CHADEMA yawavutia kasi Halima Mdee na wenzake 18

Suley2019

JF-Expert Member
Oct 7, 2019
1,815
4,565
Baraza Kuu la Chadema litaketi muda wowote baada ya viongozi wakuu wa chama hicho kumaliza ziara ya vikao vya ndani waliyoifanya zaidi ya mikoa 20 ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Pamoja na majukumu mengine, Baraza Kuu la Chadema ndilo lenye jukumu la kusikiliza na kutoa maamuzi juu ya rufaa za uchaguzi na za kinidhamu kutoka ngazi za chini pamoja na kujadili taarifa za Kamati Kuu na kutoa maamuzi na maelekezo kwa utekelezaji.

Katika kutekeleza majukumu hayo ya kikatiba, Baraza hilo bila shaka litaamua hatima ya wabunge 19 wa viti maalumu waliofukuzwa uanachama na Kamati Kuu, pale wajumbe watakapojadili rufaa zao.

Wabunge hao, baadhi yao wakiwa wajumbe wa Kamati Kuu, Baraza Kuu na viongozi wa mabaraza ya chama – Bawacha na Bavicha, walivuliwa nyadhifa za uongozi na uanachama Novemba mwaka jana, wakidaiwa kwenda kinyume na msimamo wa chama hicho wa kususia viti maalumu kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu 2020.

Baada ya kufukuzwa uanachama, baadhi yao walikata rufaa Baraza Kuu lakini tangu wakati huo lilikuwa halijaketi kuisikiliza.

Kwa nyakati tofauti, akiwa katika ziara ya kichama, Mbowe bila kutaja rufaa hizo, amekuwa akigusia kikao hicho kuwa kitajadili bajeti ya mwaka ya chama hicho, mpango kazi wa chama, ikiwemo Operesheni Haki inayoendelea.

Mwezi uliopita, akiwa Mwanza Mbowe alisema, “tukitoka hapa tunakwenda kanda za magharibi, kati, Nyasa, Kusini, Pwani, Pemba kisha tunamalizia Unguja. Tukimaliza mzunguko huu tunakwenda kufanya kikao cha Baraza Kuu taifa la chama lenye wajumbe zaidi 600.

“Kikao hiki cha siku tatu kitafanyika kwenye kanda itakayofanya vizuri kwenye Operesheni Haki. Kwa hiyo hii ngoma nawaachia nyie, maana Kanda ya Kaskazini, Serengeti, Mbeya na Dar es Salaam wote wanataka kikao hiki kifanyike kwenye maeneo yao,” alisema Mbowe.

Vilevile Julai 4 mwaka huu, akizungumza katika mkutano wa jimbo la Segerea katika mwendelezo wa vikao vya ndani, Mbowe alisema baada ya kumaliza ziara yao katika Kanda ya Pemba na Unguja wikiendi watakuwa Dar es Salaam, kwa ajili ya maandalizi ya kikao cha Baraza Kuu.

Ziara hiyo inahitimishwa leo Unguja kwa viongozi wakuu wa Chadema wakiongozwa na Mbowe aliyeambatana na naibu makatibu wakuu wa Chadema (Bara na Zanzibar), pamoja na viongozi wa Bavicha, Bazecha na Bawacha, ikiashiria kwamba muda wa Baraza Kuu ndio umewadia.

John Mrema, mkurugenzi wa Mawasiliano, itikadi, uenezi na mambo ya nje alipoulizwa na Mwananchi jana, alijibu kwa ufupi kuwa “ni kweli kikao cha Baraza kimekaribia”.

Jana Mbowe akiwa na viongozi wenzake wakuu walifunga mafunzo ya kuwajengea uwezo wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya mikoa ya Kanda ya Pemba na leo anatarajiwa kuongoza kikao cha Kamati ya Utendaji ya Kanda ya Unguja kwa ajili ya kuweka mikakati ya kuimarisha na kukijenga chama hicho.

Operesheni Haki ilianza Mei 25 mwaka huu, Jijini Arusha, pamoja na mambo mengine inahamasisha madai ya Katiba Mpya, jambo ambalo limekuwa likisisitizwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe anapohutubia vikao hivyo.

Ziara hiyo imejikita pia katika kusajili wanachama wa chama hicho kidijitali, iliyoipewa jina la ‘Tunasonga Kidijitali’ sanjari na kuwahamasisha kulipa ada na kukata kadi zinazouzwa kulingana na uwezo wa mwanachama kuanzia Sh25,00, 10,000, Sh25,000, Sh 100,000 hadi Sh200,000.

Credit: Mwananchi
 
Rekebisha hizo ada, umechanganya 2500 na 25,000 Mara mbili
 
Back
Top Bottom