Changamoto za kuingia utu uzima nimeanza kukabiliana nazo

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Mar 24, 2018
21,340
51,900
CHANGAMOTO ZA KUINGIA UTU UZIMA NIMEANZA KUKABILIANA NAZO.

Anaandika, Robert Heriel
Mtibeli

Nikiwa bado nipo kwenye sherehe ya kumbukumbu ya kuzaliwa na kuingia katika utu uzima, hata masaa 24 hayajaisha nimeanza kupata joto la jiwe. Nahisi moyo unapanuka, nahisi kichwa kinapasuka, nahisi pua zinafuka.

Nipo kwenye Rehearsal, naambiwa semina hii elekezi kuhusu utu uzima nitaimudu baada ya siku saba.
Tayari nimeshakutanishwa na Waalimu watatu ambao watanipa semina ya namna ya kuwa mtu mzima mwenye tija. Nisingekuwa Mtu mzima Hovyo.

Kila mwalimu atanifundisha siku mbili, kisha ile siku ya Saba nitafanya mtihani kuona kama nimeelewa somo au laah!

Kwenye Joining instruction ya kujiunga utu uzima nilisoma sipaswi kuwa na kiherehere wala nchecheto lakini kwaajili yenu nimejikuta nikikabwa kiherehere nikaona nije niwasimulie. Ndio kwanza hata masaa 24 hayajaisha. Iko hivi;

Mwalimu wa kwanza huyu alikuja akiwa ameongozana na Mwanamke wa makamo. Umbo lake jembamba kama namisikosita akiwa kavalia buga(suruali kubwa) na shati alilochomekea mkanda nje na kofia kichwani, mdomoni akiwa na Kiko iliyokuwa inafuka Moshi. Kwa habari ya umri mwaka huu atatimiza miaka 63 ifikapo mwezi wa saba.
Angalia yake haikuwa inanivutia sana kutokana na hiba ya macho yake. Alikuwa macho ya kuchukiza mno. Hayakunivutia sana na hii ilinifanya mara kwa mara niwe simuangalii usoni. Jambo hilo aliligundua pale aliponikaribia na kuniambia nimtazame usoni, akasema, " Nitazame! Yaangalie jinsi yalivyo. Yanaona?"
Akaniuliza, nikajikuta nababaika huku nikijikaza kumtazama usoni ingawaje rohoni nilikuwa nakereka.

"Yanaona?" Akauliza tena.
"Sijui" nikamjibu.
Akatabasamu kisha akaiweka kiko yake tena mdomoni na kuvutavuta pafu kadhaa, jambo ambalo lilifanya niweze kuona mashavu yake yaliyolegea yakiunda shimo na kujaa kila alipokuwa akivuta. Kisha akanitazama tena, hapo nikageukia upande mwingine, ambao alikuwepo yule Mwanamke ambaye nilihisi ni mke wake.
Sikuwa nimekosea, nilipogongana uso na mkewe akatabasamu, kisha akaniambia,
"Alikuwa mzuri kama wewe, mwili mkakamavu, mwenye nguvu na shupavu, alikuwa anavutia sana nyakati hizo. Ungependa kumwona akivalia zile suruali za kuachia chini huku kichwani amefuga Afro. Alafu umkute kwenye ngoma. Alikuwa mwanaume shababi mwenye haiba ya kipekee"
Hapo akanyamaza, akawa anamtazama Mwalimu wangu, ambaye bado sikuwa nimejua jina lake. Nami nikamtazama, kisha nikarudisha uso wangu kwa yule Mwanamke.
Alinielewa. Alijua ninataka anieleze nini kimetokea.

"Mitindo mipya yenye nguvu ya ushawishi ilimjia kwa nguvu. Ikamteka. Akajikuta katika mkondo wa kimbunga cha vimondo. Huyo! Huyo! Huyo! Akabebwa na maisha mapya. Tumbaku ikamdaka kama sumaku. Ikamvuta kwa nguvu ikamkamata. Niseme huyo ndio aligeuka mkewe wa pili na mimi sasa sikuwa na nafasi. Ukichanganya na Pombe ndio ikammaliza kabisa. Wala usingedhani anamwili huo kama smigo"
Hapo akawa anamnyooshea mkono nami nikawa namtazama kama ndio kwanza nimemwona.
" Alikuwa na mwili mzuri na mkubwa sana. Lakini pombe imemharibu sana...."
"Koooh! Koooh! Kwookwkooko!" Mwalimu anakohoa jambo linalomkatisha yule mwanamke asiongee.
Ukimya unatokea kwa kitambo.
Kisha yule Mwanamke anazungumza kwa sauti ya chini, " Tumbaku hiyo! Mapafu yote yameoza"

" niite mwalimu Kapoza, nitakufundisha somo la Mahusiano na Familia" Yule mwalimu akajitambulisha bila ya kumjibu yule Mwanamke jambo lolote.
Hapo nikawa nawatazama kwa zamu.
" Huyu ni mke wangu. Muite Mama Kapoza. Tutaanza somo kesho. Lakini somo letu hautakuwa na daftari wala kalamu. Jioni ya leo utakuja kulala nyumbani kwangu. Hiyo ndio itakuwa shule ambayo utajifunza kwa siku mbili tuu. Naomba ujiandae"
Mwalimu Kapoza akamaliza.

Wakaondoka, kabla sijatafakari kilichotokea, akaja mwanaume mwingine. Huyu alikuwa kavaa nguo kuukuu na kama nisingekuwa makini kutazama basi nisingeona sehemu ya shati pembeni kabisa ya kikwapa kukiwa kumechangia lakini licha ya mwonekano huo alikuwa na kitambi cha kidizaini hivi. Upara kichwani alioupuuza ambao nzi walikuwa wameugeuza uwanja wao wa kucheza licha ya kuwa hakuwa anajali.

Alikuwa juu ya pikipiki chakavu, kibao cha mbuzi. Akaniambia nipande, huyo nikapanda, tukiwa njiani akawa analalamika mno kwani pikipiki yake ilikuwa ikimsumbua, na fundi aliyempelekea naye akiwa amemuibia Spare zake na kumbadilishia zingine.

" Mafundi sio waaminifu kabisa. Hawajui kazi siku zote ni uaminifu" akawa anaongea huku shati lake likiunda puto kubwa kutokana na upepo uliosababisha na mwendo wa pikipiki. Puto lile la shati lilikuwa likipiga uso wangu. Nilikuwa najitahidi kukwepa lakini baadaye nilizoea.

Tukafika, lilikuwa ni shamba lake lenye mifugo ainaaina. Nilweza kuona Nguruwe, bata, kuku na ng'ombe. Akawa anawabadilishia chakula na kuondoa uchafu katika mabanda na sehemu zao za kula na kupumzika.
Kisha tukaenda kwenye mabanda ya kuku akaokota mayai Trei tano hivi. Huyu mwalimu hakuwa na maelezo mengi.

Walifurahisha kuwaona ingawaje niliiona kama kazi ngumu.
"Unapenda sana wanyama wako" nikasema, hapo nilimwona akiwa ameshika ng'ombe kichwani akiwa anamchezea;
" Anaitwa Amanda. Kwa siku anatoa lita 20 siku nyingine akishiba vizuri mpaka lita 30. Nampenda sana huyu. Yeye ndiye aliyenifanya niwe na yote haya. Ni zawaida kutoka shirika la kigeni la wazungu nilipewa kama tuzo"
"Huyu na huyu ni watoto wake" akamaliza, lakini nikamkatisha,
" Kwa nini unamuita Amanda, na vipi hili dume"
" Yule Mwanamke wa kizungu aliyenipa huyu ng'ombe kipindi hicho akiwa ndama jina lake aliitwa Amanda. Kwangu ni ukumbusho. Hili dume nilinunua kwenye mnada katika ranchi ya taifa"

"Muda imesonga, jua limekua kali. Tuondoke"
Hao tukaondoka, nikabeba mayai kisha nikakaa nyuma ya kibao cha mbuzi, pikipiki. Baada ya dakika 20 tulikuwa tumefika nyumbani kwa mwalimu huyu.
Nyumba yake haikuwa inaendana na mwonekano wake. Alikuwa na jumba kubwa sana. Lenye nafasi likiwa limezungukwa na miti ya kivuli na matunda.

" Karibu Taikon. Hapa ndio nyumbani. Kuanzia kule, ona kule, unaona ule mnazi pale, eeenhe! Paka kwenye zile nyumba za chini kule kote ni kwangu. Upande huu mwisho ni kwenye ule mwembe"
Alikuwa akinionyesha himaya na milki yake.
Nikawa naangaza macho yangu kutazama ufahari wa mwalimu yule.

Watoto kadhaa wakaja, wakatupokea, kisha Mwanamke mmoja wa makamo akaja akatusalimu kisha nikatambulishwa kuwa ndiye mama mjengo.

" Niite Mwalimu Zengo, nitakuwa mwalimu wa Kazi na biashara" Akaletewa jagi la maji akabwia fumba kadhaa kisha akaendelea
" Ratiba yetu itaanza siku ya tatu kutoka sasa"

Mwalimu wa tatu ndio niko njiani naenda kwake. Nitawapa mrejesho..

Acha Nipumzike sasa.

Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
Kwa sasa Dar es salaam
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom