visiwa vyetu imejaalia mchanganyiko wa makabila na tamaduni mbali mbali,
  na hata tukisema kwamba kitovu cha uzawa ni Kizimkazi au Tumbatu, tujue
  kwamba hata sehemu hizo zilikuwa zimeingiliwa na watu kutoka nje karne
  nyingi hata kabla ya kuzaliwa Nabii Issa. Yeyote ataekwenda Kizimkazi,
  Unguja Ukuu, Tumbatu na Pemba ataona ushahidi wa haya. Kwa hivyo huyo
  Mmakunduchi, Mtumbatu au Mpemba wa leo akitafuta sana nasaba yake
  asishangae akaona kwamba katika mishipa yake ya damu kuna mchanganyiko
  wa aina mbali mbali.

  Katika historia yetu maovu mengi yametokea mnamo karne za nyuma na
  hata katika miaka hii hamsini iliyopita kikiwemo pia kipindi cha tangu
  mapinduzi. Lakini kuna haja ya kukumbushana hayo? Kwanini tufungike na
  historia hiyo iliyopita badala ya kusonga mbele na kukabiliana na ya
  leo na ya kesho? Njia ya kuhakikisha kwamba maovu hayatatokea tena ni
  kuwatia wananchi imani kwamba hakutokuwepo na siasa za ubabe na kutojali,
  kwamba misingi ya demokrasia na haki za binadamu itawekwa na kuimarishwa,
  haki muhimu za mwananchi zitalindwa, kutakuwa na jitihada za makusudi
  za kuondosha ufukara na kwamba kila mwananchi atahakikishiwa elimu,
  matibabu, chakula, mahali pa kuishi, maji safi na atafunguliwa njia za
  kuendeleza maisha na kipaji chake, na kwamba kila mmoja atawajibika,
  kutakuwa na uwazi, vyombo imara vitawekwa kusimamia yote hayo, na hakuna
  hata mmoja ataekuwa juu ya sheria.

  Katika kampeni zenu, muwatake wananchi wayasamehe yaliyopita. Naambiwa
  kwamba wakati Amani anaingia kwenye boti kutoka Dar es Salaam
  akirejea Zanzibar baada ya mkutano mkuu maalumu wa CCM kule Dodoma,
  alishindikizwa huku akiwa amekamatwa mkono na Bimkubwa Said Hanga
  na Ashura Babu. Bila ya kutaka kutonesha makovu, lakini tukio hili
  lituonyesha haja ya kusameheana: Bikumbwa ni mjane wa Abdallah Kassim
  Hanga ambae 'alipotea' wakati wa awamu ya kwanza ya SMZ iliyoongozwa
  na baba wa Amani, wakati Ashura alikuwa mke wa Abdulrahman Babu ambae
  alishtakiwa na kuwekwa kizuizini kwa miaka saba kwa kutuhumiwa kwamba
  alihusika na kuuwawa kwa Mzee Karume. Lakini leo akina mama wote hao
  wawili wanamuona Amani kuwa ni 'mtoto' wao.

  Kuna njia mbali mbali ambazo nchi zilizofikwa na misukosuko kama yetu
  zimefanya ili kuleta suluhu na amani katika jamii, na zaidi kuhakikisha
  kwamba misukosuko kama hiyo hairejei tena. Baada ya vita vikuu vya
  pili, kulikuwa na Mahakama ya Nuremburg ambayo iliwahukumu wale wakuu
  wa kifeshisti walioleta maafa duniani; na Afrika ya Kusini walianzisha
  tume ya ukweli na mapatano ambapo kila mmoja anakwenda kukiri makosa
  yake na kuomba msamaha. Katika Afrika ya magharibi, miongoni mwa makabila
  mengi, kuna desturi kwamba ukimkosea mtu, bila ya kujali ukumbwa wa kosa
  lenyewe, ukaenda tu na kumpigia magoti na kumkamata mguu, basi hana budi
  ila kukusamehe.

  Ilipendekezwa mara baada ya kuchaguliwa Sheikh Idrisa Abdulwakili
  kama Rais wa Zanzibar, kwamba Rais aitishe mkutano wa hadhara ambapo
  atawataka radhi wananchi kwa makosa na maovu yote yaliyotokea huko nyuma
  na kuwataka wayasamehe. Na baada ya hapo aombe zisomwe khitma katika
  misikiti yote ya Zanzibar na duwa kwenye makanisa na nyumba nyengine
  za ibada kuwaombea wote wale ambao wamefariki kwa sababu za kisiasa. Na
  hapo kufungua ukurasa mpya. Wazo hilo lilipuuzwa.

  Tumeona katika miaka hii ya karibuni Rais Bill Clinton wa Marekani
  alipotembelea Senegal alitaka msamaha kwa maovu yaliyotendeka wakati wa
  biashara ya utumwa; Baba Mtakatifu aliomba msamaha kwa makosa ambayo
  kanisa Katoliki imeyafanya; na hivi karibuni alipokwenda Israel, Baba
  Mtakatifu ameomba msamaha kwa Mayahudi kwa kanisa katoliki kukaa kimya
  wakati wa mateso yaliofanywa na Hitler na wafuasi wake dhidi ya Mayahudi
  kule nchi za Ulaya; serikali ya Marekani imewataka msamaha Wahindi Wekundu
  (Red Indians) kule Marekani; na serikali ya Australia imewataka msamaha
  Aborigins wa nchi hiyo; Wairish wanapatana ili wawe na taifa moja; Korea
  ya kaskazini na ya kusini zimesahau chuki na uhasama wao wa zaidi ya
  miaka 50 na sasa zinazungumzia juu ya kuungana na kusahau tofauti zao;
  na Wapalastina na Mayahudi wamo katika jitihada za kutafuta mapatano
  katika migogoro yao iliyokuwepo tangu mwaka 1948. Tusistaajabu wakati
  bado tukiwa hai tukashuhudia muungano wa Palestina, Israeli, Jordan na
  Lebanon. Huo ndio mkondo wa historia ya sasa ya ulimwengu.

  Ningekuombeni mkalifany suala hili la kuomba msamaha na kuwataka
  wananchi kuyasamehe yaliyopita kuwa ni kitu cha kwanza katika kampeni
  zenu. Na yeyote kati yenu ataeshinda katika uchaguzi ujao kuliweka hilo
  kuwa ni jambo lake la kwanza katika ajenda yake ya kazi. Vyenginevyo,
  awamu itayoongozwa na yeyote kati yenu itakumbwa na hili 'jinamizi'
  la historia yetu.

  Najuwa kwamba kila mmoja wenu ana matumaini ya ushindi mkubwa. Lakini bila
  ya kutaka kukuvunjeni moyo, mimi sidhani kwamba katika uchaguzi ujao, kama
  ulivyokuwa uchaguzi wa mwaka 1995, kuwa kutakuwa na chama kitachoshinda
  kwa wingi sana wa kura au wingi mno wa viti. Na hata ikiwa chama kimoja
  kitapata asilimia thamanini ya kura na kushinda viti 40 kati ya viti 50
  vinavyowaniwa, bado chama hicho hakitoweza kuendesha nchi peke yake. Hii
  ni kwa sababu ya mgawanyiko ndani ya jamii yetu ambao nimeuelezea hapo
  juu. Mapendekezo mengi ya maana na yenye busara yalitolewa kabla na
  baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 1995, lakini yalipuuzwa na hata kufanyiwa
  kejeli. Ni busara kwamba chama chechote kitachoshinda kikikaribishe chama
  chengine na hata wananchi wengine wasiokuwa na chama kujiunga katika
  serikali. Madhumuni ni kwamba kila chama, jumuiya na kikundi kihisi kuwa
  kimeshirikishwa na kwamba kina hisa katika utawala mpya. Hiyo inaweza
  kuitwa serikali ya mseto (coalition), ya umoja wa kitaifa (national unity)
  au ya mapatano (reconciliation), lakini la umuhimu ni kwamba itamjumuisha
  kila mmoja (inclusive). Sera za serikali hiyo bila ya shaka zitatokana
  na ilani ya uchaguzi ya chama kitachoshinda, lakini wengine pia watakuwa
  wanachangia katika kufanikisha sera nzuri na zenye manufaa kwa taifa.

  Naweza kukupeni mfano wa Liberia ambako nnaishi sasa. Sisemi kuwa hii
  ni nchi ya demokrasia halisi au kwamba ni mfano wa kuigwa katika utawala
  bora, lakini kuna kitu kimoja kimenivutia. Katika uchaguzi mkuu wa mwaka
  1997, chama cha NPP kinachoongozwa na Rais Charles Taylor kilishinda
  asilimia 80 ya kura, na kina viti 49 kati ya viti 64 kwenye Baraza la
  Wawakilishi na viti 21 kati ya viti 26 ndani ya Baraza la Seneti. Rais
  Taylor angeweza kuunda serikali bila ya kuwashirikisha wapinzani
  wake. Lakini kwenye Baraza la Mawaziri kuna mawaziri 3 kati ya 21,
  akiwemo waziri wa usalama wa taifa, kutoka vyama vya upinzani; kati ya
  manaibu waziri 55 basi 29 wanatoka ama vyama vya upinzani au hawana
  vyama; Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Mawaziri (sawa na Katibu Mkuu wa
  Ikulu huko kwetu) ni kiongozi kutoka moja ya vyama vya upinzani; na kuna
  watendaji wakuu wa idara za serikali ambao ama ni washabiki wa vyama vya
  upinzani au hawana vyama. Hivi karibuni kulikuwa na jitihada kutoka chama
  tawala za kuwaondowa baadhi ya watendaji wa serikali ambao wanajulikana
  ni wapenzi wa vyama vya upinzani na kuwaweka badala yake wakereketwa wa
  chama tawala katika nafasi hizo kwa kisingizio kwamba kinataka watendaji
  wenye kuaminika na chama, lakini jaribio hili lilipingwa na kila kikundi
  na jumuyiya zinazopigania haki za binadamu. Chama tawala kimebidi iliwache
  wazo hilo. Kwa hakika katika mkutano wake mkuu uliofanyika miezi michache
  iliyopita, chama tawala kimebidi kuwataka wanachama wake wanaoshika nafasi
  za utendaji katika chama na ambao pia ni watendaji wakuu wa serikali,
  wajiuzulu moja ya nafasi hizo.

  Miongoni mwa wananchi wenzetu kumekuwepo na hisia tofauti kuhusu
  Muungano. Najuwa pia kwamba vyama vyenu vina mitizamo tofauti juu
  ya jambo hili. Na mimi sibishi kwamba kuna matatizo mengi ndani ya
  Muungano wetu. Hili ni jambo ambalo ingefaa lijadiliwe kwa uwazi, na
  mna kila haki ya kulizungumzia katika kampeni zenu. Lakini ningeshauri
  kuwa mjadala wenyewe ungefaa uwe unaambatana na ukweli halisi wa mambo,
  ukitiliwa nguvu na takwimu na nyaraka, na uzito wa hoja, na usivutiwe
  na jazba na kutaka 'ushindi' wa ufasaha wa kuzungumza. Mkumbuke kwamba
  kubomowa ni rahisi, kujenga kunataka ujasiri, subira na ustahamilivu.

  Kwa yeyote kati yenu ataechaguliwa kutakuwa na haja ya kuangalia upya sera
  za kiuchumi na kijamii. Nimekuwa nikiwambia wenzangu kwamba inaonyesha
  nchi yetu ina uwezo mkubwa wa kuwavutia matapeli. Kila mwekezaji
  tunaeambiwa anakuja amekuwa ni 'bomu'. Ahadi za kuwepo na hoteli ya
  Holiday Inn pale uwanja wa Maisara; Sun City kule kijiji cha Fumba;
  hoteli ya kisasa na uwanja wa kuchezea 'golf' kule Mangapwani; hoteli na
  bandari ya kisasa, benki za nje ya ufukwe wa bahari pamoja na chuo kikuu
  kule Nungwi, na bustani ya viumbe vya baharini kutoka Mizingani mpaka
  Mambomsiige -- yote haya tumeyasikia! Badala yake nchi yetu imekuwa ndio
  njia kuu ya kupitishia 'unga' huku vijana wetu wengi wakitumbukia katika
  utumiaji wa madawa ya kulevya na umalaya, wakiwa hawaoni mustakabali wa
  maisha yao ya baadae. Bila ya kuwa na mawazo mapya na kutekeleza sera
  za kujitegemea na kuwapa wananchi uwezo wa kiuchumi, basi nchi itazidi
  kudidimia. Na bila ya kuhifadhi, kuendeleza na kudumisha utamaduni wetu,
  na kusita kuendekeza huu 'utamaduni wa coca-cola', basi tutazama kama
  taifa. Maana ya 'taifa' sio watu tu na eneo wanaloishi bali pia utamaduni,
  historia, mila, mavazi, lugha, vyakula na desturi zao.

  Wazanzibari wenzetu wametapakaa kila pembe ya dunia. Hakuna shaka kwamba
  wametowa na wanaendelea kutowa mchango mkubwa katika ujenzi wa Oman ya
  kisasa, pia kule Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), visiwa vya Ngazija
  na kwingi kwengineko. Nakumbuka nalipotembelea kisiwa cha Aaland kule
  jamhuri ya Finland kama mjumbe wa Tume ya Nyalali naliambiwa kwamba
  alikuwepo daktari wa Kizanzibari akifanya kazi pale; kuna mji mdogo
  Ujarumani ambao wakaazi wake wanamtegemea daktari wa Kizanzibari ambae
  yeye na mkewe, ambae pia ni daktari, wana kliniki yao pale kwenye mji
  huo; kuna mji mwengine Ujarumani ambapo dakitari wa meno anaesifika hapo
  ni dada yetu wa Kizanzibari; wanataaluma wa Kizanzibari ndio waliokuwa
  miongoni mwa watu wa mwanzo kufundisha kwenye chuo kikuu cha Papua New
  Guinea; na kuna wanataaluma wa Kizanzibari kwenye vyuo vikuu mbali mbali
  vya Uingereza, Marekani, Ghana, Ujarumani, Canada, n.k. Mtunzi maarufu
  wa riwaya duniani kwa lugha ya kiingereza ni Mzanzibari aliezaliwa pale
  Malindi na anafundisha chuo kikuu cha Middlessex Uingereza. Bahati mbaya
  kwamba alipokuja Zanzibar miaka miwili iliyopita, hakuna hata mmoja
  aliyemdhukuru. Kuna pia wafanyibiashara wa Kizanzibari waliofanikiwa
  katika nchi za nje: huduma za vyakula zinazotolewa pale uwanja wa ndege
  wa Harare kwa wasafiri na ndege zinazotuwa hapo zinatolewa na kampuni
  inayomilikiwa na Mzanzibari. Sio wote walioondoka Zanzibar wameondoka kwa
  sababu za kisiasa; na baada ya Jamshid kupewa msamaha na kukaribishwa
  arejee, sioni tena hata hao walioondoka kwa sababu za kisiasa wasiweze
  nao kukaribishwa. La muhimu ni kuwaona hawa ndugu zetu waliopo nchi za
  nje kuwa ni rasilmali kubwa ambayo pindi ikihamasishwa na kuelekezwa,
  na kutotiliwa mashaka na wasi wasi, basi inaweza kusaidia sana katika
  maendeleo yetu. Wenzetu wa Jamhuri ya Watu wa China wanawatumia vizuri
  Machina wanaoishi nchi za nje kwa kuwavutia waweke rasilmali zao China,
  watowe ujuzi wao na hata kuwapeleka watoto wao kusoma China katika baadhi
  ya fani. Mayahudi kokote walipo wanaisaidia Israel; na chama cha PLO
  kwa miaka mingi kimeendeleza mipango yake ya elimu na huduma za jamii
  kwa kutegemea michango ya Wapalestina wanaoishi katika nchi mbali mbali.

  Msimamo wa Seif na chama cha CUF juu ya Tume ya Uchaguzi
  unajulikana. Sijui mawazo ya Amani kuhusu Tume hiyo; na CCM, tangu
  baada ya uchaguzi mkuu wa 1995, haikutamka kitu juu ya Tume, ijapokuwa
  tunakumbuka ile baruwa iliyopelekwa kwa Tume na Naibu Katibu Mkuu wa CCM
  Zanzibar kabla ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa mwaka 1995. Lakini
  kama washindani wakuu katika uchaguzi ujao itabidi muafikiane juu ya
  huyu msimamizi mkuu wa uchaguzi huo. Ikiwa nyote au mmoja wenu hana
  imani na Tume hiyo, basi si ajabu tukaingia kwenye mgogoro ule ule
  tunaojaribu kuuepuka safari hii. Kwa katiba na sheria ya uchaguzi
  zilivyo, hakuna mwenye madaraka ya kuwabadili wajumbe wa Tume mara
  wateuliwapo na Mheshimiwa Rais. Lakini kwa kuitakia salama Zanzibar (na
  Tanzania) na kuepusha malumbano ambayo yatazidi kuleta chuki na uhasama
  na kuirejesha nyuma zaidi nchi yetu, ningekushaurini kwamba nyote kwa
  pamoja mgewaomba wajumbe wa sasa wa Tume wakajiuzulu kwa hiari yao na
  kumuomba Mheshimiwa Rais kuteuwa wajumbe wengine ambao wataonekana na
  jamii kwamba si washabiki wa upande wowote ule. Hili linawezekana kwani
  mtakumbuka kwamba mwaka 1995 Maalim Mwinshiwesa Idarous aliombwa kujiuzulu
  kama mwenyekiti wa Tume kwa kuhisiwa kwamba kwa sababu ya mahusiano yake
  ya karibu na chama tawala, huenda akapendelea upande mmoja, na alifanya
  hivyo. Ni vizuri ikiwa nyinyi na vyama vyenu mkaingia katika mashindano
  haya mkiwa na imani na Tume kwamba itatenda na kusimamia haki.

  La mwisho ni kukuombeni kuwataka wanachama wenu na wananchi wenzetu
  kwa ujumla kuhakikisha kwamba tunakuwa na uchaguzi wa amani na
  salama. Tafadhilini msiwachie jazba na hamasa kutawala, badala yake
  muhubiri busara, hekima na upendo ambazo ndizo nguzo za mila na maadili
  yetu.

  Haya yote ninayokwambieni ni kutoka moyoni mwangu kwa kuwa, kama usemi
  wa kiswahili usemavyo, kuishi kwingi ni kuona mengi. Wajibu wangu kama
  msomi ni kushauri na kutanabahisha pale nnapoona kuna kasoro au njia
  tuifuatayo itatupeleka pabaya. Ni hiari yenu kama wanasiasa kuukubali
  au kuukataa ushauri mnaopewa. Lakini ni wajibu wa wananchi kuhakikisha
  kwamba hawaongozwi kwenye giza na ukosefu wa matumaini.

  Bahati mbaya kwamba safari hii sitoweza kupiga kura kwani nitaporejea
  nchini muda wa kujiandikisha kama mpiga kura utakuwa umemalizika. Lakini
  nakutakieni kila la kheri. Yeyote kati yenu ataeshinda kwenye uchaguzi
  ambao utaonekana na kuthibitishwa kwamba ni huru na wa haki awe na
  uhakika wa kupata ushirikiano wangu (pindipo atauhitaji).

  Wasalam,

  Profesa Haroub Othman 22 Julai 2000

  Monrovia, Liberia
   
 2. M

  Mdondoaji JF-Expert Member

  #2
  Dec 10, 2010
  Joined: Mar 17, 2009
  Messages: 5,106
  Likes Received: 45
  Trophy Points: 145
  Huyu Gwiji Mwalimu wangu Professa Haroub Othman anazijua siasa za zanzibar aliona mbali sana mmungu amlaze mahala pema peponi na nadhani viongozi wetu wa zanzibar waliisoma sana hii barua wakielewa maudhui yake ndani. Mungu amlaze mahala pema peponi alilitumikia taifa yeye Professa Issa Shivji ni katika watu wananafasi ya pekee katika taifa letu.
   
 3. M

  Mtabe JF-Expert Member

  #3
  Dec 10, 2010
  Joined: Sep 20, 2010
  Messages: 675
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  Aamin. Hata mie ni mwalimu wangu alinisomesha ds pale udsm
   
 4. M

  Mdondoaji JF-Expert Member

  #4
  Dec 10, 2010
  Joined: Mar 17, 2009
  Messages: 5,106
  Likes Received: 45
  Trophy Points: 145
  Nilikuwa nikiingia darasani kwakwe kumsikiliza jinsi alivyokutana na world leaders na decision makers and left his class with alot of admiration to this don. Aliona mbali na wazanzibari wakimsoma alichokuwa anataka kufanya zanzibar nadhani watafaidika sana. Pamoja na wasomi wengi ambao wapo hai sasa.
   
Loading...