Ndugu wana JF,
Nitakachoandika hapa ni mtizamo wangu, na niko tayari kuelimishwa na kukosolewa maana hiyo ndiyo demokrasia.
Watanzania walio wengi wanapenda mabadiliko mema na ya tija kisiasa hapa Tanzania. Pia wamechoka na ukiritimba, rushwa, wizi wa mali za umma, ufujaji wa pesa za walipa kodi, kupeana vyeo na madaraka bila kujali vigezo husika nk.
Tulikuwa na mfumo wa chama kimoja kwa muda mrefu sana hivyo chama na serikali tawala walikuwa huru kufanya watakavyo bila ya kupingwa.
Ulipokuja mfumo wa vyama vingi vya siasa, wanasiasa wengi walianzisha vyama vya upinzani kwa malengo waliyoyajua wao wenyewe. Vyama vingi kati ya hivyo vilivyoanzishwa vimekufa ama vimezorota tokana na sababu mbalimbali.
Chadema bado kipo na ndicho kinaonekana kama ndiyo mpinzani wa CCM, huku kikiungwa mkono na watanzania wengi waliopigika kimaisha. Watanzania hawa wanaamini kupigika kwao kimaisha ni sababu ya kutawaliwa na CCM kwa muda mrefu. Kila jambo lililobaya ndani ya Tanzania wanailaumu CCM na serikali yake, kwa mfano kuzorota na kushuka kwa elimu, matibabu, wizi wa mali za umma, ufujaji wa pesa za walipa kodi nk.
Chadema ambacho kinaonekana ni matumaini ya wanyonge waliopigika kimaisha kimekuwa kinapiga kelele sana za kuilaumu CCM kwa kuwasababishia maisha magumu Watanzania, na pia kinaomba watanzania wakipe ruhusa ya kutawala Tanzania.
Kwa upande wangu naona CCM na Chadema vyote ni sawa, kwa maana kwamba yanayofanywa na CCM ndiyo yanayofanywa na Chadema.
Kwa kufafanua kidogo ni kwamba nilitegemea kwamba Chadema kama chama cha upinzani, chenye uchungu wa kweli na maisha ya watanzania kingekuja na utaratibu, mipangilio na utendaji tofauti kabisa na ule wa CCM.
Chadema wanasema CCM wanafuja pesa za walipa kodi, lakini Chadema ina wabunge wengi tu ndani ya bunge la Jamhuri. Sisi sote tunajua jinsi gani wabunge wetu wanavyokula pesa za walipa kodi, kuanzia mishahara mikubwa, posho za vikao na marupurupu kibao.
Nilitegemea wabunge wa Chadema wangelikataa kuchukua mishahara mikubwa, posho za vikao na marupurupu ili kuonesha kwamba wanalipinga hilo jambo kivitendo.
Kama walishindwa kuacha kuchukua huo mshahara mkubwa na posho za vikao basi nilitegemea wachukue hizo pesa na wazirudishe kwa watanzania. Wangeweza kutoa sehemu fulani ya mshahara wao kila mwezi na kuchanga pamoja ili kulisaidia jimbo moja la chadema katika ununuzi wa madawati, madawa nk. Kama kuna wabunge wa CDM 10 bungeni, wakachanga 2,000,000 kila moja utaona wazi kwamba wanaweza pata 20,000,000 kwa mwezi kwa ajili ya kusaidia jimbo moja la Chadema. Lakini sioni tofauti kati ya yale wafanyayo CCM na CDM. Wote wanachukua mapesa kujaza matumbo yao, wanachukua ma-VX, posho za vikao nk.
Tutawaamini vipi Chadema kama kweli wanataka kuwaletea watanzania mabadiliko iwapo nao wanatenda yaleyale wanayoyapigia kelele majukwaani?. Kweli tuna upinzani wa kisiasa Tanzania?, kwa mtazamo wangu naona mpinzani wa kweli bado hajazaliwa Tanzania.